Mlango Wa Tano

Itikadi Ya Ahlu Sunna

Mtazamo Wa Mpito Wa Historia:

Kabla Ahmad bin Hanbal hajashika kiti cha enzi ya uimamu katika uwanja wa kiitikadi, masunni walikuwa katika vikundi vingi na mapote yanayohitilafiana. Kati yao akiwemo Marjaiy aonaye kuwa hapana uhusiano kati ya imani na matendo, hivyo basi maasi hayatodhuru kitu pamwe na imani, kama ilivyo utii hautokuwa na manufaa pamwe na kufuru. Na alikuwepo Qadiriya, anayekataa kadari. Na Jahmiy ambaye akataa sifa zote za Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na Kharijiy, na zisizo kuwa hizo miongoni mwa tofauti za kifikra na za kiitikadi. Mpaka alipokuja Ahmad bin Hanbal akaua madhehebu zilizokuwepo kati ya watu wa hadithi, na aliwakusanya katika misingi aliyoichagua yeye, na alijigamba kuwa hiyo ni itikadi ya wema waliotangulia katika sahaba na Tabiina.

Na kwa ukweli na uhakika hasa ni kuwa kuinasibisha misingi hii na itikadi hizi kwa Ahmad ni karibu mno na ni ukweli hasa kuliko kuzinasibisha kwa Sahaba na Tabiina. Kwa sababu hazikuwa maarufu, wala kukubaliwa na wote kabla ya kujitokeza kwa Ibnu Hanbal. Na tofauti za kiitikadi miongoni mwa masunni katika histora yao mpaka hii leo inafichua jambo hili.

Itikadi hizi za kihanbali zilianza kuenea na kusambaa siku za utawala wa Mutawakkil ambaye alimsogeza Hanbal karibu ya Ikulu yake, na kumwekea uwanja wazi mpaka akawa imamu wa itikadi bila ya mpinzani. Na aliendelea katika hali hii mpaka alipojitokeza Abul Hasan al-Ash’ariy katika uwanja wa kiitikadi, baada ya kutubu kwake kutoka itikadi ya Iitizali na kujiunga na itikadi za kihanbali. Lakini yeye hakutosheka na kumfuata Ibnu Hanbal, hivyo aliificha itikadi yake na kujitokeza na itikadi ambazo Ahmad hakuafikiana nazo kikamilifu na wala hakumkhalifu. Pamoja na yote hayo kwa kweli madhehebu yake mapya iliruhusiwa kuenea pande za nchi za kiislamu mpaka alifanikiwa kulivuta busati la uimamu wa kiitikadi kutoka chini ya miguu ya Ahmad bin Hanbal. Hivyo yakawa madhehebu ya Ash’ariya ni madhehebu rasmi ya Ahlu Sunna.

Miqriziy baada ya kuionesha misingi ya itikadi za Imam Ahmad, anasema: “Hii ni jumla ya misingi ya itikadi yake, ambayo hivi sasa ndiyo waliyonayo kundi kubwa la watu wa nchi za kiislamu, ambayo atakayedhihirisha kuwa yuko kinyume nayo damu yake itamwagwa.”1

Kwa sababu hizo moto wa mzozo ukarindima kati ya maashaira na mahanbali muda wote wa zama mbalimbali. Hivyo mahanbali wakawa wanashikamana na riwaya za kumnasibisha Mwenyezi Mungu na kiwiliwili na mwili (Tashbihi na Tajsimi) na walikuwa wanathibitisha sifa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ambazo si jaizi anasibishwe nazo (s.w.t.). Na Ashaira walikuwa wanajiepusha na mambo kama haya. Lakini endapo tutayatupilia mbali matatizo haya tunaweza kuzigawa itikadi za kisunni kwenye kambi mbili ambazo ni: Ashaira na Hanbali, hiyo ni baada ya kutoweka kwa Muutazila. Na katika mlango huu tutachukua mifano kutoka kambi hizi mbili za kiitikadi.

Kambi Ya Kihanbali (Salafiyya)

Ili kuzizungumzia itikadi za Salafiyya hapana budi kuigawa kwenye awamu tatu kihistoria nazo ni:

Awamu ya Ahmad bin Hanbal.
Awamu ya Ibnu Taymiyya.
Awamu ya Muhammad bin Abdil-Wahabi

Kwanza: Ahmad Bin Hanbal Na Utaratibu Wake Katika Itikadi:

Kiini cha itikadi katika utaratibu wa Ibnu Hanbal na mahanbali ni kusikia, yaani kuzitegemea Aya na Hadithi za Nabii (s.a.w.w) katika kuthibitisha itikadi, wala kwa hilo hawaipi dalili ya kiakili na uthibitisho mazingatio makubwa wala hima.

Huu utangulizi wenyewe wahitajia uthibitisho, kwa kuwa haiwezekani kuzingatiwe kusikia kuwe ndiyo mizani na kipimo cha kuijua itikadi peke yake bila ya akili, kwa sababu kusikia hakuwezi kuwa hoja ya lazima ila mtu kwanza akimwamini Mwenyezi Mungu (s.w.t.), kisha akamwamini Mtume wake (s.a.w.w.) na akasadiki maneno yake, kisha akawa na ithibati na utulivu wa moyo kuwa yametoka kwake (s.a.w.w).

Na daraja hizi tatu ikiwa hazikupatikana hauwezi kumlazimisha mtu na umtolee hoja kwa Aya na riwaya. Vinginevyo suala litakuwa ni mjadala mtupu unaozunguka kwenye duru isiyo na mwisho. Na ni miongoni mwa mambo yajulikanayo kiakili kutowezekana kukithibitisha kitu kwa kitu hichohicho, kwa kuwa hivyo italazimu mzunguko wa maneno usiyo na kikomo, na mzunguko usio na kikomo ni batili kulingana na kanuni za kimantiki.

Na huu hapa ni mfano: Kwa kweli kuthibitisha kuwepo kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa Aya za Qur’ani na kuzitolea hoja, kwategemea juu ya kuziamini na kusadiki Aya za Qur’ani. Na kuziamini Aya kwategemea juu ya kumwamini Mwenyezi Mungu (s.w.t.), na kumwamini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwategemea juu ya kuziamini Aya, na ili kuondoa kukariri inakuwa: Kuziamini Aya kunategemea juu ya kuziamini Aya… na hii ni batili.

Kisha tunauliza huu Wahyi umeteremka juu ya nini? Je haukuteremka juu ya mtu? Ikiwa umeteremka juu ya mtu, ni kwa nini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemfanya mtu mahsusi kwa hilo? Si kwa sababu mtu anamiliki ile johari ya thamani nayo ni akili? Jibu likiwa ndio, wapi mahali pa akili katika kipimo hiki?

Na huu ndio mwanzo wa upotovu katika fikra ya kihanbali, kwa kuwa hakuipa akili umuhimu na wala hakuiingiza katika jumla ya utoleaji wake dalili kiitikadi, hali ikiwa sisi tunajua kuwa dalili haitonyooka ila ikiafikiana na akili.

Utata ambao mahanbali wameuingia na wengine miongoni mwa mahashawi na maashaira ni kutotambua kwao ile akili ambayo haiwezi kutambulika kama ilivyo ila kwa njia ya chuo cha Ahlu Bayti (a.s.). Kwa kweli mahanbali na wengine miongoni mwa mahashawi na maashaira wanaitakidi kuwa akili huenda ikaafikiana na sharia na ikahitilafiana nayo, na ilivyo akili haifichui wala haina hoja, na ikiwa akilini mna kadiri fulani ya hoja, basi hiyo itakuwa yaipata kutokana na sharia.

Haikuwa rai hii isio ya wastani ila ni jibu la kivitendo dhidi ya utaratibu wa Muutazila, ambaye anazingatia kuwa hoja ya kiakili ni ya dhati na kuwa dalili ya kusikia isiyoafikiana na akili haina thamani. Na umeshajua kuwa Muutazila waliwachukua watu kwa kiubabe zama za Maamun na al- Muutasim na al-Wathiq ili wakubali njia yao. Hususan Wanahadithi walikabiliwa na aina fulani za adhabu, hivyo ni miongoni mwa mambo yaliyosababisha wawe na msimamo mahsusi kuihusu njia ya kiakili, kama si hivyo basi nini dalili yao ya kuiacha akili na kuganda juu ya maelezo ya dhahiri?!

Na yaliyotokea miongoni mwa mvutano katia ya Muutazila na Mahanbali yalikata baina yao utaratibu wa kufahamiana ili kuzifikia nukta za ushirika. Hivyo kila asili ilihifadhi utaratibu wake na kuupendelea. Na haiwezekani kutanzua kiini cha tatizo hili ambalo juu yake wajengeka ufahamu wa dini na itikadi zake, ila kwa kufichua kipimo thabiti kitakachoafikiwa na wote, ili iwe kigawanyo cha ushirika katika kufikiri na kuamiliana na dini.

Watunzi wawili wananakili, nao ni Hanna al-Fakhuriy na Khalilu al-Hur: “Kuna aina mbili za dalili za kiakili ambazo hazitegemei ila akili na vyanzo vyake. Na dalili ya kusikia ambayo yaitegemea Qur’ani, Hadithi na Ijmai.

Tuonavyo Muutazila hawatambui ila thamani ya ile ya kwanza, na wanazingatia kuwa kila dalili ya kusikia isiyoungwa mkono na akili haikubaliwi. Wanatheolojia wakiongozwa na Ashaira wanatilia mkazo kuwa dalili za kiakili hazina thamani isipokuwa ni kwa sababu sharia inaziamrisha, na kuwa akili yenyewe dhati yake haina thamani isipokuwa pale inapoongezewa sharia.”2

Angalia tofauti kubwa iliyopo katika mitazamo, kundi moja halitambui thamani ya akili na kuwa yenyewe ni hoja, na kundi jingine halitambui thamani ya chochote ila akili.

Na tofauti hii ya njia ndio sababu ya mfarakano wa waislamu na kujigawa katika madhehebu pindi walipohitilafiana katika misingi ya kifikra, hivyo kwa kuhitilafiana njia zimehitilafiana tija. Ikiwa kuna fikra ya kuurudisha umoja wa waislamu hapana budi uanzwe kufanywa umoja wa kanuni za kufikiri na kuimarisha njia za dalili. Kwa mfano: Ziangalie tofauti hizi ambazo zimepatikana kutokana na mgawanyiko wa misingi ya kufikiri. Kwa hiyo katika maudhui ya matendo ya waja, Muutazila wamesema: Kwa hakika mtu ni muumba wa vitendo vyake, vinginevyo itakuwa kinyume na akili. Hiyo kwa mujibu wa dhana zao.

Kwa mujibu huo riwaya zote zilizokuwa kinyume na maana hiyo zilipigwa ukutani. Na katika mtazamo ulio kinyume na huo tunawakuta mahanbali wamefikia tija kuwa vitendo vya mtu huwa si kwa utashi wake, bali ni kwa utashi wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.), hivyo mtu huwa analazimika kutenda matendo yake, walishikilia kuithibitisha rai yao hiyo kwa maana za dhahiri za baadhi ya Aya na Hadith, na wala hawakuipa akili umuhimu wowote.

Ahmad bin Hanbal anasema katika risala yake: “Zinaa, wizi, kunywa pombe, kuuwa nafsi, kula mali ya haramu, kumshirikisha Mwenyezi Mungu, dhambi na maasi, yote hayo huwa kwa maamuzi na makadirio, ni kutoka kwa Allah.”3

Riwaya Zinazoonyesha Kuwa Akili Ni Dharura:

Tukiangalia ukweli wa suala hili tunawakuta wote kati ya Ashaira, Hanbali, na Muutazila hawakuutambua ukweli wa akili, na ili tuutambue ukweli huu hapana budi tuziangalie kwanza kabisa riwaya za Ahlul-Bayt (a.s.), ili tujue umuhimu wa akili na nafasi yake.

Kutoka kwa Abu Ja’far (a.s.) Imam Muhammad al-Baqir (a.s.) alisema: “Allah (s.w.t.) alipoiumba akili aliiambia: Njoo, ikaenda. Kisha aliiambia: Geuza mgongo, ikageuza mgongo. Halafu (s.w.t.) alisema: Naapa kwa nguvu na utukufu wangu sikuumba kiumbe mzuri mno kuliko wewe, kwa ajili ya wewe tu ninaamuru, na kwa ajili ya wewe tu ninakataza, kwa ajili ya wewe tu natoa thawabu na kwa ajili ya wewe tu ninaadhibu.”4

Imekuja katika wosia wa Imam Musa bin Ja’far (a.s.) kwa Hisham bin al- Hakam, katika Hadith ndefu tumependa kuinakili kikamilifu ili kukamilisha faida:

“Ewe Hisham, kwa hakika Allah Tabaraka wa Taala katika Kitabu chake amewabashiria wenye akili na fahamu akasema:

وَالَّذِينَ اجْتَنَبُوا الطَّاغُوتَ أَنْ يَعْبُدُوهَا وَأَنَابُوا إِلَى اللَّهِ لَهُمُ الْبُشْرَىٰ ۚ فَبَشِّرْ عِبَادِ {17}

الَّذِينَ يَسْتَمِعُونَ الْقَوْلَ فَيَتَّبِعُونَ أَحْسَنَهُ ۚ أُولَٰئِكَ الَّذِينَ هَدَاهُمُ اللَّهُ ۖ وَأُولَٰئِكَ هُمْ أُولُو الْأَلْبَابِ {18}

“Basi wabashirie waja wangu; ambao husikiliza maneno, wakafuata lilio bora yao. Hao ndio aliowaongoa Mwenyezi Mungu, na hao ndio wenye akili. (Sura Zumar: 17-18).

“Ewe Hisham! Kwa kweli Allah Tabaraka wa Taala amewakamilishia watu hoja kwa akili na amewanusuru manabii kwa ubainifu, na amewaonyesha umola wake kwa dalili, akasema:

وَإِلَٰهُكُمْ إِلَٰهٌ وَاحِدٌ ۖ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ الرَّحْمَٰنُ الرَّحِيمُ {163}

إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَالْفُلْكِ الَّتِي تَجْرِي فِي الْبَحْرِ بِمَا يَنْفَعُ النَّاسَ وَمَا أَنْزَلَ اللَّهُ مِنَ السَّمَاءِ مِنْ مَاءٍ فَأَحْيَا بِهِ الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا وَبَثَّ فِيهَا مِنْ كُلِّ دَابَّةٍ وَتَصْرِيفِ الرِّيَاحِ وَالسَّحَابِ الْمُسَخَّرِ بَيْنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يَعْقِلُونَ {164}

“Na Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, hapana mungu ila Yeye. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. Hakika katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na kukhitalifiana usiku na mchana, na marekebu ambazo hupita baharini kwa viwafaavyo watu, na maji anayoyateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwa hayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake, na akaeneza humo kila aina ya wanyama; na katika mabadiliko ya pepo, na mawingu yanayoamrishwa kupita baina ya mbingu na ardhi, bila shaka zimo ishara kwa watu wanaozingatia.” (Surat Al-Baqara: 163-164).

“Ewe Hisham, Allah (s.w.t.) ameifanya hiyo kuwa ni dalili ya kumtambua kuwa wao wanaye mwendeshaji, akasema:

وَسَخَّرَ لَكُمُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ ۖ وَالنُّجُومُ مُسَخَّرَاتٌ بِأَمْرِهِ ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يَعْقِلُونَ {12}

“Na amekufanyieni usiku na mchana, jua na mwezi, na amefanya ukutumikieni usiku na mchana, na jua na mwezi, na nyota zikutumikieni kwa amri Yake. Hakika katika hayo zipo ishara kwa watu wenye akili. (Sura Nahlu: 12).

“Na amesema:

هُوَ الَّذِي خَلَقَكُمْ مِنْ تُرَابٍ ثُمَّ مِنْ نُطْفَةٍ ثُمَّ مِنْ عَلَقَةٍ ثُمَّ يُخْرِجُكُمْ طِفْلًا ثُمَّ لِتَبْلُغُوا أَشُدَّكُمْ ثُمَّ لِتَكُونُوا شُيُوخًا ۚ وَمِنْكُمْ مَنْ يُتَوَفَّىٰ مِنْ قَبْلُ ۖ وَلِتَبْلُغُوا أَجَلًا مُسَمًّى وَلَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ {67}

Yeye ndiye ambaye amekuumbeni kwa udongo, kisha kwa tone la manii, na kisha kwa pande la damu, kisha akakutoeni katika hali ya mtoto mchanga, kisha mpate kufikia utu uzima, kisha mpate kuwa wazee. Na kati yenu wapo wanaokufa kabla, na ili mfikie muda uliokwishawekwa, na ili mpate kufahamu. (Sura Ghaafir: 67)

“Na amesema:

وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَمَا أَنْزَلَ اللَّهُ مِنَ السَّمَاءِ مِنْ رِزْقٍ فَأَحْيَا بِهِ الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا وَتَصْرِيفِ الرِّيَاحِ آيَاتٌ لِقَوْمٍ يَعْقِلُونَ {5}

“Na kupishana usiku na mchana, na riziki anayoiteremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwayo akaifufua ardhi baada ya kufa kwake, na mabadiliko ya upepo, ni ishara kwa watu wenye akili.” (Surat Al-Jathiya: 5)

“Na amesema:

اعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ يُحْيِي الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا ۚ قَدْ بَيَّنَّا لَكُمُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ {17}

“Jueni kwamba Mwenyezi Mungu huifufua ardhi baada ya kufa kwake. Na tumekubainishieni ishara ili mpate kuzingatia. (Surat al- Hadid: 17)

“Na amesema:

وَفِي الْأَرْضِ قِطَعٌ مُتَجَاوِرَاتٌ وَجَنَّاتٌ مِنْ أَعْنَابٍ وَزَرْعٌ وَنَخِيلٌ صِنْوَانٌ وَغَيْرُ صِنْوَانٍ يُسْقَىٰ بِمَاءٍ وَاحِدٍ وَنُفَضِّلُ بَعْضَهَا عَلَىٰ بَعْضٍ فِي الْأُكُلِ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يَعْقِلُونَ {4}

“Na katika ardhi vimo vipande vilivyo karibiana, na zipo bustani za mizabibu, na mimea mingine, na mitende yenye kuchipua kwenye shina moja na isiyochupua kwenye shina moja, nayo inatiliwa maji yale yale. Na tunaifanya baadhi yao bora kuliko mingine katika kula. Hakika katika hayo zimo ishara kwa watu wanaotia mambo akilini. ‘’ (Surat ar-Raad: 4)

“Na amesema:

وَمِنْ آيَاتِهِ يُرِيكُمُ الْبَرْقَ خَوْفًا وَطَمَعًا وَيُنَزِّلُ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَيُحْيِي بِهِ الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يَعْقِلُونَ {24}

“Na katika ishara zake hukuonyosheni umeme kwa kukutieni khofu na tamaa. Na hukuteremshieni maji kutoka mbinguni, na kwa hayo huifufua ardhi baada ya kufa kwake. Hakika katika hayo zipo ishara kwa watu wanaozingatia.” (Sura Rum: 24)

“Na amesema tena:

قُلْ تَعَالَوْا أَتْلُ مَا حَرَّمَ رَبُّكُمْ عَلَيْكُمْ ۖ أَلَّا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۖ وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُمْ مِنْ إِمْلَاقٍ ۖ نَحْنُ نَرْزُقُكُمْ وَإِيَّاهُمْ ۖ وَلَا تَقْرَبُوا الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ ۖ وَلَا تَقْتُلُوا النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلَّا بِالْحَقِّ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُمْ بِهِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ {151}

“Sema: Njooni nikusomeeni aliyokuharamishieni Mola wenu Mlezi. Nayo ni kuwa, msimshirikishe Yeye na chochote. Na wazazi wenu wafanyieni wema. Wala msiwauwe watoto wenu kwa sababu ya umasikini. Sisi tunakuruzukuni nyinyi na wao. Wala msikaribie mambo machafu, yanayoonekana, na yanayofichikana. Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharamisha kuiuwa, ila ikiwa kwa haki. Hayo amekuusieni ili myatie akilini.” (Surat al-An’aam:151)

“Na amesema:

ضَرَبَ لَكُمْ مَثَلًا مِنْ أَنْفُسِكُمْ ۖ هَلْ لَكُمْ مِنْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ مِنْ شُرَكَاءَ فِي مَا رَزَقْنَاكُمْ فَأَنْتُمْ فِيهِ سَوَاءٌ تَخَافُونَهُمْ كَخِيفَتِكُمْ أَنْفُسَكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْقِلُونَ {28}

“Amekupigieni mfano kutokana na nafsi zenu. Je! Katika hao iliyowamiliki mikono yenu ya kulia mnaowashirika katika hivyo tulivyokuruzukuni, mkawa nyinyi katika hivyo ni sawasawa, mnawaogopa kama mnavyoogopana wenyewe kwa wenyewe? Namna hivi tunazipambanua Aya zetu kwa watu wenye akili. (Sura Rum: 28)

“Ewe Hisham, halafu aliwawaidhi wenye akili na kuwafanya waipende akhera akasema:

وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا لَعِبٌ وَلَهْوٌ ۖ وَلَلدَّارُ الْآخِرَةُ خَيْرٌ لِلَّذِينَ يَتَّقُونَ ۗ أَفَلَا تَعْقِلُونَ {32}

“Na maisha ya dunia si chochote ila ni mchezo na pumbao tu. Na hakika nyumba ya Akhera ni bora zaidi kwa wanaomcha Mungu. Basi, je hamtii akilini.” (Surat Al-An’a’am: 32)

“Ewe Hisham, halafu aliwahofisha ambao hawatumii vyema akili wajiepushe na adhabu yake, amesema (s.w.t.):

ثُمَّ دَمَّرْنَا الْآخَرِينَ {136}

وَإِنَّكُمْ لَتَمُرُّونَ عَلَيْهِمْ مُصْبِحِينَ {137}

وَبِاللَّيْلِ ۗ أَفَلَا تَعْقِلُونَ {138}

“Kisha tukawaangamiza wale wengineo. Na hakika nyinyi mnawapitia wakati wa asubuhi. Na usiku. Basi je! Hamyatii akilini? “(Surat As-Safati: 136-138)

“Na amesema:

إِنَّا مُنْزِلُونَ عَلَىٰ أَهْلِ هَٰذِهِ الْقَرْيَةِ رِجْزًا مِنَ السَّمَاءِ بِمَا كَانُوا يَفْسُقُونَ {34}

وَلَقَدْ تَرَكْنَا مِنْهَا آيَةً بَيِّنَةً لِقَوْمٍ يَعْقِلُونَ {35}

“Kwa yakini sisi tutawateremshia watu wa mji huu adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya uchafu wanaoufanya. Na tumeacha katika mji huo ishara iliyo wazi kwa watu wanaotumia akili zao.” (Surat Ankabuti: 34-35).

“Ewe Hisham, kwa hakika akili iko pamwe na elimu, akasema:

وَتِلْكَ الْأَمْثَالُ نَضْرِبُهَا لِلنَّاسِ ۖ وَمَا يَعْقِلُهَا إِلَّا الْعَالِمُونَ {43}

“Na hiyo ni mifano tunawapigia watu na hawaifahamu ila wenye ilimu.” (Surat Ankabuti: 43)

“Ewe Hisham, halafu aliwalaumu wasioitumia akili vyema, akasema:

وَإِذَا قِيلَ لَهُمُ اتَّبِعُوا مَا أَنْزَلَ اللَّهُ قَالُوا بَلْ نَتَّبِعُ مَا أَلْفَيْنَا عَلَيْهِ آبَاءَنَا ۗ أَوَلَوْ كَانَ آبَاؤُهُمْ لَا يَعْقِلُونَ شَيْئًا وَلَا يَهْتَدُونَ {170}

Wanapoambiwa: Fuateni aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, wao husema: Bali tutafuata tuliyowakuta nayo baba zetu. Je, hata ikiwa baba zao walikuwa hawaeliwi kitu, wala hawakuongoka!” (Surat Al-Baqara: 170)

“Na akasema:

وَمَثَلُ الَّذِينَ كَفَرُوا كَمَثَلِ الَّذِي يَنْعِقُ بِمَا لَا يَسْمَعُ إِلَّا دُعَاءً وَنِدَاءً ۚ صُمٌّ بُكْمٌ عُمْيٌ فَهُمْ لَا يَعْقِلُونَ {171}

“Na mfano wa walio kufuru ni kama mfano wa anayempigia kelele asiye sikia ila wito na sauti tu, ni viziwi, mabubu, vipofu, kwa hivyo hawatii kitu akilini.” (Surat Al-Baqara: 171).

