Sehemu Ya Nne

I. Maoni Ya Uislamu Juu Ya Malezi Ya Mtoto

Watoto ni maua yenye kuchanua katika maisha yetu, ni ahadi ing’aayo katika mustakbali wetu, na ni kiburudisho cha macho yetu. Wao ndiyo wanaodumisha historia adhimu ya mataifa yao. Watoto na vijana wana jukumu kubwa tena la maana la kufanya wakati wa maisha yao. Kwanza, wamekadhibiwa ulinzi wa kuhakikisha kuwa kazi kubwa inafanyika kwa ajili ya nchi zao. Pili, wanatarajiwa kutumia uwezo na ujasiri walionao ili nguvu zao ziweze kufaidisha kuinua hali ya maisha ya mataifa yao.

Na kwa sababu hiyo, ndipo Uislamu ukahimiza sana umuhimu wa malezi ya mtoto. Qur’ani ina maagizo na masharti kwa ajili ya kulinda maisha ya mtoto. Pia kumwongoza na kumpangia utaratibu katika maisha yake. Wakati Uislamu unapopanga utaratibu wa maisha ya mtoto, familia na jamii zinazingatia kwamba pana uhusiano wa ndani baina yao unaoonyesha kwamba mabadiliko au uharibifu wowote ukitokea upande mmoja basi utawadhuru wote.

Kwa hivyo fikra za Uislamu zimempangia Mwislamu njia nzuri ya maisha ambayo msingi wake ni ushirikiano, huruma na imani, ili kutoa mchango wake katika kuwatengezea maisha jamii ya kiislamu. Na ili kufanya hivyo, Uislamu unaanza kwa kumpangia mtu mmoja, kwani yeye ndicho kiungo cha mwanzo katika kuunda maisha ya familia na ya jamii ya watu, na mwishowe taifa zima.

Mtu mmoja ndiye msingi wa kitu cha kwanza, na ndipo asili ya maisha ya taifa zima yanapoanzia. Mtu mmoja ndiye chanzo, naye si mwengine bali ni mtoto ambaye huongozwa na maumbile yake ya kiasili na tabia zake alizojifunza kutoka kwa jamii yake kupitia njia ya kuishi pamoja. Kutangamana na watu wengine ndiko kunakotengeneza tabia ya mtu na kumpangia utaratibu wa heshima za kiutu (zinazothaminiwa katika jamii hiyo).

Iwapo atakuzwa katika njia bora na yenye nidhamu, basi atakuwa ni nguzo ya mafanikio katika maisha ya familia ambayo ni sehemu ndogo tu ya jamii ya watu. Kwa hivyo mafanikio katika familia (ambazo zikiungana pamoja zinaunda jamii), mwishowe yataunda taifa imara na lenye nguvu.

II. Mtoto Baina Ya Silika Na Athari Na Mazoea Ya Mazingira, Na Jukumu La Wazazi

Maendeleo makubwa sana yamepatikana katika elimu ya saikolojia (nafsi) ambayo kwayo wataalamu wa elimu hiyo huweza kumiliki kutengeneza tabia ya mwanaadamu na kuilezea nguvu ya maumbile ya kudumu ambayo inafanya mtu kutenda jambo kwa njia maalum.

Tena, wataalam hao katika utafiti wao, wanachimbua kwa undani zaidi kuhusu nafsi ya mwanaadamu na wamegundua vipengele mbali mbali vya makuzi ya maumbile ya mtoto na tabia zake kiasili. Tena wakazifafanua silika mbali mbali zinazoongoza mwenendo wa mtoto katika kila hatua ya kukua kwake. Pia wameeleza kwa urefu zaidi kuhusu mahitaji ya watoto na jinsi ya kuwatosheleza.

