read

Haki Ya Mwanamke Katika Mitala

Nukta ya pili ni kuwa uwingi wa idadi ya wanawake wanaofaa kuolewa sio tu kwamba hufanya haki kwa ajili yao, bali pia na wajibu kwa ajili ya mwanaume na mwanamke aliyeolewa.

Hapana shaka kwamba ndoa ni moja ya haki za asili na ni moja ya haki za msingi za binadamu. Kila mtu awe mwanaume au mwanamke, ana haki ya kuishi maisha ya familia na kupata watoto. Haki hii ni sawa na haki ya kufanya kazi, kuwa na nyumba, kupata elimu na huduma za afya na haki ya kufurahia uhuru na usalama.

Ni jukumu la jamii kuhakikisha kwamba hakuna kizuizi kinachowekwa katika upatikanaji wa haki ya asili na ya msingi ya binadamu. Badala yake, jamii inapaswa kutoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha lengo hili.

Ni maoni yetu kuwa moja ya dosari kubwa za Amizio la Haki za Binadamu kwa wote ni kutoipa umuhimu wowote haki hii. Azimio limeitambua haki ya uhuru na usalama, haki ya kupata huduma bora za kimahakama, haki ya kuwa na uraia na kuubadili, haki ya kuoa au kuolewa bila vipingamizi vya rangi au dini, haki ya kumiliki mali, haki ya kukusanyika na haki ya kupumzika na kupumbaa, lakini azimio hili halijaitaja haki ya mtu kuishi maisha ya ndoa halali.

Kwa mwanamke, haki hii ni yenye umuhimu mkubwa sana, kwani anayahitaji maisha ya kifamilia zaidi kuliko mwanaume. Kwa mwanaume kilicho muhimu zaidi, katika ndoa ni ngono na kwa mwanamke kilicho muhimu zaidi ni hisia za moyoni na roho. Kama mwanaume hana familia, angalau anaweza kukidhi sehemu ya mahitaji yake kwa kujiingiza katika ngono holela na ufuska. Lakini kwa mwanamke, familia ina umuhimu mkubwa zaidi. Ufuska hauwezi kukidhi japo sehemu tu ya mahitaji yake ya kimwili na kimhemko (hisia ya moyoni).

Kwa mwanaume, haki ya kuwa na familia ina maana kukidhi tamaa zake za ngono, haki ya kuwa na mwenzi maishani na haki ya kuwa na watoto halali. Lakini kwa mwanamke, ndoa inamaanisha pia kuwa na mlinzi na mwangalizi na ambaye anaweza kumpa msaada wa kimaadili.

Baada ya kuzielezea nukta hizi mbili, kwamba kwanza idadi ya wanawake wanaofaa kuolewa ni wengi kuliko idadi ya wanaume wanaofaa kuoa, na pili kwamba ni haki ya asili ya binadamu kuwa na familia, ni rahisi kutoa hitimisho kwamba ikiwa ndoa ya mume kuwa na mke mmoja itafanywa kuwa ndio ndoa pekee iliyo halali, idadi kubwa ya wanawake itakuwa katika hatari ya kunyimwa haki yao ya asili, na hivyo ni ndoa za mitala tu ndio zinaweza kuwarejeshea wanawake hao haki hii iliyo hatarini.

Ni jukumu la wanawake wa Kiislamu, kwamba kama njia ya kutetea haki za wanawake, waitake na kuishinikiza tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu kuutambua rasmi mfumo wa ndoa za Kiislamu wa kuwa na wake wengi kama haki ya binadamu, na hii itakuwa ni neema kubwa kwa mwanamke na maadili. Ukweli kwamba kanuni hii imetoka Mashariki na nchi za Magharibi zinapaswa kufuata usionekane kuwa ni dhambi.

Nadharia Ya Russel

Kama ilivyoonyeshwa hapo awali, Bertrand Russel alikuwa anaufahamu ukweli kwamba ndoa za kuoa mke mmoja kufanywa kuwa ndio ndoa pekee zilizo halali kungewanyima wanawake wengi haki ya kuolewa. Amependekeza suluhisho rahisi sana la tatizo hili. Alitaka wanawake waruhusiwe kuwashawishi wanaume na kuzaa watoto wasio na baba. Kama ambavyo baba huwa anasaidia katika matunzo ya watoto, serikali inapaswa kuchukua nafasi ya baba na watoe ruzuku kwa wanawake ambao hawajaolewa.

Russell anasema kwamba hivi sasa nchini Uingereza kuna zaidi ya wanawake milioni mbili waliozidi idadi ya wanaume ambao kamwe hawatarajii kuolewa na kupata watoto kutokana na sheria iliyopo inayotaka mwanaume awe na mke mmoja tu. Hii ni dhulma kubwa. Anasema kwamba mfumo wa mume mmoja mke mmoja umejengwa juu dhana kwamba idadi ya wanaume inalingana na idadi ya wanawake, lakini pindi idadi hizi hazilingani, hawa wanawake waliozidi huwa hatarini kubakia bila kuolewa katika umri wao wote. Aidha, ikitokea haja ya kuongeza, idadi ya watu, aina hii ya ndoa sio tu kwamba haina maslahi na umma, achilia mbali maslahi ya mtu mmoja mmoja.

Hili ni suluhisho la tatizo hili la kijamii, kama lilivyopendekezwa na mwanafalsafa mkubwa wa karne ya 20. Lakini kwa mujibu wa Uislamu, tatizo lote hutatuliwa ikiwa idadi ya kutosha ya wanaume wenye uwezo wa kifedha, wa kimaadili na kimwili watakubali kuoa mke zaidi ya mmoja na kuwatendea uadilifu na kutoonyesha upendeleo baina ya watoto wa wake hawa wawili. Mke wa kwanza anapaswa kumpokea na kumkubali kwa ukunjufu mke wa pili kwa nia na lengo la kutekeleza jukumu la kijamii ambalo ni muhimu sana na ni namna bora ya maadili.

Kinyume na kifra za Uislamu, mwanafalsafa huyu anawashauri wanawake walionyimwa haki ya kuolewa, wawaibe waume wa wanawake wengine na anatoa wito kwa serikali kuwasaidia na kuwatunza watoto hawa waliozaliwa katika mahusiano haramu.

Inaonekana kwamba mwanafalsafa huyu wa karne ya 20 anadhani kuwa mwanamke anahitaji ndoa kwa sababu tatu: kukidhi tamaa zake za ngono, kupata watoto na kukidhi mahitaji yake ya kiuchumi. Haja mbili za mwanzo zinaweza kukidhiwa kwa ulaghai na haja ya tatu itekelezwe na serikali. Anasahau kwamba mwanamke ana haja za hisia za moyoni pia. Anataka awe chini ya uangalizi wa mume anayempenda na kwamba mkataba wake na mwanaume huyo usiwe ni wa kingono peke yake.

Nukta nyingine ambayo mwanafalsafa huyu hajaipa umuhimu ni hadhi ya watoto waliozaliwa katika mahusiano haramu. Kila mtoto huhitaji wazazi wanaoeleweka vizuri na upendo wao wa dhati. Uzoefu unaonyesha kuwa mara nyingi mwanamke huwa haonyeshi upendo kwa mtoto wake ambaye baba yake hajulikani. Ni vipi ukosefu wa upendo huu unaweza kufidiwa? Je serikali inaweza kufanya chochote katika hili?

Bertrand Russell anasikitika kwamba wanawake wengi watabaki bila watoto mpaka pendekezo lake lipewe sura ya kisheria. Lakini anapaswa kujua kuwa wanawake wa kiingereza hawawezi wakasubiri sheria yoyote. Wao wenyewe tayari wameshatatua tatizo hili, wanaiba waume za watu na wanapata watoto wasio na baba.

Katika ripoti ya mwaka ya 1958, iliyoandaliwa na Dr. Z.A. Scott, Mkuu wa Idara ya Utabibu ya Halmashauri ya London, ilionekana kwamba katika watoto kumi waliozaliwa mwaka uliopita, mtoto mmoja ni wa nje ya ndoa. Ripoti hiyo pia ilisema kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa nje ya ndoa inazidi kuongezeka. Idadi ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa ilipaa kutoka watoto 33,838 mwaka 1957 hadi 54,433 katika mwaka uliofuata.

Inaonekana kwamba Waingereza wameamua kutatua tatizo lao bila kuwa na haja ya kusubiri kupitishwa kwa pendekezo la Bertrand Russell kuwa sheria.

Mitala Yakatazwa, Liwati Yaruhusiwa

Serikali ya Uingereza, badala ya kuufanyia kazi ushauri wa Russell na kutatua tatizo la wanawake ambao hawajaolewa, imechukua hatua katika mwelekeo kinyume na huu. Imezidi kumnyima zaidi mwanamke haki ya kuwa na mume kwa kuhalalisha liwati. Kwa sasa mitala hairuhusiwi nchini Uingereza lakini liwati (ya wanaume kwa wanaume) inaruhusiwa. Mbele ya macho ya Waingereza sio jambo la ubinadamu kuwa na mke wa pili.

