Sura Ya 62: Usia Ambao Haukuandikwa

Enzi za mwisho wa maisha ya Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) alipokuwa yu mgonjwa wa kitandani, ni moja ya nyakati zilizo nyeti zaidi na zenye kutatiza mno katika historia ya Uislamu. Katika siku hizo Waislamu walikuwa wakipita kwenye wakati mgumu sana. Utovu wa adabu wa dhahiri kabisa kwa upande wa baadhi ya masahaba na kukataa kwao kujiunga na jeshi la Usamah ni ushahidi wa mfululizo wa matendo ya chini chini na dhamira ya awali kabisa ya watu waliohusika ya kwamba, baada ya kufariki dunia kwa Mtume (s.a.w.w.) wataichukua serikali na mambo ya kisiasa ya Uislamu na watamsukumizia nyuma yule mtu ambaye hapo awali aliteuliwa kwenye siku ile ya Ghadiir kuwa mrithi wa Mtume (s.a.w.w.).

Kwa kiasi fulani Mtume (s.a.w.w.) naye aliitambua dhamiri yao, na ili kuyabatilisha matendo yao, alisisitiza kwamba wale masahaba watu wazima wote wajiunge na jeshi la Usamah na watoke mle mjini Madina upesi kwa kadiri ilivyowezekana na waende wakapigane na Warumi. Hata hivyo, ili kuitekeleza kivitendo mipango yao, hawa walaghai wa kisiasa walijitolea nyudhuru wenyewe za kutojiunga na jeshi la Usamah kwa visingizio mbalimbali na hata kuthubutu kulizuia lile jeshi lisiondoke, kiasi kwamba Mtume (s.a.w.w.) aliiaga dunia lakini lile jeshi la Uislamu halikuondoka pale Jurf (sehehu kambi ya kijeshi mjini Madina) na lilirejea Madina baada ya kukaa pale kwa kipindi cha siku kumi na sita.

Kule kuzuilika kwao kulitokana na kifo cha Mtume (s.a.w.w.). Hivyo basi, ile hamu ya Mtume (s.a.w.w.) kwamba siku ya kifo chake mji wa Madina utakuwa huru kutokana na waasi wa kisiasa ambao wangeliweza kujitumbukiza kwenye matendo yaliyo dhidi ya yule mrithi wake haikutimizwa. Hawakushindwa kuondoka Madina tu bali vilevile walijitahidi kukipinga kila kitendo ambacho kingeliweza kukithibitisha cheo cha Sayyidna Ali (a.s.) kuwa yu mrithi wa papo kwa papo wa Mtume (s.a.w.w.) na kumzuia Mtume (s.a.w.w.) kulizungumzia jambo hili kwa njia yoyote ile.

Mtume (s.a.w.w.) alipata kuyatambua yale matendo ya kushitusha na shughuli za siri ya baadhi ya mabinti zao, ambao walipata kuwa wakeze. Ingawa Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na homa kali, aliingia msikitini, akasimama kandokando mwa mimbari, akawageuzia watu uso wake akasema kwa sauti kuu iliyoweza kusikika hata kwa nje ya msikiti ule. “Enyi watu! Uasi umelipuka na uasi umejitokeza kama vipande vya usiku wa giza. Hamna kisingizio dhidi yangu. Sikutangaza kitu chochote kuwa ni halali isipokuwa kile ambacho Qur’ani imekitangaza kuwa ni halali na sikutangaza kitu chochote kuwa ni haramu isipokuwa kile ambacho Qur’ani imekitangaza kuwa ni haramu.”1

Kauli hii yaionyesha ile shauku kuu ya Mtume (s.a.w.w.) kuhusiana na hali ya baadae na kuhusu hatima ya Uislamu baada ya kifo chake. Alikuwa na maana gani pale aliposema uasi umelipuka? Je, maana yake yaweza kuwa yoyote nyingine zaidi ya – uasi na mfarakano ulioundwa baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w.) na miali yake bado haijazimika, bali unaendelea bado kuwaka?

