Sura Ya 57: Wawakilishi Wa Najraan Mjini Madina

Nchi yenye kupendeza ya Najraan iliyokuwa na vijiji sabini na viwili iko kwenye mpaka wa Hijaz na Yemen.

Katika siku za awali za Uislamu hili lilikuwa eneo pekee nchini Hijaz lililokuwa likikaliwa na Wakristo, ambao kwa sababu fulani fulani waliacha ibada ya masanamu na kuingia dini ya Ukristo.1

Sambamba na barua ambazo Mtume wa Uislamu aliwaandikia wakuu wa nchi mbalimbali za ulimwenguni, vilevile alimwandikia barua Abu Harith, Askofu wa Najraan, na kwa barua ile aliwalingania kwenye Uislamu watu wa eneo lile. Maneno ya barua ile yalikuwa hivi: “Kwa jina la Mola wa Ibrahim, Ishaaq, na Ya’aqub.

Hii ni barua itokayo kwa Muhammad Mtume na Mjumbe wa Allah iendayo kwa Askofu wa Najraan. Ninamsifu na kumtukuza Mola wa Ibrahim, Ishaaq na Ya’qub, na ninakuiteni nyote kumwabudu Allah badala ya kuviabudu viumbe Vyake, ili muweze kutoka chini ya ulinzi wa viumbe wa Allah na kuchukua nafasi chini ya ulinzi wa Allah Mwenyewe.

Na kama hamtaukubali mwito wangu, basi ni lazima (angalau) kulipa Jizyah (kodi) kwenye serikali ya Kiislamu (kwa malipo ambayo itachukua jukumu la kuhifadhi uhai na mali zenu), na mkishindwa kufanya hivyo, mnaonywa juu ya matokeo ya hatari.”2

Baadhi ya vitabu vya Kishia vinaongeza kusema kwamba, vilevile Mtume (s.a.w.w.) aliandika kwenye barua hii, aya ya Qur’ani ihusianayo na watu wa Kitabu ambayo ndani yake wote wameitwa kumwabudu Allah Aliye Mmoja tu. Hapa aya ya sitini na nne ya Sura Aali Imran ilizungumziwa:
“Sema: Enyi watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lililo sawa baina yetu na ninyi: Ya kwamba tusimwabudu yeyote ila Allah, wala tusimshirikishe na chochote, wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa miungu badala ya Allah….”

Mjumbe wa Mtume (s.a.w.w.) aliwasili Najraan na kumpa yule Askofu ile barua. Aliisoma barua ile kwa uangalifu mkubwa, na kisha ili kuweza kutoa uamuzi, aliitisha mkutano wa viongozi wa kidini na wa kilimwengu ili awatake ushauri. Mmoja wa wale watu walioitwa kutoa ushauri alikuwa ni mtu mmoja aliyeitwa Shurahbil aliyekuwa maarufu kwa elimu wake, hekima na ujuzi.

Alipokuwa akimjibu yule Askofu, alisema hivi: “Ujuzi wangu wa mambo ya kidini ni haba mno, na hivyo basi mimi sina haki ya kuzitoa fikiza zangu juu ya mambo hayo, lakini kama ukinitaka ushauri juu ya mambo mengine yasiyokuwa haya ninaweza kutoa maoni yangu juu ya utatuzi wa tatizo hilo. Hata hivyo, ninalazimika kusema jambo moja ambalo ni kwamba kila mara tumekuwa tukisikia kutoka kwa viongozi wetu kwamba kazi ya Utume itahamishwa kutoka kwenye kizazi cha Ishaaq kwenda kwenye kizazi cha Ismaili na kwamba si jambo lisilowezekana kwamba Muhammad ambaye yu kizazi cha Ismail, kuwa ndiye yule Nabii aliyeahidiwa!”

