read

42. Na Katika Jumla Ya Usemi Wake (A.S)

Katika kuyafuata matamanio na kuwa na matumaini marefu:

Enyi watu! Kwa kweli niliogopalo zaidi juu yenu ni vitu viwili:

1. Kuyafuata matamanio

2. Na kuwa na matumaini ya muda mrefu1

Ama kuyafuata matamanio kunazuia haki, na kuwa na matumaini ya muda mrefu kunasahaulisha akhera. Oh, jueni kuwa dunia imepita haraka sana; hakuna kilichobaki humo ila mabaki mfano wa mabaki ya maji katika chombo ambacho maji yake yamemwagwa na mmwagaji wake.

Oh! jueni kuwa akhera imewadia, na kila mmoja wao anao watoto, basi ni bora muwe miongoni mwa wana wa akhera, na wala msiwe miongoni mwa wana wa dunia; kwa kuwa kila mwana atakutanishwa na mama yake Siku ya Kiyama, kwa kweli leo ni siku ya matendo na wala hapana hesabu na kesho ni hesabu tu hakutokuwa na matendo”.

  • 1. Tuulul’amalu, kuwa na matumaini ya muda mrefu ni kujidhania kuwa muda wa maisha ni mrefu kwa hiyo nitasali nitafunga nita nita…….kwa kujimwaga na raha ya dunia ambayo ni ya muda mfupi, huku mtu yu ajiliwaza nafsi yake kuwa anayoyaacha atayadiri- ki na kuyatekeleza yote bila ya wasiwasi hapo baadae, na hii ni sifa mbaya mno. Ama nguvu ya matumaini ya kufanikisha mema, kwa kuwa na yakini na msaada wa Mwenyeezi Mungu, huo ni uhai wa kila jema na ni lenye kuleta matukufu. Na walionyimwa hilo wamekatishwa tamaa na rehema ya Mungu, waweza kuwadhania wako hai hali wakiwa wafu hawana hisia.