Tatu: Waandishi

Mchango Wao Katika Kubadilisha Ukweli

Uliendelea mchango wa wanahadithi na wanahistoria waliokuja baada yao miongoni mwa waandishi. Walitumia juhudi zao zote kubadilisha ukweli na kupotosha madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.) kwa mbinu mbalimbali za masingizio na kusambaza uwongo.

Na kwa kweli waandishi hawa wamefanikiwa mafanikio makubwa kuufanya ujinga uingie kwa ndani zaidi nyoyoni mwa wanamadhehebu wao, na kuongeza pengo kati yao na utambuzi wa ukweli. Hivyo basi waliuchora Ushia kwa sura mbaya mno iwezekanayo, kupitia njia waliyoifuma miongoni mwa uzushi na mawazo potovu.

Hili Silisemi kwa kudhania tu bali nimeishi na ujinga huu muda mrefu, na niliuhisi sana ulipofunguka uelewa wangu na Mwenyezi Mungu kuutia nuru moyo wangu kwa nuru ya Ahlilu-Bayt. Hapo niliiona jamii yangu ikisinzia kwenye rundo la ujinga na masingizio dhidi ya Shia, kila niulizapo kuhusu Shia sawa iwe anayeulizwa awe mwanachuoni au msomi alikuwa ananijibu kwa mlolongo wa uzushi dhidi ya Shia na husema: Shia wanadai kuwa ati Imam Ali (a.s.) ndiye Mtume lakini Jibril alikosea na aliiteremsha risala kwa Muhammad, au kuwa wao wanamwabudia Imam Ali… na mengine miongoni mwa uzushi ambao hauna mafungamano na ukweli. Na shida kubwa mno kuliko hiyo ni utakapoharakiwa na swali linaloduaza: Hivi Shia ni waislamu? Nini tofauti kati ya Ushia na Ukomunisti?

Kwa kweli huku kutoujua Ushia, wanakoishi nako kundi kubwa la umma wa kiislamu ni tija ya kawaida ya juhudi za hawa waandishi, ili kuulazimisha ujinga wa kugubika kwa wana wa umma huu ili wasiyatambue madhehebu ya Shia. Na huu ni mchoro wa ramani ulioanza zamani sana ili mwendo wake utimie mpaka hii leo.

Hivyo utakuta mamia ya vitabu vilivyotiwa sumu dhidi ya Shia vikiwa katika nafasi ya kufikiwa na mikono ya wote, hii ni endapo itakuwa havigaiwi bure na mawahabi. Na ilipaswa katika mazingira kama haya yaliyosheheni upinzani dhidi ya Shia waruhusiwe waandishi wa kishia pia kusambaza vitabu vyao, ili kuwe na ulinganifu, lakini hili huwa haliwi.

Hivyo ndani ya hizi maktaba za kiislamu inakaribia kuwa nadra kupatikana humo kitabu cha kishia kinyume na maktaba za kishia, sawa ziwe za kibiashara au katika taasisi ya kielimu, bali hata maktaba ya mtu binafsi miongoni mwa wanachuoni wa kishia, humo havikosi vitabu na vyanzo vya kisunni katika maandishi yake yote na mwelekeo wake.

Msiba na uchungu zaidi kuliko yote hayo ni kuwa endapo mmoja wao amepata kitabu cha kishia hatokisoma, hii ikiwa kwa bahati tu hakukiunguza kwa hoja ya kutokuwa jaizi kusoma vitabu vya upotovu.

Nakumbuka jinsi imamu wa msikiti kijijini petu alivyokuwa anasema wazi wazi kuwa mimi ni kafiri na nimepotea, na alikuwa anawakataza wote wasikae pamoja na mimi au kusoma kitabu changu. Mantiki gani hii inayompokonya mtu uhuru wake wa kufikiri! Hiyo ndiyo siasa ya ujinga na kuwafanya wengine wawe wajinga na kuwabana watu kifikra.

Baadhi Ya Vitabu Vilivyoandikwa Dhidi Ya Shia:

1) Muhadhwarati Fii Taarikhil-Umamil-Islamia, cha Al-Khidhriy
2) Sunnah Was-Shia, cha Rashid Ridhwa, mwandishi wa kitabu al- Manaar.
3) As-Swirau Baynal-Wathaniyah Wal-Islam, cha al-Qaswimiy.
4) Fajrul-Islam na Dhuhal-Islam, vya Ahmad Amin.
5) Al-Washiatu Fii Naqdis-Shiiah, cha Musa Jarullahi.
6) Al-Khututul-Ariidha cha Muhibud-Diin al-Khatib.
7) As-Shiah Was-Sunnah na As-Shiah Wal-Qur’ani na As-Shiah Wa Ahlul- Bayt na As-Shiah Wat-Tashayyuu, vya Ihsan Ilahi Dhahiir.
8) Minhajus-Sunah, cha Ibn Taymiyya.
9) Ibtaalul-Baatil, cha al-Fadhlu Ibnu Ruzbahan.
10) Usulu Madh’habi Shia, cha Dr. Nasiru al-Ghafariy.
11) Wajaa Dawrul-Majusi, cha Abdullah Muhammad al-Gharib.
12) Tuhfatul-Ithna Asharia, cha Dahlawiy.
13) Jawlatu Fii Rubuis-Sharqil-Adna, cha Muhammad Thabit al-Misriy.

Na vingine miongoni mwa vitabu vilivyolengwa. Na wanavyuoni wa Shia wamejibu vitabu hivi, na vya mfano wake majibu ya kutosheleza na ya ufafanuzi.

Na nimeona tofauti ya njia ya kiutendaji kati ya aina mbili za vitabu. Hivyo utakuta vitabu vya Shia vinalenga chimbuko na kuthibitisha usahihi wa madhehebu yake kwa njia ya dalili na thibitisho nyingi, kwa kuvitegemea vyanzo na rejea za Ahlu Sunnah, bila ya kuyahujumu madhehebu mengine. Ama vitabu ambavyo vinajaribu kuwajibu Shia, kimsingi vinalenga kuyapa pigo madhehebu ya Shia kwa njia yeyote iwayo japo iwe kwa tuhuma na masingizio. Na ushahidi juu ya tuliyosema ni mwingi, na tutaingia kwenye hilo pindi nitakapoelezea baadhi ya mifano.

Miongoni Mwa Vitabu Vya Shia Vilivyojibu Na Kuyachimbua

Madhehebu Yake:

1 – As-Shaafi Fil-Imamah:

Kina jalada nne. Humo Sharifu Murtadha amethibitisha uimamu kuwa ndio kiini cha dini kijamii na kisiasa, na amethibitisha kwa dalili za kunakiliwa na za kiakili iliyo sahihi kuwa uimamu ni jambo la dharura kidini na kijamii, na kuwa Ali (a.s.) ndiye Khalifa wa haki aliyeainishwa baada ya Mtume (s.a.w.w), na kuwa atakayepinga na kukaidi atakuwa ameipinga haki na maslahi ya wote. Sharifu amezisema shaka zote zilizosemwa na zile ambazo yawezekana zikasemwa kuhusu uimamu, na amezibatilisha kwa mantiki ya kiakili na hoja kinaifu.1

Na kitabu hiki ni mahali pa kujibu kitabu cha Al-Mughgniy cha Abdul Jabbar, Muutaziliy.

2 – Nahjul-Haqi Wakashfus-Swidqi, Cha Allama Hilliy:

Humo amezungumzia jumla ya masaili yaliyo kwenye wigo huu:

a) Utambuzi. b) Uchunguzi. c) Sifa za Allah. d) Unabii. e) Uimamu. f) Marejeo. g) Misingi ya Fiqhi. h) Yanayohusu Fiqhi.

Na itamdhihirikia msomaji wa kitabu hiki kuwa mwandishi wake alikuwa mtafiti wa kitaalamu sio mwenye upendeleo wa rai yake, wala si mwenye kuelemea itikadi za mwanzo, na wala hakutafiti kwa ajili ya kupata dalili ya itikadi yake, isipokuwa aliijaalia rai yake na itikadi yake ziwe zenye kufuata Qur’ani na utiifu wa dalili.
Kwa hakika al-Fadhlu bin Ruzibahan al-Ash’ariy alijitokeza kukikosoa kitabu hiki na alikiita kitabu chake Ibtalul-Batil Waihmalu Kashful-Aatili. Lakini yeye hakutumia mtindo wa Allamah Hilliy, yeye alikuwa apinga sana na kutukana, isipokuwa kwa jumla ni kitabu kinategemea kwa kiwango fulani hoja na mjadala wa kielimu. Kwa ajili hiyo kiliwapa msukumo wanachuo wengi wa kishia kukijibu na kubainisha maeneo ya shaka katika kitabu hicho.

3 – Ihqaqul-Haqi Cha Sayyid Nurullahi Al-Huseiniy Tustariy:

Kitabu hiki ni kinene, mwenyewe amekitunga kumjibu Ruzbahan katika kitabu chake Ibtalul-Batil, na ametoa maoni yake kukihusu kitabu hiki Ayatullahi Shihabud-Diin al-Mar’ashiy an-Najafiy. Hivyo idadi ya Jalada zake zinafikia ishirini na tano za jalada nene. Mwandishi wa kitabu hiki ametumia juhudi iliyo wazi na ya taabu katika kufuatilia dalili na kuzileta Hadithi na riwaya kutoka kwenye vitabu vya Ahlu Sunnah. Na ingependeza kitabu hiki kingekuwa kwenye nyumba za makumbusho za waislamu. Kwani chadhihirisha juhudi kubwa ya mtu pekee, juhudi ambayo kamati iteuliwayo kwa shughuli mahsusi inashindwa kuifanya juhudi kama hii.

