Sura Ya 50: Vita Vya Ta’if

Ta’if ni moja ya miji ya nchi ya Hijaz yenye ardhi yenye rutuba. Mji huu uko upande wa Kusini Mashariki mwa Makka yapata umbali wa ligi 12 (Kilomita 58). Mji huu uko meta elfu moja juu ya usawa wa bahari. Kutokana na hali ya hewa nzuri ya Ta’if, bustani na mashamba ya mitende, mji wa Taa’if ulikuwa ni kituo cha kundi moja la watu walioishi maisha ya raha mustarehe!

Mji huu ulikaliwa na kabila la Saqif lililokuwa moja ya makabila ya Kiarabu yenye nguvu na umaarufu. Waarabu wa kabila la Saqif walikuwa miongoni mwa watu wale waliopigana dhidi ya Uislamu kweye Vita vya Hunayn. Baada ya kushindwa vibaya walikimbilia kwenye mji wao wenye ngome madhubuti na zilizoinuka juu.

Ili kuukamilisha ushindi wa Hunayn, Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha ya kwamba wale watoro wa Vita vya Hunayn wafuatiliwe. Abu ‘Aamar Ash’ari na Abu Musa Ash’ari walipelekwa pamoja na kikosi cha askari wa Uislamu ili kuwafuatilia baadhi ya watoro waliokimbilia Awtaas. Yule kamanda wa kwanza (Abu Aamr Ash’ari) alipoteza uhai wake kwenye mapambano lakini yule wa pili (Abu Musa Ash’ari) alipata ushindi kamili na kuwatawanya maadui.1

Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe alikwenda Taa’if akifuatana na jeshi lililosalia2 na alipokuwa njiani aliivunja ngome ya Malik, (ambaye alivichochea vita vya Hunayn). Kwa kweli ubomoaji wa ngome ya Malik haukuchua mwelekeo wowote wa kulipiza kisasi. Bali alichokitaka Mtume (s.a.w.w.) kilikuwa kwamba asiiache sehemu inayoweza kutumika kama kimbilio la maadui.

Makundi ya jeshi la Uislamu yalisonga mbele, moja baada ya jingine na kuzifanya pande zote za mji kuwa sehemu za kupigia kambi zao. Ngome ya Taa’if ilikuwa kwenye sehemu ya mwinuko nayo ilikuwa na kuta madhubuti sana, na minara yake ya doria ililitawala eneo lote la nje. Jeshi la Uislamu lilikwenda kuizingira ngome ile, lakini ilikuwa bado haijazingirwa vya kutosha wakati maadui walipowazuia wasiendelee kwa mvua ya mishale na kuwauwa baadhi yao hapo hapo, mwanzoni kabisa.3

Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha lile jeshi lirudi nyuma na kuihamishia kambi yake kwenye sehemu isiyoweza kufikiwa na mishale ya maadui.4 Salmaan Muhammadi, ambaye mipango yake ya kijeshi iliwanufaisha Waislamu wakati wa Vita vya Handak, alimshauri Mtume (s.a.w.w.) kwamba ile ngome ya adui ipigwe mawe kwa kutumia mateo. Kwenye vita za siku zile teo ilifanya kazi inayofanywa na mizinga kwenye vita za siku zetu hizi. Maafisa wa Uislamu walitengeneza teo chini ya uongozi wa Salmaan na wakairujumu minara na sehemu za ndani za ngome ile kwa karibuni siku ishirini. Hata hivyo, maadui nao waliendelea kupiga mishale na hivyo wakawatia majeraha wale askari wa Uislamu.

