Sura Ya 56: Kufutwa Kwa Ibada Ya Masanamu Bara Arabuni

Mwishoni mwa mwaka wa tisa Hijiriya, aya za mwanzoni za Sura al- Tawbah (Baraa’at) ziliteremshwa na Mtume (s.a.w.w.) aliamrishwa kumpeleka mtu Makka wakati wa Hijja ili akazisome aya hizo pamoja na tangazo lenye ibara nne.

Kwenye aya hizi, usalama waliothibitishiwa washirikina umefutiliwa mbali na mikataba yote iliyofanywa baina yao na Waislamu (ila ule ambao pande zote mbili hawajauvunja na wameutekeleza kimatendo) imebatilishwa, na machifu wa ushirikina na wafuasi wao wameambiwa kwamba hawana budi kudhihirisha msimamo wao ndani ya kipindi cha miezi minane kuelekea kwenye serikali ya Kiislamu iliyosimamia kwenye msingi wa Upweke wa Allah na kama hawatauacha ushirikina na ibada ya masanamu, basi kule kuachiwa huru walikopewa kutakoma.

Mustashirik wanapoifikia hatua hii ya historia ya Uislamu, huishambulia dini hii vikali mno na kuuchukulia ukali huu kuwa ni kinyume na msingi wa uhuru wa kuabudu. Hata hivyo, kama wangalifanya utafiti wa historia ya Uislamu usio na upendeleo, na wakayaona mambo yaliyowajibisha kuchukuliwa kwa hatua hii iliyotajwa kwenye maelezo ya kihistoria na katika Surah al-Tawbah, bila shaka wangelikutambua kule kutofahamu vipasikavyo na wangelithibitisha kwamba katu kitendo hiki si kinyume na msingi wa ‘Uhuru wa Kuabudu’ wenye kuheshimiwa na watu wote wenye hekima wa ulimwenguni humu. Zifuatazo hapa chini ndio sababu za kutolewa kwa agizo hili:

Wakati wa Zama za Ujinga ilikuweko desturi moja miongoni mwa Waarabu kwamba mtu yeyote aifanyaye Hija ya Ka’abah alimpa maskini vazi alilofanyia Tawaf (kuizunguka Kaabah). Kama mtu yule alikuwa na nguo moja tu, kwa kawaida aliazima nyingine na akaifanya Tawaaf nayo ili kwamba asiitoe ile nguo yake na kumpa maskini.

Na kama haikuwezekana kuazima nguo, basi ile Tawaaf ilifanywa uchi! Siku moja mwanamke mnene na mwenye sura ya kupendeza aliingia msikitini.

Kwa vile hakuwa na zaidi ya nguo moja, kwa kuitekeleza ile desturi ya imani potofu tu ya zama zile, alilazimika kufanya Tawaafu akiwa yu uchi. Ni dhahiri juu ya ni kiasi gani cha athari mbaya zitakazokuwa zimetolewa na ile Tawaf ya mwanamke aliye uchi katika sehemu ile takatifu mbele ya kundi la watu.

Sura al-Tawbah ilipofunuliwa, zaidi ya miaka ishirini ilikuwa imeshapita tangu Mtume (s.a.w.w.) aianze kazi ya kuulingania Uislamu, na katika kipindi hiki mantiki ya Uislamu yenye nguvu kuhusiana na kuizuia ibada ya masanamu, tayari imeshayafikia masikio ya washirikina wa Rasi ile. Hivyo basi, kama kulikuwako na kikundi kidogo tu kilichoung’ang’ania ushirikina na ibada ya masanamu, sababu yake ilikuwa ni ushupavu wa kidini na ukaidi wao tu.
Hivyo basi sasa wakati umefika kwamba Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) aitumie dawa ya mwisho katika kuitengeneza jamii, kuharibu sura zote za uabudu-masanamu kwa nguvu, kuichukulia (yaani hiyo ibada ya masanamu) kuwa ni uasi dhidi ya ubinadamu na kuangamiza chanzo cha mamia ya tabia nyingine mbaya kwenye jamii.

Hata hivyo, mustashirik ambao huchukulia kitendo hiki kuwa kinyume na kanuni za uhuru wa imani, ambao ni msingi wa Uislamu na msingi wa utamaduni wa siku hizi, wametupilia mbali jambo moja, nalo ni kuwa kanuni ya uhuru wa imani huheshimika tu pale usipoleta madhara katika ustawi wa mtu binafsi na jamii. Vinginevyo kwa mambo yanayopingana na akili na njia wanayoifuata wanafikra wa ulimwengu, haina budi kupingwa kwa nguvu zote.