4 – Dalailus-Swidqi Cha Allamah Mudhwaffar:

Pia amemjibu Ruzbahan, Allamah Mudhwaffar, katika kitabu chenye jalada tatu, jina lake Dalailus-Swidqi humo pia amechukua hatua ya kujibu kitabu Minhajus-Sunnah cha Ibnu Taymiyya, ambaye alikiandika ikiwa ni jibu kwa Allamah Hilliy katika kitabu chake Minhajul-Karamah. Lakini yeye hakupambanua (al-Mudhwaffaru) katika kumjibu kwake (Ibnu Taymiyah) katika utangulizi, bali amefanya ishara kwa kauli yake: “Lau si uduni wa madhumuni yake na uovyo wa ulimi wa kalamu yake na urefu wa ibara zake, na kudhihiri kwa chuki yake na uadui wake kwa Nabii mwenyewe na watoto wake watoharifu angekuwa mweye haki mno ya kufanya naye utafiti.”2

5 – Mausuatul-Ghadiir, Jalada 11 Cha Allamah Abdul-Husein Al- Aminiy:

Hiyo ni juhudi kubwa mwandishi ameifanya, ni upeo wa juhudi na taabu, humo amethibitisha kwa kila njia na dalili madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.), na miongoni mwa litakalokuzidishia kustaajabishwa kwako ni kuwa mwandishi wake amekusanya humo vyanzo vinavyofikia 94,000 kutoka katika vitabu vya Ahlu Sunnah. Na amejishughulisha humo kujibu baadhi ya vitabu vya kisunni ambavyo vilijitoa kwa ajili ya Shia, mfano:

a) al- I’qdul-Fariid.
b) al-Farqu Baynal-Farqu.
c) al-Milalu Wan Nahlu.
d) Minhajus-Sunnah.
e) al-Bidaya Wan-Nihaya.
f) al-Muhdharu.
g) as-Sunna Was-Shia.
h) as-Swirau.
i) Fajrul-Islami.
j) Dhuhurul-Islam. k) Dhuhal-Islam.
l) Aqidatus-Shiah. m) al-Washiah.

Na amefanya vyema kuwajibu kwa hoja na dalili inayokiwisha macho na uthibitisho unaong’aa. Na amemayizika kwa mjadala unaofaa mahali pake, haelemei kwenye upendeleo na ubishi tu.

6 – Aqabatul-Anwar Fii Imamatil-Aimatil-At’har:

Pia miongoni mwa vitabu vikubwa mno ambavyo vimethibitisha madhe- hebu ya Shia, na kuwajibu maadui zake, ni kitabu Aqabatul-Anwar Fii Imamatil-Aimatil-At’har cha Sayyid Hamid Husein Ibnu Sayyid Muhammad Qaliy al-Hindiy. Sikuipata nakala yake ya asili,
nimepata muhtasari wake wenye jina Khulaswatu Abaqatil-Anwar mtungaji wake ni Ali al-Huseiniy al-Miilaniy. Kina Jalada 10, nacho ni jibu la kitabu at- Tuhfatul-Ithna Asharia cha Abdul-Azizi Dahlawiy, ambacho kinakosoa kitabu Aqaidus-Shia.

Kundi la wanachuoni wa Shia wamekijibu kitabu hicho at-Tuhfatul-Ithna Asharia kwa idadi kadhaa ya vitabu, miongoni mwavyo ni kitabu Saiful- Maslulu Ala Mukharibii Dinir-Rasul cha Abu Ahmad bin Abdin-Nabii an- Nisaburiy. Na kitabu chenye Jalada nne, kila Jalada katika hizo kwa jina la Sayyid Daldar Ali Taqiy. Na kitabu an-Nuzhatul-Ithna Asharia cha Mirza Muhammad al-Kashmiriy, na kitabu Al-Ajnadul-Ithna Asharia Al- Muhammadiyah cha Sayyid Muhammad Qalbiy. Nacho ni jumla ya Jalada kubwa kubwa. Na kitabu al-Wajiizu Fil-Usuli, cha Sheikh Subhan Ali Khan al-Hindiy. Na kitabu al-Imamah cha Sayyid Muhammad bin Sayyid, na huyu analo jibu lingine kwa Kiajemi, aliliita al-Bawariqul-Ilahiyah.

Na vingine miongoni mwa vitabu vilivyomjibu Dahlawiy, mwandishi wa kitabu al-Dhariah amevitaja, na kitabu Aayanus-Shia. Na kikubwa mno miongoni mwa vitabu hivi vya majibu ni kitabu Al-Aqabatu. Na humo unajitokeza utukufu wa mtungaji na umakini wake katika kufikiri, na kuizunguka kwake elimu, na ufuatiliaji wake wa kauli mbali mbali, na uaminifu wake wa kunakili kielimu kanuni za utafiti, katika utaratibu wake wa kuzijibu mishikeli au kuikosoa dalili.

Kwa kweli amezikata kwa hoja zenye nguvu mno na thibitisho madhubuti njia zote na visingizio vyote, na ameziondoa shaka na shubha zote, kiasi kwamba kwa hasimu hakukubakia kebehi yeyote dhidi ya madhehebu au kuitia dosari dalili au kuidhoofisha Hadithi, ila ataihami kwa ambalo ni zuri na kutoa jibu zuri kwa uhakiki safi na udodosaji mkali, na kwa hoja zenye uthibitisho.

Na kujiambatanisha na utoaji dalili wa hali ya juu, na… Katika yote hayo akitegemea vitabu vya Ahlus Sunna, na akitolea dalili kauli za vigogo vya wanavyuoni wao katika elimu na fani tofauti. Na amelichukua kila neno lililokuja katika At-Tuhfatu akalijibu au kulikosoa.3

Maktaba ya ukoo wake ulio mashuhuri ndiyo iliyomsaidia hayo, maktaba ambayo ina zaidi ya vitabu thelathini elfu miongoni mwa vilivyopigwa chapa na vile vilivyoandikwa tu kwa mkono ambavyo bado havijapigwa chapa, vya madhehebu na vikundi mbalimbali. Hatujakuta mpaka hii leo kitabu kinachojibu kitabu hiki Aqabatul-Anwar Fii Imamatil-Aimatil- At’har, japokuwa kitabu At-Tuhfatu, kimezungukwa na majibu. Wa kwaza kukijibu ni Sayyid Daldaaru Ali katika kitabu chake Swawarimul-Ilahiyah na kitabu Swarimul-Islam.

Ndipo Rashidu-Diin ad-Dahlawiy, mwanafunzi wa mtunzi wa At-Tuhfatu alimjibu kwa kitabu as-Shawkatul-Umriyah, na hapo Baaqir Ali alimjibu mwanafunzi huyo kwa kitabu Alhamlatul- Haydariyah, kama alivyoijibu At-Tuhfatu al-Mirza katika kitabu chake An- Nuzhatul-Ithna Asharia. Na ndipo mmoja wa masunni alijibu kwa kitabu Rujumus-Shayatiyni, hapo Sayyid Jafar Al-Musawiy alimjibu kwa kitabu Muinus-Swadiqiina Fir-Radi Rujumus-Shayatiyni.

Kama ambavyo pia Sayyid Muhammad Qiliy, baba wa mtunzi wa Al- Aqabatu ameijibu At-Tuhfatu kwa kitabu Al-Ajnadul-Ithna Asharia Al- Muhammadiyatu, ndipo Muhammad Rashid Dahlawiy naye akamjibu. Na hapo Sayyid alirudia na kumjibu kwa kitabu Al-Ajwibatul-Fakhiratu Fir- Radi Alal-Ashairah, mpaka alipolikata jambo hili mwandishi wa kitabu Al- Abaqatu, yeye hajajibiwa. Na hii yatosha kujulisha kushindwa kwa waliostahili kujibu.

7- Maalimul-Madrasatayni Cha Murtadha Al-Askariy:

Nacho ni miongoni mwa vitabu vya kulinganisha kati ya kambi ya Ahlul- Bayt na kambi ya makhalifa. Mwandishi wake ametegemea mahali muwafaka na mjadala wa kielimu wa kina. Nacho kipo katika Jalada tatu.

8- Murajaati, Cha Abdul Husein Sharafud Diin:

Na huu ni mjadala uliojiri kati yake na Sheikh wa Azhar Salim al-Bushriy. Wazingatiwa kuwa ni miongoni mwa mijadala adimu ambayo wajadili wawili waliafikiana kufuata utaratibu tulivu na mazungumzo ya tabia njema. Na Sheikh Abdul Husein ana vitabu vingine vingi katika uwanja huu. Miongoni mwavyo ni an-Nassu Wal-Ijtihadu, al-Fusulul-Muhimah Fii Taalifil-Umma, al-Kalimatul-Gharrau Fii Tafdhwiliz-Zahrau, na kitabu Abu Hurayra. Na kuna vitabu kadhaa vya wanavyuoni wa Shia kujibu vitabu vya kisunni mfano:

a) Ajwibatul-Masail Jarullahi cha Abdul- Husein Sharafud Diin al- Musawiy.
b) Maal-Khatiibu Fii Khututihi Al-Ariidhwa, cha Lutfullahi Swafiy.
c) Shubhaatu Haula Shia.
d) Kadhabu Ala Shia.

Wanazuoni Wa Kisunni Na Wasomi Wao Wanaukubali Ushia:

Kikundi miongoni mwa Sunni wateule na wanavyuoni wao wameweza kuzivunja pingu na kuvikiuka viziwizi vya mbinyo wa utoaji habari, ili elimu na maarifa mengine yafunguke, na ilikuwa kati ya elimu hizo ni Ushia ukiwa madhehebu yenye historia yake, maarifa yake na taaluma yake. Ni jambo ambalo limesababisha kutanduka kiwingu cha giza zito lililokuwa limetanda juu ya mbingu ya ukweli, hawakuwa na wasaa ila kuuinua ukelele wa ukweli na kutangaza uaminifu na utii wao kwa njia ya Ahlul-Bayt (a.s.). Na wamejiunga kwenye msafara huu maelfu ya wanafikra na kalamu zilizo huru hapo zamani na hivi sasa. Nafasi haitutoshi kuwataja ila tu tutatosheka na kutaja mifano miongoni mwao:

1 Mwana hadithi adhimu Abu Nafar Muhammad bin Masud bin Ayyashi, ambaye ni mashuhuri kwa jina la al-Ayyashiy. Kabla hajawa Shia alikuwa miongoni mwa wanavyuoni wa Sunni. Naye anahesabiwa kuwa ni miongoni mwa wanachuoni wakubwa wa Shia Imamiyah, anayo tafsiri yake katika athari iitwayo Tafsirul-Ayyashiy.

2 Sheikh Muhammad Mar’iy al-Aminiy al-Antakiy. Amehitimu chuo kikuu al-Azhar, na alishikilia cheo cha ukadhi mkuu huko Halabu.4 Akiwa na nafasi ya kielimu na kijamii Mwenyezi Mungu alimuongoza kujiambatanisha na njia ya Ahlul-Bayt (a.s.), na ana kitabu kimekwishapigwa chapa na kimesambaa, nacho ni Limadha Ikhtartu Madhhaba Shiah (Kwa nini nimechagua madhehebu ya Shia) pamwe na yeye wameikubali Shia maelfu ya watu wa Halabu.