Sasa hebu tuone jinsi Waislamu walivyotengeneza teo katika hali ile. Baadhi ya watu wanasema kwamba Salmaan yeye mwenyewe aliitengeneza na akawafunza askari wa Uislamu jinsi ya kuitumia, wengine wanaamini kwamba Waislamu waliipata silaha hii ya kijeshi wakati wa kutekwa Khaybar na wakaja nayo pale Taa’if.5 Si jambo lisilowezekana kwamba Salmaan yeye mwenyewe alitengeneza ile teo na akawafunza Waislamu jinsi ya kuijenga na kuitumia. Historia inatueleza kwamba hii haikuwa teo pekee waliyokuwa nayo Waislamu, kwa sababu sambamba na vita za Hunayn na Taa’if, Mtume (s.a.w.w.) alimpeleka Tufayl bin Amr Duwsi kuyabomoa mahekalu ya masanamu ya kabila la Duws. Alirejea baada ya kufaulu kuitimiza kazi aliyopewa na Mtume (s.a.w.w.) na akamjia Mtume (s.a.w.w.) huko Taa’if pamoja na askari mia nne, wote wakiwa ni wa kabila lake, pamoja na teo na gari la kijeshi.
Na kwenye vita hivi zana hizi za kijeshi alizokuwa amezipata Tufayl bin Amr Duwsi zikiwa ni ngawira za vita, nazo zikatumika.6

Kubomoa Ukuta Wa Ngome Kwa Kutumia Magari Ya Kijeshi

Ili kumfanya adui asalimu amri, ilikuwa muhimu kuishambulia ngome ile kutoka pande zote. Hivyo basi, iliamuliwa kwamba sambamba na usimikaji wa teo na kutupa mawe, magari ya kijeshi yatumike ili kuupasua ukuta wa ngome ile, ili lile jeshi la Uislamu liweze kuiingia. Hata hivyo, makundi ya askari wa Uislamu yalikabiliwa na ugumu mkubwa katika kuitimiza kazi hii, mishale ilitupwa vichwani mwao kutoka kwenye minara na kwenye sehemu nyingine za ngome ile, na hakuna yeyote aliyeweza kuukaribia ukuta ule.

Njia iliyokuwa bora zaidi ya kulifikia lengo hili ilikuwa ni ile ya kulitumia magari ya kijeshi yalilokuwa yakipatikana pamoja na majeshi yenye mipango mizuri ya zama zile katika maumbo ya kutokamilika.

Gari la kijeshi lilitengenezwa kutokana na mbao na lilifunikwa na ngozi nene nzito. Askari wenye nguvu walikaa humo na wakalisukuma kuelekea kwenye ngome ile na wakaanza kutoboa matundu kwenye ukuta, wakikingwa na gari hili. Kwa kutumia zana hii ya kijeshi askari wa Uislamu wakajishughulisha kishujaa katika kuuangusha ule ukuta. Hata hivyo, maadui walimwaga chuma na nyaya zilizoyeyushwa kwenye lile gari na kukichoma kile kifuniko chake na kuwajeruhi wale askari. Hivyo basi, mbinu hii ya kijeshi ilithibitika kwamba si yenye kufaulu kutokana na mipango ya adui, na Waislamu walishindwa kupata ushindi. Hivyo basi, wakati idadi fulani ya Waislamu ikiwa imejeruhiwa na kuuwawa, waliliacha jaribio lao hili.7

Pigo La Kiuchumi Na Kihamasa

Kupata ushindi hakutegemei zana za kijeshi za kimaada tu. Kamanda stadi anaweza kuimaliza nguvu ya adui kwa kupiga pigo la kiuchumi na kihamasa na kwa njia hii anaweza kumfanya asalimu amri. Mara kwa mara sana mapigo ya kiuchumi na kihamasa yanathubutu kuifanya kazi vizuri kuliko majeraha ya mwili ambayo mara kwa mara askari wa adui huyapata. Taa’if ilikuwa eneo la mitende na mizabibu na ulikuwa mji maarufu nchini Hijaz mwote kwa rutuba yake. Kwa kuwa wakazi wa mji huu walikuwa wamefanya kazi kubwa katika kuyaendeleza mashamba ya mitende na mizabibu, walikuwa makini mno katika usalama wao.

Ili kuwaogofya wale waliojifungia ndani ya ngome ile, Mtume (s.a.w.w.) alitangaza kwamba, kama wakiendelea kufanya upinzani bustani zao zitatekwa ngawira. Hata hivyo wale maadui hawakuisikiliza kauli ile ya kutishia, kwa sababu hawakufikiria kwamba yule Mtume (s.a.w.w.) aliye mpole na mwenye huruma angaliweza kufanya vile. Hata hivyo, kama walivyoona, kwa ghafla tu kwamba utekelezaji wa amri ya Mtume (s.a.w.w.), ya kuzikata zile bustani na kuangushwa mitende na zile zabibu ilikuwa tayari imeshaanza. Watu wa Taa’if wakaanza kulia na kupiga makelele na wakamwomba Mtume (s.a.w.w.) asifanye vile, ikiwa ni ishara ya heshima kwa ukaribu na uhusiano uliokuwako baina yao.

