Sura Ya 52: Matukio Ya Mwaka Wa Tisa Hijiriya

Mwaka wa nane Hijiriya, pamoja na furaha na tabu zake zote ulimalizikia, na kile kituo kikuu cha ushirikina kiliangukia mikononi mwa Waislamu. Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) alirejea Madina baada ya kupata ushindi kamili, na nguvu ya kijeshi ya Uislamu ilienea Uarabuni kote. Makabila ya Waarabu wenye kuasi ambao kabla ya hapo, kamwe hayakupata kufikiria kwamba Uislamu utapata ushindi ule, sasa yakaanza kufikiria pole pole kwamba lazima wasogee karibu na Waislamu na kufuata dini yao. Kwa mtazamo huu, wawakilishi wa makabila mbalimbali ya Kiarabu na wakati mwingine makundi yao yakiongozwa na machifu wao, walipata heshima ya kufika mbele ya Mtume (s.a.w.w.) na kuidhihirisha itikadi yao katika Uislamu. Katika mwaka wa 9 Hijiria, wawakilishi wengi wa makabila walikuja Madina kiasi kwamba mwaka ule ulianza kuitwa ni mwaka wa wawakilishi.

Safari moja kikundi cha watu wa kabila la Tayyi wakiongozwa na mtu mmoja aliyeitwa Zaydul Khayl kilikuja kuonana na Mtume (s.a.w.w.). Zayd alianza kuzungumza kama chifu wa kabila lile na Mtume (s.a.w.w.) alishangazwa na upole na hekima zake. Alisema kuhusu yeye: “Nimekutana na watu maarufu wa Uarabuni lakini nimewaona kuwa ni wenye sifa duni kuliko vile nilivyopata kusikia juu yao, lakini nimemwona Zayd kuwa yu bora zaidi ya vile atambulikavyo. Ingelikuwa bora kama angeliitwa Zaydul Khayr (Zayd mwema) badala ya Zaydul Khayl (Zaydu ngamia).”1

Kuvunjwa Kwa Hekalu La Masanamu

Lilikuwa ni jukumu kubwa zaidi na la kimsingi Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) kuitangaza dini ya Upweke wa Allah na kuuondoa ushirikina kabisa kabisa. Hivyo basi, ili kuitengeneza hali ya watu wale waliopotoka na waabudu masanamu, mwanzoni kabisa aliitumia njia ya kuhoji na mantiki na kujaribu, kwa hoja zenye nguvu ili kuwafanya wauelewe upuuzi wa ushirikina. Hata hivyo, kama akiona kwamba hoja zake hazina athari yoyote kwao, nao wanaendelea kuwa wenye kiburi na wakaidi, alijiona kuwa anayo haki ya kutumia nguvu dhidi ya watu hawa wenye maradhi ya kiroho ambao hawakuweza kurekebishika hadi waweze kuzitumia akili zao.

Kama katika nyakati hizi kipindupindu kikilipuka kwenye sehemu ya nchi, na baadhi ya watu wanakataa kuchanjwa kutokana na ukosefu wa kuona mbali, Idara ya Afya ya Nchi ile hufikiria yenyewe kuwa inawajibika kuwachanja watu wale kwa nguvu ili kuhakikisha usalama wao na halikadhalika ule wa watu wengine kutokana na ugonjwa huu wa kuambukiza.

Mtukufu Mtume amejifundisha kutokana na mafundisho ya mbinguni kwamba ibada ya masanamu ni kama vijidudu vya kipindupindu. Vinaharibu maadili, ubora na tabia njema, na kumvuta mtu chini kutoka kwenye daraja la juu, humfanya kuwa duni hata zaidi ya mawe, udongo na viumbe vingine vilivyo duni. Hivyo aliteuliwa na Allah kuyaondoa maradhi ya ushirikina, kuzikomesha aina zote za ibada ya masanamu, na kutumia nguvu dhidi ya wale walioamka na kumpinga katika kuubalighisha ujumbe wa Allah.

Ubora wa kijeshi wa Uislamu ulimpa nafasi Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) kutuma vikundi kwenye sehemu mbalimbali za Hijaz kwenda kuyavunja mahekalu ya masanamu na kutobakisha japo sanamu moja tu, kwenye eneo hili.

Mtume (s.a.w.w.) alipata taarifa mapema kwamba lilikuwepo sanamu kubwa miongoni mwa watu wa kabila la Tayyi na baadhi ya watu bado wangali wana imani juu ya sanamu lile.
Hivyo alimtuma Sayyidna Ali (a.s.), yule afisa wake mwenye hekima na mwenye uzoefu pamoja na askari wapanda wanyama mia moja kwenda kulibomoa hekalu la sanamu lile na kulivunja lile sanamu lenyewe.

Amirul-Mu’minin (a.s.) alipata kutambua kwamba kabila lile litapinga kile kitendo cha jeshi la Uislamu na jambo hili halitamalizika bila ya vita. Hivyo basi, asubuhi na mapema alianza kuishambulia ile sehemu lilipowekwa lile sanamu na akapata ushindi kamili katika kuitimiza kazi yake. Vile vile aliwakamata baadhi ya watu wa kundi lenye kupinga na kuwaleta mjini Madina wakiwa ni sehemu ya ngawira.

