Sura Ya 63: Masaa Ya Mwisho Ya Mtume (S.A.W.W.)

Mji wa Madina ulimezwa na wasiwasi na mashaka. Masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) walikusanyika karibu na nyumbani kwake wakiwa wamejawa na machozi machoni mwao na nyoyo zenye huzuni. Taarifa zilizokuwa zikimiminika nje kutoka nyumbani mle zilionyesha ya kwamba hali yake ilikuwa mbaya zaidi, na yalikuwepo mategemeo madogo mno kuhusu kupona kwake. Hii ilionyesha kwamba ni kitambo kidogo tu cha uhai wake wenye thamani kilichosalia.

Idadi fulani ya masahaba wa Mtume walikuwa na hamu kubwa ya kuonana naye kwa karibu, lakini ile hali yake mbaya haikuruhusu hivyo kwa yeyote yule ila ni watu wa familia yake tu ndio waliweza kuingia chumba alicholala.

Binti yake mwenye kuheshimiwa na kumbukumbu la pekee la Mtume (s.a.w.w.), yaani Bibi Fatimah (a.s.) alikuwa amekaa kandoni mwa kitanda cha baba yake. Alikuwa akiutazma ule uso wake mtakatifu na aliweza kuona kwamba jasho la kifo lilikuwa likimiminika kutoka usoni mwake. Akiwa na moyo mzito, macho yaliyojawa na machozi, na koo lililokabwa, alikuwa akiusoma ubeti ufuatao ambao ulisomwa na Abu Twalib katika kumsifu Mtume (s.a.w.w.):
“Uso wenye nuru ambao kutokana na heshima yake mvua ziliombwa kutoka mawinguni. Mtu aliyekimbilio la mayatima na mlezi wa wajane.”

Wakati huohuo Mtume (s.a.w.w.) aliyafungua macho yake na akamwambia yule binti yake kwa sauti ya chini: “Huu ni utungo aliousoma Abu Twalib kuhusiana nami. hata hivyo, ni bora kama badala ya utungo huo, ungeliisoma aya hii ya Qur’ani Tukufu:

وَمَا مُحَمَّدٌ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِهِ الرُّسُلُ ۚ أَفَإِنْ مَاتَ أَوْ قُتِلَ انْقَلَبْتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ ۚ وَمَنْ يَنْقَلِبْ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ فَلَنْ يَضُرَّ اللَّهَ شَيْئًا ۗ وَسَيَجْزِي اللَّهُ الشَّاكِرِينَ {144}

“Na Muhammad hakuwa ila ni Mtume tu. Wamekwishapita kabla yake mitume. Je, akifa au akauwawa ndiyo mtageuka mrudi nyuma? Na atakayegeuka akarudi nyuma huyo hatamdhuru Allah kitu. Na Allah atawalipa wanaomshukuru.” (Surat Aali Imran, 3:144).1

Mtume (S.A.W.W) Azungumza Na Binti Yake

Uzoefu waonyesha kwamba kutokana na wingi wa shughuli, hisia za watu wakubwa juu ya watoto wao hufifia, kwa sababu kujishughulisha mno na mambo ya kidunia na hatimaye huzififiza hisia zihusuzo watoto wao. Hata hivyo, wakuu wa kiroho hawakumbwi na tatizo hili. Ingawa walikuwa na malengo makuu na fikira za ulimwengu mzima na shughuli zilizokuwa zikiongezeka damia, wao walikuwa na roho kuu zaidi kiasi kwamba mwelekeo wa upande mmoja hauwazuii kuzielekea zile pande nyingine.

Huba ya Mtume (s.a.w.w.) kwa mtoto wake wa pekee ilikuwa moja ya udhihirisho mtukufu wa hisia za ubinadamu, kiasi kwamba katu hakwenda safari yoyote ile bila ya kumwaga binti yake, na aliporejea kutoka safarini kwanza kabisa alikwenda kuonana naye. Alimheshimu mno kuliko wakeze na alikuwa akiwaambia masahaba zake: “Fatimah yu sehemu ya mwili wangu. Furaha yake ni furaha yangu na ghadhabu yake ni ghadhabu yangu.”2

Kila mara Mtume (s.a.w.w.) alipomwona Fatimah alikuwa akimkumbuka Khadija, yule mwanamke aliyekuwa mchamungu zaidi na mwenye huruma zaidi ulimwenguni kote, aliyezikabili shida zisizo kifani na kuutumia utajiri wake mkubwa katika njia ya ujumbe mtakatifu wa mumewe.