Lakini ikitokea kuwa “mke” wa pili ni mwanaume, basi hapo inakuwa sio tatizo. Wanaiona liwati kuwa ni kitendo kitukufu kinachoafikiana na mahitaji ya karne ya 20. Kwa mujibu wa sheria ya mamlaka ya Uingereza, kuwa na wake wengi hakukatazwi ili mradi tu wake watakaoolewa baada ya mke wa kwanza wawe na ndevu (yaani wanaume). Inasemekana kwamba nchi za kimagharibi zimetatua matatizo ya masuala ya ndoa na familia, na kwamba sisi tunapaswa kuiga mfano wao.

Kitendo hiki cha kimagharibi hahishangazi kwani ni matokeo ya mantiki ya jinsi nchi za kimagharibi zinavyokwenda.

Kinachoshangaza ni kwamba watu wetu, hasa vijana wasomi, wamepoteza uwezo wao wa kufikiri kwa uhuru na kuchambua mambo. Wamepoteza haiba zao. Wanawaamini wamagharibi kirahisi mno. Kama wana almasi mikononi mwao na watu kutoka upande mwingine wa dunia wakisema kuwa hiyo sio almasi ni ubao wa fomaika basi huitupa almasi yao. Lakini wakiona ubao wa fomaika mikononi mwa mgeni na wakiambiwa kuwa hiyo ni almasi, wao huamini kirahisi kabisa.

Je Mwanaume Ana Asili Yakuoa Wake Wengi?

Utashangaa ukiambiwa kuwa wanasaikolojia na wanafalsafa wa huko Magharibi wanaamini kuwa mwanaume ni mwenye asili ya kuoa wake wengi na kwamba ndoa za mke mmoja ni kinyume cha maumbile yake.

Will Durant, akielezea vurugu za kimaadili leo, anasema kuwa sehemu kubwa ya matatizo haya ya kimaadili yanatokana na hamu isiyotibika ya kupenda kuwa na wanawake wa aina mbalimbali. Mwanume kwa asili, hawezi kuridhika na mke mmoja.

Anasema kwamba kwa asili mwanaume hupenda kuwa na wake wengi. Ni vikwazo vikali tu vya kimaadili, kiasi cha kutosha cha umasikini na ukakamavu wa mke wa kwanza ndio vinaweza kumlazimisha kubaki na mke mmoja.

Profesa wa Kijerumani, Schmidt, anasema kuwa katika kipindi chote cha historia, mwanaume amekuwa sio mwaminifu kwa mkewe. Kuna viashirio kuwa hata katika zama za kati, vijana wa kiume walikuwa wakibadili wapenzi wao kila mara, na nusu ya wanaume walioowa hawakuwa waaminifu kwa wake zao.

Robert Kinsey katika ripoti yake inayojulikana kama ‘Ripoti ya Kinsey’, anasema kwamba wanaume na wanawake wa Kimarekani wanawazidi watu wa mataifa mengine yote kwa kutokuwa waaminifu katika ndoa. Katika sehemu nyingine ya ripoti anasema kwamba, tofauti na mwanaume, mwanamke huwa hapendi kubadili wanaume na ndio maana mara nyingi huwa anakataa ofa za wanaume wa nje, lakini mwanamume huona kubadili wanawake kama kujifunza mambo mapya.

Kilicho muhimu zaidi kwa mwanaume ni kufurahia ngono kuliko hisia za moyoni na kiroho. Mwanaume hujifanya kuwa ana hisia za moyoni na za kiroho kabla tu hajapata ngono. Daktari mashuhuri alimwambia Kinsey kuwa ni dhahiri kuwa mwanaume ni mwenye asili ya kuwa na wanawake wengi wakati mwanamke ni mwenye asili ya kuwa na mume mmoja, kwa sababu mamilioni ya manii (mbegu za kiume) hutengenezwa kwa mwanaume wakati kwa mwanamke ni yai moja tu ambalo huzalishwa katika mwezi mzima. Mbali na nadharia ya Kinsey, itakuwa si vibaya kama tutajiuliza sisi wenyewe kama ni vigumu kwa mwanaume kuwa mwaminifu au la.

Mwanasosholojia wa Kifaransa akijibu swali hili anasema kuwa mwanaume kuwa mwaminifu katika ndoa sio tu kwamba ni vigumu bali haiwezekani kabisa. Mwanamke mmoja huzaliwa kwa ajili ya mwanaume mmoja, lakini mwanaume mmoja huzaliwa kwa ajili ya wanawake wote. Mwanaume akiwa sio mwaminifu na akimsaliti mke wake, asilaumiwe. Ni kosa la maumbile, ambayo yamemuwekea nguvu zote hizi za kutokuwa mwaminifu ndani yake.

Gazeti moja la Kifaransa lenye kichwa cha habari “Mwenendo wa Mapenzi na Ndoa wa Kifaransa”, limeandika kuwa wanandoa wa Kifaransa wameshatatua tatizo hili. Wanajua kanuni za mchezo huo. Ilimradi mwanaume havuki mipaka, mahusiano yake ya mara moja moja na wanawake wengine sio tatizo. Kama kanuni, mwanaume hawezi akaendelea kuwa mwaminifu kwa mke wake baada ya miaka miwili ya ndoa yake. Kwa kiasi fulani hali ni tofauti kwa wanawake na ni bahati kwamba wao pia wanajua tofauti hii. Nchini Ufaransa, mke huwa haoni kuwa ametendewa ubaya kama mume wake amezini.

Hujifariji kwa kusema kwamba anaweza kuwa ameupeleka mwili wake kwa mwanamke mwingine lakini roho na hisia zake za moyoni zinaendelea kuwa zake (huyu mke mwenye mume).

Miaka kadhaa iliyopita kulikuwa ubishani juu ya maoni yaliyotolewa na mwanabailojia aitwaye Dr. Russel Lee. Alikuwa na maoni kwamba kitendo cha mwanaume kuridhika na mke mmoja hudhoofisha uzao wake hivyo kitendo hiki huwa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Alifikiri kwamba mfumo wa yeye kuwa na wake wengi ulikuwa unawafanya watoto wake kuwa na afya na nguvu.

Tunaamini kwamba maelezo haya yaliyotolewa juu ya maumbile ya mwanadamu sio sahihi hata kidogo. Wasomi hawa wanaonekana kuwa wamehamasishwa na hali ya mazingira ya kimaadili katika sehemu yao ya dunia.

Hata hivyo, tunaamini kwamba kibaiolojia na kisaikolojia mwanamke na mwananume wanatofautiana na maumbile yamewafanya hivyo kwa makusudi na kwa malengo maalumu. Hivyo usawa wa haki zao usitumike kama kisingizio cha kuzifanya haki zao kuwa sawiya. Hata kwa maoni ya wale wanaounga mkono ndoa za mke mmoja, wanakiri kuwa tabia ya kisaikolojia ya mwanaume ni tofauti na ya mwanamke. Kwa asili mwanamke anapaswa kuolewa na mume mmoja tu. Yeye kuolewa na waume wengi ni kinyume na asili yake na hakuafikiani na matarajio yake kwa mumewe. Lakini mwanaume sio mwenye asili ya kuwa na mke mmoja, kwa maana kwamba kwake kuwa na wake wengi sio kinyume na tabia yake pamoja na matarajio yake kwa mkewe.

Lakini hatukubaliani na maoni kuwa ndoa za mke mmoja haziafikiani na asili ya mwanaume. Sio sahihi kabisa kusema kwamba tabia ya mwanaume ya kupenda kubadili wanawake haitibiki. Pia hatuamini kuwa mwanaume hawezi kuwa mwaminifu, au kwamba mwanamke mmoja ni wa mwanume mmoja lakini mwanaume mmoja ni wa wanawake wote.

Kwa imani yetu, sababu za kutokuwa mwaminifu kwa mwanaume zinahusiana na mazingira ya kijamii na sio maumbile ya mwanaume. Mambo yaanayosababisha kutokuwa mwaminifu yanatokana na mazingira ambayo yanamhimiza mwanamke atumie aina zote za visahwishi ili kumvuta na kumpotosha mwanaume, kwa upande mmoja na kwa upande wa pili sheria ya kuoa mke mmoja tu huwanyima mamilioni ya wanawake fursa ya kuolewa.

Katika ulimwengu wa Kiislamu, kabla ya kuja kwa mila na tabia za kimagharibi, 90% ya wanaume walikuwa wanakaa na mke mmoja tu. Hawakuwa na mke zaidi ya mmoja wala hawakuwa wakijiingiza katika uzinifu na ufuska.

Mitala Kama Njia Ya Kuokoa Ndoa Ya Mke Mmoja

Utashangaa tukisema kuwa mitala ni kipengele muhimu sana kilichohudumia ndoa za mke mmoja katika nchi za Mashariki. Uhalali wake kwa hakika ni kipengele kikubwa mno cha kuokoa, pale ambapo idadi ya wanawake wanaopaswa kuolewa inakuwa kubwa kuliko ya wanaume wanaofaa kuoa, kwa sababu kama haki ya kuolewa ya wanawake waliozidi haitatambuliwa na kama wanaume wenye maadili, uwezo wa fedha na afya njema hawataruhusiwa kuwa na mke zaidi ya moja, ngono holela na vimada lazima itajikitia mizizi, na hivyo kuharibu msingi halisi wa ndoa ya mke mmoja.