Licha ya ukweli kwamba wale waliokimbilia kwenye ngome ile walikuwa ni watu wale wale waliohusika na Vita vya Hunayn na Taa’if, na vita hivi viwili vimetokea kutia hasara kubwa, lakini Mtume (s.a.w.w.) alionyesha tena ukarimu na upole kwenye uwanja wa vita, mahali ambapo kwa kawaida ni uwanja wa maonyesho ya ghadhabu na kulipiza kisasi. Aliwaamrisha masahaba zake kuacha kuikata ile miti.

Ingawa alikuwa kapoteza maafisa na askari wengi kwenye vita hizi mbili (ambazo zilisababishwa na makri za watu wa kabila la Saqif walioendesha mashambulizi ya usiku dhidi ya jeshi la Uislamu na sasa wamekimbilia kwenye pango lao kama mbweha), na ingekuwako haki ya kuyaangamiza mashamba na bustani zao ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi, lakini upole na huruma zake viliishinda ghadhabu yake na akawaomba marafiki zake wajiepushe na vitendo vya kuadhibu.

Kutokana na tabia za Mtume (s.a.w.w.) na jinsi ambayo daima alikuwa akiwatendea maadui zake, tunaweza kusema kwamba amri alizozitoa za kukata ile miti zilikuwa tishio tu na kama silaha hii isingelifaa, bila shaka angelijizuia kuitumia.

Mkakati Wa Mwisho Katika Kuiteka Ile Ngome Ya Taa’if

Watu wa kabila la Saqif walikuwa matajiri na wakwasi nao walimiliki idadi kubwa ya watumwa na wajakazi. Ili kupata taarifa juu ya hali ya mambo ndani ya ile ngome na kuweza kuitathimini nguvu ya adui pamoja na kujenga mfarakano miongoni mwa kundi lile lililokuwa na utaratibu mwema, Mtume (s.a.w.w.) alituma itangazwe kwamba wale watumwa wa adui watakaotoka mle ngomeni na wakakimbilia kwenye jeshi la Uislamu watakuwa waungwana huru. Mbinu hii ilifanya kazi kwa kiasi fulani, na kiasi cha watumwa ishirini walitoroka kwenye ile ngome kwa ustadi mkubwa na kujiunga na Waislamu. Walipoulizwa, ilifahamika kwamba wale waliokuwamo kwenye ile ngome hawakuwa tayari kusalimu amri kwa vyovyote vile, japo kule kuzingirwa kwa ngome ile kungeliendelea kwa mwaka mzima wasingekabiliwa na upungufu wa chakula hata kidogo.

Jeshi La Uislamu Larejea Madina

Mtume (s.a.w.w.) alizitumia mbinu zote za kimwili na za kiakili za kivita katika vita hivi, lakini uzoefu alioupata hapo ulithibitisha kwamba kuiteka ngome ile kulihitaji matendo ya ziada na subira, ambapo hali iliyokuwapo wakati ule, kurefuka kwa vita na nguvu za jeshi la Uislamu, havikuruhusu kuendelea kukaa pale Taa’if, kwa sababu, kwanza kabisa kwenye kipindi cha uzingiraji huu watu kumi na watatu waliuawa, miongoni mwao watu saba walitoka miongoni mwa Waquraishi, wanne walikuwa Ansar na wawili walikuwa wa makabila mengine. Aidha, baadhi ya watu ambao kwa bahati mbaya idadi na majina yao havikurekodiwa vitabuni, waliuawa nao pia kutokana na mashambulizi ya hila ya adui kule kwenye bonde la Hunayn, na matokeo yake yakawa kwamba kulitokea utovu wa nidhamu na kukosa moyo wa kuendelea na vita kwenye jeshi la Waislamu.

