Utatu Na Kupotosha Ukweli

Kwanza: Wanahistoria

Mchango Wa Wanahistoria Katika Kuuhamasisha Umma:

Kwa kweli umma zinazoendelea ni zile zipatazo faida na mazingatio ya kihistoria, na kutwaa kilele cha uzoefu wakati wake uliopo, baada ya kuielewa mienendo ya kihistoria na kanuni zake ambazo zinauongoza umma kuelekea maendeleo na kuongeza maarifa ya sababu za kusambaratika umma na kurudi nyuma kwao. Mwenyezi Mungu hajaifanya kanuni hii kuwa mahsusi kwa umma maalumu mbali na mwingine, bali ni mwenendo mmoja haubadiliki: “Lakini hutapata mabadiliko katika kawaida ya Mwenyezi Mungu, wala hutakuta mageuko katika kawaida ya Mwenyezi Mungu.” (Sura Faatir: 43).

Hivyo basi maisha yapo katika mtindo mmoja, nao ni mapambano daima kati ya haki na batili, na matukio yote yanayoendelea katika historia ya uwanadamu hayatoki nje ya kuwa ni sehemu au upande fulani wa makabiliano kati ya haki na batili. Kwa uelewa huu tunaweza kuzama mbizi katika historia na kuifanya iwe hai, iweze kwenda sawa na maisha yetu ya kila siku.

Na tunaweza kutambua kwa undani kwa kadiri iwezekanavyo katika hali hii ya mtikisiko wa kihistoria wa umma wetu wa kiislamu, mgawanyiko mkali na mbaya sana wa kimadhehebu. Kwa ajili hiyo hapana budi tuivuke ile hali ya taathira zetu za kinafsi na mshikilio wetu wa kimhemko na hatimaye tuzifanye madhubuti kawaida zetu na uelewa wetu wa Qur’ani ilituwe na uwezo wetu wenyewe hasa wa kuchambua na kuyazingatia matukio kuanzia juu mpaka kiini chake, ili tuufikie mtazamo wa wazi na wa ukweli badala ya mtazamo wenye makosa na wenye tash’wishi. Hivyo basi natuanze kana kwamba Qur’ani imeteremka kwetu upya. Natuisome historia kutoka kwenye wahyi wa kauli yake (s.w.t.):

أَوَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنْظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ ۚ كَانُوا أَشَدَّ مِنْهُمْ قُوَّةً وَأَثَارُوا الْأَرْضَ وَعَمَرُوهَا أَكْثَرَ مِمَّا عَمَرُوهَا وَجَاءَتْهُمْ رُسُلُهُمْ بِالْبَيِّنَاتِ ۖ فَمَا كَانَ اللَّهُ لِيَظْلِمَهُمْ وَلَٰكِنْ كَانُوا أَنْفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ {9}

“Je, hawatembei katika nchi na kuona jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale waliokuwa kabla yao? Walikuwa wenye nguvu zaidi kuliko hawa, na wakiilima ardhi na kuistawisha zaidi kuliko hawa walivyoistawisha, na Mitume wao waliwafikia kwa miujiza waziwazi, basi hakuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wao wenyewe wakijidhulumu. (Sura Ruum: 9).

Ni kinyume kabisa, utaukuta umma ulioganda kifikra unashindwa kuifahamu historia na kanuni zake na uzoefu wake, kwa hiyo unakosa uoni na uelewa ambao ungeufanya uweze kuyaelewa yote ya wakati uliopo na kwenda kuelekea wakati ujao.

Tawala Na Upotoshaji Wa Historia:

Hivyo basi swali lolote au kanusho katika kuitafiti historia kwa kisingizio cha kutochochea mizozo ya kale, au kisingizio chochote kingine kile halina nafasi, na ikiwa litajulisha kitu litakuwa linajulisha ujinga wa mwenye kudai hivyo. Na ukweli ni kuwa: Ikiwa kuna mizozo ni kwa sababu ya yaliyotokea katika historia miongoni mwa uzushi na upotoshaji, kama si hivyo kwa kweli historia ikiwa ni historia kama ilivyo, huwa ni kioo safi kinachoakisi yaliyopita kwa ajili ya yaliyopo bila ya hadaa wala kufunika.

Lakini historia ilipoangukia mikononi mwa siasa zilizopotoka ndipo ikayumba sura yake na kubadilika umbo lake. Kutokana na hali hiyo, rai zikawa nyingi na madhehebu yakahitilafiana, kama si hivyo, lau historia ingekuwa salama upotoshaji ungefichuka na batili ingetambuliwa.
Na ambalo umma wa kiislamu unaumia nalo hii leo ni: Mfarakano, mparaganyiko, na safu kutawanyika, na si jambo lingine ila ni matokeo ya kimaumbile ya upotovu uliotokea katika historia, ikiwa ni matokeo ya wanahistoria kufunika na kuuficha kwao ukweli, hivyo basi wao ni sehemu isiyotengeka ya njama zilizoilenga kambi ya Ahlul-Bayt kwa ajili ya maslahi ya kisiasa. Zimefanya kazi njama hizi katika nyanja na maeneo mengi ili kutengeneza wimbi lingine lenye mandhari ya kiislamu ili kuukabili uislamu wa kweli na wa asili.

Na kwa sababu historia ni shahidi aliye bayana hunakili kila alionalo, kwa hiyo hapana budi njama hizi zimnyamazishe au kumpofusha ili asimfedheheshe na kufichua hila zake. Kutokana na hali hii historia imeshikwa na siasa inayotawala, inazunguka nayo kule izungukako.

Kwa hiyo wanahistoria wamekuwa chini ya vitisho au vishawishi vya masultani, kalamu zinatetemeka mkononi mwao ili kuufunika ukweli. Kwa kweli siasa ambayo ilikuwa ikifuatwa na wimbi la Bani Umayya na baada yao Bani Abbas ilikuwa tokea mwanzo inalenga kuwaharibia sifa Ahlul-Bayt (a.s.), kwani kule kujionyesha tu kuwa wanampenda Ali bin Abu Talib na Ahlul-Bayt wake (a.s.) kulikuwa ni mdhamini wa kubomoa nyumba na kukata riziki za watu wa namna hiyo.

Ilifikia mpaka Muawiya aliwafuatilia Shia wa Ali akisema: ‘’Waueni hao – kwa kisingizio cha – shubha na dhana,” mpaka ikawa kuzitaja fadhila zao ni kosa la jinai lisilosameheka. Na ili kujua misiba waliyokumbana nayo Maimamu wa Ahlul-Bayt na Shia wao katika historia, rejea kitabu: Maqtalut-Talibiyna cha Abul-Faraji al-Asfahaniy.

Wana nini wanahistoria, je yawezekana kwao katika hali ngumu kama ile kusajili sifa njema na fadhila za Ahlul-Bayt na kutaja sera zao zenye manukato?!

Hali ni kama hii umma umeendelea kurithishana ukweli uliopotoshwa kizazi baada ya kizazi, na hali ilikwenda mbali zaidi ya hapo, pale walipokuwa wanavyuoni waliokuja baadaye wanawatakasa waliotangulia na kunakili kutoka kwao bila ya kuzingatia wala kufikiria. Kutokana na hali hiyo uadui dhidi ya Ahlul-Bayt na Shia wao mizizi yake iliimarika na hatimaye kuenea kwa hali ya ujinga na mghafala kwa wengine.

Hivyo basi si jambo la kushangaza kwa Ibnu Kathir alipofikia kumtaja Ja’far bin Muhammad as-Swadiq (a.s.) katika matukio ya mwaka 148 A.H. hakusema kitu zaidi ya kauli yake: ‘’Na katika mwaka huo alifariki dunia Ja’far bin Muhammad as-Swadiq.” Anataja kifo chake wala hakupendezewa kutaja chochote kuhusu maisha yake. Na shuhuda za kuwa wanahistoria wamebadilisha ni nyingi. Twatosheka na kutaja mifano miongoni mwayo:

Vipi Waliandika Historia Ya Ushia?:

a)- Tabariy ameandika historia, naye ni mwanahistoria wa kwanza katika Uislamu, na walionakili kutoka kwake miongoni mwa wanahistoria kuwa, mwasisi wa Ushia ni Yahudi, jina lake Abdullah bin Saba’a, naye ni miongoni mwa watu wa Swan’aa. Ninakumbuka kwa mara ya kwanza nililisikia jina hili kutoka kwa mmoja wa ndugu zetu wa karibu naye ni mfuasi wa Uwahabi, kwa hiyo alikuwa akisema: ‘’Shia ni Mayahud, asili yao inarejea kwa Abdullah bin Saba’a Myahudi.’’

Na baada ya uchambuzi kuhusu jambo hili, nikawakuta wao wanapiga ngoma ile ile ya Ihsanu Ilahi Dhwahiri. Na mimi nikiwa naandika maneno haya, mbele yangu pana kitabu chake as-Shia Wattashayu’u, naye amenakili uwongo huu kutoka kwa Tabariy na wengine miongoni mwa wanahistoria. Na hapa tunanakili aliyoyanakili kutoka kwa Tabariy:

“Hakika amemtaja mwanahistoria wa mwanzo Tabariy kwa kauli yake: Abdullah bin Saba’a alikuwa Myahudi miongoni mwa watu wa San’aa, mama yake ni mtu mweusi aliyesilimu wakati wa Uthman, halafu alihama hama katika nchi za waislamu akifanya hila kuwapotosha. Alianzia Hijazi halafu Basra halafu Kufa halafu Sham, wala hakuweza alilokuwa analitaka kwa mmoja yoyote katika watu wa Sham, kwa hiyo walimtoa na alikuja Misri, akaishi kati yao akawaambia miongoni mwa aliyokuwa anayasema:
‘Ni ajabu kwa anayedai eti Isa atarejea na anadanganya kuwa Muhammadi atarejea, na kwa kweli Mwenyezi Mungu amesema:

إِنَّ الَّذِي فَرَضَ عَلَيْكَ الْقُرْآنَ لَرَادُّكَ إِلَىٰ مَعَادٍ ۚ{85}

“Kwa hakika yule aliyekulazimisha Qur’ani lazima atakarudisha mahala pa kurejea”
(Sura Qasas: 85).

