Dua Za Wudhu

Dua hii ni wakati unapoanza kutawadha, unaanza kwa Jina la Mwenyezi Mungu (s.w.t.), na kumshukuru Yeye kwa kuyafanya maji kuwa tohara.

Ni katika kuosha mikono, unamuomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akuweke miongoni mwa wale wanaoomba msamaha Wake na wale ambao wametoharika.

Wakati unaposukutua kuosha mdomo wako, unamuomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akufundishe njia sahihi ya kujibu maswali Siku ya Kiyama utakapokuwa kwenye Hadhara Yake Tukufu.

Wakati unaposafisha pua, unamuomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) asikunyime harufu ya Peponi na akuweke miongoni mwa wale wanaoyanusa manukato yake.

Wakati wa kuosha uso, unamuomba Allah (s.w.t.) aung’arishe uso wako katika siku ambayo Yeye atazifedhehesha na kuzifanya nyeusi nyuso za idadi kubwa ya watu.

Wakati wa kuosha mkono wa kulia, unamsihi Allah (s.w.t.) kuweka daftari ya matendo yako kwenye mkono wako wa kulia na hati ya uthibitisho wa kudumu ndani ya Pepo kwenye mkono wako wa kushoto, na kwamba Akufanyie mahesabu yako kwa wepesi wa huruma.

Wakati wa kuosha mkono wa kushoto, unamuomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) asiweke daftari ya matendo yako kwenye mkono wako wa kushoto, wala kutoka mgongoni kwako, na asikitundike kwenye shingo yako. Pia unatafuta kusalimika kutokana na Moto mkali wa kudumu wa Jahannam.

Wakati wa kupaka kichwa, unamuomba Allah (s.w.t.) akufunike na Rehema, Baraka Zake na Msamaha Wake.

Mwishowe, wakati wa kupaka miguu, unamuomba Allah (s.w.t.) akuimarishe katika Sirat Yake katika Siku ile ambapo miguu itateleza, na kuzifanya nguvu zako kama za wale ambao watamridhisha Yeye.

Imesimuliwa katika Hadithi sahihi kwamba Maimam Ma’sum (a.s.) walikuwa wakitetemeka na wakati mwingine hata rangi za nyuso zao zilibadilika, wakionyesha hofu na woga juu ya Allah (s.w.t.) wakati walipokuwa wakitekeleza hatua za wudhu. Mtu anapaswa kujenga na vilevile kudumisha hofu wakati anapotawadha.