Katika ulimwengu wa Kiislamu wa Mashariki, mitala ilikuwa inaruhusiwa kwa upande mmoja na kwa upande wa pili vishawishi vya vitendo visivyo vya maadili mema havikuwepo. Kwa hiyo, ndoa halisi za mke mmoja zilistawi na kushitadi katika familia zilizo nyingi. Tabia ya kuwa na vimada kamwe haikupata nafasi. Katika nchi za Mashariki, kamwe haikupata kudaiwa kuwa mwanaume ana asili ya kuwa na wake wengi na kwamba hawezi kukaa na mke mmoja.

Tunaweza tukauliza, mwanaume afanye nini wakati mitala imezuiwa kisheria na kama wasomi wanavyosema, mwanaume ni mwenye asili ya kuwa na wake wengi.

Kwa mujibu wa mawazo ya hawa mabwana jibu liko wazi, kisheria mwanaume awe na mke mmoja lakini kiuhalisia awe na wake wengi. Asiwe na mke zaidi ya mmoja wa halali lakini anaweze akazini na idadi yoyote ya wanawake anaotaka. Vimada ni haki ya asili ya mwanaume. Sio vizuri kumzuia mwanaume kuwa na mwanamke zaidi ya mmoja.

Tunaamini kuwa muda umefika ambapo wasomaji watakuwa wameelewa tatizo. Swali sio kwamba ndoa ipi ni bora, ya mke mmoja au wake wengi. Hapana shaka kwamba ndoa ya mke mmoja ndio ndoa inayochaguliwa na wengi, kwani ndoa ya mke mmoja ina maana maishi ya wawili tu. Utu haupaswi kuchagua kati ya ndoa ya mke mmoja na ya wake wengi.

Tatizo pekee ni kuwa ndoa ya mke mmoja tu, wakati fulani haitekelezeki katika baadhi ya hali za kijamii hasa inapokuwa idadi ya wanawake wanaohitaji kuolewa ni kubwa kuliko idadi ya wanaume wanaoweza kuoa. Ndoa za mke mmoja kutumika kama ndoa pekee ni jambo la kufikirika tu.

Kuna mambo mawili tu ya kuchagua: ama kuitambua rasmi ndoa ya wake wengi au kuhimiza wanaume kuwa na vimada. Katika chaguo la kwanza ni asilimia isiyozidi kumi tu ndio watakaokuwa na mke zaidi ya mmoja na wanawake wote wanaohitaji kuolewa watapata fursa ya kuolewa na kuwa na familia. Katika chaguo la pili, kila mwanamke asiyekuwa na mume wa halali ataweza kufanya ngono na wanaume wengi, na hivyo takribani wanaume wote walioowa kiuhalisia watakuwa na wake wengi.

Hii ndio picha sahihi ya mitala. Lakini wafuasi wa mwenendo wa kizungu hawako tayari kuielezea picha halisi ya tatizo hili. Hawataki kueleza ukweli waziwazi. Kiuhalisia wanatetea utaratibu wa kuwa na vimada. Wanamuona mke wa halali kuwa ni mzigo na kizuizi katika njia yao. Kwao hata mke mmoja ni mwingi mno, achilia mbali wawili, watatu au wanne. Wanajifanya kuwa ni watetezi wa ndoa za mke mmoja, lakini kiuhalisia wanataka ndoa zisiwepo kabisa.

Hila Za Mwanamume Wa Karne Hii

Mwanaume wa karne hii amefanikiwa kumpumbaza mwanamke katika masuala mengi yanayohusiana na haki za kifamilia. Hutumia maneno matamu matamu ya usawa, na uhuru ili kujipunguzia majukumu na kujiogezea fursa za starehe. Lakini kuna masuala machache ambayo ameyafanikisha sana ikiwa ni pamoja na kuingiza imani katika fikra za watu kwamba ndoa za mitala ni mila duni na isiyofaa.

Wakati fulani huwa tunakutana na vitabu vinavyotufanya tushangae ikiwa waandishi wake ni wapumbavu au ni wahuni. Mwandishi mmoja, anasema: Kwa sasa, katika nchi zilizoendelea uhusiano kati ya mume na mke umejengwa juu ya msingi wa haki na majukumu yanayofanana, na kwa sababu hiyo ni vigumu kwa mwanamke kukubali ndoa za mitala za muundo wowote kama ilivyo vigumu kwa mwanaume kuwavumilia waume wenza.

Hatufahamu iwapo hivi ndivyo wanavyolielewa tatizo hili au hawaelewi kuwa tatizo hili limetokana na tatizo la kijamii, ambalo huwatwisha mzigo mkubwa wanaume walioowa na wanawake walioolewa, tatizo ambalo halijapatiwa suluhisho jingine lolote zaidi ya mitala. Kulifumbia macho tatizo halisi na kuanzisha kauli mbiu za: ‘Idumu ndoa ya mke mmoja’ na “Ipotelee mbali ndoa ya wake wengi’ hakuwezi kusaidia chochote.

Je hawajui kwamba mwanamke kuolewa na wanaume wengi si sehemu ya haki za mwanamke wala za mwanaume? Ndoa ya aina hii haishabihiani kwa namna yoyote na mitala.

Ni dhihaka kusema kwamba ni vigumu kwa mwanamke kukubaliana na mitala kama ilivyo vigumu kwa mwanaume kuvumilia waume wenza. Mbali na ukweli kwamba ulinganishaji huu ni wa makosa, inaelekea kwamba mabwana hawa hawajui hali halisi ya ulimwengu wa mwanamke wa leo, kutokana na kumeremeta ambako kumewatia ushamba sana kiasi kwamba mume hutakiwa kuheshimu mapenzi ya nje ya ndoa ya mke wake na pia humtaka astahamili umewenza. Mfumo wa kimagharibi huondoa uingiliaji wowote wa mume katika masuala ya kimapenzi ya mkewe, yaani hutakiwa kutokuwa na wivu. Tunatamani kwamba vijana wetu wangekuwa na elimu kubwa zaidi juu ya kile kinachoendelea katika nchi za Magharibi.

Kwa vile mitala ni matokeo ya tatizo la kijamii na sio silika ya mwanaume, ni wazi kwamba katika jamii ambayo idadi ya wanawake ni sawa na wanume inatarajiwa kuwa mitala haitakuwepo au itakuwa kidogo sana. Lakini haitakuwa sawa hata katika hali hizo kuipiga marufuku mitala. Katazo la kisheria la mitala sio tu kwamba halitoshelezi bali pia sio jambo sahihi.

Kuna baadhi ya mambo ambayo lazima yawepo ili lengo hili liweze kufikiwa. Kwanza, uadilifu wa kijamii lazima uwepo na kila mwanaume awe na hakikisho la kupata ajira ili kila mwanaume anayefaa kuoa aweze kuoa. Sharti la pili ni kuwa kila mwanamke anapaswa kuwa huru kuchagua mume wake na asishinikizwe na walezi au wazazi wake. Ni wazi kuwa mwanamke mwenye fursa ya kuolewa na mwanaume asiyekuwa na mke hataridhia kuolewa na mume mwenye mke. Ni walezi wao ambao huwauza kwa wanaume wenye fedha kwa ajili ya fedha.

Sharti la tatu ni kuwa inapaswa pasiwepo na vishawishi vingi ambavyo huwashawishi hata wanawake wenye waume achilia mbali wasio na waume.

Kama jamii inataka kuleta mageuzi na kubakiza ndoa ya mke mmoja tu inapaswa kuyafikia masharti yote hayo matatu. Vingenevyo katazo la kisheria la kuzuia mitala litachochea tu kuporomoka kwa maadili.

Matatizo Yanayotokana Na Baadhi Ya Wanawake Kukosa Waume.

Kama wanawake wanaohitaji ndoa ni wengi kuliko wanaume wanaohitaji kuoa, katazo la mitala ni hila dhidi ya wanawake na ubinadamu. Sio suala tu la kukandamiza haki za baadhi ya wanawake. Kama ingekuwa hivyo, lingekuwa lilivumiliwa kwa kisasi fulani. Matatizo ambayo jamii inakabiliana nayo kama matokeo ya ulazimishaji wa kisheria wa ndoa ya mke mmoja, ni tishio la hatari kubwa kuliko tatizo jingine lolote, kwani taasisi ya familia ni taasisi takatifu kuliko taasisi nyingine yoyote.

Mwanamke aliyenyimwa haki yake ya asili ni kiumbe mzoefu kwenye hisia zote za viumbe hai kama vile katika hali ya ufukara. ni kiumbe ambaye ana matatizo ya kisaikolojia na hisia. Ni Eva (Hawa) aliye sheheni silaha za kumrubuni mwanaume.

Yeye sio ngano au shayiri ambayo inayozidi humwagwa baharini au kuhifadhiwa stoo kwa ajili ya matumizi ya dharura, ya baadaye. Yeye sio nyumba au chumba ambacho kisipopata mpangaji kinaweza kufungwa. Ni mtu anayeishi. Ni mwanadamu. Ni mwanamke. Ana vipaji vya ajabu.

Akipuuzwa anaweza kuiangamiza jamii. Hawezi kuwa mtazamaji tu wakati wengine wanafurahia maisha. Kunyimwa kwake haki ya ndoa kunaweza kuibua athari mbaya na uovu. Uovu na silika vikiungana pamoja, madhara yake yanaweza kuwa mabaya sana.

