Sura Ya 61: Walaghai Na Kukamatwa Kwa Urumi

Baada ya taratibu zihusianazo na uteuzi wa mrithi kumalizika pale Ghadiir Khum, watu wote waliokuja kutoka Shamu na Misri kuja kushiriki kwenye ibada ya Hijja waliachana na Mtume (s.a.w.w.) pale Juhfah na kuelekea makwao.

Na watu waliokuja kutoka Hadhramaut na Yemen, nao walijitenga na ule msafara wa Hijja mahali hapa au mahali walipopafikia mapema kabla ya hapa na wakaelekea makwao. Hata hivyo, wale watu elfu kumi waliokuja na Mtume (s.a.w.w.) kutoka Madina walifuatana naye na kurejea Madina na wakafika huko kabla ya kumalizika kwa mwaka wa kumi wa hijiriya.

Mtume (s.a.w.w.) na Waislamu walikuwa na furaha kwamba Uislamu umeenea kila mahali Bara Arabuni, utawala wa washirikina na ibada ya masanamu imekoma nchini kote Hijaz, na vizuizi vyote vilivyokuwemo kwenye njia ya uhubiri wa Uislamu vimeondolewa.

Mwezi wa Muharramu wa mwaka wa kumi na moja hijiriya ulikuwa karibu uandame mjini Madina wakati watu wawili walipowasili kutoka Yamamah kumletea Mtume (s.a.w.w.) barua kutoka kwa Musaylimah ambaye hapo baadae alifahamika kwa jina la Musaylimah Kadh-dhab (yaani Musaylimah muongo).

Mmoja wa makatibu wa Mtume (s.a.w.w.) aliifungua ile barua na kumsomea Mtume (s.a.w.w.). Ile barua ilionyesha kwamba mtu aitwaye Musaylimah alidai kwamba yu Mtume huko Yamamah. Alidai kuwa mshirika wa Mtume (s.a.w.w.) katika utume na kwa njia ya barua ile alitaka kumjulisha Mtume (s.a.w.w.) jambo lile.

Maneno ya ile barua ya Musaylimah yamehifadhiwa kwenye vitabu vya maisha ya Mtume (s.a.w.w.) na vya historia ya Uislamu. Jinsi ya utumiaji wa maneno kwenye barua ile huonyesha kwamba mwandishi alitaka kuiga jinsi ilivyo Qur’ani Tukufu.

Hata hivyo, uigaji huu umeifanya barua yake ile kuwa dhaifu, yenye kufedhehesha na isiyo na faida hata kidogo kiasi kwamba sentensi zake nyingine za kawaida ni bora zaidi kuliko hiyo.

Kwenye barua yake hiyo alimwandikia Mtume (s.a.w.w.) hivi: “Nimefanywa kuwa mshirika wako katika utume. Nusu ya nchi ni yetu na ile nusu nyingine ni ya Waquraishi. Hata hivyo, Waquraishi hawatendi haki.”

Mtume (s.a.w.w.) alipoyatambua yale yaliyomo kwenye barua ile aliwageukia wale walioileta na kuwaambia: “Kama msingelikuwa wawakilisha na wajumbe ningeliamrisha muuwawe. Mkiwa mwishasilimu tayari, na kuushuhudia utume wangu, ni kwa nini mnamfuata mtu huyu mpumbavu na kuiacha dini takatifu ya Uislamu?” Mtume (s.a.w.w.) alimwita katibu wake na kumsomea kwa njia ya imla jibu la barua ile lililo fupi lakini lililo laini lakini zito. Yafuatayo hapa chini ndio maneno ya Mtume (s.a.w.w.): “Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema, Rahimu.

Ni barua itokayo kwa Muhammad Mjumbe wa Allah, kwenda kwa Musaylimah laghai; Amani iwe juu ya wafuasi wa mwongozo. Nchi ni mali ya Allah, Naye huwapa nchi hiyo wale waja Wake walio wachamungu, Awapendao. Na watu wachamungu huupata mwishilizio mwema.”1

