Utangulizi

Baada ya miaka kumi na tatu ya mfululizo wa mateso na mapambano, Mtume wa Uislamu aliondoka Makkah na kwenda Madina. Alihisi kwamba kipindi cha uvunjaji sheria na kutangazwa kwa siri kwa Uislamu kilikwisha na kwa msaada wa masahaba wake waaminifu na jasiri angeweza kujenga jumba kubwa la dola ya Kiislamu na kuweka msingi wa serikali ya kisiyasa kama anavyotaka Mwenyezi Mungu.

Mara tu baada ya kufika Madina, Mtukufu Mtume alijenga msikiti hapo. Alijenga nyumba yake iliyotazamana na msikiti, na alifanya mlango wake wa kuingia moja kwa moja msikitini. Hapakuwepo na mabadiliko ya maisha yake tangu mwanzo hadi mwisho. Tabia, mwenendo na maadili mema yalikuwa hivyo hata baada ya kuanzisha serikali ya Kiislamu katika Arabia yote.

Mfumo wa utawala mpya na dola mpya vilitokeza na kuanza kuwepo katikati ya dola mbili za wakati huo. Kwenye Serikali hii ya Kiislamu hapakuwepo na mtawala na mtawaliwa, hapakuwepo afisa na wa chini yake, na hapakuwepo na bwana na mtumwa. Wote walikuwa sawa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Mwasisi wa mfumo huu mpaya wa utawala alitawafu na baada ya kunyang’anywa Ali urithi na kuundwa kwa vikundi vya kisiasa, mkengeuko wa kwanza ambao ulitikisa msingi wa Kiislamu ulitokeza kwenye jambo la Ukhalifa.

Mmojawapo wa masahaba waaminifu sana na jasiri sana wa Mtukufu Mtume alikuwa Abu Dharr. Alikuwa mtu wa tano kuingia kwenye Uislamu na upanga wake ulikuwa unafaa sana katika kuendeleza Uislamu. Aliona mikengeuko yote hii. Ali ambaye alikuwa mfano halisi wa wema na ukweli, alilazimika kuishi maisha ya upweke.

Maadui wa Uislamu waliopo na kwenye mfumo wa Ukhalifa na walikuwa wanauharibu Uislamu kwama mchwa. Abu Dharr alisumbuliwa sana na kushtuka na aliona kwamba hali ya Uislamu ya siku za usoni ilikuwa ya wasi wasi na kuogopesha. Hata hivyo pia aliona kwamba kwa hali yoyote ile msafara wa Uislamu ulikuwa unaendelea kwenye njia yake, ingawa haki haikutendeka. Kwa hivyo, ingawa alihuzunika na kufadhaika, alinyamaza kimya!
Mfumo wa utawala wa Uthman ulipopata uwezo kamili, haki za wafanya kazi na Waislamu wasio jiweza zilikiuka. Wala riba, wanao shughulika na watumwa, matajiri na makabaila, ambao walifika kwenye baraza la Uthman na Muawiyah.

Tofauti za matabaka na kuhodhi utajiri ni tabia zilizoanzishwa tena, na Uislamu uliotishiwa na hatari kubwa. Njia na tabia za Mtukufu Mtume ziliachwa. Maelfu ya dinari zilitumika kujenga Ikulu ya Muawiyah iliyoitwa (Green Palace) ya mtawala wa Kiislamu na utaratibu wa mabaraza ya Kifalme ulianzishwa. Umari aliendesha maisha yake kama mtu wa kawaida na Abu Bakr naye aliishi hivyo hivyo, ili kuendesha maisha yake, alikuwa anafanya kazi ya kukamua mbuzi wa Myahudi ambapo kidani cha mke wa Uthman, Khalifa wa tatu kiligharimu thuluthi moja (1/3) ya pato pote lililoletwa kutoka Afrika.

Akichukua nafuu isiyostahili ya kazi anayofanya baba yake, mtoto wa kiume wa mmojawapo wa maofisa wa ngazi ya juu sana katika utawala wa Umari alichukua farasi wa mtu kwa lazima. Kwa upande mwingine Uthman alimteua Marwan bin Hakam kama mshauri wake mtu ambaye alipewa adhabu ya uhamisho na Mtukufu Mtume na akampa zawadi ya kiunga cha Kheybar pamoja na malipo kutoka Afrika!

Abu Dharr alipochunguza shughuli hizi za kuaibisha hakuweza kuvumilia yote haya, aliamua kufanya upinzani dhidi ya mfumo huo wa kidikteta. Yalikuwa maasi ya kijasiri na ukakamavu ambayo yalisababisha Waislamu kufanya uasi dhidi ya Uthman; mawimbi yake yanayo rindima bado yanaweza kuonekana kwenye jamii nyingi za binadamu.

Abu Dharr alikuwa na shauku ya kuanzisha mfumo wa maadili ya Kiislamu, ambapo utawala wa Uthman ulikuwa unakiuka kwa kuhuisha utawala wa kitabaka. Abu Dharr aliona Uislamu kuwa ndio kimbilio la wasiojiweza, na mafakiri waliokuwa wanakandamizwa, na Uthman aliufanya utawala wake kuwa njia ya kuwafadhili jamii ya watu wakuu na wala riba. Ugomvi huu baina ya Abu Dharr na Uthman uliendelea, hatimayeAbu Dharr alipoteza maisha yake kwa sababu hii.

Abu Dharr alimtambua Mwenyezi Mungu Mweza wa yote; kwa hiyo kamwe hakutetereka katika njia Yake hata kwa nukta moja. Aligeuka kuwa mtu bora katika kundi la Uislamu na ndio jambo ambalo linatosha kuonyesha umashuhuri wake.

Abu Dharr ni mmojawapo wa wale viongozi na wakombozi wa uhuru mwanadamu anautaka leo hii. Hususan kwa vile utaratibu wa muda umefanyiza hali ya wasiwasi mkubwa katika ulimwengu wa uchumi na matatizo ya kiuchumi yanashughulikiwa kuwa ndio matatizo ya msingi zaidi ya maisha. Hali hiyo hiyo ya Syria na Madina kwa kuwakusanya wasiojiweza na kuwashawishi waasi dhidi ya wala riba na wanaohodhi utajiri, pia leo hii imejitokeza.

Waislamu hapa duniani wanakumbuka maneno yake ya kuvutia, maoni sahihi na hotuba kali. Inawezekana kwamba wanaweza kuona kwenye sehemu za mbali sana historia kwamba amewakusanya wanaokandamizwa na wasiojiweza kwenye msikiti na ana chokonowa hisia zao dhidi ya wale waishio kwenye ikulu na utaratibu mchafu wa Uthman na kutangaza hadharani:

وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنْفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَبَشِّرْهُمْ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ{34}

“Watu hao wanao hodhi dhahabu na fedha na hawatumii katika njia ya Mwenyezi Mungu, wanapaswa kujua kwamba adhabu yao itakuwa mateso makali.” (Quran 9:34).

“Ewe Muawiyah! Endapo unajenga Ikulu hii kwa fedha yako mwenyewe ni ubadhilifu, na kama unajenga kwa kutumia hazina ya taifa, huko ni kuitwalia.”

“Ewe Uthman! Masikini wamekuwa masikini zaidi na matajiri wamekuwa matajiri zaidi. Yote haya yanasababishwa na wewe.”

Wachapishaji