Sura Ya 59: Hijja Ya Mwago

Miongoni mwa kanuni za jamaa za ibada za Uislamu, kaida za Hijja ndizo ibada zilizo kuu na tukufu zaidi, kwa sababu kuzitekeleza kaida hizi na kwamba pia ni mara moja kwa mwaka ni udhihirisho mtukufu wa umoja na ushirikiano, ishara kamili ya uhuru kuanzia mali na mahali, na ni mfano mashuhuri zaidi wa usawa baina ya matabaka mbalimbali ya watu, na chanzo cha kuimarisha uhusianao baina ya Waislamu n.k. Sasa, kama sisi Waislamu tukiitumia kwa kiasi kidogo tu ile nafasi tuipatayo katika Hijja kwa ajili ya kuitengeneza hali yetu, na hatimaye kuubadili huu mkutano wa Kiislamu wa kila mwaka (ambao bila shaka unaweza kutatua mengi ya matatizo ya kijamii na unaweza kuleta mabadiliko kwenye maisha yetu) bila ya kupata faida zenye kustahili kutokana nao, si kwa sababu ya kwamba sheria ya Hijja ina upungufu bali kosa litakuwa liko kwa viongozi wa Kiislamu ambao hawaitumii vizuri sherehe hii kubwa.

Tangu siku ile Nabii Ibrahim (a.s.) alipoijenga Ka’abah na kuwaalika wenye kumwabudu Mungu Mmoja kuja kufanya Hija yake, daima sehemu hii imekuwa kituo chenye kuvutia, ambapo Tawaaf ilikuwa ikifanywa na watu wachamungu na kila mwaka makundi ya mahujaji yalikuja hapo kutoka sehemu mbalimbali za Uarabuni na kutoka kwenye pembe zote ulimwenguni kuja kufanya Hija ya Nyumba hii, nao walizitekeleza ibada walizofundishwa na Nabii Ibrahimu (a.s.).

Hata hivyo, kama matokeo ya kadiri muda ulivyopita, na vilevile kwa sababu ya watu wa Hijaz kukosa mwongozo wa Mitume, choyo cha Waquraishi, na utawala wa masanamu juu ya ulimwengu wa Kiarabu, ibada za Hijja zilipatwa na mabadiliko kutokana na mtazamo wa nyakati na mahali, na hatimaye kupoteza sura yake halisi.

Kwa sababu hizi Mtume (s.a.w.w.) aliamrishwa na Allah katika mwaka wa kumi hijiriya kushiriki kwenye ibada za Hijja yeye mwenyewe binafsi ili kwamba aweze kuwafunza watu kivitendo majukumu yao na kuweza kuyatupilia mbali desturi za kale na zisizohitajika za ibada hii, na vilevile kuwafunza watu kuhusu mipaka ya Arafat na Mina na kuwaambia kuhusu muda wa kuondoka kwenye sehemu hizo. Hivyo basi, ikilinganishwa na hali yake ya kisiasa na kijamii, safari hii ina hali ya kielimu iliyo kuu sana.

Katika mwezi wa kumi na moja wa Kiislamu (Dhil-Qa’adah) Mtume (s.a.w.w.) alitoa amri itangazwe mle mjini Madina pamoja na miongoni mwa makaliba kwamba, alidhamiria mwaka ule kufanya Hijja ya Ka’abah. Taarifa hii ilizaa shauku kubwa kwenye umma wa Kiislamu. Maelfu ya watu waliyakita mahema nje ya mji wa Madina na kusubiri kuondoka kwa Mtume (s.a.w.w.).1

Mtume (s.a.w.w.) alimteua Abu Dujanah kuwa mwakilishi wake mjini Madina na yeye mwenyewe akaondoka kwenda Makka mnamo tarehe ishirini na nane Dhil-Qa’adah akichukua wanyama sitini wa kutoa kafara. Alipofika Dhil Hulayfah alivaa Ihram kwenye Masjid Shajarah, iliyokuwa ni shuka mbili nyeupe. Na alipokuwa akivaa ile Ihram aliisoma dua maarufu inayoanza na neno Labbayk ambalo ni jibu la mwito wa Nabii Ibrahim (a.s.).

