Dibaji

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Kwanza yanipasa nimshukuru Mwenyezi Mungu Jalali, asiye kuwa na mithali, kwa neema zake za kila hali na kila mahali, hata nikaweza mimi mja mpungufu, kutimiza kazi hii tukufu ya kuipitia tarjuma hii ya Kiswahili ya Nahju 'l-Balaghah.
Nahju 'l-Balaghah ni jina la diwani mashuhuri yenye khutba, uweza wa kusema, na barua za Imam Alî bin Abu Talib (a.s.). Haya yote yamekusanywa na Sharîf Ar-Radhi. Diwani hii yenye khutba takriban 237, baru 79 na mithali 480 ilikamilika mwezi wa Rajab 400 A.H./1009 A.D. Maana ya NAHJ ni njia iliyo wazi, au barabara kuu; na maana ya Balaghah ni ufasaha (wa lugha) au ilimu ya usemaji, n.k. Kwa hivyo Nahju 'l-Balaghah yaani Barabara kuu ya ufasaha.

"Huyu Imam 'Ali ni nani? Ni vigumu mno kuzitaja sifa zake kwa ukamilifu. Yeye alikuwa mtaalamu, shujaa na khatibu kuliko wote. Uchamungu wake, mapenzi yake ya Mwenyezi Mungu, uaminifu wake na ushupavu wake wa kufuata dini ulikuwa wa darja ya juu kuliko mtu yeyote ...... akichukia diplomasia (ujanja), na akipenda haki na insafu. Sera zake ni kama zilivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu. Wataalamu wa Kiyahudi na wa Kikristo wakijaaliwa kujua daraja ya ilimu yake huisujudia ilimu hiyo isioweza kufananishwa.

Wafalme wa Ki-Rumi wangependa kuzitundika picha zake katika kasri zao, na maaskari wakubwa wa vita wangependelea kulichonga jina lake kwenye panga zao.

لآ فثي ا لاَّ ءَلِيَّ وَ لآ سَيْفَ اِلاَّ دُ و الْفقار

"Hayuko kijana shujaa mfano wa 'Ali! wala hakuna upanga mfano wa Dh-ul-Faqar (upanga wa Imam 'Alî (a.s.) aliorithi kwa Mtume)."

Allama Mustafa Beck Najeeb wa al-Azhar, Cairo amesema:

خَرَجَ اِلَي الدُّ نْيَا وَ الثَّهَادَةُ مَكْتُوْبَهَّ عَلي جَبَيْنِهِ وَ خَرجَ مِنْهَا وَ الثَّهَادَةُ مَكْتُوْبَهَّ عَلي دَ لِكَ الجَبَيْنِ بضَرْبَهِ حُسَّا مٍ لَقدْ كَمَا عَلِمْنَا فِي الْكَعْبَهِ وَ ضُربَ كَمَ عَلِمْنَا فِي الْمَسْجِدِ قأَيَّه بَدَايَهٍ وَ نِهَايَهٍ اَثْْبَهَ بالْحَيَاةِ الّتي بَيْنَهُمَا مِنْ تِلْكَ الْبدَايَهٍ وَ تِلْكَ النَّهَايَهِ؟

"Imam 'Alî amekuja duniani na shahada imeandikwa kwenye kipaji chake; na ameondoka duniani na shahada vile vile imeandikwa kwenye hicho kipaji kwa dharba ya upanga. Kama tunavyojua amezaliwa ndani ya Ka'bah, na kama tujuavyo amepigwa dharba (ya upanga) msikitini. Ilioje ajabu? Mwanzo wake na mwisho wake kupata darja ya kifo cha kishahidi."

Sheikh Abbas Mahmud al-Aqqad - mwandishi maarufu wa Ki-masri amesema:

"Mtu yeyote ambaye amebobea katika lugha ya Ki-arabu atakubali tu kwamba Nahju 'l-Balaghah inafuata kwa ubora wake baada ya maneno ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Maneno ya 'Alî ni yenye maana na fikra nzito. Kwa hivyo Nahju 'l-Balaghah lazima isomwe kwa makini, na irejewe na idondolewe na wanafunzi na walimu. Ninapenda kutilia mkazo kwamba Nahju 'l-Balaghah iingizwe kwenye mukhtasar wa masomo na mafundisho (syllabi) ya vyuo vikuu vyote vya Masri na Beirut kwenye masomo ya kiwango cha juu ya lugha na falsafa."