Katika kipindi chote cha ugonjwa wa Mtume (s.a.w.w.) Bibi Fatimah (a.s.) alibakia kandoni mwa kitanda cha Mtume (s.a.w.w.) na hakupata kuwa mbali naye japo kwa kitambo tu. Ghafla Mtume (s.a.w.w.) akamwashiria akimtaka azungumze naye. Binti wa Mtume (s.a.w.w.) aliinama na akazungumza naye kwa kumnong’oneza.

Wale watu waliokuwa wamekizunguka kitanda cha Mtume (s.a.w.w.) hawakujua ni kitu gani walichokuwa wakikizungumza. Mtume (s.a.w.w.) alipoacha kuzungumza, Bibi Fatimah alilia sana. Hata hivyo, mara tu baada ya hayo, Mtume (s.a.w.w.) alimwashiria tena na akamnong’oneza tena. Wakati huu alikiinua kichwa chake katika hali ya furaha na midomo yenye kutabasamu. Wale waliokuwapo walishangaa sana kuziona hizi hali mbili zilizotofautiana katika wakati mmoja, na wakamwomba Bibi Fatimah (a.s.) awaeleze kile alichoambiwa na Mtume (s.a.w.w.). Aliwajibu hivi: “Mimi sitaifichua siri ya Mtume wa Allah.”

Baada ya kufariki dunia kwa Mtume (s.a.w.w.) Bibi Fatimah (a.s.) aliwaeleza hali halisi ya yale aliyokuwa akiyazungumza na Mtume (s.a.w.w.), baada ya kusisitizwa na bibi Aisha akasema:

“Mara ya kwanza baba aliniarifu kuhusu kifo chake na akaeleza ya kwamba hakuna tegemeo katika kupona kwake kutokana na maradhi yake.
Hivyo basi, nilianza kulia. Hata hivyo, alipozungumza nami kwa mara ya pili aliniambia nitakuwa mtu wa kwanza kutoka miongoni mwa Ahlul-Bayt wake atakayejiunga naye. Jambo hili lilinifurahisha na nilifahamu kwamba nitakuwa pamoja na baba yangu mpenzi hivi karibuni.”3

Kupiga Mswaki

Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na kawaida ya kupiga mswaki kabla ya kwenda kulala wakati wa usiku na baada ya kuamka asubuhi. Mswaki wa Mtume (s.a.w.w.) ulikuwa ni kipande cha mti wa ‘Araak’ wenye faida sana katika kuziimarisha fizi, kusafisha meno na kuondoa chembechembe za chakula kutoka kwenye meno. Siku moja Abdur Rahman, umbu lake Bibi Aisha, alikuja kumtazama Mtume (s.a.w.w.). Wakati ule alikuwa kashika kipande cha mti mbichi mkononi mwake. Bibi Aisha alielewa kutokana na mtazamo wa Mtume (s.a.w.w.) kwamba alitaka apige mswaki na kile kipande cha mti. Hivyo basi, upesi akakichukua kile kipande cha mti kutoka kwa umbu lake na kumpa Mtume (s.a.w.w.) naye akapiga mswaki kwa kijiti kile.4

Mapendekezo Ya Mtume (S.A.W.W.)

Wakati Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa yu mgonjwa wa kitandani aliweka umuhimu zaidi katika kuwakumbusha watu juu ya mambo yaliyo wajibu, na katika siku zake za mwisho za ugonjwa wake aliwausia watu kwa nguvu zaidi juu ya kusali na kuwatendea wema watumwa. Alisema: “Watendeeni wema watumwa wenu, muwe waangalifu juu ya chakula na mavazi yao, zungumzeni nao kwa upole na zigaweni nao kazi zenu za maisha.”