Alisema Labbayk kila mara alipomwona mtu aliyempanda mnyama au alipofika kwenye sehemu iliyoinuka au iliyo chini. Alipofika karibu na mji wa Makka aliacha kulitamka lile neno Labayk. Aliwasili Makka mnamo mwezi nne Dhil Hajj na akaenda moja kwa moja hadi Masjid Haraam, akaingia humo kupitia kwenye lango la Bani Shaybah. Kisha akaanza kumtukuza Allah na kuomba baraka kwa ajili ya Nabii Ibrahimu (a.s.).

Wakati wa kufanya Tawaaf, alisimama upande wa pili wa Hajarul Aswad (Jiwe Jeusi). Mara ya kwanza aliitekeleza ‘Istilaam’2 yake na kisha akaizunguka Ka’abah mara saba. Baada ya hapo alisimama nyuma ya Maqaamul-Ibrahim na kusali sala ya Tawaaf yenye rakaa mbili. Baada ya sala ile alianza kufanya Sai baina ya Safa na Marwah.3

Kisha aliwageukia mahujaji na akasema: “Wale wasioleta wanyama wa kutoa kafara wajitoe kwenye hali ya Ihram, na mambo yote yaliyoharimishwa kwao (katika wakati wa Ihram) yatawahalalikia kwa Taqsiir (kupunguza nywele na au kukata kucha). Hata hivyo, mimi na wale wengine tulioleta wanyama wa kutoa kafara tutasalia kwenye hali ya Ihram hadi pale tutakapowachinja wanyama wetu kule Mina.”

Jambo hili lilikuwa na uzito mkubwa kwa baadhi ya watu, na udhuru walioutoa ulikuwa kwamba hawakupenda kwamba Mtume (s.a.w.w.) abakie kwenye hali ya Ihram na wao waitoke hali ile, na yale mambo yaliyoharimishwa kwake yawe halali kwao. Wakati fulani walisema: “Si sahihi kwamba sisi tuwe mahujaji wa Nyumba ya Allah na matone ya maji ya udhu yamiminike kutoka vichwani na shingoni mwetu.”4
Mtume (s.a.w.w.) alibahatika kumwona Umar aliyekuwa bado yu mwenye hali ya Ihram na akamwuliza kama alileta mnyama wa kutoa kafara. Alijibu “la”, hapo Mtume (s.a.w.w.) alisema: “Basi ni kwa nini hutoki kwenye hali ya Ihram?” Alimjibu: “Sipendelei kwamba mimi nitoke kwenye hali ya Ihramu na wewe uendelee kuwa kwenye hali hiyo hiyo.” Mtume (s.a.w.w.) akamwambia: “Utaendelea kuishikilia imani yako hii si hivi sasa tu, bali hadi kwenye siku ya kufa kwako.”

Mtume (s.a.w.w.) aliudhishwa na shaka na kutoamua kwa watu na akasema: “Kama hali ya baadae ingalikuwa dhahiri kwangu kama ilivyo kale, na nikawa nimetambua kusita na mashaka yenu yasiyothibitika, Mimi nami ningalikuja kwenye hija ya Nyumba ya Allah bila ya mnyama wa kutoa kafara kama hivyo mlivyo. Hata hivyo, sina la kufanya hivi sasa, kwa sababu nimekuja na wanyama wa kutoa kafara na kwa mujibu wa Amri ya Allah, “Hadi pale kafara itakapofika kwenye sehemu yake” Sina budi kubakia kwenye hali ya Ihram hadi nitakapowachinja wanyama hao kwenye kiwanja cha kutolea kafara cha Mina. Hata hivyo, kila mtu asiyeleta mnyama wa kutoa kafara hana budi kutoka kwenye Ihram na kulichukulia kila jambo alilolitenda kuwa ni Umrah na baada ya hapo hana budi kuvaa Ihram kwa ajili ya Hajj. 5

Saidina Ali (A.S) Arejea Kutoka Yemen Ili Ashiriki Kwenye Ibada Ya Hijja

Amirul-Mu’minin alitambua kuondoka wa Mtume (s.a.w.w.) kwenda kufanya Hijja. Yeye naye aliondoka na kwenda Makka pamoja na askari wake ili kufanya Hijja na akachukuwa wanyama wa kutoa kafara thelathini na wane. Vilevile alileta vile vipande vya nguo alivyovikusanya kutoka kwa watu wa Najran kutokana na ule ushuru ulioafikiwa kwenye mapatano tuliyoyataja kwenye sura ya hamsini na saba. Alipokuwa njiani alimpa afisa wake mmoja uongozi wa jeshi lake na yeye mwenyewe akaharakisha kwenda Makka. Alionana na Mtume (s.a.w.w.) aliyekuwa na furaha kuu kumwona na akamwuliza: “Ulinuia vipi? “ Sayyidna Ali (a.s.) akamjibu hivi: “Katika wakati uliofaa kwa kuvaa Ihraam nilivaa Ihram kwa nia yako na nikasema: “Ee Allah! mimi nami ninavaa Ihram kwa nia ile ile ambayo Mtume Wako amevalia Ihraam yake. “

