Sura Ya 58: Matukio Ya Mwaka Wa Kumi Hijiriya

Tangazo kali na chungu lililosomwa na Amirul-Mu’minin kwenye majira ya Hijja kwenye mwaka wa tisa Hijiriya kule Mina kwa niaba ya Mtume (s.a.w.w.), na tangazo rasmi alilotoa yeye kwamba Allah na Mtume Wake wanachukizwa na waabudu masanamu na wao (waabudu masanamu) waamue mara ya kwanza na ya mwisho katika kipindi cha miezi minne kusilimu na kuiacha ibada ya masanamu au kuwa tayari kwa vita kamili, lilikuwa na athari za kina na za haraka zaidi.

Makabila ya Waarabu wa mikoa mbalimbali ya Uarabuni ambayo hadi hapo walikuwa tayari wameshakataa kuzikubali hoja za Qur’ani na sheria za Allah kutokana na uadui na mfundo, na kung’ang’ania katika kuzishikilia desturi zao zilizo mbaya na chafu, mapokeo ya itikadi za kijinga na ibada za mawe na udongo, sasa wakabaki bila ya msaada wowote na wakaanza kuwapeleka wajumbe wao kwenye makao makuu ya Uislamu (Madina). Kila mmoja wa wajumbe hawa alikuwa na majadiliano na mazungumzo na Mtume (s.a.w.w.).

Ibn Saad kwenye kitabu chake Tabaqaatul-Kubra1 amesimulia taarifa za watu sabini na wawili miongoni mwao. Kuwasili kwa wawakilishi hawa kwa wingi na pia kwamba baada ya kutamka ile shahada, huonyesha kwamba mwanzoni mwa mwaka wa kumi wa Hijiriya, haikuweko ngome ya kutegemewa iliyoachwa kwa washirikina wa Uarabuni, vinginevyo wangelikimbilia huko na kupigana vita dhidi ya Waislamu kwa kushirikiana wao kwa wao.

Kile kipindi cha miezi minne kilikuwa bado hakijapita wakati pale Hijaz nzima ilipokuja chini ya bendera ya Uislamu na halikubakia humo hekalu hata moja la masanamu au sanamu au mwaabudu masanamu, kiasi kwamba idadi ya watu wa Yemen, Bahrain na Yamamah nao walisilimu.

Njama Ya Kumuuwa Mtume (S.A.W.W)

Machifu wa makabila ya Bani ‘Aamiri walikuwa maarufu mno miongoni mwa makabila ya Kiarabu kwa ukaidi na uasi wao. Watu watatu kutoka miongoni mwa machifu wao walioitwa ‘Amir, Arbad na Jabbar waliamua kuja Madina wakiuongoza ujumbe hasa kwa nia ya kutaka kumuuwa Mtume (s.a.w.w.) wakati wakiwa wanafanya majadiliano naye kwenye mkutano. Mpango wao ulikuwa kwamba ‘Amir ajishughulishe na majadiliano na Mtume (s.a.w.w.) na wakati yale mazungumzo yao yakiwa yanaendelea, Arbad amshambulie Mtume kwa upanga wake na kumuuwa.

Wale wajumbe wengine ambao hawakuujua mpango ule wa wale watu watatu, waliutangaza uaminifu wao kwa Uislamu na Mtume (s.a.w.w.). Hata hivyo ‘Amir alikataa kuonyesha mwelekeo wake kwenye Uislamu na kumwambia Mtume (s.a.w.w.) kwa kurudia rudia kwamba: “Ninataka kuzungumza nawe kwa siri.” Kila alipoitamka kauli hii alikuwa akimtazama yule Arbad. Hata hivyo, ingawa aliutazama uso wake kwa makini, alimwona kuwa katulia na shwari. Mtume (s.a.w.w.) alimjibu akisema: “Jambo hili haliwezekani mpaka pale utakaposilimu (yaani kule kuonana nawe ukiwa peke yako)”