Kwa mfano, katika Ulaya ya kisasa, kutokana na fikara zisizo sahi- hi baadhi ya watu wenye tamaa za kimwili hukiunga mkono chama cha wenye kukaa uchi kwenye jamii, na hoja iliyo ya kitoto (yaani, kuifunika sehemu ya mwili ni chanzo cha kichocheo na hivyo basi huyafisidi maadili) huunda vilabu vya siri na kuwa uchi humo mbele ya wenzao! Je, akili za mwanadamu zinaruhusu kwamba watu hawa waruhusiwe kuviendeleza vitendo vyao kwa dai la

‘Uhuru wa Kuabudu’ na iwe kwamba itikadi yao iheshimiwe? Au ni muhimu kwamba, ili kuuhami ustawi wa watu hawa pamoja na ule wa jamii, hatuna budi kupambana dhidi ya fikara hizi zilizo za kijinga kabisa?

Njia hii (yaani, kuuzuia ufisadi kwa nguvu) haitumiwi na Uislamu tu bali wenye hekima wa ulimwengu mzima hupambana mapam- bano makali dhidi ya fikra zenye madhara kwa maslahi ya jamii, na kwa kweli mapigano haya ni vita dhidi ya itikadi za kipumbavu za watu waliovunjika nyoyo. Ibada ya masanamu haikuwa chochote bali ni ukorofi wa ngano na itikadi zenye kuchekesha zilizoleta mamia ya tabia zenye kuchukiza kwenye mafundisho yake.

Na Mtume (s.a.w.w.) ameupa usikivu utoshelezao ule mwongozo wa waabudu masanamu. Hivyo basi, hivi sasa muda umeshawadia wa kuichukua hatua ya mwisho ambayo ni kuitumia nguvu ya kijeshi katika kukiangamiza hiki chanzo cha ufisadi.

Hijja ni moja ya masharti makuu ya imani ya ibada za Kiislamu na kaida za kidini, na hadi kwenye siku za kushushwa kwa Sura hii (Tawba), ugomvi na vita vilivyokuwepo baina ya Waislamu na machifu wa ushirik- ina havikuruhusu kwamba Mtume (s.a.w.w.) awafunze Waislamu kiviten- do zile ibada za Hijja kwa njia iliyo sahihi na rahisi. Hivyo, ilikuwa muhimu kwamba Mtume (s.a.w.w.) yeye mwenyewe binafsi ashiriki kwenye huu mkutano mkuu wa Kiislamu na kuwapa Waislamu mafunzo ya kivitendo jinsi ya kuifanya ibada hii kuu. Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) angeliweza kushiriki kwenye ibada hii pale tu Ka’abah tukufu na sehemu zinazoizunguka zitakapoachwa wazi na washirikina, na wakati Nyumba ya Allah itakapokuwa wazi kwa ajili ya wenye kumuabudu Allah na waja wake halisi tu.

Kutokana na sababu tatu tulizozitaja hapo juu, Mtume (s.a.w.w.) alimwita Abu Bakr na kumsomesha baadhi ya aya za mwanzoni za Sura al-Tawbah na kumuamrisha aende Makka pamoja na watu wengine arubaini1 na kuzisoma aya hizo zenye kufarakisha kutokana na ikirahi kwa waabudu masanamu katika siku ya Idd al-Udh-ha.

kama ilivyoamrishwa na Mtume (s.a.w.w.) Abu Bakr alitoka na akaelekea Makka. Huku nyuma Malaika Mkuu Jibriil (a.s.) alikuja na kuleta ujumbe wa Allah usemao kwamba ile ikirahi kwa wenye kuayaabudu masanamu ni lazima itangazwe na Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe au na mtu atokanae naye.2 Hivyo Mtume (s.a.w.w.) alimwita Sayyidana Ali (a.s.) na kumwarifu jambo lile.

Kisha alimtoa mnyama wake maalum wa kupanda na kumpa Sayyidna Ali (a.s.) na kumwamrisha atoke Madina upesi iwezekanavyo ili amkute Abu Bakr mle njiani na azichukue zile aya kutoka kwake na akazisome yeye pamoja na lile tangazo lihitajikalo katika siku ya Idd Adhha mbele ya mkusanyiko mkuu ambao watu kutoka pande zote za Uarabuni watakuwa wakishiriki humo.

Mambo yaliyokuwamo kwenye tangazo hilo yalikuwa haya: Waabudu masanamu hawana haki ya kuiingia nyumba ya Allah. Kufanya Tawafu katika hali ya kuwa uchi kumepigwa marufuku.
Hakuna mwaabudu masanamu atakayeruhusiwa kushiriki kwenye Hijja.