Siku moja Ka’ab Akhbaar alimwuliza Khalifa wa pili: “Mtume (s.a.w.w.) alisema nini muda mfupi tu kabla ya kifo chake?” Yule Khalifa alimuashiria Amirul-Mu’minin (a.s.) aliyekuwamo kwenye mkutano ule, akasema: “Muulize yeye huyo.” Sayyidna Ali (a.s.) akasema: “Wakati kichwa cha Mtume (s.a.w.w.) kilipokuwa kimeegemea begani mwangu, alisema: “Sala, Sala”. Kisha Ka’ab Akhbaar akasema: “Hii ndio njia ya Mitume waliotangulia pia.”5

Katika dakika za mwisho za uhai wake Mtume (s.a.w.w.) aliyafungua macho yake na akasema: “Mwiteni ndugu yangu, aje na akae karibu nami.” Wale wote waliokuwapo pale walielewa ya kwamba hakuwa na maana ya yeyote yule ila Sayyidna Ali (as). Ali (a.s.) alikaa karibu na kitanda chake lakini alihisi kwamba alitaka kuamka kutoka kitandani mwake. Hivyo alimwamsha Mtume (s.a.w.w.) kutoka pale kitandani pake na akamwegemeza kifuani mwake.6

Mara tu baada ya hapo, dalili za kifo zilianza kujitokeza kwenye mwili wake mtakatifu. Mtu mmoja alimuuliza Ibn Abbas: “Ni mapajani mwa nani alimofia Mtume (s.a.w.w.)?” Ibn Abbas alijibu akisema: “Mtume alitawafu wakati kichwa chake kikiwa mapajani mwa Ali.” Yule mtu aliongeza kusema: “Aisha anadai kwamba alipofariki dunia Mtume (s.a.w.w.) kichwa chake kiliegemea mapajani mwake.”

Ibn Abbas alilipinga dai lake hilo na akasema: “Mtume alifariki dunia mapajani mwa Ali, na Ali na kaka yangu Fadhl walimwosha.” 7 Katika moja ya hotuba zake, Imam Ali (a.s.) amelitaja jambo hili kwa maneno haya: “Mtume alifariki dunia kichwa chake kikiwa kifuani mwangu. Niliosha maiti yake huku malaika wakiwa wananisaidia.”8
Idadi fulani ya wanahadithi wamenukuu kwamba kauli ya mwisho aliyoitamka Mtume (s.a.w.w.) kabla ya kufariki kwake dunia ilikuwa ni: “Kuwa pamoja na Allah.”

Inaonyesha kwamba wakati wa kufariki dunia kwake Malaika Mkuu Jibriil alimpa uhuru wa kuchagua, apone kutokana na maradhi yake na kurejea kwenye ulimwengu huu au Malaika wa mauti aichukue roho yake na auendee ulimwengu wa Akhera na kwenda kuishi huko pamoja na watu waliotajwa kwenye aya hii:

وَمَنْ يُطِعِ اللَّهَ وَالرَّسُولَ فَأُولَٰئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّهُ عَلَيْهِمْ مِنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاءِ وَالصَّالِحِينَ ۚ وَحَسُنَ أُولَٰئِكَ رَفِيقًا {69}

“Na wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume, hao watakuwa pamoja na wale aliowaneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii na Wakweli na Mashahidi na Watu wema. Na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao!” (Surat al-Nisa, 4:69).

Mtume (s.a.w.w.) aliitamka kauli hiyo hapo juu na akafariki dunia.9

Siku Ya Mwisho

Roho takatifu na tukufu ya Mtume wa Allah (s.a.w.w.) ilipaa Peponi katika Siku ya Jumatatu mwezi ishirini na nane Safar (Mfungo Tano).10 Maiti yake ilifunikwa shuka la Yemen na kwa kipindi kifupi hivi iliwekwa pembeni mwa chumba. Kutokana na vilio vya wanawake na vya ndugu wa karibu wa Mtume (s.a.w.w.), watu waliokuwako nje ya kile chumba walijua kwamba Mtume (s.a.w.w.) kaishaitoka dunia. Mara tu baada ya hapo taarifa za kifo chake zilienea mjini mwote.