Nileteeni Kalamu Na Kidau Cha Wino Ili Niweze Kuwaandikieni Usia

Mtume (s.a.w.w.) aliyatambua matendo yaliyokuwa yakitendeka mbali na nyumba yake ili kunyakua Ukhalifa. Ili kuweza kuzuia kukengeushwa kwa ukhalifa kutoka kwenye mhimili wake halisi na kutokea kwa mifarakano na ugomvi, aliamua kuuthibitisha ukhalifa wa Sayyidna Ali Amirul- Mu’minin, na cheo cha Ahlul-Bayt (a.s.) kwa maandishi ili kwamba maandishi hayo yaweze kuwa ushahidi wa dhahiri juu ya jambo la Ukhalifa.

Siku moja wale masahaba wakuu walipokuja kumtazama Mtume (s.a.w.w.) aliinamisha kichwa chake kidogo na akafikiria kwa kitambo fulani hivi.
Kisha akawaambia: “Nileteeni karatasi na kidau cha wino ili kwamba nikuandikieni jambo fulani kwa ajili yenu, ambalo baada yake hamtapotea.”2

Mambo yalipofikia hapo, khalifa wa pili alikivunja kimya kilichotawala pale na kusema: “Mtume kazidiwa nguvu na ugonjwa. Mnayo Qur’ani. Kitabu Kitukufu cha Allah kinatutosha.”

Maelezo aliyoyatoa khalifa yule yakawa mada ya majadiliano. Baadhi ya watu walimpinga wakisema: “Ni lazima amri ya Mtume itiiwe. Nenda ukamletee kalamu na karatasi ili kwamba chochote kile alichonacho akilini mwake kiweze kuandikwa.” Wengine waliuchukua upande wa yule khalifa na kuzuia kule kumletea Mtume (s.a.w.w.) kalamu na wino. Mtume (s.a.w.w.) aliudhishwa mno na kule kugombana kwao na kule kutoa maneno ya ufidhuli, hivyo akasema: “Amkeni na ondokeni katika nyumba hii (tokeni hapa). “

Baada ya kulisimulia tukio hili, Ibn Abbas anasema: “Msiba mkuu kwa Uislamu ulikuwa ni kule kutoafikiana, na ule ugomvi wa baadhi ya masahaba uliomzuia Mtume kuandika usia aliokusudia kuandika.”3

Tukio hili la kihistoria limenukuliwa na baadhi ya wanahadithi na wanahistoria wa Kisunni na Kishia. Na kutokana na maoni ya wachanganuzi wa hadithi, wanaichukulia hadithi hii kuwa inaangukia kwenye mkumbo wa hadithi zilizo sahihi.

Nukta yenye kuhitaji mazingatio hapa ni kwamba, wanahadithi wa Kisunni wamenukuu maana ya jumla tu ya yale maneno ya Umar, lakini hawakuinukuu ile kauli yake ya kifidhuli. Ni dhahiri kwamba wameepuka kuinukuu kauli ile ya asili, sio kwa sababu kwamba kuinukuu kauli ile ya kiburi ni sawa na kumzoea Mtume (s.a.w.w.) kupita kiasi (cha nidhamu), bali vilevile wao wameyabadili maneno ya khalifa kwa lengo la kukihami cheo chake ili kwamba kizazi kijacho nyuma kisiwe na fikira mbaya juu yake watakapoona maneno yake ya matusi.

Hivyo basi, Abu Bakr Jauhari, mwandishi wa kitabu kitwacho ‘Al-Saqifa’ alipofika kwenye nukta hii ndani ya kitabu chake alisema, wakati akiyanukuu maneno ya Umar: “Umar alisema maneno fulani ambayo maana yake ni kwamba maradhi yamemzidi nguvu Mtume.”4

Hata hivyo, baadhi yao wanapotaka kuyanukuu yale maneno ya yule khalifa, wanaepuka kulitaja jina lake waziwazi kwa lengo la kukihami cheo chake na wanaandika tu hivi: “Na wakasema: Mtume wa Allah kazungumza akiwa kwenye hali ya kupayuka.”5

Ni ukweli ukubalikao kwamba mwenye kuyatamka maneno haya machafu na yenye kuchukiza hawezi kusamehewa, kwa sababu kama ielezwavyo dhahiri kwenye Qur’ani, Mtume (s.a.w.w.) alikuwa safi kutokana na kila aina ya makosa na kila alichokisema kilikuwa ni ufunuo uliofunuliwa kwake.