Kwa hiyo Muhammad ni mwenye haki ya kurejea kuliko Isa.’

“Alisema: Hilo likakubaliwa kwao kutoka kwake, na akawawekea Rejea wakaongelea kuhusu hilo. Halafu baada ya hivyo aliwaambia kuwa:

‘Walikuwa manabii elfu na kila nabii alikuwa na wasii na Ali alikuwa wasii wa Muhammad.’ Halafu akasema: ‘Muhammad ni hitimisho la manabii na Ali ni hitimisho la mawasii.’ Kisha baada ya hivyo akasema: ‘Nani dhalimu zaidi kuliko yule asiyejuzisha wasii wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na akaruka juu ya wasii wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na kuchukua jambo la umma.’ Halafu baada ya hivyo aliwaambia: ‘Kwa kweli Uthman aliuchukua ukhalifa bila ya haki na huyu hapa wasii wa Mtume wa Mwenyezi Mungu hivyo basi shime kwa ajili ya jambo hili watikiseni na anzeni kuwakebehi maamiiri wenu. Na dhihirisheni amri ya kuamrisha mema na kukataza maovu, kwa hilo mtawavuta watu, na waitieni kwenye jambo hili.’

“Aliwatawanya walinganiaji wake na aliwaandikia waliokwishafisidi katika nchi na walimwandikia, na walilingania kwa siri kulingana na rai yao. Na walidhihirisha amri ya kuamrisha mema na kukataza maovu, na wakawa wanaziandikia nchi barua zenye aibu za maliwali wao, na ndugu zao wakawa wanawaandikia mfano wa hayo, na watu wa kila mji wanaandikiana wanayotenda na kila miongoni mwao huzisoma katika miji yao…nk.”

Hivi ndivyo wanavyoinasibisha itikadi ya Shia na historia yake kwa Abdullah bin Saba’a, na kwa ajili ya hayo wamejaalia kizuizi cha kisaikolojia kati ya watafiti na ukweli. Na kwa hayo wamekwenda mwendo wa wanahistoria bila ya utafiti wala uchambuzi wa kina. Hivyo tunamkuta mwandishi Ahmad Amin kwa mfano, katika kitabu chake Fajrul-Islam baada ya kunakili kisa cha Abdullah bin Saba’a, amekifanya kama Hadithi iliyokubalika. Anaikuta njia mbele yake imefunguka kuilenga tuhuma na uwongo dhidi ya Shia, anasema katika Uk. 269: “Wala Ghulatu wa Shia hawakutosheka na kiwango hiki kumhusu Ali, wala hawakukinai kuwa yeye ni mbora katika viumbe baada ya Nabii na kuwa yeye ni maasum, hivyo walimfanya Mungu, miongoni mwao kuna aliyesema: ‘Ndani ya Ali kuna sehemu ya kiungu, na imekuwa kitu kimoja na mwili wake kwa ajili hiyo alikuwa anajua ghaibu.”’

Halafu baada ya hivyo ananakili hekaya za Ibnu Saba’a na anachambua humo na kutoa tija akisema: “Kwa kweli ni kwamba ushia ulikuwa kimbilio ambalo anakimbilia humo kila mwenye kutaka kuharibu uislamu kwa ajili ya uadui au chuki, na kila atakaye kuingiza mafunzo ya baba zake toka kwenye uyahudi, ukristo, Zardoshtia na uhindu.” Naye anasema hilo kwa kukurupuka bila ya utafiti wala uchambuzi wa kina, bali ni kama mchanja kuni usiku, haelewi asemalo. Lakini lawama sio juu yake, kwani aliyokuja nayo ni tija ya upotovu wa historia na wanahistoria.

Ni kama hivi historia ilivyokuwa, na usaba’a ulikuwa nyenzo muhimu ya kuupotosha ukweli na kuupoteza umma. Na kwa kweli wanavyuoni wa kishia wamejitolea kwa ajili ya fikra hii ya Saba’a na wameifanyia utafiti kwa kujiweka mbali na hisia binafasi, na hatimaye wakafanya uchambuzi wa kina, haikuwadhihirikia ila ni kuwa kisa hiki ni cha kutengenezwa. Allama Murtadha al-Askariy ameandika kitabu chenye Jalada mbili, ameziita Abdullah bin Sabaa na ngano nyinginezo,1 katika kitabu hicho amezifuatilia riwaya za Ibnu Sabaa katika kila rejea za historia. Uwanja haunitoshi kuzichambua dalili ambazo zitafichua ukweli wake, hivyo basi hapa natosheka na ishara:

Uzushi huu wote warejea kwa mpokezi mmoja tu naye ni Saifu bin Umar, naye ni mtunzi wa kitabu Al-Futuhul-Kabiir War-Ridah na Al-Jamalu Wamasiyratu Aisha wa Ali Na kutoka katika viwili hivi Tabariy amenakili katika historia yake akitawanya katika matukio ya miaka. Na Ibn Asakir na Dhahabiy katika kitabu chake cha historia kijulikanacho kwa jina la Tarikhul-Kabiir.

Kauli Za Wanazuoni Kumhusu Saifu Bin Umar:

i) Yahya bin Muiin (Amefariki mwaka 233 A.H.) amesema: ‘’Dhaifu wa Hadithi, Falsu ni bora kuliko yeye.’’

ii) Abu Daudi (Amefariki mwaka 275 A.H.): ‘’Si chochote ni mwongo.’’

iii) Nasaiy, mtunzi wa Sahih An-Nasaiy (Amefariki mwaka 303 A.H.): “Dhaifu na Hadithi kutoka kwake huachwa, si thabiti wala haaminiki.”

iv) Na Ibnu Hatim (Amefariki mwaka 327 A.H.): “Ni mwenye kutupiliwa mbali Hadithi yake.”

v) Ibnu Udiy (Amefariki mwaka 365): “Hueleza hadithi za kuzusha kutoka kwa walio thabiti, ametuhumiwa kwa uzandiki.” Na akasema: ‘’Walisema alikuwa anaweka Hadithi za uzushi.’’

vi) Na Al-Hakim (Amefariki mwaka 405 A.H.) amesema: ‘’Ni mwenye kuachwa, na ametuhumiwa kwa uzandiki.’’

vii) Na Ibnu Abdil-Bar (Amefariki mwaka 463 A.H.) amenakili kutoka kwa Ibnu Haban kuwa yeye amesema kumuhusu: “Seifu ni mwenye kuachwa, na tumeitaja Hadithi yake kwa ajili ya maarifa tu” Ibnu Abdil-Bar hakusema kitu juu ya Hadithi hii.

viii) Na amesema al-Fayruz Abadiy, mwandishi wa kitabu Tawalif, na amemtaja na wengine na akasema kuwahusu: “Ni madhaifu.”

ix) Ibnu Hajar (Amefariki mwaka 852 A.H.) amesema baada ya kuileta Hadithi ambayo katika sanadi yake kuna jina la Saif:

    a. ‘’Humo mna madhaifu wengi na ambaye ni dhaifu sana ni Saifu.’’

x) Na amesema Swafiyud-Diyni (Amefariki mwaka 923 A.H.):

    b. ‘’Wamesema kuwa ni dhaifu. Tirmidhiy alielezea riwaya inayomzungumzia, hatimaye akairudisha Hadithi. Na hii ni rai ya wanazuoni kumhusu Saifu bin Umar zama zote.’’

Basi vipi kwa urahisi kiasi hiki wanahistoria wanaizingatia riwaya yake kuwa ni riwaya salama?! Na vipi watafiti wamezijengea rai zao juu yake. Na hii ni kuachia mbali ile hitilafu iliyojitokeza kuhusu jina lake. Hivi yeye ni Ibnu Saudaau?! Au Abdullah bin Saba’a. Na tofauti ambayo imejitokeza kuhusu kudhihiri kwake baina ya riwaya. Je alidhihiri wakati wa Uthman kama asemavyo Tabariy, au kama asemavyo Saad bin Abdillahi al-Ash’ariy ndani ya al-Maqalatu Wal-Firaqu: “Yeye alidhihiri katika siku za Ali au baada ya umauti wake!” Na kwa nini Uthman alimnyamazia, Uthmani mtu ambaye hakuwanyamazia hata maswahaba wakubwa mfano wa Abu Dharr, Ammar na Ibnu Mas’ud?!

