Funga Ukiuona

Fungeni Mkiuona Na Fungueni Mkiuona (Mtume (s.a.w.).)

Ndugu Mwislamu, yakupasa kujua kwamba kufunga mwezi wa Ramadhani hakutegemei kuwa sikia watu wakizungumza kwamba "Kesho ni Saumu, kesho ni Saumu...." Na hujui sababu ya hao watu na usemi wao huo, bali na wewe mwenyewe wahitajika kujua matukio ya dini yako:

a. Utakapouona mwezi umeandama, ni lazima juu yako kuamkia kufunga na sawa watu wengine wamefunga au hawakufunga, kwako si halali kula hata kidogo na ukila ni juu yako kuilipa siku hiyo na kafara.

b. Habari zikienea mitaani, mijini au barabarani kwamba mwezi umeandama na ukaonekana, na kukawa hakuna uwezekano wa wao kusema uongo, basi ni lazima kuanza Saumu mara moja asubuhi yake.

c. Habari zikitoka mji mwengine ambao si wa mbali sana (kama hapa Kenya na Tanzania na mfano wake) kwa njia ya Radio au simu kwa ushahidi unaoaminika au kutegemewa, Saumu italazimu.

d. Watu wawili unaowaamini watakapokupa habari za kuonekana Hilal (mwezi mwandamo) utalazimika kuwaamini na kuamkia Saumu ingawa wewe mwenyewe hukuona.

e. Pengine kunaweza kuwa na mawingu ambayo yanaweza kuzuia kuonekana kwa mwezi, hapa basi lililo lazima kwako ni kutimiza 30 za Sha’bani na baadaye kuzingatia kuonekana kwa mwezi kutakuwa hakuhitajiki.

Uzindushi

Kauli ya mnajimu (yaani mtu mwenye utaalamu wa kinyota) akitoa hukumu yake ya kinyota kuhusu kuonekana kwa mwezi hazingatiwi.