Kubishana kwa masahaba mbele ya Mtume (s.a.w.w.) aliye mtakatifu kulikuwa kunakokirihisha na kuudhisha kiasi kwamba baadhi ya wakeze Mtume (s.a.w.w.) waliokuwa wamekaa nyuma ya pazia, waliuliza kwa jinsi ya kuchukizwa, ni kwa nini amri yake Mtume (s.a.w.w.) isitiiwe. Ili kuwanyamazisha, khalifa yule alijibu akisema: “Ninyi wanawake mko kama masahaba wa Nabii Yusufu: Mtume anapougua ninyi mnalia na anapopona mnamtawala.”6

Ingawa baadhi ya washupavu wa kidini wamejaribu kuunda udhuru kwa ajili ya khalifa yule kuipinga haja ya Mtume7 lakini wamemlaumu katika msimamo wa mantiki, na wameyachukulia maneno yake (kitabu cha Allah kinatutosha) kuwa yasio na msingi. Wote wamekubali waziwazi kwamba Sunna za Mtume (s.a.w.w.) ndio msingi wa pili wa Uislamu na Kitabu cha Allah hakiwezi hata kidogo kuuondolea umma wa Kislamu haja ya Sunna ya Mtume (s.a.w.w.).

Hata hivyo, inashangaza kwamba Dakta Haykal, mwandishi wa kitabu kiitwacho ‘Hayat-i Muhammad’ ameamua kuwa pamoja na yule khalifa kwa njia ya kidokezo na anaandika hivi: “Baada ya tukio hili Ibn Abbas aliamini kwamba kwa kutokuandikwa kwa kile Mtume (s.a.w.w.) alichotaka kiandikwe, Waislamu wamekipoteza kitu kilicho muhimu sana, lakini Umar aliyashikilia maoni yake, kwa sababu Allah anasema mwenye Qur’ani: “Hatukupuuza Kitabuni kitu chochote”8

Hata hivyo, kama mwandishi huyu angeyachunguza maneno yaliyotangulia na yanayofuatia ya aya hii (yaani, muktadha) asingelieleza kwa namna isiyothibitika kama hiyo na asingesimama na kumuunga mkono yule khalifa dhidi ya maneno ya dhahiri ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), kwa sababu maana ya neno Kitabu kwenye aya iliyotajwa ni uumbaji na kurasa za uhai na jamii ya viumbe mbalimbali katika ulimwengu wa uhai ni kurasa mbalimbali za kitabu cha maumbile. Na hizi kurasa zisizo na idadi hukipa umbo kile kitabu cha maumbile. Haya yafuatayo hapa ndio maneno ya aya ile:

وَمَا مِنْ دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا طَائِرٍ يَطِيرُ بِجَنَاحَيْهِ إِلَّا أُمَمٌ أَمْثَالُكُمْ ۚ مَا فَرَّطْنَا فِي الْكِتَابِ مِنْ شَيْءٍ ۚ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّهِمْ يُحْشَرُونَ {38}

“Na hapana mnyama katika ardhi, wala ndege anayeruka kwa mbawa zake mbili, ila ni umma kama nyinyi. Hatukupuuza Kitabuni kitu chochote. Kisha kwa Mola wao Mlezi watakusanywa.” (Sura al- An’am, 6:38).

Kwa vile maneno yanayoitangulia sentensi inayojadiliwa yanazungumzia wanyama na ndege, na maneno yanayoifuatia yanazungumzia juu ya Siku ya Ufufuo, basi tunaweza kusema waziwazi kwamba kwenye aya hii maana ya neno Kitabu, ambacho ndani yake hakuna kilichoachwa ni kitabu cha maumbile.