Bali kwa kweli hiyo ni duru miongoni mwa mlolongo wa uwekwaji wa Hadithi dhidi ya Shia, kama alivyosema Twaha Husein: ‘’Ibnu Saba’a ni mtu aliyehodhiwa na mahasimu wa Shia dhidi ya Shia wala hana uwepo wa nje.’’ Na jaribio hili linalenga kuzieleza vibaya itikadi za Shia ambazo zinachimbuka kutoka katika Qur’ani na Sunnah, mfano wa Usia na Umaasumu. Maadui zao hawakupata dosari kuzikebehi itikadi hizi ila kwa njia ya kuziambatanishia itikadi hizi na mzizi wa kiyahudi, bingwa wake ni mtu wa kuwazika tu, jina lake ni Abdullah bin Saba’a, hivyo huvurumishwa lawama za hayo juu yake na juu ya wale waliochukua itikadi hizo kutoka kwake.
Hii ni kuachia mbali kule kuirekebisha sura ya maswahaba kwa kuwafanya adilifu, na kuwatakasa kwa kuwaepushia lawama na manung’uniko, kwa yaliyojiri baina yao miongoni mwa mifarakano na tofauti zilizoishia kuuliwa Uthman, na vita vya Jamal, ambavyo vyazingatiwa kuwa ni huzuni kubwa baada ya maafa ya Saqifa, kwani katika tukio la Jamal wametolewa mhanga maelfu ya Swahaba.

Na kisa hiki cha kubuni cha Ibn Saba’a si lolote ila ni kufunika matukio ya zama yenye shida. Wakaliweka jukumu la yaliyotokea juu ya shakhsiya hii ya kuwazika tu na kuyasitiri yaliyojiri. Kama si hivyo Swahaba wenyewe ndio wanaowajibika na yaliyotokea, kama vile mpasuko wa umma na kufarikiana kwao kimadhehebu na itikadi zilizo katika mtawanyiko.

Lakini hilo liko mbali! Hatari inayomkabili mbunifu haizuiliki kwa kujificha kichwa chake kwenye mchanga! Hivyo kwa kweli wameleta udhuru mbaya mno kuliko dhambi husika. Vipi itafaa ingizo kama hili liweze kucheza mchezo kama huu, kiasi cha kuibadilisha historia ya kiislamu kiitikadi, hali Swahaba wakiwa mashahidi juu ya hilo?!

Mfano Mwingine:

Kuna mtindo wa kufuta kabisa fadhila za Ali (a.s.) na za Ahlul-Bayt wake kwa sura ya makusudi kutoka katika vitabu vya historia. Huyu hapa Ibnu Hisham mnakili wa Sera ya Ibnu Is’haqa, anasema kwenye utangulizi wa kitabu chake: “Na ni mwenye kuacha baadhi ya aliyoyasema Ibnu Is’haqah ndani ya kitabu hiki…...na vitu ambavyo kuvisimulia kunaumiza, na baadhi huwachukiza watu kuvitaja…”

Kwa hilo akifanya utangulizi ili afikie kuuficha ukweli na kuizika haki, na miongoni mwa vitu ambavyo watu huchukizwa vinapotajwa ni: Wito wa Mtume kumwita Abdul-Muttalib pindi Mwenyezi Mungu alipomwamuru kuwaonya jamaa wa karibu. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alipomwambia:

‘’Waonye jamaa zako wa karibu.Tabariy amekieleza kisa hiki kwa sanadi yake, amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w): “Yupi kati yenu atanisaidia jambo hili ili awe ndugu yangu na wasii wangu na khalifa wangu katika ninyi?!” Ile kaumu ya watu wote ikalinyamazia hilo. Ali (a.s.) akasema: ‘Ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu mimi nitakuwa waziri wako…’ Mtume akasema: ‘’Kwa hakika huyu ni ndugu yangu na wasii wangu na khalifa wangu katika ninyi, hivyo basi msikilizeni na mumtii.’’ Alisema: ‘’Wale kaumu ya watu walisimama hali wanacheka huku wanamwambia Abu Talib: ‘’Amekuamuru umsikilize mwanao na umtii.’2

Je riwaya hii ndio inayowachukiza watu kuisema? Au kwayo Hadith hukebehiwa?!

Kusikufurahishe Tabariy kulisema tukio hili, kwa kuwa haraka sana alirejea kinyume na usemi wake huu, kwani limeelezwa ndani ya tafsiri yake tukio hili kukiwa na aina ya kulifunika na kulipotosha katika maelezo yake: ‘’Yupi kati yenu atanisaidia jambo hili ili awe ndugu yangu wa kadhaa wa kadhaa…’’ Halafu akasema: ‘’Kwa hakika huyu ni ndugu yangu wa kadhaa wa kadhaa, hivyo basi msikilizeni na mumtii.’’3 Basi nini maana ya kadha wa kadha?!

Ama Ibnu Kathiir katika Tarikh yake alipolitaja tukio hili alifurahiwa na alilolifanya Tabariy ndani ya tafsiri yake, kwa hiyo alikwenda mwendo wake bila haya wala kuchunga amana ya taaluma, naye akasema: Kadha wa kadha…!4

Hebu angalia tukio hili moja ambalo linachukua fadhila miongoni mwa fadhila za Amirul-Mu’miniina na haki yake ya ukhalifa, halafu angalia jinsi wanahistoria walivyolifanya. Ibnu Hisham hakuweza kulifanyia hila hivyo alilifuta kabisa.
Ama kuhusu Tabariy akifuatiwa na Ibnu Kathiir waliipotosha na kuiweka maana yake katika hali ya utata. Zingatieni.

Na mfano mwingine unakujia miongoni mwa mifano ya upotoshaji wa wanahistoria kuupotosha ukweli, hivyo kama ambavyo wao wanazificha fadhila za Ali (a.s.) na Ahlul-Bayt wake, kukabiliana na hilo wanaficha kila linaloaibisha na kutia dosari haki za Swahaba na khususan makhalifa. Na hili hapa kwako tukio hili ambalo linakusanya mitazamo yote miwili kati ya kuficha fadhila za Ali (a.s.) na kuficha fedheha za makhalifa:

Wanahistoria walificha na wa kwanza wao ni Tabariy, barua ambazo zilijiri kati ya Muhammad bin Abu Bakr – amabye ni miongoni mwa Shia wa Amirul-Mu’miniina – na Muawiyyah bin Abu Sufiyani. Kwa sababu katika barua za pande mbili hizo kuna uthibitisho wa usia za Imam Ali (a.s.) na kuna ufichuaji wa mambo ya makhalifa. Hivyo basi Tabariy aliomba udhuru baada ya kuwa alikwishazitaja sanad za barua mbili, kwa kuwa humo mna lisiloweza kuvumiliwa na umma kulisikia. Halafu baada yake alikuja Ibn Athiir na alifanya alilofanya Tabariy, halafu alifuata nyayo zao Ibnu Kathiir aligusia barua ya Muhammad bin Abu Bakar, na aliifutilia mbali barua hiyo na akasema: “Ndani yake mna ugumu.” Na waliyoyafanya wanahistoria hawa watatu, ni aina mbaya sana ya kuficha ukweli, na hilo wazi kabisa linafichua kuwa hawakuwa na uaminifu wa kielimu.

Wanakusudia nini kwa kauli yao: “Kutovumilia kwa umma kusikia yaliyo kwenye barua za pande mbili hizo?” Je, hivi ni kwa sababu umma hawatobakia na imani yao kwa makhalifa baada ya kusikia yaliyomo katika barua za pande mbili?

Kwako wakujia muhtasari kutoka katika barua ya Muhammad bin Abu Bakr kumwendea Muawiyyah na jibu la wa mwisho kwake, kama ilivyo katika kitabu Murujudhahbi cha Mas’udiy:

“Kutoka kwa Muhammad bin Abu Bakr kumwendea mpotovu Muawiyyah bin Swakhar - halafu alimtaja Mtume (s.a.w.w) na sifa juu yake…- Na kutumwa kwake akiwa Mtume na mbashiri na mwonyaji. Hivyo akawa wa kwanza alieitikia na kurejea, kuamini, kusadiki na kujisalimisha, na kusilimu nduguye mtoto wa ammi yake Ali bin Abu Talib: Alimsadiki kwa ghaibu iliofichika na alijitoa kwa kila la upendo, na alimhami kwa nafsi yake kwa kila la kutisha, na alipigana kwa vita vyake na alibakia salama kwa salama yake… Hana kifani…alimfuata, hakuna anayekurubiana naye katika matendo yake. Na nimekuona unamdhalilisa… na wewe ni wewe.

Na yeye ni yeye, ni mwenye nia ya kweli mno katika watu, na ni mwenye dhuria iliyo bora mno katika watu, na mwenye mke mbora katika watu … Na wewe ni mlaaniwa mtoto wa aliyelaaniwa, ungali wewe na baba yako mnamtakia Mtume wa Mwenyezi Mungu upotovu, na mnafanya juhudi kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu, kwa hilo mnakusanya kundi la watu na kutumia mali katika kundi hilo. Na mnakusanya makabila dhidi yake, baba yako amekufa akiwa katika juhudi hiyo, na kwa hilo umechukua nafasi yake…

“Halafu aliwataja wanusuru wa Ali na wafuasi wake na akasema: Wanaiona haki iko katika kumfuata yeye, na maisha ya mashaka yapo katika kwenda kinyume naye. Basi vipi ole wako! Unalingana naye au kujikurubisha nafsi yako na Ali, na yeye ni mrithi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na ni wasii wake na ni baba wa mtoto wake: Mtu wa kwanza kumfuata, na mtu wa karibu mno naye, anamwambia siri yake, na anamjulisha mambo yake.