Wasifu Mfupi Wa Maisha Ya Musaylimah

Musaylimah alikuwa mmoja wa wale watu waliokuja Madina kwenye mwaka wa kumi wa hijiriya na kusilimu. Hata hivyo, baada ya kurejea kwenye sehemu aliyozaliwa, yeye naye alidai ya kwamba yu mtume na baadhi ya watu wajinga na vilevile baadhi ya watu washupavu wa dini walimwitikia mwito wake. Umaarufu wake huko Yamamah haukuwa udhihirisho wa sifa zake halisi. Baadhi ya watu walimkusanyikia wakijua ya kwamba yu laghai lakini mantiki yao ilikuwa hivi.
“Laghai wa Yamamah ni bora kuliko mtu mkweli wa Hijaz.” Kauli hii ilitamkwa na mmoja wa marafiki wa Musaylimah alipomwuliza: “Je, anakushukia malaika?” Alijibu: “Ndio, Jina lake ni Rahmaan.” Yule mtu aliuliza tena: “Je, malaika huyo yu katika nuru au katika giza?” Musaylimah alijibu akisema: “Yu katika giza”. Yule mtu akasema: “Ninashuhudia ya kwamba wewe u mlaghai. Hata hivyo, laghai wa kabila la Rabi’ah la Yamamah ni bora kuliko mtu mkweli wa kabila la Mazar la Hijaz.” (kwa kusema mtu mkweli wa kabila la Mazar alikuwa na maana ya Mtume wa Uislamu s.a.w.w).

Haiwezekani tena kusemwa kwamba mtu huyu alidai kuwa yu mtume na akajikusanyia watu. Hata hivyo, haikuweza kuthibitishwa kwamba alipanga kuipinga Qur’ani Tukufu. Na sentensi na aya zilizonukuliwa kwenye vitabu vya historia kama mifano yake ya upinzani dhidi ya Qur’ani Tukufu haziwezi kuwa ni mantiki na msemo wa mtu aliye fasaha kama Musaylimah, kwa sababu maneno yake ya kawaida na kauli zake zinabeba uthabiti mkubwa na kujiamini. Kwa mtazamo huu tunaweza kusema kwamba kila kilichohusishwa naye ni kama kauli zilizohusishwa na mtu wa zama zake aliyeitwa Aswad bin Ka’ab ‘Unsi aliyedai kuwa mtume nchini Yemen sambamba na Musaylimah,2na si yamkini kwamba yote hayo yawe ni madoido tu, katika hali zote, yaliyoishia kwenye sababu maalum.

Sababu ya kuyashikilia maoni haya ni kwamba, Qur’ani Tukufu ina ukuu usio kifani na ufasaha kiasi kwamba hakuna awezaye kuthubutu kufikiria kupingana nayo, na kila mwarabu alitambua wazi kwamba kibinadamu haikuwezakana hata kidogo kuiiga.

Baada ya kufariki dunia kwa Mtume (s.a.w.w.) kampeni dhidi ya murtadi ilikuwa kitendo cha kwanza cha Ukhalifa wa Kiislamu. Hivyo basi, ukanda wa ushupavu wa Musaylimah ulizingirwa na majeshi ya Uislamu.

Mzingiro ule ulipokuwa imara na hatimaye kushindwa kwa laghai huyu kulipo dhihirika, baadhi ya marafiki zake wajinga walimwambia: “Je, imetokea nini kwa ule msaada wa ghaibu uliotuahidi?” Musaylimah alijibu akisema: “Hakuna taarifa yoyote juu ya sheria na msaada wa ghaib.

Hiyo niliyokupeni ilikuwa ni ahadi ya uwongo. Hata hivyo, ni wajibu juu yenu kuihami heshima na ukuu wenu.”

Hata hivyo, ulinzi wa heshima na ukuu ulikuwa na msaada mdogo mno! Musaylimah na kikundi cha marafiki zake waliuwawa ndani ya eneo la bustani na ule utume wa uwongo ulifikia mwisho ulioustahili.

Hiyo sentensi iliyotafsiriwa hapo juu yaonyesha kwamba Musaylimah alikuwa mzungumzaji fasaha na vile vile yaonyesha kwamba kamwe yeye hakuwa mzungumzaji wa zile kauli dufu ambazo historia imezihusisha naye, kuwa mfano wa upinzani wake dhidi ya Qur’ani Tukufu.

Kukamatwa Kwa Urumi

Ingawa kutokea kwa walaghai hawa wa utume kwenye sehemu mbalimbali za Uarabuni kulileta hatari kwa umoja wa Kiislamu, Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na wasiwasi zaidi juu ya Warumi waliokuwa wakiishikilia Shamu na Palestina zikiwa ni sehemu ya makoloni yao, kwa sababu alijua ya kwamba Magavana wenye uwezo na ustadi wa Yamamah na Yemen watakuwa na uwezo wa kuwashughulikia wale walaghai wa utume. Hivyo basi, Aswad Unsi, yule laghai wa pili kwenye kipindi cha uhai wa Mtume (s.a.w.w.) aliuawa, ikiwa ni matokeo ya hatua alizozichukua Gavana wa Yemen, siku moja tu kabla ya Mtume (s.a.w.w.) kufariki dunia.

Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na uhakika kwamba watawala wenye nguvu wa Urumi, waliokuwa wakiuangalia vema upanukaji wa daima wa serikali ya Kiislamu wataingiwa na wasiwasi kwa vile Ukristo ulikuwa ukipoteza mvuto wake Uarabuni na Uislamu umewawajibisha baadhi ya Wakristo kulipa kodi kwenye serikali ya Kislamu.

Alikuwa akizingatia kwa makini kila hatari kutoka upande wa Urumi kwa muda mrefu. Ilikuwa ni kwa sababu hii kwamba kwenye mwaka wa nane hijiriya alipeleka jeshi kwenye nchi ya Kirumi chini ya uamiri jeshi wa Ja’far bin Abi Talib, Zayd bin Harith na Abdillah Rawaha, na kwenye mapambano haya hawa makamanda wote watatu waliuawa na jeshi la Uislamu lilirejea Madina, ikiwa ni matokeo ya utawala wa Khalid, bila ya kupata ushindi.

Taarifa za Warumi kuishambulia Hijaz zilipoenea mjini Madina kwenye mwaka wa 9 hijiriya Mtume (s.a.w.w.) alikwenda Tabuk, yeye mwenyewe akiliongoza jeshi madhubuti lenye askari 30,000 na akarejea Madina bila mapigano na bila ya kupambana na adui.

Akiyazingatia yote hayo Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akitambua vizuri hatari iliyokuwepo na kwa sababu hii, baada ya kurejea Madina alitayarisha jeshi walimokuwemo Muhajiriin na Ansar; walimokuwemo watu wakuu kama vile Abu Bakr, Umar, Abi Ubaydah, Sa’ad Waqqas n.k. Kusema kweli alitoa amri kwamba wale Muhajirin wote ambao walihajiri Madina mapema kuliko wenzao lazima washiriki katika vita hivi.3

Ili kuweza kuamsha hisia za kidini za mashujaa wa Kiislamu, Mtume (s.a.w.w.) alifunga bendera na kumpa Usamah kwa mkono wake mwenyewe4 na kumpa maelezo yafuatayo: “Pigana kwa jina la Allah na katika njia Yake. Pigana dhidi ya maadui wa Allah.

Washambulie watu wa Unba5 mapema asubuhi na tembea umbali huu upesi sana kiasi kwamba wewe na askari wako mfike mahali pale kabla ya taarifa za kwenda kwenu huko hazijafika pale.”

Usamah alimpa Buraydah bendera ile na akaiweka Jurf 6 kuwa sehemu yake ya kupigia kambi ili wale askari wa Kiislamu waweze kufika pale kwa makundi na kisha wote waweze kuondoka katika muda uliowekwa.

Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akiyafikiria mambo mawili pale alipomchagua kijana kuwa kiongozi wa jeshi lake na kuwaweka wazee kutoka miongoni mwa Muhajiriin na Ansar chini ya uongozi wake. Kwanza kabisa alitaka kumpa fidia Usamah kwa msiba uliompata kutokana na kumpoteza baba yake katika Vita vya Mutaah na kuliinua daraja lake.

Pili, alitaka kuihuisha sheria ya ugawaji wa kazi na vyeo kwa msingi wa sifa na uwezo wa mtu, na alitaka kudhihirisha kwamba ofisi za Umma na hali ya mazingira havihitaji chochote ila uwezo na ustadi, na mambo haya hayana lolote lihusianalo na umri, ili kwamba vijana wenye uwezo waweze kujitayarisha kuyashika majukumu ya umma yaliyo muhimu, na hawana budi kutambua kwamba katika Uislamu cheo na ofisi vinauhusiano wa moja kwa moja na uwezo na ustadi na wala si miaka na umri.