“Na amesema:

وَمِنْهُمْ مَنْ يَسْتَمِعُونَ إِلَيْكَ ۚ أَفَأَنْتَ تُسْمِعُ الصُّمَّ وَلَوْ كَانُوا لَا يَعْقِلُونَ {42}

“Na wapo miongoni mwao wanaokusikiliza. Je, wewe unaweza kuwafanya viziwi wasikie ijapokuwa hawafahamu?” (Sura Yunus: 42)

“Na amesema:

أَمْ تَحْسَبُ أَنَّ أَكْثَرَهُمْ يَسْمَعُونَ أَوْ يَعْقِلُونَ ۚ إِنْ هُمْ إِلَّا كَالْأَنْعَامِ ۖ بَلْ هُمْ أَضَلُّ سَبِيلًا {44}

“Au wewe wadhani kwamba wengi wao wanasikia au wanaelewa? Hao hawakuwa ila ni kama nyama hoa tu, bali wao wamepotea zaidi njia.” (Sura Furqan: 44)

“Na akasema:

لَا يُقَاتِلُونَكُمْ جَمِيعًا إِلَّا فِي قُرًى مُحَصَّنَةٍ أَوْ مِنْ وَرَاءِ جُدُرٍ ۚ بَأْسُهُمْ بَيْنَهُمْ شَدِيدٌ ۚ تَحْسَبُهُمْ جَمِيعًا وَقُلُوبُهُمْ شَتَّىٰ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَا يَعْقِلُونَ {14}

“Hawatapigana nanyi kwa mkusanyiko isipokuwa katika vijiji vilivyozatitiwa kwa ngome, au nyuma ya kuta. Wao kwa wao vita vyao ni vikali. Utawadhania kuwa wako pamoja, kumbe nyoyo zao ni mbalimbali. Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasio na akili.” (Surat al- Hashr: 14)

“Na amesema:

أَتَأْمُرُونَ النَّاسَ بِالْبِرِّ وَتَنْسَوْنَ أَنْفُسَكُمْ وَأَنْتُمْ تَتْلُونَ الْكِتَابَ ۚ أَفَلَا تَعْقِلُونَ {44}

“Na mnajisahau nafsi zenu, na hali nyinyi mnasoma Kitabu? Basi je, hamzingatii.
(Surat al-Baqara: 44)

“Ewe Hisham, halafu Mwenyezi Mungu ameulaumu wingi akasema:

وَإِنْ تُطِعْ أَكْثَرَ مَنْ فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ ۚ إِنْ يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ هُمْ إِلَّا يَخْرُصُونَ {116}

“Na ukiwatii wengi katika hawa waliomo duniani watakupoteza na njia ya Mwenyezi Mungu. (Surat Al-An’aam: 116)

“Na amesema:

وَلَئِنْ سَأَلْتَهُمْ مَنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ لَيَقُولُنَّ اللَّهُ ۚ قُلِ الْحَمْدُ لِلَّهِ ۚ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ {25}

“Na ukiwauliza: Nani aliyeziumba mbingu na ardhi? Bila shaka watasema: Mwenyezi Mungu. Wewe sema: Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui.” (Sura Luqman: 25)

“Na amesema

وَلَئِنْ سَأَلْتَهُمْ مَنْ نَزَّلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَحْيَا بِهِ الْأَرْضَ مِنْ بَعْدِ مَوْتِهَا لَيَقُولُنَّ اللَّهُ ۚ قُلِ الْحَمْدُ لِلَّهِ ۚ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْقِلُونَ {63}

-“Na ukiwauliza: Ni nani anayeteremsha maji kutoka mbinguni, na akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake? Bila ya shaka watasema: Ni Mwenyezi Mungu. Sema: Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Bali wengi katika wao hawafahamu.”(Surat Ankabuti: 63)

“Ewe Hisham, halafu aliusifu uchache kwa uzuri, akasema: “Ni wachache katika waja wangu wanaoshukuru.” (Sura Saba’a: 13)
“Na akasema: “Na hao ni wachache.” (Sura Swad: 24)

“Na amesema:

وَقَالَ رَجُلٌ مُؤْمِنٌ مِنْ آلِ فِرْعَوْنَ يَكْتُمُ إِيمَانَهُ أَتَقْتُلُونَ رَجُلًا أَنْ يَقُولَ رَبِّيَ اللَّهُ {28}

“Na akasema mtu mmoja muumini, aliyekuwa mmoja katika watu wa Firaun aliyeficha imani yake: Mtamuuwa mtu kwa sababu anasema Mola wangu Mlezi ni Mwenyezi Mungu?”
(Sura Ghaafir: 28)

“Na amesema:

وَمَنْ آمَنَ ۚ وَمَا آمَنَ مَعَهُ إِلَّا قَلِيلٌ {40}

“Na watu walioamini. Na hawakuamini pamoja naye ila wachache tu. (Sura Hud: 40)

Na amesema: “Lakini wengi wao hawajui.”
Na amesema: Weng wao hawatumii akili.”
Na amesema: Wengi wao hawatambui.”

“Ewe Hisham, halafu aliwataja wenye akili kwa utajo mwema na aliwapamba kwa pambo zuri, amesema:

يُؤْتِي الْحِكْمَةَ مَنْ يَشَاءُ ۚ وَمَنْ يُؤْتَ الْحِكْمَةَ فَقَدْ أُوتِيَ خَيْرًا كَثِيرًا ۗ وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ {269}

Yeye humpa hikima amtakaye, na aliyepewa hikima bila ya shaka amepewa kheri nyingi. Na hawakumbuki ila wenye akili.” (Surat Al- Baqara: 269)

“Na amesema:

وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ يَقُولُونَ آمَنَّا بِهِ كُلٌّ مِنْ عِنْدِ رَبِّنَا ۗ وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ {7}

“Na wale wenye msingi madhubuti katika elimu husema: Sisi tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu Mlezi. Lakini hawakumbuki hayo isipokuwa wenye akili.”
(
Surat Ali Imran: 7)

“Na amesema:

إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِأُولِي الْأَلْبَابِ {190}

“Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitilafiana usiku na mchana ziko ishara kwa wenye akili.” (Surat Ali Imran: 190).

“Na amesema:

أَفَمَنْ يَعْلَمُ أَنَّمَا أُنْزِلَ إِلَيْكَ مِنْ رَبِّكَ الْحَقُّ كَمَنْ هُوَ أَعْمَىٰ ۚ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ {19}

“Je anayejua ya kwamba yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako Mlezi ni haki tu, ni sawa na aliye kipofu? Wenye akili ndio wanaozingatia.” (Sura Ra’ad: 19)

“Na amesema:

أَمَّنْ هُوَ قَانِتٌ آنَاءَ اللَّيْلِ سَاجِدًا وَقَائِمًا يَحْذَرُ الْآخِرَةَ وَيَرْجُو رَحْمَةَ رَبِّهِ ۗ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ ۗ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ {9}

“Je afanyaye ibada nyakati za usiku kwa kusujudu na kusimama akitahadhari na Akhera, na akitaraji rehema za Mola wake Mlezi. Sema: Ati watakuwa sawa wale wanaojua na wale wasiojua? Hakika wanaokumbuka ni watu wenye akili. (Sura Zumar: 9).

“Na amesema:

كِتَابٌ أَنْزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُولُو الْأَلْبَابِ {29}

“Na hiki Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili.” (Sura Swad: 29)

“Na amesema:

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْهُدَىٰ وَأَوْرَثْنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ الْكِتَابَ {53}

هُدًى وَذِكْرَىٰ لِأُولِي الْأَلْبَابِ {54}

“Na kwa hakika tulimpa Musa uongofu, na tukawarithisha wana wa Israili Kitabu. Ambacho ni uwongofu na ukumbusho kwa wenye akili.” (Sura Ghaafir: 53-54)

“Na amesema:

وَذَكِّرْ فَإِنَّ الذِّكْرَىٰ تَنْفَعُ الْمُؤْمِنِينَ {55}

Na kumbusha, kwani ukumbusho huwafaa Waumini.” (Sura Dhariyat: 55)

“Ewe Hisham, kwa kweli Mwenyezi Mungu anasema katika Kitabu chake:

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِمَنْ كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ {37}

“Hakika katika hayo upo ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye yupo anashuhudia. (Sura Qaf: 37).

“Na amesema: “Kwa hakika tumempa Luqman hekima.(Sura Luqman: 12) yaani fahamu na akili.

“Ewe Hisham, kwa kweli Luqman alimwambia mwanawe: ‘Uinyenyekee haki utakuwa mwenye akili mno miongoni mwa watu, kwa kuwa ufahamu kwa mkweli ni rahisi. Ewe mwanangu kwa hakika dunia ni bahari ya kina kirefu, umezama ndani yake ulimwengu mwingi, hivyo na iwe merikebu yako katika dunia ni kumcha Mungu na shehena yake ni imani, tanga yake ni tawakuli, nguzo yake ni akili, dalili yake ni elimu, wakazi wake ni uvumilivu.’

“Ewe Hisham, kila kitu kina dalili, na dalili ya akili ni kufikiri, na dalili ya kufikiri ni kunyamaza. Na kila kitu kina kipando na kipando cha akili ni unyenyekevu. Ni ujinga tosha kwako kupanda ulichokatazwa.

“Ewe Hisham, Mwenyezi Mungu hajatuma manabii na mitume wake kwa waja wake ila watumikishe akili kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hivyo aliye mzuri mno kuitika miongoni mwao ni aliye mzuri mno wa maarifa, na mjuzi mno wa amri ya Mwenyezi Mungu ni mzuri mno wa akili, na mkamilifu mno wa akili ni mwenye daraja ya juu duniani na akhera.

“Ewe Hisham, kwa hakika Mwenyezi Mungu ana aina mbili za hoja juu ya watu: Hoja iliyo dhahiri na hoja iliyo batini. Ama hoja iliyo dhahiri ni mitume na manabii na maimamu (a.s.). Ama ya batini ni akili.

“Ewe Hisham, kwa hakika mwenye akili ni yule ambaye halali haimshughulishi dhidi ya kuishukuru, wala haramu haimzuilii kuvuta subira.

“Ewe Hisham, mwenye kuvipa nguvu vitatu juu ya vitatu ni kana kwamba ameusaidia utashi mbaya wa nafsi kuiharibu akili yake: Mwenye kuitia giza nuru ya kufikiri kwake kwa urefu wa matumaini yake, na akafuta hekima yake inayokubalika kwa maneno yake yasiyo ya lazima, na akafuta nuru ya zingatio lake kwa matamanio ya nafsi yake, ni kama kwamba ameusaidia utashi mbaya wa nafsi yake kuiharibu akili yake, na mwenye kuiharibu akili yake atakuwa ameharibu dini yake na dunia yake.

“Ewe Hisham, vipi itatakasika amali yako mbele ya Allah (s.w.t.) na wewe umeushughulisha moyo wako mbali na amri ya Mola wako, na umeutii utashi mbaya wa nafsi yako kuzishinda nguvu akili zako.

“Ewe Hisham, kuvuta subira katika hali ya upweke ni alama ya nguvu ya akili, mwenye kuwa na akili kutoka kwa Mwenyezi Mungu hujitenga mbali na wafuasi wa dunia na wenye kuipenda, na hupenda kilichokuwa kwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu huwa ndio mliwazaji wake awapo katika upweke, na atamtajirisha awapo katika umasikini, na atampa heshima bila ya ndugu.

“Ewe Hisham, isimamishe haki ili kumtii Mwenyezi Mungu wala hapana wokovu ila kwa utii, na utii huwa kwa elimu na elimu huwa kwa kujielimisha na kujielimisha huwa kwa akili na wala haipatikani elimu ila kwa mwanachuoni wa kiungu, na elimu huambuliwa kwa akili.
“Ewe Hisham, amali chache ya mwanachuoni yakubaliwa na ni yenye kuongezwa, na amali nyingi ya wenye utashi mbaya wa nafsi na majahili hukataliwa.

“Ewe Hisham, kwa kweli mwenye akili huridhika na kidogo cha dunia hii pamwe na hekima, wala haridhiki na hekima ndogo pamwe na dunia, kwa ajili hiyo imekuwa na faida biashara yao.

“Ewe Hisham, kwa kweli wenye akili wameacha ziada ya dunia, hivyo itakuwaje dhambi, na kuiacha dunia ni katika fadhila na kuiacha dhambi ni katika faradhi.

“Ewe Hisham, kwa kweli mwenye akili ameiangalia dunia na watu wake akajua kuwa haipatikani ila kwa misukosuko, na ameiangalia akhera akajua kuwa haipatikani ila kwa misukosuko, hivyo akaitafuta kwa mashaka ile yenye kubaki mno.

“Ewe Hisham, kwa kweli wenye akili wameikataa dunia na wameipenda akhera, kwa sababu wao wamejua kuwa dunia inataka na inatakiwa, na akhera inataka na inatakiwa. Hivyo basi mwenye kuitaka akhera, dunia itamtaka mpaka achukue kikamilifu riziki yake kutoka humo, na mwenye kuitaka dunia akhera itamtaka kwa umauti kumjia na wamharibia dunia yake na akhera yake.

“Ewe Hisham, mwenye kuutaka utajiri bila mali, na raha ya moyo bila ya husuda na usalama katika dini: Amnyenyekee Allah katika kumuomba amkamilishie akili yake, kwani mwenye kuitumia akili hukinai na kile kinachomtosha, na mwenye kukinai na kile kimtoshacho hutosheka, na ambaye hakinai na kinachomtosha hatoufikia utajiri abadan.

“Ewe Hisham, hakika Mwenyezi Mungu ameelezea kuhusu kaumu ya watu wema kuwa wakasema: “Mola wetu Mlezi! Usizipotoe nyoyo zetu baada ya kwishatuongoa, na na utupe rehema itokayo kwako.” (Surat Ali Imran: 8), pindi tu walipojua kuwa nyoyo hupotoka na hurejelea kwenye upofu wake na uangamivu wake.

“Hajamuogopa Mwenyezi Mungu asiyefanya kwa mujibu wa akili kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na asiyezingatia kwa akili kutoka kwa Mwenyezi Mungu, moyo wake haufungamani na maarifa thabiti kwa uoni wake, na kuupata ukweli wake moyoni mwake, mtu hawi hivyo ila mwenye kuwa kauli yake inasadikishwa na kitendo chake, na siri yake inaafikiana na uwazi wake. Kwa sababu Mwenyezi Mungu, jina lake limebarikiwa, hajaionesha batini iliyojificha mbali na akili ila kwa dhahiri itamkayo kutokana nayo.

“Ewe Hisham, Amiirul-Mu’minin, amani iwe juu yake, alikuwa anasema: ‘Mwenyezi Mungu hajaabudiwa na kitu bora kuliko akili. Na akili ya mtu haitimii mpaka awe na mambo mbalimbali: Amesalimika na kufuru na ushirikina. Uongofu na kheri vyatazamiwa kwake. Ziada katika mali yake ni yenye kutumika, na ziada ya kauli yake imedhibitiwa. Hisa yake hapa duniani ni chakula. Dahri huwa hashibi elimu, udhalili pamwe na Mwenyezi Mungu wampendeza mno kuliko utukufu pamwe na mwingine, na unyenyekevu aupenda mno kuliko utukufu, hukithirisha wema kidogo kutoka kwa mtu mwingine na huudogesha wema mwingi kutokana na yeye binafsi, na watu wote huwaona bora kuliko yeye, na kuwa yeye ni shari kwao nafsini mwake, nalo ni jambo kamili.’

“Ewe Hisham, kwa hakika mwenye akili hasemi uwongo japo iwe humo – katika kusema uwongo - kuna utashi wa nafsi yake.

“Ewe Hisham, asiye na murua hana dini, wala hana murua asiye na akili, kwa kweli mwenye thamani zaidi katika watu ni mtu asiyeiona dunia kuwa ni hatari kwake. Ama miili yenu haina thamani ila Janna, hivyo msiiuze na kitu kingine.

“Ewe Hisham, kwa hakika Amirul-Mu’minin, amani iwe juu yake, alikuwa anasema: ‘Kwa kweli alama za mwenye akili ni awe na sifa tatu: Hujibu aulizwapo, na hutamka inaposhindwa kaumu kuongea, na huelekeza rai yenye maslahi kwa wahusika nayo, hivyo basi asiyekuwa na chochote katika sifa hizi tatu ni mpumbavu.’

Kwa kweli Amirul-Mu’minin amani iwe juu yake, amesema: ‘Mtu asiketi katikati ya kikao ila mtu mwenye sifa hizi tatu au moja kati ya hizi, hivyo asiye kuwa na sifa yoyote katika hizo na akaketi huyo ni pumbavu.

“Amesema Hasan bin Ali amani iwe juu yake: ‘Muzitakapo haja zitakeni kwa wenye kustahiki.’ Ilisemwa ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu wanaostahiki ni nani? Alisema: ‘Ambao Mwenyezi Mungu amezieleza katika Kitabu chake sifa zao, amesema (s.w.t.): “Hakika wanaokumbuka ni watu wenye akili. (Sura Zumar: 9).’ Alisema: Wao ni wenye akili.

“Na Ali bin Husein (a.s.) akasema: ‘Kukaa na watu wema ni kichocheo cha mtu kuwa mwema. Na kuwatendea adabu wanavyuoni ni sababu ya kuzidi akili, na kuwatii watawala waadilifu ni ukamilifu wa utukufu, na kuzalisha mali ni ukamilifu wa murua, na kumuongoza autakaye ushauri ni kutekeleza haki ya neema, na kuzuia maudhi ni ukamilifu wa akili, na ndanimwe mna raha ya kimwili, ya sasa na ya baadae.’

“Ewe Hisham, kwa kweli mwenye akili hamsemeshi amhofiaye kumkadhibisha, wala hamuombi amuhofiaye kumnyima, wala haahidi asiloliweza, wala hatarajii atakalotendewa kikatili kwa kule kulitarajia, wala hafanyi alihofialo kumfutu kwa kushindwa.”5

Na kuna mamia ya riwaya ambazo zinaweka wazi umuhimu wa akili na nafasi yake katika chuo cha Ahlul-Bayt (a.s.). Na akili ni ile nuru ya kiungu ambayo kwayo mtu huufichua ukweli wa vitu, nayo kwa mujibu huo ni hiba ya kiungu, na wala sio jambo la dhati ndani ya mwanadamu, pamoja nalo anageuka kutoka hali ya kuwa nguvu tu na kuwa kitendo, kama ambavyo wanafalsafa walivyoamini, ambao wameitambulisha akili kuwa ni: Nguvu ile ambayo kwayo mwanadamu anakuwa na uwezo wa kuiopoa nadharia kutoka katika dharuriyati, kama muhali wa kukutana naqidhu mbili, na kuwa kila kibadilikacho ni cha kutukia.

Na pindi itolewapo nadharia kutotoka kwenye dharuriyati hizi, mtu huwa amefikia ukomo wa akili. Nayo ni daraja miongoni mwa daraja za nafsi, ikamilikapo huwa ndio akili. Hivyo tija zaitwa vizingatiwavyo, baada ya kuifikisha kwenye dharuriyati japo iwe kwa hatua ishirini.

Kwa mantiki hiyo wakachanganya kati ya akili na vizingatiwavyo, na kati ya kujua na kijulikanacho, hivyo wakajishughulisha na kijulikanacho na kizingatiwacho, wakapotea mbali na nuru ambayo kwayo walijua na walizingatia vitu, na huu ndio upotovu wa mbali, kwa sababu sisi tunaona wenyewe kuwa nuru hii ambayo kwayo tunautambua uhakika wa vitu iko nje ya dhati yetu na iko nje ya dhati ya vitu vizingatiwavyo. Hivyo hiyo ni hiba ya kiungu kwayo tunajitambua binafsi na kwayo tunafichua hakika ya vitu. Kama si hivyo huwa wapi akili hii katika hali ya utoto! Na ni wazi kuwa lau ingekuwa ni dhati basi dhati huwa haiatuki.

Amesema (s.w.t.): “Mwenyezi Mungu amekutoeni kutoka tumboni mwa mama zenu mkiwa hamjui kitu.” (Sura Nahl: 78). Na Aya hii haiachi kuwa ni tanabahisho la ukweli wa akili na elimu, kuwa wao ni nuru mbili zinazofichua ambazo hakuwa yoyote miongoni mwetu anazimiliki alipotolewa tumboni mwa mama yake. Halafu hivi sasa anazimiliki. Hivyo basi hapana budi itambuliwe kuwa hizo ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.). Kwa kuwa lau zingekuwa zatokana na yeye mwenyewe (binadamu) basi angekuwa nazo tokea utotoni.

Anasema (s.a.w.w.) akitilia nguvu ukweli huu: “Mtoto akifikia kiwango cha mtu mwanamume mtu mzima au kiwango cha mwanamke mtu mzima, huondolewa ile sitara, hivyo huingia katika moyo wa mtu huyu nuru, hivyo huwa anaielewa faradhi na Sunna, zuri na baya, tambua mfano wa akili moyoni ni mfano wa taa ndani ya nyumba.”

Hivyo basi akili ni nuru ya kiungu imehifadhiwa mbali na makosa, na wahyi pia ni nuru ya kiungu umehifadhiwa mbali na makosa, hapana tofauti kati ya wawili hawa.
Wao ni nuru mbili kutoka kwenye fanusi moja, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amejaalia nuru ya kwanza katika mwanadamu, na amejaalia nuru ya pili katika Qur’ani na Hadithi, na kila moja anamkamilisha mwingine na kumsadikisha.

Na unakuwa uhusiano kati ya akili na wahyi ni uhusiano wa kung’arisha. Kama alivyosema Amirul-Mu’minin (a.s.) akielezea umuhimu wa manabii: “Ili waitimue akili iliyozikwa.” Hivyo basi hakuna mwanya kati ya akili na wahyi kulingana na msingi wa kiakili wa Qur’ani uliopo juu ya asili ya ukumbusho. Nayo ni akili iliyo salama ambayo inatakasika na kukuwa na kutilia nguvu na kuwekwa sawa na wahyi wa kiungu. Kwa hilo huwa kipimo salama cha kufichua maarifa ya dini ni akili inayoona kwa uoni wa wahyi.

Na ukweli huu uliojificha ulikuwa ndio sababu ya waislamu kutofautiana na kugawanyika kwao kimadhehebu. Wanahadithi wameganda juu ya dhahiri ya tamko, na Mu’utazila wametegemea tafsiri ya neno mbali na maana ya dhahiri ya tamko. Na Ashaira walijaribu kukusanya kati ya tafsiri na kuganda juu ya matamko. Na wanafalsafa wamejipasulia njia yao iliyo tofauti na njia ya Mwenyezi Mungu na wamejidai kuufikia ukweli kupitia nguvu ya kibinadamu. Na wote hao hawakuupata ukweli.

