Mkakati Wa 12: Mazungumzo Yasiyo Na Maana

“Na, ifahamike kwamba, hakuna ibada bora zaidi kuliko ukimya” (Mtume s.a.w.w)

Imesimuliwa kwamba: Kimya ni sehemu ya hekima. Ni ishara ya uadilifu. Ndio njia ya wachaji wa Allah (s.w.t.), kwa sababu Allah (s.w.t.) anaupenda (ukimya). Ndio mwenendo wa Mitume (a.s.), na ni tabia ya watu wateuliwa. (As-Sadiq AS)

Kwa mujibu wa Hadithi, viungo vyote vya mwili wako vimesalimika wakati ulimi wako unapokuwa umelindika. Hata hivyo, katika mambo mengi, ukimya unakuwa ni mgumu kuutumia lakini ni wenye manufaa sana mwishoni. Kwa kuendeleza ukimya na kutafakari juu ya kila neno unalolizungumza, itakuwa vigumu sana kwako kujiingiza kwenye dhana, kusengenya, kiburi, dhihaka, uongo, n.k. Namna hii, unakuwa huna mengi ya kufikiria na huna mawazo mengi ya kukuingilia katika Swala zako za kila siku.

Ni lazima ujaribu kuvilinda viungo vyako kutokana na vitendo viovu, kwani vitasababisha ghadhabu za Allah (s.w.t.). Wanavyuoni wamesema: ‘Maongezi ya mtu yanapaswa wakati wote yawe ni katika kumkumbuka Allah (s.w.t.), kimya cha mtu kiwe ni juhudi ya kufikiri na kutafakari, na kutazama kwa mtu lazima kuwe ni kwa ajili ya kujifunza.’

Itaongezea kwenye hasara yako tu kama utajihusisha mwenyewe kwenye mazungumzo ya hovyo hovyo na yasiyo na malengo, kwa vile unaongezea nafasi ya kupoteza mlolongo wa mawazo yako katika Swala.

Unavyozidi kuwa mzembe na ulimi wako, ndivyo utakavyozidi kulazimika kujihami, na Shetani hataipoteza fursa hiyo ya kukukumbusha wewe juu ya kutokuwa sahihi kwako na hisia za hatia wakati wa Swala. Unapaswa kuwa muangalifu juu ya ulimi wako wakati wote na uutumie katika kupata radhi za Mwenyezi Mungu (s.w.t.) tu.

Imam Ali (a.s.), Bwana wa Waumini, wakati mmoja alimkemea mtu mmoja aliyekuwa anapayuka ovyo na akamuonya kwamba: “Ewe mtu! Unamsomea Malaika wako aandike barua kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.), kwa hiyo ongea yale yanayokuhusu wewe na uyawache yale yasiyokuhusu.”

Yule mchaji mwenye tafakari, maarufu wa wakati wetu, at- Tabatabai mashuhuri (r.a.) anahitimisha yafuatayo, baada ya miaka mingi ya juhudi katika utafutaji wake wa kupata ukamilifu wa kiroho:

“Nimeshuhudia athari zenye thamani sana katika ukimya. Kujizoesha ukimya kwa siku arobaini mchana na usiku, kuongea pale tu inapokuwa lazima, na kubaki umezama kwenye kutaamali na madu’a mpaka unapata ufasihi na uongofu.”