3 Sheikh Salim al-Bushriy. Naye ni miongoni mwa wanavyuoni wa Ahlu Sunna, alikuwa mkuu wa masheikh wa al-Azhar Shariif mara mbili maishani mwake. Yalijiri mazungumzo mengi kati yake na Abdul Husein Sharafud Diin naye ni mwanachuoni wa Shia, maongezi hayo yamekusanywa katika kitabu al-Murajaatu, na maongezi haya tulivu yalileta tija ya Sheikh Salim al-Bushriy kuukubali Ushia, katika maongezi yake ya mwanzo akasema wazi wazi kuwa yeye si mwenye upendeleo wa upande mmoja, kwa kauli yake: “Kwa kweli mimi ni mtafuta kilichopotea, na mtafiti wa ukweli, haki ikibainika, haki ndiyo ya kufuatwa, vinginevyo, mimi ni kama alivyonena mnenaji: Sisi na tulicho nacho, na wewe na ulicho nacho, ni mridhia na rai ni tofauti”5

Na baada ya maongezi mengi yaliyoweka wazi elimu za pande mbili, heshma yao kubwa na tabia zao njema na kutojiambatanisha kwao na upendeleo kwa ajili ya ukweli, Sheikh Salim al-Bushriy mwisho wa mzunguko anasema wazi: “Mpaka hali ya uficho ilipotoweka, na haki imebainika kwa usafi wake, asubuhi imekuwa bayana kwa mwenye macho mawili, shukurani ni zake Allah kwa mwongozo kwa ajili ya dini Yake, na kupata tawfiki ya aliloliitia kwenye njia Yake, na rehma na amani ya Allah imfikie yeye (s.a.w.w.) na ahali zake.”6

4 Sheikh Mahmud Abu Riyah. Mwanachuo na mwandishi wa Kimsri ana vitabu vingi na ubunifu, miongoni mwavyo ni Adhwau Ala Sunna Al- Muhammadiyyah, na kitabu Abu Hurayra Sheikhul-Mudhwirah.

5 Wakili Ahmad Husein Yaqubu. Na yeye ni mwandishi wa Jordan aliyeukubali Ushia, ana kitabu Nadhariyatu Adalatus-Swahabah na kitabu Alkhutatu Siyasiyatu Litawhidil-Ummatil-Islamiyyati.

6 6 Dk. Tijani Samawiy, na yeye ni Mtunisi aliyeukubali Ushia, na anajumla ya vitabu miongoni mwavyo ni: Thumma I h t a d a y t u , Liakuna maas-Swadiqiin, Fas’alu Ahladhikri na Shia hum Ahlus- Sunnah.

7 Mwandishi wa vitabu na mwandishi wa habari za magazeti Sayyid Idrisa al-Huseiniy kutoka Morocco. Ana vitabu La Qad Shayaanil- Huseinu, al-Khilafatul-Mughtaswaba, na Hakadha Araftus-Shia, hiki hakijapigwa chapa.

8 Swaibu Abdul Hamid. Ana kitabu Manhaju Fil-Intimail-Madhhabiy.

9 Said Ayyub. Ana kitabu Aqidatul-Masiihi Dajal. Anasema mwanzoni mwa kitabu chake: “Umenikuta ndani ya mjadala najaribu kuondoa rundo mbali na ukweli, ili ukweli uwe wazi mbele ya macho na akili, rundo hizo ambazo zimewekwa na walimu wa kuitia giza kadiri ya muda wa historia ya mwanadamu uendeleavyo! Na ninaposhika jembe ambalo kwalo niondoe kichaka, nina sababu za kutosha za kuitekeleza kazi hii.”7 Na ana kitabu kingine Maalimul-Fitan, kikiwa na juzuu mbili.

10 Mwandishi Mmisri Swalihul-Wurdaniy. Ana kitabu Al-Khidah, Rihlatiy Minas-Sunnah Ilas-Shiah, Harakatu Ahlul-bayt (a.s.), Shia Fii Misri, na Aqaidu Sunna Wa Aqaidus-Shia at-Taqarubu Wat-Tabaudu.

11 Mwandishi Mmisri, Muhammad Abdul Hafidh. Ana kitabu Limadha Ana Jaafariy

12 Mwandishi Msudani. Ustadh Sayyid Abdul-Mun’im Muhammad al- Hasan, ana kitabu Binuri Fatmah Ihtadaytu.

13 Sheikh Abdillahi Nasir wa Kenya, amekuwa Shia, hapo kabla alikuwa miongoni mwa masheikh wakubwa wa kiwahabi.8 Naye ana vitabu vingi katika uwanja huu miongoni mwavyo Shia na Qur’ani, Shia na Hadithi, Shia na swahaba, Shia na taqiyyah, na Shia na uimamu.

14 Samahatu Alimu na khatibu na mwanamjadala Sayyid Ali al-Badriy anatoa huduma kubwa katika kueneza madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.) baada ya kuwa Shia. Alizunguka dunia akifanya vikao vya mijadala mingi akiiambatanisha na kitabu kikubwa ambacho kipo njiani kupigwa chapa, kikiwa na anwani Ahsanul-Mawahibi Fii Haqaiqil- Madhahibi.

15 Mwandishi Msyria Sayyid Yasiyn al-Maayufu al-Badraniy. Ana kitabu kwa anuani ya Ya Layta Qawmiy Yaalamuna.

Sampuli Ya Ubadilishaji Wa Waandishi:

Nayo ni nyingi nafasi itatuwia ndefu kuiorodhesha, hivyo vilivyo vingi miongoni mwa vitabu vyote vilivyowajibu Shia havikukusudiwa ila kupotosha, kubadilisha, na kusambaza tuhuma na uwongo.

Hii ukiongezea kuwa wao masunni kuvitegemea vitabu vya kisunni katika kuzijibu itikadi za Shia, sio njia muwafaka katika mlango wa kutoa hoja na mjadala.

Sheikh Mudhaffari anasema kuhusu hilo: “Jua kuwa si sahihi kutoa dalili dhidi ya hasimu ila kwa ambalo kwake ni hoja. Kwa ajili hiyo utamwona msanifu Mwenyezi Mungu amrehemu na wengine – yaani Allamah Hilliy - waandikapo kutoa hoja dhidi ya Ahli Sunnah wamejihusisha na kutaja habari zao si habari zetu. Na hawa kaumu hawajiambatanishi na kanuni za utafiti wala hawakupita njia ya mjadala.”9

Kama ambavyo wao katika kujibu wanategemea kuileta sura ya jumla ya itikadi za Shia bila ya jibu la kimantiki kuhusisha kila kisehemu miongoni mwa sehemu za madhehebu. Na hii sio insafu katika viwango vya uaminifu wa kitaaluma. Hivyo basi utamkuta Dk. Nasirul-Ghafariy anasema katika utangulizi wa kitabu chake Usulu Madh habi Shia Uk. 15: “Kwa kuwa katika jumla ya itikadi kuna litoshelezalo kutambua hakika yake, kwa kuionyesha tu. Kwa ajili hii Sheikhul-Islam Ibnu Taymiyya amesema kuwa: ‘Kuifanyia taswira madhehebu ya batili kunatosha kubainisha uharibifu wake, wala haihitaji dalili nyingine pamwe na taswira njema.”’

Endapo hayo yatakuwa sahihi, hapana budi mfanya taswira wa itikadi awe muumini mwenye kuitakidi itikadi hiyo, ili awe na uhuru wa kutosha katika kufafanua itikadi zake. Na ni miongoni mwa dhulma, lije jicho geni lifanye taswira itikadi ya mtu mwingine kwa sura mbaya mno. Na ayasemayo Ibnu Taymiyya ni aina ya siasa ya kuwaweka ujingani wafuasi wake anapowafanyia taswira madhehebu zinazompinga kwa sura azitakazo yeye.

Lau hilo lingetosha kuwa ndio hoja ingekuwa yule kafiri anayeishi Ulaya mwenye kubeba sura iliyopotoshwa ya uislamu - fikrani mwake – kwa sababu ya taswira iliyofanywa na mustashrikina (Orientalists) na maadui wa dini, basi angekua na udhuru kwa hilo. Hivyo basi maneno haya ni dhaifu na ni njia kosefu haifai kutolea dalili. Yasikitisha kuwa hii ndio dini yao, na zakujia baadhi ya sampuli za upotoshaji wao:

Kitabu Usulu Madhhab Shia, cha Dk. Nasir Abdullahi al-Ghafariy, ambacho ni risala ya Ph.D. kutoka chuo kikuu cha kiislamu cha Muhammad bin Saudi na kwa risala hiyo ametunukiwa nishani ya daraja ya heshma ya kwanza. Miongoni mwa masingizio yake dhidi ya Shia:

a. Kauli yake: “Hivyo kwa ajili hiyo Ushia unaipiga vita Sunnah. Ndio maana Ahlu Sunnah wamekuwa mahsusi kwa jina hili kwa ajili ya kufuata kwao Sunna ya Mustafa (s.a.w.).”10

Halafu baada ya hayo anajaribu kuzitoa riwaya zile za kishia ambazo zinawajibisha kuifuata Sunnah. Kwa hiyo anasema: “Ila tu kwamba mwenye kuzisoma nususu za kishia na riwaya zake huen- da akaishia kuamua kuwa Shia, kidhahiri wanaizungumzia Sunna na wanaikanusha kindani, kwa kuwa sehemu kubwa ya riwaya zao na kauli zao zinaelekea mwelekeo unaokwenda kombo mbali na Sunnah ambayo waijuayo waislamu, katika kufahamu na kuitekeleza na katika sanadi na matamshi…”11

Ama kuhusu kauli yake: Shia yaipiga vita Sunnah, haina nafasi, kwa kuwa vitabu vya Hadithi kwa Shia vinazidi mara kadhaa vitabu vya Ahlu Sunnah, bali riwaya za al-Kafiy peke yake ni zaidi ya riwaya za Sihah Sita. Hii ni kuachia mbali vitabu vikubwa kabisa katika Hadithi kama Biharul-Anwar ambayo idadi ya Jalada zake zinafikia mia na kumi.