Wanawake walionyimwa haki ya kuwa na maisha ya kifamilia, watafanya kila waliwezalo kuwanasa wanaume na kuutumia vyema udhaifu wa wanaume katika jambo hili. Wake watakaowaona waume zao kutokuwa waaminifu watafikiria kulipiza kisasi hivyo nao watapoteza uaminifu wao. Na matokeo yake hayasemeki.

Matokea ya mwisho yamefupishwa katika ripoti mashuhuri ya Kinsey, katika sentensi moja “Wanaume na wanawake wa Kimarekani wamewazidi watu wa mataifa mengine yote kwa kutokuwa waaminifu.”

Tunaweza tukaona kwamba suala haliishii katika ufisadi na upotofu wa wanaume peke yao. Moto huu hatimaye huwakumba hata wanawake wenye waume na familia.

Matokeo Ya Kuwepo Idadi Kubwa Ya Wanawake Wasio Na Waume.

Hali ya kuwepo kwa idadi kubwa ya wanawake wasio na waume imekuwepo katika kipindi chote cha historia ya mwanadamu, lakini matokeo mabaya ya hali hii ambayo huisababishia ugumu jamii, hayajapata kuwa na ukubwa sawa katika jamii mbalimbali. Watu ambao walikuwa wameshikamana zaidi na uchamungu na usafi wa kutozini na ambao walikuwa wanaongozwa na dini tukufu zilizoletwa na mitume walilitatua tatizo hili kwa kutumia mfumo wa ndoa za mitala. Watu wengine ambao hawakuwa wachamungu sana waliitumia hali hii kama fursa ya kujiingiza katika ufuska.

Katika nchi za mashariki, mitala haikuanzishwa na Uislamu na wala kuzuiliwa kwa mitala katika nchi za Magharibi hakukutokana na dini ya Kristo. Kwani hakuna palipoandikwa katika Biblia kuwa hairuhusiwi kuwa na mke zaidi ya mmoja, wala Kristo hakuwahi kutamka kwa kinywa chake kuwa hairuhusiwi kuwa na mke zaidi ya mmoja. Mila hii ilikuwepo katika nchi za Mashariki hata kabla ya Uislamu na ikaja kuruhusiwa na dini za Mashariki. Kwenye Biblia pia kuna mifano tele ya Mitume waliokuwa wakioa mke zaidi ya mmoja.

Ndoa za mke mmoja zimepigwa pigo kubwa na mataifa yaliyoamua kuruhusu ufuska kuliko yale yaliyoruhusu ndoa za wake wengi.

Dk. Muhammad Husayn Haikal, mwandishi wa kitabu, “Life of Muhammad”, baada ya kunukuu Aya kadhaa za Qur’ani juu ya mitala, anasema: Aya hizi zinasaidia na kuimarisha ndoa za mke mmoja. Zinasema kwamba kama una hofu kwamba hutaweza kufanya uadilifu ukiwa na mke zaidi ya mmoja, basi oa mke mmoja tu. Hata hivyo Aya hizi zinahimiza kuwa kufanya uadilifu kwa ukamilifu haiwezekani. Vyoyote vile kwa mtazamo wa ukweli huu, kuna baadhi ya wakati ambapo mitala huwa haiepukiki.

Mtume mwenyewe alioa wake wengi, katika kipindi ambacho idadi kubwa ya wanawake wa Kiislamu ilipoteza waume zao katika vita vya awali vya Uislamu. Je inawezekana kusema kwamba, kufuatia vita, magonjwa ya milipuko na dharura nyinginezo ambazo husababisha vifo vya maelfu na wakati fulani mamilioni ya watu, ni bora kubaki na ndoa ya mke mmoja kuliko mitala kama hali pekee pamoja na sharti la kufanya uadilifu baina ya wake? Je watu wa Magharibi wanaweza wakadai kuwa baada ya vita vya dunia, sheria ya ndoa ya mke mmoja imeongezwa nguvu katika njia ile ile ambayo kwamba kwa sasa imebakia jina tu?

Dosari Na Kasoro Za Mitala

Maisha ya ndoa yenye furaha hutegemea, uaminifu, uvumilivu, kujitolea na umoja. Mambo yote haya huhatarishwa na ndoa za wake wengi (mitala). Mbali na mazingira ya wivu kati ya wake na watoto katika ndoa za mitala, majukumu ya mume huwa ni mazito sana na yanayovunja mgongo kiasi kwamba sio burudani kuyabeba.

Wanaume walio wengi ambao wana furaha na wameridhika na mitala, ni wale ambao katika hali halisi hukwepa majukumu yao ya kisheria na kimaadili. Humjali mke mmoja tu na huwapuuza wengine, ambao kwa mujibu wa Qur’ani huachwa wamening’inia. Kile ambacho watu wa aina hii wanakiita mitala, kiuhalisia ni ndoa za mke mmoja zilizochanganyika na ubabe, ukatili na dhulma ya jinai. Kuna methali iliyoenea sana miongoni mwa watu wa kawaida isemayo: “Mungu Mmoja, Mke Mmoja”.

Kilichosemwa ni imani ya watu walio wengi na tukilipima tatizo kwa kutumia furaha ya mtu mmoja mmoja, ni sahihi. Kanuni ya mke mmoja, hata kama haitekelezwi na wanaume wote lakini ndiyo inayotumiwa na wanaume walio wengi.

Kama mtu anafikiri kuwa mitala, pamoja na majukumu yake yote ya kisheria na kiuchumi, ni kitanda cha maua waridi, basi amekosea sana. Kwa upande wa furaha na starehe binafsi, ndoa za mke mmoja ndio zinafaa zaidi.

Tathmini Sahihi

Hata hivyo, tathmini sahihi ya mfumo wa mitala, ambao unatokana na mahitaji binafsi na ya kijamii, haiwezi ikafanywa kwa kulinganisha na ndoa za mke mmoja. Namna sahihi ya kutathmini mfumo huu ni kuzingatia sababu zinazousababisha, ili kuangalia ni madhara gani mabaya yatafuatia, na wakati huo huo tutazame dosari na kasoro za mfumo wa mitala. Ni baada tu ya kupima faida na hasara zote za mfumo huu ndio tutafikia kwenye hitimisho sahihi. Ili kufafanua nukta hii, hebu tuutazame mfano huu.

Tukiitazama sheria ya kulazimisha watu kwenda jeshini, ni wazi kwamba kwa upande wa maslahi binafsi, sheria hii sio nzuri. Ingekuwa vizuri zaidi kama sheria hii isingekuwepo, na hakuna mpendwa wa familia ambaye angeondolewa kwenye familia yake (na kupelekwa jeshini) na wakati fulani kupelekwa vitani.

Lakini hii sio tathmini sahihi ya jambo hili pamoja na ubaya wa mtoto kutenganishwa na familia yake, tunapaswa pia kutazama mahitaji ya kiulinzi ya nchi. Tukifanya hivyo tutaona kwamba ni jambo la maana kabisa kuweka idadi ya kutosha ya raia iwekwe tayari kwa ajili ya ulinzi wa nchi na familia zao zinapaswa kustahamili usumbufu na matatizo yanayosababishwa na sheria ya kulazimisha watu kuingia jeshini.

Awali tulielezea mahitaji ya mtu mmoja mmoja na ya kijamii ambayo wakati fulani huhalalisha mitala. Sasa kuandaa mazingira ya hukumu ya jumla, hebu tujadili dosari na kasoro za mfumo huu. Tunakubali kwamba mfumo huu una dosari fulani fulani, lakini hatuamini kwamba yote yaliyosemwa dhidi ya mitala ni sahihi. Tunapendekeza kwamba tuzijadili dosari zake katika mitazamo mbalimbali.

Katika Mtazamo Wa Kisaikolojia

Mahusiano ya unyumba hayaishii katika ushirikiano wa kimwili na kifedha. Kama ingekuwa hivyo, ingekuwa rahisi kuhalalisha mitala, kwani fedha na matendo ya ndoa yanagawanyika baina ya watu wengi, kila mmoja anapata gawio lake.

Msingi wa mahusiano ya unyumba ni wa kimhemko na kisaikolojia. Yamejengwa juu ya vitu kama upendo, mihemko na hisia. Maisha ya ndoa yana maana ya muungano wa mioyo. Kama ilivyo kwa vitu vyote dhahania (visivyoonekana), upendo na hisia havigawanyiki. Haviwezi kugawiwa miongoni, mwa watu wengi wala haiwezekani kila anayehitaji akapewa kijisehemu maalumu cha upendo na hisia hizo. Moyo hauwezi ukagawanywa baina ya watu wawili. Upendo na ibada vinakwenda pamoja. Havikubali mpinzani. Upendo hauwezi ukapimwa wala kugawiwa kama ngano au shayiri. Aidha, hisia haziwezi kudhibitiwa. Moyo humtawala mwanaume, mwanaume hautawali moyo. Roho ya ndoa, yaani, kipengele chake cha kibinadamu ambacho hutofautisha mahusiano kati ya wanaadamu na wanyama haigawanyiki wala haiwezi kudhibitiwa. Kwa hiyo, mitala haipaswi kuruhusiwa.