Kisha alimfahamisha Mtume (s.a.w.w.) kuhusu wale wanyama wa kutoa kafara aliowaleta. Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Wajibu wetu sote kwenye jambo hili ni moja tu na hatuna budi kubakia kwenye hali ya Ihram hadi pale tutakapowachinja wale wanyama wa Kafara.” Kisha Mtume (s.a.w.w.) alimwamrisha Sayyidna Ali (a.s.) kuwarudia wale askari wake na kuwaleta Makka.

Sayyidna Ali (a.s.) alipolifikia jeshi aliona kwamba vile vipande vya nguo vyote alivyovikusanya kutoka kwa watu wa Najraan kufuatana na mapatano yaliyofanywa kwenye ile siku ya Mubaahila, vimeshagawanywa miongoni mwa wale askari, na walikuwa wamevivaa kwa namna ya Ihraam. Ali alikasirishwa sana na kile kitendo cha yule mwakilishi wake pale yeye alipokuwa hayupo, akamwambia: “Kwa nini umevigawa hivi vipande vya nguo miongoni mwa askari kabla sijavifikisha kwa Mtume (s.a.w.w.)? “Alijibu akisema: “Walishikilia kwamba niwaazime hivi vipande vya nguo, na nivichukue baada ya kufanya ibada ya Hajj.” Sayyidna Ali (a.s.) akamwambia: “Wewe hukupewa mamlaka ya kufanya hivyo.” Kisha alivichukua vile vipande vya nguo kutoka kwa askari wale, akavifungasha na kuvipeleka kwa Mtume (s.a.w.w.) kule mjini Makka.

Watu ambao uadilifu na nidhamu ni vitu vinavyouma, na wapendao kwamba daima matukio yatokee kama wapendavyo wao, walimwendea Mtume (s.a.w.w.) na kumwelezea kuudhishwa kwao na kule kuvichukua vile vipande vya nguo alikofanya Sayyidna Ali (as). Mtume (s.a.w.w.) alimtuma mmoja wa masahaba wake kuwaendea wale walalamikaji na kuwafikishia ujumbe wake usemao: “Jiepusheni na kumsema Ali kwa ubaya. Yeye yu hodari katika kuzisikiliza sheria za Allah na wala yeye si mwenye kujipendekeza.”6

Ibada Za Hijja Zaanza

Kaida za Umrah zikamalizika, Mtume (s.a.w.w.) hakuelekea kukubali kukaa nyumbani mwa mtu yeyote baina ya kipindi cha ibada za Umrah na zile za Hajj. Hivyo basi aliamrisha likitwe hema lake nje ya mji wa Makka.

Siku ya nane ya Dhil Hajj ikafika. Katika siku hiyo hiyo, mahujaji wa Nyumba ya Allah walitoka Makka kwenda Arafat ili kwenda kutekeleza kaida za ‘Arafat tangu adhuhuri ya mwezi tisa Dhil Hajj hadi jua kuchwa katika siku ile.

Mnamo mwezo nane Dhil Hajj, ambayo vilevile huitwa siku ta Tarwiyyah,” Mtume (s.a.w.w.) alikwenda Arafat kupitia Mina na akakaa Mina hadi jua lilipochomoza mnamo mwezi tisa Dhil Hajj. Kisha akampanda ngamia wake na akaondoka kwenda Arafat na akashukia mahali paitwapo Numrah lilipokitwa hema lake. Akauhutubia mkusanyiko mtukufu uliokuwapo pale, aliitoa hotuba yake ya kihistoria akiwa amempanda ngamia wake.