Hatimaye Amir aliyapoteza matumaini yote ya kupata msaada wa Arbad katika kufaulu kwa mpango wao. Inaonekana kwamba pale Arbad alipodhamiria kuuweka mkono wake kwenye ule upanga wake alikumbwa na hofu, na ukuu wa Mtume (s.a.w.w.) ulimzuia (yeye Arbad) kuutimiza mpango ule. Ule mkutano ulipomalizika, Amir alisimama pale alipokuwapo akatangaza uadui wake kwa Mtume (s.a.w.w.) na akasema: “Nitaijaza Madina kwa farasi na askari kukudhuru.”

Hata hivyo Mtume (s.a.w.w.) kutokana na uvumilivu mkubwa aliokuwa nao, hakumjibu bali alimwomba Allah amlinde kutokana na uasi wa wale watu wawili. Dua ya Mtume (s.a.w.w.) ilitakabaliwa upesi sana. ‘Aamir alipata mashambulizi ya tauni alipokuwa njiani na akafa katika hali mbaya mno nyumbani mwa mwanamke mmoja wa kabila la Bani Salul. Ama kuhusu yule Arbad, alipigwa na radi akiwa jangwani na akaugua hadi akafa. Na maamuru waliyoyapata watu hawa waliopanga mpango mbaya dhidi ya Mtume (s.a.w.w.) yaliimarisha zaidi imani ya watu katika Uislamu.2

Amirul-Mu’minin Atumwa Yemen

Kusilimu kwa watu wa Hijaz na usalama aliouhisi Mtume (s.a.w.w.) kutoka kwenye upande wa makabila ya Kiarabu vilimwezesha kuendeleza ushawishi wa Uislamu hadi kwenye maeneo ya jirani na Hijaz. Hivyo basi, kwa mara ya kwanza alimpeleka mmoja wa masahaba zake wenye hekima aliyeitwa Mu’aaz bin Jabal Yemen ili akawaeleze Uislamu watu wa eneo lile.

Alipokuwa akimpa maelekezo kwa kirefu Mtume (s.a.w.w.) vilevile alimwambia Mu’aaz; “Jiepushe na kuwa mkali kwa watu na uwajulishe neema ya Allah iliyoko kwa ajili ya waumini wa kweli. Utakapokutana na watu wa Kitabu huko Yemen na wakakuulizia kuhusu ufunguo wa Peponi basi waambie kwamba ni utambuzi wa Upweke na kutokuwa na kifani kwa Allah.”

Mu’aaz hakuweza kutoa jibu la kutosheleza alipoulizwa kuhusu haki za Mume kwa mkewe.3
Hivyo basi, Mtume (s.a.w.w.) akaamua kumpeleka sahaba wake mwenye fadhila zaidi, Sayyidna Ali (a.s.) kwenda Yemen ili Uislamu uweze kuendelea huko chini ya mafundisho yake, hoja zake za kimantiki, nguvu za mikono yake na ushujaa wake usio kifani na uhodari.

Aidha, Khalid bin Walid naye alipelekwa na Mtume (s.a.w.w.) nchini Yemen wakati fulani kabla ya Sayyidna Ali (a.s.)4 ili akaviondoe vizuizi zilivyokuwako kwenye njia ya uendelezaji wa Uislamu kwenye eneo lile. Hata hivyo, hakuweza kufanya jambo lolote lile kuhusiana na kazi hii katika kipindi kile.

Hivyo, Mtume (s.a.w.w.) alimwita Sayyidna Ali (as) na akamwambia: “Ewe Ali! Ninakupeleka Yemen ili ukawalinganie wakazi wake kwenye Uislamu na kuwajulisha Amri za Allah pamoja na mambo yaliyo halali na yaliyo haramu.

Wakati wa kurejea kwako Madina, ukusanye Zaka kutoka kwa watu wa Najraan pamoja na kodi wapasikayo kulipa na kuiweka kwenye hazina ya Umma.”