Kwa imani yetu, maelezo haya yametiwa chumvi. Ni kweli kwamba mihemko na hisia ni roho ya ndoa. Pia ni kweli kwamba hisia hazidhibitiki. Lakini ni mawazo halisi ya kindoto, bali pia ni hoja ya uwongo kusema hisia hazigawanyiki.

Sio suala la kugawanya hisia kama vile mali au fedha. Ni suala la uwezo wa kiakili wa mwanaume, ambao ni mdogo kiasi cha kushindwa kumudu mahusiano ya watu wawili. Baba mwenye watoto kumi huwapenda wote na hujitolea mhanga kwa ajili yao.

Lakini suala moja liko wazi. Upendo hauwezi kuwa mkubwa sana katika wake wengi kama ndoa ya mke mmoja. Upendo mkubwa, haukubaliani na wingi, lakini pia haukubaliani na hoja za kiakili.

Russel katika kitabu chake, “Marriage and Morality” anasema kwamba watu wengi leo hii wanayaona mapenzi kama ubadilishanaji mzuri wa hisia. Hoja hii peke yake, bila kujali hoja nyingine zote, inatosheleza kuzishutumu ndoa za mitala.

Kama ni suala la ubadilishanaji mzuri wa hisia tu, tunashangaa kwa nini ubadilishanaji huu uhodhiwe. Baba mwenye watoto huwapenda wanaye wote nao wote humpenda. Je huu sio ubadilishanaji wa haki wa hisia? Hata baba anapokuwa na watoto wengi, upendo wa baba kwa kila mtoto, mara zote huwa ni mkubwa kuliko upendo wa kila mtoto kwa baba yao.

Sehemu inayoshangaza zaidi katika kauli hiyo ni kwamba, imetengenezwa na mtu ambaye anawashauri wanaume kuyaheshimu mapenzi ya nje ya wake zao na kwamba wasiwaingilie.

Pia anawapa ushauri kama huo wanawake walioolewa. Je bado anaamini kuwa ubadilishanaji wa hisia kati ya mume na mke utakuwa wa haki?

Kutoka Katika Mtazamo Wa Tabia

Katika ndoa za mitala, mahusiano baina ya wake wenza huwa ni balaa tupu. Kwa kawaida mwanamke humuona mke mwenzake kama adui yake mkubwa kuliko wote. Kuwa na wake wengi mara nyingi husababisha magomvi baina yao na wakati fulani dhidi ya mume wao. Huzusha uovu na huibadili hali ya hewa ya familia, kutoka katika hali ya uaminifu na utulivu iliyotarajiwa na kuwa uwanja halisi wa vita. Uadui na uhasama ambao huwepo baina ya akina mama huhamia mpaka kwa watoto na kambi mbili au zaidi huundwa. Hali ya hewa ya familia, badala ya kuwa shule ya awali ya kuwafundisha watoto maadili, hubadilika na kuwa shule ya magomvi na tabia zisizo za kibinadamu.

Hapana shaka kwamba ndoa za mitala zina athari hizi zote mbovu. Lakini nukta moja haipaswi kusahaulika. Tunapaswa kuona kama hizi ni athari za asili za mitala au zinatokana na tabia isiyofaa ya mume na mke wa pili. Tunaamini kwamba athari mbaya zilizo nyingi hazitokani na matokeo ya moja kwa moja ya mitala, bali zinatokana na utekelezaji usiofaa wa mitala.

Jaalia mume na mke wanaishi pamoja na wanaishi maisha ya kawaida. Kisha mume anakuja na mwanamke mwingine ambaye anahamishia upendo wote kwake. Baada ya maelewano ya siri baina ya wawili, mke wa pili huvamia nyumba na huutumia vibaya upendo wa mume, na huyatishia mamlaka ya mke wa kwanza. Tunaweza tukaelewa atakachokifanya mke wa kwanza. Hakuna kitu ambacho huwa kinamuudhi na kumkera mwanamke kama kitendo cha kudharauliwa na mume wake. Kushindwa kuurejesha upendo wa mume wake ni kufeli kukubwa kabisa kwa upande wa mke. Mume anapofanya jeuri na uasherati na mke wa pili ndio hubaki mwenye mamlaka pekee, hapa haitarajiwi mke wa kwanza awe na subira.

Lakini mambo yatakuwa tofauti na migogoro ya ndani itapungua sana ikiwa mke wa kwanza anajua kuwa mume wake ana haki ya kuwa na mke wa pili na kwamba hajamchoka. Mume hapaswi kuonyesha jeuri wala kujishughulisha na ngono na mke wa pili zaidi kuliko kujali hisia za mke wa kwanza. Baada ya kuwa na mke wa pili anafaa kuwa mpole zaidi kwa mke wake wa kwanza na kujali hisia zake. Mke wa pili anapaswa pia kujua kuwa mke wa kwanza pia ana haki zinazopaswa kuheshimiwa. Kwa kifupi pande zote zinazohusika, zinapaswa kukumbuka kuwa zimechukua hatua katika kutatua tatizo la kijamii.

Sheria ya mitala ni suluhisho endelevu la tatizo la kijamii na imezingatia maslahi makubwa na mapana zaidi ya jamii. Wale wanaoitekeleza wanapaswa kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri na wawe wamefundishwa vizuri mwenendo wa Kiislamu. Uzoefu unaonyesha kwamba ikiwa mume sio muasheati na sio mjeuri na mke wake akishawishika kuwa mume wake anahitaji mke wa pili, yeye mwenyewe mke wa kwanza hufanya maadalizi ya ndoa ya mke wa pili. Katika hali hii matatizo huwa hayaibuki, kwani matatizo mengi hutokana na tabia mbaya za wanaume.

Kutoka Katika Mtazamo Wa Kimaadili.

Inadaiwa kwamba mitala maana yake ni kupenda sana ngono. Maadili hutaka vitendo vya ngono vipunguzwe, kwani maumbile ya mwanaume yapo katika hali ambayo kwa kadri anavyofanya ngono ndivyo hamu ya kufanya ngono zaidi inavyoongezeka.

Montague katika kitabu chake, “Spirit of Laws”, alipokuwa akijadili suala la mitala, anasema: “Mfalme wa Morocco, katika kasri yake ana wake wa rangi zote, weupe, wa njano na weusi. Hata kama mwanaume huyu angekuwa na wanawake mara mbili ya hawa alionao bado angetaka wake zaidi. Kama ukusanyaji wa dhahabu na fedha zaidi na zaidi unavyoongeza tamaa zaidi, hali kadhalika kuoa wake wengi hukuza tabia mbaya, na zisizo za asili za kufanya mapenzi, kwani katika suala la ngono, kila kitendo kinachovuka mipaka huhimiza upotofu. Fujo zilipoibuka Istanbul, hakuna hata mwanamke mmoja aliyekutwa katika kasri la mtawala kwa sababu alijihusisha na mapenzi yasiyo ya asili (liwati).

Pingamizi hili linaweza kutazamwa katika pande mbili. Kwanza imedaiwa kuwa tendo la ndoa ni makruhu (linachukiza) mbele ya maadili safi na kwamba matamanio ya ngono yanapaswa kudhibitiwa kwa kadri inavyowezekana. Pili imedaiwa kuwa maumbile ya mwanamume ni kwamba kadri anavyofanya mapenzi zaidi ndivyo anavyopata hamu ya ngono zaidi.

Kuhusiana na hoja ya kwanza, tunaweza kusema kuwa inawakilisha fikra potofu. Inahubiriwa sana miongoni mwa wakristo, wahindu, budha na wengineo kuwa maadili maana yake ni kukaa bila kuoa au kuolewa. Kwa mtazamo wa Uislamu sio sahihi kusema kwamba kwa kadri mtu anavyofanya mapenzi kidogo (katika ndoa) ndivyo anavyokuwa na maadili safi zaidi. (Pengine kwa mujibu wa nadharia hii, maadili timilifu zaidi ina maana ni kutofanya mapenzi kabisa). Ni ngono zilizovuka mipaka tu, ndizo zinazochukiza mbele ya maadili ya Kiislamu.

Ili kuyakinisha kama ndoa za mitala maana yake ni kufanya ngono kupita kiasi, hebu tuangalie kama kwa maumbile mwanaume ni mwenye asili ya kuoa mke mmoja au la.

Kama ilivyoelezwa huko nyuma hakuna anayeamini kuwa mwanaume ni mwenye asili ya kuwa na mke mmoja kwa asilimia zote wala kwamba mitala ni kitendo cha upotofu. Kinyume chake wanasosholojia wengi wana maoni kwamba mwanaume ni mwenye asili ya kuwa na wake wengi na kwamba ndoa za mke mmoja ni kinyume na maumbile yake kama tu ilivyo kwa useja (kuishi bila kuoa wala kuolewa).

Ingawa hatuamini kuwa mwanaume ni mwenye asili ya kuwa na wake wengi, pia hatuamini kuwa ana asili ya kuwa na mke mmoja na kwamba mitala sio mwenendo wa asili na kwamba ni aina ya upotofu kama liwati.

Watu wa aina ya Montesquieu, ambao wanaziona ndoa za mitala kuwa ni sawa na uasherati, wana fikra ya ‘nyumba za wake’ – harems – vichwani mwao. Wanafikiri kwamba Uislamu, kwa kuruhusu ndoa za wake wengi, unataka kutoa kisingizio cha kuyalinda majumba ya wake ya makhalifa wa Bani Abbas na masultani wa Ottoman. Lakini, kwa kusema ukweli, Uislamu unapingana na jambo hilo kabisa. Masharti yaliyowekwa na Uislamu juu ya suala la wake wengi ni magumu kiasi kwamba uwezekano wa kuwepo na uasherati huondolewa kabisa.

