read

54. Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Na miongoni mwa khutba zake (a.s) - Ameitaja hii Ibn al-Athir katika kitabu an-Nihaya kwenye mada
ya Dakaka, jalada la pili, uk. 128. Rejea mwanzo wa hotuba ya 26.

Pindi waliposongamana watu ili kumfanyia bai’a:

“Walisongamana kwangu msongamano wa ngamia wenye kiu, siku ya kunyweshwa kwao, pale mchunga wao akiwa amewapeleka, na wameondolewa kamba; ilifika hali nidhanie wataniua, au baadhi yao watawauwa baadhi mbele yangu. Na nimeliangalia jambo hili kwa kuligeuza nje ndani kiasi cha kunizuia usingizi, sikuwa na njia ila kupigana nao, au kuyakanusha aliyoyaleta Muhammad (s.a.w): Nikaona kuikabili vita1 ni wepesi kwangu kuliko kuikabili adhabu, na mauti ya dunia ni mepesi kwangu kuliko mauti ya akhera.”

  • 1. Kuwapiga vita madhalimu ni wajibu juu ya imam pindi akiwa na wasaidizi, akiacha kufanya hivyo atakuwa amewacha kutekeleza wajibu, kwa hilo atakuwa anastahiki adhabu, na atakuwa mwenye kuitelekeza amri ya Mungu kwa kuacha alilomuwajibishia, anakuwa mwenye kupinga aliyokuja nayo Mtume wa Mungu (s.a.w.w.).