Mbali na hili, hata kama tukikubali kwamba maana ya neno Kitabu kwenye Aya hii ya Qur’ani ni Qur’ani yenyewe, hata hivyo, kufuatana na ilivyoelezwa na Qur’ani yenyewe, ni ukweli ukubalikao kwamba yenyewe Qur’ani inaweza kueleweka tu katika mwanga wa hadithi na mwongozo wa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.). Qur’ani inasema:

وَمَا أَرْسَلْنَا مِنْ قَبْلِكَ إِلَّا رِجَالًا نُوحِي إِلَيْهِمْ ۚ فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِنْ كُنْتُمْ لَا تَعْلَمُونَ {43}

بِالْبَيِّنَاتِ وَالزُّبُرِ ۗ وَأَنْزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ {44}

“Nasi hatukuwatuma kabla yako ila watu wanaume tuliowapa Wahyi. Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui. Kwa ishara wazi na vitabu. Nasi tumekuteremshia wewe ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao, wapate kufikiri.”
(Sura al- Nahl, 16:43-44).

Katika aya hii, haikusemwa: “Ili uweze kuwasomea wanadamu.” Maneno yaliyotumika ni: “ili uwabainishie watu.” Kwa hiyo, hata kama Kitabu cha Allah Kitosheleze kwa wanadamu, bado kinayo haja kubwa ya maelezo ya Mtume (s.a.w.w.).

Kama umma wa Kiislamu kwa uhakika wangeweza kuachana na hati ya maandishi kama ile, yaani yale aliyotaka kuyaandika Mtume (s.a.w.w.), ni kwa nini basi Ibn Abbas aliyatamka maneno yafuatayo, wakati machozi yakimtiririka mashavuni mwake: “Msiba ulioje wa siku ya Alhamisi; Mtume aliposema: ‘Nileteeni mfupa wa bega la mnyama na kidau cha wino au karatasi na kidau cha wino ili nikuandikieni jambo fulani na baadae msije mkapotoka.’ Baadhi ya watu wakasema: ‘Mtume ana…..”9

Itawezekanaje kusemwa kwamba pamoja na hisia hizi zilizoelezwa na Ibn Abbas, na ule msisitizo alioufanya Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe, Qur’ani imeuwezesha umma wa Kiislamu kuachana na usia huu? Na kwa vile Mtume (s.a.w.w.) hakufaulu kuutamka usia ule ili uandikwe, je inaweza kukisiwa kwa njia zozote za dalili zilizowazi kile alichokusudia kukiandika kwenye usia wake huo?

Usia Ulilenga Juu Ya Nini?

Moja ya njia zilizo bora zaidi za kuzielezea aya za Qur’ani, ambazo hata hivi sasa bado zinaamrisha mazingatio na upendeleo wa utafiti wa wanachuoni na ulamaa wa wakati huu, ni kwamba ufupi na utata wa aya iliyoshushwa juu ya jambo fulani unaweza kuondolewa kwa njia ya aya nyingine juu ya jambo hilo hilo, ambayo kutegemeana na aina ya maelezo yake inakuwa yenye kueleweka vizuri zaidi kuliko ile ya awali. Kwa mujibu wa tafsiri ya Qur’ani, njia hii inaitwa kuitafsiri aya moja kwa msaada wa aya nyingine.

Njia hii si njia pekee ya kuzifasiri aya za Qur’ani Tukufu tu ambayo hutumika kwenye mafundisho ya Kiislamu, kwani halikadhalika utata wa hadithi moja unaweza kuondolewa kwa msaada wa hadithi nyingine, kwa sababu viongozi wetu wakuu wametilia mkazo na maelekezo ya mara kwa mara juu ya masuala nyeti na yenye kuonekana, ambayo maelezo yao kuhusiana na lengo lao si yenye kutambulika dhahiri na kwa kiwango kilekile. Wakati mwingine lengo lao limeelezwa waziwazi na kwa wakati mwingine limechukuliwa kiushauri tu.

Kama ilivyoelezwa hapo juu, Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa yu mgonjwa kitandani, aliwataka masahaba wake wamletee kalamu na karatasi ili aweze kutamka usia na usia huo uandikwe.

Vilevile aliwaambia ya kwamba usia huo utawathibitishia kutopotea kwao wakati wowote ule. Baadae, kutokana na tofauti baina ya wale waliokuwapo, Mtume (s.a.w.w.) alilitupilia mbali wazo lile la kuuandika ule usia.

