read

32. Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Kuhusu dhulma ya zama:

“Enyi watu, kwa kweli sisi tupo katika muda wa dhulma na zama za kufuru,1 mwema humo ahesabika muovu, na dhalimu huzidi humo kiburi, hatunufaiki na tulilojua, wala hatuulizi tusilolijua wala hatuogopi msiba mpaka utufike, na watu wako aina nne: Miongoni mwao kuna ambaye hakuna kinachomzuia kufanya ufisadi katika ardhi isipokuwa unyonge wa nafsi yake na ubutu wa silaha zake na uchache wa mali yake.

Na miongoni mwao kuna mwenye kujitokeza na upanga wake na kuitangaza shari yake, na ambaye ameleta askari wake wapanda farasi na askari wake waendao kwa miguu, ameiandaa nafsi yake kwa shari na ufisadi, ameiangamiza dini yake kwa ajili ya mali yenye kuvunjika afaidikayo nayo haraka, au kundi la farasi analolichunga au mimbari aipandayo.2

Biashara mbaya ni kuiona dunia kuwa ina thamani kwa ajili yako, na uliy- onayo yatakuwa fidia kwa Mungu!

Na miongoni mwao kuna ambaye aitaka dunia kwa kazi ya akhera, wala haitafuti akhera kwa kazi ya dunia, ameishusha chini haiba yake, na kuzifanya hatua zake karibu, na kupania nguo yake, na amejipamba nafsi yake ili aaminike, na ameifanya sitara ya Mungu kuwa ni kichaka cha kufanyia maasi.3

Na miongoni mwao kuna ambaye unyonge wa nafsi yake umemuweka mbali na kuutaka ufalme,4 na kukatika kwa sababu zake, hali hii imemzuia kuifikia nafasi yake, kutokana na hali hiyo akajipamba kwa jina la kutosheka, na kujipamba na vazi la walioipa nyongo dunia, na katika hilo hana safari ya matembezi ya jioni wala asubuhi.

Na wamebakia watu ambao kumbukumbu ya marejeo imeyafumba macho yao,5 na woga wa kukusanywa umebubujisha machozi yao, (kukusanywa baada ya kufufuliwa watu Siku ya Kiyama), kwa hiyo wao wapo kati ya mwenye kukimbia kiasi cha kujitenga, na mwenye kuogopa aliyekandamizwa, na aliye kimya aliyefumbwa mdomo, na mlinganiaji aliye na ikhlasi, na mwenye kuhuzunika na anayeumia.

Taqiiya imewazimisha,6 wamekumbwa na udhalili, hivyo wao wako ndani ya bahari ya chumvi,7 vinywa vyao vimenyamaza, na nyoyo zao zimejeruhiwa. Wamewaidhi mpaka wamechoka, wamekandamizwa mpaka wamekuwa dhalili, na wameuliwa mpaka wamebaki wachache.

Dunia iwe kitu kidogo machoni mwenu kuliko majani ya mti yaliyopukutika, na mabaki ya manyoya ya ngamia yaliyotindwa.8 Waidhikeni na waliokuwa kabla yenu, kabla hawajawaidhika na ninyi wale watakao kuwa baada yenu, ikataeni dunia ikiwa ni ya kulaumiwa, kwa kuwa hiyo imewakataa walioipenda zaidi kuliko ninyi.

Maelezo: Amesema Ar-Radhiy: Hutba hii huenda asiyejua akainasibisha na Muawiya; hali ikiwa ni miongoni mwa manemo ya Amirul-Mu’uminina (a.s) yasiyo na shaka. Basi wapi na wapi dhahabu na udongo! Na wapi na wapi maji baridi na ya chumvi! Na hilo limethibitishwa na dalili yenye umahiri. Na mkosoaji mwerevu Amr bin Bahri Al’Jahidh, amekosoa hilo kwa kuwa yeye ameitaja hutba hii ndani ya kitabu Al-Bayan wat-Tabyiin na amemtaja aliyeinasibisha na Muawiyah, kisha aliongea baada yake maneno kuhusu maana yake, kwa ujumla wake ni kuwa yeye alisema: “Maneno haya yashabihiyana mno na maneno ya Ali (a.s) na madhehebu yake katika kuzigawa aina za watu, na katika kutoa habari ya walivyo miongoni mwa makandamizo na udhalili, na miongoni mwa Taqiiyah na hofu yalingana mno.” Amesema: “Basi lini tumemkuta Muawiyah katika hali miongoni mwa hali, na katika usemi wake akienda mwenendo wa watu wenye zuhdi mwenendo wa wachamungu!”

  • 1. Al-Kanuudu: yaani kafiri mno. Na huelezwa (kwenye riwaya nyingine) Wa zamanun shadiidu, yaani, zama zenye ubakhili: Kama ilivyo katika kauli Yake Ta’ala: (Wa innahul hubil khair lashadiidu - kwa hakika yeye hupenda kheri mno - al-Aadiyat: 8). Yaani, kwa hakika mwanadamu, kwa sababu ya kupenda kwake mali, ni bakhili, na sifa ni ya watu wa zama na dahari kama ilivyo dhahiri. Na ubaya wa tabia za watu, huwafanya kumhesabu mtu mwema kuwa ni mbaya.
  • 2. Mimbari aipandayo: Yaani, katika kupanda mimbari na kuwahutubia watu ni miongoni mwa daraja ya juu inayomfanya mtu aitafute, kwa hiyo sehemu hii ya vitu au ya watu ime- haribu watu katika kutafuta umashuhuri huu uliotajwa.
  • 3. Kichaka: Na hili ni kundi la tatu.
  • 4. Na hili ni kundi la nne, wala si katika kuipa nyongo dunia, si katika kutenda wala kuacha.
  • 5. Hili ni kundi la tano la watu wote, na makundi manne ya watu walio maarufu walio katika maono ya watu wa kawaida, hivyo basi kauli yake ya hapo mwanzo (watu ni makundi manne) anakusudia kwayo ambao wanajulikana kwa mtazamo wa wazi wa watu, ama watu ambao waliofumba macho mbali na tamaa za dunia; kwa kuiogopa akhera, na kukum- buka kwao marejeo yao, hawa hawajulikani kwa watu wa kawaida, ila tu hutambuliwa hali zao na walio mfano wao, hivyo kana kwamba wao katika mtazamo wa watu, wao si watu.
  • 6. Taqiiyah imewazimisha: Imeangusha utajo wao kiasi cha kuwa hawakumbukwi na watu. Na taqiiyah hapa ni kujikinga dhidi ya dhulma kwa kuificha hali halisi.
  • 7. Wako katika bahari ya chumvi: Yaani wao kati ya watu ni kama aliyetumbukia katika bahari ya chunvi, hapati cha kuzima kiu yake wala.
  • 8. Amewataka waidharau dunia baada ya mgao uliotangulia; kwa sababu imethibiti kuwa dunia haiko safi isipokuwa kwa watu wa shari, ama wachamungu aliowataja wao hawakuambua kitu kutoka dunia hii isipokuwa kutaabika, na kila ambaye hali yake ni kukimbilia kwa watu wa shari, na kujikausha mbele ya watu wa kheri basi yeye ndiye afaa mno kudharauliwa.