Sura Ya 54: Wajumbe Wa Kabila La Thaqif Waenda Madina

Vita vya Tabuk pamoja na matatizo na taabu zake vilimalizika, na Mujahidiin wote walirejea Madina wakiwa wamechoka kabisa. Askari wa Uislamu hawakupambana na adui yeyote mle njiani na hawakupata ngawira yoyote.

Kwa sababu hii, baadhi ya watu wenye uoni mfinyu waliichukulia safari hii kuwa ni isiyo na faida. Hata hivyo, wao hawakuzifikiria faida zake za ndani. Mara tu baada ya hapo faida hizi zikawa za dhahiri na makabila ya Waarabu wakaidi ambao hapo kwanza hawakuwa tayari kusalimu amri au kusilimu kwa hali yoyote ile, walianza kuwaleta wawakilishi wao kwa Mtume (s.a.w.w.) na wakatangaza kuwa kwao tayari kusilimu, na kuyafungua malango ya ngome zao na kwamba masanamu yaliyowekwa humo yaweze kuvunjwa, na bendera ya Uislamu na Dini ya Allah iweze kudu- mishwa badala ya hii ya masanamu haya.

Kama jambo la kanuni, watu wapumbavu na wasioona mbali daima waliyapa umuhimu matokeo ya dhahiri. Kwa mfano, kama wakati wa safari hii wale askari wangelipambana na adui na baada ya kumshinda wakainyakua mali yake, watu hawa wangelisema kwamba matokeo ya vita vile yalikuwa mazuri sana. Hata hivyo, watu wenye kuona mbali huyatafi- ti matukio na kuuchukulia kuwa ni mzuri na wenye matunda mazuri ule ukweli usadiao katika kuifikia nia na madhumuni.

Kwa bahati njema Vita vya Tabuk vilikuwa na faida katika kulifikia lengo halisi la Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.), yaani kuyavutia makabila ya Kiarabu kwenye dini ya Uislamu. Ilikuwa hivyo kwa sababu taarifa zilizoenea kila mahali nchini Hijaz kwamba Warumi (Wale wale ambao kwenye vita vyao vya mwisho dhidi ya Wairani ambao kwa muda mrefu sana walikuwa wakitawala nchi ya Yemen na maeneo jirani yake, waliwashinda Wairani na wakaurudisha ule Msalaba kutoka kwao na kuuleta Yerusalem) wametishwa na nguvu ya kijeshi ya Waislamu nao hawakuthubutu kupigana nao.

Kuenea kwa taarifa hii kulitosha kuyafanya makabila ya Kiarabu yaliyokuwa makaidi, ambayo hadi kwenye siku iliyopita walikuwa kwa vyovyote iwavyo bado hawajakubali kukaa kwa amani na Waislamu, kufikia kushirikiana nao na kujiunga nao katika kujisalimisha kutokana na uasi wa Warumi na Wairani, haya mataifa makuu mawili ya ulimwengu wa wakati ule. Ufuatao hapa chini ni mfano wa mabadiliko yaliyotokea miongoni mwa makabila makaidi ya Kiarabu

Mfarakano Miongoni Mwa Watu Wa Kabila La Thaqif

Watu wa kabila la Thaqif walikuwa maarufu miongoni mwa Waarabu kwa ukaidi na ugumu wao. Walilipinga jeshi la Waislamu kwa mwezi mzima chini ya hifadhi ya ngome madhubuti ya Ta’aif nao hawakukubali kusalimu amri mbele yao.1
Urwah bin Mas’ud alikuwa mmoja wa machifu wa kabila la Thaqif. Alipopata kuutambua ushindi mkubwa wa jeshi la Uislamu kule Tabuk alikutana na Mtume (s.a.w.w.) kabla ya kuwasili kwake mjini Madina, akasilimu na akamwomba ruhusa arejee kwenye kabila lake na akaitangaze dini ya Allah miongoni mwao. Mtume (s.a.w.w.) alimwonya kuhusu matokeo ya ujumbe wake ule na akasema: “Mimi ninachelea kwamba unaweza ukaupoteza uhai wako kwenye njia hii.” Alijibu, akisema: “Wananipenda zaidi kuliko macho yao.”

Kabila lake na machifu wengine walikuwa bado hawajautambua ukuu alioupata Urwah kutokana na Uislamu. Hivyo basi, waliamua kwamba pale mubalighi wa kwanza wa Uislamu atakapojishughulisha katika kuwalingania watu Uislamu, wao wamnyeshee mvua ya mishale mwilini mwake na wamuuwe. Matokeo ni kwmaba, Urwah alishambuliwa na alipokaribia kufa, alisema: “Kifo changu ni baraka ambayo Mtume ameniarifu.”

Wajumbe Wa Thaqif Wakutana Na Mtume (S.A.W.W.)

