Sura Ya 49: Vita Vya Hunayn

Ilikuwa ni desturi ya Mtume (s.a.w.w.) kwamba kila alipoliteka eneo fulani, yeye mwenyewe alikuwa akiyaangalia matatizo yale ya kisaiasa na mambo ya kidini ya wakazi wake kwa kadiri akaavyo kwenye eneo lile, na anapoondoka kwenye eneo hilo aliwateua watu waliofaa kuzishika nafasi mbalimbali.

Sababu yake ilikuwa kwamba, watu wa eneo lile walioizoea mipango ya kale na iliyozongwa zongwa hawakuwa na ujuzi wa mpango mpya na ulioichukua nafasi ya ile ya kale.

Uislamu ni mpango wa kijamii, kimaadili, kisiasa na kidini. Sheria zake zinatokana na ufunuo, na kunawajuvya watu sheria hizi na utelekezaji wake miongoni mwao kunahitaji watu wanaotambulika waliokomaa kiakili na wenye elimu, watakaowafunza misingi sahihi ya Uislamu kwa hekima, na vilevile kusimamia utekelezaji wa mfumo wa Kiislamu miongoni mwao.

Mtume (s.a.w.w.) alipoamua kuondoka mjini Makka na kuiendea nchi ya makabila ya Hawaazin na Saqif, alimteua Mu’aaz bin Jabal kuwa kiongozi ili awaelimishe na kuwaelekeza watu, na akaiweka serikali na utawala wa mji ule na vile vile uimamu (wa Sala) mle msikitini mikononi mwa ‘Atab bin Usayd, mtu aliyekuwa na uwezo. Baada ya kukaa mjini Makka kwa muda wa siku kumi na tano Mtume (s.a.w.w.) alikwenda kwenye nchi ya kabila la Hawaazin.1

Jeshi Lisilo Na Kifani

Katika siku ile Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na askari elfu kumi na mbili wenye silaha waliokuwa chini ya bendera yake. Miongoni mwao askari elfu kumi walikuwa wale waliofuatana naye kutoka Madina, na walishiriki katika kutekwa kwa mji wa Makkah, na wale elfu mbili wangine waliotoka miongoni mwa Waquraishi waliosilimu karibuni tu. Ukamanda wa kundi hili ulikuwa mikononi mwa Abu Sufyani.

Katika siku zile jeshi kubwa kiasi kile halikuweza kuonekana mahali popote pale, na nguvu yao hii ya wingi ikawa ndio sababu ya kushindwa kwao. Ilikuwa kwa sababu, kinyume na siku za nyuma, walijifaharisha kutokana na idadi kubwa ya askari wao na wakazitupilia mbali mbinu za kijeshi na kanuni za kivita. Macho ya Abu Bakr yalipoiangukia ile idadi kubwa ya askari alisema: “Katu sisi hatuwezi kushindwa hata kidogo, kwa kuwa idadi ya askari wetu imezidi sana ile ya adui.”2 Hata hivyo, yeye hakuzingatia ukweli kwamba ukubwa wa idadi sio sababu pekee iletayo ushindi, na kwa kweli sababu hii ni ya umuhimu mdogo tu.

Qur’ani Tukufu yenyewe inautaja ukweli huu na inasema:

لَقَدْ نَصَرَكُمُ اللَّهُ فِي مَوَاطِنَ كَثِيرَةٍ ۙ وَيَوْمَ حُنَيْنٍ ۙ إِذْ أَعْجَبَتْكُمْ كَثْرَتُكُمْ فَلَمْ تُغْنِ عَنْكُمْ شَيْئًا وَضَاقَتْ عَلَيْكُمُ الْأَرْضُ بِمَا رَحُبَتْ ثُمَّ وَلَّيْتُمْ مُدْبِرِينَ {25}

“Hakika Allah amekunusuruni katika mapigano mengi, na siku ya Hunayn ambapo wingi wenu ulikupandisheni kichwa, lakini haukukufaeni kitu. Na ardhi ikawa finyu kwenu juu ya upana wake. Kisha mkageuka mkarudi nyuma.” (Sura al-Tawbah, 9:25).

Upatikanaji Wa Taarifa

Baada ya kutekwa kwa mji wa Makka msisimko na shauku kubwa viliweza kuonekana kwenye maeneo yaliyokaliwa na makabila ya Hawaazin na Saqif. Mawasiliano maalum yalikuwapo baina yao. Kiunganisho baina yao kilikuwa ni mtu wa kupenda vita aliyeitwa Malik bin Awf Nasri. Matokeo ya mawasiliano yao yalikuwa kwamba kabla ya lile jeshi la Kiislamu kuonyesha kuwajali, wao wenyewe walijitokeza kupambana nalo ili kwamba kabla ya Waislamu kutoka, wao wenyewe wawashambulie vikali mno kwa mbinu za kijeshi. Vile vile walimchagua kutoka miongoni mwao mtu mwenye umri wa miaka thelathini aliyekuwa shujaa na shupavu ili awe kamanda wao.

Zaidi ya hayo makabila mawili tuliyoyataja, makabila ya Bani Hilal, Bani Nasr na Bani Jasham nayo yalishiriki vilevile kwenye vita hivi na wote walitoka kama jeshi moja lenye kushambulia.

