read

19. Miongoni Mwa Semi Zake (A.S)

Alimwambia Al-Ash’ath bin Qays, naye (a.s) akiwa juu ya mimbari ya al-Kufa akitoa hutba, kulipita jambo katika baadhi ya usemi wake ambalo Al-Ash’ath alilipinga. Akasema al-Ash’ath: “Yaa Amiral-Mu’minin, hili liko dhidi yako haliko kwa upande wako.”1 Aliinamisha macho yake (a.s) na kutikisa kichwa na kumwangalia, kisha akasema:

“Ni jambo gani linalokujulisha lililo dhidi yangu na ambalo ni langu! Laana ya Mungu iwe juu yako, na laana ya wenye kulaani, umfumaji, mtoto wa mfumaji,2 wewe ni mnafiki mtoto wa kafiri. Wallahi ukafiri ulikuteka mara moja na uislamu mara nyingine.3 Hukufidiwa kutoka mojawapo, si kwa mali yako wala kwa ukoo wako.

Mtu huyu aliwafanyia hila watu wake wakapigwa kwa upanga na aliwasukumia kifo na maangamizi, anastahili kuchukiwa na watu wa karibu na haaminiwi na watu wa mbali.

Maelezo: ar-Radhiyu (r.a.) amesema: “Amirul-Mu’minin (a.s) anakusudia kwamba huyu Ash’ath alitekwa akiwa mfungwa wa vita katika vita zama za ukafiri mara moja na katika Uislamu mara moja. Ama usemi wake (a.s.): (Dalla alaa Qaumihi saifa) alikusudia tukio lilikuwa kati ya Ash’ath na Khalid bin Al’Waliid huko Yamamah, aliwaghuri watu wake na kuwafanyia hila mpaka akasababisha Khalid awapige vita kwa upanga. Na baada ya hapo watu wa kaumu yake walikuwa wanamwita: “urfu nnari” nalo ni jina la mtu mdanganyifu kwao.”

  • 1. Amirul-Mu’minin alikuwa anazungumzia kuhusu suala la mahakimu wawili, mtu mmoja katika sahaba zake alisimama akasema: “Ulitukataza kupitisha hukumu, kisha ulituamrisha tufanye hukumu, hivyo hatujui ipi kati ya amri mbili hizi yenye mwongozo kwa kuilinganisha na nyingine!” Yeye (a.s.) akapiga mkono wake juu ya mwingine na akasema: “Haya ni malipo ya mwenye kuacha itikadi.” Hapo ndipo al-Ash'ath alisema alilosema, na Amirul-Mu’minin anakusudia kuwa: Haya ndiyo malipo yenu kwa vile muliacha uthabiti na kufanya ghasia na mukanifanya nilazimike kukubali maamuzi yenu.
  • 2. Mfumaji: Na yasemekana kuwa wafumaji wanajulikana kwa upungufu wa akili sana katika watu, na Wayemeni huaibishwa kwa kuitwa wafumaji. Na Ash'ath ni mtu wa Yemen kutoka kijiji cha Kinda. Ash'ath alikuwa katika Sahaba wa Imam Ali (a.s) kama alivyokuwa Abdullah bin Ubayy bin Salul katika maswahaba wa Mtume wa Mungu (s.a.w.w), kila mmoja kati ya hawa wawili ni kiini cha unafiki katika zama zake.
  • 3. Ametekwa mara mbili: Mara akiwa kafiri katika baadhi ya vita vya kijahiliya, na hivyo ilikuwa kabila la Muradi lilimuua Qais al-Ashaji, baba wa Ash’ath, yeye al-Ash’ath alitoka ili kulipiza kisasi cha baba yake.