Sura Ya 17: Kuondoka Husein Madina Na Kuchukua Hifadhi Huko Makkah

Husein aliondoka Madina mwezi 28 Rajab, mwaka wa 60 A.H, na akafika Makkah ndani ya juma moja tarehe 3 mwezi wa Shaaban.

Ingekuwa kinyume cha ushuhuda wa ukweli, ambao Husein lazima awe mwenyewe ameuona kufikiria kwamba kama angebakia kukaa Madina wenyeji wa mji huo wangemweka mbali asifikiwe na maadui zake, au wangetoka kuja kumpa msaada. Kwani baada ya kifo cha Mtume watu fulani wenye ushawishi, ambao walikuwa hawana mapenzi kwa Ahlul Bait wa Mtume (watu wa nyumba ya Mtume), walikuwa wamepata madaraka.

Hivyo ilikuwa kwamba wakati Mtume alipokuwa amefariki, binti yake, Fatimah, alihatarishwa kwa ufidhuli mwingi, madhara na kunyang’anywa mali yake mjini Madina. Ilikuwa tena ni hapo hapo Madina ambapo kwa kipindi cha robo karne (miaka 25) ilibidi Ali avumilie na kustahimili uchungu mkubwa sana wa masikitiko yake makali na kuzimwa kwa madai yake ya haki juu ya kumrithi Mtume, na pia kuvumilia kupuuzwa na kud- halilishwa. Hakuna faraja, hakuna msaada na hakuna neno la kutia moyo lililotolewa imma kwa Fatimah au kwa Ali, na mkazi yeyote yule wa Madina katika msiba wao.

Na halafu ilikuwa ni hapo hapo Madina ambapo Bani Umayyah walikuwa wametumia vurugu kuuzuia mwili wa Hasan usichukuliwe kwenda kuzikwa karibu na kaburi la Mtume. Hakuna mkazi wa Madina aliyenyanyua sauti yake katika kupinga dhidi ya udhalimu huu.

Ukweli huu na yaliyokuja kujiri baadaye yalionyesha kwamba kama Husein asingetazamia matatizo mjini Madina, na akaondoka kwenda Makkah, Marwan angemchochea Yazidi kuchukua hatua kali zaidi dhidi yake (Husein), ili kwamba damu ya Husein iweze kumwagwa katika mji wa Madina wenyewe. Barua zilizoandikwa kati ya al-Walid, gavana wa Madina, na Yazid zinaonyesha kwamnba jukwaa lilikuwa limekwisha andaliwa kwa ajili ya mauaji ya Husein. Al-Walid alikuwa ametoa taarifa kwamba: “… Husein haukubali Ukhalifa wako… sasa yote yanategemea juu ya ridhaa yako.” Yazid alijibu, “Nitumie orodha kamili ya watu wote walio maarufu ambao wamekula kiapo cha utii kwangu, na pia ya wale ambao hawakufanya hivyo. Kichwa cha Husein bin Ali ni vizuri kifuatane na jibu lako.” Jibu hili lilimfikia al-Walid baada ya Husein alipokuwa amekwishaondoka Madina.

Kama Husein angeuawa mjini Madina, Bani Umayyah wangeliwasilisha tukio hili kama kadhia ya kawaida. Muhanga wa Husein ungewasilishwa katika hali isiyo na maana yoyote.

Muuaji wa kudharaulika kama Ju’da, bint ya al-Ash’ath au waasi fulani walioritadi kutoka kwenye Uislamu kama Ibnu Muljam, wangeweza kukodiwa kumuua Husein, ili kwamba lawama kwa kosa hilo isingeweza kuwekwa mlangoni mwa serikali ya Syria. Muhanga wa Husein pale Karbala, kama hali ilivyokuwa, ulimweka Yazid kizimbani, kama adui wa Uislamu, na kumfanya Husein kuwa mwokozi wa Uislamu huo.

Husein aliwachukua pamoja naye dhuria wote wa babu yake Abu Talib, na dada zake, Zainab na Umm Kulthumu. Muhammad bin al-Hanafiyya hakuambatana na Husein kwa sababu ya matatizo fulani, na Umm Hani, dada ya baba yake (shangazi yake), aliachwa nyuma kutokana na umri wake mkubwa (mzee). Mbali na kizazi cha Abu Talib, hapakuwepo na dhuria wengine wa Bani Hashim waliokuwa pamoja na Husein hapo Karbala.
Ukweli kwamba Husein alikuwa amewachukua pamoja naye wale ndugu tu, waliokuwa karibu naye mno ulidhihirisha kwamba yeye hakutiwa hamasa na shauku yoyote ya kivita wakati alipoondoka Madina. Kituo chake Makkah, kilikuwa pia kielekezi chenye nguvu sana kwenye upande huohuo, kwani Makkah kwa desturi ni mahali pa amani ambapo haparuhusiwi kutoa uhai wa kiumbe chochote kile cha Mwenyezi Mungu.

Hapo Makkah Husein aliishi Shi’b-Ali katika hali ya ukimya wa amani. Hakuwa na shauku ya kushughulikia na utawala wa masuala ya kila siku yahusianayo na sera za taifa. Hakujiingiza katika kufanya mawasiliano na mtu yeyote yule na hakuwashawishi watu kutoa misaada yao kwake.

Abdallah bin Zubeir ambaye alikuwa amewasili Makkah siku chache mapema zaidi kabla ya Husein alikwishaanza kuwavutia wageni kutokana na kule kujitokeza kwake kwa ghafla hapo (Makkah), na kwa hiyo alikuwa amepata nafasi ya umaarufu, ambayo aliipoteza mara tu kwa Husein wakati alipowasili mjini hapo. Abdallah bin Zubeir alizitambua sifa za daraja la juu sana za Husein na cheo chake kikubwa na akaona inafaa kumtembelea (Husein) kila wakati.

Husein alifanya makazi Makkah kama sehemu ya hifadhi. Kwa sura ya nje, kukaa kwake hapo kulikuwa kama kwa kudumu. Alikuwa hana lengo maalumu mbele yake. Ilikuwa ni ile fursa ya hifadhi tu ambayo Makkah ilikuwa inatoa kwake katika wakati uliomchukua Husein kwenda huko.

Na hili liliafikiana na ushauri uliotolewa kwake na Muhammad ibn Hanafiyya kwamba kama mambo yatageuka na kutoridhisha, basi aende Makkah au maeneo ya jangwani na maeneo mapana yasiyo na rutuba na maeneo makubwa ya milimani na kuhama kutoka mji hadi mji mpaka atakapoweza kuunda mawazo ya wazi juu ya mwelekeo wa watu ili kuweza kufikia uamuzi wa mwisho.