read

30. Na Miongoni Mwa Semi Zake (A.S)

Kuhusu maana ya kumuuwa Uthman:

“Lau ningeamuru hilo ningekuwa muuwaji, na lau ningekataza ningekuwa mwenye kunusuru,1 ila ni ukweli kuwa aliyemnusuru hawezi kusema kuwa: Ametelekezwa na ambaye mimi ni bora kuliko yeye, na aliyemtelekeza hawezi kusema: Amemnusuru ambaye ni bora kuliko mimi.2

Na mimi nayajumlisha mambo yake kwenu. Amejitwalia na kuyatumia vibaya aliyoyatwaa. Na mmekosa uvumilivu, mkafanya vibaya kutovumilia kwenu.3 Na Mungu anayo hukumu muwafaka kwa mwenye kujitwalia na mtovu wa uvumilivu”.

  • 1. Anasema: Kwa hakika yeye hakutoa amri ya kuuliwa Uthman, lau angefanya hivyo angekuwa muuwaji, na hali halisi yeye hana hatia ya mauwaji yake. Na wala hakukataza, yaani hakumlinda kwa upanga wake wala hakupigana badala yake, vinginevyo angekuwa mwenye kumnusuru. Ama kukataza asiuliwe kwa ulimi wake, ni jambo lililothibiti, kwani yeye ndiye aliyewaamuru Hasan na Husain wawaziwie watu mbali na yeye.
  • 2. Ila ni ukweli kuwa aliyemnusuru… maana yake ni kuwa waliomtelekeza walikuwa bora kuliko waliomnusuru; kwa sababu waliomnusuru wengi miongoni mwao walikuwa mafasiki, mfano wa Marwan bin Al-Hakam na walio mfano wake. Na walio mtelekeza ni Muhajirun na Ansar. Kwa hiyo waliomnusuru hawakuwa bora zaidi yawaliomtelekeza. Kwa ajili hiyo aliyemnusuru hawezi kusema mimi ni bora kuliko aliyemtelekeza, wala hawezi aliyemtelekeza kusema kuwa: Mwenye kumnusuru ni bora kuliko mimi, anakusudia nyoyo zimeafikiana kuwa waliomnusuru hawakuwa na ubora wowote juu ya waliomtelekeza.
  • 3. (Waanaa jamiun lakum amrahu......) mpaka mwisho wa mlango, maana yake ni kwamba yeye Uthman amefanya lisilofaa, na ninyi mmefanya lisilofaa, ama yeye amejitwalia akafanya vibaya, yaani aliyahodhi mambo akafanya vibaya katika kuhodhi, na ilikuwa inambidi afanye wepesi ili asikuudhini, ama ninyi mlikosa subira kwa aliyoyafanya, yaani mlihuzunika mkafanya vibaya katika huzuni; kwa sababu ninyi mmemuua, hamkufanya upole katika kukatishwa tamaa kwenu wala hamkusimama kwenye mpaka ulio bora kwenu, ilikuwa inawabidi muishie kulalamika, wala msiende kwenye kufanya ubaya kiasi cha kuua, na Mungu anayo hukumu kumhusu aliyehodhi, naye ni Uthman, na aliyekatishwa tamaa, nao ni ninyi, imma amchukulie yeye na awachukulie ninyi au amsamehe na awasamehe ninyi.