Kuhusiana na nukta ya pili kwamba tamaa ya ngono huongezeka kwa kadri tamaa hizo zinavyokidhiwa, na kwamba kwa kadri zinavyokandamizwa ndivyo zinavyotulia, hoja hii inapingana moja kwa moja na nadharia mashuhuri ya Freudi.

Kwa mujibu wa wafuasi wa Freud, tamaa za kisilika hutulia zikikidhiwa, lakini zikikandamizwa, hulipuka. Hii ndio sababu wafuasi wa nadharia hii wanatetea kuwepo kwa uhuru kamili na kuondolewa kwa vikwazo vyote katika suala la ngono. Natamani Montesquieu angekuwa hai leo hii ili aone jinsi nadharia yake inavyokejeliwa na wafuasi wa nadharia ya Freud.

Kwa maoni ya Uislamu, nadharia zote ni potofu. Maumbile ya mwanadamu yamejiwekea sheria na mipaka yake ambayo lazima itambuliwe. Huwa na hisia kali katika hali zote kwa matokeo ya ufukura na halikadhalika uhru usio na mipaka.

Muhimu ni kuwa, ndoa za mitala sio kinyume na maadili wala haziharibu amani ya kiroho, kama Montesquuieu na wenzake wanavyodai, wala sio kinyume na maumbile ya mwanadamu, kuridhika na mke mmoja au wake zaidi ya mmoja wa halali kama inavyodaiwa na wafuasi wa nadharia ya Freud.

Kutoka Katika Mtazamo Wa Kisheria

Kwa asili ya mkataba wa ndoa, mume na mke kila mmoja ni mali ya mwenzake na kila mmoja wao ana haki ya kumfurahia mwenzake. Kutokana na faida za kiunyumba, mkataba wa ndoa huunda kitu kama haki miliki. Katika mitala ni mke wa kwanza ambaye ana stahili ya awali kwenye manufaa ya unyumba, na hivyo mkataba wowote na mwanamke mwingine ni batili, kwani mali zilizoko chini ya mkataba, kama manufaa ya unyumba yanavyoweza kuitwa, tayari yameshauzwa kwa mke wa kwanza. Hivyo hakuna makubaliano yoyote ya faida hizo za unyumba yanayoweza kufanywa bila idhini ya mke wa kwanza. Hivyo, kama mitala inaruhusiwa, lazima iwe ni kwa idhini ya mke wa kwanza. Anapaswa kuwa na haki ya kuamua iwapo mume wake ana haki au hana haki ya kuoa mke mwingine.

Hii ina maana kuwa kuoa mke wa pili, wa tatu au wa nne ni kana kwamba mtu alimuuzia mtu mwingine mali yake na kisha akaiuza tena kwa mteja wa pili, wa tatu na wa nne. Uhalali wa makubaliano unategemeana na idhini ya mnunuzi wa kwanza, wa pili na wa tatu sawia. Mchuuzi akiwauzia wanunuzi wengine bila idhini hiyo, anastahili kushitakiwa.

Pingamizi hili lemewekwa juu ya dhana kwamba asili ya kisheria ya ndoa ni ile ya kubadilishana faida, na kwamba mume na mke kila mmoja anamiliki faida za unyumba zinazotokana na mwenzake, ingawa dhana hii haifai, kwa sasa hatutaki kuibishia. Tujaalie kuwa ilivyoelezwa ndio hivyo hivyo ilivyo. Lakini pingamizi hili linaweza kuwa halali tu ikiwa mume atachukua mke mwingine kwa burudani tu.

Ni wazi kwamba kama ikikubaliwa kuwa asili ya kisheria ya ndoa ni ile ya kubadilishana faida za unyumba, ndoa za wake wengi (mitala) hazitakubalika tu ikiwa mke anakidhi mahitaji yote ya halali ya mume wake. Lakini ikiwa kutakuwa na sababu yoyote inayokwamisha upatikanaji wa mahitaji ya mume kutoka kwa mkewe basi pingamizi hilo huwa batili. Kwa mfano ikiwa mke ni tasa au amefikia umri wa kuacha kuzaa na mume anahitaji mtoto au mke ni mgonjwa na hawezi kumudu kujamiiana, haki ya mke haitakuwa kizuizi cha mume kuoa mke au wake wengine.

Hukumu inakuwa hivi kama mitala ni mahitaji binafsi ya mume. Lakini kama ni mahitajio ya jamii, kwa mfano ikiwa wanawake ni wengi kuliko wanaume au kama jamii inahitaji watu wengi, zaidi, basi hapa mambo huwa tofauti. Katika hali hiyo, ndoa za wake wengi huwa ni wajibu unaopaswa kutekelezwa na idadi ya kutosha ya wanaume.

Ni jukumu linalopaswa kutekelezwa ili kuiokoa jamii dhidi ya ufisadi na umalaya au ili kuongeza idadi ya watu katika jamii. Linapokuwa ni suala la jukumu la kijamii, ni wazi kwamba hapa ruhusa ya mke huwa haitajiki. Jaalia katika jamii idadi ya wanawake ni kubwa kuliko ya wanaume au jamii inahitaji idadi kubwa zaidi ya watu, basi hapa jukumu la kijamii huenda kwa wanaume na wanawake wote walio na ndoa, jukumu ambalo linapaswa kufanywa na idadi yao ya kutosha kwa moyo wa kujitolea. Hii inafanana sana na sheria ya kuingizwa jeshini kwa nguvu. Ulinzi wa nchi hupeleka jukumu kwa familia zote ili ziwapeleke wapendwa wao vitani kwa ajili ya jamii. Katika hali hizi huwa hakuna suala la idihini kutoka katika pande zinazohusika, wale wanaoshikilia kuwa uadilifu unataka mitala itegemee idhini ya mke wa kwanza wanaliangalia suala hili kwa mtazamo finyu.

Wanafikiri kwamba kila mume anapoongeza mke huwa anafanya hivyo kwa ajili ya raha zake na kutaka kubadilibadili wanawake. Wanasahau kwamba kunaweza kuwepo matatizo mengine ya mtu mmoja na jamii pia. Kimsingi ndoa za wake wengi hazipaswi kukubaliwa hata kwa idhini ya mke wa kwanza, ikiwa hakuna mahitaji ya mtu mmoja mmoja au ya kijamii.

Kwa Mtazamo Wa Kifalsafa

Sheria ya mitala inachukiza mbele ya kanuni ya usawa kati ya mwanaume na mwanamke kama wanaadamu. Kwa kuwa mwanaume na mwanamke wote wana haki sawa, ama wote waruhusiwe kuwa na mwenzi zaidi ya mmoja au wote wakatazwe. Ni ubaguzi wa wazi kumruhusu mwanaume kuwa na wake wengi huku wanawake wakizuiwa kuwa na waume wengi. Kumruhusu mwanaume kuwa na wake mpaka wanne. Kunamaanisha kuwa thamani ya mwanamke ni robo ya thamani ya mwanaume. Hili ni tusi kubwa kwa mwanamke. Hali iko hivi hivi hata katika mfumo wa Uislamu wa mirathi na ushahidi. Katika suala la kutoa ushahidi, wanawake wawili wanahesabiwa kuwa ni sawa na mwanaume mmoja.

Hili ni pingamizi lilichoka kuliko yote. Inaelekea kwamba wakosoaji hawa hawajazingatia mahitaji ya mtu mmoja mmoja na yale ya kijamii yanayosababisha mitala. Wanafikiri kuwa ni suala la mvuto wa kimapenzi tu. Hivyo mwanaume na mwanamke wanapaswa kutendewa kwa usawa. Tayari tumeshaeleza mazingira ambayo yakiwepo kunakuwa na uhalali wa mitala. Pia tumeonyesha hali ambazo zikiwepo jukumu la wanawake wasio na waume huenda kwa wanaume waliooa na wanawake walioolewa. Hivyo hakuna haja ya kulirudia swali hili tena.

Inatosha kusema kwamba mafundisho ya Uislamu katika masuala ya mitala, mirathi na ushahidi hayajamfanyia ukatili wala dharau yoyote mwanamke katika haki zake, na kwamba Uislamu ungekuwa unawabagua wanaume na wanawake kama wanaadamu, ungekuwa na mitazamo sare sare katika masuala yoyote.

Katika suala la mirathi, Uislamu usingekuwa umeamuru nusu ya gawio katika baadhi ya hali, na gawio kamili katika baadhi ya hali. Halikadhalika katika suala la ushahidi kusingekuwa na kanuni tofauti katika masuala tofauti. Yote hii inaonyesha kwamba Uislamu una falsafa nyingine, sio kumbagua au kumdhulumu mwanamke.

Tayari tumeshajadili suala, la mirathi katika sura zilizopita. Pia katika maeneo mengine tumeonyesha kuwa kwa mtazamo wa Uislamu, usawa kati ya mwanaume na mwanamke kama binadamu ni sehemu ya haki za msingi za binadamu. Hata hivyo, tunapojadili haki za kifamilia, Uislamu umezingatia mambo mengine pia ambayo ni muhimu kuliko usawa.