Pili, mwezi wa Shawwal ulikuwa unamalizika na mwezi wa Dhil-Qaad (ambao kupigana vita humo kumeharimishwa miongoni mwa Waarabu na baadaye Uislamu nao uliithibitisha desturi hii) ulikuwa ukija mbiombio.8

Ili kuihami desturi hii, ilikuwa muhimu kwamba kule kuzingira kukome mapema iwezekanavyo ili kwamba, lile kabila la Kiarabu la Bani Saqif liseweze kumlaumu Mtume (s.a.w.w.) kwa kosa la kuivunja desturi ile iliyo njema.

Aidha, majira ya Hija yalikaribia, na ukaguzi wa ibada za Hija ulikuwa ni jukumu la Waislamu, kwa sababu kabla ya hapa ibada zote za Hija zilikuwa zikiendeshwa chini ya uongozi wa washirikina wa Makka. Idadi kubwa sana ya watu walikuja Makka kutoka kwenye sehemu zote za Uarabuni kuja kushiriki kwenye ibada ya Hija na huu ulikuwa wakati muafaka zaidi kuuhubiri Uislamu na kuwazoeza watu ukweli wa hii dini ya Allah.

Ilikuwa muhimu kwamba Mtume (s.a.w.w.) aitumie kikamilifu nafasi hii aliyoipata kwa mara ya kwanza, na ayafikirie mambo yaliyo muhimu zaidi yalinganishwapo na kule kutekwa kwa ngome ile. Kwa kuyazingatia mambo yote hayo, Mtume (s.a.w.w.) aliukomesha yale mzingiro wa Taa’if na akaenda Jiraanah pamoja na askari wake.

Matukio Ya Baada Ya Vita

Vita vya Hunayn na Taa’if viliahirishwa na bila ya kupata matokeo ya mwisho, Mtume (s.a.w.w.) akaenda Ji’raanah kwenda kuzigawa ngawira za Vita vya Hunayn.

Ngawira walizozipata Waislamu kwenye vita ya Hunayn zilikuwa nyingi kuliko ngawira walizopata Waislamu mwenye Vita vyovyote vile vingine, kwa sababu Mtume (s.a.w.w.) alipofika Ji’raanah alikuwa na wafungwa

6000, ngamia 24,000 zaidi ya kondoo 40,000 na fedha gramu 852 za fedha,9 na kwenye siku zile sehemu ya gharama za jeshi la Uislamu vilevile zilipatikana kutokana na chanzo hiki cha mapato.

Mtume (s.a.w.w.) alikaa pale Ji’raanah kwa muda wa siku kumi na tatu. Kwenye kipindi hiki alijishughulisha na ugawaji wa ngawira za vita kwa njia maalum akiwaachilia baadhi ya wafugwa na kuwarejesha kwa ndugu zao; akitengeneza mpango kwa ajili ya kusalimu amri na kusilimu kwa Malik ibn Awf (yule mtu ambaye aliwajibika moja kwa moja na vita vya Hunayn na Taa’if); akionyesha moyo wa kuridhika na kushukuru kwa huduma zilizotolewa na watu mbalimbali; akizivutia, kwa sera zake za hekima, nyoyo za maadui wa Uislam kwenye dini hii ya haki; na kumaliza, kwa njia ya hotuba ya kuvutia, mgogoro ambao ulikuwa umezuka baina yake na kikundi cha Ansari.

Haya hapa ni maelezo ya masuala yaliyotajwa hapo juu:

1. Moja ya sifa zilizojitokeza zaidi za Mtume (s.a.w.w.) ilikuwa kwamba katu hakuzibeua huduma walizozitoa watu au haki zao, japo ziwe ndogo kiasi gani. Na kama mtu yeyote yule akimpatia huduma alimfidia kwa ajili ya huduma ile kwa kiasi kilichosawa nayo. Mtume ameutumia muda wa utotoni mwake miongoni mwa kabila la Bani Sa’ad lililokuwa tawi la Khawaazin, na Bibi Halima Sa’adiyah alimnyonyesha na amemlea kwenye kabila lake kwa kipindi cha miaka mitano.

