Sura Ya 55: Mtume (S.A.W.W.) Amuomboleza Mwanawe

“Kipenzi Ibrahim! Hatuwezi kufanya lolote lile juu yako. Mapenzi ya Allah hayawezi kubadilishwa na machozi, na moyo wangu unasikitika na kuhuzunika kwa kifo chako. Hata hivyo, sitasema lolote lile liwezalo kule- ta ghadhabu ya Allah. Kama isingalikuwako ahadi ya kweli na ya uhakika kwamba sisi nasi tutakuja baada yako, ningalilia sana kuhuzunika zaidi kwa kutengana nawe”1

Sentensi hizi zilitamkwa na Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) alipokuwa akimuomboleza mwanawe mpenzi, Ibrahim aliyekuwa akikata roho akiwa mapajani mwa baba yake.

Mtume (s.a.w.w.) alikuwa ameiweka midomo yake ya huruma kwenye uso wenye rangi ya waridi wa mwanawe na kumpa kwaheri huku akiwa mwenye uso wenye huzuni mno na moyo mzito na wakati huo huo akiwa kwenye kujinyenyekeza kwenye mapenzi ya Allah.

Mapenzi kwa dhuria wake mtu ni moja ya udhihirisho halisi mno na mtukufu zaidi wa moyo wa ubinadamu, na ni dalili ya afya na utakaso halisi wa nafsi yake mtu.

Mtume (s.a.w.w.) alikuwa kila mara akisema: “Kuwa mpole kwa watoto wako na uonyeshe hisia za huruma kwao. “2 Zaidi ya hapo, huruma na upendo kwa watoto ilikuwa moja ya sifa zake zenye kupendeza.3

Katika miaka iliyopita, Mtume (s.a.w.w.) alikabiliwa na vifo vya wanawe watatu ambao ni Qaasim, Taahir na Tayyib4 na mabinti watatu ambao ni Zaynab, Ruqayyah na Ummu Kuluthumu, na amekuwa akihuzunika sana kutokana na jambo hili. Baada ya vifo vyao, mwanawe pekee aliyesalia hai, na kumbukumbu ya mkewe kipenzi, Bibi Khadija (a.s.) alikuwa ni Bibi Fatimah (a.s.).

Katika mwaka wa sita Hijiriya aliwapeleka wajumbe wake kwenye nchi za kigeni ikiwa ni pamoja na Misri. Alimpelekea barua mtawala wa Misri akimwita kwenye Uislamu. Ingawa hakuujibu mwito wa Mtume (s.a.w.w.) kwa jibu la dhahiri, lakini alimpelekea jibu la heshima pamoja na zawadi fulani fulani zikiwa ni pamoja na mjakazi aliyeitwa Maarya. Baadae mjakazi huyu alipata heshima ya kuwa mkewe Mtume (s.a.w.w.) na kumzalia mwana aliyeitwa Ibrahim, aliyependwa sana na Mtume (s.a.w.w.).

Kuzaliwa kwa Ibrahim kulimaliza kwa kiasi fulani zile athari mbaya zilizoletwa na vifo vya watoto wake sita, na kulimpa faraja. Hata hivyo, kwa masikitiko yake makubwa Ibrahim naye alifariki dunia baada ya miezi kumi na minane. Ilikuwa Mtume (s.a.w.w.) ametoka nyumbani mwake kwa kazi fulani alipoitambua hali ngumu ya mtoto wake.

Alirejea nyumbani akamchukua mtoto kutoka mapajani mwa mama yake, na wakati dalili za hali ngumu zilipokuwa zikijidhihirisha usoni mwake, alizitamka zile kauli tulizozitaja hapo juu.

Maombolezo ya Mtume (s.a.w.w.) kwa ajili ya mwanawe ni dalili ya hisia za ubinadamu ulioendelea hata baada ya kifo cha mtoto yule.

Na ule mdhihiriko wa hisia na kuzionyesha huzuni ulikuwa ni dalili ya upole wake uliojidhihirisha bila ya kukusudia maishani mwake mwote. Ama kuhusu kutotamka neno lolote lililo dhidi ya radhi ya Allah, ilikuwa ni dalili ya imani yake na kuyapokea Mapenzi ya Allah, ambayo hakuna yeyote awezaye kuyaepuka.

Kizuizi Kisicho Na Msingi

Abdur-Rahman bin Awf aliyekuwa wa familia ya Ansar, alishangaa alipomwona Mtume (s.a.w.w.) akitokwa na machozi. Alimzuia akisema: “Umekuwa ukituzuia tusililie maiti. Basi inakuwaje kwamba hivi sasa wewe unatokwa na machozi kwa kifo cha mwanao?” Mzuiaji huyu, sio tu kwamba hakutambua misingi mitukufu ya Uislamu lakini vile vile alikuwa mjinga wa moyo na hisia maalum ambazo kwazo Allah Mwenye nguvu zote amemjaalia mwanadamu. Silika zote za kibinadamu zimeumbwa kwa lengo maalum na ni muhimu kwamba kila moja ijidhihirishe kwenye wakati na sehemu yake maalumu. Mtu asiyeshitushwa na kifo cha ndugu yake wa karibu zaidi, ambaye moyo wake haushituki, ambaye macho yake hayatiririkwi na machozi, kwa kifupi mtu asiyezidhihirisha athari zozote kutokana na kutengwa, basi yeye si chochote kile zaidi ya kuwa ni jiwe, na hastahili kuitwa mwanadamu.