Ile halmashauri ya ushauri iliamua kwamba kikundi cha watu kiende Madina wakiwa ni wawakilishi wa Najraan ili waweze kuonana na Muhammad na kuzichunguza habari za Utume wake. Waliteuliwa watu sita waliokuwa wataalamu na wenye hekima zaidi kutoka miongoni mwa watu wa Najraan. Kikundi hiki kiliongozwa na viongozi wa kidini watatu ambao majina yao yalikuwa haya:

Abu Harith bin Alqamah, Askofu Mkuu wa Najraan aliyekuwa mwakilishi maalumu wa Kanisa Katoliki nchini Hijaz.

Abdul Masih, Mkuu wa kamati ya wawakilishi, aliyekuwa maarufu kwa hekima zake, busara na uzoefu.

Ayham, mtu mzima aliyekuwa akichukuliwa kuwa yu mtu mwenye kuheshimiwa wa jumuiya ya watu wa Najraan.3

Wajumbe hawa waliwasili msikitini wakati wa alasiri wakiwa wamevaa nguo za hariri, pete za dhahabu na misalaba shingoni mwao, wakamsalimu Mtume (s.a.w.w.). Hata hivyo, hali yao yenye kuchukiza na isiyo sahihi, na pia ikiwa ni msikitini, ilimchukiza Mtume (s.a.w.w.). Walitambua kwamba wamemuudhi, lakini hawakuelewa ni kipi kilichomuudhi.

Hivyo basi, upesi sana walionana na Uthman bin Affan na Abdur-Rahman bin Awf, waliokuwa wakiwajua kabla ya hapo na wakawaeleza jambo lile. Uthman na Abdur-Rahman waliwashauri kwamba ufumbuzi wa tatizo lao uko mikononi mwa Sayyidna Ali bin Abu Twalib (as). Hapo wakakutana na Amirul-Mu’minin (a.s.), naye akiwajibu, akiwaambia: “Lazima mbadilishe mavazi yenu na kwenda kwa Mtume mkiwa mmevaa nguo zilizo rahisi na bila ya kuwa na mapambo yoyote yale. Hapo mtapata heshima na taadhima.”

Wale wawakilishi wa Najraan wakavaa nguo rahisi na wakavua zile pete na kisha wakamjia Mtume (s.a.w.w.). Mtume (s.a.w.w.) akaijibu salam yao kwa heshima kuu na vilevile alizipokea baadhi ya zawadi walizozileta. Kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya pande zote mbili wale wajumbe walisema kwamba muda wao wa sala ulikuwa umewadia, Mtume (s.a.w.w.) aliwaruhusu kusali sala zao msikitini mle wakizielekeza nyuso zao upande wa Mashariki.4

Wajumbe Wa Kutoka Najraan Wajadiliana Na Mtume (S.A.W.W.)

Idadi kubwa ya waandishi wa wasifu, wanahadithi na wanahistoria wa Kiislamu, wameyanukuu maneno ya mazungumzo baina ya wawakilishi wa Najraan na Mtume (s.a.w.w.). Hata hivyo, Marehemu Sayyid bin Taawus ameyanukuu maneno ya majadiliano yale na tukio la Mubahila (Maapizano) katika hali iliyo sahihi zaidi, kwa upana zaidi na kwa namna ya maelezo marefu zaidi, ukilinganisha na waandishi wengine. Ameyanukuu mambo yote na Mubahila tangu mwanzoni hadi mwishoni kutika kitabu kiitwacho “Kitabu Mubaahila’ cha Muhammad bin Abdul Muttalib Shabaan na ‘Kitab ‘Amaali Dhil Haj cha Hasan bin Ismail.5

Hata hivyo, ni nje ya upeo wa kitabu hiki kutoa maelezo marefu ya tukio hili la kihistoria, ambalo kwa bahati mbaya hata halikudokezwa na baadhi ya waandishi wa wasifu. Kwa hiyo, tunataja hapa mambo machache juu ya mazungumzo yale, kama yalivyoelezwa na Halabi katika kitabu chake kiitwacho Siiratu.6

Mtume (s.a.w.w.): “Ninakuiteni kwenye dini ya Upweke wa Allah na ibada ya Allah Aliye Mmoja tu na kuzitii amri Zake.” Kisha Mtume (s.a.w.w.) akazisoma baadhi ya aya za Qur’ani mbele yao.