Adyy bin Haatim, ambaye baadaye alijiunga na safu za wapiganaji mashujaa wa Kiislamu na akaushika uchifu wa sehemu ile baada ya babu yake aliyekuwa na fikira tukufu Haatim, anasimulia kisa cha kukimbia kwake kwa maneno haya: “Kabla ya kusilimu kwangu, nilikuwa na uadui dhidi ya Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) kutokana na propaganda za kinyume zilizokuwa zikiendeshwa dhidi yake. Vilevile sikukosa kuutambua ushindi mkubwa nchini Hijaz na nilikuwa na uhakika kwamba siku moja mamlaka yake itafika kwenye eneo la Tayyi’ pia, ambalo mimi nilikuwa mtawala wake.

Hata hivyo, kwa kuwa mimi sikutaka kuiacha dini yangu, na vilevile sikutaka kuwa mfungwa na kuangukia mikononi mwa Waislamu, nilimwamrisha mtumwa wangu kumweka ngamia mmoja tayari tayari kwa ajili ya kusafiri ili kwamba wakati wowote ule nikabiliwapo na hatari niondoke kwenda Sham kuepuka kukamatwa na Waislamu.

Ili nisije kukamatwa bila ya kujua niliweka doria kwenye sehemu mbalimbali za njia kuu, ili waweze kuniarifu wakati wowote waonapo vumbi litimuliwalo na msongo wa jeshi la Uislamu au watakapoiona dalili ya bendera zao.

Siku moja, mmoja wa watumwa wangu alikuja kwa ghafla na akanipa tahadhari na akaniarifu kuja kwa jeshi la Waislamu. Siku ile ile, mimi nikifuatana na mke na watoto wangu, tukatoka kwenda Sham, nchi iliyokuwa kituo kikuu cha Ukristo kule Mashariki. Dada yangu, binti yake Haatim alibakia na kabila lile na alikamatwa na Waislamu.

Baada ya dada yangu kupelekwa Madina, alifungiwa kwenye nyumba karibu na Masjidun-Nabi ambamo vile vile waliwekwa wale wafungwa wengine. Yeye amekieleza kisa chake hivi: “Siku moja wakati Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa akienda kusali mle msikitini, alipata bahati ya kupita karibu na ile nyumba walimowekwa wale wafungwa.

Niliitumia nafasi ile na nikiwa nimesimama upande wa pili wake nilimwambia: “Ewe Mtume wa Allah! Baba yangu amefariki dunia na mlezi wangu ametoweka. Basi nifanyie upendeleo fulani. Allah Atakufanyia upendeleo.”

Mtume akaniuliza: “Ni nani aliyekuwa mlezi wako?” Nilimjibu nikasema: “Ni kaka yangu Adyy bin Haatim.” Mtume akasema: “Je, yeye ndiye yule mtu aliyemkimbia Allah na Mtume Wake na akaenda Shamu?” Kisha akaelekea msikitini. Siku iliyofuatia, mazungumzo yale yale yalifanyika tena baina yangu na Mtume (s.a.w.w.) lakini mazungumzo hayo hayakuzaa matokeo. Siku ya tatu nilikuwa nimeyapoteza matumaini yoyote yale ya mazungumzo kama hayo na Mtume (s.a.w.w.) yenye kuthubutu kutokuwa na uwezo wa kuzaa matunda yoyote yale.

Hata hivyo, Mtume alipokuwa akipita kutoka kwenye sehemu ile ile, nilimwona mtu akija nyuma yake. Alinifanyia ishara niamke na niseme maneno yale yale niliyokuwa nikiyasema kwenye zile siku mbili zilizopita. Ile ishara aliyofanya yule mtu iliyahuisha matumaini yangu. Hivyo, nilisimama na nikayarudia yale maelezo niliyoyataja hapo juu mbele ya Mtume, kwa mara ya tatu. Alinijibu akisema: “Usifanye haraka kwenda. Nimeamua kukurejesha makwenu na mtu aaminikaye; lakini kwa wakati huu, matayarisho ya sarafi yako bado hayajakamilika.”

Dada yangu anasema kwamba, yule mtu aliyekuwa akimfuatia Mtume kwa nyuma na aliyenifanyia ishara kuyarudia yale maneno mbele ya Mtume, alikua ni Ali mwana wa Abu Talib.
Safari moja msafara uliokuwa na baadhi ya ndugu zetu, nao pia ulikuwa ukisafiri kutoka Madina kwenda Sham. Dada yangu alimwomba Mtume amruhusu kwenda Sham na msafara ule na kwenda kujiunga na kaka yake. Mtume alilikubali ombi lake na akaandaa mahitaji yote ya safari. Huko Shamu, mimi nilikuwa nimeketi karibu na dirisha la nyumba yangu. Mara kwa ghafla nikaona kwamba ngamia kasimama nyumbani kwangu.