Na kwa kuwa mazungumzo yetu hivi sasa ni kuwahusu mahanbali, hivyo kuikataa kwao akili na kutoitendea kazi hakuna sababu. Na ambaye ataangalia vitabu vya mahanbali atazikuta itikadi zile zinazopingana zenyewe kwa zenyewe, au zinazopingana na akili ya mwanadamu na umbile lake.

Hivyo basi wao wanaziamini riwaya ambazo zinathibitisha maumbile na mfanano kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.), hivyo utaziona itikadi zao hazitofautiani sana na itikadi za kiyahudi, kinaswara na kimajusi. Kwa ajili hiyo kati yao kumejitokeza madhehebu ya Mungu kuwa na maumbile, Mungu kufanana na kitu, Kumwona Mungu na Kutenzwa nguvu na Mungu, na nyingine miongoni mwa itikadi za Ahlul- kitabi.

Na hayo yote yanarejea kwenye utendeaji kazi Hadithi, usio makini na Hadithi, ambazo hawakufuatilia kwa undani maana zinazozijulisha au hawakuangalia sanad zake, na bila ya kuzimulika na mwaga wa Qur’ani na akili, lakini wameziamini tu moja kwa moja.

“Hivyo kufuata tu kumewafikisha katika upeo ambao wamekuwa wanachukua dhahiri za kila yaliyoelezwa na msimulizi miongoni mwa habari na athari zilizokatwa, zisizo na nyororo ya wasimulizi wake, zilizozushwa na kuwekwa na zilizotengenezwa.

Japo ziwe za aina ya pekee au za kuchukiza au ngeni, au miongoni mwa Israiliyati,6 mfano wa zilizoelezwa kutoka kwa Ka’ab na Wahab na wengineo, au inayopingana na Hadithi ambazo ni yakinifu, zinazohesabika kuwa ni miongoni mwa matamko ya kisheria, na zinazodirikiwa na hisia na yakini za kiakili. Na wanamzingatia mwenye kuzikataa kuwa ni kafiri na anaye zikhalifu kuwa ni fasiki.”7

Na endapo itakuwa kuitendea kazi Hadithi ni kwa sura hii, hapana kizuizi ziwe itikadi za kiislamu mateka wa maelfu ya Hadithi zilizozushwa na kuwekwa na Israiliyati ambazo Mayahudi waliziingiza katika itikadi za kiislamu.

Na kujigamba kwa mahanbali kuwa ni wenye kushikamana na Kitabu na Sunna, na kuwashambulia wengine kuwa wapotovu na makafiri, ni madai yasiyokuwa na maana na yasiyo na dalili, kwa kuwa wote wanatambua kuwa Sunna ni hoja na kuitendea kazi, lakini tofauti ni kuwa Mahanbali wanaamini kila kilichoelezwa kuwa ni kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) bila ya uthibitisho na bila ya kufahamu au kuelewa kinachomaanisha, kama alivyosema Zamakhshariy:
“Ukisema ni miongoni mwa wafuasi wa hadithi wanasema: Ni Taysu hatambui wala hafahamu. Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) amesema: ‘Mwenye kunisingizia makusudi na aandae makazi yake motoni,’ ni ishara bayana kuwa maadui wa dini watakuja kumnasibishia Mtume (s.a.w.w) na uislamu kila linalomuumbua na kuzifuta itikadi zake.

Kwa mujibu huo hapana budi somo la Hadithi liwe chini ya utaratibu wa kielimu na kimantiki. Sio kama walivyofanya Mahanbali, wanaamini kila kilichokutwa ndani ya vitabu miongoni mwa Hadithi, ikubalikayo kiakili au haikubaliki, inaafikiana na Qur’ani au haiafikiani.”

Ibnu Hanbal anasema katika risala yake: “Tunaieleza Hadithi kama ilivyokuja vile ilivyoelezwa, tunaisadiki na tunajua kama ilivyokuja.’’8

“Amesema: Na amenipa habari Ali bin Isa kuwa mhanbali mmoja aliwahadithia akasema: ‘Nikamuuliza Abu Abdillah kuhusu Hadithi ambazo huelezwa kuwa Allah huteremka kila usiku mpaka mbingu ya dunia, au kuwa Allah ataonekana, au kuwa Allah ataweka unyayo wake. Na zinazoshabihiana na Hadithi kama hizi. Abu Abdillahi alisema: Tunaziamini na tunazisadiki bila ya vipi wala maana. Yaani hatusemi ziko hivi wala hatuzibadilishi kwa taawili, eti tuseme maana yake ni hivi, wala hatukatai kitu kutoka humo.”9

Huu ndio mwendo wao kuhusu Hadithi, hawakatai kitu kutoka humo na wanasadiki kila kitu. Na visingizio wanavyovitumia kujikosha navyo ni hafifu, humchekesha mwanamke mwenye huzuni. Kwa kuwa kuzizingatia Hadithi kama hizi kuwa thabiti na sahihi ni kuthibitisha kuwa Allah (s.w.t.) ni kiwiliwili na kuwa anashabihiana na viumbe.

Na baadhi katika Mahashawiy wamedai kuwa kiwiliwili ni thabiti kwa Allah (s.w.t.).

Shahristani amesema: “Ama Washabihishi wa kihashawiy wamejuzisha kwa Mola kumgusa na kupeana naye mkono, na kuwa waislamu wenye ikhlasi wanamkumbatia (s.w.t.) duniani na akhera, ilimradi tu wafikie katika riyadha10 na juhudi, upeo wa ikhlasi.”11

Mifano Ya Hadithi Za Kumnasibisha Mwenyezi Mungu Na Kiwiliwili:

Hizi hapa kwako jumla ya riwaya, ni kama mfano tu na wala sio kuzizingira, nimezichagua kutoka katika kitabu Kitabus-Sunna ambazo zimeelezwa na Abdullah bin Ahmad kutoka kwa baba yake Ahmad bin Hanbal, na katika kitabu Kitabut-Tawhiidi cha Ibnu Khuzayma.

1. Ameeleza Abdullah bin Ahmad kwa sanad yake amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) amesema: ‘Amecheka Mola wetu kwa sababu ya kukata tamaa waja Wake na ukaribu wa wengine.’ Alisema: Nilisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) hivi Mola hucheka? Alisema: Ndio. Nikasema: Hatukosi kheri kutoka kwa Mola anayecheka.”12

Na nyingine miongoni mwa riwaya zinazothibitisha kicheko kwa Allah (s.w.t.).

2. Abdullah akasema: “Nilimsomea baba yangu... Halafu aliisema isnad mpaka kwa Said bin Jubair, kuwa wao wanasema: “Hakika roho ni katika yakuti yake. Sitambui kama amesema nyekundu au la? Na mimi ninasema: Said bin Jubair anasema: Hiyo ilikuwa zamaradi na maandishi yake ni ya dhahabu na Rahman aliiandika kwa mkono wake, na wakazi wa mbinguni wanasikia kelele ya kalamu.”13

3. Alisema: Baba yangu alinihadithia… kwa sanadi yake kutoka kwa Abi Attaqi akasema: “Allah aliandika Taurati kwa ajili ya Musa kwa mkono wake hali akiwa ameegemeza mgongo wake kwenye jabali katika mbao za duri, sauti ya kalamu inasikika, hakuna kati yake na Musa ila pazia.”14

Je, yafahamika kutoka katika riwaya hizi kama si mwili hasa na mshabaha wa wazi. Amedanganya mwenye kuamini Hadithi hizi kisha awe hamtii mawazoni Mola wake na kumfanyia sura, lakini wao wanamfanyia sura na kumuwaza.

Siku moja kulitokea mjadala kati ya ndugu yangu na mmoja wa masheikh wa kiwahabi, ambao ndio mtiririko wa kawaida wa itikadi ya Mahanbali, mjadala ulikuwa unahusu sifa za kiungu. Ndugu yangu alikuwa anamuepusha Allah mbali na sifa hizi, na kumthibitishia kwa kila njia uharibifu wa itikadi hizo, lakini bila faida, mwishowe ndugu yangu alimuezeka swali akisema:

Endapo atamthibitishia (s.w.t.) sifa kama hizi: Mahali, upande, mikono miwili, miguu miwili, macho mawili…mpaka mwisho wa wanayomsifu nayo Mola wao, je haiwezekani mtu kumfanyia sura na kumuwaza? Lakini bila shaka atamuwaza kwa kuwa nafsi ya mwanadamu imeumbika katika hali ya kufanya taswira na kuwaza baada ya sifa. Majibu yake yalikuwa yanaweka wazi kwa ukamilifu itikadi yake ya kumwekea Mungu kiwiliwili na taswira. Alisema: “Muwaze na mfayie taswira lakini usimfanyie habari…!”

Ndugu yangu alimuuliza: Nini tofauti kati ya uweke sanamu mbele yako na uliabudie, na uwe unaliwaza sanamu na unaliabudia? Akasema: “Huu ni usemi wa Rafidhu Mungu awalaani, wanamwamini Mungu wala hawamsifu sifa hizi, hivyo wao wanamwabudu Mola asiyekuwepo.”
Ndugu yagu alimwambia:

Kwa hakika Mungu wa kweli na ambaye akili hazimzunguki wala hadirikiwi na macho hafanyiwi mahali kuwa yu wapi, wala haulizwi yu vipi, wala haambiwi kwa nini na vipi, kwa kuwa yeye ndiye aliyeifanya wapi – yaani mahali – na ameifanya vipi - yaani umbile. Hivyo kile usichokifanyia taswira ndio Mungu na kila kifanyiwacho taswira ni kiumbe. Tumejifunza kwa maimamu wa Ahlul-Bayt (a.s.) kauli yao: “Kila mkifanyiacho taswira katika maana ya undani zaidi ni kiumbe mfano wenu, kinarudishwa kwenu.” Hivyo ukamilifu wa kumtambua Mwenyezi Mungu ni kushindwa kumtambua.

Akasema hali ameghadhibika: “Sisi tunathibitisha ambalo Mwenyezi Mungu amejithibitishia binafsi na yatosha.”

Halafu angalia jinsi walivyodai kumthibitishia Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala kidole, Mwenyezi Mungu awalaani, halafu katika vidole wanadai kumthibitishia kidolepete, na baada ya kutoka katika kidolepete ni pingili, kama alivyosema Ibnu Khuzayma katika Kitabut- Tawhiidi. Amesema kwa sanad ya Anas bin Malik amesema: “Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.): Mola wake alipojidhihirisha jabalini alinyanyua kidole chake cha mwisho na akashika sehemu ya pingili, jabali likadidimia.” Hapo Hamiidu alimwambia: Wahadithia hilo? Akasema: Anas ametuhadithia kutoka kwa Nabii (s.a.w.w.) na unasema usiihadithie?15

Na Ibn Hanbal ameeleza riwaya kutoka kwa baba yake mfano wa habari kama hii kwa sanad yake kutoka kwa Anas, kutoka kwa Nabii (s.a.w.w.): “Mola wake alipodhihiri kwenye jabali alisema hivi...... na hapo alionyesha kwa ncha ya kidole cha mkono cha mwisho akiigiza.”16

Wafahamu nini katika hayo ewe msomaji mwenye busara? Wamedai kuwa Mwenyezi Mungu ana mkono na mkono una kidole, na miongoni mwa vidole ni kidolepete, kisha wamesema: Na kidolepete kina pingili…!!! Simama hapo ili tukukamilishie picha.
Wamedai kuwa Mungu ana dhiraa mbili na kifua, Abdullah amesema: “Amenihadithia baba yaangu… na alitaja sanad kutoka kwa Abdullah bin Amri amesema: Malaika wameumbwa kwa nuru ya dhiraa mbili na kifua.”17

Na amesema kwa sanadi yake kwa Abu Hurayra kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.): “Maki ya ngozi ya kafiri ni dhiraa sabini na mbili kwa dhiraa ya Jabari, na jino lake ni mfano huohuo.”18

Na pia hufahamika kutokana na Hadithi hii ukiachia mbali kifua na dhiraa mbili ni kwamba dhiraa mbili zina urefu wenye kikomo, kama sivyo haiwezekani iwe kipimo cha urefu. Hawakusimama hapo bali wamemfanyia Mwenyezi Mungu mguu. Amesema Abdullahi bin Ahmad bin Hanbal kwa sanadi yake kutoka kwa Anas bin Malik akasema: “Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.): Watatiwa (waja) motoni, na (moto) utasema: Je kuna ziyada? mpaka Mwenyezi Mungu ataweka unyayo wake au mguu wake juu yake, hapo (moto) utasema basi basi.”19

Na Ibnu Khuizayma ameeleza kutoka kwa Abu Hurayra kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) amesema: “Ama moto hautozimika mpaka Mwenyezi Mungu aweke mguu wake humo, hapo utasema: Basi basi. Hapo utajaa.”20

Baada ya hayo njoo pamoja na mimi ewe msomaji mtukufu ili tuone wao wamevuka hayo na wamedai kumthibitishia Mwenyezi Mungu pumzi, Abdallah bin Hanbal kwa sanadi yake kwa Ubayy bin Ka’ab alisema: “Msiutukane upepo kwa kuwa ni katika pumzi za Rahman.”21

Panabakia nini mpaka picha ikamilike, khususan baada ya kuwa wamedai kumthibitishia uso. Je ni maneno na sauti?! Wamedai kumthibitishia bali wamemshabihisha na sauti ya chuma. Abdullah bin Ahmad amesema kwa sanad yake: “Mwenyezi Mungu akiongea kwa wahyi wakazi wa mbingu husikia sauti kama sauti ya mgongano wa chuma katika jangwa.”22

Halafu wamedai kuthibitisha kuwa Mwenyezi Mungu ana uzito na uzani, kwa minajili hiyo husikika kiti kikitoa sauti ya mlio pindi anapokaa, ikiwa hana uzito basi nini maana ya sauti ya mlio? Ameeleza Abdullah bin Ahmad bin Hanbali kwa sanadi yake kutoka kwa Umar amesema: “Akiketi kitini husikika kutokana naye sauti kama sauti ya kiti kipya cha mnyama wa kupanda.”23Yaani kama sauti ya kiti cha ngamia kwa mpandaji mzito.

Na amesema kwa sanadi yake kwa Abdillah bin Khalifa amesema: “Alikuja mwanamke kwa Nabii (s.a.w.w) na akasema: Muombe Mwenyezi Mungu aniingize Janna. Akasema: Alimtukuza Rabi, na akasema: Kiti cha enzi yake kimetanda mbinguni na duniani, kwa hakika yeye hukaa juu yake hakibakii ila kiasi cha vidole vinne, na kuwa yeye ana sauti ya mlio kama sauti ya mlio wa ngamia akipandwa.”24 Na Ibnu Khuzayma amezidisha: “Kwa uzito wake.”25

Inakamilika sura hii ya mchezo wa kuigiza. Hivyo basi Mwenyezi Mungu anakuwa mtu mwenye sifa ambazo mwanadamu huwa nazo, mfano wa kiwiliwili, kuwa na kikomo, viungo vya mwili na muundo. Na hii ndio dhahiri japo waikanushe bali wamebainisha zaidi ya hivyo.

Imekuja katika Hadithi kuwa Mwenyezi Mungu amemuumba Adam kwa sura yake - kwa sura ya Mungu - urefu wake dhiraa sabini. Na wanadai uwezekano wa kuonwa na kuangaliwa. Kama alivyoeleza Ibnu Khuzayma kwa sanadi yake kwa Ibnu Abbas kuwa Nabii (s.a.w.w.) alisema: “Nimemuona Mola wangu katika sura nzuri, akasema: Ewe Muhammad.

Nikasema: Labaika Wasaadayka. Akasema: ‘Katika nini wanagombana wakuu wa juu?’ Nilisema: ‘Ewe Mola wangu sitambui.’ Alisema: ‘Aliweka mkono wake kati ya bega langu, nilipata ubaridi wake kati ya ziwa langu, nikayajua yaliyo kati ya Mashariki na Magharibi.”26

Na akasema kwa sanadi yake kuwa Abdullah bin Umar bin al-Khattabi alimtuma mtu kwa Abdullah bin Abbas amuulize: ‘Je Muhammad (s.a.w.w.) alimwona Mola wake?’ Abdullah bin Abbas alimtumia jibu kuwa ndio. Abdullah bin Umar alimrudisha mjumbe wake na swali: ‘Alimwona vipi?’ Alisema: Alimtumia kuwa alimwona katika bustani ya kijani chini ya godoro la dhahabu juu ya kiti cha dhahabu akibebwa na malaika wanne. Malaika katika sura ya mtu, na malaika katika sura ya maksai, na malaika katika sura ya furukombe, na malaika katika sura ya simba.27

Na hizi ni chache kutoka katika nyingi. Tutosheke na kadiri hii ndogo ya itikadi ya Mahanbali na waliovaa kilemba chao kuhusu sifa za Mwenyezi Mungu (s.w.t.). Na tumezifumbia macho itikadi zao zingine, tulizozitaja zinatosha kufichua itikadi zao.

Baadhi ya Mahanbali walipoona uovu walioufanya wamejaribu kuyakwepa hayo kwa kisingizio cha kauli yao: Bila ya namna?

Ash’ariy ametegemea ukwepaji huu, hivyo katika kitabu chake al-Ibana Uk.18 anasema: “Kwa kweli Allah (s.w.t.) ana uso bila ya namna, kama alivyosema: ‘Na utabakia uso wa Mola wako Mwenye utukufu na heshma.’

Na kwa hakika Yeye anayo mikono miwili bila namna, kama alivyosema: ‘Nimeumba kwa mkono wangu.’

Kauli ya mshairi ni ya kweli kuwahusu:

Wamemshabihisha na viumbe Vyake na wakahofia kebehi ya watu, wakajisitiri kwa ‘bila namna.’”

Na ni wazi, kwa kila mwenye akili timamu kuwa aina hii ya kujikwepesha hakubadilishi sura ya suala, kwa kuwa kutojua namna yake hakuleti faida yoyote, wala kulirejesha suala kwenye maana sahihi, na hiyo ni karibu mno na kufumba na kitandawili. Kwa kuwa kuthibitisha matamko haya kwa maana yake ya ukweli ni kuyathibitishia namna, kwa kuwa matamko huwa kwa ile namna yake. Na kuzithibitisha sifa hizi kwa maana zake zilizo maarufu ndio kumnasibishia kiwiliwili na kumshabihisha kwenyewe. Na kutoa udhuru kwa kauli yao: ‘Bila ya namna’, ni tamko tu la ulimi lisilo na maana.

Nakumbuka siku moja nilikuwa najadiliana na mmoja katika maustadhi wangu huko chuo kikuu kuhusiana na istiwai ya Allah juu ya Arshi, na alipohemewa akasema: “Sisi tunasema waliyoyasema Salafu: ‘Istiwau yajulikana na namna haijulikani na kuiulizia ni bidaa.”’ Nilimwambia: Haukuzidisha kwenye suala hili ila utata, na maji baada ya juhudi umeyatafsiri kuwa ni maji. Akasema: “Vipi? Hali mjadala umekwenda sawa.”

Nilimwambia: Ikiwa istiwau inajulikana na namna yake pia inajulikana. Na ikiwa namna haijulikani, na istiwau ni hivyo hivyo wala haitengani. Hivyo kuijua istiwau ni ujuzi uleule wa kuijua namna. Kwa kuwa akili haitenganishi kati ya sifa ya kitu na namna yake, kwa kuwa hivyo viwili ni kitu kimoja.
Hivyo ukisema fulani amekaa, ujuzi wako wa kukaa kwake ndio ujuzi wako wa namna alivyokaa. Hivyo wewe unaposema: Istiwau yajulikana, ujuzi wako ule wa istiwau ndiyo ujuzi wako wa namna yake, vinginevyo maneno yako yatakuwa yanapingana, bali ndiyo kupingana dhati yake. Hivyo unakuwa mjuzi wa Istiwai wakati huo huo haujui namna yake.

Alinyamaza kwa muda hakuwa na jibu, halafu alitoa udhuru kuwa ana haraka aliomba idhini na alikwenda. Hivyo yote wasemayo kuwa hakuna namna pamwe na kuthibitisha maana ya matamko ya kweli ni kupingana na ni kupayuka. Hivyo hivyo usemi wao kuwa Mwenyezi Mungu ana mkono wa kweli lakini si kama mikono, ni maneno ambayo mwisho wake unapingana na mwanzo wake na kinyume chake. Kwa sababu mkono kwa maana yake halisi una ile namna inayojulikana, na kuuondolea namna ni kuifutilia mbali hakika yake.

Na ikiwa matamko haya matupu yanatosheleza kumthibitishia utakatifu Allah, basi yawezekana ikasemwa kuwa: Mwenyezi Mungu ana mwili bila ya namna na si kama miili, na anayo damu isiyo na namna, nyama na nywele bila ya namna. Mpaka mmoja miongoni mwa washabihishaji akasema: “Nimeona haya tu kuthibitisha uchi na ndevu, na niwieni radhi na hivi viwili, na ulizeni vilivyo nyuma ya hivyo.”28

Wala haifahamiki kutokana na hayo kuwa sisi tunaamini taawili, bali katika Aya kama hizi haijuzu kuifanyia taawili dhahiri ya Kitabu na Sunna kwa madai kuwa zahitilafiana na akili, bali hakuna ndani ya Kitabu na Sunna kinachopingana na akili.

Na kinachoharakia miongoni mwa dhahiri kuwa chapingana na akili, huwa si dhahiri isipoku watu wanawaza kuwa ni dhahiri, lakini ukweli si dhahiri. Na katika mfano wa Aya kama hizi suala halihitaji taawili, kwa sababu lugha katika dalili zake za maana inagawanyika sehemu mbili: Dalili ya msamiati mmoja. Na dalili ya muundo wa sentensi.

Huenda maana ya hali ya msamiati mmoja ikatofautiana na maana ya muundo ndani ya sentensi endapo kutakuwa na muktadha unaolazimu hivyo, na maana huafiki msamiati endapo hakuna muktadha unaoitoa mbali na maana ya msamiati mmoja.

Kwa mfano: Usemapo: Simba, na ni msamiati mmoja, itaharakia akilini yule mnyama mkali anayeishi mbugani, na pia hufahamika maana hii hii katika hali ya muundo wa sentensi endapo hakuna muktadha unaoondoa maana hiyo, mfano wa kauli yako: Nilimuona simba anakula windo lake mbugani.

Lakini maana hii hubadilika kabisa tusemapo katika jumla ya muundo: Nilimuona simba anaendesha gari. Makusudio ya simba hapo ni mtu shujaa. Na huu ni mwenendo wa waarabu katika kufahamu maneno, hivyo mshairi asemapo: ‘’Kwangu ni simba, vitani ni mbuni, ni tai akimbiaye uruzi wa mpiga mruzi.’’ Hatuwezi kufahamu kutokana na hiyo beti ila ni yule mtu anayejionesha ushujaa mbele ya watu dhaifu, na akimbiaye kwa woga akutanapo na maadui.

Na ambaye anafahamu maneno haya haiwezekani tumwite mfanya taawili wa matamko, na kuwa ametoka nje ya dhahiri ya maneno.

Hali ni hiyo hiyo katika Aya hizi. Kwa mfano Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaposema: “Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao.” Maana ya mkono inakuwa uwezo bila ya taawili. Hiyo ni kama mtu asemapo: “Nchi iko mkononi mwa Sultani.” Yaani iko chini ya amri yake na idara yake. Na kauli hii ni sahihi japo Sultani huyo awe ni mtu aliyekatika mkono. Na ni hivyo hivyo katika Aya zingine. Huwa tunazitendea kazi maana za muundo wa sentensi, ambazo hudhihiri kupitia mfululizo wa sentensi, wala hatugandi kwenye maana ya msamiati mmoja, na hiyo sio taawili wala. Na huko ni kuitendea kazi maana ya dhahiri, lakini ni dhahiri zinazodhihiri kutokana na muundo wa sentensi.
Na hao mahanbali wanawapoteza watu wa kawaida kwa kuzitumia vibaya dhahiri za maneno na msamiati mmoja mmoja, na si kwa muundo wa sentensi.

