read

28. Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Katika kuhamasisha maandalizi ya masurufu ya akhera:

“Hivyo sasa kwa kweli dunia imetupa mgongo na kutangaza msafara kuaga kwake. Na kwa kweli akhera imewadia na kupiga mbiu ya kuja kwake ghafla.

Lo! Kwa kweli leo ni siku hasa ya maandalizi, na kesho ndio mashindano ya mbio, na nishani ni (Jannah) Pepo, na mwisho wake ni moto; je hakuna mwenye kutubu kwa makosa yake kabla ya mauti yake? Je hakuna wakutenda mema kwa ajili yake kabla ya siku atakayokuwa na haja kubwa.
Angalia! ninyi mpo katika siku za matumaini, ambazo nyuma yake kuna mauti.

Hivyo mwenye kutenda mema katika siku zake za matumaini kabla ya kufikiwa na ajali yake, atakuwa amenufaishwa na matendo yake, na kifo chake hakitomdhuru, na mwenye kufanya uzembe katika siku zake za matumaini kabla ya kufikiwa na ajali yake, atakuwa amepata hasara kazi yake, na ajali yake itamdhuru. Angalia! fanyeni wema wakati wa upendo wenu kama mfanyavyo wakati wa hofu.

Angalia! kwa hakika mimi sijaona kilichotelekezwa kama jannah (Pepo) kwani amelala mwenye kuitafuta, wala kuona kitu kilichopuuzwa kama moto amelala aukimbiaye.1

Angalia, asiyenufaika na ukweli bila shaka batili itamdhuru,2 na ambaye hawi mnyofu kwa mwongozo, upotovu utamkokota na kumzamisha kwenye maangamizi.

Alaa! kwa kweli ninyi mmeamriwa kufanya msafara,3 na mmeoneshwa masurufu; na kwa kweli ninalohofia mno kwenu ni kufuata utashi mbaya wa nafsi na kurefusha matumanini, basi chukueni masurufu kutoka hapa duniani ambayo kwayo mutakayojihifadhi nayo kesho nafsi zenu”.

Maelezo: Sharifu Ar-Radhiy (r.a) amesema; (Nasema): Kuwa lau kungekuwa kuna maneno yawezayo kumshika mtu shingo na kumfanya aipige pande dunia na kulazimika kutenda mema kwa ajili ya akhera, yangekuwa maneno haya. Na yanatosha kuwa yenye kukata viambatisho vya matumaini (makubwa ya kubaki duniani). Na ni yenye kuwasha msukumo wa kuonyeka na kujikataza.

Na la kustaajabisha mno ni usemi wake (a.s) Alaa! Leo ni siku ya maandalizi, na kesho ndio mashindano ya mbio, na nishani itakuwa pepo na mwisho wake ni moto. Kwa kuwa humo, pamoja na utukufu wa tamko, na adhama ya thamani ya maana, na ukweli wa mithali na uhakika wa tash’biihi, kuna siri ya kustaajabisha, na maana nzuri.

Nayo ni ile kauli yake (a.s): WA SABAQATU AL JANNATU WAL GHAAYATU ANNARU, akatofautisha kati ya matamko mawili kwa sababu ya kutofautiana maana mbili, wala hakusema; WASABAQATU ANNARU WALGHAAYATUL JANNAH kama alivyosema; ASSABAQATU AL-JANNATU, kwa sababu (al-Istibaq - kushindana) huwa kwenye jambo lipendwalo na lengo litakiwalo. Na hiyo ni sifa ya Jannah, wala maana hii haipo katika moto.

Tunajilinda kwa Mungu tuwe mbali nao, kwa hiyo haikufaa aseme: WASABAQATU ANNARU bali amesema; WALGHAAYATU ANNARU kwa kuwa ALGHAYA ni mwisho wa jambo, au matokeo yake, kwani mwisho huwa kwa aupendaye na asiyeupenda kwa hiyo ndiyo maana ikawa yafaa alitumiye neno hilo kwa ajili ya mambo mawili yote. Kwa hiyo neno hilo mahali hapa ni kama matokeo na mwisho wa jambo.

Mungu (s.w.t) amesema; QUL: TAMATAU FA INNA MASWIRAKUM ILANNARI - sema: Stareheni! Kwani marejeo yenu ni motoni; 14:30). Wala haifai mahali hapa aseme; (FAINNA SABAQATAKUM ILANNARI) - Na kwa hakika nishani yenu itakuwa moto. Zingatia hilo, undani wake wastaajabisha, na kina chake ni cha mbali, kizuri, na hivyo hivyo maneno yake mengi (a.s). Na katika baadhi ya nakala, imekuja ndani ya riwaya nyingine (WAS’SUBAQATUL AL JANATU) SIYNI ikiwa na ‘dhummah,’ na Subaqatu kwao ni jina la kitu ana- chopewa mshindi, kama vile mali au nishani mfano wa kikombe, na maana hizo mbili zipo karibu, kwa kuwa hiyo haiwi tuzo kwa kitendo cha jambo la kulaumiwa, bali huwa tuzo kwa ajili ya kitendo cha jambo linalohimidiwa.

  • 1. Sijaona akalala mwenye kuitaka pepo, anasema: Ni miongoni mwa ajabu kubwa mno ambayo hajapata kuiona mfano wake ni ambaye anaamini kwamba kuna Jannah na utukufu wake, na kukamilika sababu za maisha ya furaha humo, vipi anaitaka na kisha analala! Na miongoni mwa maajabu makubwa, ni ambaye ana yakini na Moto, na kutisha kwake, na ni mkusanyiko wa sababu za mashaka, vipi haukimbii bali analala! Yaani, haimpasi alale mtakaji wa hii wala mkimbiaji wa hii.
  • 2. Manufaa yote sahihi yapo katika haki tu, endapo msemaji atasema kuwa: haki haikum-nufaisha, hivyo batili ni yenye kumdhuru mno. Na ambaye haukumnyoosha mwongozo wa mwongozaji kuielekea haki, yaani, haikumfikisha kwenye utashi wake wa maisha mema, upotofu utamkokota kwenye limbi la maangamizi.
  • 3. Msafara ni kuiacha dunia, na tumeamrishwa nao ni amri ya kimaumbile, yaani kama Mungu alivyotuumba, ametuumbia kuyaacha maisha ya dunia ili tukakae milele akhera, na masurufu aliyotuonyesha ni matendo mema na kuacha maovu.