Sheikh Muhammad 'Abdo - Mufti wa Masri na Profesa wa lugha ya Kiarabu na falsafa amesema:

تَحْتَ كَلاَمِ الْخَالِق وَ فَوْقَ كَكَ مِ الْمَخْلُوق

"Mtu yeyote hawezi kukataa kwamba 'Alî alikuwa Imamu wa makhatibu, mwalimu na kiongozi wa waandishi na wanafalsafa. Bila ya shaka khutba zake na maneno yake ni yenye kiwango cha juu kabisa kushinda maneno ya mtu ye yote isipokuwa maneno ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake:"

'Abd-ul-Masîh al-Antaqi - Mhariri wa Kikristo wa gazeti la Ki-masri Al- Ahram amesema:

'Alî alikuwa Imamu kwenye nyanja za vita, Imamu wa siasa, Imamu wa dini, Imamu wa falsafa, Imamu wa maadili, Imamu wa maandiko mbali mbali, na Imamu wa ilmu na hikma."

Profesa Muhammad Kamil, Cairo amesema:

فاِ دَا لَمْ يَكُنْ عَلِيًّّ نَبِيًّا فلَقدْ كَانَ خُلُقُهَ نَبَو تًّا

"Ijapokuwa Imam 'Alî alikuwa si nabii, lakini khulqa yake ilikuwa ya kinabii."

Shaykh Nasif al-Yazidi alipokuwa akimwaidhi mwanawe alimwambia: “Kama unataka mamlaka ya juu kabisa dhidi ya wenzako katika masomo, hikma, maandiko, inshaa n.k. basi hifadhi Qur'ani Tukufu na Nahju 'l- Balaghah”.

Amîn Nakhlah anasema: “Mtu yeyote anayetamani kuikata kiu yake (ya kiroho) kwa maneno ya 'Ali (a.s.) lazima ausome kila ukurasa wa Nahju 'l- Balaghah kwa uangalifu.

Nahju 'l-Balaghah ni diwani ambayo humfanya kila mtu kuukubali ubingwa wa Imam 'Ali (a.s.). Hakuna kitabu kinachoweza kuishinda Nahju 'l- Balaghah isipokuwa Qur'ani Tukufu.

Humo ndani ya Nahju 'l-Balaghah utazikuta lulu za maarifa zilizotungwa kwenye mikufu mizuri, utayakuta maua ya lugha ambayo huifanya akili ya binadamu inukie kwa harufu nzuri ya ushujaa na uungwana; vile vile humo utaikuta mito ya lugha safi ambayo ni mitamu na baridi zaidi kuliko mto wa al-Kauthar.

Imam 'Alî (a.s.) anawaidhi juu ya maudhui mbali mbali, k.m. Kuumbwa kwa ardhi na mbingu, tawhîd, taqwa, malaika, zuhd, Qiyamah, kiburi, tamaa, vita vya Jamal, Siffin, Nahrawan, ibada, maarifa, tamaa, imani, insafu, n. k.

Katika mithali yake mashuhuri Imam 'Alî (a.s.) anatuwaidhi sisi wanaadamu kutobaguwana kwa makabila.

"Watu kwa makamu ni sawa sawa
Baba ni Adamu na mama Hawa
Ukijia'dhimu kwa kuzaliwa
Maji na kinamu uliumbiwa
Fahamu na jua mwana Adamu"

Maneno haya ya Sayyidna 'Alî yamo katika msingi wa Qur'ani Tukufu. (Sh. 'Alî Muhsin al-Barwani).

Tunatumai wasomaji wetu watastafidi sana na tarjama hii ya Nahju 'l-Balaghah (kwa lugha ya Kiswahili) ambayo imefanywa kwa kifundi na ujuzi mkubwa. Mwenyezi Mungu atujaalie tawfiq ya Kutenda Kheri na atuepushe na kila shari.

Wa Billahi Tawfîq,
Dr. Ja'far A. Tijani
May 2007