Uislamu umetangulia elimu hiyo katika kupambanua hatua mbali mbali za makamuzi ya mtoto, haki zake, na mahitaji yake. Kazi hii iliyotangulia iliyofanywa na Uislamu inatoa mchango mkubwa katika kuleta ustaarabu wa binaadamu. Kabla hatujaenda mbali zaidi katika kueleza jinsi Uislamu unavyotoa maoni yake kuhusu malezi ya mtoto, hatuna budi kwanza kufafanua mambo muhimu yafuatayo:

Kuna baadhi ya watu wanaounga mkono fikra kwamba mtoto huzaliwa mwema kimaumbile. Hii ina maana kwamba mtoto, kiasili, huzaliwa katika hali ya kuwa mwema ila tu ni ulazimishaji wa mazingira ndio unaogeuza na kuathiri mwenendo wake, na ndio unaoamua iwapo atadumisha mwenendo wake mzuri ama la.

Kwa upande mwingine kuna wengine wanaoshikilia mawazo yanayosisitiza kwamba, mtoto huzaliwa akiwa ni karatasi nyeupe (yaani si mwema wala si mwovu) ila ni kutokana na mazingira (anamoishi) ndipo huanza pole pole kujizoesha kushika mwenendo na tabia za mazaingira hayo. Mtoto huyo hushika tabia tofauti zinazomfanya kuwa ni sehemu ya mazingira yale anayoishi, mwishowe huunda tabia yake.

Basi kwa vyovyote, aidha iwe maoni ya kwanza ama ya pili ndiyo yenye nguvu zaidi, hapana shaka yoyote kwenye njia zote mbili kwamba, yale mazingira anayoishi mtoto yana mchango mkubwa na wa muhimu katika kuunda tabia, mwenendo, na maisha yote.

Miongoni mwa watu wa kwanza katika mvuto wa kitabia wa mtoto, ni wazazi wake. Mtoto huwachukulia wazazi wake kuwa ndiyo kielelezo katika maisha, na ni kwa sababu hii muhimu ndipo wazazi siku zote wanatakiwa wawe mfano bora wa kufuatwa na watoto wao katika jambo walisemalo ama walifanyalo.

Ikiwa ni hivyo, ni dhahiri kwamba maumbile ya kiasili anayozaliwa nayo mtoto na mazingira anayoishi yana athari kubwa katika kumjenga na kumwendeleza awe raia mwema. Kwa sababu hii, ndipo Uislamu kama tulivyoelezwa hapo mwanzo, unamlinda mtoto hata kabla hajazaliwa.

Mwenyezi Mungu amewataka watu kuwaangalia vizuri sana watoto wao. Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: “Wapendeni watoto wenu na muwahurumie, na mtakapowaahidi (kitu) basi watimizieni, kwani wao hawaoni anayewapatia mahitaji yao ila nyinyi.”

Hadithi hiyo iliyotangulia inafafanua mambo matatu yaliyo adhimu kabisa:

1. Upendo: Huu ni dhamana inayokusanya watu pamoja kwenye huruma na ihsani, na hasa kwa wale waliofungamana nasi zaidi kushinda jamaa zetu wote, nao ni kiwiliwili chetu na damu yetu, yaani watoto.

2. Huruma: Hili ni kimbilio kubwa la binaadamu ambalo hukusanya mapenzi na uaminifu katika ukumbi wake. Mambo mawili haya husaidia kuleta yaliyo bora kwa watu.

3. Kutelekeza ahadi: Kufanya hivyo kwa baba juu ya watoto wake kunaonyesha namna upendo wa ndani ulio imara na huruma vinavyoun- ganisha uhusiano wao, na hivyo ndivyo tulivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu. Fikra za mzazi anayemtimizia ahadi mtoto wake baadaye huwa maishani mwake ni moja kati ya kukuza tabia ya kutangamana. Kutangamana kwa wazazi na watoto wao, humpatia mtoto sifa na tabia njema na hutengeneza mwenendo wake. Amesema Mtume (s.a.w.): “Kueni dhamana (mtangamane) na watoto wenu.” Hapa Mtume (s.a.w.) anakusaidia kwamba watoto wasiachiwe bila ya kupatiwa chakula, wasitupwe, au kuachiwa watu wengine (wasiohusika) kuwaangalia, kwani kufanya hivyo kutawafadhaisha na kuwatia hatarini.