Mchango Wa Uislamu Katika Uboreshaji Wa Mitala.

Uislamu imma haukuanzisha ndoa za mitala (kwani zilikuwepo kabla ya Uislamu), wala Uislamu haukuzipiga marufuku, kwani hapakuwepo suluhisho mbadala kwa baadhi ya matatizo ya kijamii. Uislamu ulichokifanya ilikuwa ni kuiboresha tu hii desturi ya kale.

Mipaka (Ya Idadi).

Kabla ya Uislamu mtu alikuwa na uwezo wa kuwa na idadi isiyo na mipaka ya wake na aliweza kuunda (harem) ‘nyumba ya wake.’ Uislamu uliweka kikomo. Haukumruhusu yeyote kuwa na wake zaidi ya wanne. Wale waliokuwa na wake zaidi ya wanne waliposilimu walipaswa kuwaacha wale waliozidi.

Tunakutana na majina ya watu wengi wa aina hii katika historia ya Uislamu. Mtu mmoja aliyeitwa Ghaylan bin Aslmah alikuwa na wake kumi. Mtu mwingine aliyeitwa Nawfal bin Muawiyah alikuwa na wake watano. Mtume aliwaamuru kuwaacha wake zao waliozidi ile idadi iliyoruhusiwa.

Hadithi za Kishia zinasimulia kuwa katika enzi za Imam Sadiq (as) Mzoroastria alisilimu. Alikuwa na wake saba. Imam aliulizwa yule mtu afanye nini na hiyo idadi iliyozidi? Imam akasema lazima awaache watatu.

Uadilifu Na Kuwatendea Kwa Usawa.

Mageuzi mengine yaliyoletwa na Uislamu ilikuwa ni sharti la kuwatendea kwa usawa wake wote. Uislamu hauruhusu ubaguzi wowote baina ya wake au watoto wao. Qur’ani Tukufu wazi wazi inasema,

فَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا تَعْدِلُوا فَوَاحِدَةً

“Ikiwa mna hofu kuwa hamtatenda uadilifu basi oeni mmoja tu.” (Suratul Nisaa, 4:3).

Kabla ya Uislamu watu walikuwa hawatendi uadilifu kwa wake zao wala watoto wao. Tumeshanukuu maoni ya Christenson na wengine ambao wamesema kwamba katika kipindi cha Sassania, mitala ilikuwa ni mila iliyozoeleka nchini Iran. Mke mmoja au zaidi waliitwa wake vipenzi na walipata haki zote na wengine walijulikana kama wake wafanyakazi na walikuwa na haki chache zaidi za kisheria. Ni watoto wa kiume tu wa wake wafanyakazi walioingizwa katika ukoo wa baba.

Uislamu ulipiga marufuku mila na desturi zote hizi. Hauruhusu mke yeyote au watoto wake kuonekana kuwa ni wa cheo cha chini kuliko wa mke mwingine au watoto wengine wa mume wake.

Will Durant katika kitabu chake, History of Culture, juz.1 amesema, “Mtu alipokusanya mali alihofu kuwa ikiwa itagawiwa kwa watoto wake wote, kila mmoja angepata sehemu ndogo tu. Hivyo alihisi kuwa aweke tofauti kati ya mke wake kipenzi na wale wengine ili kuwawezesha watoto wa mke kipenzi tu ndio warithi mali yake.”

Hii inaonyesha kuwa enzi za kale ubaguzi kati ya wake na kati ya watoto wao ulikuwa jambo la kawaida. Hata hivyo cha kushangaza ni kuwa Will Durant anaongeza kwa kusema, “Mpaka hivi karibuni hali imekuwa hivi huko Asia. Popepole mke halisi alichukua nafasi ya mke pekee. Wake wengine ama walitoweka au walikuwa wake wa siri”.

Will Durant hakuujuwa ukweli au hakutaka kufanya hivyo, kuwa karne 14 zilizopita Uislamu ulitokomeza ubaguzi kati ya watoto, kuwa na mke mmoja halisi na vimada wengine wengi wa siri ni mila ya Kizungu sio ya Kiasia. Ni hivi karibuni tu imeanza kujipenyeza Asia.

Hata hivyo mageuzi ya pili ambayo Uislamu uliyaleta katika ndoa za mitala ilikuwa ni kupiga marufuku ubaguzi baina ya wake na watoto wao. Upendeleo wa aina yoyote hauruhusiwi. Mafakihi wote wanakubaliana juu ya hili. Ni matapo machache tu ya kifakihi ambayo yamezitafsiri haki za wanawake katika namna ambayo inaashiria upendeleo. Lakini ni ukweli usiopingika kuwa tafsiri hii inapingana na tafsiri sahihi ya Qur’ani.

Mtukufu Mtume ameripotiwa na wote, Shia na Sunni kuwa amesema: “Yule mwenye wake wawili lakini akawa hawatendei kwa usawa na akaonyesha kumpendelea mmoja wao atafufuliwa siku ya kiama hali ya kuwa upande mmoja wa mwili wake unamvutia chini. Hatimaye atapelekwa Motoni.”

Haki ni sifa kubwa kuliko zote za maadili. Kuweka sharti la haki na kuwatendea sawa inamaanisha kuwa mume anapaswa kuwa na sifa za juu kabisa za uadilifu. Kwa kuwa hisia za mwanaume kwa wake zake haziko sawa, kuzingatia uadilifu na kujiepusha na ubaguzi ni moja ya majukumu yanayohitaji jitihada kubwa.

Wote tunajua kuwa Mtukufu Mtume, katika miaka kumi ya mwisho ya uhai wake, yaani katika kipindi alipokuwa akiishi Madina alioa wake wengi. Hiki kilikuwa ni kipindi cha vita vya Kiislamu (Jihad) na wakati huo idadi ya wanawake ambao hawakuwa na watu wa kuwatazama ilikuwa kubwa kabisa. Wengi wa wake za Mtume walikuwa wazee na wajane. Wengi wao walikuwa na watoto wa waume zao wa zamani.1

Mwanamwali pekee aliyemuoa na Aisha, ambaye alikuwa akisema mara kwa mara kwa kujivuna kwamba yeye ndiye mwanamke pekee ambaye hakuna mume mwingine mbali na Mtume aliyewahi kumgusa kwamwe.

Mtukufu Mtume mara zote alikuwa akiwatendea wake zake kwa usawa na uadilifu na hakubagua kati yao. Urwah bin Zubayr alikuwa ni mtoto wa dada yake na Aisha. Alimuuliza mama yake mdogo juu ya jinsi Mtume alivyokuwa akiwatendea wake zake. Aisha alisema kuwa alikuwa akiwatendea kwa uadilifu na usawa kabisa. Kamwe hakuwa akimpendelea yeyote miongoni mwao. Kila siku alikuwa akimtembelea kila mke na kumuuliza juu ya afya yake n.k. Kila siku moja alilala kwa mke mmoja. Ikiwa alitaka kulala kwa mke ambaye sio zamu yake alikuwa akimuomba ruhusa yule mke ambaye ndiyo zamu yake (mwenye zamu). Alikuwa akienda kama akiruhusiwa vinginevyo asiporuhusiwa alikuwa haendi. Aisha mwenyewe anasema kuwa alikuwa anakataa kutoa ruhusa pindi alipokuwa akiombwa.

Hata katika maradhi yake ya mwisho yaliyosababisha kifo chake na alipokuwa dhaifu kiasi cha kushindwa kutembea, bado Mtume alikuwa anazingatia uadilifu kwa kuwatendea kwa usawa wake zake wote. Kitanda chake kilihamishwa kutoka chumba kimoja kwenda kingine kila siku. Hatimaye, siku moja aliwaita wake zake wote na kuwaomba akae kwenye chumba kimoja. Baada ya kumruhusu alikaa kwenye chumba cha Aisha kwa vile chumba chake kilikuwa karibu zaidi na msikiti.

Wakati alipokuwa na wake wawili, Imam Ali (a.s) alikuwa anazingatia uadilifu kwa kiasi kuwa hata udhu alikuwa anachukulia kwa yule mke mwenye zamu.

Uislamu umeweka umuhimu mkubwa kwenye uadilifu na usawa katika kuwatendea wake kiasi kwamba haumruhusu mwanaume kuingia mkataba wa ndoa na mke wa pili kwa sharti kuwa mume atampa mke wa pili upendeleo katika maisha yao. Hii ina maana kuwa ni wajibu wa lazima kwa mume kuwatendea kwa usawa na uadilifu wake zake na kwamba hawezi kulikwepa jukumu hili kwa kuingia mkataba kabla na mke yeyote kuwa yeye atapendelewa (kama sharti la lazima la ndoa).

Mke wa pili anachoweza kukifanya ni kwa hiari kusamehe baadhi ya haki zake akipenda kufanya hivyo kwa sababu za msingi alizonazo. Lakini sharti hili haliwezi kuwekwa kwenye mkataba wa ndoa. Halikadhalika mke wa kwanza anaweza kusamehe baadhi ya haki zake kwa hiari yake na kwa sababu maalum, lakini hawezi kuzikataa moja kwa moja.