Hotuba Ya Kihistoria Ya Mtume (S.A.W.W) Wakati Wa Hijja Yake Ya Kuaga

Siku ile, Arafat ilishuhudia mkusanyiko mkuu na mtukufu, ambao hadi siku ile mfano wake haukupata kuonwa na watu wa Hijaz. Sauti ya Upweke wa Allah na hamasa ya ibada ya Allah Mmoja tu zilikuwa zikilia nchini. Sehemu ambayo hadi muda mfupi tu uliopita ilikuwa makazi ya washirikina na waabudu masanamu ikawa daima kituo kikuu cha wenye kumwabudu Allah Mmoja. Mtume (s.a.w.w.) akasali sala yake ya Adhuhuri na ya al-Asri hapa Arafat pamoja na watu 100,000, na hapo ushindi wa Uislamu juu ya ukafiri ukapatikana.

Baada ya hapo Mtume (s.a.w.w.) alimpanda ngamia wake na akatoa hotuba yake ya kihistoria iliyorudiwa na mmoja wa masahaba wake aliyekuwa na sauti kubwa, ili kwamba wale waliokuwa mbali nao waweze kukielewa kile alichokuwa akikisema. Katika siku ile alianza hotuba yake kwa kusema: “Enyi watu! Yasikilizeni maneno yangu, kwa vile yawezekana kwamba nisikutane nanyi mahali hapa wakati ujao.

Enyi watu! Damu yenu na mali zenu (heshima na sifa)7 ni vyenye kuheshimiwa miongoni mwenu, kama ilivyo siku hii na mwezi huu, hadi siku ambayo mtakutana na Allah, na kila uasi katika jambo hili ni haramu.”

Ili kuthibitisha kwamba watu wanalipata wazo lihitajikalo kutokana na maneno yake kuhusu kuheshimika kwa uhai na mali za Waislamu, Mtume (s.a.w.w.) alimwomba Rabi’ah bin Umayyah awaulize hivi: “Ni mwezi gani huu?” Wote walijibu wakisema: “Ni mwezi wenye kuheshimiwa na kupigana katika mwezi huu kumekatazwa na ni haramu.” Kisha Mtume (s.a.w.w.) alimwambia Rabiah: “Waambie: Allah Ametangaza kwamba damu yenu na mali zenu ni haramu na ni vyenye kuheshimika juu ya kila mmoja wenu kama ulivyo mwezi huu hadi pale mtakapoutoka ulimwengu huu.”

Akamwambia tena Rabiah: “Waulize ni ardhi gani hii?” Wote wakajibu “Ni ardhi yenye kuheshimika na umwagaji wa damu na uasi ndani yake vimekatazwa kabisa.” Kisha akamwambai Rabiah: “Waambie: Damu yenu na mali zenu ni vitu viheshimikavyo kama ilivyo ardhi hii na kila aina ya uasi ndani yake ni vitu vilivyokatazwa.”

Baada ya hapo Mtume (s.a.w.w.) alimwambia Rabia’ah: “Waulize ni siku gani hii?” Wakajibu wakasema: “Ni siku ya Haj-i Akbar (Hija kubwa).” Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Waambie: Damu yenu na mali zenu ni vyenye kuheshimika kama ilivyo siku hii.”8
“Ndio, enyi watu! Hamna budi kutambua kwamba damu iliyomwagwa katika Siku za Jahilia haina budi kusahauliwa na isilipiziwe kisasi. Hata damu ya Ibn Rabiah (ndugu wa Mtume s.a.w.w) ni lazima isahauliwe.

Hivi karibuni mtarejea kwa Allah, na katika ulimwengu huo amali zenu njema na mbaya zitapimwa. Ninakuwambieni: Mtu yule ambaye kitu fulani kiliwekwa amana kwake, hana budi kukirejesha kwa mwenyewe.

Ndio, enyi watu! Hamna budi kutambua kwamba riba imeharimishwa kabisa kwenye dini ya Uislamu. Wale waliowekeza mitaji yao katika kuchuma riba wanaweza kuichukua mitaji yao tu. Wasiwaonee watu wala wao wasionewe. Ama kuhusu riba ambayo wadeni wa Abbas walipaswa kulipa kabla ya Uislamu, riba hiyo imekwisha kupita, naye hana haki ya kuidai.

Enyi watu! Shetani kaishapoteza matuamini ya kuabudiwa humu nchini mwenu. Hata hivyo, iwapo mtamfuata kwenye mambo madogo madogo atakuwa kwenye furaha na kupendezwa. Hivyo basi, msimfuate shetani.