Wajumbe wa Najraan: “Kama Uislamu una maana ya kumwamini Mola wa Ulimwengu, sisi tayari tumeshamwamini na tunazitekeleza amri zake.”

Mtume (s.a.w.w.): “Uislamu una dalili chache na baadhi ya matendo yenu yanaonyesha kwamba hamuuamini Uislamu. Mnawezaje kusema kwamba mnamwanini Allah Aliye Mmoja tu na hali mnauabudu msalaba na hamjiepushi na nyama ya nguruwe na mnaamini kwamba Allah anaye mwana?”

Wajumbe wa Najraan: “Tunamwamini yeye (yaani Isa) kuwa yu mungu kwa sababu aliwafufua wafu, aliwaponya wagonjwa, alimtengeneza ndege kutokana na udongo na kumfanya aruke, na mambo yote haya yaonyesha kwamba yeye ni mungu.”

Mtume (s.a.w.w.): “Hapana! Yeye yu mja wa Allah naye yu kiumbe chake. Allah Alimweka kwenye tumbo la uzazi la Maryamu. Na uwezo na nguvu yote hii alipewa na Allah.”

Mjumbe mmoja: “Ndio! Yeye yu mwana wa Muumba, kwa sababu Maryamu alimzaa bila ya mume yeyote, na hivyo basi, ni muhimu kwamba baba yake ni Yeye yule Mola wa ulimwengu.”

Kufikia hapa, Malaika Mkuu Jibriil (a.s.) alishuka na kumshauri Mtume (s.a.w.w.) awaambie: “Kwa mujibu wa maoni hayo, hali ya Isa ni kama ile ya Adamu aliyeumbwa na Allah kwa nguvu Zake zisizo kifani, kutokana na udongo bila ya yeye kuwa na baba wala mama.7 Kama mtu kutokuwa na baba ni uthibitisho wa kuwa kwake mwana wa Mungu, basi Adamu anastahiki zaidi cheo hiki kwa sababu yeye hana baba wala mama.”

Wajumbe wa Najraan: “Maneno yako hayatutoshelezi. Njia iliyo bora zaidi ya kulitatua swali hili ni ile ya kwamba tufanye Mubahala (Maapizano) baina yetu katika muda utakaowekwa na kumlaani yule aliye mwongo baina yetu na tumwombe Allah kwamba Amwangamize yule aliye mwongo.”8

Wakati huo huo Malaika Mkuu Jibriil (a.s.) alikuja na akaileta ile Aya ihusianayo na Mubaahila na kuiwasilisha kwa Mtume (s.a.w.w.) amri ya Allah kwamba yeye Mtume (s.a.w.w.) afanye hicho kiapo na wale washindanao na kumbishia, na makundi yote mawili yaombe kwa Allah kwamba Amnyime yule mwongo baraka Yake. Qur’ani Tukufu inasema: “Watakao kuhoji katika haya baada ya kukufikia ilimu hii waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake zetu na wanawake zenu, na nafsi zetu na nyinyi nafsi zenu, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Allah iwashukie waongo.” (Sura Aali Imran 3:61).

Pande zote mbili zilikubali kulitatua suala hili kwa njia ya kulaaniana, na iliamuliwa kwamba wote wajiweke tayari kwa ajili ya maapizano hayo katika siku inayofuata.

