Sura Ya 60: Uislamu Wakamilishwa Kwa Uteuzi Wa Mrithi

Kutokana na maoni ya wanachuoni wa Kishia, Ukhalifa ni kazi ya Allah apewayo mtu aliye bora zaidi, afaaye zaidi na aliye na hekima zaidi miongoni mwa watu wa umma (taifa) wote. Mpaka ulio wazi zaidi baina ya Mtume na Imamu (Mrithi wa Mtume) ni kwamba Mtume huweka msingi wa dini, anapata wahyi na anacho Kitabu.

Hata hivyo kuhusu Imamu, ingawa hana chochote kati ya vyeo hivi, vivyo ukiachilia mbali kule kuwa na cheo cha mtawala, yeye yu mtu yule azifafanuaye na kuifikisha sehemu ya dini ya Allah ambayo haingeweza kufafanuliwa hadharani na Mtume (s.a.w.w.) kutokana na kukosa fursa au kutokana na hali ya mambo kuwa isiyofaa, na hivyo basi alimwachia mrithi wake awaambie watu.

Hivyo basi, kutokana na maoni ya Mashia, Khalifa si mtawala wa wakati ule tu, kiongozi wa Uislamu, mwenye mamlaka ya kiutawala, mlinzi wa haki na mwenye kuzihami ngome na mipaka ya nchi, bali vile vile yu mwenye kuyafafanua masuala yenye utata ya dini na kuikamilisha ile sehemu ya amri na sheria ambayo kutokana na sababu fulani fulani haikuweza kuelezwa na yule mwanzilishi wa dini hii.

Hata hivyo, kufuatana na maoni ya Ahlul Sunna, Ukhalifa ni cheo cha kawida na cha kidunia na lengo la kuasisiwa kwake ni kwa ajili ya kuyahami mambo ya kidunia tu na maslahi ya kilimwengu ya Waislamu. Kufuatana na imani yao, Khalifa huchaguliwa kwa kurejea kwenye maoni ya watu kwa ajili ya kuyatawala mambo ya kisiasa, kisheria na kiuchumi.

Ama kuhusu ufafanuzi wa mambo ya kidini ikiwa ni pamoja na ufafanuzi wa sheria uliosimamishwa wakati wa Mtume (s.a.w.w.) lakini haukuenezwa kutokana na sababu mbalimbali, hiyo ni kazi ya wanachuoni wa Uislamu na ni juu yao kuyatatua magumu hayo na masuala yenye utata kwa njia ya Ijtihad.

Kutokana na tofauti hii ya maoni, ya Waislamu kuhusu ukweli wa ukhalifa mabawa mawili tofauti yalijitokeza miongoni mwao na kuwafanya makundi mawili. Tofauti hii inaendelea hadi leo hii.

Kwa mujibu wa maoni ya kwanza, Imamu anashirikiana na Mtume (s.a.w.w.) kwenye baadhi ya sifa, na zile sifa ambazo kuzitimiza kunafikiriwa kuwa ni muhimu kwa Mtume (s.a.w.w.) vile vile huwa muhimu kwa Imamu. Yafuatayo ndiyo yale masharti yapasikayo kutimizwa na Mtume na hata Imamu naye:

Ni lazima Mtume awe mtakatifu. Yaani ni lazima asitende dhambi yoyote ile kwenye kipindi chote cha uhai wake na asitende kosa lolote wakati wa kuzieleza amri na habari za dini au anapoyajibu maswali ya watu. Imamu naye hana budi kuwa vivyo hivyo, na hoja iliyoko kuhusiana na wote wawili ni sawa.

Mtume hana budi kuwa mtu mwenye busara zaidi kuhusiana na mambo ya sheria za kidini na lisiwepo jambo lihusianalo na dini lijifichalo kwake. Na kwa vile Imamu yu mtu aitimizaye au aifafanuaye ile sehemu ya sheria za kidini isiyofafanuliwa kwenye wakati wa Mtume wa Allah, yeye (yaani Imamu) naye hana budi kuwa mwenye kukubalika zaidi kuhusiana na maamrisho, kisheria na kanuni za dini.

