Neno La Mchapishaji

Dua ni ulingano ambapo mja hudhihirisha ufukara, unyonge na udhaifu wake kwa Mola Mkwasi, Mwenye kumiliki kila kitu. Mja huinyosha mikono yake mitupu kwa unyenyekevu na unyonge, na kutaka msaada kutoka kwa Mkamilifu Muumba Mwenye uweza juu ya kila kitu, Mwingi wa huruma na ukarimu, Mwenye busara Mjuzi kwa kila jambo, Mwenye kusikia maombi ya kila anaemuomba. Dua ni lugha ya mapenzi na ni chimbuko la mahaba ya mja kwa Mola wake na ndiyo taa ya waliyo kizani na ni tulizo la wanaohangaika.

Chanzo Cha Dua Hii:

Kumayl Ibn Ziyad Nakha'i alikuwa sahaba muaminifu miongoni mwa sahaba wa Amir al Muminin, Imam Ali Ibn Abi Talib (as) na Dua hii ilisikika kwa mara ya kwanza kutoka kwenye sauti ya kupendeza (ingawa ilikuwa yenye uchungu mkali), ya Imamu Ali (as).

Kwa mujibu wa Allama Majilisi (Allah amrehemu), Kumayl alihudhuria hafla moja msikitini mjini Basra ambayo ilikuwa ikuhutubiwa na Imamu Ali (as), katika khutba ambayo kwayo usiku wa mwezi 15 Shaban ulitajwa:

"Yeyote ambaye atakaa macho kwa mapenzi katika usiku huu na kusoma Dua ya Khidhr, hapana shaka maombi ya mtu yule yatakubaliwa." Wakati watu msikitini pale walipotawanyika, Kumayl alikwenda nyumbani kwa Imamu Ali na akamuomba amzoeshe Dua ya Mtume Khidhr. ImamuAli akamuambia Kumayl; kaa chini, andika na ihifadhi moyoni. Kumayl akaiandika kwa imla ya Imamu Ali (as). Kisha Imamu Ali akamshauri kuisoma Dua hii usiku wa kuamkia Ijumaa, au mwezi mara moja au angalau mwaka mara moja. Imamu Ali akaongeza: "Allah akulinde kutokana na uovu wa maadui na njama zilizopangwa na walaghai. Ewe Kumayl! Kwa kuzingatia uswahiba na ujuzi wako, ninakupa heshima hii ya kuaminisha Dua hii kwako."

Kutokana na umuhimu wa du'a hii tumeona tuitoe kwa lugha ya Kiswahili, ili wasoji wetu wa Kiswahili wapate kunufaika kutokana na Dua hii muhimu.

Tunamshukuru Ndugu yetu Sayyid Ahmad Aqyl kwa kukubali jukumu hili la kukifanyia tarjuma kitabu hiki. Vile vile tunawashukuru wale wote walioshiriki katika kusahihisha na kukipitia hadi kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hiki. Ni matumaini yetu kwamba kitabu hiki kitakuwa ni chenye manufaa kwa wasomaji wetu na kuzidisha upeo wao wa elimu katika dini.

Mchapishaji:
Al’Itrah Foundation
S. L. P. 19701,
Daressalaam.Tanzania.