Mtume (S.A.W.W) Aenda Kwenye Maapizano

Tukio la Mubaahilah ya Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) na wajumbe wa Najraan ni moja ya matukio yenye kuvutia na mazuri sana ya historia ya Uislamu. Ingawa baadhi ya wanahadithi na waandishi wa wasifu wa Mtume (s.a.w.w.) wameepuka kuzitaja taarifa zake kwa urefu na vilevile katika kulifafanua, lakini idadi yao kubwa kama vile Zamakhshari kwenye Kashshaf,9 Imamu Raza kwenye Tafsiir10 yake na Ibn Athir kwenye Kaamil11 wametamka kwa ufasaha zaidi kuhusu jambo hili. Tunanukuu hapa chini sehemu ya maelezo ya Zamakhshari kuhusu jambo hili.

“Muda wa Mubaahilah ukawadia Mtume (s.a.w.w.) na wajumbe wa ujumbe wa Najraan walikuwa wamekwisha kukubalina kwamba hafla ya Mubaahilah ifanyike mahali fulani nje kidogo ya mji wa Madina, kwenye jangwa. Mtume (s.a.w.w.) aliwachagua watu wanne tu wa kushiriki kwenye tukio hili muhimu mno miongoni mwa Waislamu na ndugu zake wengi. Watu hawa wanne walikuwa ni Ali bin Ali Twalib, Fatimah binti yake Mtume (s.a.w.w.), Hasan na Husein (a.s.), kwa kuwa miongoni mwa Waislamu wote hakuna nafsi zilizo safi zaidi ya hizi. Alitembea kutoka nyumbani kwake hadi kwenye ile sehemu iliyochaguliwa kwa ajili ya Mubaahilah kwa jinsi maalumu. Aliingia kwenye uwanja wa Mubaahilah akiwa amempakata Husain na kumshika Hasan kwa mkono wake, na Fatimah alikuwa akimfuatia, na Ali bin Abi Twalib alikuwa akiwafuatia nyuma yao.12

Kabla ya kuwasili kwenye ile sehemu ya Mubahilah aliwambia masahaba zake: “Dua yoyote nitakayoitamka ninyi hamna budi kuomba kutakabaliwa kwake na kusema: Amin.”
Kabla ya kumkabili Mtume (s.a.w.w.) machifu wa wajumbe wa Najraan walikuwa wakiambiana: “Kama mkiona Muhammad amewaleta mashujaa na maafisa wake kwenye uwanja wa Mubahilah na kuuonyesha utukufu wake wa kidunia na nguvu ya nje, basi mfahamu kwamba lengo lake si la kweli na kwamba hauamini utume wake.

Hata hivyo, iwapo atakuja kwenye Mubahila pamoja na watoto wake, na walio wapenzi, na anakuja mbele ya Allah, Mwenye nguvu zote akiwa bila ya nguvu na utukufu wa kidunia, itakuwa na maana ya kwamba yu Mtume wa kweli na anayo imani kubwa sana na kujitegemea, kiasi kwamba sio tu kwamba yuko tayari kuangamia mwenyewe binafsi, bali yuko tayari kwa ujasiri kamili kuwafanya wale walio wapenzi wake nao kukumbwa na maangamizi na kutoweka.”

Wakati wale machifu wa wajumbe walipokuwa wakijishughulisha na yale mazungumzo, Mtume (s.a.w.w.) alijitokeza kwa ghafla mbele ya Wakristo wa Najraan pamoja na watu wanne kutoka miongoni mwa wale walio wapenzi wake zaidi, ambao watatu miongoni mwao walikuwa kizazi chake mwenyewe. Wote walishikwa na mshangao kuona kwamba amewaleta kwenye uwanja wa Mubaahilah hata watoto wasio na hatia wa binti yake mpenzi, na wakasema: “Mtu huyu anayo imani kamili katika mwito na dai lake kwa kuwa mtu mwenye mashaka hawaleti watu walio wapenzi wake zaidi kwenye sehemu ya ghadhabu ya Allah.”