III. Mwalimu Aliye Mfano Bora, Na Kumfundisha Mtoto Nid- Hamu

Amesema Utba bin Sufyani wakati alipokuwa akimweleza mwalimu wa mtoto wake: “Mfano kwa mtoto wangu uwe ni mfano wako (vile ufanyavyo), kwani macho yao (watoto) siku zote huwa yanaangalia machoni kwako. Chochote kizuri watakachokiona machoni kwao kitakuwa ndicho kile kizuri ulichokiona wewe, na chochote kiovu watakachokiiga kitakuwa ni kile ulichokionelea.”
Amesema Ibn Khaldun akieleza kuhusu Rashid alipokuwa akimwambia mwalimu wa mtoto wake Al-Amin kwamba: “Kiongozi amekuamrisha kwa furaha ya moyo wake uwe dhamana kwake (mtoto), na umfanye akutii, uwe kama anavyokutaka uwe: Msomeshe Qur’ani, mfundishe elimu na bayana, mfundishe namna ya kuhifadhi na kusoma mashairi, mfafanulie kuhusu elimu ya Hadith za Mtume, muonyeshe namna ya kuanza na kumaliza hotuba, asicheke ila kwa sababu.

Tena usiache hata saa moja ipite bila kutumia nafasi hiyo kwa kumfundisha jambo lenye faida, na usiache kujihusisha na hivyo kumsumbua na kuichosha akili yake. Usimwache awe goigoi, mfundishe adabu kadri ya uwezo wako lakini kwa uaminifu na huruma.”

Wanavyuoni mabingwa wa fikra za kiislamu kama al-Ghazaali, Ibn Khaldun na Ibn Muskawieh, wamesisitiza umuhimu wa malezi mazuri ya mtoto, adabu na mwenendo mzuri. Mtume (s.a.w.) amesema: “Kila mtoto huzaliwa katika maumbile ya kihulka.” Amesema Mwenyezi Mungu: “....ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilowaumba watu…..” (30:30).

Kufunza adabu ni jambo la kwanza linalotakiwa apatiwe mtoto wakati wa utoto ili ajizoeshe kuwa na mwenendo mwema na tabia nzuri. Amesema Mtume (s.a.w.): “Kumfunza adabu mmoja wenu mtoto wake ni bora kwake kuliko kutoa sadaka ya nusu pishi kila siku.”

Tunapowafunza adabu watoto wetu, huwa tunasaidia kuweka msingi imara kwa taifa letu na hivyo ndivyo mafunzo ya Kiislamu yanavyotutaka tutekeleze. Uislamu kwa kufuatilia unatutaka tufanye hivyo na kwa njia kama hiyo na ndio maana ukayapita majaribio yote ya kumfunza adabu mtoto.

Uilsamu umeunganisha malezi mazuri na zawadi ambayo inatunzwa na kupewa wenye kufunza adabu. Kwa maana hiyo, Uislamu umewa- pa moyo wazazi kuwalea vizuri watoto wao. Mtume (s.a.w.) amesema: “Wakirimuni watoto wenu na muwape adabu.”

IV. Uislamu Na Malezi Ya Kujitegemea Kwa Mtoto

Wakati Uislamu ulipowapa wazazi jukumu la kuwalisha watoto wao na kuwaongoza, haukudharau kwa vyovyote vile uwezo alionao mtoto mwenyewe, kwa kufanya hivyo, Uislamu haukusudii kuwafanya wazazi wa mtoto kuyafikiria na kuyapanga maisha yake yote kabisa na wakati huo huo awe akiwategemea wao kabisa.

Hata hivyo, Uislamu umekusudia kuwafanya wazazi wawalinde na kuwaongoza watoto wao wadogo, wasiwapotee njia kwa kuingia mashakani na kwenye dhana.

Uislamu umewaamuru wazazi kuwaongoza na kuwalisha watoto wao tu, bila kujiingiza sana katika shughuli zao. Maoni ya Uislamu kuhusiana na malezi ya mtoto yamefafanuliwa zaidi na Muhammad Rashid Ridha kwa mifano mingi katika tafsir ya Al Manar. Imethibithishwa katika matukio mbali mbali kwamba kujitegemea kwa mtoto ndiyo mwanzo wa kuunda vizazi vyema na watu barabara wa kutegemewa watakaoweza kuchukua jukumu la kujenga taifa.