Kama ilivyoamrishwa na yule kamanda wao mkuu, wale wote walioshiriki kwenye vita hivi waliwaweka wanawake wao na wale wawategemeao nyuma ya kikosi cha mwisho cha jeshi lile.

Alipoulizwa sababu ya uamuzi ule, alijibu akisema: “Wanaume hawa watasalia thabiti katika mapigano yao ili kuwahami wanawake na mali zao na kamwe hawatafikiria kukimbia au kurudi nyuma.3

Pale Durayd bin Sammah, mzee na shujaa mzoefu alipovisikia vilio vya wanawake na watoto aligombana na Malik na akakichukulia kitendo chake hiki kuwa ni kosa kwa mtazamo wa kanuni za kivita, alimwambia: “Matokeo ya kitendo hiki yatakuwa kwamba kama mkishindwa mtakuwa mmewatoa wanawake na mali zenu zote kwa jeshi la Waislamu bila ya sababu.” Malik hakuyasikiliza maneno ya askari huyu mzoefu, nae akamjibu akisema: “Wewe umeshazeeka na umeshapoteza hekima na ujuzi wako wa mbinu za kivita.” Hata hivyo, matokeo ya baadae yalidhihirisha kwamba yule mzee alikuwa sahihi na kuwako kwa wanawake na watoto kwenye eneo la shughuli za kijeshi ambamo mtu anapaswa kupiga na kukimbia kulithibitisha kuwa hakuna faida yoyote, ila tu kwamba wale askari walijitia kwenye matatizo na mishughuliko yao ilitatizwa.

Mtume (s.a.w.w.) alimtuma Abdullah Aslami bila ya kutambulika ili akakusanye taarifa juu ya zana, malengo na utaratibu wa safari ya adui. Alitangatanga miongoni mwa jeshi zima la adui, akakusanya taarifa muhimu na kumletea Mtume (s.a.w.w.). Malik naye aliwatuma majasusi watatu kwa Waislamu kwa njia maalum ili wamletee tarifa zihitajikazo. Hata hivyo, wao walirejea kwa Malik wakiwa na nyoyo zilizojawa na hofu na woga.

Kamanda wa lile jeshi la adui akaamua kufanya mabadiliko yatakayofaa kwa ule uduni wa idadi na udhaifu wa nyoyo wa askari wake kwa njia ya hila za kijeshi, yaani kufanya mashambulizi ya kushitukiza, kusababisha mchafuko miongoni mwa jeshi la Waislamu ili kwamba nidhamu ya vikosi vyao ivurugike na mpango wa uongozi wao mkuu uharibike.

Ili kulifikia lengo hili, alipiga kambi mwishoni mwa njia ya kuingilia kwenye eneo la Hunain. Kisha aliwaamrisha askari wote kujificha nyuma ya mawe, majabali na vipenyo vya milima na kwenye sehemu za miinuko ziizungukazo njia ile, na mara tu jeshi la Uislamu liwasilipo kwenye njia hii ndefu na yenye kina kirefu, wote watoke kwenye maficho yao na kuvishambulia vikozi vya Uislamu kwa mishale na mawe. Baada ya hapo, kikundi maalum kishuke kutoka kule milimani kwa utaratibu mzuri na kuwauwa Waislamu kwa msaada wa kukingwa na wapiga mishale wao.

Zana Za Waislamu

Mtume (s.a.w.w.) aliitambua nguvu na ukaidi wa adui yule. Hivyo basi, kabla ya kutoka Makka alimwita SafwAn bin Umayyah na kuazima deraya mia moja kutoka kwake na akamhakikishia kuzirejesha kwake. Yeye mwenyewe alivaa deraya mbili, akavaa kofia ya chuma, akampanda yule nyumbu mweupe aliyewasilishwa kwake, na akatembea nyuma ya jeshi la Uislamu.

Wakati wa usiku jeshi la Uislamu lilipumzika kwenye mlango wa kuingilia wa njia ile, na ilikuwa bado hakujakucha vizuri pale kabila la Bani Salim lilipowasili kwenye ile njia ya Hunayn likiwa chini ya uamiri jeshi wa Khalid bin Walid. Wakati sehemu kubwa ya jeshi la Uislamu ilipokuwa bado imo kwenye njia ile, kelele za ghafla za mvumo ya mishale na mingurumo ya askari waliokuwa wakiotea nyuma ya majabali zilisikika na zikaleta hofu isiyo kifani na woga miongoni mwa Waislamu. Mishale ilikuwa ikimiminwa juu yao na kikundi cha maadui kikaanza kuwashambulia kikilindwa na wapiga mishale.