Kama watu fulani walifanya mapatano ya kutoshambuliana na Mtume (s.a.w.w.) nao wameyatekeleza majukumu yao chini ya mapatano hayo kwa ukamilifu basi mapatano hayo yaliyofanywa baina ya Mtume (s.a.w.w.) na watu hao yataendelea kuheshimiwa na uhai wao mali zao vitaheshimiwa hadi uishe muda wa mapatano hayo.

Hata hivyo, wale washirikina wasio na mapatano yoyote na Waislamu, au kivitendo wameyavunja masharti ya mapatano wanapewa muda wa miezi minne kuanzia leo (mwezi kumi Dhil Haj) kuueleza msimamo wao kuhusu serikali ya Kiislamu. Hawana budi kujiunga kwenye itikadi ya Upweke wa Allah (Waislamu) na kuiacha kila aina ya ushirikina au wajitayarishe kwa ajili ya vita.3

Amirul-Mu’minin (a.s.) alitoka na kwenda Makka akiwa amempanda yule mnyama maalum aliyepewa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Alifuatana na baadhi ya watu akiwemo Jaabir bin Abdullah Ansaari. Alimkuta Abu Bakr mahali paitwapo Juhfah na akampa ule ujumbe wa Mtume (s.a.w.w.). Abu Bakr akampa Sayyidna Ali (a.s.) zile aya. Wanahadithi wa Kishia pamoja na wa Kisunni wengi wanamnukuu Sayyidna Ali (a.s.) kwamba amemwambia Abu Bakr: “Mtume amekupa uchaguzi wa kufuatana nami hadi Makka au kurudi Madina.”

Abu Bakr alichagua kurudi, na baada ya kufika kwa Mtume (s.a.w.w.) alimwuliza akisema: “Ulinifikiria kuwa ninafaa kuitekeleza kazi ambayo watu wengine nao walikuwa na shauku ya kuitenda na kupata utukufu kutokana nayo, lakini nilipokuwa bado ningali njiani uliniondolea kazi ile. Je, kuna lolote lililofunuliwa juu yangu?” Mtume (s.a.w.w.) alimjibu kwa upole akisema: “Alikuja Jibril na kuleta ujumbe wa Allah kwamba hakuna awezaye kulitekeleza jukumu hili ila mimi mwenyewe au mtu atokanaye na mimi. “4

Hata hivyo, kutokana na masimulizi ya Ahlus-Sunna inaonekana kwamba Abu Bakr aliishika ofisi ya ukaguzi wa ibada za Hijja ambapo Sayyidna Ali (a.s.) aliteuliwa kuzisoma tu zile aya za Allah na lile tangazo la Mtume (s.a.w.w.) mbele ya watu katika siku ya Mina.5

Amirul-Mu’minin aliwasili Makka. Siku ya kumi ya Dhil Haj aliipanda Jamrah ‘Aqibah (Guzo la mwisho katika yale maguzo matatu ambayo Hujaji huyatupia kokoto saba kila moja), na akazisoma aya kumi na tatu za mwanzoni za Surat al-Baraa’at.

Vile vile alilisoma lile tangazo la Mtume (s.a.w.w.) kwa moyo uliojawa na ushujaa na nguvu na kwa sauti kuu iliyoweza kusikiwa na watu wote waliokuwepo pale, na kuwadhihirishia washirikina wasiokuwa na mapatano yoyote na Waislamu kwamba wanao muda wa miezi minne tu mbele yao, ambapo kwenye muda huo hawana budi kuyatoharisha mazingira yao kutokana na kila aina ya ufisadi na fikra zenye kukaidi, na wauache ushirikina na ibada ya masanamu, na wakishindwa kufanya huvyo, basi ule upendeleo wanaopewa utakomeshwa.

Athari za aya na tangazo hili zilikuwa kwamba ule muda uliotolewa wa miezi minne ulikuwa bado haujamalizika pale washirikina waliposilimu kwa makundi, ilipofika katikati ya mwaka wa kumi Hijiriya ibada ya masanamu ilifutiliwa mbali kabisa kwenye Rasi ya Uarabuni yote.

Chuki Mbaya Katika Kulitathmini Tukio Hili

Kumvua Abu Bakr jukumu la kwenda kuzisoma zile aya za Surat al- Baraa’at na kumteua Amirul-Mu’minin (a.s.) badala yake kwa kuafikiana na amri ya Allah, bila shaka hicho ni moja ya sifa bayana zisizokanushika za Sayyidna Ali (as). Hata hivyo, kikundi sha waandishi washupavu katika mambo ya dini wameyashika maoni ya ukaidi katika kulitathmini tukio hili.

