read

46. Na Katika Maneno Yake (A.S)

Alipoazimia safari ya Sham:

Oh, Ewe Allah! kwa hakika mimi ninajilinda kwako na mashaka ya safari, na huzuni ya marejeo, na ubaya wa mandhari katika watu wa ndani na mali na mtoto.

Oh Ewe Allah! Wewe ni mwenzi safarini, na wewe ndio wa kuachwa nyuma na familia, wala havikusanyi viwili hivi asiyekuwa wewe, 1 kwa kuwa mwenye kuachwa nyuma hawezi kuwa mwenzi safarini, na ambaye ni mwenzi safarini hawi muachwa nyuma.2

Sayyid ar-Radhiy (r.a.): “Na mwanzo wa maneno haya imeelezwa kutoka kwa Mjumbe wa Mungu (s.a.w.w.) na Amirul-Mu’mini (a.s.) ameyafuatilia kwa balagha zaidi, na kuyahitimishia kihitimisho kizuri, kwa usemi wake (walaa yaj’mau’huma ghairuka) mpaka mwisho wa mlango.”

  • 1. Maneno ya kwanza yameelezwa kutoka kwa Mtume wa Mungu (s.a.w.w.) ndani ya vitabu sahihi na ameyakamilisha Amirul’Mu’minna (a.s) kwa kauli yake: (wala havikusanyi viwili hivi mwingine asiyekuwa Wewe) kwa kuwa dhati ya Mungu (swt) huwa sawa kwake kati ya mahali na zama - yaani huwezi kusema hapa Mungu hayupo au wakati huu Mungu hayupo - hivyo basi nyumbani na safarini kuihusu dhati Yake (swt) ni sawa.
  • 2. Dua hii ameitaja Nasr bin Muzahim katika Kitabu “Siffiin,” na wengine miongoni mwa waelezaji wa Sira pia wameitaja. Aliomba dua hii Amirul-Mu’mini na (a.s) baada ya kuweka mguu wake juu ya kipando chake katika msafara kutoka nyumbani kwake mjini Kufa akielekea Sham (Syria) kwa ajili ya kupigana vita na Muawiyah na swahaba zake, na tukio hilo lilikuwa baada ya vita vya Jamal (Ngamia), kwa kuwa Muawiyah bin Abi Sufyan alimkinza Imam Ali (a.s) wala hakuingia katika bai’a yake, na alibuni madai ya damu ya Uthman, hivyo watu wa Sham walivutwa na madai hayo, aliwaomba nusra kwa ajili ya rai yake, wakampa nguvu ya kwenda kinyume. Hivyo basi Amirul-Mu’uminina akafanya safari kumwendea, na walikutana mahali pakiitwa Siffiin. Walipambana muda si mfupi, vitaviliishia katika tah’kiimu ya mahakimu wawili: Amru bin Al’Aas na Abii Musa Al-Ash’ariy.