Mkakati Wa 20: Dunia Na Anasa Zake

Daylami, katika Irshadul Qulub, akimnukuu Amir-ul-Mu’minin (a.s.), anasema kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema:

“Katika Usiku wa Mi’raj, Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema: ‘Ewe Ahmad! Kama mja atatekeleza Swala yake kwa kiwango kama kile cha watu wa duniani na wa mbinguni, na akafunga kwa kiwango kama kile cha watu wa duniani na wa mbinguni, na akajizuia, kama Malaika, kuhusu chakula, na akajivisha mavazi ya mchaji, kisha nikaona moyoni mwake chembe ya mapenzi juu ya dunia hii au ya hadhi ya kidunia, uongozi, umaarufu na mapambo, yeye hatakuwa kwenye makazi yaliyo jirani na Mimi na nitayaondoa mapenzi Yangu kutoka kwenye moyo wake na kuufanya mweusi mpaka yeye anisahau Mimi. Sitamfanya yeye auonje utamu wa mapenzi Yangu.’”(Irshadul Qulub, Juz. 1, uk.206)

Kwa mujibu wa Ayatullah Ibrahim Amini, moja ya vikwazo vikubwa katika kufikia hali ya imani thabiti juu ya Allah (s.w.t.) ni kufungamana kikamilifu na matamanio ya dunia, yaani, utajiri, mali, madaraka na cheo. Kuvutiwa kwa mtu kwenye vitu hivi kunafanya mazingatio ya mwenye kuabudu kuwa kwenye vitu hivi vya mpito. Kwa hiyo, ni lazima uyaanche matamanio haya kwa gharama yoyote ile, na kwa wakati wote, ili kwamba mahudhurio na mazingatio ya moyo kuelekea kwa Allah (s.w.t.) yaweze kuwa rahisi wakati wa Swala.

Kuna tafsiri mbalimbali juu ya neno Dunia. Kilicho cha muhimu hapa ni kuielewa ile Dunia Isiyoridhiwa. Kwa mujibu wa al-Majlisi (r.a.): “Vitu vyote vinavyozuia wanaume na wanawake kumtii Allah (s.w.t.) na kuwaweka mbali na Mapenzi Yake, na mbali na kuitafuta akhera, vinajulikana kama Dunia Isiyoridhiwa.

Itambulikane kwako kwamba linaloweza kufasiriwa kutoka kwenye Aya zote za Qur’an na Ahadith kuhusu jambo hili, kulingana na kuzielewa kwetu, ni kwamba dunia iliyolaaniwa (isiyoridhiwa) ni hesabu ya jumla ya vile vitu vyote ambavyo vinamzuia mtu kumtii Allah (s.w.t.) na kumuweka mbali na Mapenzi Yake na kutokana na kuitafuta Akhera.’

Vivutio hivi vinaweza kujumuisha na runinga (televisheni) na radio na burudani zake haramu zinazohusika nazo; ikiwa ni sehemu ya kundi ambalo linasengenya watu na linalotumia lugha chafu; kujaza tumbo lake mtu na chakula wakati wote; kuwa mvivu na kupoteza wakati kwa mambo yasiyo na maana, na kadhalika. Hii ndio dunia ambayo mtu anapaswa kujizuia nayo.

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na ushauri huu kwa sahaba wake Abu Dharr (r.a.) kuhusiana na Dunia Isiyoridhiwa, nao upo kama ifuatavyo: “Ewe Abu Dharr! Dunia (isiyoridhiwa) imelaaniwa! Laana imo katika vyote vilivyomo ndani yake isipokuwa vile vinavyotafuta radhi za Allah (s.w.t.). Na hakuna kinachomchukiza zaidi Allah (s.w.t.) kuliko hiyo dunia (isiyoridhiwa). Aliiumba hiyo kisha akaiacha. Hakuiangalia na hataiangalia mpaka ile Saa ya Mwisho (Siku ya Kiyama). Na hakuna kinachopendeza zaidi kwa Allah (s.w.t.) zaidi ya imani juu Yake na kuyaacha yale anayoyakataza.

“Ewe Abu Dharr! Waliobarikiwa ni wale watu wanaokaa mbali na dunia hii, na wale wanaoisubiri Akhera. Wanaichukulia ardhi ya Mwenyezi Mungu kama busati, udongo wake kama mito ya kulalia na maji yake kama marashi. Wanakisoma Kitabu cha Allah (s.w.t.) kwa sauti kubwa, wanamwita Yeye kwa sauti kubwa na wanajitenga na mambo ya kidunia.’

Dunia iliyoridhiwa ni:

Makazi ya kweli kwa yule anayeukubali ukweli wake, ni mahali pa usalama kwa yule anayeielewa, ni machimbo ya hazina kwa yule anayekusanya mahitaji toka kwenye dunia hiyo (kwa ajilil ya ile ya akhera), na ni nyumba ya maelekezo kwa yule anayechukua masomo kutokana nayo.

Ni mahali patakatifu kwa wale wanaompenda Allah (s.w.t.), ni nyumba ya ibada kwa ajili ya Malaika Zake, ni mahali ambapo wahyi wa Allah (s.w.t.) unashuka, na ni mahali pa soko kwa wale watiifu Kwake. Humo, wao wanajipatia Neema Zake na humo wanaipata Pepo kama namna ya faida. (Imam Ali (a.s.)

Kumuabudu Mwenyezi Mungu zaidi ya zile swala za wajibu; kutumia muda katika ulimwengu huu katika mambo yenye faida na kusaidia watu; kuiangalia vema familia yake mtu na kuingiza mapato ya halali; kujizua katika yale yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu, na kadhalika, ni vitendo ambayo vitapanda mbegu zenye afya katika dunia hii kwa ajili ya mtu huyo kufaidi matunda yake katika ulimwengu ujao. Hii ndio hiyo Dunia Iliyoridhiwa.