Sura Ya 51: Hotuba Maarufu Ya Wasifu Ya Ka’ab Bin Zuhayr

Kijana Mdogo Awa Gavana Wa Makka

Katikati ya mwezi Dhul Qa’ad ya mwaka wa nane wa Hijiriya, Mtume (s.a.w.w.) alizitoa ngawira zote za Hunayn pale Ji’raanah. Siku za Hija zilikuwa zikikaribia upesi upesi na huu ulikuwa ni mwaka wa kwanza ambao Waarabu washirikina na Waislamu walikuwa wafanye ibada za Hija pamoja chini ya ukaguzi wa serikali ya Kiislamu ya Makka. Kushiriki kwa Mtume (s.a.w.w.) kwenye ibada hizi kutaongezea fahari na utukufu wa Hija, na ilikuwa chini ya mwongozo wake wenye hekima kwamba utangazaji wa kweli na wa msingi wa Uislamu ungelifanyika kwenye ule mkusanyiko mkubwa wa watu.

Hata hivyo vilevile ilimbidi Mtume (s.a.w.w.) azifanye kazi fulani kule makao makuu (Madina), kwa sababu baada ya miezi mitatu ya kuondoka kwake mahali pale, mambo yaliyombidi ayaangalie yeye mwenyewe binafsi yalibaki bila kushughulikiwa kabisa.

Hivyo basi baada ya kuchunguza ubaya na uzuri wote wa jambo hili, Mtume (s.a.w.w.) aliona kwamba ingelifaa kutoka Makka baada ya kufanya Umrah na afike Madina upesi iwezekanavyo.

Ilikuwa muhimu kwamba awateue baadhi ya watu wa kuyatawala mambo ya kisiasa na kidini ya lile eneo lililotekwa hivi karibuni tu, ili kwamba isitokee migogoro wakati akiwa hayupo na mambo ya eneo lile yaweze kutawaliwa vizuri. Kwa kuzingatia hili, alimteua kijana aliyekuwa mvumilivu na mwenye hekima aliyeitwa Ataab bin Usayd, ambaye wakati ule umri wake ulikuwa bado haujazidi miaka ishirini, kuwa gavana wa Makka kwa kumlipa mshahara wa kila mwezi wa dirhamu moja.

Hivyo basi kwa kumpa ugavana kijana ambaye ndio kwamba kasilimu, na kwa kule kumpendelea kijana yule kuliko watu wazima wengi, alikiondoa kizuizi cha hofu isiyokuwa na msingi na akathibitisha kivitendo kwamba kushika ofisi za Umma hutegemea uwezo tu, na umri mdogo usimzuie mtu kukifikia cheo na ofisi ya juu kabisa ya umma. Yule gavana wa Makka aliuhutubia mkutano mkubwa na akawaambia watu: “Mtume ameweka kiwango cha mshahara wangu, basi kuhusiana na jambo hili, mimi si mhitaji wa zawadi au msaada wenu.”1

Uchaguzi mwingine mzuri aliofanya Mtume (s.a.w.w.) ni kwamba alimteua Mu’aaz bin Jabal kuwasomesha watu Qur’ani na sheria za Uislamu. Yeye alikuwa mtu maarufu miongoni mwa masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) kwa elimu yake ya Qur’ani, fiqhi, na maamrisho ya Uislamu. Mtume (s.a.w.w.) alipomtuma kwenda Yaman, kwenda kuwa hakimu huko, Mtume (s.a.w.w.) alimwuliza: “Utategemea nini katika kutatua kutoelewana baina ya watu?” Alimjibu akisema:

“Kitabu cha Allah, Qur’ani.” Mtume (s.a.w.w.) alimwuliza: “Je, kama hakuna uamuzi maalumu upatikanao kwenye Kitabu cha Allah kuhusiana na jambo lihusikalo, utahukumu chini ya msingi gani? “ Alijibu akisema: “Nitahukumu kwa mujibu wa hukumu za Mtume wa Allah (s.a.w.w.). Kwa kuwa mimi nimezishuhudia hukumu zako kwenye mambo mbalimbali na ninazikumbuka. Kama likitokea jambo lifananalo na lile ambalo wewe umelitolea hukumu, nitaitumia hukumu ile na kuhukumu kama ulivyohukumu wewe.”