Na wewe ni adui yake na mtoto wa adui yake. Basi starehe katika dunia yako na batili yako uwezavyo. Acha Ibnu Al-Aswi akusaidie katika upotovu wako. Kana kwamba muda wako umekwisha na vitimbi vyako vimedhoofika halafu itabainika nani atakayekuwa na mwisho wa hali ya juu. Na jua kuwa wewe unamfanyia vitimbi Mola Wako ambaye umekuwa na amani na vitimbi vyake, na umekatishwa tamaa na rehema Zake. Hivyo yeye yu akuangalia na wewe umeghurika mbali naye, na amani iwe pamoja na afuataye mwongozo.”5

Barua Ya Muawiya Kumjibu Muhammad Bin Abu Bakri, Kwa Ufupi:

“Kutoka kwa Muawiyya bin Swakhar, kumwendea aliyemdhihaki baba yake Muhammad bin Abu Bakr… (Anaiongelea barua ya Muhammad bin Abu Bakr anasema): Umemtaja humo mtoto wa Abu Talib, na kutangulia kwake na ukaribu wake kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na usaidizi wake kwake katika kila la kutisha na kuogofya, imekuwa hoja yako dhidi yangu, na kuniaibisha kwako mimi ni kwa ubora wa mtu mwingne si kwa ubora wako. Hivyo basi namuhimidi Mwenyezi Mungu aliyeuepusha ubora huu mbali na wewe na ameujaalia kwa mtu mwingine si wewe.

“Kwa kweli tulikuwa na baba yako akiwa kati yetu, tunazijua fadhila za mtoto wa Abu Talib, na haki yake ya lazima juu yetu inakubalika kwetu, basi Mwenyezi Mungu alipomchagulia Nabii wake juu yake iwe rehma na amani yaliyo Kwake (s.w.t.) na akamkamilishia aliyomuahidi, na kuipa ushindi daawa yake na kuing’arisha hoja yake, na Mwenyezi Mungu akamchukua kwake (s.a.w.w), baba yako na Faruqu wake walikuwa ni wa kwanza kuipora haki yake, na alihalifu amri yake, na kwenye hilo walikubaliana (Abu Bakr na Umar) kwa makubaliano mazuri.

Halafu wao wawili (Abu Bakr na Umar) walimwita Ali achukuwe kiapo cha utii, lakini alikawia, na hakuwasikiliza. Hapo walimkusudia kusudio baya na walitaka dhidi yake jambo kubwa.

“Halafu yeye aliwapa kiapo cha utii na kuwakabidhi, na walibaki hawamshirikishi kwenye mambo yao wala hawamwambii siri yao mpaka Mwenyezi Mungu alipowachukua. Baba yako aliandaa tandiko lake na alitengeneza mto kwa ajili ya ufalme wake. Ikiwa sisi tuliyonayo ni sahihi basi baba yako alihodhi na sisi ni washirika wake. Lau si aliyofanya baba yako hapo kabla tusingemuwendea kinyume mtoto wa Abu Talib, tungesalimu amri kwake.

Lakini tulimuona baba yako amemfanyia hivi kabla yetu tukachukua mfano wake. Hivyo basi mwaibishe baba yako upendavyo au acha hilo. Wasalamu ala man anaba.6

Kwa hayo umejua siri iliyomzuia Tabariy na Ibnu Athiir na Ibnu Kathir kunakili habari hizi, kwa sababu zinafichua ukweli wa mieleka na tofauti zilizotokea baina ya waislamu kuhusiana na suala la ukhalifa, ambao ulikuwa ni haki ya Ali. Hivyo basi huyu Muawiyah anakiri hilo lakini yeye anatoa udhuru kuwa ukhalifa wake ni muendelezo wa ukhalifa wa Abu Bakr, na kwa hilo anamkejeli mtoto wake (Muhammad bin Abu Bakr) ili amnyamazishe kusema lolote kuhusu jambo hili.

Lakini lawama si juu yako ewe Muawiyyah, ikiwa Muhammad bin Abu Bakr hakulinyamazia na wala hakulisitiri jambo lako, Tabariy, Ibnu Athiir na Ibnu Kathiir wamelinyamazia. Na shuhuda za hilo ni nyingi, miongoni mwazo ni upotoshaji wa wanahistoria kuzua na kupotosha ukweli, nafasi itatuwia ndefu kama tutazifuatilia kwa undani. Mwenye kufuatilia historia atayakuta hayo waziwazi. Na ni ajabu ilioje kuwa wanahistoria hawajisitiri kwa upotoshaji walioufanya!

Kwani utaikuta ishara ya wazi juu ya waliyoyatenda. Kwa mfano yaliyomtokea Abu Dharr miongoni mwa udhalil- ishaji alioupata kutokana na kutendewa vibaya na Uthman, kutokana na hilo Tabariy anasema: “Kwa hakika imesemwa sababu za kumtoa kwake nje ya mji wa Shammambo mengi, sikupenda kuyataja yaliyo mengi!” Kutokana na sura hii ya wazi inatufichukia kuwa Tabariy ameuficha ukweli.

Pili: Wanahadithi

Ukisimama mbele ya njama zilizofumwa katika Hadithi, na kuubadili ukweli wake, utahisi kuwa nadharia ya Shia ni dharura, nayo ni: Hapana budi kuwepo na hakimu na Imamu maasumu anayezihifadhi sheria za Mwenyezi Mungu na kuimarisha nguzo zake. Ikiwa hatokuwa maasumu aliye msafi ataitiisha dini ili kutekeleza malengo yake na siasa yake na atazipotosha Hadithi kwa ajili ya maslahi yake binafsi.

Hii ni endapo hatoipiga vita na kuzuia isiandikwe na isienezwe, kama ambavyo yamekupitia miongoni mwa mataendo ya makhalifa watatu – Abu Bakr, Umar na Uthman – ambao waliuzuia uelezwaji wa Hadithi na kuziunguza walizokuwa nazo waislamu na waliwatia mahabusu baadhi ya maswahaba huko Madina ili wasieneze Hadithi sehemu zingine za nchi. Imam Ali (a.s.) akasema kuhusu hilo: ‘’Nimewajua mawalii kabla yangu wametenda matendo ambayo kwayo wamemkhalifu Mtume wa Mwenyezi Mungu makusudi kwa kufanya kinyume naye, wakitangua ahadi yake, wenye kubadilisha sunna yake… ‘’

Na mimi sitouchukua muda huu ndani ya mlango huu, kuzungumzia hilo bali nitatosheka na ishara zilizopita. Ambalo nitajihushisha nalo hapa ni zama za kusajili Hadithi tu, zama ambazo zinazingatiwa na Ahlu Sunna kuwa ni zama dhahabu kwa ajili ya Hadithi, pamoja na kuishiria aliyoyafanya Muawiyyah kama vile kuzua Hadithi na kuzificha fadhila za Ahlul- Bayt.

Hadithi Katika Zama Za Muawiyyah:

Tunaweza kuukunja muda wa Muawiyyah kwa aliyoyanakili Madainu ndani ya kitabu al-Ahdathu, anasema: ‘’Muawiyyah aliandika nakala moja kwa magavana wake baada ya mwaka wa al-Jamaa7kuwa: “Nimeiepusha dhima ya mwenye kueleza kitu kuhusu fadhila za Abu Turabi – yaani Imam Ali (a.s.) – na Ahlul-Bayt wake” hivyo wakasimama makhatibu katika kila wilaya, na juu ya kila mimbari wakimlaani Ali na kujiepusha naye, wakimshambulia yeye na Ahlul-Bayt wake. Na waliokuwa na mtihani mkali sana wakati ule ni watu wa Kufa kwa kukithiri huko Shia wa Ali (a.s.), kwa hiyo akamfanya gavana wake kwao Ziyad bin Sumayyah, na mkoa wa Basra akauambatanisha na yeye, na alikuwa anawafuatilia Shia akiwa anawatambua kwa kuwa yeye alikuwa miongoni mwao katika siku za Ali (a.s.).

“Hivyo aliwaua kila mahali na aliwahofisha, na aliikata mikono na miguu na aliwatoboa macho na chuma kilichookwa na aliwatungika msalabani juu ya vigogo vya mitende, aliwafukuza na kuwafurusha kutoka Iraqi wala hakubakia mtu maarufu katika wao. Na Muawiyya aliwaandikia wafanyakazi wake kila mahali kuwa: Wasimruhusu yeyote miongoni mwa Shia wa Ali na Ahlul-Bayt wake kutoa ushahidi. Na aliwaandikia kuwa: Angalieni waliokuwa kabla yenu miongoni mwa Shia wa Uthman na wapenzi wake, na walio katika upendo naye na wanaoelezea fadhila zake na sifa zake njema, kuweni karibu na vikao vyao, wakaribieni na wakir imuni na niandikieni kila mtu anayeeleza miongoni mwao, jina lake jina la baba yake na la ukoo wake.

“Na walifanya hivyo mpaka walikithirisha fadhila za Uthmani na sifa zake njema, kwa sababu ya chochote kitu Muawiyyah alichokuwa anawatumia kama vile nguo, zawadi, vipande vya ardhi, na anawatukuza katika waarabu miongoni mwao. Mambo hayo yakakithiri katika kila nchi, na watu walishindania madaraka na dunia, wala haji mtu mtakiwa katika watu gavana miongoni mwa magavana wa Muawiyyah, na aeleze riwaya kuhusu fadhila za Uthman au sifa njema ila jina lake litaandikwa na ataso- gezwa karibu na kumlipa mara mbili, walibaki katika hali hiyo kwa muda.”