Watu wa kabila la Thaqif walijuta kwa kumuuwa Urwah na wakatambua kwamba ilikuwa ni jambo lisilowezekana kwao kuishi katikati ya nchi ya Hijaz wakati bendera ya Uislamu ilikuwa ikipepea kandokando yao, na malisho na njia za biashara zilitishiwa na Waislamu. Kwenye mkutano waliouitisha ili kulitatua tatizo hili, iliamuliwa kwamba wampeleke mjumbe wao Madina akakutane na Mtume (s.a.w.w.) na amweleze kuhusu kuwa kwao tayari kusilimu chini ya masharti fulani fulani.

Wote kwa pamoja walimteua mmoja wa wazee wao aliyeitwa Abd Yaalayl kwenda Madina na kuufikisha ujumbe wao kwa Mtume (s.a.w.w.), lakini alikataa kulibeba jukumu lile na akasema: “Si jambo lisilowezekana kwamba baada ya kuondoka kwangu mkayabadili mawazo yenu na mimi nami yakanipata yale yaliyompata Urwah.” Na akaongeza kusema: “Niko tayari kuwa mwakilishi wenu kwa masharti ya kwamba wazee wengine watano wa kabila la Thaqif niende nao na sisi sote tuwe na majukumu yaliyo sawa katika jambo hili.”

Ushauri aliotoa Abd Yaalayl ulikubaliwa na watu wale. Hivyo basi, watu wote sita walitoka na kwenda Madina na wakatua kwenye kijimto kilichokuwa kandokando ya chemchemu karibu na Madina.

Mughirah bin Shu’ubah Thaqafi aliyewaleta farasi wa masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) malishoni aliwaona wale machifu wa kabila lake pale ukingoni mwa ile chemchemu.

Upesi sana aliwaendea na akapata kuitambua shabaha ya safari yao ile. Kisha aliwaachia wale farasi na akarejea Madina upesi ilivyowezekana kwenda kumjulisha Mtume (s.a.ww) kuhusu ule uamuzi uliochukuliwa na watu wakaidi wa kabila la Thaqif. Alipokuwa njiani alikutana na Abu Bakr na akamweleza jambo lile. Alimwomba Mughirah amruhusu azifikishe zile taarifa za kuwasili kwa wajumbe wa Thaqif kwa Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe.

Hatimaye Abu Bakr alimwarifu Mtume (s.a.w.w.) kuhusu kuwasili kwa wajumbe wa kabila la Thaqif na akaongeza kusema kwamba walikuwa tayari kusilimu ili mradi tu baadhi ya masharti yao yakikubaliwa na ukafanyika mkataba. Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha likitwe hema karibu na msikiti kwa ajili ya hawa wajumbe wa Thaqif na kwamba Mughirah na Khalid bin Sa’id wawapokee.

Hawa wajumbe wa msafara wa Thaqif walimjia Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.). Mughirah aliwashauri kwamba wajiepushe na aina zote za salam za zama za ujinga na watoe salam kama Waislamu. Hata hivyo, kwa vile fahari na majivuno ilikuwa sifa ya pili ya kabila hili walimsalimu Mtume (s.a.w.w.) kwa desturi ya zama za kabla ya Uislamu. Kisha waliuwakilisha ujumbe wa kabila la Thaqif na kuwa kwao tayari kusilimu na wakaongeza kusema kwamba huko kusilimu kwao kutakuwa chini ya masharti fulani watakayoyaeleza kwenye mkutano utakaofuatia.
Majadiliano ya wale wajumbe wa kabila la Thaqif yaliendelea kwa siku kadhaa na Khalid aliendelea kumwarifu Mtume (s.a.w.w.) kuhusu taarifa zao.

Masharti Ya Ujumbe Wa Thaqif.

Mtume (s.a.w.w) aliyakubali mengi ya masharti waliyoyatoa kiasi kwam- ba alikubali kufanya nao mkataba wa usalama na akazihakikishia nchi zao. Hata hivyo, baadhi ya masharti yao hayakuwa sahihi hata kidogo, yenye kuchukiza na yasiyo ya adabu njema kiasi kwamba Mtume (s.a.w.w.) aliudhika. Masharti yao yalikuwa kama ifuatavyo hapa chini:

Kwamba watu wa Taa’if wasilimu kwa sharti la kwamba hekalu kubwa la masanamu la Taa’if libakishwe kwa kipindi cha miaka mitatu, na sanamu kubwa la kabila lao liitwalo Laat liendelee kuabudiwa. Hata hivyo, walipotambua kwamba sharti lao hili limemuudhi Mtume (s.a.w.w.) walil- isahihisha na wakaomba kwamba lile hekalu la masanamu libakie kwa kipindi cha mwezi mmoja. Kumwomba Mtume (s.a.w.w.) jambo hili, ambaye lengo lake kimsingi lilikuwa ni kuidumisha ibada ya Allah Aliye Mmoja tu, na kuyabomoa mahekalu ya masanamu na masanamu yenyewe kulikuwa aibu kubwa, ilionyesha kwamba waliutaka Uislamu ambao hautayadhuru maslahi na mwelekeo wao, na kama hilo haliwezekani basi dini hii haikubaliki kwao. Walipoutambua ubaya wa ombi lao hili, walianza kuomba msamaha na kusema.