Mtume (s.a.w.w.) akamwuliza kwa mara ya tatu: “Ni njia ipi utakayoifuata endapo litatokea tatizo ambalo hakuna hukumu ya dhahiri kwenye Kitabu cha Allah wala kwenye hukumu zangu?” Alijibu, akisema: “Katika mambo ya aina hiyo, nitatumia Ijtihad (njia ya kuzifasiri sheria za kiislamu) na kutoa uamuzi kwa msingi wa Qur’ani Tukufu na Ahadith zako kwa usawa na uadilifu.” Hapo Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Na ashukuriwe Allah kwamba, Amemwezesha Mtume wake kumchagua mtu wa kutawala kwa uadilifu, ambaye matendo yake yanalingana na mapenzi Yake.”2

Hadith Ya Ka’ab Bin Zuhayr Bin Abi Sulma

Zuhayr bin Abi Sulma alikuwa mmoja wa mshairi wa Zama za Ujinga aliyeandika moja ya Mu’allaqaat (yaani kazi za kishairi bora zaidi) saba zilizobakia zimening’inizwa kwenye kuta za Ka’abah kwa muda mrefu kabla ya kushushwa kwa Qur’ani, nazo zilikuwa chanzo cha fahari na utukufu katika fasihi ya ulimwengu wa Waarabu. Zuhayr alifariki dunia kabla ya kuanza kwa Utume wa Mtume (s.a.w.w.), na akaacha wana wawili walioitwa Buhayr na Ka’ab. Buhayr alikuwa mfuasi mwaminifu wa Mtume (s.a.w.w.), lakini Ka’ab alikuwa akifikiriwa kwamba yu mmoja wa maadui zake wakali. Kwa vile alijaaliwa kipaji chenye nguvu cha kurithi, (yaani ushairi – kutoka kwa mzazi) alimzulia na kumtusi Mtume (s.a.w.w.) kwenye mashairi yake na akawachochea watu kuamka dhidi Uislamu.

Mtume (s.a.w.w.) aliwasili Madina mnamo mwezi 24 Dhil-Qa’ad. Buhayr yule nduguye Ka’ab alikuwa amefuatana na Mtume (s.a.w.w.) wakati wa kuuteka mji wa Makka na kuzingiwa kwa Taa’if vilevile pamoja na wakati wa kurejea kwake Madina.

Aliona kwamba Mtume (s.a.w.w.) aliwatishia kifo washairi fulani fulani waliokuwa na kashfa kama yule ndugu yake, na waliowachochea watu kuupinga Uislamu, na ametangaza damu yao kuwa ni halali na hatimaye mmojawao aliuawa na wengine wawili walikimbilia kwenye sehemu zisizojulikana.
Buhayr alimwandikia barua nduguye Ka’ab akimwarifu hali ile na mwishoni mwa barua ile ikiwa ni dalili ya kumtakia wema, alitaja kwamba kama akiendelea kuwa adui kwa Mtume (s.a.w.w.), basi atayapoteza maisha yake, lakini kama akija kwa Mtume (s.a.w.w.) na kudhihirisha kuyajutia kwake matendo yake, atasamehewa, kwa sababu Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na tabia za kuyakubali maombi ya msamaha na majuto ya wakosefu na hatimae kuwasamehe.
Ka’ab aliyekuwa na imani thabiti juu ya ndugu yake, alikuja Madina. Alipowasili kwenye Masjidun-Nabi, Mtume (s.a.w.w.) alikuwa yu tayari kwa kusali sala ya Alfajiri. Ka’ab akasali kwa mara ya kwanza pamoja na Mtume (s.a.w.w.). Kisha alikwenda na kukaa ubavuni pake na kuuweka mkono wake mkononi mwake Mtume (s.a.w.w.), na kusema: “Ewe Mtume wa Allah! Ka’ab anaona haya mno na yu mwenye kuyajutia matendo yake na hivi sasa amekuja kusilimu. Je, utayakubali maombi yake ya msamaha kama akikujia mbele yako yeye mwenyewe?” Mtume (s.a.w.w.) alimjibu akisema: “Ndio.” Baada ya hapo Ka’ab akasema: “Mimi ndimi Ka’ab bin Zuhayr mwenyewe.”