Na Madainu anaongeza kauli: ‘’Halafu aliwaandikia wafanyikazi wake kuwa Hadithi kumhusu Uthmani zimekuwa nyingi na zimevuma kila nchi na kila upande. Ikiwafikeni barua yangu hii walinganieni watu kwenye riwaya za fadhila za Swahaba na makhalifa wa mwanzo. Wala mtu yeyote katika waislamu asielezee habari yeyote kuhusu fadhila za Abu Turabi ila muniletee inayopingana na hiyo katika maswahaba. Kwa kuwa hilo lanipendeza sana mimi na latuliza mno jicho langu, na zipondeni hoja za Abu Turabi na Shia wake na wakazieni sifa nzuri za Uthman na fadhila zake dhidi yao.’’

Halafu anaongezea kauli yake: ‘’Hivyo basi watu walisomewa barua zake, habari nyingi zilielezwa kuhusu sifa njema za maswahaba za uzushi zisizokuwa na ukweli, watu walifanya juhudi kueleza riwaya zilizo katika mtiririko huu mpaka walinyanyua utajo wa sifa hizo juu ya mimbari,
na waliwapa waalimu wa madarasa na wao waliwafudisha watoto wao na watwana wao mengi kama hayo, na walijifundisha kama wanavyojifundisha Qur’ani hata waliwafundisha mabinti zao na wanawake wao na watumishi wao na waliendelea katika hali hiyo kiasi Mwenyezi Mungu ali- chopenda.’’

Na anaongeza: ‘’Halafu aliwaandikia watendaji wake nakala kwa nchi zote: ‘Angalieni, mwenye kuthibiti dalili kuwa yu ampenda Ali na Ahlul- Bayt wake, mfuteni na kumtoa kweye daftari na ondoeni alichokuwa anapewa na riziki yake.’ Aliongezea juu ya hiyo nakala nyingine: ‘Yoyote mtakayemtuhumu kuwa anawapenda watu hao muadhibuni adhabu ya mfano, bomoeni nyumba yake.’ Na haikuwa balaa mbaya na kali zaidi ya hiyo kama ile ya Iraqi, na hasa mji wa Kufa. Hali ilifikia mtu miongoni mwa Shia wa Ali (a.s.) anajiwa na mtu anayemwamini, anaingia nyumbani mwake na anamwambia siri yake, lakini anamwogopa hata mtumishi wake na mtumwa wake, hamhadithii jambo mpaka achukue kiapo kwake kizito, kuwa atawafichia siri yao hiyo.

“Hivyo zikajitokeza Hadithi nyingi za uzushi na uwongo ulioenea. Na kama hivyo walifanya wanazuoni, makadhi, na maliwali. Na watu waliokumbwa na balaa hilo sana ni wasomaji wa Qur’ani wenye kujionyesha na wanyonge wanaojionyesha kwa unyenyekevu na ibada, hivyo walikuwa wanatengeneza Hadithi ili wapate hadhi kwa maliwali wao na kuvipa hadhi vikao vyao, na wapate kwa ajili yake mali, eneo na majumba, mpaka habari hizo na Hadithi zilihamia mikononi mwa wanadini ambao hawahalalishi uwongo na uzushi na walizikubali na kuzieleza, hali wao wakidhania kuwa ni za kweli, lau wangejua kuwa ni za batili wasingezieleza wala kuzitumikisha kwenye dini yao.’’8

Hivyo inakuwia wazi ukali wa njama iliyofumwa ili kuuficha ukweli, kwani ilifikia daraja walihalalisha kumzulia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na yote haya yanarejea kwenye uadui mkali aliokuwa nao Muawiyah dhidi ya Ali na Shia wake, kwa ajili hiyo Muawiyah alikusanya uwezo wake wote ili asimame kumkabili Ali na Shia wake. Hivyo hatua ya kwanza ilikuwa kumuondolea Ali fadhila zote na sifa njema bali kumlani kwenye mimbari kwa muda wa miaka themanini.

Pili: Kujenga wigo wenye kujitokeza kwa mandhari nzuri yenye kuvutia kulizunguka kundi la swahaba ili iwe mfano badala ya Imamu Ali (a.s.). Vitisho vya Muawiyyah na vivutio vyake vilizoa kundi kubwa la wanafiki kumhudumia yeye Muawiyah. Walikuwa wanaweka Hadithi kumsingizia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) chini ya kivuli cha kuwa wao ni swahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w).

Abu Jafar al-Iskafiy amesema: “Kwa kweli Muawiyyah aliiweka kaumu miongoni mwa Swahaba na kaumu miongoni mwa tabiina ili waelezee habari mbaya kumhusu Ali zinazolazimu kukebehiwa yeye na kujiepusha naye, na alijaalia kwa kazi hiyo chochote kitu ambacho mtu hupendezewa nacho. Hivyo walizua Hadithi zilizomridhisha yeye, miongoni mwao ni Abu Hurayra, Amru bin Al-Aswi na Mughiyra bin Shu’ubah. Na miongo- ni mwa tabiina ni Urwa bin Zubair…”9

Ni kama hivi waliiuza watu hawa dini yao kwa dunia ya Muawiyah, basi huyu ni Abu Hurayra kama anavyoelezea al-Aamash. Amesema: “Abu Hurayra alipowasili Iraqi pamoja na Muawiyyah mwaka wa Jamaa, ali- wenda kwenye msikiti wa Kufa, na alipoona watu wengi waliokuja kumlaki alipiga magoti, halafu alikipigapiga kipara chake mara kadhaa, na akasema: ‘Oh ninyi Wairaqi mwadhania kuwa mimi namsingizia Mwenyezi Mungu na Mtume wake, nijiunguze binafsi na moto?! Wallahi nimemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) anasema: ‘Kwa hakika kila Nabii ana heshima na kwa kweli heshima yangu ni Madina kati ya Iir na Thaur10 basi mwenye kuzua jambo katika eneo hili laana ya Mwenyezi Mungu na ya malaika na watu wote imshukie.’ Na Mwenyezi Mungu ni shahidi kuwa Ali amezua uzushi ndani ya eneo hilo.’ Na kauli yake hii ilipomfika Muawiyyah alimlipa, nakumpa heshma, na alimchagua kuwa liwali wa Madina.”11
Na huyu hapa Samurata bin Jundub ni sampuli nyingine miongoni mwa watendaji wa Muawiyyah katika kuzua Hadithi. Imekuja katika kitabu Sharhu Nahjul-Balagha cha Ibnu Abul-Hadid: “Imeelezwa kuwa Muawiyyah alitumia kwa ajili ya Samurata bin Jundub Dirham mia moja elfu ili alete riwaya inayoelezea kuwa Aya hii ilishuka kumhusu Ali:

وَمِنَ النَّاسِ مَنْ يُعْجِبُكَ قَوْلُهُ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيُشْهِدُ اللَّهَ عَلَىٰ مَا فِي قَلْبِهِ وَهُوَ أَلَدُّ الْخِصَامِ {204}

وَإِذَا تَوَلَّىٰ سَعَىٰ فِي الْأَرْضِ لِيُفْسِدَ فِيهَا وَيُهْلِكَ الْحَرْثَ وَالنَّسْلَ ۗ وَاللَّهُ لَا يُحِبُّ الْفَسَادَ {205}

“Na katika watu yuko ambaye hukupendeza maneno yake hapa ulimwenguni, na humshuhudisha Mwenyezi Mungu kwa yaliyomo moyoni mwake, na hali yeye ni hasimu mkubwa kabisa. Na anapoon- doka, huenda katika ardhi ili kufanya uharibifu humo na kuangamiza mimea na watu, na Mwenyezi Mungu hapendi uharibifu.’ (Surat Al- Baqarah: 204-205)

“Na kuwa Aya ya pili ilishuka kumhusu Ibnu Muljim (Laanatu’llah) aliyemuua Ali bin Abu Talib (a.s.), nayo ni kauli yake (s.w.t.):

وَمِنَ النَّاسِ مَنْ يَشْرِي نَفْسَهُ ابْتِغَاءَ مَرْضَاتِ اللَّهِ ۗ وَاللَّهُ رَءُوفٌ بِالْعِبَادِ {207}

“Na miongoni mwa watu kuna ambaye huiuza nafsi yake kwa ajili ya kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma juu ya waja.”
(Sura Al-Baqarah: 207)

Samurata hakuzipokea, Muawiyyah alitoa kumpa Samurata Dirham mia mbili elfu hakuipokea pia. Alimpa Dirham mia nne elfu akakubali.”12

Tabariy ameeleza: “Ibin Siyrin aliulizwa: Je hivi Samurata alimuua yeyote?! Akasema: Hivi wanahesabika aliowauwa Samurata bin Jundub?! Ziyad alimfanya Khalifa huko Basra, na alikuja Kufa akiwa amek- wishauwa watu elfu nane. Na imeelezwa kuwa asubuhi moja aliuwa watu arobaini na saba wote wakiwa wamekusanya Qur’ani.”13

Jamani hivi hawa waliouliwa sio Shia wa Ali (a.s.)?!