Kabila la Bani Sa’ad ambalo lilishiriki katika vita vya Hunayn dhidi ya Uislamu, idadi fulani ya wanawake na watoto wao pamoja na mali zao viliangukia mikonini mwa Waislamu, sasa walikuwa wakijuta kwa kile walichokitenda. Hata hivyo, walikuwa wakifikiria akilini mwao kwamba Muhammad amekulia kwenye kabila lao na amelelewa na wanawake wao, na kwa kuwa yu mpole, mwema na mtu mwenye shukrani, bila shaka atawaachia wafungwa wao kama atakumbushwa kuhusu utotoni mwake. Hivyo basi, machifu kumi na wanne wa kabila lile ambao wote walikuwa wamesilimu, walimjia Mtume (s.a.w.w.). Waliongozwa na watu wawili, mmoja wao alikuwa ni Zuhayr bin Sard na mwingine alikuwa ni mjomba wa kunyonyeshwa wa Mtume (s.a.w.w.) na walisema hivi:

“Miongoni mwa hawa wafungwa wamo mama zako wa kunyonyesha, na dada zako wa kunyonyeshwa pamoja na wale waliokuhudumia wakati wa utoto wako, na upole na huba huhitaji kwamba kuzingatia haki walizonazo baadhi yao juu yako, huna budi kuwaachia mateka wetu wote, ikiwa ni pamoja na wanawake, wanaume na watoto. Na kama tungeliyapeleka maombi haya kwa Nu’waan bin Munzir au Harith bin Abi Shamir, mtawala wa Iraq na Shamu, tungelitegemea kukubaliwa kwa maombi haya na viongozi hawa, achilia mbali wewe uliye kigezo cha upole na huba.”

Akijibu ombi hili, Mtume (s.a.w.w.) aliwauliza: “Je, ni kitu gani mnachokithamini zaidi, wanawake na watoto wenu, au mali zenu?” Walimjibu wakisema: “Hatutawabadilisha wanawake wetu na watoto wetu kwa kitu chochote.” Mtume akasema: “Niko tayari kusamehe fungu langu pamoja na lile la dhuria wa Abdul Muttalib, lakini mafungu ya Muhajiriin, Ansar na Waislamu wengine yanawahusu wao wenyewe na ni muhimu kwamba wao wenyewe wazisamehe haki zao. Nitakapomaliza kusali sala ya Adhuhuri msimame baina ya safu za Waislamu na mseme nao hivi: “Tunamfanya Mtume kuwa mwombezi wetu mbele ya Waislamu na kuwafanya Waislamu kuwa waamuzi wetu mbele ya Mtume ili tuweze kurudishiwa wanawake na watoto wetu.” Wakati huo huo, mimi nitasimama na kukurudishieni fungu langu pamoja na lile fungu la dhuria wa Abdul Muttalib na vilevile nitawashauri wengine kufanya vivyo hivyo.”

Wale wajumbe wa Haazin walizungumza na Waislamu baada ya sala ya Adhuhuri kama walivyoshauriwa na Mtume (s.a.w.w.) na Mtume (s.a.w.w.) aliwapa zawadi lile fungu lake pamoja na lile la dhuria wa Abdul Muttalib. Wakimfuatisha Mtume (s.a.w.w.), Muhajiriin na Ansar nao walikubali kuyasamehe mafungu yao. Hata hivyo, ni watu wachache tu kama vile Aqra’ bin Haabis na ‘Uyainah bin Hisn Fazaari waliokataa kutoa mafungu yao. Mtume (s.a.w.w.) aliwaambia hao: “Kama mkiwatoa wafungwa wenu nitakupeni wafungwa sita kwa kila mfungwa mmoja mumtoaye, kutokana na wafungwa watakaoangukia mikononi mwangu katika vita ya kwanza vitakayopiganwa baada ya hapa.”10