Ili kuyasahihisha matusi na masengenyo ya tangu kale, Kaab alikuwa tayari kaishatunga maneno ya wasifu wa kifasaha akimsifu Mtume (s.a.w.w.).3 Aliyasoma maelezo hayo ya wasifu mle msikitini mbele ya Mtume (s.a.w.w.) na masahaba zake. Wasifu huu mzuri sana ni kazi ya sanaa mahiri kabisa miongoni mwa hotuba za wasifu za Ka’ab. Tangu siku uliposomwa mbele ya Mtume (s.a.w.w.) Waislamu wamekuwa wakiukariri na kuueneza miongoni mwa watu wengine. Wanachuoni wa Kiislamu nao wameandika sherehe (mafafanuzi) yake. Wasifu huu uliandikwa kwa mtindo wa ‘Laamiyah4 nao una beti hamsini na nane.

Kama wale washairi wa zama za Ujinga waliozianza sifa zao kwa kuwataja wapenzi wao au kwa kuyataja magofu ya minara, yeye anaanza wasifu wake kwa kumkumbuka binamu na mpenzi wake Sa’ad. Alipoifikia hatua ya kutubia kwa ajili ya matendo yake ya kale yaliyokuwa mabaya, anasema: “Nimearifiwa ya kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu amenitishia, ambapo kile kitakiwacho kutoka kwake ni msamaha na maghfira.” Na kisha anasema: “Mtume yu mshumaa uwakao, ambao chini ya mwanga wake watu hupata mwongozo moja kwa moja, naye yu ‘upanga uliofutwa’ wa Allah ambao daima ni wenye kushinda.”

Huzuni Iliyochanganyika Na Furaha

Mwishoni mwa mwaka wa 8 Hijiriya, Mtume (s.a.w.w.) alimpoteza binti yake mkubwa Zaynab.5 Zaynab alikuwa kaolewa na mwana wa mama yake mkubwa (au mama yake mdogo) aliyeitwa Abul Aas, kabla ya kuanza kwa Utume wa Mtume (s.a.w.w.), naye alikuwa akitangaza kumwanini kwake baba yake mara tu baada ya kuanza kwa Utume. Hata hivyo, mumewe aliendelea kuwa mshirikina na akashiriki kwenye vita vya Badr dhidi ya Uislamu na akatekwa.

Mtume (s.a.w.w.) alimwachilia kwa sharti la kwamba akamlete Zaynab Madina. Abul Aas aliitimiza ahadi yake na akampeleka Zaynab Madina lakini machifu wa Waquraishi walimtuma mtu mmoja aende akamrudishe, na mtu huyo alimrudisha Zaynab alipokuwa njiani akienda Madina. Yule mtu aliyetumwa alifaulu kufika karibu na kitundu cha ngamia aliyekuwa akisafiria Zaynab mle njiani na akauchoma mkuki wake kwenye kile kitundu alimokuwamo Zaynab.

Kutokana na hofu iliyokithiri, yule binti wa Mtume (s.a.w.w.) asiyekuwa na ulinzi aliharibu mimba mle njiani. Hata hivyo hakukata tamaa kuhusu kwenda Madina, na alifika kule katika hali ya ugonjwa. Aliitumia sehemu iliyosalia ya maisha yake akiwa yu mgonjwa na akafariki dunia mwishoni mwa mwaka wa 8 Hijiriya.

Huzuni ile iligeuka kuwa furaha, kwa sababu mwishoni mwa mwaka uleule Mtume (s.a.w.w.) alijaaliwa kupata mwana kutoka na Marya [mjakazi ambaye Muqawqis, mtawala wa Misri alimpa zawadi Mtume (s.a.w.w.)], naye akamwita mwana yule Ibrahim.

Wakati mkunga (Salma) alipompasha Mtume habari njema kwamba Allah kamjaalia mwana, alimpa bibi yule zawadi zenye thamani.
Katika siku ya saba, alitoa kafara ya kondoo ili kufanya ‘Aqiqah6 ya mtoto yule, na akamnyoa nywele mtoto yule na akatoa sadaka ya fedha iliyokuwa na uzito sawa na zile nywele za mtoto, katika njia ya Allah.

  • 1. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 500.
  • 2. Tabaqaatil-Kubra, Juz. 2, uk. 147.
  • 3. Siratu Halabi, Jz. 3, uk. 242.
  • 4. Kila ubeti unamalizikia na herufi ya Kiarabu ya Laam (Yaani L).
  • 5. - Hii ni kwa yule anayedhani kuwa alikuwa ni binti yake wa kuzaa. lakini kilichothibiti kwetu ni kuwa hakuwa binti wake wa kuzaa bali wa kulea. –Mhariri-
  • 6. Kuzinyoa nywele za kichwa za mtoto.