Na akasema tena At-Tabariy: “Ziyad amekufa na hali Basra kuna Samurata bin Jundub, Muawiyyah alimlaghai miezi kadhaa halafu alimuengua, Samurata akasema: ‘Mwenyezi Mungu amlaani Muawiyyah, wallahi lau ningemtii Mwenyezi Mungu kama nilivyo mtii Muawiyyah hangeniadhibu abadan.”14

Ama al-Mughiira bin Shu’ubah aliueleza wazi mbinyo aliofanyiwa na Muawiyyah. Kutoka kwake Tabariy ameeleza kuwa: “al-Mughiira bin Shu’ubah alimwambia Swaa’swa bin Suuhan al-Abdiy – na Mughiira wakati ule alikuwa amiri wa mji wa Kufa kwa niaba ya Muawiyyah: ‘Ole wako inifikie habari kutoka kwako kuwa eti wewe unamuaibisha Uthman kwa yeyote miongoni mwa watu, na ole wako inifikie kuwa wewe unataja kitu chochote miongoni mwa fadhila za Ali waziwazi, wewe si mwenye kutaja kitu chochote miongoni mwa fadhila za Ali isipokuwa naijua fadhi- la hiyo, bali mimi nazijua mno.

Lakini huyu Sultani-anamkusudia Muawiyyah – ameshinda na ametushika tudhihirishe aibu yake – yaani Ali– kwa watu, na sisi tunaacha mengi aliyotuamrisha, tunataja kitu ambacho hatuna budi ili tujilinde nafsi zetu mbali na hawa watu kwa ajili ya taqiya, na nikiwa ni mwenye kutaja fadhila zake huzitaja mbele yako na swahiba zako, na ndani ya nyumba zenu kwa siri. Ama kuzitaja wazi wazi msikiti- ni Khalifa hatuvumilii wala hatupi udhuru kwa hilo.”15
Kama hivi, kundi la maswahaba na tabiina walimkubalia Muawiyyah, na mwenye kukataa huuliwa, kama vile shahidi Hajar bin Adiy na Maytham Tamariy na wengine. Ndio maana katika muda ule maelfu ya Hadithi za uwongo zilijitokeza ambazo zilikuwa zinafuma ubora na ushujaa wa maswahaba, hususan makhalifa wa tatu – Abu Bakr, Umar na Uthman. Halafu walizinakili Hadithi hizi kizazi baada ya kizazi zilisajiliwa katika vyanzo vinavyotegemewa.

Hivyo hapa zakujia baadhi ya sampuli za Hadithi za uwongo. Na mwenye kutaka ziada basi arejee kitabu al-Ghadir cha Allama al-Amini, Juz. 7, uk. 8.

1 -Jua Linamfanya Abubakr Wasila:

Nabii (s.a.w.w.) akasema: ‘’Nilionyeshwa kila kitu usiku wa Miraji hadi jua, kwa kweli mimi nililisalimia na nikaliuliza kuhusu kupatwa kwake, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alifanya litamke na likasema: ‘Mwenyezi Mungu Mtukufu ameniweka juu ya gurudumu linakwenda atakako, hivyo huwa najiangalia binafsi katika hali ya kustaajabishwa, gurudumu hilo huniteremsha na natua baharini na huko nawaona watu wawili mmoja wao anasema: Ahadu Ahadu, na mwingine anasema: Swidiqun swidqun. Kupitia wawili hao nafanya wasila wa kunifikisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu naye ananiokoa na kupatwa. Na huwa ninasema kuuliza: Yaa Rabi, ni nani hawa?! Anasema: Ambaye anasema: Ahadun Ahadun ni mpenzi wangu Muhammad (s.a.w.w) na ambaye anasema: Swidqun swidqun ni Abu Bakr Swidiq radhi za Allah zimfikie.”16

2 – Abubakr Katika Umbali Wa Pinde Mbili:

Imetufikia habari kuwa Nabii (s.a.w.w) alipokuwa umbali wa pinde mbili au karibu zaidi17alijisikia ukiwa na akasikia katika hadhara ya Allah (s.w.t.) sauti ya Abu Bakr (r.a), ndipo moyo wake ukawa na matumaini na kujisikia furaha kwa sauti ya swahiba yake.18

3 – Abubakri Ni Alifu Ya Qur’ani:

Aya zilizoteremka kumhusu Abu Bakr ndani ya Qur’ani ni nyingi. Tutosheke na Alifu ya Qur’ani:

الم {1}

ذَٰلِكَ الْكِتَابُ لَا رَيْبَ ۛ فِيهِ ۛ هُدًى لِلْمُتَّقِينَ {2}

“Alif, Lam, Miym. Hicho ni Kitabu kisicho na shaka ndani yake” (Surat Al-Baqarah: 1-2)

Hivyo basi Alif yamaanisha Abu Bakr, na Lam, ni Allah, na Miym ni Muhammad.19

Hawakuiacha fadhila yoyote iliyokuwa ya Nabii au Mtume ila wamemjaalia yeye hisa. Ama kuhusu fadhila za Umar, sema lolote hapana shida. Na tunataja miongoni mwazo zinazohusu mamlaka ya uumbaji. Bwana Raziy amesema ndani ya tafsiri yake: “Kulitokea tetemeko la ardhi huko Madina, hivyo basi Umar alipiga mjeledi ardhini, na akasema: ‘Tulia kwa idhini ya Allah.’ Ikatulia wala halikutokea tetemeko la ardhi tena Madina baada ya hilo!”(Tabaqaat as-Shafi’iya, Jz. 2, uk. 328)

Pia amenakili: “Uliibuka moto kwenye baadhi ya nyumba za Madina, hivyo Umar aliandika kwenye kitambaa: ‘Ewe moto tulia kwa idhni ya Allah.’ wakakitupa kwenye moto ukazimika papo hapo!” Tabaqaat as- Shafi’iya, Jz. 2, uk. 328)

Wanahadithi Waficha Ukweli:

Kuna fani nyingi kemkemu za kupotosha ukweli na kuubadilisha kwa waandishi wa Hadithi, hivyo tabia ya ushabiki iko wazi katika vitabu vyao. Kwa hiyo wanapokabiliwa na Hadithi yenye fadhila za Imam Ali (a.s.) au inayogusa na kufichua dosari kwa makhalifa na maswahaba, mikono yao hunyooka kwenye Hadithi ile au fadhila ile ili kugeuza ukweli. Na hii hapa yakujia sampuli ya fani hizo ili utambue mchango hatari walioutoa wanahadithi katika kubadilisha ukweli.

Sampuli Ya Kwanza:

Muawiya alipotaka kumchukulia baia Yazid, Abdur Rahman bin Abu Bakr alikuwa miongoni mwa wapinzani wakubwa wa baia ya Yazid. Marwani alihutubu kwenye msikiti wa Mtume (s.a.w.w) naye akiwa liwali aliyewekwa na Muawiyyah huko Hijazi, akasema: “Kwa kweli Amiirul- Muuminina amekuchagueni, hakuacha juhudi, amemfanya mtoto wake kuwa khalifa baada yake.” Hapo Abdur Rahmani bin Abu Bakr alisimama na akasema: “Wallahi umesema uwongo ewe Marwani! Na Muawiyyah amesema uwongo. Hamkusudii kheri kwa umma wa Muhammad, lakini ninyi mnataka ufalme kila akifa mfalme anachukua nafasi yake mfalme.” Marwan akasema: “Huyu ndiye ambaye Mwenyezi Mungu ameteremsha kumhusu:

وَالَّذِي قَالَ لِوَالِدَيْهِ أُفٍّ{17}

“Na ambaye anawaambia wazazi wake: Ah! Nanyi!” (Surat Ahqaaf: 17).”

“Aisha alisikia usemi wake nyuma ya pazia, akasimama nyuma ya pazia na akasema: ‘Ewe Marwani! ewe Marwani!’ hapo watu walinyamaza, Marwani alielekea kwa uso wake, Aisha akasema: ‘Hivi wewe ndiye uliyemwambia Abdur Rahman kuwa ndiye aliyeshukiwa na Qur’ani, Wallahi umesema uwongo yeye siye, lakini ni fulani bin fulani, lakini yeye ni sehemu ya waliolaaniwa na Mwenyezi Mungu.’ Na katika riwaya nyingine akasema: ‘Amesema uwongo! Wallahi si yeye, lakini Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alimlaani baba wa Marwani, na Marwani akiwa mgongoni mwake, kwa hiyo Marwani ni mtawanyiko wa waliolaaniwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu.”20

Halafu njoo uone jinsi Bukhari alivyoyabadilisha yamtiayo dosari Muawiyyah na Marwani: “Marwani alikuwa Hijazi, Muawiyyah alimfanya kuwa gavana wake, Marwani alihutubia akawa anamtaja Yazid bin Muawiyyah ili apewe baia baada ya baba yake, Abdur Rahman bin Abu Bakr akasema kitu. Marwani alisema: Mchukueni. Ndipo Abdur Rahman alipoingia chumbani kwa Aisha na hatimaye hawakumuweza. Marwani akasema: ‘Huyu ndiye ambaye Mwenyezi Mungu aliteremsha kumhusu: “Na ambaye anawaambia wazazi wake: Ah nanyi!” (Surat Ahqaaf: 17).” Je mwanipa udhuru?!’ Aisha nyuma ya pazia akasema: ‘Mwenyezi Mungu hakuteremsha kitu kumhusu yeye katika Qur’ani, isipokuwa Mwenyezi Mungu aliteremsha humo udhuru wangu.” 21

Amelifuta neno la Abdur Rahman na alilibadilisha kwa neno ‘kitu’, kama alivyobadilisha kauli ya Aisha. Hayo yote ili kuhifadhi sura ya Muawiyyah na Marwan. Na tukio hili amelileta Ibnu Hajar katika Fathul-Baariy kwa ufafanuzi. Basi angalia upeo wa usafi alioufikia Bukhari katika kunakili ukweli.

