read

43. Na Miongoni Mwa Maneno Yake (A.S)

Walimshauri Sahaba zake kujiandaa kwa vita baada ya kuwa alikwisha mtuma Jarir bin Abdillah Al’Bajaliyi kwa Muawiyah:
“Kwa kweli kujiandaa kwangu kuwapiga vita watu wa Sham hali Jarir akiwa kwao ni kuifunga Sham, na kuwatowa watu wake mbali na kheri endapo wataitaka.1

Lakini nimemuwekea Jarir wakati ambao hatobaki baada ya wakati huo, ila endapo atakuwa amehadaiwa au ameasi. Rai sahihi iko pamwe na utulivu, basi kuweni watulivu, wala sichukii kujiandaa kwenu.2

Kwa kweli nimelichunguza suala hili kwa undani kupitia pande zote sikuona njia nyingine ila ni vita au kuyakufuru aliyoyaleta Muhammad (s.a.w.w.). Kwa hakika umma huu ulikuwa na mtawala aliyezusha uzushi - alizua bid’a - aliwafanya watu wamkasirikie, na walisema, kisha walichemka na kubadilisha kila kitu.

  • 1. Anasema (a.s.): Kuwa yeye alimtuma Jarir ampe habari Mu’awiyah na watu wa Sham kuwa wamfanyie ba’iya yeye Imam, na waingie katika utii wake, na hajakatishwa tamaa nao. Hivyo basi kujiandaa kwake kuwapiga vita, na kukusanya jeshi, na kulipeleka kwenye ardhi yao, ni kuifunga milango ya amani kwa watu wa Sham, na kuwaondolea kheri endapo wataitaka, hivyo basi rai sahihi ni kufanya upole. Lakini yeye hachukii kujiandaa, yaani kila mmoja ajiandae binafsi na yale anayoyahitajia katika vita kama vile silaha na mfano wake, na aiweke nafsi yake mbali na yanayomshughulisha mbali na vita lau ikitokea, kiasi kwamba akiitwa, asiwe goigoi kuitika, na asiwe na kinachomzuia kuikabili.
  • 2. Kuwakatalia kwake kujiandaa na usemi wake: “Wala sichukii kujiandaa kwenu” si maneno yanayopingana; kwa kuwa alichukia kujionyesha kwao maandalizi na kusema wazi wazi, wala hakuchukia kujiandaa kwa siri. Na yawezekana isemwe kuwa alikuwa anachukia kujiandaa kwake mwenyewe binafsi, wala alikuwa hachukii kujiandaa kwa sahaba zake; na haya mawili yako mbalimbali. Na mtazamo huo ameuchagua Al-Qut’bu Ar-Rawandiy.