Kwa sababu zisizoeleweka hadi hivi sasa, Khalifa wa pili alipiga kelele huko nje ya nyumba kwamba Mtume hajafa bali amekwenda mbele ya Allah kama alivyofanya Nabii Musa (a.s.). Alilishikilia jambo hili sana, na ulikuweko uwezekano kwamba angeliweza kuwafanya watu wengine kumuunga mkono katika maoni haya, lakini wakati ule mmoja wa masahaba 11wa Mtume (s.a.w.w.) alimsomea aya ifuatayo:

وَمَا مُحَمَّدٌ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِهِ الرُّسُلُ ۚ أَفَإِنْ مَاتَ أَوْ قُتِلَ انْقَلَبْتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ ۚ وَمَنْ يَنْقَلِبْ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ فَلَنْ يَضُرَّ اللَّهَ شَيْئًا ۗ وَسَيَجْزِي اللَّهُ الشَّاكِرِينَ {144}

“Na Muhammad hakuwa ila ni Mtume tu. Wamekwishapita kabla yake mitume. Je, akifa au akauwawa ndiyo mtageuka mrudi nyuma? Na atakayegeuka akarudi nyuma huyo hatamdhuru Allah kitu. Na Allah Atawalipa wanaomshukuru.” (Surat Aali Imran, 3:144)12

Aliposikia aya hii aliliacha dai lake hilo na akatulia.13

Imamu Ali (a.s.) aliiosha maiti takatifu ya Mtume (s.a.w.w.) na kumkafini kama alivyoelekeza yeye mwenyewe Mtume (s.a.w.w.) kwamba maiti yake ioshwe na mtu aliyekuwa karibu zaidi naye,14 na mtu huyo hawezi kuwa yeyote mwingine ila Sayyidna Ali (a.s.). Kisha aliufunua uso wa Mtume (s.a.w.w.) huku akiwa analia sana, na akasema: “Ewe Mtume wa Allah! Nilikupenda mno kuliko vile nilivyowapenda wazazi wangu. Kifo chako kimeishilizia Utume, Wahyi, na Mitume watokao kwa Mola. Wakati kifo cha Mitume wengine hakikufanya hivyo.
Kifo chako kimeleta huzuni ambayo huzuni yoyote nyingine imesahaulika. Huzuni ya kutengana nawe imekuwa huzuni kubwa na kila mtu ameihisi. Kama usingetuamrisha kuwa na subira, na kutoomboleza na kulia kwa sauti kuu, tungeliendelea kulia na kuomboleza bila ya kukoma, ingawa maombolezo yote haya yasingelikuwa chochote kile yanapolinganishwa na hasara halisi ya kutengwa kwetu na wewe. Lakini kifo ni tukio lisiloepukika, hakuna awezaye kukipa kisogo kifo na hakuna awezaye kukizuia kisije. Tafadhali utukumbuke uwapo mbele ya Allah.”15

Mtu wa kwanza kumsalia Mtume (Sala ya maiti) alikuwa ni Imam Ali (a.s.). Baada ya hapo waliingia masahaba wengine kwa vikundi na kumsalia Mtume (s.a.w.w.) na ibada hizi ziliendela hadi adhuhuri ya Jumanne. Baada ya hapo iliamuliwa ya kwamba maiti takatifu ya Mtume (s.a.w.w.) izikwe kwenye nyumba ileile alimofia. Kaburi lilitayarishwa na Abu Ubaydah bin Jaraah na Zayd bin Sahl na mazishi yalifanywa na Imam Ali (a.s.) akisaidiwa na Abbas na Fadhl.

Tukio hili lilikuwa ni tukio la masaibu makubwa mno. Huyu mtu mashuhuri aliyeibadili hali ya wanadamu kwa juhudi zake na kujitoa mhanga na akazifungua kurasa mpya katika ustaarabu wa binadamu amefariki dunia.16

Bila shaka mtu aliye na fikira zisizo na upendeleo anapochunguza mambo mbalimbali ya sifa za mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kama mwanadamu, mkuu wa familia, mwanajamii, hakimu, mtawala, mwalimu, kamanda wa jeshi na kiongozi, huufikiria uamuzi wa kwamba ukamilifu wake katika kila jambo ni ushuhuda wa dhahiri wa kuwa yeye yu Mtume wa Allah. Historia ya mwanadamu haijawahi kuona mtu yeyote mwingine aliyelifikia daraja la ukamilifu kama huyu.