Sampuli Ya Pili:

Bukhari aliifutilia mbali fatwa ya Umar ya kutowajibika Swala. Muslim ameeleza kutoka kwa Shuubah. Alisema: “Al-Hakam alinihadithia kutoka kwa Dhar, kutoka kwa Said bin Abdur Rahman, kutoka kwa baba yake kuwa: Mtu mmoja alimjia Umar akasema: ‘Mimi nimekuwa na janaba sikupata maji.’ Umar akasema: ‘Usiswali.’ Ammar akasema: ‘Ewe Amiirul-muuminina hukumbuki tulipokuwa mimi na wewe katika tume tukawa tuna janaba na hatukupata maji,
ama wewe hukuswali na mimi nilijigaragaza kwenye mchanga na nikaswali. Hapo Nabii (s.a.w.w) akasema: ‘Yakutosha upige kwa viganja vyako ardhi halafu upulize halafu upake kwa hivyo viganja uso wako na dhiraa zako!’ Umar akasema: ‘Mche Mwenyezi Mungu ewe Ammar.’ Ammar akasema: ‘Ukipenda silihadithii hili.’’22

Hadithi yadhihirisha hali ya Umar kutojua hukumu ndogo mno ambayo ni dharura ya kisheria, ambayo waislamu wengi wanaijua na ambayo Qur’ani imeieleza wazi, ambayo Mtume (s.a.w.w) aliwafundisha utaratibu wake. Pamoja na yote hayo, Umar anatoa fatwa ya kuacha Swala, kwanza ni miongoni mwa yajulishayo hali ya kutojua kwake. Pili yajulisha kutotilia kwake maanani swala, bali kutoswali kwake akiwa katika hali ya janaba endapo atakosa maji, kama ambavyo riwaya imelieleza hilo waziwazi.

Nakumbuka hapa kuwa mmoja wa marafiki alikuwa ananijadili kuhusu elimu ya Umar, aliniambia: ‘’Kwa hakika Umar Qur’ani ilikuwa inamuafiki kabla haijateremshwa.’’

Nilimwambia: Hizo ni simulizi tu zisizo na ukweli wowote, kama si hivyo basi itakuwaje iafikiane naye kabla haijateremshwa na yeye hakuafikiana na Qur’ani baada ya kuteremka katika tukio la kutayamamu na kiwango cha mahari ya wanawake!

Hadithi hii kwangu ilikuwa ni pigo kubwa lilinikumba katika utafiti wangu kuhusu hadhi ya Umar, kwa kuwa inaweka wazi kabisa wizani wake wa kielimu na kidini. Na ambalo lilinizidishia mshangao ni ile hali ya Umar kung’ang’ania ujinga wake baada ya Ammar kumpa habari ya hukumu ya kisheria katika suala hii.

Halafu mwangalie Bukhari ambaye hakupenda kuieleza fatwa hii ambayo hawawezi kufutu fatwa kama hii hata wasiojua. Hivyo ameieleza katika Sahihi yake kwa sanadi ileile na kwa tamko lilelile ila tu ameondoa fatwa: “Mtu mmoja alikuja kwa Umar bin al-Khattab na akasema: ‘Mimi nimekuwa na janaba na sikupata maji.’ Ammar bin Yaasir alimwambia Umar bin al-Khattab: ‘Je hukumbuki…’’23

Sampuli Ya Tatu:

Ibnu Hajar ameeleza katika Fathul-Bariy katika ufafanuzi wa Sahih Bukhari Juz. 17, Uk. 31 Hadithi: “Mtu mmoja alimuuliza Umar bin al- Khattab kuhusu kauli yake (s.w.t.): “Na matunda na malisho” (Surat Abasa: 31), malisho ni nini? Umar akasema: ‘Tumekatazwa kwenda kwa ndani zaidi na kujikusuru.’’’

Ibnu Hajar amesema kuwa: ‘’Imekuja katika riwaya nyingine kutoka kwa Thabit kutoka kwa Anas kuwa Umar alisoma: “Na matunda na malisho” (Surat Abasa: 31) na akasema: ‘Malisho ni nini!?’ Halafu akasema: ‘Hatukukalifishwa’ au akasema: ‘Hatukuamrishwa hili.’”

Halafu angalia uzalendo binafsi umemfanya nini Bukhari! Hivyo yeye anafanya juhudi yake yote ili amtakase Umar na makhalifa na kila waliloambatanishwa nalo, basi vipi aieleze Hadithi hii ambayo yathibitisha Umar kutoijua vyema Qur’ani, kwa sababu aliloulizwa ni katika upeo wa urahisi kwa aijuaye Qur’ani na taratibu zake. Na hoja ya Umar kuwa hapana wajibu, haina msingi, kwa kuwa si mahala miongoni mwa mahali pa wajibu.

Kwa hiyo udhuru ni mbaya zaidi kuliko dhambi. Na alipoulizwa Imam Ali (a.s.) swali hili hili, akasema jibu lipo katika Aya yenyewe “Na matunda na malisho. Kwa manufaa yenu na wanyama wenu” (Surat Abasa: 31-32), yaani tunda ni chakula chetu sisi binadamu na malisho ni chakula cha wanyama, nayo ni aina ya nyasi.

Bukhari amesema katika Sahih yake kutoka kwa Thabit kutoka kwa Anas akasema: ‘’Tulikuwa kwa Umar akasema: ‘Tumekatazwa kujikusuru.’’24
Kwa kweli Hadithi hii ni kama nyingine miongoni mwa makumi ya Hadithi ambazo zilikuwa hazilingani na itikadi ya Bukhari, hivyo alifanya makusudi kushika njia hii ya kuondoa, kubadili, na kuifuta habari kamili, kama alivyoifanya Hadithi ya Vizito Viwili: “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu” ambayo Muslim na al-Hakim wameiandika kulingana na sharti yake, na Hadithi zingine zilizo sahihi ambazo Bukhari hakuweza kuzinyoosha wala kuzibadili, hivyo alijiepusha kuzisajili katika kitabu chake. Na hii ndio sababu ya msingi iliyofanya Sahih Bukhari kwa watawala kuwa ni kitabu sahihi mno baada ya kitabu cha Mwenyezi Mungu (s.w.t.), siijui sababu nyingine isiyokuwa hii.

Sampuli Ya Nne:

Kwako lakujia tukio hili ambalo kupitia hili itakudhihirikia ni kwa kiwango gani Bukhari alikuwa anakusudia kuubadili ukweli. Wamelieleza wanachuoni wa kisunni na mahafidhu wao mfano wa Tirmidhiy ndani ya Sahihi yake, al-Hakimu ndani ya Mustadrak yake na Ahmad bin Hanbali ndani ya Musnad yake. Na pia amelieleza Nasaiy ndani ya Khaswais yake, Tabariy ndani ya Tafsiir yake, Jalaludiyni Suyutiy ndani ya Tafsiir yake ad- Durul-Manthur, al-Mutaqiy al-Hindiy ndani ya Kanzul-Ummal. Na Ibnu Athiir ndani ya Tariikh yake na wengine wengi, wameeleza kuwa:

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alimtuma Abu Bakr (r.a) na alimuamuru anadi maneno haya nayo ni:

Tangazo la kujitoa katika dhima, litokalo kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake.”

Halafu akamwamuru Ali (a.s.) amfuate na alimuamuru ayanadi yeye Ali (a.s.), ndipo aliposimama katika siku za Tashriiq na akanadi:

“Hakika Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamejitoa katika dhima. Basi tembeeni katika nchi miezi minne, na baada ya mwaka huu asihiji mshirik- ina yeyote yule, na wala asiizunguke nyumba akiwa utupu.”

“Abu Bakr (r.a) alirejea na akasema: ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kimeteremshwa kitu kunihusu mimi?’ Alisema (s.a.w.w):

‘Hapana isipokuwa Jibril alinijia na akasema hatekelezi kwa niaba yako ila wewe au mtu kutokana na wewe.’”

Hapa ndipo Bukhari ameangukia kwenye mkasa, riwaya hii inapingana kabisa na madhehebu yake na itikadi yake, kwani yathibitisha ubora wa Ali (a.s.) na ni ubora mtukufu ulioje! na kinyume chake yapunguza au haithibitishi kitu chochote kuhusu ubora wa Abu Bakr, basi vipi ataigeuza riwaya hii iwe kwenye maslahi yake na itikadi yake, na kwa riwaya hii athibitishe sifa njema za Abu Bakr na Ali asiwe na kitu. Njooni, ili muone jinsi gani Bukhari alivyojitoa kwenye shida hii. Bukhari katika Sahih yake ameweka kitabu kwa jina la Tafsiri ya Qur’ani, mlango wa kauli yake:

Safirini katika nchi miezi mine. Amesema humo: Alinipa habari Humaydu bin Abdir Rahman kuwa Abu Hurayra (r.a) amesema: “Abu Bakr alinituma katika Hijja ile niwe kati ya waadhini aliowa- tuma siku ya kuchinja, aliwatuma watoe tangazo Mina kuwa asihiji baada ya mwaka huu mshirikina wala asifanye tawafu ya nyumba hali akiwa uchi. Humaydu bin Abdir Rahman akasema, halafu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alipanda mnyama mmoja na Ali bin Abu Talib na alimuamuru atangaze tamko la kujitoa kwenye dhima, Abu Hurayra akasema: Ali alitangaza tamko la kujitoa kwenye dhima akiwa pamoja nasi siku ya kuchinja katika watu wa Mina, na kuwa asihiji baada ya mwaka ule mshirikina wala asitufu nyumba akiwa tupu.”25

Ewe msomaji nitakuachia nafasi ya kutia neno lako, ili uone kupotosha na kubadilisha kama huku, na jinsi Bukhari alivyoipoteza fadhila ya Ali bin Abu Talib na alivyomthibitishia sifa njema Abu Bakr, sifa ambazo hakuwa anaziotea baada ya Mwenyezi Mungu kumwengua kwa wahyi kutoka kwake.
Jibril alimwambia Mtume (s.a.w.w): “Hatekelezi kwa niaba yako ila wewe au mtu kutokana na wewe.” Halafu, tazama jinsi alivyolijaalia jambo mkononi mwa Abubakr, kwa hiyo akawa yeye ndio mwamrishaji na ndio mtume na mwendeshaji wa mambo mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu …! Utakatifu ni wa Mgeuza hali kutoka hali mpaka hali.

