Mkakati Wa 5: Matamshi Sahihi

Lugha ya Kiarabu inafikiriwa kuwa tamu zaidi katika lugha zote. Kwa hiyo, kuswali Swala kwa matamshi sahihi (Makhaarij) na kufuata kanuni za lugha ya Kiarabu (Tajwiid) na kujifunza kanuni za kusoma Qur’an Tukufu, kutazifanya juhudi zako katika kudumisha uzingatiaji kuwa rahisi mno.

Kuisikiliza sauti yako mwenyewe (na sauti za watu wengine), na jinsi zinavyoweza kusikika vibaya na butu wakati mwingine ni njia nyingine mbadala. Unapaswa kujaribu kubadili sauti yako hadi kufikia ile inayofaa.

Kuchanganya hizo kanuni za usomaji na marudio ya kusoma kwako ndio kunakotakikana na kunahitaji kufanyiwa mazoezi. Sifa hizi kwa Mtume (s.a.w.w.) ndizo zilizokuwa zikiwafanya watu kukaa na kumsikiliza Mtume (s.a.w.w.) akisoma Qur’an Tukufu.

Kama utakuwa nazo sifa hizi katika sauti yako, basi kamwe hutajihisi kuchoka na kuishiwa nguvu ya kusoma Sura ndefu za Qur’an tukufu au kusoma nyiradi ndefu na za kurudiarudia wakati wa Swala, kwa sababu utakuwa umezama kabisa katika sehemu za kisomo chenyewe. Hii ni njia yenye nguvu sana ya kurefusha kuinama (rukuu) kwako na kusujudu, na ni njia ya kurefusha Swala yako bila ya adha yoyote.

Kwa wale Waislamu wachamungu ambao lughamama yao sio Kiarabu na bado wanapaswa kumudu usomaji sahihi wa vifungu vya kiarabu vinavyohusika kwenye Swala, wanashauriwa angalau kujifunza kusoma zile sehemu za lazima za Swala kwa usahihi zaidi na kwa matamshi sahihi.

Kwa njia hii watakuwa na uhakika kwamba Swala zao zinaswihi. Mtu huyu anapaswa pia ajaribu kutokuweka mazingatio kwenye kisomo chake tu, kwani anaweza akapoteza mazingatio yake juu ya Allah (s.w.t.). Kwa hali yoyote ile, hakuna kisingizio cha kutojifunza kusoma kwa Makhaarij na Tajwiid sahihi.