“Tumetoa ombi hili kuwanyamazisha wanawake wetu na watu wetu walio wajinga na kwa njia hii tuweze kuviondoa vizuizi vyote vilivyomo kwenye njia ya kuwasili kwa Uislamu mjini Taa’if. Sasa kwa vile Mtume hakubaliani nalo, basi tafadhalini na awasamehe watu wa kabila letu kutokana na kuyavunja masanamu kwa mikono yao wenyewe na waweze kuwateua watu wengine waifanye kazi hii.” Mtume (s.a.w.w.) alikubaliana na wazo hilo. Kwa kuwa lengo lake lilikuwa kwamba miungu wa uwongo na ujinga vifutiliwe mbali basi hapo suala la nani ayavunje lilikuwa ni jambo lisilo na maana kwake, ni sawa kwake kama kazi hii ikifanywa na watu wale wenyewe au na mtu yeyote mwingine.

Sharti lingine lilikuwa kwamba Mtume (s.a.w.w.) awasamehe kusali. Walikuwa wakidhania kwamba kama walivyo viongozi wa watu wa Kitabu, Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) anaweza kuziingilia sheria za Allah na hivyo akazitumia kanuni fulani fulani kwa ajili ya kundi moja na kuwaacha wengine wasizitumie kanuni zile. Hawakutambua kwamba ilimbidi kuutii wahyi wa Allah na kwamba asingeliweza kuufanyia mabadiliko. Sharti hilo lilionyesha kwamba moyo wa kujitoa kabisa kabisa katika kuyatimiza mapenzi ya Allah ulikuwa bado haujashamirisha mizizi yake akilini mwao, na kusilimu kwao ni kwa kujionyesha tu. Au la, haikuwepo haki yoyote katika kufanya upendeleo kwao kwenye sheria za Uislamu na kuzikubali baadhi yao na kuzikataa nyingine. Uislamu na kumwamini Allah ni sharti la kujitoa kabisa kabisa ili kuyatimiza mapenzi ya Allah ambayo chini yake amri za Allah zote hutiiwa bila ya kusitasita na hakuna ubaguzi baina yao. Akiwajibu, Mtume (s.a.w.w.) aliwaambia: “Hakuna faida yoyote kwa dini isiyo kuwa na sala.”

Kwa kauli nyingine ni kwamba, mtu asiyemwinamishia Allah kichwa chake wakati wa mchana na vilevile wakati wa usiku, atakuwa hamkumbuki Mola wake na si Mwislamu wa kweli.

Baada ya hapo, hatimaye yale masharti yalitiwa saini na Mtume (s.a.w.w.) na kisha akawaaga wale wajumbe wa msafara ule waliokuwa wakirejea kwenye kabila lao. Miongoni mwa wale watu sita, alimteua kwa ajili ya uongozi kijana mdogo zaidi miongoni mwao ambaye katika kile kipindi cha kukaa kwao mjini Madina alionyesha shauku kubwa ya kujifunza Qur’ani na amri za Allah. Alimteua kuwa mwakilishi wake wa kidini na kisiasa miongoni mwa watu wa Taa’if na akamshauri kwamba atakapokuwa akisalisha sala ya jamaa, awafikirie watu wanyonge hivyo asiirefushe sala. Kisha Mughirah na Abu Sufyani waliteuliwa kufuatana na wale wajumbe hadi Taa’if kwenda kuyavunja yale masanamu yaliyokuwako pale. Abu Sufyani ambaye hadi katika siku iliyopita alikuwa mlinzi wa masanamu na amesabahisha umwagaji wa damu mwingi mno kwa ajili ya kuyahami, sasa aliishika shoka na kishoka kidogo na kuyavun- ja vipande vipande hadi yakalichukua umbile la kichuguu cha kuni. Akayauza mapambo ya yale masanamu, na kama alivyoelekezwa na Mtume (s.a.w.w.) akayalipa madeni ya ‘Urwah na ndugu yake aliyeitwa Aswad kutokana na mauzo ya yale mapambo.2

  • 1. Maelezo ya mazingiwa ya Ngome ya Taa’if yamekwishakutolewa kuhusiana na matukio ya mwaka wa 8 Hijiriya.
  • 2. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 542; Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 243