Usiigeuze Furaha Kuwa Karaha

Mtume (s.a.w.) alisema, "Mwenye kafunga Saumu ana furaha mbili (yaani hufurahi mara mbili). Hufurahi anapofuturu, na pia hufarahi akutanapo na Mola."

Furaha hizi alizozigusia Mtume (s.a.w.) kila mmoja wetu anazielewa na kuzithibitisha, kwani wakati wa kufuturu ima jioni magharibi aidha wakati wa siku ya Idd al Fitri Mwislamu na hata asiye Mwislamu hujawa na furaha tele.

Furaha hizi kwa hakika hukusanya mafungu tofauti, na miongoni mwayo huwa na kundi ambalo furaha hii hulifanya kutenda kinyume cha inavyotakikana.

Wakati wa furaha ya kwanza, yaani wakati wa futari ya kila siku, utashangaa kumwona mtu amejikusanyia mrundiko wa vyakula vya aina mbali mbali ambavyo hata nusu yake haiishi kwa wingi wake. Hii ni Israfu. Na Mungu asema, "Hakika wabadhirifu ni ndugu zake mashetani."

Ama wakati wa kuimaliza Ramadhani, katika pilika pilika za furaha ya sherehe za Iddi, utajionea mwenyewe namna mwanadamu anavyoghilibiwa kwa haraka na kuchezewa shere na Shetani.

Hayo utayashuhudia katika Makadara, sinema na hata katika tamasha za disco na dansi - na Mungu atuepushe.

Ni kweli kwamba, Mtume alisema "Mambo mema huyafuta maovu" Lakini papo hapo maovu nayo huyafuta mema.

Sheikh mmoja alipokuwa akisoma darsi msikitini alisema, "Mwenye kulisema neno hili 'Laahaula Walaa Quwwata Illaa Billahil Adhim' mara moja tu, Mwenyezi Mungu Humpandia mti wa mtende peponi. Na kila msomapo hupandiwa na hivyo basi kuifanya idadi ya mitende apandiwayo kuwa sawa na idadi ya mara alizosoma."

"Si mitende hiyo itaijaza pepo hata kukosekana nafasi?" Aliuliza mmoja waliokuwepo. Sheikh akamjibu "La, haitajaa maana hata mashoka ya kuikata na kuibwaga ni mengi.

Kwa mfano: Mtu aIiyepandiwa mti huo baadaye atasengenya, au atadanganya, au atafanya kosa lolote lile na kila kosa fanyalo huwa mtende mmoja wabwagwa. Jee! mtu huyo atabakisha kitu? Na vivyo hivyo sisi lau tutausahau wajibu wetu wa kumtii na kumnyenyekea Mwumba wetu, bila shaka tutakuwa taabani hapo kesho tutakapotiwa adabu.

Hakuna faida yoyote ile kwa mtu kushinda mchana kutwa au mwezi mzima akiabudu na kufika usiku au siku ya kufuturu akaasi, maana kufanya hivyo kutakuwa sawa na aliyepeleka Benki Shs. 100,000/- na kabla ya kuzifikisha akazitumia zote. Je, mtu huyo ana kitu alichoweka?