Bila shaka mtu anaweza kuuliza: “Ni juu ya jambo gani ambalo Mtume (s.a.w.w.) alitaka kuliandikia usia?” Jibu la swali hili ni dhahiri kabisa, kwa sababu tukiuchukulia ukweli wa kimsingi uliotajwa hapo mwanzoni mwa majadiliano haya, hatuna budi kusema kwamba lengo la Mtume (s.a.w.w.) katika kuuandika usia ule, halikuwa lolote jingine ila kuuthibitisha Ukhalifa na urithi wa Sayyidna Ali Amirul-Mu’minin (as), na kuwawajibisha watu kuwafuata watu wa nyumba yake.

Tunaweza kuamua hivi kwa kuchunguza Hadith Thaqalayn ambayo imekubaliwa kwa pamoja na wanahadithi wa Kisunni na Kishia kwa pamoja, kwa sababu alisema hivyo kuhusiana na usia aliotaka kuuandika: “Ninaiandika hati hii ili kuthibitisha kwamba hampotei baada yangu.”

Na kwenye Hadith Thaqalayn, vilevile alitumia maneno yenye kuanisha na akasisitiza kwamba watu lazima wafuate zile ‘Thiql’ mbili (Vitu viwili vizito au vyenye thamani, yaani Qur’ani Tukufu na dhuria wake) ili kwamba wasipotee baada yake. Yafuatayo hapa ndio maneno ya Hadith Thaqalayn: “Ninakuachieni vitu viwili vizito (vyenye thamani) miongoni mwenu. Kwa kadiri mvifuatavyo vyote viwili hamtapotea. Vitu hivi viwili vyenye thamani ni Kitabu cha Allah (Qur’ani Tukufu) na dhuria wangu Ahlul-Bayt.”

Je, haiwezi kuamuliwa kutokana na maneno ya hizi hadith mbili, na kule kufanana kuliko ndani yao, kwamba lengo la Mtume (s.a.w.w.) katika kule kutaka aletewe kalamu na karatasi lilikuwa ni kuyaandika maneno ya Hadith Thaqalayn katika hali iliyo waziwazi zaidi na kuuthibitisha utawala na ukhalifa wa papo kwa papo wa mrithi wake, ambao ulitangazwa kwa maneno tu mnamo mwezi kumi na nane Dhil Hajj wakati mahujaji wa Iraq, Misri na Hijaz walikuwa wakiagana pale Ghadir Khum?

Aidha, upinzani wenye nguvu wa mtu mmoja, ambaye mara tu baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w.) aliasisi halmashauri ya ushauriano kwenye Saqifah Bani Saidah kwa ajili ya uchaguzi wa khalifa na akamfanya rafiki yake wa tangu kale na kale kuwa mgombea uchaguzi wake kwa namna maalumu na baadae yule rafiki akamteua yeye awe khalifa kwa kubatilisha kanuni zote, labda kwa ajili ya kumlipa fadhila kwa msaada wake, huonyesha kwamba kulikuwa na dalili katika mkusanyiko ule na katika khutba ya Mtume kwamba, alitaka kuandika jambo fulani kuhusu ukhalifa na utawala wa Waislamu. Hivyo yeye alipinga vikali kule kuleta kalamu na karatasi, kwa kuwa kama si hivyo haikuwapo sababu ya yeye kushikilia mno kiasi hicho kwamba isiletwe kalamu na karatasi.

Kwa Nini Mtume (S.A.W.W) Hakushikilia Kuandika Ule Usia?

Kwa nini Mtume (s.a.w.w.) hakutumia nguvu yake katika kuuandika ule usia wakati ambapo licha ya kuwepo upinzani wa baadhi ya watu lakini angeliweza kabisa kumwita katibu wake na kumtolea imla ya kuuandika usia ule?

Vilevile jibu la swali hili liko wazi. Kama Mtume (s.a.w.w.) angelishikilia kuuandika ule usia, wao, wale ambao walikuwa wakisema kwamba maradhi yamemzidi nguvu, wangelishikilia zaidi ukosa adabu wao na mafuasi wao wangeyaeneza maoni haya na wakajitahidi kuyathibitisha maoni yao.