Imetajwa katika ushauri kwa mzazi ya kwamba: “Cheza na mtoto wako mpaka atakapofikia umri wa miaka saba, kisha mfundishe adabu kwa miaka mingine saba ijayo, kisha uwe suhuba naye kwa miaka mingine saba ijayo, kisha baadaye mwache ajitegemee.”

Ni jambo la muhimu sana kumruhusu mtoto ahudhurie katika majadiliano na kutoa maoni yake, japo maoni yake yatakuwa ni ya kijuujuu tu, na ya kuchekesha, au yasiyohusiana na suala linalozungumziwa hapo, inaweza kuwa pia kumdhihaki si jambo la busara, bali ni vizuri wazazi wawe na bidii ya kumfahamisha pale anapokosea wakati wa kutafakari au kuamua. Anapaswa kutiwa moyo kusema kwa kile hasa anachokifikiria kuwa ni sawa. Kwa kufanya hivyo, bila shaka kutanufaisha mambo yafuatayo:

1. Siku zote hataogopa kutoa maoni yake.

2. Ataweza kujisahihisha na kila alilokosea ama kwa kutofahamu vizuri upande wake, na hilo litamfanya kurekebisha maoni yake na kuchukua uamuzi ufaao.

3. Wakati watu wazima watakapopata shauri (juu ya jambo fulani) atajifunza kutoka kwao uamuzi wa sawa, na jinsi ya kukata shauri katika mambo mbali mbali.

4. Atakuwa anafahamu jinsi ya kujadiliana katika mambo na kuweza kupata suluhisho la matatizo, ili asiachwe hivi hivi tu bila ya kuweza kutatua matatizo.

5. Atakuwa ameandaliwa katika kupambana na mikasa ya kimaisha.

6. Hii pia itamsaidia kutojiamulia tu bila ya kufikiri, na itamfanya atambue matatizo, kwa hivyo, atajua jinsi ya kuyaelezea na kuyatatua yatakapomkabili wakati wa maisha yake na hatofadhaika.

Mfano ni ule uliotokea kwa Abdalla bin Abbas, wakati Mtume (s.a.w.) alipowaambia maswahaba zake: “Mwenyezi Mungu amemfananisha Mwislamu mwenye imani na mti ambao hautupi ovyo majani yake. “Kisha akawauliza: “Je mwajua ni mti gani huo?” Wote wakanyamaa, kisha Mtume (s.a.w.) mwenyewe akajibu: “Huo ni mtende.”

Walipokuwa wakienda nyumbani, Abdallah bin Abbas huku akifuatana na baba yake alimwambia baba yake kuwa alijua jibu la swali alilouliza Mtume (s.a.w.) lakini aliogopa kusema mbele za kadamnasi ya watu, kwani huenda ikawa ni makosa kufanya hivyo. Baba yake akamwambia:

“Lau kama ungelijibu, basi ingekuwa jambo kubwa kwangu kuliko kupata mifugo iliyo bora.”

V. Uislamu Na Kumuelimisha Mtoto

Uislamu unawataka waislamu kutafuta elimu. Kutafuta elimu ni wajibu kwa kila Mwislamu awe ni mwanamume au mwanamke. Haikuamrishwa kwa jinsia moja ya watu au nyingine tu, au kikundi fulani cha watu au kingine, kwani (elimu) inaongoza maisha ya watu. Jamii ya watu iliyoundwa kwa elimu na yenye watu walioelimika, ndiyo jamii iliyo bora kushinda zote, kwa kuwa watu wamepata umashuhuri na ufanisi kwa ajili ya elimu.

Kwa sababu kama hizo, kanuni za Kiislamu zinapigania sana elimu ambayo itaongoza watu (ya mwenye kuelimika), na itastawisha jamii ya watu wote.

Ili kufikia lengo hili, inasemekana kwamba katika vile vita mashuhuri vya Badr, Mtume (s.a.w.) aliamuru kila mateka anayejua kusoma na kuandika, aliyeshikwa katika vita hivi, aachiliwe huru iwapo atawafundisha watoto kumi wa kiislamu jinsi ya kusoma na kuandika. Vile vile Mtume (s.a.w.) amesema: “Wafundisheni watoto wenu kwani, wao wamezaliwa katika zama tofauti na zama zenu.”