Hivyo ikiwa Shia wanaipiga vita Sunnah basi hivi vitabu vikubwa ni kwa ajili ya nini?! Au anakusudia nini kwa neno Sunnah?

Je hiyo Sunnah ni ile iliyokuja katika riwaya za Ahlu Sunnah pekee ndani ya Sihah zao? Endapo jibu litakuwa ni ndio, hii bila shaka itakuwa hoja dhidi yao sio dhidi ya Shia.

Na usemi wake: “Kwa kuwa sehemu kubwa ya riwaya zao na kauli zao zinaelekea mwelekeo unaokwenda kombo.” Hii ni miongoni mwa kauli za kustaajabisha, ikiwa Shia tokea asili wanaafikiana na massuni katika nyanja zote za Hadithi, sanad, matamshi, utekelezaji na kufahamu hapangekuwa na sababu ya tofauti. Kwa hiyo Shia wanaamini Sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na wanalazimika nayo. Ama dai la kuwa wao ndio mahsusi kwa Sunna ndio maana wameitwa Ahlu Sunna kwa kuwa ndio wanaoshikamana na Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ni dai lisilo kuwa na insafu.3

Halafu pili: Hivi wewe na kaumu yako ni kigezo cha dini, kwamba kila kitu unakipima kwa kigezo chako mwenyewe binafsi?! Ni uadilifu gani unahukumu hivyo!

b. Kubadilisha kwake ukweli katika kunakili nususu zilizokatwa ambazo hubadilisha maana. Naye anasema mwishoni mwa utangulizi wake: “Aghlabu nimetilia umuhimu kunakili herufi kwa herufi, ili kuchunga neno mahali pake na dharura ya umakini kati- ka kunakili na…. Na hili ndilo linalolazimishwa na njia ya kielimu katika kunakili maneno ya hasimu.” – Je, mstahiki Dk. amejilaz- imisha na hilo?

Katika ukurasa wa 252 Juz. 2, ametaja Hadithi katika usemi wake kuhusu kumuona Mwenyezi Mungu kutoka kwa Ibnu Babuwayh al-Qummiy kutoka kwa Abu Baswiri kutoka kwa Abu Abdillahi (a.s.), alisema: Nilimwambia: Nipe habari kuhusu Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla, waumini watamuona siku ya Kiyama? Alisema: Naam.

Na anainakili riwaya hii katika kitabu Tawhidu Uk.117 lakini hakuisema riwaya kamilifu, ni jambo ambalo limebadilisha maana kamili. Riwaya kamili yakujia na uamuzi ni wako.

“Alisema: Nilimwambia: Nipe habari kuhusu Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla. Waumini watamuona Siku ya Kiyama? Alisema: Ndio, na walikwishamuona kabla ya Siku ya Kiyama. Nilisema: Lini? Alisema: Alipowaambia, Je siko Mola wenu. Wakasema: Uko Mola wetu.

Halafu alinyamaza – yaani Imam – kwa muda halafu akasema: Kwa kweli waumini ni wenye kumuona duniani kabla ya Siku ya Kiyama, je humuoni katika muda wako huu? Abu Baswiru anasema: Nilimwambia: Nimejitoa muhanga kwa ajili yako, nitahadithia haya kutoka kwako.

Akasema: - Imam: Hapana, kwa kuwa wewe ukihadithia hayo, mkanushaji akikanusha akiwa hajui maana ya usemayo halafu akadirie kuwa hiyo ni tashbihu, atakufuru. Kuona kiroho si kama kuona kwa macho, Mwenyezi Mungu yu mbali na wanayomsifu nayo mushabihuna na waliopotoka.”

Waona umbali ulioje kati ya maana ya kwanza na ya pili, bali maana ya kwanza kwa tamko kamili la riwaya ni miongoni mwa kauli za Mushabihuna na wapagani waliopotoka mbali na itikadi sahihi ya Mwenyezi Mungu.

Kwa nini hakunakili kauli ya Imam Baqir alipoulizwa na al- Kharijiy. “Alimwambia: Ewe Abu Jafar waabudu kitu gani? Akasema: Allah. Al-Khaarijiy akasema: Umemuona? Akasema: Ndio. Macho hayajapata kumuona kwa kushuhudiwa na uoni wa macho lakini nyoyo zimemuona kwa imani ya kweli. Hajulikani kwa kukisia wala kudirikiwa kwa hisi. Yuasifika kwa alama, maarufu kwa dalili. Hafanyi dhulma katika hukumu yake, huyo ni Mwenyezi Mungu hapana Mola apasaye kuabudiwa ila Yeye.12

Na miongoni mwa ushahidi pia wa kuikata riwaya ni maneno yake kuhusu jinsi Mwenyezi Mungu alivyo. Hivyo ananakili riwaya kutoka Biharul-Anwar kutoka kwa Abu Abdillahi Ja’far Sadiq (a.s.) kuwa aliulizwa kuhusu Allah: “Je ataonekana siku ya miadi?”
Akasema: “Ametakasika Subhana na Yu mbali na hayo, yuko juu kabisa…Kwa kweli macho hayawezi kudiriki ila chenye rangi na umbo na Mwenyezi Mungu ni Muumba wa rangi na umbo.”13

Na anasema baada ya hayo: “Na inadhihiri hoja waliyoitoa hao walioiweka riwaya hii kuwa ni ya Ja’far Sadiq (a.s.), ndani yake mna maana ya kukanusha kuwepo kwa haki, kwa sababu kisichokuwa na umbo kabisa hakipo.”14

Kwanza tunatoa maoni kuihusu kanuni hii, halafu tutataja ushahidi wa kuikata Hadithi.

Kauli yake: Kisichokuwa na umbo kabisa maana yake hakipo. Na ameitaja kanuni hii ya ajabu ya aina yake! ili kuitangua Hadithi ya Imam Sadiq (a.s.) iliyotangulia. Na ukweli ni kwamba akili haikupata nuru kwa riwaya ya Ahlul-Bayt, na imeleleka kwa riwaya za Kaabul-Akhbari na Wahbu bin Munabih, hafahamu Hadithi za Ahlul-Bayt. Basi nini anakusudia kwa kauli yake: Kabisa. Je anakusudia kisichokuwa na umbo katika jumla ya yasemwayo kuwa yana umbo?

Ikiwa anamaanisha hivyo ndivyo, kwa kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) Yu nje ya yasemwayo kuwa yana umbo. Hazungukwi na maana iliyo kwenye neno wapi, upande, au mahali. Na asemaye kuwa Mwenyezi Mungu anajaaliwa umbo kwa haya yasemwayo yaliyo maarufu katika umbo, atakuwa amekufuru, na amemsifu Mwenyezi Mungu kwa sifa za mada – matter, kwa sababu umbo ni miongoni mwa yanayolazimiana na mwili – matterial – na vyenye mipaka, na Mwenyezi Mungu hana mpaka na Yeye si mada (matter).

Na hili ndio kosa ambalo mwandishi ameliingia, alipofanyia taswira kuwa Allah (s.w.t.) anaweza kufanyiwa taswira kwa umbo, na hili linarejea kwenye upinzani wa hisia zake, hivyo hawezi kufahamu ila kwenye mipaka ya hisi. Kwa ajili hiyo anakanusha kuwepo kwa kila chenye kuwepo ambacho kipo nje ya wigo wa umbo.

Ama ikiwa anakusudia umbo nje ya yasemwayo kuwa yana umbo yaliyo maarufu, haya hayaitwi umbo. Hivyo basi maneno yake hayana msingi.

Halafu anataja sehemu tu ya riwaya ili atiliye nguvu kwayo maneno yake na athibitishe kuwa riwaya za Shia zinapingana, anasema: “Kama ambavyo haya yanapingana na aliyoyaeleza mwandishi wa kitabu al-Kafiy kutoka kwa Abu Abdillahi kuwa: walakini hapana budi kuthibitisha kuwa yeye analo umbo ambalo mwingine hastahiki mbali na yeye wala hashirikishwi humo wala hazungukwi nalo, wala halijui asiyekuwa Yeye.”15

Riwaya hizo zakujia kikamilifu ili nikuthibitishie kinyume na alivyodai:

“Muulizzaji akasema: ‘Utakuwa umemfanyia mpaka ukithibitisha kuwepo kwake.’ Abu Abdillahi (a.s.) akasema: ‘Sijamfanyia mpaka, lakini mimi nimemthibitisha, kwa kuwa hakuna kati ya kukanusha na kuthibitisha daraja.’ Muulizaji akasema: ‘Hivyo anayo wapi na dhati?’ Akasema: ‘Kitu hakithibiti ila kwa wapi na dhati.’ Muulizaji akasema: ‘Analo umbo?’ Alisema (a.s.): ‘La kwa kuwa umbo ni upande wa sifa na kuzingira.

Lakini hapana budi kutoka upande wa kubatilisha na wa kushabihisha, kwa kuwa mwenye kumkanusha amemkataa na kuondoa umola Wake na ameubatilisha. Na mwenye kumshabihisha na kingine anakuwa amemthibitisha kwa sifa za viumbe wenye kusikika ambao hawastahiki umola, lakini hapana budi kuthibitisha kuwa analo umbo ambalo hastahiki mwingine, wala hashirikiani katika hilo wala halizingirwi wala halijui mwingine.’’16

Soma na zingatia maana inayofidishwa na riwaya hii, ni tofauti kabisa na aliyoyasema: “Kisichokuwa na umbo kabisa hakipo” Kwa hiyo muulizaji kumwambia Imam: ‘Analo umbo?’ Alisema (a.s.): ‘La’ kuipinga kanuni hii aliyoitolea ushahidi kwa Hadithi iliyokatika.

Hivyo umbo ambalo mwandishi analikusudia na kuitakidi ni umbo ambalo ni miongoni mwa ambayo maudhui hukumbwa nalo. Imam amemtakasa mbali nazo kwa jibu lake kwa muulizaji: ‘Kwa kuwa umbo ni upande wa sifa na kuzingira.’ na hii haijiri kwa Allah (s.w.t.).
Ama umbo ambalo Imam amelisema mwisho wa Hadithi: “Umbo ambalo hastahiki mwingine, wala hashirikiani katika hilo wala halizingirwi wala halijui mwingine” umbo hili japo liitwe umbo uitwaji huo ni aina ya majazi, kwa sababu ya upungufu wa msamiati wa Lugha na haikuitwa umbo ila ni katika mlango wa ushirikiano wa kitamko. Hivyo tamko limeshirikiana na maana iko tofauti.