Yule Askofu wa Najraan akasema: “Ninaziona nyuso ambazo kama wakiinua mikono yao na kuomba dua na kumwomba Allah kwamba mlima ulio mkubwa sana usogee kutoka kwenye sehemu yake, utasogea mara moja.

Kwa hali yoyote ile iwavyo tusijitie kwenye Mubahilah na watu hawa watakatifu na wachamungu, kwa sababu si jambo lisilowezekana kwamba tutaangamia, na vilevile ni jambo liwezekanalo kwamba ghadhabu ya Allah inaweza ikatanuka na kuuzingira ulimwengu mzima wa kikristo na asiwepo hata mkristo mmoja atakayebakia hai kwenye uso wa ardhi.”13

Wajumbe Wa Najraan Wajitoa Kwenye Mubahilah

Baada ya kuiona hali tuliyoitaja hapo juu, wale wajumbe wa Najraan walishauriana na wote kwa pamoja wakaamua ya kwamba wasishiriki kwenye Mubaahilah kwa vyovyote vile iwavyo. Vilevile walikubali kulipa kiasi kilichowekwa kwa kila mwaka ikiwa ni Jizyah na wakaomba kwamba badala ya malipo hayo, serikali ya Kiislamu ihifadhi uhai na mali zao. Mtume (s.a.w.w.) aliyakubali hayo na ikakubaliwa hivyo kuwa kwa malipo ya kiasi kile, wao wawe na haki ya kupata fursa zitolewazo na serikali ya Kiislamu. Kisha Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Matatizo yameeneza kivuli chake cha ndege mbaya (kisirani) vichwani mwa wale wajumbe wa Najraan na kama wangeliamua kushiriki kwenye Mubaahila na kulaaniana wangelilipoteza umbile lao la kibinadamu na wangelichomwa kwenye moto uliokuwa ukiwashwa kule jangwani na mateso yangalienea hadi kwenye nchi ya Najraan.”

Imenukuliwa na Bibi Aisha kwamba, katika siku ya Mubaahilah Mtume (s.a.w.w.) aliwaweka dhuria wake wapenzi wanne chini ya shuka lake jeusi na akaisoma aya isemayo: “...Hakika Allah Anataka kukuondoleeni uchafu enyi Ahlil-Bayti na kukutoharisheni kabisa kabisa…”
(Surat al- Ahzaab, 33:33)

Kisha Zamakhshari anayataja mambo yahusianayo na ile aya ya Mubaahilah na mwishoni mwa mazungumzo yake anasema: “Tukio la Mubahilah na kiini cha aya hii ni ushahidi mkuu zaidi wa fadhila (ubora) za wale ‘watu wa shuka’ (Ahlu’l-Kisaa) na ni uthibitisho wa dhahiri wa usahihi wa Uislamu!”

Yaliyomo Katika Mkataba Uliofikiwa Kati Ya Pande Mbili Hizo

Wale wajumbe wa Najraan walimwomba Mtume (s.a.w.w.) kwamba, kile kima wapasikacho kulipa kila mwaka na usalama wa jimbo la Najraan viandikwe na yahakikishwe na Mtume (s.a.w.w.) kwenye hati. Amirul-Mu’minin aliwaandikia mkataba ule kama alivyoamrishwa na Mtume (s.a.w.w.), kama ifuatavyo: “Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

Huu ni hati itokayo kwa Muhammad Mjumbe wa Allah, kwa ajili ya watu wa Najraan na vitongoji vyake. Amri na uamuzi wa Muhammad juu ya mali na utajiri wote wa watu wa Najraan ni kwamba kila mwaka wataipa serikali ya Kiislamu nguo elfu mbili ambazo bei ya kila moja haitazidi dirhamu arobaini. Watakuwa huru kutoa nusu ya idadi hiyo kwenye mwezi wa Safar na ile nusu iliyosalia kwenye mwezi wa Rajab.