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amechagua mambo mengi katika ustawi wa mwanadamu kwa ujumla. Kwanza, yeye mwenyewe alifanya kazi ya kuufikisha Ujumbe, aliutekeleza Ujumbe wa Allah na kisha akawaita watu wamfuate.

Alizidumisha haki za watu katika zama ambazo haki za watu zilikuwa zikinyakuliwa; alidumisha uadilifu wakati dhuluma ilikuwa ikienea kila mahali; aliasisi usawa wakati ubaguzi usiofaa ulikuwa jambo la kawaida; na aliwapa watu uhuru walipokuwa wakiugua kwenye uonevu, ukatili na dhuluma.

Aliuleta ujumbe uliomfunza mwanadamu kumtii na kumcha Allah tu, na kuomba msaada kutoka kwake tu. Ujumbe wake ulioletwa kwa ajili ya wanadamu unayahusu mambo yote ya maisha ya mwanadamu ikiwa ni pamoja na haki, uadilifu, usawa na uhuru. Huu ni ujumbe ambao kutokana nao, mwanadamu anakipata tena kile ambacho ni kinyimwa. Basi kwa nini tusiingie tena kwenye ulezi wake, ili mwanadamu aweze kuokolewa kutokana na maangamizi, na kuweza kuipata amani, maendeleo na furaha.

 • 1. Soma Al-Irshaad, cha Shaykh Mufid, uk. 98.
 • 2. Sahih Bukhari, Juz. 5, uk. 21
 • 3. Tabaqaatu Ibn Sa’ad, Juz. 2, uk. 247; Tarikhul Kamil, Juz. 2, uk. 219.
 • 4. Tabaqaatu Ibn Sa’ad, Juz. 2 uk. 23; Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 654.
 • 5. Tabaqaatu Ibn Sa’ad, Juz. 2, uk. 254.
 • 6. Tabaqaatu Ibn Sa’ad, Juz. 2, uk. 263
 • 7. Tabaqaatu Ibn Sa’ad, Juz. 2 uk. 263
 • 8. Nahjul-Balaghah
 • 9. Aa’lamul Waraa’, uk. 83.
 • 10. Wanahadithi na waandishi wa wasifu wa Mtume (s.a.w.w.) wa Kishia wote wanaikubali tarehe hii, na kwenye Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 658, imenukuli- wa katika hali ya masimulizi.
 • 11. Kwa mujibu wa Sahih Bukhari (uk. 7) alikuwa ni Abu Bakr (r.a).
 • 12. Soma Al-Irshaad, cha Shaykh Mufid, uk. 98
 • 13. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 656.
 • 14. Tabaqaatu Ibn Sa’ad, Juz. 1, uk. 57.
 • 15. Nahjul Balagha, Hutuba na. 23
 • 16. Baada ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kufariki matatizo mengi sana yalijitokeza katika kazi yake na utekelezaji wa kazi yake. Lililokuwa chanzo kikuu miongoni mwao lilikuwa ni swala la Ukhalifa na uongozi wa Umma wa Kiislamu. Hata kati- ka siku za kabla ya kifo chake dalili za tofauti na mfarakano ziliweza kuonekana waziwazi miongoni mwa Waislamu. Licha ya ukweli kwamba suala hili lilikuwa moja ya masuala yaliyokuwa nyeti na sura muhimu za historia ya Uislamu, ni nje ya upeo wa mazungumzo yetu ya hivi sasa. Hivyo basi, tunaweza kuyaishilizia masimulizi yetu hapa, na tunamshukuru Allah, kwa baraka Yake. (Kwa maelezo zaidi, tafadhali soma vitabu vitolewavyo na: “Islamic Seminary, P.O. Box 5425, Karachi, Pakistani au vya Al-Itrah Foundation)”