Sampuli Ya Tano:

Muslim katika Sahihi yake ameshirikiana na Ibnu Hishamu na Tabariy katika kufuta sehemu ya Hadithi inayotia dosari daraja la Abu Bakr na Umar.

Baada ya Ibnu Hisham kunakili habari ya shambulio la Badri na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na Swahaba zake kuupinga msafara wa biashara wa makurayshi. Ametaja tukio la Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kuwataka ushauri swahaba wake na akasema: “Habari ya msafara wa makuraishi ilimjia, ili wauzuie msafara wao aliwataka ushauri watu na aliwapa habari ya makuraishi. Ndipo Abu Bakr Swidiqi alisimama na akasema na alifanya uzuri. Halafu alisimama Umar na akasema umesema vyema.

Kisha al-Mikdad bin Amri alisimama na akasema: ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) endelea na alilokuonyesha Mwenyezi Mungu sisi tu pamoja na wewe, wallahi hatukwambii kama vile Bani Israil walivyomwambia Musa: ‘Nenda wewe na Mola wako mkapigane sisi tuko hapa tumeketi.’ Lakini nenda wewe na Mola wako mpigane na sisi tuko pamoja na ninyi tukiwa ni wenye kupigana. Naapa kwa aliyekutuma kwa haki lau ungekwenda na sisi mpaka Birkulghimadi26 tungekuwa pamoja na wewe mpaka ufike.’ Hapo Mtume wa Mwenyezi Mungu akamwombea kheri na dua njema.”

Je nini ilikuwa kauli ya Abu Bakr na Umar kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu?! Kama ilikuwa njema kwa nini basi hakuitaja! Na kwa nini aliitaja kauli ya Miqdad bila ya kauli ya wawili hawa?!

Halafu tunarejea kwa Muslim ili tuone je yeye pia aliendeleza udanganyifu, awe amefanya kama alivyofanya Ibnu Hishamu na Tabariy. Muslim ameeleza kuwa: ‘’Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), aliwashauri swahaba zake ilipomfikia habari ya kuja kwa Abu Sufiani. Amesema: Abu Bakri aliongea Mtume alitupilia mbali, halafu Umar aliongea na alitupilia mbali …”27 hapo aliitaja Hadithi yote iliyobaki.

Muslim pia hakutaja alilolisema Abu Bakr na Umar ila yeye kiasi fulani ni mkweli kuliko Ibnu Hishamu na Tabariy, kwani yeye amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu alitupilia mbali.” Wala hakusema: “Alifanya vyema.” Japokuwa alilofanya ni kosa la jinai katika haki ya Hadithi kwani ilipasa aziseme kauli zao, na hilo ni miongoni mwa yajulishayo kuwa katika kauli hizo kuna linalochukiza. Kwa nini Mtume wa Mwenyezi Mungu atupilie mbali kauli zao lau ni kauli njema?!

Inatuwia wazi kutokana na habari hizi mbili baada ya kupatikana ufichaji wa wazi kutoka kwao, kuwa kulikuwa na jambo ambalo halilingani na hadhi ya masheikh wawili ndio maana hawakulisema, lakini Mwenyezi Mungu aliidhihirisha nuru yake japo wachukie makafiri.

Imeelezwa katika kitabu al-Maghaziy cha al-Waaqidiy na kitabu Imtaul- Asmai cha Miqriiziy, baada ya kuitaja habari: Umar akasema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), kwa kweli hao wallahi ni Makuraishi na utukufu wao, wallahi hawajadhalilika toka walipokuwa na utukufu, na wallahi hawajaamini toka walipokufuru, wallahi hawatoukabidhi utukufu wao abadan, na watapigana na wewe, jiandae kwa hilo maandalizi yake na jizatiti kwa hilo ipasavyo.”

Hapo sasa tunatambua sababu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kutupilia mbali usemi wao.

Maneno haya aliyoyasema Umar hayalingani na Swahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) vipi anadai kuwa makuraishi wana utukufu? Hivi Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alikusudia kuwadhalilisha?

Lakini yasikitisha, haya ndiyo maarifa yake Umar ya uislamu na ndio njia yake ya kimaendeleo.

Ni kama hivi Bukhari na Muslim huchanganya haki na batili, na wanazibadilisha Hadithi ambazo wazitambua kuwa zitawadhalilisha na kuwapunguzia hadhi Abu Bakr na Umar.

 • 1. Kitabu hiki kwa sasa kinapatikana kwa lugha ya Kiswahili kwa jina hilohilo.
 • 2. Tabariy Bitalkhiiswi - Chapa ya kwanza Misri, Juz. 2, Uk. 216 – 217.
 • 3. Tafsirut-Tabariy, chapa ya Buulaq, Juz.19, Uk. 72.
 • 4. Al-Bidaya Wan-Nihaya, Juz. 3, Uk. 40.
 • 5. Murujud-Dhahab cha Al-Mas’udiy Jalada ya 3, Uk. 20, iliyohakikiwa na Muhammad Muhiyudiyn, chapa ya Darul-Maarifah. Beirut.
 • 6. Murujud-Dhahab, cha Al-Mas’udiy, Jalada ya 3, Uk. 21, iliyohakikiwa na Muhammad Muhiyudiyn, chapa ya Darul-Maarifah. Beirut.
 • 7. Nao ni mwaka ambao Muawiyyah aliwakusanya wafuasi wake ambao ni mwaka wa 42 A.H. na akawapa jina kuwa wao ni Ahlu Sunnah Wal-Jamaa, kwa ajili hiyo umekuwa mashuhuri kuwa ni mwaka wa al-Jamaa .
 • 8. Taamulatu Fii Swahihayni, Uk. 42- 44.
 • 9. Abu Hurayra – Mahmud Aburayhi, Uk. 236.
 • 10. Ibnu Abul-Hadid amesema katika ufafanuzi wake: Inaonyesha ni kosa la mpokezi, kwa sababu Thaur ipo Makkah … na sahihi ni: Kati ya Iir na Uhud.
 • 11. Ahadithu Ummul-Muuminina Aisha, Uk. 399.
 • 12. Ahadithu Umuml-Muuminina Aisha, Uk. 400.
 • 13. Katika matukio ya mwaka wa hamsini katika Tarikh Tabariy, Juz. 6, Uk. 132. Na Ibnul-Athiir, Juz. 3, Uk. 193.
 • 14. Miongoni mwa matukio ya mwaka wa 50 ndani ya Tariikh At-Tabariy Juz. 6, Uk. 164. Na Ibnul-Athiir Juz. 3, Uk. 195.
 • 15. Tarikhut-Tabari Juz.6. Uk.108 Katika kutaja matukio ya mwaka wa 43.A.H.
 • 16. al-Ghadir Juz. 7, Uk. 288. Akinakili kutoka kwenye kitabu Nuzhatul-Majalisi Juz. 2, Uk. 184.
 • 17. Rejea Surat An-Najmi Aya ya tisa, ikizungumzia miraji na yaliyojiri.
 • 18. Al-Ghadir Juz. 7, Uk. 293. Nakala kutoka kwa Abdiy al-Maliky katika Umdatut-Tahqiiq. Uk. 154. Na akasema: Hizi ni karama za As-Swidiq za peke yake.
 • 19. Al-Ghadir Juz.7. Imenakiliwa kutoka katika kitabu Umdatut-Tahqiiq, Al- Aabidiy Al-Malikiy.Uk.134.
 • 20. Tarikh Ibnul-Athiir Juz. 3, Uk. 149, katika kutaja matukio ya mwaka wa 56. A.H.
 • 21. Bukhari, Juz. 3, Uk. 126. Mlango wa “Na ambaye anawaambia wazazi wake: Ah nanyi!” tafsiri ya Surat Ahqaaf.
 • 22. Sahih Muslim, mlango wa Tayammum Juz. 1.
 • 23. Sahih Bukhari Juz. 1, Kitabu Tayammum. Babu Tayammum.
 • 24. Sahih Bukhari Juz. 9, Kitabu Al-Iitiswam.
 • 25. Sahih Bukhari. Juz. 5, Uk. 202.
 • 26. Yasemekana kuwa Birkulghimad ni jina la eneo fulani huko Yemen.
 • 27. Sahih Muslim kitabu cha jihadi, mlango wa vita vya Badri.