Amesema tena: “Tafuteni elimu hata kama ni (kwenda) China.”

Uislamu unaagiza kwamba, waislamu wafanye kila wawezalo kutafuta elimu hata kama itawabidi kusafiri mbali kama China kwa ajili ya kutafuta elimu. Ni dhahiri Uislamu jinsi unavyotetea elimu, hasa tukizingatia kwamba aya yake ya kwanza tu kushuka inazungumzia elimu kama alama ya uongofu. Imetajwa katika Qur’ani:

اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ {1}

خَلَقَ الْإِنْسَانَ مِنْ عَلَقٍ {2}

اقْرَأْ وَرَبُّكَ الْأَكْرَمُ {3}

الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ {4}

عَلَّمَ الْإِنْسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ {5}

“Soma! Kwa jina la Mola wako aliyeumba. Amemuumba mwanaadamu kwa pande la damu. Soma! Na Mola wako ni Mkarimu sana, ambaye amemuelimisha mwanaadamu kwa njia ya kalamu. Amefundisha mwanaadamu mambo aliyokuwa hayajui.” (96:1-5).

Kisha amesema tena:

الرَّحْمَٰنُ {1}

عَلَّمَ الْقُرْآنَ {2}

خَلَقَ الْإِنْسَانَ {3}

عَلَّمَهُ الْبَيَانَ {4}

“(Mwenyezi Mungu) Mwingi wa Rehma; amefundisha Qur’ani, amemuumba mwanadamu, akamfundisha kusema (kwa ufasaha).” (55:1-4).

Elimu katika Uislamu haikuwekewa mipaka ya kusoma kitabu maalum au mtunzi maalum tu, bali inahusisha chochote kile ambacho akili inahitajia kusoma na kuongeza mbinu mbalimbali za maarifa. Amirul-Mu’minin, aliwataka Waislamu kuwafunza watoto wao hata kuogelea, kutupa mishale na kutoa shoti farasi. Kutupa mishale na kupanda farasi ilikuwa ndiyo burudani (kubwa) ya maisha yote ya Waarabu zama hizo, na lau Amirul-Mu’minina angeishi hivi leo, basi angeongezea mengine mengi katika hayo aliyoyasema, (kama kompyuta n.k) ili yaende sambamba na wakati na hali ya mabadiliko ya jamii katika maisha ya kisasa.

VI. Umuhimu Wa Vidude Vya Kuchezea Watoto (Toys) Katika Uislamu

Vijidude vya kuchezea na michezo mbali mbali (toys), vinaleta furaha na burudani katika maisha ya mtoto. Vijidude hivyo pia hupanua akili ya mtoto ya kielimu. Mtume (s.a.w.) amesema: “Mwenye kwenda sokoni, na akanunua kitu cha kuchezea (watoto) akakichukua mpaka kwa watoto wake, huwa ni kama aliyechukua sadaka na kuwapelekea watu wahitaji, basi na aanze kuwapatia watoto wa kike kwanza kabla ya watoto wa kiume.” Umuhimu huu alioupa Mtume (s.a.w.) kuhusiana na vitu vya kuchezea sijambo la kupuuzwa, kwani kufanya hivyo ni muhimu kama kutoa sadaka kwa wahitaji.

Imeelezwa kwamba watoto wa kike wapatiwe kwanza, ili kuwaridhisha na kuwafurahisha. Haya ndiyo mambo ambayo Uislamu unayapigania ambayo lau tutayatafuta, maisha yetu na ya watoto wetu yatajawa na furaha na Baraka.

Nguvu na uzuri wa misingi hii inatoa mfano mzuri kwa jinsi ilivyoamuru kuhusiana na watoto wetu - kiburudisho cha macho yetu. Mtoto mwema huwa ni mwenye kuendeleza ufanisi wa baba yake, na ni hazina nzuri kwa taifa lake. Mtume (s.a.w.) amesema: “Mtoto mwema ni mrihani (mti wenye harufu nzuri) miongoni mwa mirihani ya Peponi.”

Mwenyezi Mungu atuangazie na atuongoze katika kuwalea vizuri watoto wetu ambao ni furaha ya maisha yetu, Amin.