Wakati fulani Imam Baqir (a.s) aliulizwa kuwa inawezekana kuamriwa kwa makubaliano na mmoja wa wake kuwa mume angemtembelea mmoja wa wake zake (huyo aliyetoa ruhusa) mara moja kwa wiki au mara moja kwa mwezi au kwamba gharama za matunzo za mmoja wake huyo aliyetoa ruhusa zitakuwa pungufu za zile anazopata mwenzake. Imam alisema kuwa hilo halikubaliki hata kwa ridhaa ya huyo mke anayataka kusamehe haki zake. Kwa asili ya ndoa kila mke anastahili haki zote za unyumba. Anachoweza kukifanya ni kusamehe baadhi au haki zake zote iwe kwa kumridhisha mume wake au ka sababu nyinginezo.

Kwa masharti haya magumu mitala huwa ni jukumu badala ya raha na burudani. Raha na uasherati vinawezekana tu katika mazingira ya uhuru kamili wa kukidhi matamanio yao. Lakini panapokuwa panahitajika nidhamu, uadilifu na majukumu (wajibu), hapawezi kuwa na nafasi ya uzinifu.

Wale wanaojiingiza katika uasherati kwa kisingizio cha mitala wanaitumia vibaya sheria ya Kiislamu na jamii ina kila haki ya kuwaita wajieleze na kuwaadhibu.

Wasiwasi Wa Kutotenda Uadilifu.

Kuwa wakweli, lazima tukiri kuwa idadi ya wale wanaotenda uadilifu na kuzingatia masharti yote yaliyowekwa na Uislamu juu ya mitala ni ndogo sana. Kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu, ikiwa mtu atahofia kuwa akitumia maji yatamdhuru basi hatakiwi kutawadha kwa maji, na kama atakuwa na wasiwasi kuwa akifunga (Saumu) atadhurika basi anapaswa asifunge. Unakutana na watu wengi wanaouliza kama wachukue au wasichukue udhu (kwa maji), au kama wafunge au wasifunge, kwani wana wasiwasi kuwa kutawadha (kwa maji) na kufunga saumu kutawadhuru. Maswali kama haya ni sawa kabisa. Watu kama hao hawapaswi kutawadha wala kufunga.

Lakini Qur’ani Tukufu inaeleza wazi wazi kuwa kama mnahofu kuwa hamtatenda uadilifu basi mnapaswa kuoa mke mmoja tu. Lakini bado hakuna mtu hata mmoja anaweza kusema kuwa ana wasiwasi kuwa hawezi kuwatendea wake zake wawili kwa usawa, na anaweza kuuliza kuwa katika hali hii awe na mke wa pili au asiwe naye. Ni dhahiri kuwa baadhi ya watu wanajua fika kuwa hawataweza kufanya uadilifu, lakini bado wana wake wengi. Wanafanya hivyo chini ya kivuli cha sheria ya Kiislamu. Hawa ndio watu wanaochafua jina la Uislamu kwa matendo yao yasiyofaa.

Nyumba Za Wake (Harem).

Sababu nyingine inayofanya Uislamu ushutumiwe kwa mitala ni mfumo wa mwanaume kumiliki nyumba ya wake uliokuwa ukitumiwa na makhalifa na masultani waliopita. Baadhi ya waandishi wa Kikristo na Wamisionari wamezielezea ndoa za mitala katika Uislamu kuwa ni sawa na mfumo wa ‘nyumba ya wake’ ambao umejaa mambo ya aibu na ukatili.

Kwa bahati mbaya baadhi ya waandishi wetu, kama kasuku, wanarudia yale yale mawazo yaliyoelezwa na wazungu, bila ulazima wanahusisha ndoa za mitala na nyumba hizi. Hawana uwezo wa kutosha wa kufikiri wenyewe kwa uhuru ili kutofautisha mambo haya mawili.

Masharti Mengine.

Mbali na sharti la uadilifu na usawa kuna masharti mengine pia ambayo mume anapaswa kuyatimiza. Wote tunajua kuwa mke ana haki nyingi za kifedha na nyinginezo ambazo mume anapaswa kuzitekeleza. Mume ana haki ya kuwa na mke zaidi ya mmoja ikiwa uwezo wa kifedha unamruhusu kufanya hivyo. Uwezo wa kifedha ni sharti la msingi hata kwa ndoa ya mke mmoja. hata hivyo hatutalijadili zaidi hili kwa sasa.

Uwezo wa kiafya na urijali ni sharti jingine la msingi. Imesimuliwa katika Alkafi na AlWasail kuwa Imam Sadiq amesema kuwa ikiwa mtu atakusanya wake wengi, wakati hana uwezo wa kuwaridhisha (kimapenzi) wote, atabeba jukumu la madhambi yoyote watakayofanya.

Historia ya ‘nyumba za wanawake’ inasimulia visa vya wanawake vijana, ambao kwa kuelemewa na hamu ya ngono, walilazimika kutenda madhambi (kuzini) na wakati fulani ilisababisha uhalifu na mauaji.

Mpaka sasa wasomaji wanapaswa kuwa wamefahamu sababu zilizosababisha mitala na kwa nini Uislamu haukuipiga marufuku mila hii. Wanapaswa pia kuwa wamefahamu masharti na mipaka iliyowekwa na Uislamu juu ya mitala. Uislamu haujamshushia hadhi mwanamke kwa kuruhusu mfumo huu, bali umewasaidia. Ikiwa mitala haitaruhusiwa, hata pale ambapo idadi ya wanawake wanaostahili kuolewa inazidi ya wanaume, wanawake wanaweza kuwa ni midoli isiyo na thamani mikononi mwa wanaume. Wanaweza kutendewa vibaya zaidi kuliko wasichana watumwa, kwa vile mwanaume anajua kuwa mtoto wa msichana mtumwa ni wake humthamnini, lakini hawaheshimu hawa vimada wake au mahawara.

Mwanaume Wa Sasa Na Mitala.

Mwanaume wa sasa hapendi mitala, sio kwa sababu anataka kuridhika na mke mmoja, bali kwa sababu anataka kuridhisha hamu yake ya kuwa na aina mbali mbali za wanawake kwa kujiingiza katika uzinifu na wanawake wasio na idadi, njia ambayo ni rahisi zaidi na kuna mazingira mazuri zaidi kwa hilo. Dhambi na sio uaminifu, imechukua nafasi ya mitala. Hii ndio sababu mwanaume wa sasa anachukia mitala ambayo humtwisha majukumu mengi ya kifedha na vinginevyo.

Zamani, hata kwa mwasherati, fursa za kufanya hivyo hazikuwa nyingi. Hii ndio sababu aliamua kuoa wake wengi na licha ya kukwepa majukumu mengi bado alilazimika kubeba majukumu fulani kwa ajili ya wake na watoto wake. Mwanaume wa sasa ambaye ana fursa nyingi za kufurahi na wanawake, haoni haja yoyote ya kuwajibika hata kidogo. Na kwa hiyo anakirihika kabisa na mitala.

Mwanaume wa sasa anaajiri wanawake kama makatibu muhtasi, wapiga chapa, nk. kwa ajili ya raha zake, na gharama zake hulipwa na serikali, kampuni yake au mashirika mengine anapofanyia kazi, bila yeye kuwa na haja ya kulipa hata shilingi kutoka mfukoni mwake.

Mwanaume wa leo anaweza kubadili wanawake kila baada ya siku chache bila kuwa na shida ya kufuata taratibu za mahari, matunzo na talaka. M.Tshombe alikuwa anapinga vikali sana mitala lakini alikuwa na katibu muhtasi wa kike kijana na aliyeumbika vizuri pembeni yake na ambaye alikuwa akimbadilisha (akiajiri mwingine) kila mwaka. Kwa kuwepo fursa hizi ni dhahiri kuwa mwanaume hana haja ya kuoa wake wengi.

Tunasoma katika historia ya Bertrand Russell ambaye alikuwa ni mpinzani mkubwa wa mitala, kuwa wanawake wawili, pembeni kwa bibi yake, walikuwa na mchango mkubwa katika maisha yake. Mmoja alikuwa ni mke wake, Alice, na mwingine alikuwa ni mpenzi wake, Morrel. Morrel ambaye alikuwa mmoja wa wanawake mashuhuri wa wakati ule alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na waandishi wengi wa karne ya 20. Ni wazi kuwa mwanaume wa aina hii asingeunga mkono wazo la mitala.

Inavyoonekana ni kuwa ilikuwa ni mapenzi ya nje ya ndoa ya Russel yaliyovunja ndoa yake na Alice. Yeye mwenyewe anaandika kuwa siku moja alasiri akiwa anaendesha baiskeli yake kwenda kwenye migahawa nje ya mji, ghafla alihisi kuwa hampendi Alice tena.

  • 1. Wake aliowaoa wakiwa hawana watoto ni Bibi Khadija, Aisha na Hafsa. Japo kwa makosa ya kihistoria inadaiwa kuwa Bibi Khadija alipata kuolewa na waume wengine na akazaa watoto, lakini ukweli ni kuwa Mtume ndio alikuwa mume wa kwanza wa Bibi Khadija na wale watoto wanaodaiwa kuwa Bibi Khadija alizaa na wanaume wengine walikuwa ni watoto wa dada yake aliokuwa anawalea baada ya dada yake kufariki.