read

55. Miongoni Mwa Maneno Yake (A.S)

Swahaba zake waliona kwamba ameichelewesha idhini ya kupigana huko Siffiin:

“Ama kauli yenu kuwa: ‘yote haya yanatokana na kuuchukia umauti?’ Namuapa Mungu sijali iwe nimeingia kwenye umauti au umauti umenijia.1

Ama kauli yenu kuwa amekuwa na shaka ya kuwapiga watu wa Shamu! Wallahi sikuacha vita hata siku moja ila nikiwa na matumaini kuwa kundi la watu likutane na mimi na liongoke na mimi, liangaze kwa mwanga wangu japo kwa mtazamo finyu2 na hilo lanipendeza mno kuliko niliuwe (kundi la watu) hali likiwa ndani ya upotovu; japokuwa linarejea na dhambi zake.

  • 1. Watu wake waliona amechelewesha idhini yake kuwapiga watu wa Sham (Syria). Walihitilafiana kuhusu sababu ya kuchelewa. Baadhi yao walisema: “ni kwa sababu ya kuchukia mauti.” Na baadhi yao wakasema: “Ni shaka ya kuwa je! Yafaa kuwapiga watu wa Sham!” Hapo akawajibu: “Kuhusu mauti hakuwa wa kuyaogopa, na kuhusu shaka haina nafasi, isipokuwa anataraji kwa kuzuia vita wapate kuiepuka na wamjie bila ya vita, kwani hilo lampedeza mno kuliko kupigana hali watu wakiwa ndani ya upotovu, japo iwe dhambi ni yao.”
  • 2. Amewashabihisha na ambao huenda wangejiunga na yeye miongoni mwa watu wa Sham na ambaye anabubusa usiku kuuelekea moto; na hivyo ni kwa sababu macho yao ni dhaifu, hivyo wao kuongoka na mwongozo wake (a.s.) ni kama anayebubusa kwa udhaifu wa macho yake kuuelekea moto wakati wa usiku. Alisema: Hilo ni bora kwangu kuliko niwauwe wakiwa katika upotofu, ingawa endapo nitawaua nao wakiwa katika hali hii watarejea na dhambi zao. Yaani, watakuwa wamerejea, amesema swt: “Mimi ninataka urejee na dhambi zangu na zako!” al-Maida: 29