Baada ya kutazama kwa makini, nilimwona dada yangu akiwa ameketi kwenye kitundu cha ngamia. Nilimshusha kutoka mle kitunduni na nikamwingiza nyumbani. Alianza kunilalamikia kuhusu kumwacha kule kwenye eneo la kabila la Tayyi’ na kushindwa kuja naye Sham.

Nilimchukulia dada yangu kuwa ni mwanamke mwenye hekima na akili. Siku moja nilizungumza naye juu ya Mtume na nikamuuliza: “Nini maoni yako juu yake?” Alijibu akisema: “Nimeona maadili yaliyo bora zaidi na sifa zilizo bora zaidi kwake, nami ninaona kwamba ni jambo lifaalo mno kufanya naye mapatano ya urafiki mapema iwezekanavyo.

Ninasema hivi kwa sababu, kama yeye ni Mtume wa Allah, ubora utakuwa ni wake yule amwaminiye mapema zaidi kuliko wengine, na kama akiwa mtawala wa kawaida, katu hutapata dhara lolote kutoka kwake na utafaidika kutokana na mamlaka aliyonayo.”

Adyy Bin Haatim Aenda Madina

Adyy anasema: “Maneno ya dada yangu yalinivutia mno kiasi kwamba niliuandaa moyo wangu juu ya kuelekea Madina. Nilipofika kule, nilikwenda moja kwa moja kumuona Mtume na nilimkuta mle msikitini. Niliketi karibu naye na kujitambulisha kwake. Mtume aliponitambua aliamka kutoka pale alipokuwa ameketi na akiwa ameushika mkono wangu, alinichukua nyumbani kwake. Tulipokuwa njiani, ajuza mmoja alikuja mbele yake na akazungumza naye maneno fulani.

Nilimwona akimsikiliza ajuza yule kwa makini na kumjibu. Tabia zake njema zilimvutia na nikasema moyoni mwangu: “Bila shaka mtu huyu si mtawala wa kawaida.” Tulipofika nyumbani kwake, maisha yake ya kawaida yalinivutia. Aliniwekea mkeka uliotengenezwa kwa nyuzi za mtende uliokuwamo nyumbani mle na akaniomba nikae. Mtu wa juu zaidi nchini Hijaz, aliyekuwa akiziogofya dola zote alikaa chini ardhini. Nilistaajabu mno kuyaona ya adabu zake na nilitambua kutokana na tabia zake njema maadili ya hali ya juu na heshima alizomtendea kila mtu, kwamba hakuwa mtu wa kawaida au aina ya mtawala wa nchi ya kawaida.

Wakati huo huo Mtume aliugeuzia uso wake kwangu na akayataja maelezo halisi ya maisha yangu na akasema: “Je, wewe hukuwa mfuasi wa dini ya Rakusi?2 Nikajibu: “Ndio.” Kisha akaniuliza: “Kwa nini ulijitwalia robo ya mapato ya taifa lako peke yako? Je dini yako ilikuruhusu kufanya hivyo?” Nikajibu: “Hapana.” Kutokana na ujuzi wake wa ghaibu nilishawishika kuamini kwamba alitumwa na Allah.

Nilipokuwa bado ninafikiria hivyo, alizungumza nami kwa mara ya tatu, na akasema: “Umaskini na ufukara wa Waislamu usikuzuie kusilimu, kwa sababu iko siku inakuja ambayo utajiri wa ulimwengu utawatiririkia na hatakuwako wa kuukusanya na kuuweka.

Na kama nguvu ya kiidadi ya maadui na udogo mno wa idadi ya Waislamu unakuzuia kuipokea dini hii, mimi ninaapa kwa jina la Allah, siku ile inakuja ambapo kutokana na kushinda kwa Uislamu, idadi kubwa ya wanawake wa Kiislamu wasio na ulinzi watakuja kutoka Qaadisia kwa ajili ya Hija ya Ka’abah na hakuna yeyote atakayewaudhi.

Na kama leo hii utaona nguvu na mamlaka viko mikononi mwa watu wengine, nakuahidi kwamba itakuja siku ambayo majeshi ya Uislamu yatayakalia makasiri yenu yote haya na yataiteka Babylon.”

Adyy anaendelea kusema: “Niliishi na nikaona kwamba chini ya usalama uliotolewa na Uislamu, wanawake wasio na ulinzi walikuja kutoka sehemu za mbali, kuja kufanya Hija kwenye Ka’abah na hakuna yeyote aliyewaingilia katika shughuli zao. Vile vile niliona kwamba, nchi ya Babylon ilitekwa na Waislamu, walikikalia kiti cha enzi cha Kisra. Ninategemea kwamba nitaliona jambo la tatu; yaani utajiri wa ulimwengu utatiririka kuelekea Madina na hakuna atakayeelekea kuukusanya na kuuhifadhi.”3

  • 1. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 577.
  • 2. Dini ya ‘Rakusi’ ni dini iliyo baina ya Ukristo na Usabiya.
  • 3. Maghaazil-Waaqidi, Juz. 3, uk. 988 - 989; Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 578-581; Darajaatur Rafi’ah fi Tabaqaatish Shi’ah Imamiyah, uk. 352-354.