read

25. Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Habari zimeenea na kumfikia kuwa watu wa Muawiyah wameteka nchi (Yemen) na wafanyakazi wake wawili wa Yemen walimjia, nao ni Ubaidullahi bin Abbas na Saeed bin Namran alipowashinda nguvu Busru bin Abii Artaat. Hapo (amani imfikie), alisimama juu ya mimbari akiwa ameudhika na watu wake kuwa wazito kwenye jihadi na kuwa kwao kinyume na yeye katika rai, akasema:

“Hakuna kilichobakia isipokuwa (mji wa) Kufah, naweza kuukunja na kuukunjua,1 kama haukuwa ila ni wewe2 kimbunga chako kinavuma Mungu akuweke katika hali mbaya!”

Alitolea mfano ubeti wa shairi:

Oh! ewe Amr uzuri wa maisha mema ya babako,
Nimeambulia makombo kidogo mchuzi wa kile chombo.

Hatimaye alisema (a.s):

“Nimepata habari kuwa Busra amehujumu na kuitwaa Yemen, nami namuapa Mungu nina yakini watu hawa watawashindeni na watakuwa na dola juu yenu kwa sababu ya kushikamana katika batili yao, na kwa sababu ya kufarikiana kwenu katika haki yenu, na kwa kumuasi kwenu Imam wenu akiwa katika haki, na kwa kumtii kiongozi wao akiwa katika batili, na kwa kutekeleza amana kwa kiongozi wao na kwa hiyana yenu, na kuwa kwao wema katika nchi yao, na kwa kuwa kwenu waovu.

Kama mmoja wenu ningemwamini na bilauri ya kunywea maji, ningeogopa huenda akaondoka na mkono wake. Oh! ewe Allah, kwa kweli wamenichafua moyo na nimewachafu mioyo, nimewachoka nao wamenichoka.
Basi nibadilishie walio bora kuliko wao nami nibadilishe kwao na mwingine ambaye ni mshari zaidi kuliko mimi!
Oh! ewe Allah, ziyayushe nyoyo zao kama iyayukavyo chumvi ndani ya maji. Wallahi natamani lau ningekuwa na askari wapanda farasi elfu moja kutoka kwa Bani Firasi ibni Ghanmin kama asemavyo mshairi:

Lau utawaita watakujia miongoni mwao
Wapanda farasi kama wingu la kiangazi”.

Kisha aliteremka kutoka mimbari. Ar-Radhwiyu amesema: “Nasema Al’armiyatu ni wingi wa neno Ramiy, ni mawingu. Na Hamimu hapa: ni wakati wa kiangazi. Na mshairi ameyataja khususan mawingu ya wakati wa kiangazi, kwa sababu yanakwenda haraka mno kwa kuwa hayana maji, na mawingu huenda kwa uzito kwa kujawa na maji. Hali hiyo haiwi aghalabu ila wakati wa masika. Na mshairi alikusudia kuwasifu kuja kwao haraka waitwapo na kutoa msaada waombwapo msaada. Na dalili ni usemi wake: hunalika lau daauta ataaka min hum - hapo endapo utawaita watakujia miongoni mwao.”

  • 1. Aqbidhuha wa absutuha: Yaani, nafanya humo kama afanyavyo mwenye nguo katika nguo yake, anaikunja na kuikunjua.
  • 2. (Fa inlam takuni .........): Yaani, kama sina ninachomiliki katika dunia ila mji wa Kufah wenye fitna, ewe Allah itolee mbali!