Hatua za kivitendo alizozichukua Mtume (s.a.w.w.) na maneno yake ya kuvutia yalifikisha kwenye kuachiliwa kwa wafungwa wote wa kabila la Bani Hawaazin ila ajuza mmoja ambaye ‘Uyainah alikataa kumwachilia. Hivyo basi, kitendo chema na cha uchamungu ambacho msingi wake ulijengwa na Bibi Halimah Sa’adiyah miaka sitini iliyopita kwenye kabila la Bani Sa’ad, kilizaa matunda baada ya miaka mingi kama matokeo yake, wafungwa wote wa kabila la Bani HawAzin waliachiwa huru. Kisha Mtume (s.a.w.w.) alimwita Shaymah, Dada yake wa kunyonya na baada ya kulitandaza joho lake chini, alimfanya akae juu yake na akamwuliza kuhusu hali ya ustawi wake pamoja na wa familia yake.11 Kwa kuwaachilia wafungwa wao, Mtume aliwafanya watu wa kabila la Bani Hawaazin wauelekee Uislamu. Hivyo basi, wote walisilimu kwa moyo mmoja na matokeo yake yakawa kwamba, Taa’if nayo vilevile ikampoteza mshiriki wake wa mwisho.

Malik Bin ‘Awf Asilimu

2. Wakati uleule Mtume (s.a.w.w.) alipata nafasi ya kutatua suala la Malik, kupitia kwa wajumbe wa Bani Sa’ad, yule chifu mwenye kichwa kigumu wa kabila la Nasr aliyevichochea vita vya Hunayn, na hatimaye akamvutia kwenye Uislamu. Kuhusiana na jambo hili, aliulizia kuhusu hali ya mambo yake na alielezwa kwamba, yeye (Malik) amekimbilia Taa’if na kwamba alikuwa akishirikiana na Bani Saqif. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Mfikishieni salamu zangu kwamba kama akisilimu na kujiunga na sisi, nitawaachia watu wake na vilevile nitampa ngamia mia moja.” Wale wajumbe wa Bani Hawaazin walimfikishia Malik ujumbe wa Mtume (s.a.w.w.). Malik alitambua kwamba nguvu ya Bani Saqif imedhoofika na vilevile alitambua kuongezeka kwa nguvu za Uislamu kunakoendelea kila uchao. Hivyo basi, aliamua kuondoka Taa’if na kwenda kujiunga na Waislamu.

Hata hivyo, alikuwa akichelea kwamba kama Bani Saqif watautambua uamuzi wake ule, watamzuia mle mwenye ngome yao. Hivyo basi aliunda mpango fulani. Aliagiza kwamba awekewe kitundu cha kupakia mtu juu ya ngamia kwenye sehemu iliyokuwa mbali na Taa’if. Baada ya kuifikia sehe- mu ile alimpanda ngamia wake na akaenda upesi sana hadi pale Ji’raanah na akasilimu. Mtume (s.a.w.w.) akamtendea kama alivyokwisha kuahidi na baadae alimteua kuwa kiongozi wa Waislamu wa makabila ya Bani Nasr, Bani Thamaalah na Bani Salimah. Kutokana na heshima na hadhi yake aliyoipata kutoka kwenye upande wa Uislamu, aliyafanya maisha kuwa mabaya kwa watu wa kabila la Bani Saqif na akawatia katika dhiki ya kiuchumi.
Malik aliona haya kutokana na ule upole aliotendewa na Mtume (s.a.w.w.) na akazisoma beti fulani fulani za mashairi akiusifu utukufu wake: “Mimi sijapata kuona au kusikia miongoni mwa wanadamu wote, mtu yeyote awezaye kuwa kama Muhammad!”12

Kugawanywa Kwa Ngawira Za Vita

3. Masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) walishikilia ya kwamba zile ngawira za vita zigawanywe mapema iwezekanavyo. Ili Mtume (s.a.w.w.) kuthibitisha kutokuwa kwake na mvuto na jambo lile, alisimama ubavuni mwa ngamia, akachukua kiasi fulani cha sufu kutoka kwenye nundu yake na akiwa ameibana katikati ya vidole vyake, aliwageukia watu na kusema: “Mimi sina haki yoyote kwenye ngawira zenu, hata kwenye sufu hii, ila hiyo ‘Khums’ niliyo na haki nayo. Hivyo kila mmoja wenu naarudishe kila aina ya ngawira, japo iwe ni sindano na uzi, ili kwamba igawanywe miongoni mwenu kwa usawa.”

