Neno La Mchapishaji

Kitabu kilichoko mikononi mwako, ni tarjuma ya kitabu cha Kiingereza, kwa jina la Concentration In Prayer (Umakini katika Swala) kilichoandikwa na Jameel Kermalli, Daktari mwanasaikolojia.

Kitabu hiki kinafundisha namna ya mtu kuwa makini katika Swala yake. Kilichomsukuma mwandishi huyu kuandika kijitabu hiki, ni ukweli kwamba sisi kama binadamu hatuko huru kutokana na mawazo ya aina aina ambayo humjia mtu hata wakati akiwa katika Swala, wakati mwingine mawazo huwa makali sana kiasi cha kumbatilishia mtu Swala yake. Ni tatizo kubwa sana ambalo wengi wetu tunalo. Kwa hakika hali hii hutokea kwa kuchezewa na shetani aliyelaaniwa.

Kwa hiyo mwandishi katika kijitabu hiki ameonyesha njia mbali mbali za kuepukana na hali hii, hususan wakati wa Swala; ametumia mifano na mazoezi ya kufanya ili mtu aweze kuwa makini katika Swala yake.

Tumekiona kijitabu hiki ni chenye manufaa sana, na kitawafaa sana Waislamu wa rika na wa jinsia zote. Kama ilivyo ada yetu tumeona tukitoe kijitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili kwa nia ile ile ya kuwahudumia Waislamu wazungumzaji wa Kiswahili.

Tunamshukuru Ndugu yetu al-Akh Ramadhani Kanju Shemahimbo kwa kukubali jukumu hili la kukifanyia tarjuma kitabu hiki. Vile vile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hiki.

Ni matumaini yetu kwamba kitabu hiki kitakuwa ni chenye manufaa kwa wasomaji wetu na insha-Allah kuwafanya kuwa makini katika Swala zao, na hivyo kuwa zenye kutakabaliwa.

Mchapishaji:
Al-Itrah Foundation
S. L. P. 19701
Dar-es-Salaam