Na kama itakuwako hatari ya vita kutoka upande wa Yemen, wao (watu wa Najraan) ikiwa ni dalili ya ushirikiano wao na serikali ya Kiislamu, watatoa deraya thelathini, farasi thelathini na ngamia themanini kulipa jeshi la Uislamu kwa njia ya mkopo ulio dhaminiwa. Na vilevile watawajibikiwa kuwafanyia takrima wawakilishi wa Mtume (s.a.w.w.) kwenye jimbo la Najraan kwa kipindi cha mwezi mmoja. Aidha, atakapofika mjumbe wa Mtume (s.a.w.w.) nchini mwao, watampokea. Na uhai, mali, ardhi na sehemu za kuabudia za watu wa Najraan zitakuwa chini ya ulinzi wa Allah na Mtume Wake, ili mradi tu kwamba upesi sana wataacha kula rushwa. Na endapo watashindwa kufanya hivyo, Muhammad hatakuwa na jukumu lolote juu yao na hatawajibika kulitekeleza lolote katika aliyoyaahidi.”14

Mkataba huu uliandikwa kwenye ngozi nyekundu. Masahaba wawili wa Mtume (s.a.w.w.) wakatia saini zao chini yake wakiwa ni mashahidi na baada ya hapo Mtume (s.a.w.w.) akayatia muhuri. Mkataba huu wa amani ambao tafsiri yake imetolewa kwa mukhtasari hapo juu, huidhihirisha haki na usawa wa hali ya juu zaidi kama ulivyotekelezwa na Mtume (s.a.w.w.). Na unaonyesha kwamba Serikali ya Kiislamu haikuwa kama zilivyo nchi zenye nguvu za ulimwenguni zinazojinufaisha visivyostahili kutokana na unyonge wa watu wengine na kuwatoza kodi. Daima Uislamu ulizingatia moyo wa upatanishi na uadilifu na misingi ya ubinadamu; na daima ulikomesha hujuma.

Tukio la Mubaahila na aya iliyoshushwa kuhusiana nayo, vimekuwa ni fadhila kubwa zaidi na utukufu kwa Uislamu na wafuasi wa Ahlil Bayt (a.s.) kwenye kipindi chote cha historia, kwa sababu maneno na maelezo ya aya hii hukionyesha cheo cha juu zaidi walichokuwa nacho wale waliofuatana na Mtume (s.a.w.w.) kwenda kwenye sehemu ile iliyoteuliwa kwa ajili ya Mubaahila, kwa kuwa baada ya kuwaita Hasan na Husain wana wa Mtume (s.a.w.w.) na kumwita Bibi Fatimah (a.s.) kuwa mwanamke pekee wa nyumba yake, inamwita Sayyidna Ali (a.s.) ‘nafsi’ yaani nafsi hasa ya Mtume (s.a.w.w.). Ni heshima gani iwezayo kuwa kubwa zaidi ya hiyo kwa mtu yeyote yule?

Je aya hii si ushahidi wa fadhila za Amirul-Mu’minin (a.s.) juu ya Waislamu wengine wote wa humu ulimwenguni? Fakhri Razi, ambaye msimamo wake juu ya majadiliano ya hali ya theolojia na mambo yahusianayo na Uimamu ni maarufu, amezitaja hoja za Kishia na ameyamalizia majadiliano hayo kwa ukinzani ulio dhaifu na mdogo. Jibu lake ni dhahiri kabisa kwa watu wenye fikira zisizo na upendeleo.