Kufanya mabadiliko9 kwenye miezi mitakatifu (yaani kwenye ile miezi ambayo kupigana n.k ni haramu) huonyesha kukithiri katika kufuru, na wale makafiri wasioifahamu miezi mitakatifu wamepotoka kutokana na mabadiliko haya, na matokeo yake ni kwamba mwezi mtakatifu huwa halali kwenye mwaka mmoja na huwa ulioharimishwa vita kwenye mwaka mwingine. Wanadhania kwamba kwa kufanya hivyo, wanayabadili mambo yaliyohalalishwa na Allah na kuwa haramu na kinyume cha hivyo.

Ni muhimu kwamba mpango wa miezi iliyo halali na iliyo mitakatifu iwe ni kwa mujibu wa siku ambazo Allah aliziumba mbingu na nchi, mwezi na jua. Mbele ya Allah idadi ya miezi ni kumi na miwili na miongoni mwao Ameamua ya kwamba miezi minne iwe mitakatifu. Miezi hiyo ni Dhil Qa’adah, Dhil Hajj na Muharram, miezi ambayo inafuatana, na kisha ni mwezi wa Rajab.

Ndio, enyi watu! Wanawake wenu wanayo haki juu yenu na ninyi nanyi nnayo haki juu yao. Haki yenu ni kwamba wasimkaribishe mtu yeyote nyumbani bila ya idhini yenu, na wasiwe wakosefu wa jambo lolote lisilo la haki, ambalo kutokana na kushindwa kwao kulitoka na kushindwa kwao kutekeleza, Allah amekupeni mamlaka ya kuvitoka vitanda vyao na vile vile kuwaadhibu. Hata hivyo, kama wakirejea njia ya ukweli, hamna budi kuwatendea upole na huba na kuwapa njia ya maisha ya raha.

Ninakuusieni katika ardhi hii kwamba muwe wapole kwa wanawake wenu, kwa sababu ninyi mnawachukua kwenye dhamana itokayo kwa Allah, nao wamekuwa halali kwenu kwa mujibu wa sheria Zake. Ndio, enyi watu! Yasikilizeni maneno yangu kwa makini na yafikirieni. Ninakuachieni vitu viwili vya kumbukumbu: Kimoja kati yao ni Kitabu cha Allah na kingine ni Kauli yangu na Sunna,10 na kama mkijiambatisha navyo, katu hamtapotea.

Ndio, enyi watu! Yasikilizeni maneno yangu na yafikirini. Kila Mwislamu yu ndugu wa Mwislamu mwingine na Waislamu wote ulimwenguni ni ndugu wao kwa wao. Na chochote kile kinachotokana na mali ya Waislamu si halali kwa Mwislamu ila pale akipatapo kwa dhamiri ya uadilifu.11

Ndio, enyi watu! Wale walioko hapa wawafikishie maelezo haya wale wasiokuwepo. Baada yangu hatakuwepo Mtume, na baada yenu ninyi Waislamu hautakuwepo umma12 mwingine.

Enyi watu! hamna budi kutambua kwamba leo ninatangaza kwamba nimezipiga marufuku ibada na itikadi zote za Zama za Ujahilia na ninakuarifuni juu ya uwongo wao. “13

Alipofika hapa, Mtume (s.a.w.w.) aliisimamisha hotuba yake na akafanya ishara kuelekea mbinguni kwa kidole chake cha shahada, na akasema: “Ee Allah! Nimeufikisha ujumbe Wako.” Kisha baada ya kusema mara tatu: “Ee Allah! Shuhudia.” Alimalizia hotuba yake.

Mtume (s.a.w.w.) alikaa Arafat siku ya mwezi tisa Dhil Hajj hadi lilipozama jua, na kabla ya jua kuzama kabisa kwenye upeo wa macho wa Magharibi na hali ya hewa kuwa na giza kidogo alimpanda ngamia wake na akaitumia sehemu ya usiku ule mahali paitwapo Muzdalifah, na muda wa baina ya alfajiri na kuchomoza kwa jua mahali paitwapo Mash’ar.

Katika siku ya kumi alikwenda Mina na kufanya ibada ya ‘Rami-i’ Jamrah, akatoa kafara kwa kuwachinja wale wanyama na taqsiir (kupunguza nywele na kucha). Kisha alirudi Makka kwenda kuzifanya ibada nyinginezo za Hijja na hivyo akawafunza watu ibada hizo kivitendo.

Katika istilahi ya hadith na historia safari hii ya kihistoria inaitwa ‘Hijjatul Widaa’ (Hija ya mwago), na wakati mwingine vilevile huitwa ‘Hajul Balaagh’ (Hija ya Ufikishaji ujumbe) na Hajul Islam (Hija ya Uislamu). Kila moja ya majina haya lina uhusiano na ibada hii, tena ulio dhahiri kabisa.