Hata hivyo, hapa kuna jambo lililo nyeti na listahililo kuzingatiwa, kwa sababu ingawa kizuizi hiki hakikuwa na msingi lakini kinatufahamisha ya kwamba uhuru kamili na demokrasia halisi ilikuwepo kwenye jamii mpya ya Waislamu wakati ule, ili kwamba mtu angeliweza kuwa na moyo wa kuyafasiri matendo ya mtawala wake pekee kwa uhuru halisi na bila ya kuwapo woga wowote au hofu na vile vile akaweza kupata jibu. Mtume (s.a.w.w.) alimjibu akisema: “Mimi katu sikusema kwamba msililie vifo vya wapenzi wenu, kwa sababu huko kulia ni dalili ya huruma na masikitiko, na mtu ambaye moyo wake hauhuzunishwi na matatizo yawapatayo wenzie hana haki ya kuipata baraka ya Allah.5 Nimesema kwamba msip- ite kiasi katika maombolezo kwa ajili ya vifo vya ndugu zenu wa karibu zaidi, na katu msitamke neno chafu au lisilofaa wala kupasua mavazi kutokana na huzuni iliyokithiri.”6

Kama alivyoeleza Mtume (s.a.w.w.) Amirul-Mu’minin (a.s.) aliiosha maiti ya Ibrahim na kuikafini. Kisha Mtume (s.a.w.w.) na baadhi ya masahaba wake waliisindikiza maiti na kumzika mtoto yule kwenye mava ya Baqi.7

Mtume (s.a.w.w.) aliangalia kaburi la Ibrahim na akaona shimo kwenye pembe ya kaburi lile. Ili kulifukia alikaa chini akalisawazisha lile kaburi kwa mikono yake, na akatamka kauli ifuatayo: “Kila mmoja miongoni mwenu anapoifanya kazi fulani hana budi kujitahidi kuifanya kwa ufanisi zaidi.”

Kampeni Dhidi Ya Usihiri

Jua lilipatwa siku ya kufariki dunia kwa Ibrahim. Baadhi ya watu wajinga wasiozijua kanuni za maumbile walifikiria kwamba jua limepatwa kutokana na kifo cha Ibrahim. Ingawa fikira hizi hazikuwa na msingi, kwa dhahiri ingelikuwa na faida kwa Mtume (s.a.w.w.). Hivyo basi, kama angelikuwa yu mtu wa kawaida na kiongozi wa kiulimwengu, angeliy- athibitisha maoni haya na hivyo akauthibitisha ukuu na utukufu wake.

Hata hivyo, kinyume na fikira hii, aliipanda mimbari na akawaarifu watu kuhusu hali halisi. Alisema: “Enyi watu! Naifahamike wazi kwenu kwam- ba jua na mwezi ni dalili ya uwezo wa Allah.
Vinasogea kwenye njia zao maalumu alizoziamrisha Allah kwa ajili yao kwa mujibu wa kanuni za maumbile.
Havipatwi kutokana na kifo au kuzaliwa kwa yeyote yule. Ni jukumu lenu wakati wa kupatwa kwa jua kusali.”8
Kinyume na walivyofikiria wengi ambao sio tu kwamba walizitafsiri kweli kutegemeana na wapendavyo, lakini vile vile hujinufaisha na kule kutojua kwa watu na fikira za ngano zao, lakini Mtume (s.a.w.w.) hakuzificha kweli wala hakujaribu kujinufaisha kutokana na ujinga wa watu.

Kama katika siku ile angeliithibitisha dhana hii potovu, basi asingeliweza kujitukuza na kudai kwamba yeye yu kiongozi wa milele wa wanadamu na mwakilishi na mteule wa Allah kwenye zama hizi wakati elimu ya unajimu imeshachukua hatua ndefu na sababu za kupatwa kwa jua na kwa mwezi zimeshafahamika kwa mwanadamu.

Sheria na mwito wake kwa Allah si kwa Waarabu peke yao na havitumiki kwenye wakati au sehemu maalum. Kama yeye Mtume (s.a.w.w.) yu kiongozi wa wale walioishi kwenye zama za awali, vile vile yeye yu Mtume wa hawa waishio kwenye zama za anga na wa zama za ugunduzi wa siri za maumbile. Kila uwanja wa elimu wowote ule aliouzungumzia, maneno yake ni dhahiri kabisa kiasi kwamba mageuzi ya kisayansi ya hivi karibuni yaliyozitangua dhana nyingi za wanachuoni wa kale, hayakuweza kupata japo nukta moja iliyo dhaifu katika kauli zake.

  • 1. Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 34; Bihaalul-Anwaar, Juz. 22, uk. 157.
  • 2. Biharul-Anwaar, Juz. 23, uk. 114.
  • 3. Muhajjatul Bayzah, Juz. 3, uk. 366.
  • 4. Bihaarul Anwaar, Juz. 22, uk. 166. Hata hivyo, baadhi ya wanachuoni wa Kishiah wamesema kwamba alikuwa na wana wawili tu kutokana na bibi Khadija (a.s.) (Bihaarul Anwaar, Juz. 2, uk. 151-Toleo jipya).
  • 5. Bihaarul-Anwaar, Juz. 22, uk. 151.
  • 6. Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 348.
  • 7. (Bihaarul-Anwaar, juz. 22, uk. 156) kufuatana na maelezo ya Halabi, kule kuosha na kukafini kwa mwana wa Mtume (s.a.w.w.) Ibrahimu, kulifanywa na Fazal mwana wa binamu yake Mtume (s.a.w.w.) Abbas.
  • 8. Al-Muhaasin, uk. 313 na Siiratu Halabi, juz. 3, uk. 348.