read

34. Na Miongoni Mwa Khutba Zake

Katika kuwaandaa watu ili kuwakabili watu wa Sham:

“Ole wenu! Kwa kweli nimechoka kuwakemea! Je mmeridhika na maisha ya dunia yawe badala ya akhera na unyonge mahali pa utukufu? Endapo nikiwaita kumpiga vita adui yenu, macho yenu huzunguka kana kwamba mmefunikwa na mauti na kutokwa na fahamu kwa (kufunikwa na mauti).

Hufungika kwenu hutba yangu, kwa hiyo mnakanganyikiwa kana kwamba nyoyo zenu zimepagawa kwa hiyo hamuitii akilini. Ninyi kwangu hamuaminiki kamwe. Ninyi si nguzo itegemewayo, ninyi sio jamaa wa kuhitajiwa. Ninyi mko mfano wa ngamia ambao wachungaji wake wamepotea, kila wakusanywapo upande mmoja wanatawanyika upande mwingine, Wallahi wachochezi wabaya wa vita ni ninyi! Mnachokozwa wala hampigani, ncha zenu zinapunguzwa wala hamghadhibiki; adui halali na akawaacha na hali ninyi mpo katika mghafala mmesahau. Wallahi wamezidiwa wenye kutelekezana.

Wallahi mimi nakudhanieni endapo vita vitakuwa vikali, na mauti ikawa imeshika kasi mtakuwa mmejitenga na ibn Abi Talib kama kinavyojitenga kichwa.

Wallahi kwa kweli mtu anatoa mwanya kwa adui yake; anakuwa yu aila nyama yake, na anavunja mfupa wake na anachana ngozi yake, (huyu) kushindwa kwake ni kukubwa mno, kilichokusanya pande za kifua chake ni dhaifu (yaani yeye ni dhaifu). Wewe kuwa yeye ukipenda; ama mimi Wallahi simwezeshi binafsi adui yangu… viganja na nyayo zitadondoka na baada ya hivyo Mungu atafanya apendavyo.

Enyi watu, kwa hakika mimi nina haki juu yenu na ninyi mna haki juu yangu: Na haki yenu juu yangu ni kuwapeni nasaha, na kuwarahisishia ruzuku zenu, na kuwaelimisheni ili msiwe wajinga, na kuwaadabisheni ili mjue. Ama haki yangu juu yenu ni kuitekeleza bai’a, na nasaha mbele ya macho yangu na mbali nayo, na kuniitika niwaitapo, na kutii ninapowaamrisha”.