Mtume (s.a.w) aliigawa mali yote iliyokuwamo kwenye hazina miongoni mwa Waislamu na pia aliigawa ‘Khums’ yake iliyokuwa fungu lake miongoni mwa machifu wa Waquraishi waliosilimu karibuni tu. Alimpa kila mmoja wao ngamia mia moja, ikiwa ni pamoja na Abu Sufyan, mwanawe Muawiyah, Hakim bin Hizaam, Harith bin Harith, Harith bin Hisham, Suhayl bin ‘Amr, Huwaytab bin Abdul ‘Uzzaa, Alaa bin Jaariyah na wengineo, wote wakiwa machifu wa kufuru, ushirikina na maadui wakuu wa Uislamu hadi kwenye siku chache tu zilizopita.

Kwa watu wa kundi jingine ambao cheo chao kilikuwa chini ya kile cha wale tuliowataja hapo awali, kila mtu alipata ngamia hamsini. Kutokana na zawadi hizi kubwa kubwa na mafungu maalum, watu hawa walianza kuwa na hisia za huba na upendo kwa Mtume (s.a.w.w.), lakini pia walivutika na Uislamu. Katika sheria za Kiislamu, watu wa aina hii huitwa ‘Mu’allafatul Qulubi’ (Wale ambao yahitajika kuwatia moyo) na moja ya malengo ambayo ‘Zaka’ yaweza kutumiwa ni matumizi juu yao.13

Ibn Sa’ad anasema: “Zawadi zote hizi zilitolewa kutokana na khums iliyokuwa mali ya Mtume (s.a.w.w.) na haikuwapo japo dinari moja iliy- otumiwa kutokana na mafungu ya watu wengine kwa ajili ya kuwatia moyo watu wa kundi hili.”14

Zawadi na matumizi haya aliyoyaruhusu Mtume (s.a.w.w.) zilikasirikiwa mno na baadhi ya Waislamu na hasa baadhi ya Ansar.

Wale ambao kwamba hawakuweza kuyatambua maslahi makubwa aliyoyazingatia Mtume (s.a.w.w.) katika kuzitoa zawadi hizi, walifikiria kwamba mahusiano ya udugu yamemsukuma kuigawa ile Khums ya ngawira ile miongoni mwa ndugu zake. Mtu mmoja aliyeitwa Zul Khuwaysirah wa kabila la Bani Tamim alionyesha ufidhuli mwingi mno kiasi kwamba alimwambia Mtume (s.a.w.w.): “Leo nimeyachunguza matendo yako kwa makini sana, na nimeona kwamba hukuwa mwadilifu katika kuzigawa ngawira.” Mtume (s.a.w.w.) alichukizwa alipoyasikia maneno yake.

Dalili za hasira zilijitokeza usoni mwake, na akasema: “Ole wako! Kama mimi sifanyi uadilifu na haki, basi ni nani mwingine awezaye kufanya hivyo?” Khalifa wa pili alimwomba Mtume amruhusu amwue mtu yule, lakini Mtume (s.a.w.w.) alisema: “Mwache. Hapo baadae atakuwa kiongozi wa kikundi kitaka- choutoka Uislamu kwa jinsi ile ile ambayo mshale huutoka upinde.”15

Kama alivyotabiri Mtume (s.a.w.w.), mtu huyu alikuwa kiongozi wa Khawarij (wenye kuritadi) wakati wa utawala wa Sayyidna Ali (a.s.) na akautwaa uongozi wa kikundi kile hatari. Hata hivyo, kwa vile ni kinyume na misingi ya Uislamu kwamba adhabu itolewe kabla ya kutendeka kosa, Mtume (s.a.w.w.) hakuchukua hatua yoyote dhidi yake.