Na riwaya hii ameieleza Ibnu Babuwayh al-Qummiy kwa sanadi hii hii na matamshi haya haya: “Lakini hapana budi kuithibitisha dhati bila umbo, hastahiki mwingine wala hashirikishwi katika hiyo wala kuzingirwa wala haijui mwingine.”

Riwaya hii inaondoa mashaka na yabainisha makusudio kamili, nayo ni kukanusha sura zote za umbo. Kwa kuwa kumthibitishia nazo Mwenyezi Mungu ndiyo tashbihi yenyewe bali makusudio ya hizo sifa ni kuthibitisha sifa zake zote za ukamilifu nazo ndio Dhati Yake.

2) Ihsan Ilahiy Dhahiir: Naye ni miongoni mwa waandishi maadui wakubwa wa Shia. Na ana jumla ya vitabu katika kuwajibu Shia, vya msitari wa mbele katika hivyo ni vinne:

Shia na Sunnah.

Shia na Ahlul-bayt.

Shia na Qur’ani.

Shia na Tashayuu.

Na kwa kweli ametumia uwezo wake wote kuwajibu na kujiingiza kwenye fikra zao. Tunatamani angekuwa msafi mwaminifu mwenye tabia njema na adabu. Amewasingizia Shia ambayo yawezayo muotesha mvi kijana mdogo na kumfanya mtu mzima awe mzee. Na mimi namuita kila mwenye akili timamu avisome vitabu vyake, halafu aangalie. Kwanza: Utaratibu wake, pili: Masingizio yake. Tatu: Kubadilisha kwake baada ya kufanya rejea vitabu vya Shia ambavyo vinachukua maudhui hiyo hiyo.

Na hapa natosheka na kutaja baadhi ya shuhuda kwa sababu nafasi hairuhusu kujibu na ufafanuzi. Na kabla sijajishughulisha na kubadilisha kwake ukweli, nakuelekeza kwenye mazingatio mawili ya haraka, njia yake ya kutupa na njia yake ya kutoa fikra.

a. Zingatio la kwanza: Njia yake inajikita katika kuorodhesha itikadi za Shia kwa utaratibu potovu chini ya vichwa vya habari vinavyochukiza, ili afanye kizuizi kati ya msomaji na itikadi za Shia. Ambalo lingepaswa liwe ni angekuwa anafuata njia salama katika kujibu, kwanza azitaje itikadi za Shia, halafu azitaje dalili zao na baada ya hapo azijibu kwa dalili na burhani, halafu alete dalili za anayoyaamini.

Na mfano wa hilo, anasema katika kitabu chake Shia na Sunna Uk. 53, chini ya anwani ‘Mas’ala ya Badau’: “Ilikuwa kati ya fikra alizozieneza Myahudi na Abdullah bin Saba’a ni kuwa Mwenyezi Mungu hupatwa na Badau. Yaani kusahau na kutojua, Mwenyezi Mungu Yu juu mbali na wanayoyasema.”

Halafu anazitaja riwaya kutoka vitabu vya Shia kuhusu Badau bila ya kuz- itaja dalili za Shia kuihusu Badau kutoka vitabuni na riwaya za Bukhari na Muslim, na kauli za wanavyuoni wa kisunni, na dalili ya kiakili, na bila ya kuweka wazi ufahamu wa Badau kwa Shia, isipokuwa huitambulisha kulingana na utashi wake kuwa ni kusahau na ujinga.

Na anajengea juu ya utambulisho huu wa makosa tafsiri yake ya riwaya ya Shia kuwa ndio tafsiri ya Shia ya Badau. Hali yake hii ni sawa na hali yake katika mas’ala ya Taqiyah, hivyo anasema katika Uk. 127 chini ya anwani ‘Shia na uwongo.’ Anaanza kwa kusema: “Shia na uwongo kana kwamba ni matamko mawili yenye maana moja hakuna tofauti kati yao. Yamekuwa pamoja toka siku ambayo madhehebu hii iliasisiwa na yakawa humo. Hivyo basi mwan- zo wake si kingine ila ni uwongo na kwa ajili ya uwongo…”

Halafu analitolea hoja hilo anasema: “Madamu Ushia ni mtoto wa uwon- go walioupaka rangi ya utakaso na utukufu na kuuita jina si lake, na kwa ajili yake wamelitumia neno Taqiyyah…”

Nakuulizeni – kwa jina la Mungu – ni njia gani hii katika mjadala wa kielimu, unahujumu na kudhihaki bila ya fahamu vipi imekuwa jaizi kwake aifasiri Taqiyyah kuwa ni uwongo? Hali ikiwa Qur’ani imelitumia neno hili, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema:

لَا يَتَّخِذِ الْمُؤْمِنُونَ الْكَافِرِينَ أَوْلِيَاءَ مِنْ دُونِ الْمُؤْمِنِينَ ۖ وَمَنْ يَفْعَلْ ذَٰلِكَ فَلَيْسَ مِنَ اللَّهِ فِي شَيْءٍ إِلَّا أَنْ تَتَّقُوا مِنْهُمْ تُقَاةً ۗ وَيُحَذِّرُكُمُ اللَّهُ نَفْسَهُ ۗ وَإِلَى اللَّهِ الْمَصِيرُ {28}

Wenye kuamini wasiwafanye makafiri kuwa viongozi badala ya wenye kuamini, na atakayefanya hivyo, basi hana chochote kwa Mwenyezi Mungu, ila mtakapojilinda nao kwa kujihifadhi. Na Mwenyezi Mungu anawatahadharisha na nafsi yake, na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo.” (Surat al-Imran: 28).

Na kwa maana kama hiyo katika Aya nyingine:

مَنْ كَفَرَ بِاللَّهِ مِنْ بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَٰكِنْ مَنْ شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِنَ اللَّهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ {106}

“Anayemkataa Mwenyezi Mungu baada ya imani yake isipokuwa yule aliyelazimishwa hali moyo wake unatulia kwa imani, lakini anayefun- gua kifua kwa kufru, basi ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yao, na watapata adhabu kubwa.” (Surat an-Nahl: 106).

Taqiyah maana yake ni: Kuficha imani na kudhihirisha kinyume chake, endapo mtu atahofia nafsi yake, mali yake, na heshima yake. Na hili mwislamu yoyote hayuko kinyume nalo, kwa sababu anayekirihishwa hana hesabu iwapo atafanya analokirihishwa kulifanya.

Bali wakati mwingine huwa wajibu kufanya Taqiyah, ikiwa kutokufanya taqiya kutasababisha madhara kwa wengine au kwa maslahi ya risala na dini, kama walivyofanya muumini wa Aali Firaun, na hivyo katika hali ya dharura hukumu yatoweka mbali na maudhui yake.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema:

فَمَنِ اضْطُرَّ غَيْرَ بَاغٍ وَلَا عَادٍ فَلَا إِثْمَ عَلَيْهِ ۚ إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَحِيمٌ {173}

“Basi mwenye kushikwa na haja kubwa pasi na kutaka wala kutoka katika mpaka, huyo hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.” (Sura al-Baqarah: 173).

Ihsan Dhwahir hakukusudia kwa hili ila kufanya hadaa na laghai kwa njia ya werevu. Kwa hiyo Taqiyah anaipa tafsiri kuwa ni uwongo na kuiweka katika habari ambazo huzingatiwa kuwa salama. Na hili linapothibiti katika akili ya msomaji humkusanyia kundi la riwaya za kishia ambazo zinasema wazi Taqiyah, na anamuwekea msomaji mahali pa Taqiyyah neno uwongo, na hatimaye kupata maana inayomfanya ayachukie yale wase- mayo Shia.

Na mimi hapa sipo katika hali ya kujibu au kuthibitisha wasemayo Shia, kwa sababu hakua tayari kufanya naye mjadala, na hajatoa dalili hata moja iliyo kinyume ili ipate kujibiwa. Ambalo ni muhimu kwetu hapa ni kubainisha utaratibu wake na njia yake tu.

b. Zingatio la pili: Sio mantiki kuidhihaki itikadi ya mtu mwingine na kuihukumu kuwa ni batili kwa sababu tu inapingana na itikadi yako. Lakini yasikitisha, huu ndio utaratibu wake na utaratibu wa wengine miongoni mwa waandishi. Kila kitu ni kinyume na tuliyosema. Swala yao sio kama swala yetu, swaumu yao sio kama swamu yetu na zaka yao si kama zaka yetu…

Kama kwamba wao ndio kigezo cha dini na ni maimamu wa waislamu, kwamba hapana budi kila kitu kizunguke kwenye jiwe lao.

Wakiwa kwa hilo wanavuka kanuni isemayo: Sisi tu pamwe na dalili tunaelemea ielemeako.
Na hii ni kinyume na utaratibu wa Qur’ani katika utafiti na mjadala wa kielimu ambao unatambua pande mbili, Mwenyezi Mungu anamfundisha Mtume wake jinsi ya kusema na makafiri na washirikina. Anasema (s.w.t.):

وَإِنَّا أَوْ إِيَّاكُمْ لَعَلَىٰ هُدًى أَوْ فِي ضَلَالٍ مُبِينٍ {24}

“Na bila shaka sisi au nyinyi tuko juu ya uongofu au katika upotovu ulio wazi.”
(Sura Sabaa: 24).

Angalia muamala huu wa tabia njema, hakusema kuwa mimi niko kwenye haki na ninyi mko kwenye upotovu, bali amesema ima ni sisi au ninyi tuko katika haki au katika batili, huu ndio utaratibu wa Qur’ani ilipoiletea jamii uhuru wa kujadili ikisema: “Sema: Leteni dalili yenu kama nyinyi ni wakweli” (Surat Al-Baqarah: 111).

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alikuwa anasikiliza uthibitisho wao na kuujibu kwa jibu lile ambalo ni jema. Qur’ani imesajili mifano mingi sawa iwe pamoja na Mtume Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) au pamoja na manabii waliopita.

Katika kisa cha Ibrahim na Namrudu, Musa na Firauni, ni mazingatio bora. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amethibitisha hoja na thibitisho nyingine za makafiri katika Qur’ani yake na amezipa utakatifu ule aliozipa Aya zingine miongoni mwa Aya za Qur’ani, wala hakujuzisha kwa mwislamu aziguse bila ya udhu. Kwa mujibu wa fiqhi ya Shia.