Mwishoni tunaweza kutaja kwamba, inafahamika mno miongoni mwa wanahadithi kwamba Mtume (s.a.w.w.) aliitoa hotuba hii kwenye siku ya Arafah, lakini baadhi yao wanaamini kwamba hotuba hii ilitolewa kwenye siku ya kumi ya Dhil Hajj.14

 • 1. Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 289.
 • 2. Maana ya ‘Istilaam’ ni kupangusa mikono kwenye Hajar’ul Aswad kabla ya kufanya Tawaaf; lengo la kitendo hiki ni kwamba, pale Nabii Ibrahim (a.s.) alipokuwa akiijenga Ka’abah, alisimama juu yake. Hivyo basi, Jiwe hili lilipata heshima isiyo na kifani. Kwenye kipindi chake cha miaka kumi ya kuishi kwake mjini Madina Mtume (s.a.w.w.) alifanya ‘Umrah mara mbili, mara ya kwanza kwenye mwaka wa saba na mara ya pili kwenye mwaka wa nane wa hijiriya, ilikuwa ni baada ya kutekwa kwa mji wa Makka. Umrah ya mara hii ilikuwa ni ya tatu ambayo aliifanya pamoja na ibada za Hijja. (Tabaqaatul-Kubra, juz. 2, uk. 174).
 • 3. Safa na Marwah ni majina ya vilima viwili vilivyoko karibu na Masjidul Haraam. Na Sai maana yake ni kutembea baina ya hivyo vilima viwili. Sai huanzia kwenye kilima cha Safa na kumalizikia kwenye kilima cha Marwah.
 • 4. Ni kidokezo cha kujamiiana na kuoga kunakowajibishwa nako, kwa kuwa moja ya mambo yaliyoharimishwa wakati mtu awapo kwenye hali ya Ihraam, ni tendo la ngono na mwanamke na uharamu wake unaishia kwa Taqsiir.
 • 5. Bihaarul-Anwaar, Juz. 21, uk. 319.
 • 6. Bihaarul-Anwaar, Juz. 21, uk. 185.
 • 7. Khisaal cha Shaukh Saduq, Juz. 2, uk. 84.
 • 8. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 605.
 • 9. Wadhamini wa Ka’abah walikuwa wakiibadilisha miezi mitakatifu baada ya kutwaa fedha kutoka kwa watu waliokuwa na shauku ya kupigana vita kwenye miezi hiyo.
 • 10. Kwenye hotuba hii ya kihistoria Mtume (s.a.w.w.) aliwausia watu kuhusu Qur’ani Tukufu na Sunnah; na kwenye ile hotuba aliyoitoa pale Ghadiir na wakati wa kufariki dunia kwake aliwausia Kitabu cha Allah na Dhuria wake. Hakuna upinzani wowote ule baina ya haya maelezo mawili yaliyotolewa kwenye matukio mawili tofauti, kwa sababu, hakuna yeyote awezaye kumkanusha Mtume (s.a.w.w.) kule kuifanya kwake Sunna kuwa sawa na Qur’ani na kuvitaja vyote viwili (Sunna na Qur’ani) kuwa kumbukumbu kwenye tukio moja, na kuusia dhuria na warithi wake kwenye tukio jingine na kusisitiza juu ya kuwafuata, jambo ambalo kwa kweli ndio huko kumfuata Mtume (s.a.w.w.) na Sunna yake. Baadhi ya wanachuoni wa Ahlil Suna kwenye tafsiri zao wamedhania kwamba Mtume (s.a.w.w.) aliyasema maneno haya kwenye tukio moja tu, na wamewataja dhuria wake kwenye tanbihi (maelezo ya chini ya kurasa) kama kauli mbadala, ambapo sisi hatuhitaji masahihisho yoyote ya aina hiyo. Kwa sababu kimsingi, hakuna kutoafikiana kokote baina ya haya maelezo mawili.
 • 11. Siiratu Ibn Hisham, juz. 2, uk. 605.
 • 12. Khisaal’ cha Shaykh Saduq, uk. 84.
 • 13. Bihaaru-Anwaar, Juz. 21, uk. 405.
 • 14. Tabaqaatu Ibn Sa’ad, Juz, 2, uk. 184-186.