Hili shambulio la ghafla liliwaogofya mno Waislamu kiasi kwamba walianza kukimbia na wao wenyewe walisababisha mvurugiko wa safu za jeshi lao zaidi ya vile walivyofanya wae adui. Matokeo haya yalikuwa chanzo cha furaha kubwa mno kwa wanafiki waliomo kwenye jeshi la Waislamu, kiasi kwamba Abu Sufyani akasema: “Waislamu watakimbia hadi kwenye ufuko wa bahari.” Mnafiki mwingine akasema: “Uchawi umebatilishwa.” Mtu wa tatu miongoni mwao alidhamiria kuulia mbali Uislamu kwenye ile hali ya machafuko ya mambo kwa kumuua Mtume (s.a.w.w.) na hivyo kuiangamiza itikadi ya Upweke wa Allah na Utume wa Uislamu, vyote jumla.

Uimara Wa Mtume (S.A.W.W.) Na Kikundi Cha Watu Wenye Kujitoa Mhanga

Mtume (s.a.w.w.) aliingiwa na wasiwasi sana kutokana na kukimbia kwa marafiki zake ambapo kulikuwa ndio sababu kuu ya mshituko na mvurugiko, na alijihisi kwamba kama mambo yakiruhusiwa kwenda kama yalivyo, japo kwa kitambo kidogo tu zaidi ya hapo, basi mhimili wa historia utakuwa tofauti, binadamu wataubadili mwelekeo wake na nguvu za ushirikina zitaliangusha jeshi la itikadi ya Upweke wa Allah. Hivyo basi, akiwa amempanda ngamia wake, alisema kwa sauti kuu: “Enyi Wasaidizi wa Allah na Mtume Wake! Mimi ni mja wa Allah na Mtume Wake.”

Aliitamka sentensi hii na kisha akamgeuzia yule nyumbu wake kwenye uwanja wa vita uliokuwa ukikaliwa na askari wa Malik, ambao tayari waliishawauwa baadhi ya Waislamu na walikuwa wakiendelea kuwauwa wengine. Kikundi cha watu waliojitoa mhanga, kama vile Sayyidna Ali Amirul-Mu’minin (a.s.), Abbas, Fadhl bin Abbas, Usamah na Abi Sufyan bin Harith, ambao walikuwa hawakumwacha Mtume (s.a.w.w.) akiwa peke yake na bila ya ulinzi tangu mwanzoni mwa vita vilipoanza, vile vile walisonga mbele pamoja naye.4

Mtume (s.a.w.w.) alimwomba ami yake Abbas, aliyekuwa na sauti kuu mno, kuwaita Waislamu warudi kwa namna hii: “Enyi Ansar, mliomsaidia Mtume! Enyi mliokula kiapo cha utii kwa Mtume chini ya mti wa Peponi! Mnakwenda wapi? Mtume yuko hapa!” Maneno haya ya Abbas yaliyafikia masikio ya Waislamu na kuamsha moyo wa dini na nguvu. Mara moja wote wakaitika kwa kusema: “Labbayk! Labbayk” na wakarudi vitani kishujaa, wakimrudia Mtume (s.a.w.w.).

Mwito wa Abbas uliorudiwa rudiwa, uliobashiria usalama wa Mtume (s.a.w), uliwafanya wale watu wanaokimbia wamrudie Mtume (s.a.w.w.) kwa masikitiko yasiyo kifani na majuto na ukawafanya wazisimamishe safu zao upya. Kwa kuitika maamrisho ya Mtume (s.a.w.w.) na vile vile kulifuta lile doa lenye kuabisha la kuukimbia uwanja wa vita, Waislamu walifanya mashambulizi ya pamoja na kwa muda mfupi tu wakawalazimisha maadui kurudi nyuma au kukimbia. Ili kuwatia moyo Waislamu, Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akisema: “Mimi ni Mtume wa Allah nami kamwe sisemi uwongo na Allah ameniahidi ushindi.”

Mbinu hii ya kivita iliwafanya wapiganaji wa Hawaazin na Saqif kukimbilia kwenye eneo la Autas na Nakhlah na kwenye ngome za Taaif na kuwaacha wanawake wao na watu walioandamana nao na idadi kadhaa ya wale waliouawa katika vita hivyo.

Ngawira Za Vita

Katika vita hivi wale waliouawa katika upande wa Waislamu walikuwa wengi, lakini waandishi wa wasifu hawakuitaja idadi ya wale waliouawa. Hata hivyo, Waislamu waliweza kupata ushindi na maadui wakakimbia wakiacha nyuma yao mateka elfu sita, ngamia elfu ishirini na nne, kondoo elfu arobaini na Waqih5 elfu nne za fedha. Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha kwamba watu na mali zote vipelekwe Ji’raanah. Vile vile aliwateuwa watu fulani kuziangalia ngawira zile. Wale mateka waliwekwa kwenye nyumba maalum na Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha kwamba ngawira zote zibakie hapo zilipo hadi atakaporejea kutoka Taaif.

  • 1. Tabaqaatil-Kubra, Juz. 2, uk. 137.
  • 2. Tabaqaatil-Kubra, Juz. 2, uk. 150
  • 3. Maghaazil-Waaqidi, Juz. 3, uk. 897.
  • 4. Kwenye Maghaazil, Juz. 3, uk. 602, Waaqidi ameyataja baadhi ya matendo ya kijasiri ya Amirul-Mu’minin (a.s.) kwenye hali ile ngumu sana.
  • 5. Waqih moja ni karibuni sawa na gramu 213.