Ihsanu Dhwahiri na walio mfano wake wako wapi wao na njia hii ya Qur’ani ya asili. Na yeye - yaani Ihsanu Dhwahiir - anajifaharisha binafsi na jamaa zake akisema: “Wasomaji wa Qur’ani ambao wanaisoma nyakati za usiku na nyakati za mchana.”17

Nini faida ya aisomaye Qur’ani na kuzifanyia tartili Aya zake wala hazizingatii, apate kutoka humo uoni na uelewa, ambao utamfichulia njia yake maishani na ajifunze kutokana nayo jinsi ya kuwatendea watu wengine wanaokuwa kinyume naye katika itikadi na madhehebu, lakini Imam Ali (a.s.) amesema kweli aliposema: “Ni wasomaji wangapi wa Qur’ani hali Qur’ani yawalaani.”

Mifano Ya Ubadilishaji Wake:

i) Amenakili katika kitabu chake Shia Wa Ahlul-Bayt, Uk. 40 tamko la Imamu Ali (a.s.) kutoka katika Nahjul-Balaghah, akitolea dalili kuwa Imam Ali anaikubali Shura wala hatambui tamko rasmi, na kuwa Shura ya Muhajirina na Answar ndio ridhaa ya Allah. Uimamu hauwi bila yao. Hiki ndicho alichokichopoa kutoka katika maelezo ya Ali (a.s.). Nayo kama ujuavyo ni utanguzi kamili wa wayasemayo Shia. Na haya hapa maelezo ambayo yeye ameandika akidai kuwa ndani yake ametoa tija hiyo:

“Kwa kweli Shura ni ya Muhajirina na Answari tu. Wakiafikiana kwa ajili ya mtu, na wakamuita imamu hiyo huwa ndio ridhaa ya Mwenyezi Mungu, endapo akitoka mtokajinje ya Shura hii - kwa kebehi au uzushi watamrudisha alikotoka, akikataa watampiga kwa sababu ya kufuata kwake njia isiyokuwa ya waumini, na Mwenyezi Mungu atamuweka alipojiweka.”

Na baada ya kufanya kwangu rejea kwenye vyanzo imenibainikia kuwa huyu mtu si mwaminifu katika kunakili kwake, kwa kuwa yeye amekata alichopenda katikati ya maneno na ameacha mwanzo wake na mwisho wake ili apotoshe ukweli na aubadilishe.

Haya hapa maelezo ya Imam (a.s.) yakiwa kamili ambayo kwa kukamilika kwake ufahamu wote hubadilika, na itabainika kuwa alilosema Imam (a.s.) lilikuwa katika mlango wa mithali isemwayo:
Walazimisheni ambalo wenyewe wamejilazimisha nalo. Na hii ni hotuba kutoka kwa Imam Ali (a.s.) kwa Muawiyyah.
“Kwa kweli wamenifanyia baia kaumu ile ambayo ilimfanyia baia Abu Bakr, Umar na Uthman kwa taratibu zile ambazo ziliwafanya wawafanyie baia. Aliyekuwa hadhiri hakuwa na hiari wala asiyekuwa hadhiri hakuwa na haki ya kukataa, kwa kuwa Shura ni ya Muhajirina na Answari tu, wakiafikiana.

Kwa umri wangu ewe Muawiyah lau ungeangalia kwa akili zako si kwa utashi wa nafsi yako ungenikuta mimi ni asiye na dhambi kabisa miongoni mwa watu kuihusu damu ya Uthman, na ungejua kuwa mimi nilikuwa nimejitenga mbali nayo, ila ikiwa utasingizia basi singizia upendavyo wasalamu.”18

Hivyo basi Amirul-Muuminina alileta hoja dhidi ya Muawiyyah ile ambayo Muawiyah alikuwa anaileta na bado wafuasi wake wanaileta hoja hiyo mpaka hii leo, kutetea usahihi wa ukhalifa wa Abu Bakr, Umar na Uthman. Ali (a.s.) akawalazimisha kwa hoja yake mwenyewe, yaani hoja ya Muawiyyah mwenyewe.

Alisema: Ikiwa baia ya makhalifa waliokuwa kabla yangu ilikuwa sahihi kwa hiyo baia yangu ni mfano wa yao. Watu wamekwisha nifanyia baia wala hapana njia kwa mwenye kukataa baada ya baia kutimia, hana haki ya mwenye kuhudhuria baia achague kama ilivyotokea katika ile baia ya Umar baada ya Abu Bakr kumwainisha. Wao hawakuwa na hiari baada ya kuainishwa kwake, wala kwa asiye kuwepo kuikataa, kama ambavyo Imam (a.s.) hakuweza kuikataa baia ya Abu Bakr iliyofanyika ndani ya saqifa, kwa kuwa ilikuwa kwa kificho.

Hii ndio Shura mliyojigamba nayo, sawa iwe kuhusu uamiiri wa Abu Bakr, Umar, au Uthman. Hiyo ni ridhaa ya Mwenyezi Mungu kama mnavyodai. Haifai atoke humo mtokaji vinginevyo atarudishwa kama walivyorudishwa wazuia zaka walipokataa kumpa Abu Bakr, kwa sababu hawakumtambua kuwa ni khalifa kisheria kwa maoni yao. Kwa mantiki hiyo ewe Muawiyah hauna nafasi kwa kuwa watu wameafikiana kunifanyia baia ila ikiwa utafanya uovu basi fanya uovu upendavyo.

Hii ndiyo maana inayofidishwa na muktadha wa jumla, lakini haikupendezewa na utashi wa binafsi wa Ilahiy Dhwahiir.

ii) Katika kitabu chake ameileta Hadithi kutoka katika tafsiri iliyonasibishwa na al-Hasan al-Askariy, anasema humo: “Mtu miongoni mwa wanaowachukia Aali Muhammad na swahaba wake wa kheri..... au mmoja katika wao Mwenyezi Mungu atamwadhibu adhabu….. lau igawanywe sawa ya idadi ya viumbe wa Mwenyezi Mungu ingewahilikisha wote.”19

Halafu anasema: “Kwa ajili hiyo babu yake mkubwa Ali bin Musa aliye na lakabu ya ar-Ridha – Imamu wa nane kwa Shia – alipoulizwa kuhusu kauli ya Nabii (s.a.w.w): ‘Swahaba wangu ni kama nyota, yeyote mumfuataye mtaongoka.’ Na kuhusu kauli yake: ‘Niachieni swahaba wangu.’ alisema (a.s.): ‘Hii ni sahihi.”’20

Anataka kuleta dalili kwa hayo kuwa mtazamo wa Ahlul-Bayt kwa swahaba ulikuwa unazingatia kuwa wote ni waadilifu, hivyo si haki kwa Shia kumkebehi na kumuumbua yeyote katika wao, vingievyo inakuwa wanakhalifu kauli za Maimamu wao.

Zingatia uwongo huu wa wazi nitakaponakili kwa ajili yako maelezo kamili:

“Alisema: Baba yangu alinihadithia, akasema: Aliulizwa ar-Ridha (a.s.) kuhusu kauli ya Nabii (s.a.w.w): ‘Swahaba wangu ni kama nyota, yeyote mumfuataye mtaongoka.’ Na kuhusu kauli yake: ‘Niachieni swahaba wangu,’ akasema (a.s.):

‘Hii ni sahihi. Anamkusudia yule asiyegeuza baada yake wala kubadilisha.’ Palisemwa: Vipi atajua kuwa wao waligeuza na kubadilisha? Akasema: ‘Ni vile wapokeavyo kuwa (s.a.w.w.) alisema:
Watakuja kuzuiliwa watu miongoni mwa swahaba wangu siku ya Kiyama mbali na hodhi yangu kama wazuiliwavyo ngamia wa kigeni mbali na maji, hivyo nitakuwa ninasema: Ewe Mola wangu, swahaba wangu swahaba wangu. Nitaambiwa: Kwa hakika wewe hujui waliyoyazusha baada yako. Hivyo watachukuliwa upande wa kushoto nitakuwa ninasema: Wawe mbali wawe mbali. Hivyo utaona hii ni kwa asiye geuza wala kubadili.”21
.
Angalia yaliyofanywa na khiyana katika kunakili Hadithi, ni jinsi gani ilivyobadilisha kabisa ufahamikaji wake, je sijakuambieni kuwa yeye ni mwongo?!

Na kauli ya Imam (a.s.): “Ni vile wapokeavyo” yaani hiyo ni riwaya wanayoieleza wanahadithi wao na mahafidhu wao katika Ahlu Sunnah. Na ili kusadikisha kauli ya Imam (a.s.) nitakunakilia baadhi ya riwaya ambazo zimekuja katika al-Bukhariy na Muslim.

Bukhari katika tafsiri yake ya Surat al-Maidah, mlango wa: Ewe Nabii fikisha yaliyoteremshwa juu yako. Na tafsiri ya Surat Anbiyai kama alivyoeleza Tirmidhi katika milango ya sifa ya Kiyama, mlango wa mkusanyiko. Na tafsiri ya Surat-Taha: “Kwa kweli wataletwa watu katika umma wangu watachukuliwa kushoto.

Nitakuwa ninasema: Ewe Mola wangu hao ni swahaba wangu, patasemwa: Kwa kweli wewe hujui waliyoyazusha baada yako, hapo nitakuwa ninasema kama alivyosema mja mwema: Na nilikuwa shahidi juu yao nilipokuwa nao, na uliponifisha, wewe ukawa Mchungaji juu yao, na wewe ni shahidi juu ya kila kitu. Patasemwa: Kwa kweli hao waliendelea kuritadi kinyume mbali na itikadi yao toka ulipofarakana nao.”

Na Bukhari ameeleza katika kitabu Daawati, mlango wa Hodhi. Na Ibn Majah katika Kitabu cha ibada za Hija, mlango wa hotuba ya siku ya kuchinja. Hadithi namba 583. Kama ambavyo Ahmad ameileta katika Musnad yake kwa njia nyingi: “Watanijia watu miongoni mwa swahaba wangu kwenye Hodhi mpaka nitakapowatambua, wataburuzwa mbali na mimi, nitakuwa ninasema: Swahaba wangu. Patasemwa: Hujui waliyoyazusha baada yako.

