read

52. Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Miongoni mwa khutba zake (a.s) - Hotuba hii inaifuata hotuba iliyotangulia katika nakala ya ibn Abil-Hadid.

Kuhusu kujinyima:

“Lo! Kwa kweli dunia imekwisha na imetoa ilani kwisha kwake. Mema yake, yameondoka yametokomea haraka, inawasukumia mwisho wakazi wake, inawasukuma kwenye umauti majirani zake. Vilivyokuwa vitamu imevifanya kuwa vichungu, na kuvichafua vilivyo kuwa safi, hakikubakia humo ila mabaki kidogo kama mabaki ya maji katika chombo au mfano wa funda la mgao, lau wenye kiu wawili wafyonze hawangekata kiu.

asi enyi waja wa Mungu azimieni msafara wa kuitoka nyumba hii ambayo wakazi wake wamepangiwa kutoweka, wala yasikushindeni nguvu humo matumaini, wala muda msiufanye kuwa mrefu humo.
Wallahi hata mlie mfano wa ngamia walio huzunika kwa kuwakosa watoto wao au muite kwa mnung’uniko wa huzuni wa njiwa, au mnyanyue sauti kwa unyenyekevu mfano wa watawa (waliojitenga na dunia wakimuelekea Mungu,) na muwe mmejitowa mbali na mali na watoto mkimuelekea Mungu; kutaka ukaribu na yeye, ili kuinyanyua daraja kwake au kughufiriwa ovu lililohesabika na vitabu Vyake, na kuhifadhiwa na malaika Wake, ingekuwa thawabu kidogo kulinganisha na ninavyowatarajia thawabu Zake, na ninavyo wahofia adhabu Zake.

Namuapa Mungu hata nyoyo zenu ziyayuke kabisa na macho yenu yatiririshe machozi ya damu aidha mkimtarajia au kumhofia, kisha mbakishwe kuishi duniani muda wake wa kudumu, matendo yenu hayangetoa malipo ya neema Zake kubwa - hata kama msingebakisha kitu katika juhudi zenu - zisingelipia chochote katika fadhila Zake nyingi juu yenu - na kuwaongozeni kwake kwenye imani.”