read

27. Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Katika kuhimiza jihadi na kuwalaumu wanao kaa nyuma:

“Kwa hiyo kwa kweli jihadi ni mlango katika jumla ya milango ya Jannah (peponi), Mwenyezi Mungu ameufunguwa kwa ajili ya wapenzi Wake makhsusi. Nayo ndio vazi la taqwa (uchamungu), na ni ngao ya Mungu yenye kuhifadhi, na stara yake thabiti.

Hivyo basi, mwenye kuiacha kwa kutoipenda, Mungu atamvisha nguo ya udhalili na balaa litamuenea na atadhalilishwa kwa kutwezwa, na kudharaulika, na moyoni mwake kuondolewa akili na fahamu. Ukweli umeondolewa kutoka kwake kwa sababu ya kuipoteza jihadi. Atakumbwa na aibu na kunyimwa insafu.1

Angalieni mimi nimekuwa nikikuiteni kupambana na watu hawa usiku na mchana, kwa siri na kwa tangazo la wazi, na nilikuambieni (washambulieni kabla hawajakushambulieni, wallahi watu hawajapata kushambuliwa katu katika kitovu cha nyumba yao ila watadhalilishwa) mkategeana na mkadhoofu, mpaka mliposhambuliwa na miji yenu ikatekwa; basi huyu nduguye Ghamid farasi wake wameingia Anbaar,2 na amemuua Hasan bin Hasan Al’Bakriy, na wamewaondoa farasi wenu kwenye ngome yao.

Na habari zimenifikia kuwa mtu miongoni mwao huingia kwa mwanamke Mwislamu na mwanamke dhimiy na anampora pambo la mguuni, bangili, kidani chake, na shanga na huwezi kumziwia ila kwa kusema; (Innaa lil lahi wain naa ilayhi raajiuna 2:156) na istir’haam – kupiga kelele ili kuomba rehema kisha wakaondoka bila ya kupunguwa mtu kati yao. Hakupata mtu kati yao jeraha, wala kumwagika damu yao; lau mtu Mwislamu akifa baada ya hali hii, majonzini hangepaswa kulaumiwa, bali kwa mtazamo wangu angekuwa amestahiki!

Oh! Ajabu ilioje inavunja moyo na inahuzunisha, kuona hawa watu walivyokuwa na mshikamano katika matendo yao batili, na kusambaratika kwenu mbali na haki yenu! Ubaya na huzuni ilikufikeni, mlipokuwa lengo la kutupiwa mishale. Mnashambuliwa wala hamshambulii, mnahujumiwa wala hamhujumu. Mungu anafanyiwa maasi mmebaki mmeridhika.

Nikiwaamuruni kuwaendea siku za joto mnasema hili ni joto kali, tungojee joto lipungue, na nikikuamuruni kuwaendea wakati wa baridi mnasema hii ni baridi kali, tungojee baridi iondoke. Hivyo yote ni kukimbia joto na baridi; na mkiwa mwalikimbia joto na baridi, basi ninyi wallahi upanga mtakuwa ni wenye kuukimbia zaidi!”

Oh! Enyi mlio mfano wa wanaume wala si wanaume, fikra za kitoto, na mna akili mfano wa akili za wanawake watunza “nyumba ya mapambo.” Natamani nisingewaona wala nisingewatambua kabisa - wallahi kuwajua huku kumeleta aibu na kumalizikia huzuni na hasara. Mungu awalaani, mmeujaza moyo wangu usaha na kuusheheni hasira, na mmeninywesha konga la huzuni konga baada ya konga, mmeichafua rai yangu kwa kuasi na kunitelekeza, kiasi cha kufikia makuraishi kusema; ‘hakika mwana wa Abi Talib ni mtu shujaa lakini hana maarifa ya vita’

Mungu awahurumie, hivi kuna yeyote miongoni mwao mkali na mwenye uzoefu zaidi na wa tangu zaidi kuliko mimi. Nimeinukia nayo nikiwa sijafikia umri wa miaka ishirini, na bado, mimi huyo niko humo nikiwa nimevuka miaka sitini, lakini hana rai muwafaka asiyetiiwa!”

  • 1. Insafu ni uadilifu; atanyimwa uadilifu kwa kuwa Mungu atajaalia mtu atakayemzidi nguvu na kumdhulumu haki yake.
  • 2. Anbaar: Ni mji ulioko ukingo wa mashariki wa mto wa Furati.