104 - Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake (a.s) - Mwanzo wa khotuba hii umetangulia katika namba 33.

“Sasa basi! Kwa kweli Allah (swt) alimtuma Muhammad (s.a.w.w.) wakati hapakuwa na yeyote katika waarabu aliyekuwa akisoma kitabu, wala kudai unabii wala wahyi (ufunuo).

Na alimpiga vita aliyemuasi akisaidiwa na wanaomtii, akiwaongoza kwenye uokovu wao, na anawaharakishia saa isije kuwashukia,1 anashindwa mwenye kushindwa, na anasimama aliyevunjika 2 anamsimamia mpaka amfikishe kwenye lengo lake.3

Isipokuwa aliyeangamia asiye na kheri, mpaka alipowaonesha uokovu wao, na aliwakalisha mahali mwao, mambo yao yakaenda sawa, na yalitengenea.
Naapa Mungu, kwa kweli nilikuwa miongoni mwa waswagaji wake 4 - mpaka walirudi nyuma wote, na kujikusanya kwenye kamba yao, sikuonyesha udhaifu au kutokuwa na hima, au kuhini wala sikuonyesha unyonge, namuapa Mungu nitaitumbua batili mpaka niitoe haki kutoka kiunoni mwake!”

Sayyid Ar-Radhiy (r.a) amesema: Yaliyoteuliwa katika khutba hii yametangulia, ila tu mimi nimeikuta katika riwaya hii kukiwa na tofauti na iliyotangulia, kati ya ziada na upungufu, kwa hiyo hali imewajibisha kuithibitisha tena.

  • 1. Anawaharakishia saa: Yaani kana kwamba alikuwa akiogopa wasije wakatanguliwa na saa ya kiyama, kwa hiyo anaharakisha kwa kuwaongoza kabla haijafika, nao wakiwa kati- ka upotovu wao.
  • 2. Alievunjika: Yaani mwenye kudhoofu itikadi yake, au azma yake kuwa butu, na akanyo’ngea mwendo wake katika njia ya waumini, au wasiwasi umejipenyeza na kuivunja miguu ya hima yake, kwa kuitikisa itikadi yake, kwa kweli Nabii (s.a.w.w) alikuwa ana- jishughulisha kumuangalia na kumtibu mpaka aepukane na maradhi yake haya, na aungane na walio wanyoofu, isipokuwa aliyepungukiwa na utayarifu mwenye asili mbaya, dawa kwa huyu haitokuwa na mafanikio, kwa hiyo anahiliki.
  • 3. Mpaka amfikishe kwenye lengo, nalo ni itikadi ya haki, na utulivu wa nafsi kwenye Uislamu. Na hiyo ndiyo maana ya kauli yake ijayo: “wa bawa’ahum mahalatahum.”
  • 4. Mswagaji: Kutokana na neno saaiqu makusudi ni yule anaye liswaga kundi la wanyama kwa mfano mbuzi au ‘ngombe na mradi wake ni: Ujahiliyah aliufanya mfano wa kundi la ng’ombe lililokutana kwa bahati na kundi la uislamu, kwa hiyo yeye akaliandama kulishambulia kwa upanga wake mpaka lilipokimbia na kutokomea.