Kwa njia hii dhahiri za Kitabu na Sunna zinakuwa hoja haijuzu kuziacha wala haifai kwa yeyote kuzifanyia taawili, baada ya kuangalia kwa makini muktadha zile zilizo katika mfululizo wa sentensi husika na zile zilizo pembeni ya sentensi husika. Na ambaye hutoa hoja kwa kutumia dhahiri za misamiati mmoja mmoja, amepotea na ameghafilika mbali na maneno ya waarabu.

Na kabla hatujamuaga Ahmad bin Hanbal na itikadi zake, tungependa kumjulisha msomaji mtukufu maneno ya Ahlul-Bayt na Hadithi zao kuhusiana na sifa za Mwenyezi Mungu (s.w.t.), ili ajue kuwa nuru hii kutoka maneno yao ni kutoka mwanga wa Qur’ani tukufu.

Na kuwa maafa makubwa ambayo yameikabili fikra ya kiislamu ni tija ya kawaida – kimaumbile – kutokana na kuwa mbali kwetu na maneno haya na Maimamu wa Ahlul-Bayt.

Imam as-Sadiq (a.s.) amesema kweli aliposema: “Watu wangetambua uzuri wa maneno yetu wangetufuata.”

Na ninanakili maneno haya kwa ajili yako kutoka kitabu Tawhiid cha Sheikh Saduq, nacho ni kitabu kikubwa kimehifadhi johari za maneno ya Ahlul-Bayt katika mlango wa tawhiid. Na ninamsihi msomaji mtukufu azingatie maneno haya kwa jicho la uelewa na ufahamu, halafu ayalinganishe na yaliyokuja katika kile Kitabus-Sunna cha Abdullah bin Ahmad bin Hanbal na Kitabut-Tawhiid cha Ibnu Khuzayma, au kitabu chochote cha Ahlus Sunna kilichokusanya Hadith za tawhiid na sifa za Mwenyezi Mungu (s.w.t.).

Hotuba Ya Mtukufu Mtume Wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.W.)

“Alhamdu lillahi – Sifa zote ni Zake Ambaye alikuwa katika umwanzo wake pekee, na katika umilele wake ni Mtukufu kwa uungu, Mwenye kujitukuza na ukuu Wake na nguvu Zake.

Ameanza alivyoviumba, na amevifanya alivyoumba, bila ya mfano uliokitangulia kitu chochote miongoni mwa alivyoviumba. Mola wetu ni wa milele kwa wema wa ulezi Wake. Na kwa elimu ya habari Yake ameatua, na kwa hukumu ya uwezo Wake ameumba yote aliyoyaumba. Na kwa nuru ya alfajiri amepambazua.

Hapana cha kubadili uumbaji Wake, wala cha kugeuza aliyotengeneza. Hapana kitakachochukua nafasi ya hukumu Yake, wala cha kupinga amri Yake, wala pumziko mbali na wito Wake, wala hautoweki ufalme Wake, wala muda Wake haukatiki.

Na Yeye ndiye Mwenye kuwa kwanza na wa kudumu abadan. Mwenye kujificha kwa nuru yake mbali na viumbe Wake katika zoni ya malengo, na enzi ya juu na ufalme mtukufu. Ni Mtukufu juu ya kila kitu, na Yuko karibu na kila kitu. Amekuwa dhahiri kwa viumbe Wake bila ya kuwa aonwa, Naye yuko kwenye maono ya juu kabisa.

“Alipenda kuwa mahsusi kupwekeshwa, alipojificha kwa nuru yake, na amepaa kwa kuwa kwake juu, na amejisitiri mbali na viumbe wake, na amewatumia mitume ili awe na hoja kinaifu kwa viumbe Wake, na mitume Wake wawe mashahidi dhidi yao.

Na amewatuma kwao manabii wenye kutoa bishara na wenye kuonya, ili ahiliki mwenye kuhiliki akiwa yuaelewa, na awe hai mwenye kuwa hai katika hali ya uelewa, na ili waja waelewe kutoka kwa Mola Wao ambayo waliyokuwa hawayajui, kwa hiyo wamtambue kwa ulezi Wake hali walikuwa wanakanusha, na wampwekeshe kwa uungu baada ya kuwa walisaidiana.”29

Hadith Ya Imam Ridhaa (A.S)

Kutoka kwa al-Fat’hu bin Yazid al-Jurjaniy amesema: Nilikutana naye (a.s.) akiwa njiani nilipotoka Makka nikienda Khurasani, na yeye akielekea Iraq, nikamsikia akisema: “Mwenye kumcha Mwenyezi Mungu huheshimiwa na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu hutiiwa.” Niliomba kwa upole ili kumfikia, nilimfikia na nilimsalimia, alinijibu salamu halafu akasema:

“Ewe Fat’hu! Mwenye kumridhisha muumba hatojali kukasirika kwa kiumbe, na mwenye kumkasirisha muumba inamfalia dhidi yake liwezeshwe kasiriko la kiumbe. Kwa hakika Muumba hasifiwi ila kwa alichojisifu nacho mwenyewe, na vipi asifiwe ambaye hisi zinashindwa kumdiriki, na mawazo kumuwaza, na ushauri kumfanyia mpaka, na macho kumzunguka? Ametukuka mbali na waliyomsifu wenye kumsifu, na amekuwa juu mbali na maelezo ya waelezaji, Yuko mbali katika ukaribu Wake, na amekurubia katika umbali Wake, hivyo Yeye katika umbali Wake yuko karibu, na katika ukaribu Wake yuko mbali.

“Aliweka namna, basi haulizwi yuko vipi. Na akaweka eneo, basi haulizwi yuko wapi. Kwa kuwa yeye ndiye aliyebuni namna na eneo. Ewe Fat’hu! kila mwili hulishwa kwa chakula isipokuwa muumba mwenye kuruzuku. Kwa kuwa Yeye ameifanya miili na Yeye si mwili wala sio umbo, hajawa sehemu ya kitu kizima, na hajawa na ukomo. Hajazidi wala hajapungua……..Yeye ni mwema mwenye habari, msikivu, muoni, Mmoja wa pekee, wa milele, hakuzaa wala hakuzaliwa, wala hajawa na kifani. Mbunifu wa vitu, na mfanyaji miili na mfanyaji wa sura.

Lau angekuwa kama wanavyosema wenye kumshabihisha basi hangetambulika kati ya Muumba na kiumbe. Wala mtoa riziki na anayepewa riziki, wala mfanyaji na kilichofanywa. Lakini yeye ni mfanyaji. Ni tofauti kati ya aliyeufanya mwili na kuifanya sura na kukifanya kitu, kwa kuwa hashabihiani na kitu.”

Nilisema: Mwenyezi Mungu ni Mmoja na mtu ni mmoja, je umoja si umeshabihiana? Akasema: “Umechanganya namuomba Mwenyezi Mungu akuimarishe. Kushabihiana huwa katika maana tu, ama majina ni mamoja, nayo hujulisha muitwa. Hivyo ni kwa sababu mtu japo isemwe kuwa ni mmoja hiyo huwa yahabarisha kuwa ni mwili mmoja sio miwili.

Ama kumhusu mtu mwenyewe sio kitu kimoja, kwa kuwa viungo vyake vya mwili vi tofauti, rangi zake tofauti sio kitu kimoja. Yeye ni viungo vilivyofanywa sehemu sehemu, nazo hazipo sawa. Damu yake sio nyama yake, na nyama yake sio damu yake. Mshipa wake wa fahamu sio mshipa wake wa damu, na nywele zake sio ngozi yake, weusi wake sio weupe wake.

“Hivyo hivyo viumbe wengine wote. Hivyo basi mtu ni mmoja katika jina sio mmoja katika maana, na Allah ni mmoja hapana mmoja halisi asiye kuwa Yeye, wala hapana hitilafu katika Yeye wala tofauti wala ziada wala nuksani. Ama mtu aliyeumbwa aliyetengenezwa ni mwenye kuundika kutokana na sehemu tofauti na johari mbalimbali, ila tu kwa kuzikusanya pamoja ni kitu kimoja.”

Nilisema: Umenifariji Mwenyezi Mungu akufariji, isipokuwa wewe ulise- ma: Mwenye kusikia, mwenye kuona. Je ni mwenye kusikia kwa masikio mwenye kuona kwa macho? Alisema: “Kwa kweli Yeye anasikia kwa anachoonea, na anaona kwa anachosikilizia. Mwenye kuona sio kwa macho mfano wa macho ya kiumbe.

Na msikivu sio mfano wa usikiaji wa wasikiaji, lakini maadamu hakifichiki kwake cha kufichika kama athari ya dhara nyeusi iliyopo juu ya jabali lisilosikia katika usiku wa giza chini ya udon- go na bahari, twasema: Ni Mwenye kuona, sio kwa macho mfano wa macho ya viumbe. Na maadamu Yeye hachanganyikiwi na lugha tofauti wala hashughulishwi na kusikia mbali na kusikia kwingine, twasema: Ni Mwenye kusikia sio mfano wa kusikia kwa wasikiaji.30

Hotuba Ya Amirul-Mu’minina (A.S.)

“Himidi ni yake Ambaye hakuwa kutokana na kitu, wala yaliyokuwa hakuyafanya kutokana na kitu. Kutukia kwa vitu ni ushahidi wa ubila mwanzo wake, na kwa aliyoyawekea alama ya kushindwa ni dalili ya uwezo wake, na kwa aliyoyafanya yalazimike kuisha ni dalili ya udaima kwake. Mahali hapajawa tupu bila ya Yeye hata atambuliwe kwa eneo, wala hana mshabaha wa mfano ili ielezwe kuwa yuko hivi, wala kitu hak- ijawa ghaibu mbali na elimu yake kiasi cha kuwa ajulikane kwa namna.

“Ana pambanuka mbali na yote aliyoyabuni kwa sifa, hawezi tambulika kupitia alivyovibuni kwa kutumia dhati ya vitu. Na ametoka kwa ukuu na utukufu mbali na harakati za hali zote. Inazuilika kwa utambuzi wa hali ya juu kumwekea mipaka, na kwa fikra ya undani zaidi kumfanyia namna, na kwa fikra zizamazo mbizi kumfanyia taswira.

“Kwa utukufu Wake habebwi na mahali, wala hakadiriwi kwa vipimo kwa utukufu Wake, wala hapimiki kwa vipimo kwa ukuu Wake, anazuilika mbali na mawazo kuufikia uhakika Wake, na kwa fahamu kumuelewa kwa undani, na akili kumfanyia methali. Akili zenye tamaa zimekatishwa matumaini ya kumzunguka. Bahari za kielimu zimenywea bila ya kumwonesha kwa upeo, na wamerejea udogo bila ya kupanda kwenye kuusifu uwezo Wake mahasimu wema.

“Mmoja sio kwa idadi, na wa daima sio kwa muhula, mwenye kusimama sio kwa nguzo. Sio jinsi hata alingane na jinsi, wala sio kivuli hata vivuli vifanane naye, wala sio kama vitu hata sifa ziangukie juu Yake. Akili zimepotea kwenye mikondo ya mawimbi ya kumdiriki. Dhana zimeduwaa bila ya uwezo wa kuuzunguka utajo wa umilele Wake. Fahamu zimezingirwa mbali na kuzitambua sifa za uwezo Wake. Uelewa umezama kwenye bahari kuu ya falaki ya milki Yake.

“Muweza kwa neema na Mwenye kuziwilika kwa ukuu, Mwenye kujimiliki juu ya vitu, dahari haimchakazi wala wasifu kumzunguka. Magumu yaliyo thabiti yamenyenyekea Kwake mahali pa ukomo.

“Jumla ya jinsi zilizopo ni ushahidi wa kuwa Yeye ni Mlezi, pia kwa kushindwa kwao uwezo Wake. Na kwa kusimama Kwake ni dalili ya uzamani Wake. Na kwa kutoweka kwa jinsi hizo ni dalili ya kubaki Kwake, wala hakuna upenyo wa zenyewe kumdiriki, wala kutoka nje ya uwezo Wake wa kuzizunguka, wala zenyewe kujificha mbali na hesabu Yake, wala kuukataa uwezo Wake juu ya jinsi hizo.

“Unatosha umadhubuti wa utengenezaji wa hivyo kuwa ni alama, na kwa muundo wa tabia ni dalili, na kwa kutukia umbo juu yake (jinsi hizo) ni dalili ya uzamani (wake Allah), na kwa umadhubuti wa utengenezaji wa hivyo ni funzo. Hakuna mpaka uliowekwa kwake, wala hapigiwi mfano, wala kitu kujificha mbali na Yeye. Ametukuka yuko juu mbali mno na kupigiwa mifano, na yuko juu mbali mno na kusifika na sifa za viumbe.”

Pili: Awamu Ya Ibnu Taymiya, Ahmad Bin Abdil’haliim:

Baada ya kuenea itikadi ya Ashaira, ambayo ilitanda sehemu kubwa za nchi za kiislam, mpaka iliibuka na kuwa madhehebu rasmi katika misingi ya dini, kwa kundi kubwa la waislamu, utajo wa Ibnu Hanbal ulikuwa mdogo na madhehebu yake kiitikadi yalizuilika, mpaka alipodhihiri Ibnu Taymiyya ambaye alizaliwa 661 A.H. ndani ya nyumba ya masheikh wa kihanbal na ni katika mojawapo miongoni mwa ngome za Mahanbal katika mji wa Haraan.

Alikulia katika ukoo huu na kusoma mkononi mwa mzazi wake ambaye alimtengea kiti huko Damascus baada ya kuhamia kwake huko. Na alisoma kwa wengine elimu ya Hadith, elimu ya hali za wapokezi, lugha, tafsiri, fiq’hi na usulu.

Na baada ya kufa mzazi wake Ibnu Taymiyya alitawalia duru ya kudarisisha, na hii ilikuwa fursa yake ya kuurudishia Uhanbali utukufu wake, hivyo basi aliitumia mimbari hii kuzungumzia sifa za Mwenyezi Mungu, akitaja thibitisho zinazonusuru itikadi ya wasemao Mungu ana kiwiliwili, na jambo hili lilidhihiri wazi alipokuwa akijibu maswali ya jamaa walipomwandikia kumuuliza Aya za sifa, mfano wa kauli yake:

“Rahmani ametawala juu ya Arshi”

Na kauli yake:

“Kisha akaitawala mbingu.”

Na mfano wa kauli yake (s.a.w.w): “Kwa hakika moyo wa mwanadamu uko kati ya vidole viwili miongoni mwa vidole vya Rahman.”

Aliwajibu kwa risala ndefu, iliyoitwa Aqidatu Al-Hamawiyatu. Humo ali- fichua itikadi yake ya kumnasibisha Allah na kiwiliwili na kumshabihisha na viumbe, bila ya kuweka wazi hilo, akijisitiri kwa matamshi na maneno lau yangeondolewa ukweli wa mambo ungedhihiri. Risala hii ilizua zogo baina ya duru za wanazuoni, na walimpinga, kwa hiyo akajihami kwa kukimbilia kwa Amiri wa Damascus ambaye alimnusuru.

Na Ibnu Kathir ananukuu hilo: “Damascus ulitokea mtihani kwa Sheikh Taqiyu Diyn Ibnu Taymiyya, na walijitokeza dhidi yake jamaa miongoni mwa wasomi wa fiqhi, walitaka kumfikisha kwenye kikao cha Kadhi Jalalu Diyn al-Hanafiy, wala hakuhudhuria. Mkanadiwa nchini humo kuhusu itikadi ambayo watu wa Hamatu walimuuliza, inayoitwa al-Hamwiyah. Amiri Saifu Diyn Jaan alimnusuru. Na alituma kuwatafuta waliompinga, wengi miongoni mwao walijificha, na walipigwa jamaa miongoni mwa walionadi dhidi ya itikadi ile na waliobaki walinyamaza.”31

Hivyo hivyo wanavyuoni walizinyamazia itikadi zilizopotoka kwa nguvu za Sultani. Hapo Ibnu Taymiyya alipata ukumbi aongee apendavyo. Na ametunakilia shahidi wa macho itikadi ya Ibnu Taymiyya kumhusu Mwenyezi Mungu (s.w.t.), naye si mwingine ila ni yule mwana misafara mashuhuri Ibnu Batuta, ilitokea kwa bahati siku moja alihudhuria darasa la Ibnu Taymiyya katika msikiti wa Amawiy. Alisema:

“Wakati huo nilikuwa Damascus nilihudhuria siku ya Ijumaa naye alikuwa anawawaidhi watu akiwa juu ya mimbari ya msikiti, akiwakumbusha, na alisema katika jumla ya maneno yake: ‘Kwa hakika Mwenyezi Mungu huteremka mpaka mbingu ya dunia kama uteremkaji wangu huu’ na aliteremka ngazi moja ya mimbari. Mwanachuoni mmoja wa Madhehebu ya Malik, aliyekuwa anajulikana kwa jina Ibnu Zahraa alimpinga aliyoyasema.

Mashabiki wake walimvamia mwanachuoni huyu wakampiga sana kwa ngumi na kwa viatu mpaka kilemba chake kilidondoka na kilidhihiri kichwani mwake kitambaa cha hariri. Walilipinga vazi lake hilo na walim- beba mpaka nyumba ya Izzu Diyn bin Muslim Kadhi wa mahanbali, naye aliamuru afungwe na baada ya hapo walimuadhibu.”32

Na usemi huu wa mwana wa Taymiyya umetajwa pia na Ibnu Hajar al- Asqalaniy katika kitabu Durarul-Kaaminah, Jalada 1, Uk.154. Na itakubainikia wazi upendeleo wake mkali kwa wanaothibitisha sifa, kiasi kwamba alifikia kujishabihisha na Mwenyezi Mungu (s.w.t.), na hii ni kufuru na uzandiki hasa.

Na amejisitiri na itikadi hii kwa kauli yake kuwa ni itikadi ya Salafu na ndivyo yalivyojiri mambo ya waislamu. Kwa hivyo anawasingizia Salafu na kujisitiri kupitia wao ili aifiche itikadi yake mbaya, hali ikiwa inajulikana kuwa pazia ya Salafu mahanbali wamejaribu toka zamani kujifunika kwalo, lakini bila mafanikio, kwa sababu ya kukithiri itikadi za kimadhehebu ambazo zilikuwa kabla ya Ahmad na baada yake.
Na tofauti hizi zinatilia mkazo kuwa waislamu hawakuwa na umoja katika itikadi, na kila madhehebu inajigamba kuwa ina mawasiliano na Layla, na hali Layla hawakubalii hilo.

Na Shahristaniy anayakadhibisha madai ya Ibnu Taymiyya kuwa yuafuata madhehebu ya Salaf, kama alivyosema katika kitabu al-Milalu Wan- nahlu: “Kisha kwa hakika jamaa miongoni mwa waliokuja nyuma wamezidisha zaidi ya waliyoyasema Salafu, wamesema: Hapana budi Aya hizi zitumike kama dhahiri yake ilivyo, na kuitafsiri kama ilivyokuja bila ya kujiingiza kwenye taawili wala kusimama kwenye dhahiri.

Kwa hiyo wakatumbukia kwenye tashbihi tupu. Na hivyo ni kinyume na walivyokuwa Salafu wanaitakidi. Na tashbihi ilikuwa khususan kwa kundi katika mayahudi, si katika wote. Bali huenda wasomaji miongoni mwao, walipokuta katika Tawrati matamshi mengi yanajulisha hilo – yaani tash- bihi.”33

Ibnu Taymiyya amewahadaa watu wa kawaida kwa kauli zake nyingi za wazi, mfano wa kauli yake: “Ama ambalo nilisemalo hivi sasa na ninaliandika, japo iwe sikuliandika hapo kabla miongoni mwa majibu yangu, ila tu mara nyingi hulisema katika vikao: Hakika yote yaliyomo katika Qur’ani miongoni mwa Aya za sifa, kwa maswahaba hakuna tofauti katika taawili yake.

Kwa hakika nimezisoma tafsiri zilizonakiliwa kutoka kwa swahaba, na Hadithi walizozieleza, na nimefahamu ambalo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amependa, miongoni mwa vitabu vikubwa na vidogo, zaidi ya tafsiri mia, mpaka saa yangu hii sijakuta yeyote miongoni mwa swahaba kuwa alifanya taawili chochote katika Aya za sifa au Hadithi za sifa, kinyume na muktadha wake unaofahamika ulio maarufu.”34

Na kwa kuuacha wazi usemi kama huu, watu wa kawaida wanasadiki usemi wake, ila tu kwa kurejea kidogo katika vitabu vya tafsiri vilivyokutwa unatudhihirikia uwongo wa Ibnu Taymiyya. Ima katika kutorejea kwake tafsiri au kwa madai ya kutokuwepo taawili katika Aya za sifa kutoka kwa maswahaba, nami hapa nitakutosheleza kwa shuhuda.

Endapo tutarejea tafsiri ya Tabariy, nayo ni ambayo Ibnu Taymiyya anaisifu kwa kauli yake: “Ndani yake hakuna bidaa wala haelezi riwaya kutoka kwa watuhumiwa.”35

Tunaporejea humo Ayatul-Kursiy ambayo Ibnu Taymiyya ameizingatia kuwa ni Aya tukufu mno miongoni mwa Aya za sifa, kama ilivyo katika al- Fatawal-Kubra Juz. 6, Uk. 322.

Tabariy analeta riwaya mbili sanadi yake ni kutoka kwa Ibnu Abbas, kati- ka tafsiri ya kauli yake (s.w.t.): “Elimu yake imeenea mbingu na nchi” (Surat Al-Baqarah: 255). Amesema: “Wametofautiana wafanyao taawili kuhusu maana ya Kursiy. Baadhi yao wamesema kuwa ni elimu ya Mwenyezi Mungu, umetukuka utajo Wake.” Na hapo alitaja waliosema hivyo kwa sanad yake kuwa Ibn Abbas akasema: “Kursiyyuhu ni elimu Yake.” Riwaya nyingine pia kwa sanadi yake kutoka kwa Ibnu Abbas, akasema: “Kursiyyuhu ni elimu Yake, hauoni katika kauli yake: Wala hakumchoshi kuzihifadhi.” (Surat Al-Baqarah: 255)36

Angalia na staajabu, uwongo safi, kwani yeye anasema kuwa: “Salafu hawakuhitilafiana kitu chochote kuhusu sifa.” Na Tabariy anasema: “Wamehitilafiana ahlu taawili.” Na Ibnu Taymiyya ameiacha wazi kauli yake: “Sijamkuta yoyote katika swahaba mpaka saa yangu hii amefanya taawili kitu katika Aya za sifa.” Japokuwa amejigamba amefanya rejea za tafsiri mia, lakini na Tabariy anataja riwaya mbili kutoka kwa Ibnu Abbas!

Kwako wakujia ushahidi wa pili: Kutoka katika tafsiri ya Tabariy, katika kuitafsiri kauli yake (s.w.t.):
Tabariy anasema: “Watafiti wametofautiana katika maana ya kauli yake baadhi yao wamesema: “Kwa hilo anamaanisha Yeye yuko juu bila kifani, wala kushabihiana.”

Na wamekanusha kwamba iwe Yamaanisha yuko juu kwa maana ya mahali, na wamesema: “Sio jaizi mahali pawe tupu mbali na Yeye, wala kusifika kwake na ujuu hakulengi mahali, kwa kuwa hivyo itakuwa ni kumwelezea kuwa Yuko mahali na hayupo mahali pengine.”37

Hii ndio kauli ya Salafu. Lakini Ibnu Taymiyya amejichagulia binafsi njia nyingine, na hakumpata anayemuunga mkono, hivyo ikambidi aiegemeze kauli yake kwa Salafu. Tunaona hapa kuwa Salafu hawaamini kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ana mahali mahsusi.

