read

33. Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Alipokuwa akitoka ili kupigana na watu wa Basra:

Abdullah bin Abbas alisema: “Niliingia kwa Amirul’Mu’minina (a.s) alipokuwa Dhuqaar, 1naye akiwa yuashona ndara zake, akaniambia: “Nini thamani ya ndara hizi?” Nikamwambia: “Hazina thamani yoyote.” Akasema (a.s): “Wallahi hizi nazipenda mno kuliko uamiri wenu (ukhalifa) ila tu endapo nitatenda haki au kuzuia batili” Hatimae alitoka na kuwahutubia watu akisema:

Kwa kweli Mwenyezi Mungu swt. alimtuma Muhammad (s.a.w) hapakuwa na mmoja yeyote katika waarabu asoma Kitabu, wala kudai unabii, basi yeye akawaongoza watu mpaka aliwafanya wakae mahali mwao,2 na kuwafikisha kwenye uokovu wao, hivyo wakawa katika istiqama ndani ya Uislamu na kuimarika nyayo zao.3

Wallahi nilikuwa miongoni mwa waliokuwa wakiongoza, nikiwafurusha mpaka walitokomea wote, sikudhoofu wala sikuwa mwoga.

Kwa kweli mwendo wangu ni ule ule, Wallahi nitaitoboa batili mpaka haki ijitokeze pembezoni mwake.4 Wana nini makuraishi na mimi!

Wallahi niliwapiga vita wakiwa makafiri, na nitawapiga vita wakiwa wamedanganyika, kwa kweli mimi ni mwenzao wa hapo jana na ni mwenzao hii leo. Wallahi hawatuadhibu makuraishi ila ni kwa sababu Mungu ametuchagua juu yao, na tumewaingiza ndani ya mamlaka yetu, kwa hiyo wamekuwa kama alivyosema wa kwanza (mshairi):

“Kwa maisha yangu, ungali wanywa maziwa mapya asubuhi,
Na kula kwako tende kwa jibini.

“Sisi ndio tuliokupa daraja, wala hukuwa wa juu,
na kukuzungushia ulinzi (kwa farasi) na mikuki.”

  • 1. Dhuqaar: Ni kitongoji kati ya Waasiti na mji wa Kufa, nacho kipo karibu na mji wa Basra, na hapo ilipiganwa vita kati ya waarabu na wafursi (wa-Irani), waarabu walipata nusra, hilo lilikuwa kabla ya Uislamu.
  • 2. Kukaa mahali mwao, kwamaanisha watu kabla ya Uislamu kana kwamba walikuwa wageni waliosambaratishwa, na Uislamu ndiyo nyumba yao wanayoishi na kuwa na amani bila ya hofu, kwa hiyo Nabii (s.a.w.w.) amewaongoza watu mpaka amewafikisha nyumbani mwao - Uislamu - kwamba walikuwa wamepotea mbali nao, aliwafikisha mahali pao pa uokovu mbali na kuangamia.
  • 3. Ukatuama mpini wao: Yaani walituama ndani ya Uislam, yaani mpini wao ulikuwa umepinda ukanyooka, na Qaana: mpini na mkuki, na maneno haya ni mfano wa kunyooka kwa hali zao.
  • 4. Wallahi nitaitoboa batili: Kana kwamba ameifanya batili ni kitu kimeizingira haki na kuificha, na haki ikawa iko ndani mwake kama kitu kilichojificha na kujistiri humo, hivyo basi akaapa kuitoboa ile batili mpaka haki ijitokeze pembezoni mwake, batili inakimbilia kwenye dhana na kuishughulisha mbali na haki, na inakuwa kizuizi kinachozuia uoni wa haki, kwa hiyo ni kama kitu kimeienea haki na kuificha, na haki inakuwa katika mficho wake. Na maneno haya ni methali ya hali ya batili na haki, na hali ya Imam katika kuifichua batili na kuidhihirisha haki.