Utume ni cheo akipatacho mtu kwa njia ya kuteuliwa na Allah na wala si kwa njia ya uchaguzi wa watu. Mtume hutangazwa na Allah na anateuliwa na kuishika kazi ya utume na Yeye Allah, kwa sababu ni Yeye tu awezaye kuainisha baina ya mtu aliye maasum na asiye maasum, na ni Yeye tu awezaye kuelewa kwamba ni nani aliyeifikia daraja hiyo.

Hata hivyo, kutokana na maoni ya aina ya pili, (yaani yale ya Masunni), si lazima kwamba lolote katika masharti hayo yaliyopo katika Utume liwepo kwa Imamu. Si muhimu kwamba awe mtakatifu, mnyoofu, mwenye elimu au mjuzi wa sheria za dini au ateuliwe au kuwa na uhusiano wowote na ulimwengu wa ghaibu.

Inatosha tu kwamba auhami utukufu na maslahi ya kidunia ya Uislamu kwa kuzitumia busara na hekima zake pamoja na kupata ushauri wa Waislamu na athibitishe upatikanaji wa usalama wa eneo lile kwa kutekeleza sheria ya adhabu na ajitahidi katika kuitanua nchi ya Uislamu kwa mwito wa Jihad.

Utume Na Uimamu Vilihusiana

Ukiziachilia mbali zile hoja za kimantiki na kifalsafa ambazo hatimaye huudhihirisha usahihi wa ule mtazamo wa awali, hadithi na masimulizi tuliyoyapokea kutoka kwa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) pia yanathibitisha maoni ya wanachuoni wa Kishia. Katika kipindi cha Utume wake, Mtume (s.a.w.w.) mara kwa mara alimuainisha mrithi wake na kulitoa suala la Uimamu kutoka kwenye eneo la uchaguzi au utegemezi wa kura za umma.

Sio tu kwamba alimuainisha mrithi wake kwenye Siku za mwishoni za uhai wake, bali hata pale mwanzoni kabisa mwa utume wake, wakati ambapo sio zaidi ya watu wawili ambao wamesilimu, alimtangaza mrithi wake.

Siku moja aliamrishwa na Allah kuwaonya ndugu zake wa karibu zaidi kuhusu adhabu ya Allah na kuwaita kwenye mwito wake hadi kuwafikia watu wote. Kwenye mkutano uliohudhuriwa na wazee arobaini na watano wa familia ya Bani Hashim, alisema: “Mtu wa kwanza atakayenisaidia atakuwa ndugu yangu na mrithi wangu.” Sayyidna Ali (as) aliposimama na kukiri utume wake, Mtume (s.a.w.w.) aliwageukia wale waliokuwapo pale na kusema: “Kijana huyu yu ndugu yangu na mrithi wangu.1Hadith hii ni maarufu miongoni mwa wafasiri wa Qur’ani na wanahadithi kwa jina la ‘Hadith Yaumud-Dar na ‘Hadith Bid’ul Da’wah.’

Si katika kuanza kwa utume wake tu, bali katika matukio mbalimbali mengine pia Mtume (s.a.w.w.) alitangaza utawala na urithi wa Sayyidna Ali (as). Hata hivyo, hakuna hata moja ya matangazo haya lililopata kuwa sawa na ‘Hadith ya Ghadiir’ katika ukuu wake, udhahiri wake na ueneaji wake.

Kaida za Hijja zilimalizika na Waislamu walijifunza moja kwa moja kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) matendo ya kidini yaliyohusu Hijja. Mtume (s.a.w.w.) aliamua kuondoka mjini Makka. Ilitolewa amri ya kuondoka, ule msafara ulipofika kwenye ukanda wa Raabigh2 ulioko umbali wa maili tatu (kilometa tano) kutoka Juhfah,3 Malaika Mkuu Jibriil alishuka mahali paitwapo Ghadiir-Khum na kumfikishia Mtume (s.a.w.w.) Aya ifuatayo: “Ewe Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake. Na Allah Atakulinda na watu. Hakika Allah Hawaongoi watu makafiri.” (Surat al-Maidah, 5:67).

Mahadhi ya aya hii yaonyesha kwamba Allah Alimpa Mtume (s.a.w.w.) kazi iliyokuwa muhimu mno. Na ni kazi ipi iwezayo kuwa muhimu mno kuliko kwamba amteuwe Sayyidna Ali (a.s.) kuwa Khalifa na mrithi wake mbele ya macho ya mamia ya maelfu ya watu.