Na tunamuona Ibnu Taymiyya anakusanya kundi la Hadithi ili kwazo athibitishe mahali mah- susi pa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) katika risala yake kwa watu wa Hamaatu, mpaka anafikia kusema: “Kwa hakika Allah (s.w.t.) Yuko juu ya Arshi, na kuwa yenyewe ipo juu zaidi ya mbingu.”38 Na kwa hilo anakusudia mahali.

Ama katika tafsiri ya Ibnu Attiya ambayo Ibnu Taymiyya anaizingatia kuwa ni miongoni mwa tafsiri za maana, amezileta riwaya za Ibnu Abbas alizozileta Tabariy, halafu amezifanyia maelezo baadhi ya riwaya ambazo Tabariy amezitaja na Ibnu Taymiyya kushikamana nazo kwa kauli yake: “Hizi ni kauli za wanaomnasibisha Allah na kiwiliwili, wajinga, na wajibu ilikuwa zisisemwe.”39

Na huu ni ushahidi mwingine katika tafsiri ya kauli yake (s.w.t.): “Kila kitu kitaangamia isipokuwa Yeye.” (Sura Qasas: 88).

Na kauli yake: “Na itabaki dhati ya Mola wako, Mwenye utukufu na heshma. (Sura Rahman: 27) ambazo kwazo Ibnu Taymiyya anathibitisha kuwa ni uso hasa.

Tabariy amesema: “Na imepatikana tofauti kuhusu maana ya kauli yake: “ila uso wake.” baadhi yao wamesema: Kila kitu kitahiliki isipokuwa Yeye.40 Na wengine wamesema: Maana ya hiyo ni: Isipokuwa kilichokusudiwa kwa ajili yake Yeye. Na wameitolea ushahidi taawili yao kwa kupitia kauli ya mshairi:

Namuomba Mwenyezi Mungu ghufrani ya dhambi nisizozidhibiti kwa hesabu. Mola wa waja, kwake amali hukusudiwa.”41 Hakuzidisha juu ya hilo.”

Al-Baghwiy amesema: “Yaani, ila Yeye, na imesemwa: Ila ufalme Wake.”

Abul Aliya amesema: “Ila ambalo limekusudiwa kwa ajili yake.”42 Wala hakuzidisha juu ya hilo.

Na katika ad-Durru al-Manthuur kutoka kwa Ibnu Abbas amesema: “Maana ila linalokusudiwa Yeye.”

Na kutoka kwa Mujahid: “Ila lililokusudiwa Yeye.”

Na kutoka kwa Sufiyan: “Ila lililokusudiwa Yeye miongoni mwa amali njema. “

Hizo ni kauli za Salafu. Wala kati yao hakuzidisha yoyote zaidi ya hizo, basi wapi baada ya hivyo Ibnu Taymiyya aseme hii ni kauli ya Salafu…!

Wala hatutamwambia ila kauli yake (s.w.t.):

تَلْبِسُونَ الْحَقَّ بِالْبَاطِلِ وَتَكْتُمُونَ الْحَقَّ وَأَنْتُمْ تَعْلَمُونَ {71}

“Kwa nini mnachanganya haki na batili, na mnaficha haki hali mna- jua?!”
(Surat Aali Imran: 71)

إِنَّ الَّذِينَ يَكْتُمُونَ مَا أَنْزَلْنَا مِنَ الْبَيِّنَاتِ وَالْهُدَىٰ مِنْ بَعْدِ مَا بَيَّنَّاهُ لِلنَّاسِ فِي الْكِتَابِ ۙ أُولَٰئِكَ يَلْعَنُهُمُ اللَّهُ وَيَلْعَنُهُمُ اللَّاعِنُونَ {159}

“Hakika wale wanaoficha tuliyoyateremsha katika dalili zilizo wazi na mwongozo, baada ya sisi kuzibainisha kwa watu Kitabuni, hao hulaaniwa na Mwenyezi Mungu, na hulaaniwa na wenye kulaani.” (Surat Al-Baqarah: 159)

Kwa ajili hiyo wanavyuoni wa wakati wake hawakuinyamazia kauli yake, na walitoa fatwa na kuwafanya watu wamchukie, mpaka alifungwa na alizuiliwa kuandika ndani ya jela, na alikufa jela huko Damascus kwa ajili ya itikadi yake mbaya na rai yake ya kipekee. Wanachuoni wengi na mahafidhu waliipinga. Na Dhahabi alimtumia risala akimlaumu katika hiyo risala kwa aliyoyaleta miongoni mwa itikadi alizoleta, nayo ni ndefu, tutatosheka na baadhi ya shuhuda. Allama Amini ameiandika kwa urefu wake wote katika kitabu al-Ghadiir Juz. 7, Uk. 528…akinakili kutoka kwenye kitabu Takmilatu Saifus-Swaqiilu cha Kauthariy Uk. 190.

“Kufeli kulioje kwa mwenye kukufuata, kwani atakuwa yuko kwenye hatari ya uzandiki na kuchanguka, na hasa anapokuwa na elimu ndogo na dini kidogo, mwenye undani na utashi mbaya wa nafsi. Lakini yeye atakunufaisha na atapigana kwa ajili yako kwa mkono wake na ulimi wake, na kwa undani ni adui yako kwa hali yake na moyo wake. Je si wengi miongoni mwa wafuasi wako, kuna ambaye ni bwete aliyefungwa mwenye akili nyepesi? Au mtu wa barabarani mwongo sana pumbavu wa akili? Au mgeni mkimya mwenye vitimbi sana? Au mgumu muovu asiye na fahamu? Ikiwa hautonisadiki basi wapekue na wapime kwa uadilifu.....”

Na imekuja katika kitabu ad-Durarul-Kaminah cha Ibnu Hajar al- Asqalaniy Juz. 1, Uk. 141: “Kutoka huku na kule walimpinga yeye na kilichozushwa na mkono wake muovu miongoni mwa uzushi usio na maana na rai zilizozushwa, za aina ya pekee, zilizo mbali na Kitabu Kitukufu na Sunna, Ijmai, na Kiyasi. Na palinadiwa huko Damascus kuwa: Mwenye kuwa na itikadi ya Ibnu Taymiyya damu yake na mali yake ni halali.”

Na al-Hafidh Abdul-Kafiy as-Sabakiy, ametunga kitabu kumpinga Ibnu Taymiyya alichokiita Shifaul-Asqami Fii Ziyarati Khayril-Anami (a.s.). Na amesema katika hotuba ya kitabu chake Ad-Duratu al-Mudhwiia Fii Radi Ala Ibn Taymiyya: “Amma baad, ni kwamba Ibnu Taymiyya alipozua aliyoyazua katika misingi ya itikadi, na akatangua miongoni mwa nguzo za uislamu, misingi na makubaliano, hali akiwa mwenye kujisitiri kuwa ni mfuasi wa Kitabu na Sunna, akijionesha kuwa ni mlinganiaji wa haki, mwenye kuongoza kuelekea Janna.

Kwa kufanya hivyo akatoka na kuwa mbali na ufuataji, na akawa mzushi. Na akawa pekee mbali na jamaa ya waislamu kwa kuhalifu Ijmai, na amesema yanayolazimu Mungu kuwa na kiwiliwili na mpandano wa viungo katika kuundika Dhati takatifu. Na kwamba kuhitajia sehemu si muhali. Na amesema matukio huingia katika Dhati ya Allah (s.w.t.) …”43

Na makumi ya wanachuoni waliompinga, nafasi haitoshi kufuatilia maneno yao na kuelezea kauli zao. Katika kuhitimisha twatosheka na kauli ya Shihabu Diyni Ibn Hajar al-Haithamiy. Amesema katika wasifu wa Ibnu Taymiyya: “Ibnu Taymiyya ni mja ambaye Mwenyezi Mungu amemtelekeza na amempoteza, amemfanya kipofu, kiziwi, na amemdhalilisha. Kwa ajili hiyo maimamu walieleza waziwazi kuharibika kwa hali zake, na walizikadhibisha kauli zake.
Mwenye kutaka hayo yampasa amsome Imam mujtahidu ambaye uimamu wake umeafikiwa na utukufu wake, na kufikia daraja ya ijtihadi Abul Hasan as-Sabakiy na mwanawe Taji na Sheikh al-Imamu Al-Izzi bin Jamaa, na watu wa zama zake na wengine miongoni mwa mashafii na mamaliki na mahanafii. Na wala hakuishia upinzani wake kwa Salafu masufi waliokuja nyuma bali alimpinga hata mtu mfano wa Umar bin Al-Khattab na Ali bin Abu Talib (r.a.).

“Kwa jumla maneno yake hayapewi uzito wowote bali hutupwa kwenye kila ardhi ngumu na ya miinuko, na yaaminika kuwa yeye ni mtu wa bidaa mpotovu, mpotoshaji aliyevuka mipaka. Mwenyezi Mungu amtendee kulingana na uadilifu Wake, na atuepushe na njia mfano wa njia yake na itikadi yake, na matendo yake, amiin!” Aliendelea mpaka akasema: “Kwa kweli yeye katika kuthibitisha ni mwenye kusema upande (Yaani Mungu yupo upande maalumu), na ana sehemu, na yawalazimu wanamadhehebu hii kumnasibisha Mwenyezi Mungu na kiwiliwili, na mlingano na utulivu.”44

Tutosheke na kiasi hiki kumhusu Ibnu Taymiyya, na tutazungumzia baadhi ya fikra zake kwa uchambuzi wa kielimu na kuzipa majibu tutakapozungumzia uwahabi, kwa sababu huo ni uendeleaji wa kihistoria wa itikadi ya Ibnu Taymiyya, ambayo nayo kwa mchango wake ni kuendelea kwa itikadi ya Mahanbali.

Mtu huyu ametumia fani katika kuchanganya haki na batili, kwa ajili hiyo walimdhania baadhi ya waislamu kuwa ni mtu wa kheri, wakamwita Sheikhul-Islam, jambo lake likawa mashuhuri na kuenea, vinginevyo ni batili tupu haina wa kuinusuru. Amirul-Mu’minin (a.s.) alikwishasema kuhusiana na hilo: “Kwa kweli chanzo cha kutokea fitna ni kule kufuatwa matamanio ya nafsi, na kuzushwa kwa hukumu inayokhalifu Kitabu cha Allah. Na watu kuwafanya watu mawalii kwa yasiyokuwa ya dini ya Mwenyezi Mungu. Lau batili haingechanganyika na haki, haingefichika kwa wenye kuitafuta. Na lau haki ingeepuka kufunikwa na batili zingekatika ndimi za wakaidi.

Lakini huchukuliwa mchanganyiko kutoka hili na mchanganyiko wa hili na huchanganywa, hapo Shetani huchukua nafasi kwa wapenzi wake, na wataokoka ambao wametanguliwa na wema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.”45

Tatu: Hatua Ya Muhammad Bin Abdul’wahabi:

Ibn Abdul’wahabi alikuwa mfanya upya wa itikadi ya Mahanbali baada ya kunyweshwa moyoni mwake fikra ya Ibnu Taymiyya. Hapo alitangaza harakati zake huko Najdi na ilianza harakati yake katika eneo ambalo lilishuhudia aina mbaya mno ya ukandamizaji, dhuluma, mauwaji na watu kufurushwa.

Na itikadi kavu ya kihanbali ilifikia ukubwa na utukufu wake na iliingia katika wigo wake wa utekelezaji kwa ukweli wa nje, kwa mara ya kwanza katika historia yake baada ya kuzipita hatua mbili ambazo haikupata katika hatua mbili hizo hadhi kubwa na kutiliwa maanani. Na sababu ya hali hiyo ni kuwa Ashaira baada ya Ahmad bin Hanbal tu walihodhi uwanja wa kiitikadi.

Ama katika hatua ya pili: Kwa kweli Ibnu Taymiyya alikosa nafasi ya dhamana ya kufanikisha daawa yake kwa kuwa yeye aliitangaza itikadi yake katika mazingira ya kielimu, walikuwepo humo wanavyuoni na wanafiqhi wakubwa, hivyo walizimisha kelele zake kwa dalili na uthibitisho, walimpinga usoni pake upinzani uliozimisha daawa yake na kubatilisha vitimbi vyake, na utawala pia ulikuwa unawanusuru wanachuoni katika makabiliano yao na yeye.

Hivyo mbegu ya ufisadi haikuwa na hadhi isipokuwa kujificha katika kunjo za vitabu, au kufuzu katika wagonjwa wa moyo.46
Kinyume na hivyo mazingira yalikuwa katika utayarifu kwa Muhammad bin Abdil’wahabi kuzitangaza fikra zake na sumu yake katika umma.

Kwani ujinga na kutojua kusoma na kuandika kulienea kila mahali katika wilaya za Najdi, kuongezea juu ya hapo ni kule kuwepo utawala wa familia ya Saudi ambao wenyewe binafsi ulitawalia kueneza daawa hii kwa upanga. Kwa sababu hizo waliwachukua watu kimabavu kuamini Uwahabi.

Wasiofanya hivyo walihukumiwa kuwa makafiri na washirikina na walihalalisha mali zao na damu zao. Mawahabi wakijitakasa kwa matendo hayo kwa kutumia baadhi ya itikadi mbaya chini ya anwani ya Tawhid sahihi.

Muhammad bin Abdil’wahabi anaanza maneno kuihusu Tawhid kwa kauli yake: “Nayo ni aina mbili: Tawhidi ya urabi, na Tawhid ya uungu. Ama Tawhidu ya urabi anakiri tawhidi hii kafiri na mwislamu. Ama Tawhidi ya uungu ndiyo kitenganishi kati ya ukafiri na uislamu.

Hivyo basi yatakikana kila mwislamu apambanue kati ya hii na hii, na atambue kuwa makafiri hawakatai kuwa Allah ndiye muumba mtoa riziki mratibu.

“Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema:

قُلْ مَنْ يَرْزُقُكُمْ مِنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّنْ يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَنْ يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَنْ يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ {31}

“Sema: Ni nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini? Au ni nani anayemiliki kusikia na kuona? Na ni nani anayemtoa hai kutoka maiti, na akamtoa mfu katika uzima? Na ni nani atengenezaye mambo yote? Basi watasema: Ni Allah. Waambie basi: Je, hamumchi Mwenyezi Mungu?” (Sura Yunus: 31).

Na amesema:

وَلَئِنْ سَأَلْتَهُمْ مَنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ لَيَقُولُنَّ اللَّهُ ۖ فَأَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ {61}

“Na kama ukiwauliza ni nani aliyeumba mbingu na ardhi na akavitiisha jua na mwezi? Bila shaka watasema Allah” (Surat Ankabuti: 61)

“Ikikuthibitikia kuwa makafiri wanakiri hilo, utatambua kuwa kauli yako haumbi wala hapandi riziki isipokuwa Mwenyezi Mungu, wala haendeshi jambo ila Allah, haikufanyi uwe Mwislamu, mpaka useme: La ilaha illa llahu pamwe na kuyatendea kazi maana yake.”47

Na kwa uelewa mdogo wa juujuu kama huu ambao hautokani ila na ujinga dhidi ya hekima za Mwenyezi Mungu na Aya Zake, anazikufurisha jamii zote baada ya kuufikia mradi wake kwa kauli yake: “Kwa kweli washirikina wa zama zetu - yaani waislamu – ushirikina wao una makini zaidi kuliko waliokuwapo kwanza, kwa kuwa wale walikuwa wanamshirikisha wakati wa raha na wanakuwa na ikhlasi katika shida, ama hawa ushirikina wao ni katika hali zote mbili kulingana na usemi wa Mwenyezi Mungu (s.w.t):

فَإِذَا رَكِبُوا فِي الْفُلْكِ دَعَوُا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ إِذَا هُمْ يُشْرِكُونَ {65}

“Na wanapopanda katika jahazi, wanamuomba Mwenyezi Mungu, wakimtakasishia utii, lakini anapowafikisha salama barani, mara wanamshirikisha.” (Surat Ankabuti: 65).”48

Hivyo basi kila anayefanya tawasulu kupitia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) na Ahlul-Bayt wake (a.s.) au kuzuru mahali mwao, yeye ni mshirikina aliye kafiri, na ushirikina wake ni mkubwa mno kuliko ushirikina wa waabudia Laat, na Uzza, Manata na Hubal.

Chini ya itikadi hii ziliuwawa nafsi, zikaporwa mali, wakabakwa wajakazi miongoni mwa waislamu wa Najdi na Hijazi, huku kaulimbiu yao ikiwa: “Ingia uwahabi vinginevyo kuuliwa ni kwako, na ujane kwa wake zako na uyatima kwa watoto wako.”

Na anasema nduguye, yaani Sulayman bin Abdil’wahabi akimpinga ndani ya kitabu as-Swawaaiqul-Ilahiya Fii Raddi Alal-Wahabiyah: “Imetokea kabla ya zama za Imam Ahmad katika zama za maimamu wa kiislamu mpaka imejaa miji yote ya kiislamu wala haijaelezwa kutoka kwa mmoja yeyote miongoni mwa maimamu wa kiislamu kuwa walikufurisha kwa hilo wala hawakusema kuwa hao ni murtadi wala hawakuamuru wapigwe vita, wala hawakuziita nchi za kiislamu kuwa ni nchi za kishirikina na kuwa ni nchi za vita kama mlivyosema nyinyi. Bali mmemkufurisha asiyeweza kukufurishwa kwa matendo haya japo hakuyatenda.

“Na karne zinawapitia maimamu miaka mia nane, pamoja na hivyo haijaelezwa kutoka kwa mwanachuoni miongoni mwa wanachuoni wa kiislamu kuwa alikufurisha bali halidhanii hili mwenye akili, bali wallahi kauli yenu italazimu umma wote baada ya zama za Ahmad – Mungu amrehemu - wanavyuoni wake na maamiri wake na watu wa kawaida wake, wote wawe ni makafiri, walioritadi.

Kwa hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na hakika sisi ni wenye kurejea Kwake. Naomba msaada wa Mwenyezi Mungu! kisha naomba msaada, msije mkasema kama wasemavyo baadhi ya watu wenu walio wengi kuwa, kwa kweli hoja haimsuti ila nyinyi. …”49

Pia anasema katika Uk. 4: “Leo watu wamepatwa na balaa la mtu ambaye ananasibishwa na Kitabu na Sunna, na anatoa hukumu kutoka katika elimu za viwili hivyo – kitabu na Sunna - wala hamjali anayempinga. Na endapo utamtaka ayalete maneno yake mbele ya wenye elimu hatofanya, bali anawajibisha juu ya watu wafuate kauli yake na kwa ulewa wake yeye, na atakayempinga basi yeye ni kafiri kwa mtazamo wake.

Hali yeye hana sifa hata moja ya vitendo vya wenye ijtihadi wallahi, wala moja ya kumi (katika sifa hizo). Pamoja na hivyo maneno yake yanaenda na kuwavaa walio wengi miongoni mwa wajinga. Kwa hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na hakika sisi ni wenye kurejea kwake. Umma wote unapiga ukelele kwa tamko moja, lakini pamoja na haya bado hawajibu neno, bali (kwa kauli yake) wote ni makafiri majahili: Oh Allah! muongoze mpotovu huyu na mrudishe kwenye haki.”

Mahojiano Kuhusu Tawhidi Ya Urabi:

Ili tubainishe kosa analolifanya Ibnu Abdil’Wahabi kwa makusudi, na wafuasi wake wengi kuingia katika mbabaiko; na ndio msingi ambao kwao wanawakufurisha waislamu wengi mpaka hizi zama zetu, hapana budi tuziweke fikra zake juu ya meza ya utafiti na udodosi.

Na hapa tunaanza na Tawhidi inayohusu urabi: Kwa hiyo neno Rabi kulitafsiri kwa maana ya muumba, ni mbali na mradi wa Qur’ani. Kwa kuwa maana ya Rabi katika lugha na katika Qur’ani tukufu haitoki nje ya maana ya: Yule ambaye mkononi mwake mna mamlaka ya uwekaji mipango, idara na uratibu.

Na huenda maana hii ya jenasi ikaafikiana kiutekelezaji na vielelezo vingi, mfano wa malezi, urekebishaji, utawala na umiliki, wala haiwezekani kulibebesha neno Rabi maana ya uumbaji, kama ulivyofanya uwahabi ambao juu ya msingi wake wamejenga fikra za kiparamidi zilizopotoka. Na ili kosa hili lithibitike kwa uwazi njoo tuzizingatie Aya hizi za Qur’ani ili tufichue kutoka humo maana ya Rabi ndani ya Kitabu Kitukufu.
Amesema (s.w.t.):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ{21}

“Enyi watu! Mwabuduni Rabi wenu, aliyewaumba nyinyi...” (Surat Al- Baqarah: 21)

Na amesema:

قَالَ بَلْ رَبُّكُمْ رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الَّذِي فَطَرَهُنَّ{56}

“Akasema: Bali Rabi wenu ndiye Rabi wa mbingu na ardhi ambaye aliziumba” (Surat Anbiya: 56).

Kama ingekuwa Rabi maana yake ni muumba hapangekuwa na haja ya kutaja: Aliyewaumba nyinyi, au Ambaye aliziumba kwa mara nyingine. Kama si hivyo inakuwa kukariri kusiko na maana. Tukiweka neno muumba badala ya Rabi katika Aya hizi mbili, hakuna haja ya kuweka kauli yake: Aliyewaumba nyinyi au Ambaye aliziumba.

Kinyume na tusemapo kuwa maana ya Rabi ni msimamizi, au mratibu, hivyo inakuwepo haja ya kuwepo jumla ya mwisho. Hivyo basi inakuwa maana ya Aya ya kwanza: Ambaye amekuumbeni ni mratibu wenu. Na katika Aya ya pili ni kuwa: Muumba wa mbingu na ardhi ndiye mratibu humo, mmiliki wa mipango humo. Na shuhuda juu ya hayo ni nyingi nafasi ya ufafanuzi zaidi haipo.

Kwa mujibu huo usemi wake: “Ama Tawhid ya urabi anakiri tawhidi hii kafiri na mwislamu,” ni maneno yasiyo na mashiko na matamko yanayopingwa na maelezo ya Qur’ani yaliyo safi, amesema (s.w.t.):

قُلْ أَغَيْرَ اللَّهِ أَبْغِي رَبًّا وَهُوَ رَبُّ كُلِّ شَيْءٍ ۚ{164}

“Sema: Je nishike Rabi asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ndiye Rabi wa kila kitu?” (Surat An’aam: 164).

Huu ni usemi kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kumwambia mjumbe Wake (s.a.w.w.), ili aiambie kaumu yake, je mnaniamrisha nijichukulie Rabi, nikiri uungu kwake na uratibu wa asiyekuwa Mwenyezi Mungu ambaye hapana mratibu mwingine asiyekuwa Yeye, kama ambavyo ninyi mnajichukulia sanamu zenu na kukiri kuwa ndizo zinazoratibu.

Na ikiwa makafiri wanakiri kuwa uratibu au uangalizi ni wa Mwenyezi Mungu pekee, kama anavyodhania Ibnu Abdil’wahabi, Aya hii haingekuwa na maana, hivyo inakuwa imezidi na kushuka kwake ni mchezo. Kwa kuwa watu wote kulingana na dhana yake, waislamu na makafiri wanamfanyia Mungu tawhiidi katika urabi wake, wala hawamwamrishi Mtume (s.a.w.w.) amfanye asiyekuwa Mwenyezi Mungu Rabi. Na mfano wa Aya hii ni wa ile iliyoteremka kumhusu muumini wa Aali Firauni, Mwenyezi Mungu amesema:

أَتَقْتُلُونَ رَجُلًا أَنْ يَقُولَ رَبِّيَ اللَّهُ وَقَدْ جَاءَكُمْ بِالْبَيِّنَاتِ مِنْ رَبِّكُمْ ۖ{28}

“Je mtamuuwa mtu kwa sababu anasema Rabi wangu ni Allah? Na kwa hakika yeye amekuleteeni dalili za wazi zitokazo kwa Rabi wenu.” (Sura Ghafir: 28).

