Khutbatu Shaabaaniyya

Khutba hii ilitolewa na Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi wa Shaabaan. Imepokewa na Imam Ali (a.s) amesema; "Mtume (s.a.w.) alituhutubia siku hiyo na alisema:

'Enyi watu! kwa hakika umewakaribieni mwezi wa Mwenyezi Mungu, kwa baraka na rehma na maghfira, (huo ni) mwezi ambao mbele ya Mwenyezi Mungu ni bora ya miezi yote, na masiku yake ni bora ya masiku yote, na usiusiku zote, na masaa yake ni bora ya masaa yote. Huo ni mwezi ambao mmekaribishwa ndani yake kuwa wageni wa Mwenyezi Mungu, na mmefanywa kuwa ni watu wenye karama ya Mwenyezi Mungu.

“Pumzi zenu katika mwezi huo ni tasbihi, na usingizi wenu katika mwezi huo ni ibada, na amali zenu katika mwezi huo ni zenye kukubaliwa, na du'a zenu ni zenye kujibiwa, basi muombeni Mwenyezi Mungu, Mola wenu kwa niyya zenye ukweli, na mioyo misafi ili awawezeshe kuufunga mwezi huo na kukisoma kitabu chake, kwani yule aliyepata hasara ni yule aliyekosa maghfira ya Mwenyezi Mungu katika mwezi huu mtukufu. Na kumbukeni kwa njaa yenu na kiu yenu katika mwezi huo, njaa na kiu ya siku ya kiyama.

“Wapeni sadaka mafakiri wenu na masikini wenu, na waheshimuni wakubwa wenu, na wahurumieni wadogo wenu, na dumisheni undugu wenu, na chungeni ndimi zenu, na kifungieni macho kile ambacho hakifai kutizamwa na macho yenu, na kile ambacho hakifai kusikizwa na masikio yenu, wafanyieni upole mayatima wa watu wengine ili nao wawafanyie upole mayatima wenu. Na tubieni kwa Mwenyezi Mungu madhambi yenu, na mnyanyulieni mikono yenu mnapo omba du'a katika nyakati za sala zenu, kwani hizo ni nyakati bora zaidi, Mwenyezi Mungu huwatizama waja wake katika nyakati hizo kwa upole, huwajibu pindi wanapomuomba, huwapa wanapomuuliza.

“Enyi watu, hakika nafsi zenu zimewekwa rehani kwa amali zenu, basi zifungueni kwa kuomba kwenu msamaha, migongo yenu ni mizito kwa mizigo yenu ya madhambi, ipunguzieni uzito huo kwa kurefusha sajda zenu, na jueni ya kwamba Mwenyezi Mungu ameapa kwa utukufu wake kuwa hatawaadhibu wenye kusali na kusujudu, na kwamba hatawaadhibu kwa moto siku watakapo simama watu kwa Mola wa walimwengu.

“Enyi watu, mwenye kumfuturisha mtu mu'umin aliyefunga miongoni mwenu katika mwezi huu, jambo hilo mbele ya Mwenyezi Mungu ni sawa na kumuachilia mtumwa huru, na husamehewa madhambi yake yaliyopita.
Ikasemwa:-
'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, sio wote kati yetu wanaoweza jambo hilo.'

Mtume (s.a.w.w.) akasema:-
'Ogopeni moto japo (mfuturishe) kwa tende moja, ogopeni moto japo kwa kunywesha maji'.

“Enyi watu! mwenye kuifanya tabia yake iwe nzuri miongoni mwenu katika mwezi huu, malipo yake ni kuweza kupita katika Swiraat kwa usalama siku ambayo miguu ya watu wengine itakapokuwa ikiteleza. Na mwenye kumpunguzia katika mwezi huu kazi, mjakazi ambaye amemumiliki kwa mkono wake wa kulia, Mwenyezi Mungu atampunguzia hesabu (madhambi) zake.

“Na atakayezuia shari yake katika mwezi huu, Mwenyezi Mungu atazuia ghadhabu zake siku atakayo kutana naye. Na atakayemkirimu yatima katika mwezi huu, Mwenyezi Mungu atamkirimu mtu huyo siku ya Kiyama. Na atakaye dumisha undugu katika mwezi huu, Mwenyezi Mungu atamdumishia rehma zake siku atakayokutana naye. Na atakayevunja undugu ndani yake, Mwenyezi Mungu atamvunjia rehma zake siku atakayokutana naye.

“Na atakaye sali sunna ndani yake, Mwenyezi Mungu atamwandikia awe mbali na moto. Na atakayetimiza faradhi moja ndani yake, atakuwa na thawabu amabazo atakuwa sawa na atakayetimiza faradhi sabini zenye kuwa sawa katika miezi mingine. Na mwenye kukithirisha kuniswalia mimi ndani ya mwezi huu, Mwenyezi Mungu atamfanyia uwepesi mizani yake siku itakayokuwa ni mzito mizani nyengine (kwa madhambi). Na atakayesoma ndani yake aya moja ya Qur'ani malipo yake yatakuwa ni sawa na yule aliyehitimisha Qur'ani katika miezi mingine isiyokuwa Ramadhani.

Enyi watu! hakika milango ya pepo katika mwezi huu iko wazi, basi muombeni Mola wenu asiifunge kwenu nyinyi. Na milango ya moto imefungwa, muombeni Mwenyezi Mungu asiifungue kwenu. Na Mashetani wamefungwa, basi muombeni Mola wenu wasije wakawatawala juu yenu..."

Imam Ali Ibn Abi Talib (a.s) alimuuliza Mtume (s.a.w.):

"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni tendo gani lililo bora kabisa katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani?"

Mtume Mtukufu (s.a.w.w) alijibu:
"Ewe Abu'l Hasan, bora ya matendo yote katika mwezi huu Mtukufu ni kujiweka mbali kabisa na yale yaliyoharamishwa na Allah s.w.t.

“Enyi mlioamini! Mmelazimishwa kufunga (saumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu, Siku chache tu (kufunga huko). Na atakaye kuwa mgonjwa katika nyinyi au katika safari (akafungua baadhi ya siku), basi (atimize) hisabu katika siku nyingine.
Na wale wasioweza, watoe fidia kumlisha masikini. Na atakayefanya wema kwa radhi ya nafsi yake, basi ni bora kwake. Na (huku) kufunga ni bora kwenu. Ikiwa mnajua (haya sasa basi fuateni). Al Baqarah 2: 183 - 184