Hivyo watu wote waliamrishwa kutua. Wale watu waliotangulia walikoma kuendelea mbele na wale walioachwa nyuma walijiunga na wale waliotangulia pale. Huo ulikuwa ni wakati wa adhuhuri na hali ya hewa ilikuwa ya joto sana. Watu walivifunika vichwa vyao kwa sehemu za majoho yao na kuweka ile sehemu nyingine chini ya miguu yao. Kilitengenezwa kivuli kwa ajili ya Mtume (s.a.w.w.) kwa kutumia joho lililotandazwa kwenye mti. Alisali sala ya adhuhuri kwa jamaa. Baada ya hapo, watu walipokuwa wamemzunguka, alisimama kwenye mimbari iliyotengenezwa kwa matandiko ya ngamia na akatoa hotuba ifuatayo kwa sauti kuu:

Hotuba Ya Mtume (S.A.W.W) Pale Ghadiir Khum

“Utukufu wote wamstahiki Allah. Tunauomba msaada wake na tunamwamini na kumtegemea. Tunakimbilia Kwake kutokana na matendo maovu na machafu. Yeye ndiye Mola ambaye hakuna kiongozi ghairi Yake. Hatakuwepo mtu wa kupotosha ya kwamba hakuna mungu ila Allah na Muhammad ni mja wake na Mtume Wake. Ndio, enyi watu! Hivi kari- buni ninaweza kuukubali mwito wa Allah, na ninaweza kutoka miongoni mwenu. Mimi nina jukumu na ninyi pia mnalo jukumu. Mna maoni gani kuhusiana nami?”

Katika hatua hii wale wote waliokuwepo pale walisema kwa sauti kuu: “Tunashuhudia ya kwamba umeitekeleza kazi yako na umefanya juhudi kuhusiana na jambo hili. Allah akujazi kwa hili.” Mtume (s.a.w.w.) akase- ma: “Je, mnashuhudia ya kwamba Mola wa Ulimwengu Yu Mmoja na Muhammad yu mja na Mjumbe Wake na kwamba hakuna shaka juu ya ulimwengu wa Akhera?”

Wote wakajibu wakasema: “Ni sahihi na tunalishuhudia hilo.”
Kisha Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Enyi wafuasi wangu! Ninakuachieni rasilimali mbili (vitu viwili) zenye thamani kama urithi kwenu na itaangaliwa ni jinsi gani mlivyojihusisha na hizi rasilimali zangu mbili”

Kufikia hapa, mtu mmoja alisimama na kusema kwa sauti kuu: “Una maana gani unaposema vitu viwili vilivyo bora sana?” Akilijibu swali hili, Mtume (s.a.w.w.) alisema: “Kimoja kati yao ni Kitabu cha Allah, ambacho upande wake mmoja unahusiana na Allah na upande mwingine umo mikononi mwenu. Na kitu kingine ni dhuria wangu na Ahlu Baiti wangu.

Allah ameniarifu ya kwamba vitu hivi viwili vya kumbukumbu havitatengana. Ndio, enyi watu! Msitake kuitangulia Qur’ani na dhuria wangu, na msizembee katika tabia zenu kuhusiana navyo, ili msije mkaangamia.”

Alipofika hapo aliushika mkono wa Sayyidna Ali (a.s.) na kuuinua hadi weupe wa makwapa yao wote wawili ukaonekana kwa watu. Alimtambulisha Sayyidna Ali (a.s.) kwa watu wote na kisha akasema: “Ni nani aliye na haki zaidi juu ya waumini kuliko wao wenyewe?” Wote wakajibu wakasema: “Allah na Mtume Wake wanajua zaidi.” Kisha Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Allah Yu Mwenye kutawalia mambo yangu na mimi ni mwenye kutawalia mambo ya waumini, nami nina haki zaidi juu yao kuliko wao wenyewe.

Ndio, Enyi watu! Yeyote yule ambaye mimi ni mwenye kutawalia mambo yake, huyu Ali naye yu mwenye kutawalia mambo yake.4 Ee Allah! Wapende wale wampendao Ali na uwe adui kwa wale walio maadui wa Ali. Ee Allah! Wasaidie marafiki wa Ali; wafedheheshe maadui wake na umfanye kuwa kitovu cha ukweli.”