Katika hali hiyo, mbali na ukweli kwamba ukosa adabu kwa Mtume (s.a.w.w.) ungeenea na kuendelea, ule usia nao ungepoteza thamani yake. Hivyo basi, wakati baadhi ya watu walipotaka kujisahihisha kutokana na matendo yao mabaya, walipomuuliza Mtume (s.a.w.w.) kama walete kalamu na karatasi, aliingiwa mno na wasiwasi na akasema: “Baada ya yote hayo mliyoyasema, mnataka kuleta kalamu na karatasi? Mimi ninakuusieni tu kwamba muwe wema kwa dhuria wangu.”

Baada ya kusema hivyo aligeuzia mbali uso wake kutoka kwa wale waliokuwepo pale, nao waliamka na kutawanyika. Pale wakabakia Sayyidna Ali (as), Abbas na Fazdhl tu! 10

Kufanya Masahihisho Ya Jambo Hili

Ingawa ule upinzani wa dhahiri uliofanywa na baadhi ya masahaba ulimfanya Mtume (s.a.w.w.) aache kuandika ule usia, alilitambulisha lengo lake kwa njia nyingine. Historia inashuhudia ya kwamba alipokuwa yu mgonjwa sana aliuweka mkono wake mmoja begani mwa Sayyidna Ali (a.s.) na ule mwingine begani mwa Maiymunah mjakazi wake, na akaenda msikitini. Ingawa alikuwa na maumivu makali na hali isiyokuwa nzuri lakini alijikusuru hadi akaifikia mimbari na akaipanda.

Machozi yalitiririka machoni mwa watu na kimya halisi kikatanda msikitini mle. Watu walikuwa wakisubiri kuyasikia maneno yake ya mwisho na mapendekezo yake.

Mtume (s.a.w.w.) alikivunja kimya cha mkusanyiko ule na akasema: “Ninaacha miongoni mwenu vitu viwili vyenye thamani” Hapo akasimama mtu mmmoja na kuuliza: “Ni nini maana ya vitu viwili vyenye thamani?” Kisha akaongeza kusema: “Kimojawapo ni Qur’ani na kingine ni dhuria wangu.”11
Ibn Hajar Askalaani ametoa tafsiri nyingine ya kufanya masahihisho ya jambo hili na inalingana na ile ya awali. Anasema: “Siku moja, wakati Mtume alipokuwa mgonjwa, na kitanda chake kilikuwa kimezungukwa na masahaba wake, aliugeuzia uso wake kwao na kuwaambia:

“Enyi watu! Muda wa kifo changu umewadia na hivi karibuni nitakuacheni. Tambueni ya kwamba ninakuachieni miongoni mwenu Kitabu cha Allah na dhuria wangu, Ahlul Bayt wangu miongoni mwenu.” Kisha aliushika mkono wa Ali na kuuinua juu, akasema: “Ali yu pamoja na Qur’ani na Qur’ani iko pamoja na Ali na havitatengana hadi Siku ya Kiyama.”12

Mtume (s.a.w.w.) ameisimulia Hadith Thaqalaini kwenye matukio mbalimbali na kwa njia mbalimbali kabla ya kuugua kwake, na amekuwa akiwatahadharisha watu kuhusu vitu hivi viwili vizito, lakini pale alipokuwa yu mgonjwa kitandani alikuwa akiwatahadharisha tena watu juu ya uwiano baina ya Kitabu na dhuria wake na akasisitiza kuhusu umuhimu wao mbele ya watu walewale waliopinga kule kuandika kwake usia. Hii humfanya mtu aamini kwamba lengo la kurudiarudia huku lilikuwa ni kufanya masahihisho kwa kule kutokuwapo kwa maandishi ya usia ule.13

Ugawaji Wa Dinari

Sera ya Mtume (s.a.w.w.) kuhusiana na hazina ya umma (Baytul Mal) ilikuwa kwamba katika fursa ya awali kabisa aligawa mali ya hazina ile miongoni mwa maskini na alijiepusha na kuiweka mali ya hazina ya umma kwa muda mrefu. Hivyo basi, alipokuwa mgonjwa wa kitandani na dinari fulani alikuwa nazo mmoja wa wakeze, alimwamrisha azilete kwake.