Sayyidna Ali (a.s.) alimjibu Mtume (s.a.w.w.) kwa heshima mno, kwa maneno haya: “Mimi bado ni kijana, maishani mwangu mwote bado sijawahi kupatanisha na katu sikupata kukikalia kiti cha hakimu.” Mtume (s.a.w.w.) aliubandika mkono wake kifuani mwa Sayyidna Ali (a.s.) na kumwombea kwa maneno haya: “Ee Allah! Uongoze moyo wa Ali na uhifadhi ulimi wake kutokana na makosa.” Kisha akasema: “Ewe Ali! Usigombane na yeyote yule na jaribu kuwaongoza watu kwenye njia iliyonyooka kwa hoja na tabia njema.
Ninaapa kwa jina la Allah! Kama Allah anamwongoza mtu kwenye njia iliyonyooka kupitia kwako, ni bora zaidi kuliko vile viangazwavyo na jua.”

Mwishoni Mtume (s.a.w.w.) alimpa Sayyidna Ali (a.s.) mapendekezo manne: Kuifanya Sala na kumtukuza Allah ni kazi yako kwa sababu Sala ni yenye kutakabaliwa. Kuwa mwenye shukrani kwa Allah kwenye hali zote, kwa sababu shukrani huongeza baraka. Kama ukifanya mapatano na mtu, au kikundi cha watu yaheshimu. Jiepushe na kuwahadaa watu, kwa sababu udanganyifu wa watenda maovu unawarudia wao wenyewe.

Sayyidna Ali (a.s.) kwenye kile kipindi cha kukaa kwake nchini Yemen alikata hukumu zenye kustaajabisha ambazo nyingi kati ya hizo zimerekodiwa kwenye vitabu vya historia. Mtume (s.a.w.w.) hakutosheka na mwongozo ule, bali vile vile aliwaandikia barua watu wa Yemen akiwaita kwenye Uislamu akampa Sayyidna Ali (as) barua ile na akamwelekeza kwenda kuwasomea.

Bara’ bin Azib alikuwa mhudumu wa Sayyidna Ali (a.s.) kule nchini Yaman. Anasema kwamba Sayyidna Ali (a.s.) alipofika kwenye mpaka wa Yemen, alizipanga safu za askari wa Uislamu waliokuwa tayari wameshapelekwa kule chini ya uongozi wa Khalid bin Walid na akasali sala ya jamaa ya alfajiri pamoja nao. Kisha akaliita kabila la Hamdan lililokuwa moja ya makabila makuu zaidi ya Yemen, kuusikia ujumbe wa Mtume (s.a.w.w.).

Kwanza alimtukuza Allah. Kisha akawasomea ujumbe wa Mtume (s.a.w.w.). Utukufu wa mkutano ule, utamu wa maelezo na ukuu wa maneno ya Mtume (s.a.w.w.) valiwavutia mno watu wa kabila la Hamdan kiasi kwamba walisilimu katika siku moja. Imamu Ali (a.s.) alimwandikia barua Mtume (s.a.w.w.) akimweleza maendeleo yaliyopatikana. Mtume (s.a.w.w.) alifurahi sana kuzisikia habari njema. Alimshukuru Allah akasema: “Na libarikiwe kabila la Hamdan.” Kusilimu kwa kabila la Hamdan ilikuwa chanzo cha watu wengine wa Yemen kusilimu upesi sana.5

  • 1. Tabaqaatul-Kubra, Juz. 2, uk. 230-291.
  • 2. Siiratu Ibn Hisham Juz. 2, uk. 568-569.
  • 3. Siiratu Ibn Hisham Juz. 2, uk. 590.
  • 4. Sahih Bukhari, Juz. 5, uk. 163.
  • 5. Tarikhul-Kamil, Juz. 2, uk. 305; Bihaarul-An’waar, Juz. 21, uk. 360-363.