Na Aya kadhaa zinatilia mkazo kuwa tamko “Rabi” halimaanishi muumba, bali linamaanisha mpangaji ambaye mkononi mwake mna mamlaka ya upangaji wa mambo. Na Rabi kwa maana hii kama ambavyo Aya zinatilia mkazo, halijakuwa mahali pa maafikiano kati ya wanadamu.

Na Ibnu Abdil’wahabi hakuwa chochote ila ni mwanafunzi amfuataye Ibnu Taymiyya. Amenakili kutoka kwake fikra hii bila ya kuizingatia ndani yake, hivyo hatari yake imewaelemea vikali waislamu, kwa kuwa Ibnu Taymiyya hakuitoa fikra hii kutoka katika wigo wa istilahi na njia ya kielimu, kinyume na Ibnu Abdil’wahhabi ambaye hali ya mambo imemsaidia kuifanya fikra hii iwe katika ukweli kiutendaji na kuitekeleza kwa waislamu. Tija yake ikawa kuwakufurisha waislamu wote isipokuwa mawahabi, na ili hilo likuwie wazi tunauleta mtazamo wake kuhusu tawhidi ya Uungu.

Mahojiano Kuhusu Tawhidi Ya Uungu:

Mawahabi wanakusudia kwa tamko Tawhidi ya uungu umoja wa uungu, kuwa ibada ni ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) peke yake, kwamba haifai ashirikishwe katika ibada yake na mwingine. Na hii ndio tawhidi ambayo kwayo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewatuma manabii na mitume.

Hapana tatizo wala kilichofunikwa na vumbi kwenye ufahamu huu, na ikiwa kutakuwa na tatizo ni kwenye istilahi yenyewe, kwa kuwa neno Allah katika Qur’ani halimaanishi mwabudiwa. Hivyo tunaweza kuiita tawhidi hii kuwa ni tawhidi ya ibada, lakini sisi hatuna maneno ya kusema kuihusu istilahi ikiwa tutaafikiana katika ufahamu.

Waislamu wameafikiana juu ya wajibu wa kujiepusha na ibada ya asiyekuwa Allah (s.w.t.) na ni lazima Mwenyezi Mungu afanyiwe ibada peke yake. Lakini tofauti ipo katika kuainisha kufahamika kwa neno ibada. Na hiki ni kitu muhimu mno katika mlango huu, kwa kuwa ndipo mahali ambapo nyayo za mawahabi zimeteleza. Tukisema kuwa tawhidi halisi ni ibada kuwa ni ya Allah tu, usemi huo hautokuwa na maana endapo hatutaweka mpaka wa maana ya tamko la uja, na tujue mpaka wake na dhibiti zake, ili tuwe na kipimo thabiti ambacho kwacho tumjue mwana tawhiidi na mshirikina.

Kwa mfano ambaye anafanya tawasuli, na anazuru makaburi ya mawalii na kuwatukuza, je anahesabiwa kuwa ni mshirikina au mwanatawhidi? Na kabla ya kujibu hapana budi sisi tuwe na kidhibiti ambacho kwacho tuweze kufichua mfano halisi wa ibada kiinje na kiutendaji.

Kuhoji Fikra Ya Kiwahabi Kuhusu Uwelewa Wa Ibada:

Uwahabi umezingatia kuwa aina zote za unyenyekevu na kujitweza na kuheshimu ni ibada. Hivyo basi kila anayenyenyekea au anayejitweza kwa ajili ya kitu huzingatiwa na mawahabi kuwa anakiabudu kitu hicho, kwa hiyo mwenye kunyenyekea na kujitweza kwa nabii miongoni mwa manabii wa Allah (s.w.t.) au walii miongoni mwa mawalii Wake kwa sura yeyote ile ya unyenyekevu huwa ni mwenye kumwabudia. Kwa hiyo anakuwa ni mwenye kumshirikisha Allah (s.w.t.).

Kwa hivyo anayesafiri akikata masafa kwa minajili ya kumzuru Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) na kulibusu kaburi lake takatifu na kujipakaza nalo - mwili wake - ili kutabaruku, anazingatiwa kuwa ni mshirikina, na kadhalika anayejenga makaburi na kuba juu ya makaburi ili kuwapa heshima na kutukuza.

Ibnu Abdil’wahabi anasema ndani ya mojawapo ya risala zake: “Mwenye kukikusudia kitu kama vile kaburi, mti, nyota au malaika aliyekurubishwa au Nabii aliyetumwa, kwa ajili ya kumletea manufaa au kuondoa dhara amekifanya kitu kile au akawa amemfanya nabii yule ni Mungu mbali na Allah, ameikadhibisha Laa ilaaha ila llahu, itapaswa aamriwe kutubia, akitubu hapana maneno, waila auliwe, japo aseme mshirikina huyu: Sikukusudia ila ni kutabaruku tu. Na mimi najua fika kuwa Allah ndiye anayenufaisha na anayedhuru.

“Mwambiye: Kwa hakika Bani Israil hawakukusudia ila ulilolikusudia, ni kama ambavyo Mwenyezi Mungu ametoa habari kuwahusu kuwa walipovuka bahari wakakuta kaumu ya watu wanafanya ibada ya sanamu zao, wakasema: “Ewe Musa tufanyie Mungu kama wao walivyo na miungu, aliwajibu kwa kauli yake: ‘Kwa kweli ninyi ni kaumu ya watu waliojingikiwa...”50

Na anasema katika risala nyingine: “......na pia mwenye kutabaruku kwa jiwe au mti au kujipangusa kwenye kaburi au kwenye kuba na kutaka baraka nao, anakuwa amewafanya wao kuwa miungu…”51

Halafu mwangalie Wahabii huyu, Muhammad Sultan al-Maasumiy, jinsi alivyowaelezea waislamu wanatawhidi ambao wanazuru kaburi la Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) wanaotabaruku na mahali pake penye tohara na wanasema: Nashuhudia kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allah. Na hakika Muhammad ni mja na Mtume Wake. Anasema kuwahusu:

“…na mja mnyonge katika ziyara zangu nne za Madina njema, niliangalia kwa makini nikaona katika msikiti wa Nabii na kwenye kaburi lake tukufu, kuna linalopingana na imani na kuuharibu uislamu na kubatilisha ibada miongoni mwa ushirikina na uabudia sanamu unaotokana na uvukaji mipaka, na kulundikana kwa ujinga na ufuataji ulioganda wa kiupofu au upendeleo ulio batili. Na aghlabu wafanyao haya yasiokubalika ni baadhi ya wageni miongoni mwa watu wa nchi mbalimbali, kutoka kwa ambaye hana ujuzi wa hakika ya dini, kwani wao wamelifanya kaburi la Nabii (s.a.w.w.) sanamu kwa mahaba ya kupita kiasi, hali wao wakiwa hawatambui.”52

Na ili uwe wazi ujinga na kuchanganyikiwa kwa Uwahabi, hapana budi utaratibu huu walioutegemea kuwa ndiyo kipimo cha kuitambua ibada utanguliwe, nao ni unyenyekevu, kujitweza na kuheshimu. Haiwezekani kisheria wala kiakili kuzifanya aina zote za unyenyekevu na kujidhalilisha kuwa ndio ibada, kwa sababu sisi tunayaona mambo mengi ayafanyayo mwanadamu katika maisha yake ya kawaida kimaumbile huingiliwa kati na unyenyekevu na kujidhalilisha. Kwa mfano: Mwanafunzi kumnyenyekea mwalimu wake na askari kwa kamanda wake, wala mtu haiwezekani athubutu kukieleza kitendo chake hiki kuwa ni ibada.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametuamuru kuonyesha unyenyekevu kwa ajili ya wazazi wawili, amesema (s.w.t.): “Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa huruma” (Surat Is’raa: 24) na hapa unyenyekevu ni unyenyekevu sana, wala haiwezekani kiitwe kitendo hiki kuwa ni ibada, bali kauli-mbiu ya mwislamu ni kujidhalilisha na kunyenyekea kwa ajili ya muumini na kujitukuza juu ya kafiri, amesema (s.w.t.):

فَسَوْفَ يَأْتِي اللَّهُ بِقَوْمٍ يُحِبُّهُمْ وَيُحِبُّونَهُ أَذِلَّةٍ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ أَعِزَّةٍ عَلَى الْكَافِرِينَ{54}

“Basi hivi karibuni Mwenyezi Mungu ataleta watu atawapenda, nao watampenda, wanyenyekevu kwa waumini, wenye nguvu juu ya makafiri.” (Suratul-Maida: 54).

Hivyo basi ikiwa kujidhalilisha kutakuwa ni ibada kulingana na uelewa wa ndugu zetu Mawahabi, basi Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atakuwa amewaamuru waumini waabudiane wao kwa wao, na hilo ni muhali.

Na kuna Aya zilizo wazi mno katika jambo hili, zinakanusha kabisa waliyodai Mawahabi. Miongoni mwazo, ni Aya inayoelezea malaika kumsujudia Adam (a.s.).

Na izingatiwe kuwa kusujudu ni daraja ya juu mno ya unyenyekevu na kujidhalilisha. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema: “Kumbuka tulipowaambia malaika msujudu kwa ajili ya Adam..(Surat Al-Baqarah: 34).

Hivyo basi ikiwa kumsujudia asiyekuwa Mwenyezi Mungu na kudhihirisha kilele cha unyenyekevu na kujidhalilisha ni ibada kama wanavyodai Mawahabi, yalazimu kulingana na dhana hiyo malaika waitwe washirikina makafiri. Basi wana nini hawaizingatii Qur’ani? Au juu ya nyoyo zao kuna kufuli?

Kwa mujibu wa Aya hii tunatambua kuwa kilele cha unyenyekevu ambacho ni kusujudu sio ibada, wala mpinzani hawezi kupinga kwa kauli kuwa: Kusujudu si kwa maana yake ya uhakika. Au mradi wa kumsujudia Adam (a.s.) ni kumfanya Qibla kama waislamu waifanyavyo Al-Kaaba tukufu Qibla.

Kwa kweli yumkini hizi mbili zote ni batili, kwa kuwa maana ya sijda kulingana na dhahiri ya Aya hii ni ile sura inayotambulika. Wala si jaizi kuipeleka kwenye maana nyingine. Ama kuifanya maana yake kuwa ni Qibla hiyo ni taawili isio na chanzo sahihi wala dalili.

Kama ambavyo kumsujudia Adam lau maana yake ingekuwa ni kwamba Adam (a.s.) ni kibla, Ibilisi hangekuwa na la kuutetea upinzani wake, kwa kuwa sijda hapa inakuwa siyo ya Adam dhati yake. Qur’ani tukufu imetilia mkazo kuwa ni kinyume na hivyo kwa kauli ya Ibilisi “Nimsujudie yule uliyemuumba kwa udongo!” Ibilisi alifahamu kutokana na amri hii ya Kiungu kuwa sijida ni ya Adam (a.s.) dhati yake, kwa ajili hiyo alipinga kwa kauli yake: Mimi ni bora kuliko yeye. Itakuwaje aliye bora amsujudiye aliye na daraja ya chini kiubora!

Na endapo yatakuwa makusudio ya kusujudu ni kumfanya Adamu Qibla hailazimu Qibla iwe bora kuliko anayesujudu. Kwa mujibu huo Adamu hatokuwa na hadhi yoyote, na hiyo ni kinyume na dhahiri ya Aya, na linalotilia nguvu hilo ni kauli ya Ibilisi: “Je nimsujudiye uliyemuumba kwa udongo? Akasema: Unaonaje, huyu ndiye umempa heshima zaidi kuliko mimi!” (Surat Israil: 61-62). Hivyo kujizuia Ibilisi asisujudu kulikuwa kwa sababu ndani ya sijda hii ya Adam (a.s.) kuna daraja na ubora mkubwa.

Siku moja mtu mmoja miongoni mwa mawahabi alinipinga katika mjadala huu, naye alikuwa amiri wa kundi la Answar Sunna katika mji wa Barbar Kasikazini mwa Sudan, kwa usemi wake: “Kwa kweli kusujudu kwa malaika kulikuwa ni kwa amri ya Mwenyezi Mungu.” Naye akiwa kwa kauli yake hii adhani kuwa amenikwamisha jiwe kooni na kuibatilisha hoja yangu. Nikamwambia: Hivyo wewe bado ungali wanga’ng’ania kuwa kitendo hiki – sijda – ni miongoni mwa mifano halisi ya ushirikina bali huo ni ushirikina hasa. Lakini Mwenyezi Mungu ameiamrisha! Akasema: Ndio. Nikasema: Je hii amri ya kiungu inaiondolea sijda ya malaika kwa Adam (a.s.) ushirikina? Akasema: Ndio.

Nikasema: Maneno haya hayana maana, wala mtu jahili hawezi yakubali sembuse mwanachuoni, kwa kuwa amri ya Mwenyezi Mungu haibadilishi dhati ya kitu wala kuigeuza maudhui yake, kwa mfano hakika dhati ya kutukana ni kudhalilisha. Endapo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atatuamuru kumtukana Firauni je hivi amri hii ya Kiungu inageuza dhati ya kutukana, na kuwa kumtukana kwetu yeye ni sifa njema na heshima kwa Firauni…?!

Pia endapo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akituharamishia kumkirimu mtu maalumu, kuharamisha huku hakubadilishi dhati ya takrima, ambayo ni kutukuza na kuheshimu na kuwe kukaribisha ni kumdhalilisha mgeni. Hivyo basi ukiizingatia sijda kuwa ni ushirikina na ni ibada, Mwenyezi Mungu akiiamrisha, amri hii haitobadilisha dhati yake, na iwe sijda kwa amri ya kiungu ni tawhidi halisi, huo ni muhali. Hivyo maneno yako yanalazimu uwatuhumu ushirikina malaika.

Kuchanganyikiwa kulidhihiri usoni kwake na alibaki kimya. Nilikatisha kimya chake nikasema: Mbele yako kuna mambo mawili, ima kimsingi sijda hii iwe nje ya wigo wa ibada, na hili ndilo tusemalo.

Au sijda hii iwe miongoni mwa mifano halisi ya wazi mno ya ibada, hivyo malaika waliosujudu walikuwa washirikina, lakini ni ushirikina ambao Mwenyezi Mungu ameuidhinisha na kuujuzisha, hili ni miongoni mwa asiloweza kulisema mwislamu mwenye akili, na linapingwa na kauli yake (s.w.t.):

قُلْ إِنَّ اللَّهَ لَا يَأْمُرُ بِالْفَحْشَاءِ ۖ أَتَقُولُونَ عَلَى اللَّهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ {28}

“Sema: Hakika Mwenyezi Mungu haamrishi mambo mabaya. Je, mnasema juu ya Mwenyezi Mungu msiyoyajua?” (Surat A’araf: 28).

Lau sijda ingekuwa ibada na ni ushirikina basi Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hangeiamuru. Pia Qur’ani imetupa habari ya kusujudu kwa nduguze Yusuf na baba yake, na sijda hii haikutokana na amri ya kiungu, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuisema kuwa ni ushirikina, na wala hakuwatuhumu nduguze Yusuf na baba yake kwa hilo. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema:

وَرَفَعَ أَبَوَيْهِ عَلَى الْعَرْشِ وَخَرُّوا لَهُ سُجَّدًا ۖ وَقَالَ يَا أَبَتِ هَٰذَا تَأْوِيلُ رُؤْيَايَ مِنْ قَبْلُ قَدْ جَعَلَهَا رَبِّي حَقًّا ۖ{100}

“Na akawanyanyua wazazi wake na kuwaweka katika kiti chake na wote wakaporomoka kumsujudia, na akasema: Ewe baba yangu, hii ndio tafsiri ya ndoto yangu ya zamani. Bila shaka Mola wangu Mlezi amehakikisha.” (Sura Yusuf: 100)

Ndoto hii ni ile iliyokuja katika Aya ya nne:

إِذْ قَالَ يُوسُفُ لِأَبِيهِ يَا أَبَتِ إِنِّي رَأَيْتُ أَحَدَ عَشَرَ كَوْكَبًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ رَأَيْتُهُمْ لِي سَاجِدِينَ {4}

Yusufu alipomwambia baba yake: Ewe baba yangu hakika mimi nimeona nyota kumi na moja na jua na mwezi, nimeviona vikinisujudia.” (Sura Yusuf: 4)

Mwenyezi Mungu swt. amefanya taabiri kama hii ya sijda kwa ajili ya Yusuf katika sehemu mbili, kutokana nazo hufaidisha kuwa sijda yenyewe peke yake au tendo lolote lioneshalo unyenyekevu, kujidhalilisha na kutukuza sio ibada.

Kwa mantiki hiyo haitowezekana tumuite mwislamu yule mwana tawhidi ambaye anaonesha unyenyekevu na kujidhalilisha kwenye kaburi la Mtume wa Mwenyezi Mungu au makaburi ya maimamu na mawalii kuwa ni mshirikina mwenye kuliabudia kaburi, kwa sababu kunyenyekea hakumaanishi kuwa ni ibada.

Lau ingekuwa mfano wa tendo kama hili ni kuliabudia kaburi matendo ya waislamu katika Hijja mfano wa ufanyaji tawafu kuizunguka Nyumba tukufu na pia kukimbia kati ya Swafa na Marwa na kulibusu jiwe jeusi kungekuwa ibada!

Kwa kuwa matendo haya hali ya sura yake na yalivyo dhahiri hayatofautiani na kuzunguka kwenye kaburi la Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.), kulibusu au kujipaka nalo, japo kuwa hivyo tunamkuta Allah (s.w.t.) anasema: “Na waizunguke Nyumba ya kale.” (Surat al-Hajj: 29) Na amesema:

إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِنْ شَعَائِرِ اللَّهِ ۖ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَنْ يَطَّوَّفَ بِهِمَا ۚ{158}

“Hakika Swafa na Marwa ni miongoni mwa alama za Mwenyezi Mungu, basi mwenye kuikusudia Nyumba au kuizuru, si vibaya kuizunguka.” (Surat Al-Baqarah: 158)

Je waona kuyazunguka mawe na udongo ni kuyaabudu? Lau ingekuwa aina yoyote ya unyenyekevu ni ibada ingelazimu vitendo hivi viwe ibada, wala amri ya kiungu hapa haiwi upenyo, kama tulivyokwisha weka wazi kuwa amri ya kiungu haibadilishi hakika ya kitu au kitendo.

Lakini tatizo la mawahabi ni kwamba wao hawakuifahamu ibada wala hawajatambua kiini na uhakika wake, hivyo wao hujihusisha tu na maana ya juu juu na sura ya nje ya tamko.

Hivyo wamuonapo yule mfanya ziara anabusu mahali alipozikwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) akili zao zinakwenda kwa yule mshirikina ambaye analibusu sanamu lake, hivyo hutolewa hukumu kutokana na hali ile ya kiakili na kuinasibisha kwa yule mwana tawhidi anayebusu sehemu aliyozikwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.), na hii ni kushabihisha, ni kosa la kutopambanua kati ya suala moja mbali na lingine.

Lau ingekuwa sura ya nje peke yake yatosha kuitolea hukumu ingekuwa wajibu juu yao hao mawahabi wamkufurishe kila anayebusu jiwe jeusi, lakini ukweli ulivyo sio hivyo, kwa kuwa mwislamu kulibusu jiwe jeusi ni Tawhidi halisi, na kafiri kulibusu sanamu huhesabika kuwa ni ushirikina halisi.

Tofauti ni nini? Kuna udhibiti mwingine ambao kwa huo tunaifafanua ibada nao ni:

Utambulisho Wa Ibada Kwa Uwelewa Wa Qur’ani:

Ibada ni unyenyekevu kwa njia ya tamko au tendo kwa itikadi ya uungu wa mwabudiwa au kuwa yeye ndio Rabi, au itikadi kuwa anajitegemea katika kitendo chake au ni kuwa yeye anamiliki hali miongoni mwa hali za kuwepo kwake au uhai wake kwa namna isiyo tegemezi. Hivyo basi kila tendo lenye kuwa na itikadi hii linahesabiwa kuwa ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu. Kwa minajili hiyo tunawakuta washirikina wa zama za jahiliya walikuwa wanaitakidi uungu wa walivyokuwa wanaviabudia. Qur’ani imebainisha hilo, amesema Taala: “Na walifanya waungu badala ya Mwenyezi Mungu ili wawe nguvu kwao.” (Sura Maryam: 81). Yaani hawa walikuwa wanaitakidi uungu wa waabudiwa wao.

Mwenyezi Mungu amesema:

الَّذِينَ يَجْعَلُونَ مَعَ اللَّهِ إِلَٰهًا آخَرَ ۚ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ {96}

“Ambao wanaofanya kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu, mungu mwingine basi karibuni watajua.” (Sura Hijri: 96)

Hivyo Aya hizi zinawarudisha mawahabi nyuma kwa kuwa zinabainisha kuwa ushirikina ambao waliokuwa wanauingia waabudia masanamu ni upande ule wa itikadi yao ya uungu wa waabudiwa wao, na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amebainisha jambo hili katika kauli yake:

فَاصْدَعْ بِمَا تُؤْمَرُ وَأَعْرِضْ عَنِ الْمُشْرِكِينَ {94}

إِنَّا كَفَيْنَاكَ الْمُسْتَهْزِئِينَ {95}

الَّذِينَ يَجْعَلُونَ مَعَ اللَّهِ إِلَٰهًا آخَرَ ۚ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ {96}

“Basi yatangaze uliyoamrishwa na ujitenge mbali na washirikina. Hakika sisi tunakutosha kwa wafanyao dhihaka. Ambao wanaofanya kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu, mungu mwingine basi karibuni watajua (Sura Hijri: 94-96).

Aya hizi zinaoredhesha kigezo cha msingi katika suala la ushirikina, nao ni itikadi ya uungu wa mwabudiwa, kwa ajili hiyo walikanusha na walifanya kiburi dhidi ya itikdi ya tawhidi ambayo Mtume (s.a.w.w.) aliileta. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema:

إِنَّهُمْ كَانُوا إِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا إِلَٰهَ إِلَّا اللَّهُ يَسْتَكْبِرُونَ {35}

“Hakika wao walipokuwa wakiambiwa: Hakuna aabudiwaye isipokuwa Mwenyezi Mungu tu, wakijivuna.” (Sura Safaati: 35).

Kwa minajili hiyo kwao wito wa manabii ulikuwa ni kuipiga vita itikadi yao ya mungu asiyekuwa Allah (s.w.t.), kwa kuwa kiakili inazuilika kumwabudu usiyeamini uungu wake, hivyo kwanza mtu huamini kisha ndipo pili huabudu. Amesema (s.w.t.):

يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّهَ مَا لَكُمْ مِنْ إِلَٰهٍ غَيْرُهُ{59}

“Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu; nyinyi hamna Mungu ila yeye.”
(Sura Aaraf: 59).

Kwa hilo Qur’ani tukufu imebainisha kupotoka kwao kando na Mungu wa kweli.