Imefahamika kutokana na maelezo yaliyonukuliwa kutoka kwa viongozi wetu wa kidini kwamba, Mubaahila si hususani kwa Mtume (s.a.w.w.) tu, kila Mwislamu anaweza kupambana na mpinzani wake kwa njia hii.
Dua zinazohusiana nayo zimeandikwa kwenye vitabu vya Hadith, na kitabu kiitwacho ‘Nuruth-Thaqalayn’ kinaweza kurejewa katika kupata taarifa zaidi.15 Kwenye kijitabu kilichoandikwa na mwalimu mheshimiwa Allamah Tabatabai tunasoma hivi: “Mubaahilah ni moja ya miujiza ya kudumu ya Uislamu na kila Muumini wa kweli anaweza kupambana na mpinzani wake kwa njia ya Mubaahilah ili kuuthibitisha ukweli wa Uislamu, kwa kumfuata kiongozi wa kwanza wa dini hii, na anaweza kumwomba Allah kumwadhibu mpinzani yule na kumlaani.”16

 • 1. Yaqut Hamawi ameieleza sababu ya kuingia kwao Ukristo kwenye kitabu chake kiitwacho Majma’ul Buld?n, Juz. 5, uk. 266-267.
 • 2. Al-Bidayah Wan-Nihayah, uk. 54 na Bihaarul Anwaar, Juz. 21, uk. 285.
 • 3. Tarikhu Yaqubi, Juz. 2, uk. 66.
 • 4. Siiratu Halabi, Juz.3, uk. 239.
 • 5. Maelezo kwa kirefu ya tukio hili la kihistoria yameelezwa kwenye kitabu kiitwacho ‘Iqbal’ cha marehemu Ibn Taawusi, uk. 496-513.
 • 6. Siiratu Halabi, juz. 3, uk. 239.
 • 7. Hii ndio maana ya Aya: “Hakika mithili ya Isa mbele ya Allah ni kama mithili ya Adamu; Alimuumba kutokana udongo, kisha akamwambia kuwa na akawa.” (Surah Aali Imran, 3:59)
 • 8. Bihaarul-Anwaar, Juz. 21, uk. 32 kama ilivyonakiliwa kutoka ‘Al-Iqbal’ cha Ibn Taawus. Hata hivyo kutoka kwenye ‘Siirah Halabi’ tunajifunza kwamba Mubaahila ulipendekezwa na Mtume (s.a.w.w.)mwenyewe.
 • 9. Kashaf, Juz. 1, uk. 282-283.
 • 10. Tafsiirul-Mafaatihul Ghayb, Juz. 2, uk. 481-482.
 • 11. Tarikhul-Kamil, juz. 2, uk. 112.
 • 12. Kwenye maelezo mengine imeelezwa kwamba Mtume (s.a.w.w.) alikuwa ameishika mikono ya Hasan na Husain na Sayyidna Ali (as) alikuwa mbele ya Mtume (s.a.w.w.) na Fatimah alikuwa akifuatia nyuma ya Mtume (s.a.w.w.). Bihaarul Anwaar, Juz. 21, uk. 338.
 • 13. Ibn Taawus ananakili hivi kutoka kitabu ‘Al-Iqbal’: Kwenye siku ya Mubaahilah idadi kubwa ya Muhajiriin na Ansar walijikusanya karibu na ile sehemu ambapo Mubaahila ulikuwa ufanyike. Hata hivyo, Mtume alitoka nyumbani kwake na wale watu wanne tuliowataja hapo juu tu na hakuna yeyote miongoni kwa Waislamu aliyekuwako pale kwenye ile sehemu iliyoteuliwa kwa ajili ya kazi ile ila hawa watu watano. Mtume (s.a.w.w.) alilivua joho lake kutoka mabegani mwake na kulitanda kwenye miti miwili iliyokuwa karibu karibu. Kisha akakaa chini ya kivuli cha joho lile pamoja na wale wajumbe wa Najraan kwenye Mubaahilah.
 • 14. Futuhul Buldaan, uk. 76.
 • 15. Nuruth-Thaqalayn, Juz. 1, uk. 291-292.
 • 16. Maudhui hii imefafanuliwa kwenye baadhi ya masimulizi ya Kiislamu. Kuhusiana na jambo hili, rejea kwenye Usulul Kaafi’ Kitabu cha Dua, Sura ya Mubaahilah uk. 538.