Wakati huo huo Malaika Mkuu Jibriil alishuka na kuileta aya hii: “…Leo mimekukamilishieni Dini yenu, na kukutimiziezi neema Zangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu; …” (Surat al-Ma’idah, 5:3).

Hadi hapo Mtume (s.a.w.w.) aliitamka ‘Takbir’ kwa sauti kuu na kisha akaongeza kusema: “Ninamshukuru Allah kwa kuikamilisha Dini Yake na kuzitimiza fadhila zake na kuuridhia utawala na urithi wa Ali baada yangu.” Kisha Mtume (s.a.w.w.) alishuka pale mimbarini na akamwambia Sayyidna Ali (a.s.): “Kaa hemani ili kwamba machifu na watu wakuu wa Uislamu waweze kukupa mkono wa hongera.”

Wale masheikh wawili, Abu Bakr na Umar walimpongeza Sayyidna Ali mbele ya wengineo wote nao walimwita mtawalia wa mambo yao.

Hassan bin Thabit mshairi maarufu, baada ya kupata idhini ya Mtume (s.a.w.w.) alizisoma beti zifuatazo: “Alimwambia Ali: Simama kwa kuwa nimekuchagua unirithi kuwaongoza watu baada yangu. Yeyote yule ambaye mimi ni mtawalia wa mambo yake, Ali yu mtawalia wa mambo yake naye. Mpendeni kwa ukweli na mfuateni.”

Vyanzo Sahihi Vya Hadith Ghadiir

Miongioni mwa Hadith na masimulizi yote ya Kiislamu hakuna Hadith yoyote nyingine iliyoenezwa na kunukuliwa kama ilivyo Hadith Ghadir. Kutoka miongoni mwa Ulama wa Ahlul Sunna pekee, ulamaa 353 wameinukuu kwenye vitabu vyao na idadi ya wasimuliaji wao wategemewao inafikia masahaba 110. Wanachuoni 26 wa Uislamu wameandika vitabu vinavyotegemewa kuhusu wasimuliaji na njia (asnad) za Hadith hii.
Mwanahistoria maarufu wa Uislamu Abu Ja’afar Tabari amekusanya orodha ya watu wenye maarifa juu ya Hadith hii na njia zake kwenye vitabu viwili vikubwa.

Katika maadiko yote ya historia hadithi hii imekuwa simulizi kubwa ya maarifa kuhusu Imamu Ali (a.s.) kupewa umuhimu wa kwanza juu ya masahaba wote wengine wa Mtume (s.a.w.w.). Na Imamu Ali Amirul- Mu’minin (as), yeye mwenyewe alithibitisha juu ya msingi huu kwenye kamati ya ushauri (shuura) iliyofanyika baada ya kifo cha Khalifa wa pili, na halikadhalika katika kipindi cha Ukhalifa wa Uthuman na wakati wa ukhalifa wake yeye mwenyewe.

Ukimwachilia mbali Amirul-Mu’minin (a.s.) watu wakuu wengine wengi daima wamekuwa wakiitegemea Hadithi hii katika kuwajibu wapinzani na wenye kuikanusha haki ya Sayyidna Ali (a.s.).

Tukio la Ghadir5 lina umuhimu mkuu mno kiasi kwamba, kama ilivyonukuliwa na wafasiri wengi wa Qur’ani Tukufu na wanahadithi, aya za Qur’ani Tukufu zimefunuliwa kuhusina na tukio la siku ile.

  • 1. Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 216 na Tarikh Kamil, Juz. 2, uk. 410.
  • 2. Raabigh ni mahali palipo baina ya Makka na Madina.
  • 3. Ni moja ya Miqaat (Yaani sehemu ya kuvulia Ihraam). Kutoka hapa njia za watu wa Madina, Misri, na Iraq ziligawanyika.
  • 4. Ili kuthibitisha kwamba hakuna kueleweka vibaya kutokeako baada ya hapo, Mtume (s.a.w.w.) aliirudia sentensi hii mara tatu.
  • 5. Kwa maelezo zaidi soma kitabu ‘al-Ghadiir’ cha Allamah Amini, Juz.1.