Zile dinari zilipoletwa mbele yake alizishika mkononi mwake na akasema: “Vipi Muhammad atategemea kitu chochote kile kutoka kwa Allah kama atakutana Naye huku akiwanazo hizi?” Kisha alimwamrisha Amirul- Mu’minin kuigawa fedha ile miongoni mwa maskini.14

Mtume (S.A.W.W.) Akasirika Kutokana Na Dawa Aliyopewa

Wakati wa kuishi kwake nchini Ethiopia, Asmaa’ binti wa ‘Umays aliyekuwa ndugu wa karibu wa mkewe Mtume (s.a.w.w.) Maymunah alijifunza mchanganyiko wa dawa iliyokuwa majimaji ya mimea fulani. Alifikiria kwamba Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akiugua ugonjwa wa ngozi ya nje ya mapafu (Pleurisy) na huko Ethiopia ugonjwa huu ulikuwa ukitibiwa kwa mchanganyiko huo.

Hali ya Mtume (s.a.w.w.) ilipozidi kuwa mbaya zaidi na akawa na maumivu makali mno alimnywesha dawa ile. Hali ya Mtume ilipoanza kuwa nzuri kwa kiasi fulani, na akapata kulitambua tukio lile alichukia mno na akasema: “Katu Allah hamfanyi Mtume wake kuugua ugonjwa wa aina hii.”15

Buriani Kwa Marafiki

Katika kipindi cha maradhi yake, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na kawaida ya kuja msikitini katika baadhi ya nyakati na kusali na masahaba wake, na pia aliweza kuzungumzia juu ya mambo fulani fulani. Katika moja ya siku hizi aliingia msikitini, akiwa amefunga kitambaa kichwani mwake na Sayyidna Ali (as) na Fadhl bin Abbas wakimshika makwapani mwake, na alikuwa akitembea kwa kuburuza miguu. Alipanda mimbari na akaanza kuzungumza, akisema: “Enyi watu! Umefika wakati wa kukuacheni, kama nimefanya ahadi na mtu yeyote yule niko tayari kuitimiza, na kama nimekopa chocote kile kutoka kwa mtu aseme, ili niweze kumlipa.”

Hadi hapo, mtu mmoja alisimama na kusema: “Katika kipindi fulani kilichopita uliniahidi kwamba kama nikioa, utanisaidia kwa kunipa pesa.” Mtume (s.a.w.w.) alimwamrisha Fadhl kumpa mtu yule kiasi kinachohitajika mara moja. Kisha alishuka kutoka mimbarini na akaenda nyumbani. Baada ya hapo alikuja tena msikitini siku ya Ijumaa (yaani siku tatu kabla ya kifo chake) na akaanza kuzungumza, na akazungumza mambo mengi ikiwa ni pamoja na haya: “Mwenye haki yoyote ile juu yangu naasimame na aitaje, kwa kuwa adhabu kwenye ulimwengu huu ni nyepesi kuliko adhabu kwenye Siku ya Hukumu.”

Hapo Sawadah bin Qays alisimama na kusema: “Wakati wa kurejea kutoka kwenye Vita ya Taa’if, ulipokuwa umempanda ngamia, uliinua fimbo yako ili umpige mnyama wako, lakini kwa bahati mbaya fimbo ile ilinipiga tumboni. Sasa ninataka kulipiza kisasi.”

Fursa iliyotolewa na Mtume (s.a.w.w.) haikuwa ya urasimu wa kinidharia tu, kwa kuwa yeye alidhamiria kweli kuelekea kwenye kuwafidia watu hata kwa ajili ya zile haki ambazo kwa kawaida si zenye kuwekwa maanani na watu.16 Hivyo basi, aliamrisha iletwe fimbo ileile kutoka nyumbani kwake. Baada ya hapo alivua shati lake ili kwamba Sawadah alipize kisasi. Masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) walikuwa wakiitazama mandhari ile kwa nyoyo zilizojawa na huzuni, na machozi yakiwatiririka machoni mwao, nao walikuwa wakisubiri waone jambo lile litaishia wapi, na iwapo kama Sawadah atalipiza kisasi kweli. Hata hivyo kwa ghafla walimwona Sawadah akilibusu tumbo na kifua cha Mtume (s.a.w.w.). Hapo, Mtume (s.a.w.w.) alimwombea du’a Sawadah na akasema: “Ee Allah! Msamehe Sawadah kama vile alivyomsamehe Mtume wa Uislamu!”17

