Utumwa Katika Zama Za Kale

"Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na wanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni aliye mchamungu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari." (Qur'an 49:13).

Utumwa sio taasisi iliyoanzishwa na Ukristo au Uislamu. Ni Utumwa ulikuwepo kwa muda mrefu hata kabla ya kuanzishwa hizi dini mbili. Kwa mtazamo wa haraka kuhusu utumwa wa kale, ninamnukuu Jaji Ameer Ali:

“Shughuli ya Utumwa ina rika moja sawa na kuwepo kwa binadamu. Kihistoria dalili zake zinaonekana katika kila zama na kila taifa…Wayahudi, Wayunani, Warumi na Wajerumani wa kale, watu ambao taasisi zao za kisheria na za kijamii zilizoathiriwa mno na tabia na desturi za kisasa, walizitambua na kuzifanya aina zote za utumwa, utumwa wa kazi za kiuchumi na wa kazi za nyumbani. Baada ya kuanzishwa kwa makundi ya washenzi wa Magharibi na Kaskazini katika mabaki ya dola ya Warumi, zaidi ya utumwa wa mtu binafsi, utumwa wa taifa moja kulifanya taifa lingine kuwa mtumwa, ambao haukujulikana sana kwa Warumi, ukashamiri kwenye nchi zote mpya zilizo kaliwa… kanuni za kishenzi, kama zile za Warumi, ziliona utumwa kama hali ya kawaida ya binadamu; na kama mtumwa alipewa ulinzi, ilikuwa kwa sababu mtumwa alikuwa mali inayo milikiwa na bwana wake, ambaye ni yeye peke yake baada ya nchi, alikuwa na mamlaka juu ya uhai na kifo kwa mtumwa.1
Katika nchi ya Uajemi (Persia) ikulu ya Mfalme ilikuwa na watumwa wanawake elfu kumi na mbili. Wakati Mfalme wa Byzantine anaketi kwenye kiti chake cha enzi, maelfu ya watumwa walikuwa tayari kutoa huduma kamili na mamia ya watumwa waliinama kuonyesha heshima wakati mfalme anainama kuvaa viatu. Huko Ugiriki au Uyunani, idadi ya watumwa ilikuwa kubwa zaidi ya watu walio kuwa huru, licha ya kwamba Ugiriki ilitoa watetezi wakubwa wa ubinadamu na haki.

Kila jeshi la Kiyunani ambalo lilirudi nyumbani na salamu za ushindi, lilifuatwa na kuindi la watumwa. Aristotle, mwanasalsafa maarufu wa zamani, alipokuwa anazungumzia suala la iwapo kila mtu alikusudiwa na maumbile kuwa mtumwa au la, anasema: “Hakuna ugumu katika kujibu swali hili, katika misingi yote miwili, ya akili na kweli.

Ya kwamba watu baadhi fulani watawale na wengine watawaliwe si tu kwamba ni jambo muhimu bali ni kitu chenye manufaa kuanzia saa ya kuzaliwa kwao, watu wengine wameumbwa ili wawe watumwa, wako kwa ajili ya kutii tu, na wengine wameumbwa kwa ajili ya kutawala.” Halafu anahitimisha; “…watu wengine kwa asili wako huru, na wengine ni watumwa, na kwa utumwa huu (uliotajwa) wa mwisho, wote ni wenye manufaa na haki.”2 Katika utawala wa Rumi, utumwa wa kale ulifika kilele chake, lakini Dola ya Kirumi ilipoanza kuanguka, watumwa wengi wakaanza kuwa na hali nzuri kwa kiwango kidogo.

Lakini uovu wa utumwa ulionekana wazi kabisa. Uovu huu ulishinda ujuzi wa uhalali wa Kiyunani kama ambavyo imeshinda falasfa stadi ya Kigriki.

Kuonyesha mapenzi kwa watumwa lilionekana si tendo la hisia za kawaida lakini ilikuwa tabia pekee ya mtu mwenyewe binafsi. Mtumwa hakuonekana kama binadamu, hakuwa na haki, hakuwa na roho.3 Wakati huo wa ujio wa Uislamu (mnamo karne ya 7 CE) utumwa ulikwisha enea kote kote huko India, Ajemi, Rumi, Rasi ya Arabia, Romania na Ugiriki. Watu waliokuwa na hali nzuri na nafasi nzuri na wasomi wa nchi hizi hawakuwatilia maanani watumwa kustahiki kupatiwa hata angalao pia haki za msingi za kibinadamu.

Mtumwa alikuwa anaonekana kama bidhaa isiyo na thamani zaidi kuliko hata ya ng’ombe.4 Mara nyingi mtumwa aliuzwa kwa bei rahisi kuliko kondoo na mbuzi. Kwenye hafla maalum za kijamii wageni waheshimiwa wa nchi walikuwa na tabia ya kukusanyika pamoja na Kiongozi wa Nchi kutazama michezo ya kupigana watu na katika michezo hii watumwa walifanywa wapigane kwa kutumia mapanga na mikuki kama vile maonyesho ya mapigano ya jongoo wawili na kware katika kipindi cha zamani cha jamii ya kikabaila. Watu walishangilia kwa kupiga makofi hadi mtu mmoja miongoni mwa wapiganaji aliuawa. Watazamaji walimshangilia sana mshindi.5

Kwa upande mwingine, Rasi ya Arabia ilizunguukwa na nchi ambazo bado zilikuwa na dalili za ufahari wa ustaaraabu wa Kirumi na Kiyunani uliokuwa unaporomoka, na kwa upande mwingine, ilizunguukwa na nchi zilizogubikwa na imani za dini za “Zoroastria” na “Uhindi.” Kama ilivyo tajwa hapo juu, kwenye nchi zote hizi utumwa ni taasisi iliyo tambuliwa.

Vibao kumi na mbili vya maandiko (ya sheria zao) vilitoa mhuri wake rasmi kuithibitisha taasisi hii. Ukali usiopunguka wa matatizo na ukatili ambao watumwa walifanyiwa, haukupungua, lakini, kwa namna yoyote ile, watumwa sasa walikubaliwa kama wanyama (hayawani) ambao hatima yao ilikuwa ni kufanya kazi na kufa tu kwa manufaa ya hao walio wamiliki.

Sina nia ya kukifanya kitabu hiki kuwa historia ya unyama waliofanyiwa watumwa lakini itoshe tu kusema kwamba mtu lazima siku zote abebe hatia katika dhamira yake kwamba wakati fulani alijiingiza kwenye uovu wa utumwa.

  • 1. Ameer Ali, Spirit of Islam (London: University paper back, 1965), PP. 259-261; pia
    angalia Will Duratnt, The Story ofa Civilisation, juzuu ya III (New York, 1944), P.397.
  • 2. Aristotle, Politics, Book one, Sura ya 5 (New York: Modern Library, 1943), uk. 58-60.
  • 3. Durant, W., op.cit., Juzuu ya III uk. 397, Juzuu IV (New York), uk. 29).
  • 4. Ibid
  • 5. Ibid.