Hivyo kigezo katika ushirikina, ni kule kunyenyekea kulikoambatana na itikadi ya uungu. Na ushirikina waweza kuwa tija ya itikadi ya urabi wa mwabudiwa, yaani kuamini kuwa yeye ni mmiliki wake, mwenye kutawalia mambo yake kuanzia riziki, uhai hadi kifo, au yeye ni mmiliki wa uombezi na maghfira. Hivyo basi anayekinyenyekea kitu hali akiamini urabi wake, huwa ni mwenye kukiabudia.
Kwa minajili hiyo Aya za Qur’ani zimekuja zikiwalingania makafiri na washirikina kumwabudia Rabi wa kweli.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema:

وَقَالَ الْمَسِيحُ يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اعْبُدُوا اللَّهَ رَبِّي وَرَبَّكُمْ ۖ{72}

“Na Masihi alisema: Enyi wana wa Israili! Mwabuduni Mwenyezi Mungu Rabi wangu na Rabi wenu.” (Surat al- Maida: 72)

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema:

إِنَّ هَٰذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاعْبُدُونِ {92}

“Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Rabi wenu, kwa hiyo niabuduni.” (Surat Anbiyaa: 92).

Na kuna kigezo cha tatu, nacho ni kuamini kuwa kitu kwa dhati yake kinajitegemea au kinajitegemea katika vitendo vyake bila ya kumtegemea Mwenyezi Mungu, hivyo basi unyenyekevu wowote unaoambatana na itikadi kama hii wahesabiwa kuwa ni ushirikina.

Kwa mantiki hiyo endapo utanyenyekea mbele ya mtu kwa kumzingatia kuwa ajitegemea katika kutenda kwake, sawa kitendo hicho kiwe miongoni mwa vitendo vya kawaida mfano wa kuongea na kutikisika au mfano wa miujiza ambayo manabii walikuwa wakiifanya, unyenyekeaji huu huwa ni ibada. Lau mtu akiamini kuwa kidonge cha kuponya maumivu ya kichwa kinaponya chenyewe peke yake mbali na uwezo Wake Mwenyezi Mungu (s.w.t.), itikadi hii huwa ni ushirikina.

Kwa minajili hiyo tunatambua kuwa zingatio katika ibada, ili ihesabike kuwa ni ushirikina au si ushirikina sio kudhihirisha unyeyekevu na kujidhalilisha peke yake, bali zingatio sahihi ni kunyenyekea na kujidhalilisha kwa kauli au kitendo kwa anayeaminiwa kuwa ni Mungu au Rabi au mwenye kukimiliki kitu na hali zake kwa namna ya kujitegemea.

Imani Ya Kujitegemea Na Kutojitegemea, Ni Kigezo Kati Ya Tawhid Na

Ushirikina:

Ninatilia mkazo maana hii kwa sura ya kujitegemea, kwa kuwa katika hilo kuna nukta ya kina, ambayo huzingatiwa kuwa ni kitenganishi kati ya tawhidi na ushirikina, ambacho mawahabi hawajakisitukia, nacho hapana budi kitambuliwe ili tujue jinsi ya kuitendea kazi mienendo ya kimaumbile na ya ghaibu.

Mawahabi wamekwenda na itikadi kuwa kutawasali na sababu za kimaumbile hakuna vumbi juu yake, kama vile kuzitumia sababu za kimada katika hali ya kawaida. Ama kutawasali na sababu za ghaibu kama kumwomba mmoja yeyote kitu kisichoweza kupatikana kwa njia ya maada na hupatikana kwa njia ya ghaibu, ni ushirikina.

Na ni dhahiri kuwa huku ni kuchanganyikiwa, kwa kuwa wamezijaalia sababu za maada na za ghaibu kuwa ndio kigezo katika Tawhidi na ushirikina. Hivyo kuichukua sababu ya kimaada inakuwa ndio tawhidi yenyewe na kuichukuwa sababu ya ghaibu ndio ushirikina wenyewe.

Tukiangalia katika desturi kwa pande zake mbili, tunakuta kuwa kigezo cha tawhidi na ushirikina kipo nje ya wigo wa hizi desturi zenyewe, bali kigezo kinarejea kwa mtu mwenyewe na aina ya kuziamini kwake desturi hizi.

Mtu anapoamini kuwa njia hizi na sababu ni zenye kujitegemea dhati yake, yaani zipo mbali na kumtegemea Mwenyezi Mungu, imani hii ndio ushirikina.

Kwa mfano, akiamini kuwa dawa fulani inaponya maradhi katika hali ya kujitegemea na kwa dhati yake, hapo amali yake itakuwa ushirikina, aina ya sababu vyovyote itavyokuwa, nyepesi au nzito, ya kimaumbile au ya ghaibu, haina maingiliano na suala lenyewe, bali msingi ni itikadi ya kujitegemea na kutojitegemea. Hivyo mtu akiamini kuwa sababu zote hazijitegemei si katika kuwepo kwake wala katika taathira yake bali zimeumbwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t.), zenye kufuata amri Yake na utashi Wake, itikadi yake hii ndio tawhidi yenyewe.

Wala siamini kuwa kuna mwislamu juu ya ardhi hii kuwa anaiamini sababu yeyote kuwa ina taathira katika hali ya kujitegemea. Hivyo basi sio haki kwetu kuwaambatanisha na ushirikina na ukafiri. Hivyo kumfaya Mtume na mawalii kuwa ni wasila kwao au kutabaruku na athari zao ili kuomba kuponywa au kitu kingine, hakuhesabiki kuwa ni ushirikina, kwa kuwa ni hali ya kimaumbile katika kuzichukua sababu mbalimbali.

Qur’ani tukufu imeongelea kuhusu sababu kwa namna ambayo baadhi ya vitu hunasibishwa kwa Mwenyezi Mungu, na mara nyingine anavinasibisha na sababu za vile vitu moja kwa moja, na miongoni mwavyo mifano hiyo yakujia.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema:

إِنَّ اللَّهَ هُوَ الرَّزَّاقُ ذُو الْقُوَّةِ الْمَتِينُ {58}

“Kwa hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mtoaji wa riziki, Mwenye nguvu, Madhubuti.”
(Surat al-Dhaariyatu: 58).

Hiyo yatilia nguvu kuwa rizki ni kwa mkono wa Mwenyezi Mungu.

Na tuiangaliapo kauli Yake (s.w.t.): “Na walisheni katika hayo na muwavishe” (Sura Nisaa: 4) Aya hii inanasibisha riziki kwa mwanadamu.

Na katika Aya nyingine yamfanya Mwenyezi Mungu kuwa ndiye mkulima halisi, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema:

أَفَرَأَيْتُمْ مَا تَحْرُثُونَ {63}

أَأَنْتُمْ تَزْرَعُونَهُ أَمْ نَحْنُ الزَّارِعُونَ {64}

“Je, mmeiona mnayoilima? Je, nyinyi mmeiotesha au tumeiotesha sisi?” (Surat al-Waqiah: 63-64)

Na katika Aya nyingine Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amejaalia sifa ya ukulima kwa mwanadamu amesema (s.w.t.): “Ukawafurahisha walioupanda, ili awakasirishe makafiri kwa ajili yao.” (Sura al- Fat’hu: 29).

Na katika Aya nyingine Mwenyezi Mungu anajaalia kufishwa kwa nafsi mkononi Mwake, amesema (s.w.t.):“Mwenyezi Mungu hupokea roho wakati wa mauti yao” (Sura Zumar: 42)

Na katika Aya nyingine anajaalia ufishaji kuwa ni kitendo cha malaika. Amesema (s.w.t.):

حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ تَوَفَّتْهُ رُسُلُنَا وَهُمْ لَا يُفَرِّطُونَ {61}

“Hata mmoja wenu anapofikiwa na mauti, wajumbe wetu humfisha nao hawalegei.”
(Surat An’aam: 61)

Na katika Aya hii Qur’ani yazingatia uombezi kuwa ni haki mahsusi ya Mwenyezi Mungu peke yake. Amesema (s.w.t.): “Sema: Uombezi wote ni kwa Mwenyezi Mungu.” (Sura Zumar: 44).

Na Qur’ani yatoa habari katika Aya nyingine kuwepo kwa uombezi wa wengine ambao si Mwenyezi Mungu (s.w.t.), kama vile malaika, amesema (s.w.t.):

وَكَمْ مِنْ مَلَكٍ فِي السَّمَاوَاتِ لَا تُغْنِي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا إِلَّا مِنْ بَعْدِ أَنْ يَأْذَنَ اللَّهُ لِمَنْ يَشَاءُ وَيَرْضَىٰ {26}

“Na wako malaika wangapi mbinguni ambao uombezi wao hautafaa chochote isipokuwa baada ya Mwenyezi Mungu kutoa idhini kwa amtakaye na kumridhia.” (Surat an-Najm: 26)

Na katika Aya hii Mwenyezi Mungu anajaalia kuyatambua yaliyo ghaibu kuwa ni jambo mahsusi kwake (s.w.t.). Amesema (s.w.t.):

قُلْ لَا يَعْلَمُ مَنْ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّهُ ۚ وَمَا يَشْعُرُونَ أَيَّانَ يُبْعَثُونَ {65}

“Sema: Hakuna aliyoko katika mbingu na ardhi ajuaye yasiyoonekana ila Mwenyezi Mungu tu, nao hawajui ni lini watafufuliwa.” (Surat an-Naml: 65)

Na tunakuta katika Aya nyingine kuwa Mwenyezi Mungu amechagua kutoka miongoni mwa viumbe Wake wajumbe ili kuwatambulisha ghaibu anaposema:

وَمَا كَانَ اللَّهُ لِيُطْلِعَكُمْ عَلَى الْغَيْبِ وَلَٰكِنَّ اللَّهَ يَجْتَبِي مِنْ رُسُلِهِ مَنْ يَشَاءُ ۖ{179}

Wala hakuwa Mwenyezi Mungu kuwajulisheni mambo ya ghaibu, lakini Mwenyezi Mungu huchagua katika Mitume yake amtakaye.” (Surat Aali Imran: 179)

Na Aya zingine mbali na hii.

Hivyo basi liangaliwalo katika Aya hizi kwa mtazamo wa mwanzo kabisa bila ya kuzingatia humfanya mtu adhanie kuwa kuna hali ya kupingana. Na ukweli wake si hivyo, bali Aya hizo zinakiri tulilolisema, nalo ni kuwa Allah (s.w.t.) ndiye mwenye kujitegemea katika kutenda kila kitu, na sababu zingine zilizobaki ambazo zifanyazo matendo hayo hayo, huyafanya kwa kufuatia na chini ya kivuli cha uwezo wa kiungu. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amefanya muhtasari kubainisha jambo hilo kwa kauli yake:

وَمَا رَمَيْتَ إِذْ رَمَيْتَ وَلَٰكِنَّ اللَّهَ رَمَىٰ ۚ{17}

“Na hukutupa wakati ulipotupa, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyetupa.” (Surat al-Anfal: 17).

Anaeleza kuwa Nabii alitupa, aliposema: Wakati ulipotupa, na hapohapo amejieleza binafsi kuwa ndiye mtupaji wa hakika: “lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyetupa,” kwa kuwa Nabii (s.a.w.w.) hakutupa ila kwa uwezo ambao Mwenyezi Mungu alimtunukia nao, hivyo yeye anakuwa mtupaji wa kufuata, yaani asiyejitegemea moja kwa moja.

Twaweza kuvigawa vitendo vya kiungu katika aina mbili: Kitendo bila kupitia sababu yoyote mfano wa ‘kuwa na kinakuwa.’ Na Kitendo kupitia sababu, mfano wa Mwenyezi Mungu kuteremsha mvua kupitia mawingu ili kuotesha mimea. Au kumponya mgonjwa kupitia dawa za tiba, na mifano mingi kama hiyo. Hivyo basi endapo mtu atajiambatanisha na kupitia sababu hizi hali akiwa anaitakidi kuwa hizi sababu hazijitegemei, mtu huyu ni mwanatawhidi, na kinyume na hivyo anakuwa mshirikina.

Uwezo Na Kutokuwa Na Uwezo, Je, Ni Kigezo Cha Tawhidi Na Ushirikina?

Mawahabi wana aina nyingine ya kuchanganyikiwa na kuingiwa na shubha katika suala la Tawhidi na ushirikina, na yashabihiana kikamilifu na ile iliyotangulia. Wanajaalia uwezo wa mwenye kuombwa na kutokuwa kwake na uwezo ni miongoni mwa vigezo vya Tawhidi na ushirikina. Endapo atakuwa na uwezo hapana mushkeli, vinginevyo atakuwa mshirikina. Na huu ni ujinga wa kipumbavu.

Jambo hili halijaingia katika Tawhidi na ushirikina, wala utafiti hapa hauvuki kwenye kupata ukiombacho au kutokukipata. Basi wamekuwaje mashupavu wa kiwahabi wanawakaripia wamfayiao ziara Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) huku wakisema: Ewe mshirikina, je Mtume wa Mwenyezi Mungu anakunufaisha chochote! Wakiwa wamesahau au majahili, nao wapo karibu mno na ujahili. Kwa kuwa manufaa na kutokuwa na manufaa hakuingiliani na Tawhidi na ushirikina.

Na huu ni mfano wa ujahili mwingine kwa mawahabi, nao ni kutojuzisha kufanya tawasuli na kuomba kutoka kwa wafu. Ibnul-Qiyami ambaye ni mwanafunzi wa Ibnu Taymiyya anasema: “Na miongoni mwa aina za ushirikina ni kuomba haja kutoka kwa wafu na kuomba uombezi kutoka kwao na kuwaelekea, na hii ndio asili ya ushirikina wa aliye mjuzi, kwa kuwa aliyekufa amali yake imekatika naye hamiliki madhara kwa nafsi yake wala manufaa.”53

Na hii ni miongoni mwa kauli za ajabu mno na ngeni, ambayo haitoki ila kwa asiyekuwa na hisa katika dini na elimu na fahamu. Basi vipi iwe kutaka kitu maalumu kutoka kwa aliye hai ndio Tawhidi, na kutaka kitu kile kile kutoka kwa maiti ni ushirikina?! Na ni wazi kuwa mfano wa kazi kama hii iko nje ya wigo wa Tawhidi na ushirikina.

Na tunaweza kuiweka katika wigo wa kufaa kwa utakaji huu na kutofaa kwake, kwa hiyo unakuwa ni utakaji usiokuwa na faida, na wala si ushirikina.

Kama tulivyokwishaishiria kuwa kigezo cha msingi katika Tawhidi na ushirikina ni itikadi, na itikadi hapa ni kwa sura ya jumla haiwi makhsusi katika hali ya uhai au umauti. Kwa mantiki hiyo ni dhahiri kuwa maneno ya Ibnul-Qiyami ni batili, na kauli yake: “Kwa hakika maiti amali yake imekatika” ikiwa kauli hii ipo sahihi maana yake haitokuwa zaidi ya kuwa kuomba kwa maiti hakuna faida, sio kuwa ndio ushirikina.

Na kauli yake: “Hamiliki madhara kwa nafsi yake wala manufaa.” Ni maneno enezi au jenasi yanamuingiza maiti na aliye hai, kwa kuwa kila ambacho kipo hakimiliki kitu chochote chenyewe binafsi, sawa kiwe hai au maiti, humiliki tu kwa idhini na irada ya Allah (s.w.t.) katika hali zote mbili, uhai na umaiti.

Na kuna mkusanyiko mwingne wa utata wao, ila tu ni mdogo si kiasi cha kuujadili, ewe msomaji waweza kuupatia jibu kulingana na ilivyokubainikia kutoka katika misingi iliyotangulia. Hivyo basi ni jaizi kwa kila mwislamu kuomba uombezi na kufanya wasila kupitia mawalii wa Mwenyezi Mungu katika jambo lolote, liwe la ghaibu au la maada, ilimradi tu awe anatunza sharti zilizotangulia kutajwa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema:

قَالَ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ أَيُّكُمْ يَأْتِينِي بِعَرْشِهَا قَبْلَ أَنْ يَأْتُونِي مُسْلِمِينَ {38}

قَالَ عِفْرِيتٌ مِنَ الْجِنِّ أَنَا آتِيكَ بِهِ قَبْلَ أَنْ تَقُومَ مِنْ مَقَامِكَ ۖ وَإِنِّي عَلَيْهِ لَقَوِيٌّ أَمِينٌ {39}

قَالَ الَّذِي عِنْدَهُ عِلْمٌ مِنَ الْكِتَابِ أَنَا آتِيكَ بِهِ قَبْلَ أَنْ يَرْتَدَّ إِلَيْكَ طَرْفُكَ ۚ فَلَمَّا رَآهُ مُسْتَقِرًّا عِنْدَهُ قَالَ هَٰذَا مِنْ فَضْلِ رَبِّي لِيَبْلُوَنِي أَأَشْكُرُ أَمْ أَكْفُرُ ۖ وَمَنْ شَكَرَ فَإِنَّمَا يَشْكُرُ لِنَفْسِهِ ۖ وَمَنْ كَفَرَ فَإِنَّ رَبِّي غَنِيٌّ كَرِيمٌ {40}

“Akasema: Enyi wakuu wa baraza! Ni nani atakayeniletea kiti chake cha enzi kabla hawajafika kwangu, hali ya kuwa wamekwisha kusilimu? Akasema Afriti katika majini: Mimi nitakuletea hicho kabla hujasimama kutoka mahala pako, na mimi bila shaka ninazo nguvu za hayo, mwaminifu. Akasema yule aliyekuwa na elimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea hicho kabla ya kupepesa jicho lako. Basi alipokiona kimewekwa mbele yake, akasema: Haya ni kwa fadhila za Rabi wangu.....” (Surat an-Naml: 38-40)

Ikiwa Sayyidina Sulayman (a.s.) aliomba jambo hili la ghaibu kwa wafuasi wake, na ikiwa mtu aliyekuwa na elimu miongoni mwa elimu ya kitabu aliweza kulitekeleza hilo, inakuwa jaizi kwetu tuombe kwa ambaye anayo elimu yote ya kitabu. Na hilo kwa kutilia mkazo kabisa lipo kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) na Ahlul-Bayt wake (a.s.).

Je Kutawasali Kupitia Nabii Na Watu Wema Ni Haramu?

Tumetambua kutokana na utafiti uliotangulia kuwa kutawasali na kuomba msaada ni vitu vipo nje ya wigo wa Tawhidi na ushirikina. Kumebaki kitu kingine nacho ni kujuzu kwa jambo hili au kuwa ni la haramu. Hajasema mwanachuo yeyote miongoni mwa wanavyuoni wa kiislamu kuwa tawassuli ni haramu, sawa iwe wanachuoni wa hapo zamani au wa hivi sasa, bali zimekuja riwaya nyingi zinazohalalisha hilo. Na ni hizi hapa kwako baadhi ya Hadithi:

Hadithi Ya Uthmani Bin Haniif:

“Kuna mtu mmoja kipofu alimjia Nabii (s.a.w.w.) akasema: ‘Mwombe Mwenyezi Mungu anipe uzima.’ Nabii akasema: ‘Ukipenda nitaomba na ukipenda fanya subira, nayo ni kheri kwako.’ Yule mtu akasema: ‘Omba.’ Nabii (s.a.w.w.) alimuamuru atawadhe na afanye wudhu wake vyema na aswali rakaa mbili na aombe kwa dua hii: ‘Oh! Ewe Allah! Kwa hakika mimi nakuomba na ninaelekea kwako kupitia Nabii wako Muhammad nabii wa rehema, ewe Muhammad kwa hakika mimi ninamuelekea Mola wangu kupitia kwako wewe katika haja yangu ili uikidhi. Ewe Allah mpe uombezi kunihusu.’ Ibnu Haniif akasema: ‘Wallahi hatukutawanyika na wala mazungumzo hayakuwa marefu kati yetu aliingia kwetu kana kwamba hakuwa na upofu.”54

Sanad ya Hadithi hii ameijadili Shaikh Ja’far Subhaniy katika kitabu chake Maal-Wahaabiyiina Fii Khutatihim Waaqaidihim na amesema: “Hapana shaka katika usahihi wa Hadithi hii na sanad yake, kiasi kwamba Imam wa kiwahabi (Ibn Taymiyya) ameutambua usahihi wa sanadi yake akisema:
‘Kwa kweli makusudio ya jina la Abu Ja’far lililokuja katika sanad ya Hadith, ni Abu Ja’far al-Khatiy na yeye ni mwaminifu. ‘“

Rufaiy ambaye ni mwandishi wa kiwahabi wa zama hizi, ambaye anafanya juhudi kuzidhaifisha Hadithi, khususan za Tawassuli, anasema kuihusu Hadithi hii: “Hapana shaka Hadithi hii ni sahihi na ni mashuhuri, na imethibiti katika Hadithi hii bila ya shaka wala wasiwasi kurejea kwa uoni wa kipofu kwa dua ya Mtume wa Mwenyezi Mungu.”55

Na Rufaiy anasema katika kitabu chake at-Tawassulu: “Na maneno haya ameyaleta an-Nasaiy, al-Bayhakiy, at-Tabaraniy, Tirmidhiy, na al-Haakim katika Mustadrak yake. Lakini Tirmidhiy na al-Haakim wameileta jumla ya ‘Ewe Allah nipe uombezi humo.’ badala ya jumla ‘Ewe Allah mpe uombezi kunihusu.’ Zayniy Dahlani ameandika katika Khulaswatul-Kalaami, ameitaja Hadithi hii pamwe na sanad zilizo sahihi, zote kutoka kwa Bukhari katika Taariikh yake, na Ibnu Majah na al-Haakim katika Mustadrak zao, kama alivyoisema Jalaludini Suyutiy katika kitabu chake al-Jaamiu.”56

Na kuna Hadith na riwaya zingine nyingi tumeacha kuzitaja kwa kutaka muhtasari. Na ukitaka ziada rejea Hadithi ya tawassuli ya Adam kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kama ilivyokuja katika kitabu Mustadrak cha al- Haakim Jalada la 2, Uk. 615, na katika ad-Durrul-Manthur. Jalada la 1, Uk. 59, ikiwa ni nukuu kutoka kwa Tabaraniy na Abu Nua’im Asfahaniy na Bayhaqiy.

Na Hadithi ya tawassuli ya Nabii (s.a.w.w.) kwa haki ya manabii waliokuwa kabla yake, kama ilivyoelezwa na Tabaraniy katika kitabu al- Kabiir na katika al-Awsat na Ibnu Habbani na al-Hakim, na wamesema ni sahihi.

Na Hadithi ya tawassuli kupitia haki ya waombaji, iliyopo ndani ya Sahih Ibnu Majah Jalada 1, Uk. 261, mlango wa misikiti. Na Musnad Ahmad Jalada la 3, Uk. 21. ..Na riwaya zingine.

Kwa kuongezea hayo lijulishalo kujuzu kwa Tawassuli ni ijmai ya waislamu na sera ya mweka sheria, kwani waislamu walikuwa toka zamani mpaka hii leo wanatawassali kupitia manabii na watu wema, na hapana mwanachuoni yeyote aliwapinga au kuharamisha hilo.

Tunatosheka na kadiri hii ya muhtasari dhidi ya itikadi za kiwahabi, kwa kuwa mjadala na wao utakuwa mrefu na wahitajia kitabu cha peke yake.

Na wanachuoni wamewajibu katika vitabu na makala nyingi. Na miongoni mwa yanayofurahisha kuyataja ni kuwa Allama Muhsin al-Amiin amewajibu mawahabi kwa njia ya kaswida ndefu yenye itikadi zao, na amezijibu ishkali zao. Kaswida yenye beti 546 ameileta mwishoni mwa kitabu chake Kashful-Irtiyabi Fii Atbaai Muhammad bin Abdil’wahaabi.

Kubabaika Kwa Ashaira

Historia imetaja kuwa Abul Hasan al-Ash’ariy alihama madrasa ya kifikra ya kimuutazila, na kutangaza kujiunga kwake na madrasa ya kifikra ya Hanbali. Lakini uhamaji huu haukutosha kuuacha kikamilifu utaratibu wa madhehebu ya kimuutazila, kwani mambo yake ya kinyumenyume yalijitokeza waziwazi katika utaratibu wake mpya. Alijaribu kuipaka rangi itikadi ya Salafi kwa rangi ya kiakili, hakupata tawfiki kwa hilo. Hivyo ni kwa sababu itikadi za Salafi ni itikadi za kusikia zinazotegemea Hadithi. Na hali yajulikana kuwa Hadithi zilizo nyingi si sahihi zimeingizwa katika turathi za kiislamu na maadui wa dini.