Uislamu ni nidhamu halisi kwa mujibu wa mafundisho ya Allah; na Mwislamu halisi ni yule ambaye mbele ya maamrisho ya Allah yu kama alivyo askari katika uwanja wa mapambano, na anayakubali maamrisho hayo kwa uaminifu, yawe matokeo yake ni faida kwa mtu yule au ni hasara, na iwe ni kwa mujibu wa mapenzi yake au dhidi yake. Sayyidna Ali Amirul-Mu’minin (as) anaufafanua ukweli wa Uislamu kwa sentensi fupi mno na yenye maana. Anasema: “Uislamu si chochote kingine ila kujitoa barabara ili kuzitekeleza amri zake.”7

Baadhi ya watu hufanya ubaguzi kuhusiana na maamrisho na kanuni za Uislamu, na kila wazionapo kuwa zinapingana na matakwa yao ya binafsi, mara moja hukataa na hutafuta sababu za kujitoa kwenye uwajibikaji wa maamrisho hayo. Watu hawa wanaikosa nidhamu ya Kiislamu, nao hawana shauku halisi ya kujitoa barabara kwa ajili ya sheria hizo.

Ukamanda wa kijana Usamah bin Zayd, ambaye wakati ule umri wake haukuzidi miaka ishirini,8 ni uthibitisho wa dhahiri wa yale tuliyoyasema hapo juu, kwa sababu cheo chake kiliwaudhi baadhi ya masahaba waliokuwa na umri mkubwa kuliko wake.

Walianza kumdhihaki na kukana na kutamka maneno yaliyoonyesha utovu wa nidhamu ya kijeshi na ukosefu wa moyo wa utii wa amri za Amiri jeshi Mkuu wa Uislamu (yaani, Mtume). Sababu yao kubwa waliyotoa ilikuwa kwamba Mtume (s.a.w.w.) amemteua kijana kuwa kamanda wa masahaba wazee.9

Hata hivyo, wao hawakuyatambua yale maslahi makubwa yaliyokuwemo kwenye jambo lile kama tulivyoyaeleza kwenye mistari iliyotangulia, walilikasimia jambo hili kutegemeana na hekima zao chache na maslahi yao ya kibinafsi.

Licha ya ukweli kwamba walijihisi kwamba Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akijitahidi kuliandaa jeshi hili, watu wenye njama za siri walikuwa wakichelewesha kuondoka kwake kutoka pale penye kambi yake pale Jurf, na lilikuwa likipanga mipango miovu.
Siku iliyofuatia baada ya Mtume (s.a.w.w.) kuifunga ile bendera ya vita kwa ajili ya Usamah, alipatwa na homa kali sana na kuumwa na kichwa. Ugonjwa huu uliendelea kwa siku kadhaa na hatimaye kutokea kifo chake cha kimasaibu.

Wakati wa kipindi cha kuumwa kwake, Mtume (s.a.w.w.) alitambua kwamba kuondoka kwa jeshi lile kutoka kwenye ile kambi yake kulikuwa kukizuiwa, na baadhi ya watu walikuwa wakiudhihaki ukamanda wa Usamah.

Jambo hili lilimuudhi mno Mtume (s.a.w.w.), na huku akiwa kaweka taulo begani mwake na kitambaa kilichofungwa kichwani mwake, alikwenda msikitini ili akazungumze na Waislamu kwa karibu zaidi na kuwaonya juu ya kuzivunja amri za Allah.

Alikuwa ana joto kali sana mwilini, alipanda mimbari na baada ya kumtukuza Allah alisema hivi: “Ndio, enyi watu! Ninasikitika sana kutokana na kuchelewa kuondoka kwa jeshi. Inaonyesha kwamba ukamanda wa Usamah umekataliwa na baadhi yenu, nanyi mmeanza kutoa udhuru. Hata hivyo, udhuru na uasi wenu si kitu kigeni, hapo awali mliulaumu ukamanda wa baba yake Usamah, Zayd. Ninaapa kwa jina la Allah kwamba yeye alistahiki kukishika cheo kile na mwanawe naye anastahiki kukishika pia. Yeye ni mpendwa kwangu mimi. Enyi watu! Kuweni wema kwake na vilevile mpendekezeni kwa wenzenu kwamba wawe wema kwake. Yeye yu mmoja wa wale walio wema wenu.”

Mtume (s.a.w.w.) aliimalizia hotuba yake hapa, akashuka kwenye mimbari na akaenda kulala akiwa yu mwenye homa kali na mwili mzito. Kwa kurudiarudia alikuwa akiwaambia wale masahaba wakubwa wakubwa waliokuja kumtazama: “Lifanyeni jeshi la Usamah liondoke.”10 Na wakati mwingine alisema: “Lipatieni silaha jeshi la Usamah” au “Lipelekeni jeshi la Usamah.”

Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na shauku mno juu ya kuondoka kwa jeshi la Usamah kiasi kwamba alipokuwa yu mgonjwa wa kitandani aliwataka masahaba wake walipatie silaha jeshi la Usamah ili liweze kuondoka. Vilevile aliwalaani wale waliotaka kujitenga na jeshi lile na kubakia pale Madina.11

Maagizo haya ya Mtume yaliwafanya wazee wale kutoka miongioni mwa Muhajiriin na Ansar waliokuja kumtazama Mtume (s.a.w.w.) kumuaga na kisha kuondoka Madina kwa shingo upande na kwenda kujiunga na lile jeshi la Usamah kule kwenye kambi ya Jurf.

Katika kile kipindi cha siku mbili au tatu Usamah alipokuwa akijishughulisha kufanya matayarisho ya kuondoka, taarifa juu ya hali mbaya zaidi ya Mtume (s.a.w.w.) ilifika kule kambini kutoka Madina na kuzidhoofisha nyoyo za watu kuhusiana na kuondoka hadi ikafika siku ya Jumatatu, yule kamanda wa jeshi lile alikuja kumuaga Mtume (s.a.w.w.) na akaiona hali ya Mtume (s.a.w.w.) ikiwa na afadhali kidogo.

Mtume (s.a.w.w.) akamtaka aendelee na safari yake upesi iwezekanavyo. Alirejea kule kambini na kutoa amri ya kuondoka kwa jeshi lile. Ilikuwa bado jeshi halijaondoka pale Jurf (penye kambi) ilipofika taarifa kutoka Madina kwamba Mtume (s.a.w.w.) alikuwa mahututi.

Baadhi ya watu waliochelewesha kule kuondoka kwa jeshi kwa kipindi cha siku kumi na sita kwa kutoa udhuru wa aina mbalimbali, waliifanya ile hali mbaya ya Mtume (s.a.w.w.) kuwa sababu na wakarejea Madina na wengine wakafanya vivyo hivyo. Hivyo moja ya shauku kuu ya Mtume (s.a.w.w.) haikuweza kutimizwa kwenye kipindi cha uhai wake kutokana na utovu wa nidhamu wa baadhi ya maafisa wa jeshi lile.12

Udhuru Usiofaa

Haiwezekani kulielezea hasa kosa hili kwa upande wa baadhi wa masahaba wale ambao baadae walizishika hatamu za Ukhalifa wa Mtume (s.a.w.w.)! Baadhi ya wanachuoni wa Ahlus-Sunna wamejitahidi kuelezea na kutetea utovu wao wa nidhamu kwa njia mbalimbali. Ili kudurusu nyudhuru zao zisizo na msingi soma vitabu: ‘Al-Muraji’at 13 na Al-Nass Wal-ijtihad.14

Kuwaombea Msamaha Wale Waliozikwa Baqii

Baadhi ya waandishi wa wasifu wameeleza kwamba: “Siku ambayo joto la mwili wa Mtume (s.a.w.w.) liliongezeka sana, na akawa amelala kitandani, alikwenda kwenye mava ya Baqii wakati wa usiku wa manane akifuatana na mtumwa wake aliyeitwa Abi Muwayhabah15 kwenda kuwaombea msamaha wale waliozikwa pale.

Baadhi ya wanahistoria wanaamini ya kwamba siku ambayo Mtume (s.a.w.w.) aliugua, aliushika mkono wa Sayyidna Ali (a.s.) na kwenda kwenye mava ya Baqii pamoja na kundi la watu waliokuwa wakiwafuata, na akawaambia wale waliokuwa wakifuatana naye: “Nimeamrishwa na Allah kuwaombea msamaha watu wa Baqii.”

Alipoubandika mguu wake kwenye mava yale, aliwasalimu wale waliozikwa pale, na akasema hivi: “Ninakutoleeni salaam, ninyi mliozikwa chini ya ardhi. Hali mliyonayo hivi sasa na iwe ya furaha na nzuri kwenu. Misukosuko imetokea kama sehemu za usiku wa giza na imeungana pamoja.” Kisha aliwaombea msamaha watu wa Baqii.