Na katika Sahih Muslim, Kitabu cha fadhila, mlango wa kuthibitisha Hodhi ya Mtume wetu, Hadithi ya 40: ‘’Watanijia kwenye Hodhi watu miongoni mwa waliokuwa swahaba wangu, mpaka nitakapokuwa nimewaona, watanyanyuliwa na kuburuzwa mbali na mimi, kwa hakika nitakuwa ninasema: Ee Mola wangu! Swahaba zangu, kwa kweli nitaambiwa: Kwa hakika wewe haujui waliyozusha baada yako.’’

Na Bukhariy ameeleza pia: ‘’Kwa hakika mimi ni mtangulizi wenu kwenye Hodhi, mwenye kunipitia atakunywa, na mwenye kunywa hatokuwa na kiu abadan. Watanijia kaumu ya watu, nawatambua na wananitambua, halafu patazuiliwa kati yangu na wao, nitakuwa ninasema: Swahaba wangu, patanenwa: Kwa kweli wewe hujui waliyoyazusha baada yako, nitasema: Awe mbali, awe mbali aliyebadili baada yangu.’’

Lau si kuhofia kutoka nje ya maudhui ningepanua maelezo katika nafasi hii.

Ewe Ihsan, ikiwa mkono wako umenyooka ili ubadilishe yaliyokuja katika Hadithi za Shia, kwa hakika wewe hautoweza kubadilisha yaliyokuja katika Sahihi zenu.

iii) Ameleta katika Uk.66. Katika kitabu hicho hicho Hadithi ya Imam Ali (a.s.) kutoka katika Nahjul-Balaghah, alichonakili yeye ni hiki hapa: ‘’Niacheni na mumtafute mtu mwingine, na mimi ni kama mmoja wenu na huenda mimi ni mwenye kusikiliza mno na mtii mno wa mliyemtawaza jambo lenu. Na mimi nikiwa waziri ni bora kwenu kuliko nikiwa amiri.”

Na niliporejea kwenye chimbuko la maelezo nilikuta ujanja na hila zake, kwa kuwa amechukua mwanzo wa maneno na mwisho wake na akaacha yaliyo kati ya sehemu mbili hizo, kwa kufanya hivyo maana inabadilika. Basi ni haya hapa maelezo kamili
Alisema watu walipomtaka kwa ajili ya baia, baada ya kuuliwa Uthman: “Niacheni na mtafuteni mwingine, kwa kweli sisi tunalingoja jambo lenye njia nyingi na rangi nyingi, nyoyo hazisimami kwa hilo wala akili hazithibiti juu yake. Kwa kweli pambizo zimetanda mawingu na nyoyo zimekataana. Na juweni kuwa mimi nikikuitikieni nitawatwisheni nijuwavyo wala sitosikiliza usemi wa msemaji wala lawama ya mwenye kulaumu, endapo mtaniacha basi mimi ni kama mmoja wenu na huenda mimi ni msikivu mno na mtii mno wa mtakayemtawaza jambo lenu, na mimi kuwa waziri ni bora kwenu kuliko kuwa amiri.’’22

Angalia sehemu ya maelezo aliyoifuta, ni jinsi gani maana inavyogeuka kichwa chini miguu juu, hii itaitwaje, ewe Ihsan?! Na ni nani ambaye anawasingizia Ahlul-Bayt?! Aina za uwongo sio tu kusema neno na kulinasibisha kwa asiyelisema, bali ni uwongo pia ubadilishe makusudio ya usemi wa msemaji wake na udai ndivyo alivyokusudia.

Subhanallah! Amirul-Muuminiina alijua kuwa wao hawatokuwa thabiti juu ya baia hii na watageuka dhidi yake na kumpiga vita katika Jamal, Swifin, na Nahrawan, na watamletea hoja kwa maelfu ya kujiosha, kwa ajili hiyo aliwawekea hoja, na aliwaambia mbinu zake katika kuhukumu, na si nyingine ila ni haki, na haki ni chungu na ngumu., kama alivyosema (s.w.t.): “Na wengi wanaichukia haki” (Surat Muuminuna: 70).

Lilitokea hili alilosema (a.s.) kivitendo. Lakini nilikuwa sitazamii kuendelea mapinduzi na kujikosha huku mpaka hii leo, kwani bado wangali wanabadilisha usemi wake, hilo linaweka wazi nia mbaya na kupotoka kwa waliomfanyia baia.

iv) Ninahitimisha kwa udanganyifu huu na kubadilisha huku kuliko wazi, na ninakuachia wewe utoe maoni yako na nitatosheka nayo, kwa kuwa mimi lau ningeendelea na mfumo huu wa udanganyifu na kubadilisha nafasi ingetuwia ndefu, na kwa muhtasari huyu mtu hakuwa mkweli hata kwake mwenyewe binafsi. Na lililomfanya afanye matendo haya ni uadui wake mkali dhidi ya Ahlul-Bayt na Shia wao, vinginevyo kwa nini ushupavu huu wa wazi? Je yuataka kuwathibitishia watu haki iliyopotezwa? Hali akiwa anafuata batili na udanganyifu kuwa ndio njia na lengo?!

Ameleta katika kitabu chake Shia Wa Ahlul-Bayt Uk. 67: “Na Tabrasiy pia ananakili kutoka kwa Muhammad al-Baqir, linalokata shauri kuwa Ali alikuwa anaukubali ukhalifa wake na anatambua uimamu wake, na ni mwenye kula kiapo cha utii wa uamiri wake, kama anavyosema kuwa, Usama bin Zayd aliyekuwa mpenzi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu alipokuwa anataka kutoka, Mtume wa Mwenyezi Mungu aliaga dunia. Barua ilipomfika Usama alitoka pamoja na aliokuwanao mpaka aliingia mji wa Madina, alipoona mkusanyiko wa watu kwa Abu Bakr, alikwenda kwa Ali bin Abu Talib (a.s.), akasema: ‘Nini hiki?’ Ali (a.s.) akasema: ‘Hayo ndio uyaonayo.’ Usama akasema: ‘Je umemfanyia baia?’ Akasema: ‘Ndio’”.

Na anadai amenakili tukio hili kutoka katika kitabu Ihtijaju cha At- Tabrasy, sasa haya hapa maelezo kamili kutoka chanzo chake:

“Imeelezwa kutoka kwa al-Baqir (a.s.) kuwa, Umar bin al-Khattabi alimwambia Abu Bakr: ‘Mwandikie Usama bin Zayd aje kwako kwa sababu kuja kwake ni kuwakata Shia mbali na sisi.’ Ndipo Abu Bakr akaandikia: ‘Kutoka kwa Abu Bakr Khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kumwendea Usama bin Zayd. Ama baad, angalia ikikufikia barua yangu njoo kwangu wewe na ulionao, kwa kuwa waislamu wameafikiana juu yangu na wamenitawaza jambo lao, usifanye kinyume, utakuwa umeasi na yatakujia kutoka kwangu usiyoyapenda. Wasalaam.’

“Alisema: Usama alimwandikia jibu la barua yake: ‘Kutoka kwa Usama bin Zayd mtendaji wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) katika shambulio la Sham. Ama baad.

Imenijia barua kutoka kwako ambayo mwanzo wake unapingana na mwisho wake, umesema mwanzoni kuwa wewe ni Khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, na umesema mwishoni mwake kuwa waislamu wameafikiana juu yako wewe na wamekutawaza jambo lao na wamekuridhia.
Hivyo, jua kuwa mimi na nilio pamoja nao miongoni mwa jamaa wa kiislamu na Answar, hapana wallahi hatujakuridhia na wala hatujakutawaza jambo letu. Na angalia uitoe haki kwa wenyewe, uwaachie jambo hili wao kwa kuwa wao ndio wenye haki mno ya jambo hili kuliko wewe.

“Umejua kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) ilivyokuwa kumhusu Ali siku ya Ghadir muda haujawa mrefu iwe umesahau, angalia nafasi yako wala usiende kinyume utakuwa umemuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake (s.a.w.w) na kumuasi aliyefanywa na Mtume wa Mwenyezi Mungu kuwa khalifa juu yako na juu ya swahiba wako, wala hakuniengua mpaka amekufa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) na kwa kweli wewe na swahiba wako mlirejea na mliasi - anamkusudia Umar - na mlibaki Madina bila ya idhini.’

“Abu Bakr alitaka kuuvua ukhalifa kutoka shingoni mwake, Umar alimwambia: ‘Usifanye hivyo, kanzu Mwenyezi Mungu amekuvisha usiivue utakujajuta, lakini mshikilie kwa barua na wajumbe, na mwamrishe fulani na fulani wamwandikiye Usama asiitenganishe jamaa ya kiislamu na aingiye pamoja nao katika walilofanya. Ndipo Abu Bakr alimwandikia na pia wale watu miongoni mwa wanafiki nao walimwandikia: ‘Ridhia tuliloafikiana, na ole wako uwaingize waislamu kwenye machafuko kutoka kwako, kwa kuwa wao wana muda mfupi kutoka katika ukafiri.’

“Alisema: Barua zilivyomfika Usama aliondoka pamoja na alionao mpaka aliingia Madina. Alipoona mkusanyiko wa watu kwa Abu Bakr alikwenda kwa Ali bin Abi Talib (a.s.) na akamwambia: ‘Nini hii?’ Ali alimwambia Usama: ‘Hivi ni kama uonavyo.’ Usama alimwambia: ‘Je umemfanyia baia?’ Akasema: ‘Ndio ewe Usama.’ Alisema: ‘Kwa utii au kwa kukirihishwa?’ Akajibu: ‘Hapana bali kwa kukirihishwa.’

“Akasema: Usama aliondoka na aliingia kwa Abu Bakr na alimwambia:

‘Assalamu alayka ewe khalifa wa waislamu.’ Abu Bakr alimjibu na akasema: ‘Assalamu alayka ewe amiri.”23

Wala hatutamwambia zaidi ya alivyosema Mwenyezi Mungu katika kitabu chake kilichozatitiwa kitukufu:

انْظُرْ كَيْفَ يَفْتَرُونَ عَلَى اللَّهِ الْكَذِبَ ۖ وَكَفَىٰ بِهِ إِثْمًا مُبِينًا {50}

Tazama namna wanavyotunga uongo juu ya Mwenyezi Mungu, na linatosha hilo kuwa ni dhambi iliyo wazi.” (Surat An-Nisai: 50).