 • 1. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 654; Tabaqaatu Ibn Saad, Juz. 2, uk. 216.
 • 2. Kwa dhahiri alichomaanisha ilikuwa kwamba Mtume (s.a.w.w.) atamke usia na mmoja wa makatibu wake auandike, kwa sababu Mtume (s.a.w.w.) katu haku- pata kushika kalamu mkononi mwake au kuandika jambo lolote lile.
 • 3. Sahih Bukhari, Kitabul’ilmi’, Juz. 1, uk. 22, na Juz. 2, uk. 14; Sahihi Muslim, Juz.14; Musnad Ahmad, Juz.1, uk. 325; na Tabaqaatul Kubra, Juz. 2, uk. 244.
 • 4. Sharhu Nahjul-Balagha, Ibn Abil Hadid, Juz. 2, uk. 20.
 • 5. Sahih Muslim, Juz. 1, uk. 14, na Musnad Ahmad, Juz. 1, uk. 155.
 • 6. Kanzul‘Ammal, Juz. 3, uk. 138 na Tabaqaatul Kubraa, Juz. 2, uk. 244.
 • 7. Marehemu Allamah Mujaahid Sharfuddin amekusanya nyudhuru zote kwenye kitabu chake kitwacho Al-Muraaji’aat na akazikanusha katika njia iliyo bora zaidi.
 • 8. Hayaatu Muhammad, uk. 475.
 • 9. Musnad Ahmad bin Hanbal, Juz. 1, uk. 355.
 • 10. Bihaarul Anwaar, Juz. 22, uk. 469, kama ilivyonukuliwa kutoka Al-Irshaad ya Shaykh Mufid na Aa’lamul Wara’ cha Tabrsi.
 • 11. Biharul Anwaar, Juz. 22, uk. 476; kama ilivyonukuliwa kutoka Majaalis, cha Shaykh Mufid.
 • 12. As-Sawa’iq, Sura ya 9, ya Juz. 2, uk. 57 na Kashful Ghummah, uk. 43
 • 13. Hadith Thaqalayn ni moja ya zile hadith zikubaliwazo na wanahadithi wa Kisunni na Kishia kwa pamoja, na imesimuliwa na masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) katika njia sitini tofauti tofauti. Ibn Hajar Askalaani anaandika hivi: “Mtume (s.a.w) aliutaka uangalifu wa watu juu ya uwiano baina ya Kitabu na dhuria wake kwenye matukio mbalimbali kama vile kwenye Siku ya Arafa, Siku ya Ghadir Khum, alioporejea kutoka Taa’if, na hata pale alipokuwa yu mgonjwa wa kitandani.” (Soma kitabu Al-Sawaaiq al-Muhriqah, uk. 136).
  Marehemu Mir Ahmad Husayn wa India ameweka sehemu ya kitabu chake kwa ajili ya masimulizi ya asili za Hadith Thaqalayn. Kimetolewa hivi karibuni mjini Isfahan (Iran) katika juzuu sita. Katika mwaka 1374 Hijiriya, kitabu kidogo juu ya Hadith hii kilichapishwa na Darut Taqrib Foundation (Misri). Muhimu wake kuhu- siana na asili ya Hadith hii na heshima iliyopata kutoka kwa wanahadithi kwenye zama mbalimbali za historia ya Kiislamu vimenukuliwa kwa ufupi ndani ya kitabu hiki
 • 14. Tabaqaatul-Kubra, Jz. 2, uk. 238
 • 15. Tabaqaatul-Kubra, Jz. 2, uk. 236
 • 16. Manaaqib Ali ibn Abi Talib, Jz. 1, uk. 164
 • 17. Zaidi ya hapo, kwa vile Mtume hakulipiga tumbo la Sawadah kwa kukusudia, Sawadi hakuwa na haki ya kulipiza kisasi, lakini kitendo kile kingeliweza kufidiwa kwa kulipa fedha ya dia (fidia iliyoamrishwa). Ingawa ilikuwa hivyo, Mtume (s.a.w.w.) aliamua kuitekeleza haja yake.