Mkakati Wa Kwanza: Kuelewa Na Kutambua Kuwepo Kwa Allah (S.W.T.)

Ni kwa faida yako kama wakati wote utakuwa unatafakari kuwepo kwa Allah (s.w.t.) na Nguvu Zake, Dalili na Maamuzi Yake kuhusiana na dunia hii na ile ijayo. Kutambua kuweko Kwake ni njia mojawapo ya kuleta hushui kwenye moyo wako na Kujinyenyekeza mwenyewe katika Swala yako iliyoswaliwa kwa uangalifu na kwa makini. Ni Yeye tu ambaye anakuangalia kwa upole kabisa wakati wa Swala yako, na unapaswa kuliweka hili akilini kila wakati unaposwali.

Abu Ja’far, mtoto wa Babawayh al-Qummi (r.a.) anasema:

“.......Allah (s.w.t.), Aliyetukuka, ni Mmoja na wa Pekee Kabisa. Hakuna mwingine kama Yeye. Ni Mkubwa; Yeye kamwe hakuwa, na kamwe hatakuwa, ila Mwenye kusikia na Mwenye kuona. Mjuzi wa yote; Mwenye Hekima; Aliye Hai; Wa Milele; Mwenye nguvu; Mtukufu; Mwenye Kujua; Mwenye Uwezo; Mwenye Kujitosheleza.

Yeye ni wa Pekee, Kimbilio la Milele; Hakuzaa kwamba anaweza kurithiwa, wala Hakuzaliwa kwamba Anaweza kushirikishwa na wengine. Hakuna mwingine kama Yeye.

Hana anayelingana naye wala mpinzani, mwenza wala wa kuandamana naye.
Hakuna kinachoweza kufananishwa Naye. Yeye hana adui wala mshirika. Macho ya mwanadamu hayawezi kumuona, ambapo Yeye anatambua uwezo wa macho. Fikra za wanadamu haziwezi kumzingira, ambapo Yeye anazielewa. Usingizi haumpitii, wala halali. Yeye ni Mwingi wa Rehema na Mjuzi, Muumba wa vitu vyote. Hakuna mungu ila Yeye. Uwezo wa kuumba na Mamlaka ni Vyake peke Yake. Baraka ni za Allah (s.w.t.), Mola wa Ulimwengu.”

Kwa hiyo, uchamungu, ustahimilivu na kumtambua Mwenyezi Mungu na Uweza Wake ni viambato vyenye athari sana katika kujenga na kudumisha uangalifu wako katika Swala. Kwa njia hii, unaweza kujinyenyekeza mwenyewe katika Swala

Mfano mzuri ni kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) aliyekuwa akiiendea swala kwa dhati kabisa na alitoa uangalifu wake wote na umakinifu. Alimtambua na kumuelewa Muumba wake kiasi cha kutosha kuhofia Kuwepo Kwake na kuhudhuria kwa umakinifu kamili wakati anaposimama mbele Yake. Imam al-Khumein (r.a.) anasimulia Hadithi kwamba, Kwa miaka kumi Mtume wa Allah (s.w.t.) alisimama kwa vidole vyake (katika Swala) mpaka miguu yake mitukufu ikavimba na uso wake ukapauka. Na angeweza kusimama wima usiku wote, hadi ukafika muda ambapo Mwenyezi Mungu akamliwaza (kwa Aya ifuatayo):

مَا أَنْزَلْنَا عَلَيْكَ الْقُرْآنَ لِتَشْقَىٰ {2}

Hatukukuteremshia Qur’an ili upate mashaka (20: 2)

As-Saduq (r.a.) anasimulia ushauri ufuatao kutoka kwa Imam as- Sadiq (a.s.) ambao aliutoa kwa mmoja wa wafuasi wake waaminifu:

‘Ewe mja wa Allah! Wakati unaposwali, swali kama mtu anayeaga na anayehofia kwamba hatarudi tena kamwe (yaani, swali kwa namna kama unaswali swala ya mwisho ya maisha yako). Kisha elekeza macho yako kwenye sehemu yako ya kusujudia. Kama unapojua kuwa kuna mtu kulia au kushotoni kwako, huwa unakuwa muangalifu sana katika kutekeleza Swala yako; basi ufahamu kwamba unasimama mbele ya Anayekuona na wewe humuoni.’
(Al-Hurr al-Amili, katika Wasa’il as-Shi’ah, juz. iv, uk.685)