Alipokuwa akilitathmini tukio hili, Alusi Baghdadi anasema kwenye Tafsiri yake hivi: “Abu Bakr alikuwa maarufu kwa huruma zake ambapo Ali alikuwa kinyume chake kwa sababu ya ushujaa na nguvu zake. Kwa kuwa kule kuzisoma zile aya za Sura al –BarA’at na kuwatisha washirikina kulihitaji ushujaa na nguvu za akili zaidi kuliko jambo lolote lile jingine na Ali alikuwa navyo vitu hivi zaidi kuliko Abu Bakr, hivyo, aliteuliwa badala yake.”6

Maelezo haya yaliyosimuliwa katika msingi wa ushupavu wa dini hayalandani na kauli ya Mtume (s.a.w.w.), kwa sababu alipokuwa akimjibu Abu Bakr alimwambia: “Wahyi wa Allah umeamrisha ya kwamba ni lazima aya hizi zisomwe na mimi mwenyewe binafsi au na mtu atokanaye na mimi.” Hivyo basi huruma au ushujaa havina lolote kwenye jambo hili. Aidha, Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe alikuwa mdhihiriko kamili wa huruma.

Hivyo basi, kutokana na maelezo tuliyoyatoa hapo juu, Mtume (s.a.w.w.) naye asingelitakiwa kuwasomea watu aya za Surat al–Baraa’at yeye mwenyewe kwa sababu amri ya Allah ilikuwa kwamba yeye mwenyewe au mtu atokanaye na Ahlul Baiti wake alitekeleza jukumu hili. Alipokuwa akiifasiri Sura hii, Ibn Kathir Shaami, akiyafuata maoni ya Maqrizi, amelieleza jambo hili kwa njia nyingine, kwenye kitabu chake Al- Imta’a anaandika hivi: “Desturi iliyoko miongoni mwa Waarabu kuhusiana na kuyavunja mapatano ilikuwa kwamba mtu aliyemshirika kwenye mapatano yale, au mmoja wa wale wenye uhusianao naye, hana budi kuanza kuyavunja mapatano yale, na kama akishindwa kufanya hivyo, yale mapatano hubakia kuwa sahihi. Na kwa vile Ali alikuwa mmoja wa ndugu wa karibu wa Mtume (s.a.w.w.) aliwajibishwa kuzisoma aya hizi.”

Hata hivyo, maelezo haya nayo si sahihi, kwa sababu miongoni mwa ndugu zake Mtume (s.a.w.w.) vile vile alikuwamo Abbas, ami yake ambaye uhusiano wake naye kwa vyovyote vile si mdogo kuliko ule wa Sayyidna Ali (a.s.). Hivyo basi, swali litabakia palepale kwamba, kwa nini jukumu hili hakupewa yeye Abbas?

Kama tukiombwa kutoa uamuzi usio na upendeleo juu ya tukio hili la kihistoria hatuna budi kusema kwamba huku kutolewa na kuteuliwa hakukutokana na nguvu ya roho ya Sayyidna Ali (a.s.) au uhusiano wake na Mtume (s.a.w.w.), lakini lengo halisi la badiliko hili lilikuwa kwamba kufaa kwa Amirul-Mu’minin (a.s.) kuhusu mambo yahusianayo na serikali ya Kiislamu hakuna budi kudhihirika kivitendo. Na watu hawana budi kutambua kwamba kutokana na fadhila na uwezo wa mtu binafsi, yeye yu mshirika na sahaba wa Mtume (s.a.w.w.).

Na kama baada ya muda utume utakoma, basi mambo ya kisiasa na mambo yenye kuhusiana na mamlaka ya ukhalifa hayana budi kushikwa na yeye, na hakuna mwingine afaaye zaidi kwa mamlaka haya ila yeye binafsi. Na baada ya kufariki dunia kwa Mtume (s.a.w.w.) Waislamu wasipate taabu yoyote, kwa sababu wameona kwa macho yao wenyewe kwamba Sayyidna Ali (a.s.) ameteuliwa kwa amri ya Allah kuyatangua mapatano, na utenguzi ule ni haki pekee ya yule mtawala na mrithi wake tu.

  • 1. Waaqidi ameitaja idadi yao kuwa ni watu mia tatu (Maghaazi-i Waaqidi, Juz. 3, uk. 1077).
  • 2. Katika maelezo mengine, maneno ‘au mtu atokanaye na Ahlul Bayt wako’ hutokea (Siiratu Ibn Hisham Juz. 6, uk. 545 na Bihaarul-Anwaar, Juz. 21, uk. 267)
  • 3. ‘Furu’ Kaafi, Juz. 1, uk. 326.
  • 4. Al-Irshaad Mufid, uk. 33.
  • 5. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 546.
  • 6. Ruhul Ma’aani, katika tafsiri ya Sura al-Tawbah.