Hivyo basi Hadithi hizi hazikuafikiana na kanuni za kiakili, na ni miongoni mwa yaliyozusha hali ya kupingana kwa wazi katika utaratibu wa Abul Hasan al-Ash’ariy. Na tija yake ikawa ni mbabaiko mwingi alipotaka kuthibitisha itikadi za Ahlul’hadithi kwa njia ya kiakili.

Na hapa tunaonyesha sampuli moja miongoni mwa mibabaiko yake, nao watosha kuonesha uwezo wa kiakili wa kiash’ariy, nao ni suala la kumwona Mwenyezi Mungu. Ahlu Sunna wameafikiana kuwa yawezekana. Abul Hasan al-Ash’ariy na mwanafunzi wake walijaribu walitoe suala hili nje ya wigo wa Hadithi, na kuliingiza kwenye wigo wa dalili za kiakili. Kwa ajili hiyo tumewachagua wao katika mlango huu ili tubainishe rai zao.

Kwa hakika vitabu vya kisunni vimejaa riwaya za wazi kabisa katika kuonekana Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa macho. Na sampuli ya baadhi ya Hadithi hizo ni hizi hapa kwako kabla ya kuingia kwa undani katika utafiti.

“Kutoka kwa Jabir. Alisema: Tulikwa tumeketi kwa Nabii wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) na aliuangalia mwezi usiku wa tarehe kumi na nne, na akasema: “Kwa kweli ninyi mtamuona Mola wenu kama muuonavyo huu mwezi, hamtofanyiwa nuksani kumuona, basi endapo mtapenda msizidiwe kuswali kabla ya kuchomoza jua na kabla halijazama fanyeni.” Halafu alisoma:

وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ {39}

“Na mtukuze Mola Wako Mlezi kwa kumsifu kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa.” (Sura Qaf: 39)”57
Na imekuja katika Hadithi ndefu kuwa Abu Hurayra aliwapa habari kuwa: “Watu wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je tutamuona Mola wetu siku ya Kiyama? Alisema: ‘Je mnazuilika katika kuuona mwezi usiku wa kumi na nne ukiwa hauna mawingu?’ Wakasema: Hapana, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Nabii (s.a.w.w.) akasema: ‘Hamtozuilika kumuona Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama ila kama mzuilikapo kumuona mmoja wenu.’

Aliendelea mpaka akasema: ‘Mpaka itapokuwa hapana aliyebakia isipokuwa aliyekuwa anamwabudia Mwenyezi Mungu miongoni mwa wema na waovu, atawaendea Mola wa ulimwengu katika sura ya chini miongoni mwa sura zake kuliko ile waliomuona nayo, na itasemwa: Mwangojea nini? Kila umma utafuata kile ulichokuwa unakiabudu.

“Watasema: ‘Tuliwaacha watu duniani, wakiwa wahitaji mno kuliko tulivyokuwa kwao, na hatukuwa pamoja nao na hali sisi tunamngoja Mola wetu ambaye tulikuwa tunamwabudu.’ Atasema: ‘Mimi ndimi Mola wenu.’ Watasema: ‘Hatumshirikishi Mola wetu na kitu.’ mara mbili au tatu. Kiasi kwamba baadhi yao watakaribia kupinduka, atasema: ‘Je kuna alama kati yenu na yeye ambayo kwayo mtamtanbua?’ Watasema: ‘Ni muundi.’ Hapo atafunua muundi.”58

Kutoka kwa Jarir bin Abdillah amesema: “Nabii (s.a.w.w.) akasema: ‘Kwa hakika ninyi mtamuona Mola wenu bayana.”59

Na zingine miongoni mwa hadithi kadhaa ambazo zimekuja katika vitabu Sahihi. Ibnu Hajar anasema kuhusu Hadith za kumuona Allah: “Daruqutniy amekusanya Hadithi zilizokuja kuhusiana na kumuona (s.w.t.) akhera, zinazidi ishirini. Na Ibnul-Qiyami amezifuatilia katika kitabu Haadil-Arwahi zikafikia thelathini, na zilizo nyingi ni nzuri. Na Daruqutniy amefanya sanad kwa Yahya bin Muiin, amesema: ‘Nina Hadithi kumi na saba kuhusiana na kumuona, nazo ni sahihi.”60

Hivyo kwa Hadithi hizi walizozidhania kuwa ni sahihi wamejengea itikadi yao kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ataonekana Siku ya Kiyama, mpaka imamu wa kihanbali amekwenda mbali zaidi kiasi cha kumkufurisha kila aendaye kinyume na itikadi hii, na wala hakuishia kiwango hiki bali amevuka na amejuzisha uwezekano wa kuonekana (s.w.t.) hata hapa duniani.

Asfarayiniy amesema: “Ahlus-Sunna wameafikiana kuwa Allah (s.w.t.) atakuwa mwenye kuonekana kwa waumini Akhera. Na wamesema kuwa kuonekana kwake ni jaizi kwa hali yeyote, na kwa kila aliye hai kwa njia ya akili, na ni wajibu kila muumini kumuona khususan Akhera kwa njia ya khabari.”61

Bali wamesema hutokea kumuona usingizini. Wamefanya madai ya uwongo na uzushi kuwa wa kwanza aliyemuona Mola wake usingizini ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.), maelezo ya habari hizi yametangulia.

Na baada ya hayo wanavyuoni wao wamekuwa wakifanya madai ya kumuona Mwenyezi Mungu (s.w.t.) usingizini. Sha’araniy, Ibnul-Jawziy, na Shablanjiy wameeleza kutoka kwa Abdillah bin Ahmad bin Hanbali, amesema: “Nilimsikia baba yangu akisema: ‘Nimemuona Mola wa enzi aliyetukuka usingizini nikasema: ‘Ewe! Mola wangu, ni kitu gani walichojikurubisha nacho wenye kujikurubisha Kwako?’ Akasema: ‘Maneno yangu ewe Ahmad.’ Nikasema: ‘Ewe Mola wangu pamwe na ufahamu au bila ya ufahamu?’ Akasema: Pamoja na ufahamu au bila ya ufahamu.”62
Na Alusiy ndani ya tafsi yake Ruhul-Maaniy anadai kumuona Mwenyezi Mungu mara tatu: “Walilahi taala alhamdu nimemuona Mola wangu usingizini mara tatu, na mara ya tatu ilikuwa mwaka 1246 A.H. Nilimuona Jalla Shaanuhu akiwa na nuru ilioje, akielekea upande wa Mashariki. Alinisemesha maneno niliyasahau nilipoamka.

Na mara nilimuona katika usingizi mrefu kana kwamba nipo Peponi nikiwa mbele yake Taala, kati yangu na Yeye kuna pazia iliyofumwa kwa lulu ya rangi tofauti. Subhanahu aliamuru aende na mimi mahali pa Isa (a.s.), halafu mahali pa Muhammad (s.a.w.w.), basi alikwenda na mimi kwao, na niliona niliyoyaona, na upaji fadhila ni wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.).”63

Huu ni muhutasari wa itikadi zao kuhusu kumuona Mwenyezi Mungu (s.w.t.). Mwenyezi Mungu ametukuka utukufu mkubwa mno, yu mbali na wayasemayo.

Na ni wazi kuwa itikadi hii bila shaka inalazimu kwa uchache tu wa fikra haya yafuatayo:

a) Uoni wa hisia unaokazaniwa na Hadithi hizi walazimu kionwacho kiwe ni mwili wenye unene na rangi ili uoni uweze kutimia. Kwa kuwa miongoni mwa lazima za kuona ni kiwe kionwacho ni kitu chenye mwili, ambao humo hupatikana akisi ya mwanga, na ni lazima pia kionwacho kiwe mkabala, au ukitaka sema upande wa mbele wa mwonaji, na kuwe na masafa kati ya mwonaji na kionwacho, ukiongezea usalama wa hisia yenyewe. Na kwa sharti hizi ndio Mwenyezi Mungu inabidi awe. Yaani Mwenyezi Mungu inabidi awe mwili wenye rangi na wenye mpaka na mahali. Na hayo ni muhali kumhusu Mwenyezi Mungu.

b) Na pia inabidi Mwenyezi Mungu awe anabadilika badilika na kuchukua sura tofauti “Mwenyezi Mungu atawajia katika sura sio ile walikuwa wanamjua, na atawaambia: Mimi ndimi Mola wenu, watakuwa wanasema: Tunajikinga kwa Mwenyezi Mungu dhidi yako, hapo basi atawajia katika sura wanayomjua.” Na njia wanayomjua nayo ni muundi, hufunuliwa na hufunikwa…!!

Na itikadi hizi zinazolazimu ukafiri uliowazi ni tija ya kawaida ya Hadithi za Israiliyati ambazo wamezikumbatia ndugu zetu Ahlu Sunna, kwa sababu ya ujio wa Hadithi hizo ndani ya Bukhari na Muslim. Kuvitakasa vitabu viwili hivi kwatangulizwa kabla ya kumtakasa Mwenyezi Mungu (s.w.t.). Lau si hadithi hizi akili iliyo salama haingekwenda kwenye kauli hii.

Kwa minajili hiyo tunawakuta Ahlul-Bayt (a.s.) walisimama kidete dhidi ya itikadi kama hizi na dhidi ya kila itikadi ambayo inakuwa sababu ya itikadi za kumnasibisha Allah na kiwiliwili, na kumshabihisha na viumbe.

Na walizikadhibisha Hadith hizo ambazo ameziingiza Kaabul Akhbaar Myahudi, na Wahabu bin Munabih Myamaniy, ambao ndio watu waliozieneza kwa wingi fikra za Allah kuwa na mwili na kumwona. Na fikra hii imejaa ndani ya vitabu vya Ahlul’kitabi, nayo iko mbali mno na maarifa ya Qur’ani.

Dondoo la maneno: Kwa kweli Hadithi hizi japo ziwe nyingi hazina thamani katika misingi ya itikadi baada ya hukumu ya akili. Na endapo tutalegeza msimamo na kukubali kuingia kwake katika nyanja za mgawanyo wa fikra za kiitikadi, zitakuwa zinakabiliwa na kundi kubwa la riwaya zenye kusaidiana zenye kuenea kutoka kwa Ahlul-Bayt (a.s.) zinazokataa fikra ya Allah kuwa na kiwiliwili, na yanayo lazimiana nazo, kama kumwona na rangi, na kila aina za kumzingira Allah (s.w.t.).

Mifano Ya Hadithi Za Ahlul-Bayt Kukanusha Kuonekana

Mwanahadith Abu Qurah aliingia kwa Abul Hasan ar-Ridhaa (a.s.) na aka- muuliza mambo ya halali na haramu na hukumu mpaka swali lake lilifikia Tawhidi, Abu Qurah akasema: “Kwa hakika sisi tumezieleza riwaya kuwa Allah amegawanya maono na maneno kati ya wawili, Musa (a.s.) alim- gawia kusema na Muhammad (s.a.w.w.) kuona.”

Abul Hasan (a.s.) akanena: “Basi ni nani aliyewafikishia majini na watu kutoka kwa Mwenyezi Mungu:

لَا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ {103}

“Maono hayamfikii, bali yeye anayafikia maono, naye ni Mwenye kujua, Mwenye habari.” (Surat An’aam: 103)

Wala hawawezi kumjua(Sura Twaha: 110), je sio Muhammad (s.a.w.w.)?

Alisema Abu Qurah: ‘Ndio.’ Akanena (a.s.) “Vipi mtu awajie viumbe wote na awape habari kuwa atoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba yeye anawalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa amri ya Allah na anasema:

لَا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ {103}

“Maono hayamfikii, bali Yeye anayafikia maono, Naye ni Mwenye kujua, Mwenye habari.” (Surat An’aam: 103);

Wala hawawezi kumjua” (Sura Twaha: 110) halafu yeye aseme: Mimi nimemwona kwa jicho langu, na nimemzunguka kwa elimu, na Yeye (s.w.t.) yuko katika sura ya kibinadamu!! Hamuoni haya? Mazandiki hawakuweza kumsingizia haya, awe analeta kutoka kwa Allah kitu, halafu anaamini kwa sura nyingine!!”

Abu Qurah akasema: Kwa hakika Yeye (s.w.t.) anaseama: “Na bila shaka yeye amemwona kwa mara nyingine.” (Sura Najm: 13). Abul Hasan (a.s.) akasema: “Kwa kweli kabla ya Aya hii kuna linalojulisha ali- chokiona, aliposema: “Moyo haukusema uwongo uliyoyaona.” (Sura Najim: 11)

Anasema: Moyo wa Muhammad (s.a.w.w.) haukukosea kutambua kilichoonwa na macho yake, halafu alitoa habari ya alichokiona, ali- posema: “Kwa hakika aliona katika dalili za Mola wake zilizo kuu.” (Sura Najm: 18) na dalili za Mwenyezi Mungu sio Mwenyezi Mungu, na kwa kweli akasema: Wala hawawezi kumjua” (Sura Twaha: 110), ikiwa macho yatamuona yatakuwa yamemzunguka, kumjua na kumtambua kikamilifu.”

Abu Qurah akasema: Hivyo wazikadhibisha riwaya? Abul Hasan (a.s.) ali- nena: “Endapo riwaya zitakuwa kinyume na Qur’ani mimi nitazikad- hibisha. Na lile ambalo waislamu wameafikiana ni kuwa hazungukwi na elimu ya kiumbe, wala macho hayamfikii na wala Yeye si mfano wa kitu.”64

Abu Abdillah bin Sinan alikuwa hadhiri kwa Imam Abu Ja’far (a.s.), punde aliingia kwake (a.s.) mtu mmoja miongoni mwa Khawarij, akamwambia: “Ewe Abu Ja’far! Kitu gani wakiabudia?” Alisema (a.s.): “Allah.” Yule mtu akasema: “Umemwona?” Alisema (a.s.): “Hajaonwa na macho kwa kumshuhudia wazi wazi, lakini nyoyo zimemuona kwa hakika ya imani. Hatambuliwi kwa kumlinganisha wala hadirikiwi kwa hisia, wala hashabihishwi na watu. Ni Msifiwa kwa dalili, maarufu kwa alama. Hadhulumu katika hukumu Yake. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu hapana Mungu wa haki ila ni Yeye.” Abu Abdillah bin Sinan akasema: “Yule mtu alikuwa ana- toka nje huku akisema: “Mwenyezi Mungu anajua pa kuijaalia risala yake.”65
Ahmad bin Is’haq alimwandikia Abul Hasan wa tatu (a.s.) akimuuliza kuhusu kumwona (Allah) na waliyonayo watu. Na yeye (a.s.) alimwandikia:

“Kumwona haitokuwa jaizi maadamu kati ya mwonaji na kinachoonwa hakuna hewa ambayo jicho linapenya, hewa inapokatika na kukosekana mwanga kati ya muonaji na kionwacho muono hausihi, na huwa katika hali hiyo ishtibahi, kwa kuwa muonaji ni yule ambaye huwa sawa na kionwacho katika sababu inayosababisha uoni kati yao. Ishtibahi itakuwa wajibu na hilo litasababisha tashbihi, kwa kuwa sababu hapana budi ziungane na visababishi vyake.”66

Muhammad bin Ubayd alimwandikia Imam Abul Hasan ar-Ridha (a.s.) akimuuliza kuhusu kumwona na inavyoelezwa na Masunni na Shia. Aliandika (a.s.) kwa maandishi yake: “Wameafikiana wote hapana kizuizi kati yao, kuwa maarifa kwa njia ya kuona ni dharura, hivyo endapo itakuwa jaizi kumwona Mwenyezi Mungu kwa jicho, maarifa yatathibiti kwa dharura.

Kisha maarifa hayo hayatokosa, ima yawe imani au si imani, na endapo maarifa hayo kwa njia ya kuona ni imani, basi maarifa ya duni- ani ambayo ni kwa njia ya kuchuma sio imani.

Kwa kuwa maarifa hayo ni kinyume chake. Hivyo basi duniani yeyote hawezi kuwa muumini, kwa sababu wao watu wa duniani hawajamwona Mwenyezi Mungu. Na endapo yale maarifa kwa njia ya kuona sio imani, basi maarifa haya ambayo ni kwa njia ya kuchuma hayatokosa kutoweka katika miadi. Basi hii ni dalili ya kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) haonekani kwa macho, kwa kuwa jicho hulazimu tuliyoyaeleza.”67

 • 1. Al-Khutatul-Miqriziyah Juz.2.Uk.390.
 • 2. Tarikhul-Falfasafatil-Arabiyah Juz. 1, Uk. 179.
 • 3. al-Milalu Wan-Nahlu cha Shahristaniy, Juz.1, Uk. 164.
 • 4. Mir’atul-Uquul Fii Sharhi Akhbari Aalir-Rasul Juz.1, Uk. 84.
 • 5. Mir’atul-Uquul Fii Sharhi Akhbari Aalir-Rasul Juz. 1, Uk. 84.
 • 6. Zilizochomekwa na Mayahudi.
 • 7. Ni maneno ya Sayyid Rashid Ridha, mwanafunzi wa Muhammad Abduh. Tazama kitabu Adh’wau Alas-Sunnati Al-Muhammadiyah, cha Mahmud Aburiyah Uk. 23.
 • 8. Al-Milalu Wannahlu cha Shahristaniy jalada la 1,Uk.165.
 • 9. Fii Aqaidil-Islami – miongoni mwa risala za Sheikh Muhammad bin Abdil- Wahabi Uk. 155.
 • 10. Huu ni mfumo maalumu wa malezi ya kiroho, ni mfumo wa kiibada, na katika aina za usufi.
 • 11. Al-Milalu Wannahlu cha Shahristaniy jalada la 1, Uk. 105
 • 12. Kitabus-Sunna, Uk. 54.
 • 13. Kitabus-Sunna, Uk. 76.
 • 14. Kitabus-Sunna, Uk. 76.
 • 15. Kitabu-Tawhiidu Uk. 113.
 • 16. Kitabus-Sunna, Uk. 65.
 • 17. Kitabus-Sunna, Uk. 190.
 • 18. Kitabus-Sunna, Uk. 190.
 • 19. Kitabus-Sunna, Uk. 184.
 • 20. Kitabus-Sunna, Uk. 184.
 • 21. Kitabus-Sunna, Uk. 190.
 • 22. Kitabus-Sunna, Uk. 71.
 • 23. Kitabus-Sunna, Uk. 79.
 • 24. Kitabus-Sunna, Uk. 80.
 • 25. Kitabu-Tawhiidu Uk. 106.
 • 26. Kitabu-Tawhiidu Uk. 217.
 • 27. Kitabu-Tawhiidu Uk. 198.
 • 28. Ashahristaniy, Juz. 1, Uk. 105.
 • 29. At-Tawhidu cha Sheikh Saduq Uk. 44. Hadithi ya 4.
 • 30. At-Tawhidu cha Sheikh Saduq Uk. 61.
 • 31. al-Bidaaya Wan-Nihaya. Juz. 14, Uk. 5, matukio ya mwaka 698 A.H.
 • 32. Rihlatu Ibnu Batutu, Uk. 95.
 • 33. Al-Milalu Wan-Nn-ahlu Uk. 84.
 • 34. Tafsiris-Surat an-Nuur, cha Ibnu Taymiyya Uk.178-179.
 • 35. Al-Muqadima Fii Usulit-Tafsir Uk. 51.
 • 36. Tafsyiru Tabariy Juz. 3, Uk. 7.
 • 37. Tafsyiru Tabariy Juz. 3, Uk. 9.
 • 38. Al-Aqidatul-hamwiyatul-Kubra, Majmuur-Rasailul-Kubra cha Ibn Taymi Uk. 329- 332.
 • 39. Fat’hul-Qadii,r cha Shaukaniy.
 • 40. Yaani kwa maana ya Mwenyezi Mungu tu, Dhati Yake ndiyo itakayobakia kwa
  kuwa hakuna maana ya kuhiliki kila kitu na kubaki uso tu!
 • 41. Tafsyiru Tabariy Juz. 2, Uk. 82.
 • 42. Tafsirul-Baghawiy
 • 43. Al-Milalu Wan-Nahlu ya Shahrustaniy Juz. 4, Uk. 42.
 • 44. Al-Milalu Wan-Nahlu ya Shahrustaniy Juz. 4, Uk. 48.
 • 45. Nahjul-Balagha, hotuba ya 49.
 • 46. al-Milalu Wan-Nahlu cha Subhaaniy.
 • 47. Fii Aqaidil-Islam, katika jumla ya risala za Sheikh Muhammad bin Abdil’wahabi Uk. 38.
 • 48. Risalatu Arbau Qawaid cha Muhammad bin Abdul-wahabi Uk. 4.
 • 49. as-Swawaaiqul-Ilahiya Fii Raddi Alal-Wahabiyah, Uk. 38.
 • 50. Aqaidul-Islami, miongoni mwa risala za Sheikh Muhammad bin Abdul-wahabi Uk. 26.
 • 51. Aqaidul-Islami, miongoni mwa risala za Sheikh Muhammad bin Abdul-wahabi Uk. 26.
 • 52. al-Mushahadaatu al-Maasumiya Inda Qabri Khayril-Bariya Uk. 15
 • 53. Fat’hul-Majiid. Utunzi wa Mufiidu Ibnu Abdil’Wahaabi.Uk. 67, chapa ya 6.
 • 54. Sunan Ibnu Maajah. Jalada 1, Uk. 313; Musnad ya Ahmad Juz. 4, Uk. 138. al- Jaamius-Swaghiiru, Uk. 59. Talkhiisul-Mustadrak cha ad-Dhahabi.
 • 55. at- Tawassul Ilaa Hakiiqati-Tawassul. Uk. 158.
 • 56. Kashful-Irtiyabi, Uk. 309, nukuu kutoka katika Khulaswatul-Kalami; at- Tawassul Ilaa Hakiiqati-Tawasul, Uk. 66.
 • 57. Sahih Bukhari Jalada 1. Mlango wa ubora wa swala ya Alasiri. Sahih Muslim Juz. 2, Mlango wa ubora wa swala ya Adhuhuri na Alasiri.
 • 58. Sahih Bukhari Juz. 6, Tafsiri ya Sura Nisai Juz. 9, Kitabu cha Tawhidi. Sahih
  Muslim Juz. 1, mlango wa kutambua njia za kumwona.
 • 59. Sahih Bukhari Juz. 9. Kitabu cha tawhidi, kauli yake Taala “Nyuso siku hiyo zitang’aa. Zikingoja malipo kwa Mola wao.” (Sura Qiyamah: 22-23).
 • 60. Fat’hul-Bariy Fii Sharhis-Swahihil-Bukhariy Juz.13, Uk. 371.
 • 61. Alfarqu Baynal-Firaqi, Uk. 5
 • 62. Tabaqatus-Sha’araniy Juz. 1, Uk. 44. Na kutoka kwa Ibnul-Jawziy katika
  Manaqib Ahmad Uk. 343. Nurul-Abswar cha Shablanjiy, Uk. 225.
 • 63. Tafsiru Ruhul-Maaniy Juz. 9, Uk. 52 chapa ya Daru ihyai turathil-arabiy, Beirut. chapa ya 1985 A.D.
 • 64. at-Tawhidu cha Saduq Uk. 112 , Hadith ya 9 .
 • 65. at-Tawhid cha Saduq Uk. 10 , Hadith ya 1.
 • 66. at-Tawhid cha Saduq Uk. 108 , Hadith ya 5.
 • 67. at-Tawhid cha Saduq Uk. 108 , Hadith ya 8.