Baada ya hapo alimgeukia Sayyidna Ali na kusema: “Nimekabidhiwa funguo za hazina ya ulimwengu na maisha yaliyorefushwa ndani yake na nimepewa nichague baina ya hizo na kukutana na Allah na kuingia Peponi, lakini nimependelea kukutana na Mola wangu na kuingia Peponi. (Kama ilivyonukuliwa na wasimuliaji wa Tabaqaat n.k aliugeuzia uso wake kwa Abi Muwayhabah) “Malaika Mkuu Jibriil alikuwa akiniletea Qur’ani mara moja kwa mwaka, lakini mwaka huu ameniletea mara mbili. Hapawezi kuwa na sababu yoyote ile kwa jambo hili ila tu kwamba muda wa kuondoka kwangu umekaribia.”16

Watu wauonao ulimwengu huu kwa macho ya kimaada tu, nao hawalifikirii lengo la uumbaji kuwa ni chochote kile nje ya maada na midhihiriko yake, pengine wanaweza kuwa na shaka juu ya jambo hili na wanaweza kusema nafsini mwao: “Basi ni vipi mtu aweza kuwasiliana na roho na kuzungumza nazo na ni vipi mtu aweza kutambua muda wa kufa kwake?”

Hata hivyo, wale watu walioyakana mambo ya kidunia nao wanaamini kuwako kwa roho iliyo huru kutokana na mwili wa kimaada, katu hawakani kuwasiliana na roho na hulichukulia jambo hili kuwa ni lenye kuwezekana na la ukweli.17

Mtume ambaye ameungana na ulimwengu wa wahyi na dunia zingine zilizo huru kutokana na maada, na aliye huru kutokana na kukosea, bila shaka anaweza kutoa taarifa kuhusiana na matakwa ya Allah kuhusu kifo chake.

 • 1. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 600-601.
 • 2. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 599.
 • 3. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 6452; ‘Al-Nass wal Ijtihad’, cha Sharafuddin Aamili, uk. 12.
 • 4. Kufuatana na vitabu vya kihistoria vya Ahlil Sunna ile bendera ilifungwa mnamo mwezi 26 Safar na kwa mujibu wao, kufariki dunia kwa Mtume (s.a.w.w.) kulitokea mnamo, mwezi 12 Rabi’ul Awwal; hivyo basi matukio yote atakayoyasoma msomaji yaelekea kutokea kwenye kipindi cha siku kumi na sita. Hata hivyo, kwa vile wanachuoni wa Kishia wanawafuata dhuria wa Mtume (s.a.w.w.) huichukulia tarehe ya kufariki dunia kwa Mtume (s.a.w.w.) kuwa ni 28 Safar, hivyo itakuwa muhimu kwamba matukio haya yalitokea siku kadhaa kabla ya 28 Safar.
 • 5. Ni ukanda wa nchi kwenye jimbo la Balqa nchini Shamu nao uko baina ya ‘Asqalaan na Ramlah karibu na Mutaah.
 • 6. Ni sehemu iliyoko maili tatu kutoka Madina kuelekea upande wa Shamu.
 • 7. Nahjul Bahagha, Kalimaatul-Qisaar (Hadith namba, 125).
 • 8. Baadhi ya waandishi wa wasifu wa Mtume (s.a.w.w.) kama vile Halabi wameutaja umri wake kuwa ulikuwa miaka 17 na kwa mujibu wa wengine alikuwa na umri wa miaka 18. Hata hivyo wote wanakubaliana kwamba umri wake wakati ule haukuzidi miaka 20.
 • 9. Tabaqaatu Ibn Sa’ad, juz. 2, uk. 120.
 • 10. Tabaqaatu Ibn Sa’ad Juz. 2, uk. 190.
 • 11. Al-Milal Wan-Nahl’ cha Shahristani utangulizi wa nne, uk. 29; na Sharhu Nahjul Balaghah, cha Ibn Abil Hadid Mutazili, Juz. 2, uk. 20.
 • 12. Tabaqaatu Ibn Sa’ad, juz. 2, uk. 190.
 • 13. Al-Muraji’at, uk. 310-311.
 • 14. An-Nass Wal-ijtihad, uk. 15-19.
 • 15. Baadhi ya wanachuoni wanasema kwamba alifuatana na Abu Raafi’ au na Burayrah, mtumishi wa Aisha (Tabaqaatu Ibn Sa’ad, juz. 2, uk. 204).
 • 16. Tabaqaatu Ibn Sa’ad, Juz. 2, uk. 204; Bihaarul An’waar, Juz. 21, uk. 366.
 • 17. Hata hivyo, kama tulivyoelezea kwenye majadiliano yahusianayo na mawasil- iano na roho, si sahihi kumsikiliza kila mwenye kudai hivyo.