Akiwawakilisha Ansar, Sa’ad bin Ubaadah alizifikisha huzuni zao kwa Mtume (s.a.w.w.), ambapo Mtume (s.a.w.w.) alimwambia: “Wakusanye wote mahali pamoja ili niwaeleze jambo hili.” Mtume (s.a.w.w.) aliwasili kwenye ule mkutano wa Ansar kwa heshima kubwa na aliwahutubia akisema: “Mlikuwa kundi la watu waliopotoka, nanyi mmepata mwongozo kupitia kwangu mimi. Mlikuwa maskini nanyi mkawa matajiri. Mlikuwa maadui nanyi mkawa marafiki.” Wote wakasema: “Ewe Mtume wa Allah! Yote hayo ni sawa.”

Kisha Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Mnaweza kunijibu kwa njia nyingine vile vile na kinyume na huduma zangu na mnaweza kutaja haki mlizonazo juu yangu na mnaweza kusema: “Ewe Mtume wa Allah! Waquraishi walipokukataa, sisi tulikutambua. Hawakukusaidia, nasi tumekusaidia. Walikufanya usiyekuwa na hifadhi yoyote, nasi tulikupa kimbilio, ulikuwapo wakati ambapo wewe hukuwa na hata senti moja, nasi tukakusaidia.”

Enyi kundi la Ansar! Kwa nini mlihuzunika kwa sababu nimewapa Waquraishi mali kidogo ili waweze kuwa imara kwenye Uislamu na nimekupeni Uislamu? Je, hamridhiki kwamba watu wengine wachukue ngamia na kondoo ambapo ninyi mumchukue Mtume pamoja nanyi? Ninaapa kwa jina la Allah! Kama watu wengine wakiifuata njia fulani, na Ansari wakaifuata njia nyingine isiyokuwa ile, mimi nitaifuata ile njia waliyoifuata Ansar.”

Baada ya hapo Mtume (s.a.w.w.) aliwaombea Ansar na watoto wao baraka za Allah. Maneno ya Mtume (s.a.w.w.) yaliziibua mno hisia zao kiasi kwamba wote walianza kulia, na wakasema: “Ewe Mtume wa Allah! Tumetosheka na mafungu yetu (tuliyopata) nasi hatuna malalamiko japo yaliyo madogo mno juu ya jambo hili.”

 • 1. Maghaazil-Waaqidi, Juz. 3, uk. 915-916.
 • 2. Bihaarul-An’waar, Juz. 21, uk. 162.
 • 3. Siiratu-Halabi, Juz. 3, uk. 132.
 • 4. Tabaaqatil-Kubra, Juz. 2, uk. 158.
 • 5. Siiratu-Halabi, Juz.3, uk. 134.
 • 6. Tabaaqatil-Kubra, Juz. 2, uk. 157.
 • 7. Maghaazil-Waaqidi, Juz. 3, uk. 928.
 • 8. Kauli hii inaungwa mkono na ukweli uliokuwapo kwamba Mtume (s.a.w.w.) alitoka Makka mnamo tarehe 5, Shawwal na kipindi cha kuzingira kilikuwa ni siku 20 na siku tano za mwezi huu zilizosalia zilitumiwa kwenye Vita vya Hunayn na katika kusafiri. Ama kuhusu kile kipindi cha kuzingira, kuwa siku 20, ni kwa mujibu wa masimulizi aliyoyanukuu Ibn Hishamu. Hata hivyo, Ibn Sa’ad ameki- taja kipindi cha mzingiro kuwa ni siku 40 (Tazama Tabaqaatil-Kubra, Juz. 2, uk.
 • 9. Tabaqaatil-Kubra, Juz. 2, uk 152.
 • 10. Maghaazil-Waaqidi, Juz. 3, uk. 949-953.
 • 11. Tabaaqatil-Kubra, juz. 2, uk 153-154; Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 49.
 • 12. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 491.
 • 13. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 3, uk. 493.
 • 14. Tabaqaatil-Kubra, Juz. 3, uk. 153.
 • 15. Maghaazi anasema kwamba Mtume (s.a.w.w.) alizungumzia juu yake (yaani Zul Khuwaysirah) kuwa: “Atakuwa na marafiki ambao ibada zao zilinganishwa na sala na funga zako, basi hizo sala na funga zako vitakuwa vichache mno. Wataisoma Qur’ani, lakini usomaji wao hauyavuka mitulinga yao. Watatoka nje ya dini ya Uislamu kama vile mshale ukimbiavyo upinde.” (Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 496).