Na kama alivyosema:

فَبِمَا نَقْضِهِمْ مِيثَاقَهُمْ لَعَنَّاهُمْ وَجَعَلْنَا قُلُوبَهُمْ قَاسِيَةً ۖ يُحَرِّفُونَ الْكَلِمَ عَنْ مَوَاضِعِهِ ۙ وَنَسُوا حَظًّا مِمَّا ذُكِّرُوا بِهِ ۚ وَلَا تَزَالُ تَطَّلِعُ عَلَىٰ خَائِنَةٍ مِنْهُمْ إِلَّا قَلِيلًا مِنْهُمْ ۖ فَاعْفُ عَنْهُمْ وَاصْفَحْ ۚ إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ {13}

“Basi kwa sababu ya kuvunja kwao ahadi yao, tuliwalaani na tukazifanya nyoyo zao kuwa ngumu. Wanayabadilisha maneno toka mahala pake, na wameacha sehemu ya yale waliyokumbushwa. Na huachi kuvumbua khiyana kutokana nao, isipokuwa wachache miongoni mwao, basi wasamehe na waache, hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.” (Surat al-Maidah: 13).

3) Kitabu Tabdidudhilami Watanbihun-Niam Ila Khatar Shia Alal- Muslimiin Wal-Islam (Kuiondawa giza na kuwazindua waliolala juu ya hatari ya Shia dhidi ya waislam na uislamu), cha Ibnu Jabhan.

Sijapata kuona kitabu chenye uadui dhidi ya Ahlul-Bayt na Shia wao kama hiki. Amepania kuwakebehi na kuwasingizia bila ya utaratibu wa kimjadala au njia ya mazungumzo. Yote yaliyo humo ni kukufurisha na kuwafanya mafasiki na kukebehi rai za wengine.
Na atakaye kisoma kitabu hicho atanikuta msamehevu mno.

Imenithibitikia kuwa hakuna katika kitabu chake hiki zaidi ya kuchochea fitna kati ya Shia na Sunni na kuzisambaratisha safu za waislamu kwa njia nyingi tofauti. Ili wazidishe balaa na udhaifu juu ya udhaifu wao. Ilikuwa bora aelekeze kitabu chake kwa maadui wa kiislam, kijidola cha (Israeli).

Na kwa kuwa hakina hadhi ya kujadiliwa kwa sababu hakutaja dalili ili kiwe na stahiki ya hilo, bali ni mkusanyiko wa uwongo na masingizio dhidi ya Ahlul-Bayt na Shia wao. Kwa hiyo anakataa kila fadhila iliyokuja kwa ajili yao, na azikataa Aya zilizo za wazi na Hadithi zinazojulisha wajibu wa kushikamana na wao.
Hii hapa mifano miongoni mwa njia zake za jinsi ya kuzifanya dhaifu Hadithi zinazotaja kitu kuhusu fadhila za Ahlul-Bayt.

a) Baada ya kuleta jumla ya Hadithi anasema: ‘’Na tutazikanusha na kuwakanusha watu waliomaskhiwa (waliogeuzwa kuwa wanyama) aliojiambatanisha nao.”24

Hadithi ya kwanza:

“Mfano wa Ahlul-bayt wangu katika nyinyi ni mfano wa mlango wa msamaha (Hitwa) mwenye kuuingia atakuwa na amani.”

“Mfano wa Ahlul-Bayt wangu kwenu ni kama mfano wa Safina ya Nuhu mwenye kushikamana nayo ataokoka na mwenye kuwa khilafu nayo atazama.”

Anaidhoofisha Hadithi hii kwa dalili isio na uzito kabisa, hivyo anasema: “Hakika hadithi hii inawajibisha uokovu na amani kwa kushikamana na Ahlul-Bayt, na kuhiliki na kupotea kwa kukhalifiana nao, na hili haliruhusiwi kwa mujibu wa tamko la Qur’ani, kwa sababu Qur’ani katika uokovu haitoi sharti ila imani na matendo mema, na wala haihadharishi suala la kuhiliki ila kwa ukafiri na kutenda maasi. Na ndani ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu hamna hata Aya moja inayoitangua kauli yetu hii.25

Nasema: Lakini kuna uhusiano gani kati ya kauli yako na Hadithi hii! Kwa sababu kuthibitisha kitu hakumaanishi kukanusha kitu kingine. Hiyo ni hoja ya kwanza. Pili: Qur’ani yote inaitangua kauli yako hii. Qur’ani ni hii mbele yako inatuamuru kushikamana na manabii na mitume, na yamhukumu kuwa ni kafiri asiyeshikamana nao:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانْتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّهَ ۖ إِنَّ اللَّهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ {7}

“Na anachokupeni Mtume basi pokeeni, na anachokukatazeni basi jiepusheni, na mcheni Mwenyezi Mungu, kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.” (Surat al-Hashr: 7).

Kama ambavyo inatuamuru kushikamana na mawalii: “Enyi mlioamini! mtiini Allah na mtiini Mtume na wenye mamlaka miongoni mwenu.” (Surat Nisaa: 59) Amri katika Aya hii ni wazi kuwa ni amri ya wajibu hivyo basi ni lazima kushikamana nao, na Mwenyezi Mungu pia amewajibisha juu yetu kushikamana na waumini na kufuata njia yao. Mwenyezi Mungu amesema:

وَمَنْ يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِنْ بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا {115}

“Na anayempinga Mtume baada ya kumdhihirikia uongofu, Na akafuata njia isiyo ya waumini, tutamwelekeza alikoelekea na tutamwingiza Jahannam. Na ni marejeo mabaya.” (Surat Nisai: 115).

Hivyo kutoshikamana nao kunamaanisha maangamizi, na yasikitisha kuwa al-Jabhanu hakurejea kwenye kitabu cha Mwenyezi Mungu ili aone vipi ilikuwa kuingia kwenye mlango kwa wana wa Israil ni sababu ya kughofiriwa dhambi zao:

وَإِذْ قُلْنَا ادْخُلُوا هَٰذِهِ الْقَرْيَةَ فَكُلُوا مِنْهَا حَيْثُ شِئْتُمْ رَغَدًا وَادْخُلُوا الْبَابَ سُجَّدًا وَقُولُوا حِطَّةٌ نَغْفِرْ لَكُمْ خَطَايَاكُمْ ۚ وَسَنَزِيدُ الْمُحْسِنِينَ {58}

“Na ingieni katika mlango kwa unyenyekevu, na semeni: Tusamehe! Tutakusameheni makosa yenu, na tutawazidishia ujira wafanyao wema.” (Surat Al-Baqarah: 58)

Jabhanu sio kuwa hajui hayo isipokuwa tu ni uadui wake mkali dhidi ya Ahlul-Bayt umemfanya afanye hivyo. Na twamzidishia hasira kwa kauli yake (s.w.t.):

قَالَ رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا ۖ إِنْ كُنْتُمْ مُوقِنِينَ {24}

“Sema kwa haya siombi malipo yoyote kwenu isipokuwa mapenzi katika karaba.”
(Surat Shura: 23).

Mwenyezi Mungu amejaalia malipo ya risala yake ni kuwapenda Ahlul- Bayt.

Na anaidhaifisha akitegemea kauli yake: “Kwa nini tuwafuate Ahlu-Bayt, je wao wana elimu ambayo Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) hakuifikisha kwa waislamu wote, kwa kweli kuitakidi hivyo kwamaanisha kumtuhumu Nabii (s.a.w.w) kuwa ni mwenye upendeleo na mwenye kuificha risala…Na maadamu dini imekamilika ni kipi tunakihitajia kutoka kwa Ahlul-Bayt!”

Angalia dalili hii ya kipuuzi, ikiwa kufikisha hukumu za dini na kuzifafanua kwa baadhi ya watu mbali na wengine ni upendeleo ingekuwa lazima kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), naye ni Mtume wa kila mtu, aufikishe ujumbe yeye mwenyewe binafsi kwa kila mtu mmoja mmoja, au kwa uchache kwa wale walio katika zama zake. Na hili halisemwi na mwenye akili tu ya kawaida sembuse mwanachuoni, kama ambavyo jambo hili liko nje ya nyanja za tablighi.

Ahlul-Bayt wamebainika kwa sifa zinazowafanya wafae kuuongoza umma. Ni wazi kuwa watu upeo wao wa kufahamu unatofautiana na wa kukielewa kwao kitu katika ujumla wake, na pamoja na kutofautiana kwao katika daraja za imani, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alifikisha ujumbe kwa wote, lakini Ahlul-Bayt walikuwa mbele kati ya watu katika kuamini na ni wapambanaji hodari katika jihadi na wabora sana katika taq’wa na uchamungu. Kwa ajili hiyo Mwenyezi Mungu amewatoharisha kwa kuwaepusha na uchafu katika kitabu chake.

Basi ni kwa nini uwe na hikidi iliyojificha kama hii ewe mwana wa Jabhani?!

Ama kauli yako eti kukamilika kwa dini kunaondoa haja ya waislamu kuwafuata Ahlul-Bayt. Basi ni kwa nini tunawahitajia Swahaba na Salafu wema ili tuwafuate bila hoja?!26

Na kwa dalili kama hizi za kipuuzi ameikanusha Hadithi hii.

Hadithi ya pili:

“Hakika mimi ni mwenye kuwaachia kati yenu vizito viwili: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu.”

Anasema: “Imegeuzwa maana, na usahihi wake ni:

“Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu.”

Na kwa mfano hebu tuseme haikubadilishwa. Ni akina nani hawa kizazi walioonyeshwa katika hadithi hii?”27

Kwa urahisi kama huu ameipinga Hadithi ya “Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu.” Na tayari utafiti umeshapita kuihusu hadithi hiyo mwanzoni mwa kitabu.

Ni wazi kama walivyokiri wanavyuoni wa misingi ya sheria, kuwa: Kadhia haithibitishi maudhui yake, hivyo Hadithi hapa ipo katika kuthibitisha kadhia kwa ujumla wake, nako ni kuwa kushikamana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi Ahlul-Bayt ni wajibu. Ama kujua je Kitabu ni nini, na kizazi ni kitu gani, hilo halijulikani kwenye Hadithi hii, yahitajika dalili nyingine nje ya Hadithi hiyo ili iweke wazi makusudio ya kizazi. Kwa hiyo vipi anaitilia mashaka Hadithi kwa kauli yake: “Ahlul-Bayt ni akina nani?!”

Swali hili yalazimu lielekezwe kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kwa kuwa yeye anaona ulazima wa kusihi Hadithi hii.

Hadithi ya tatu:

“Ewe Ali hatokupenda ila muumini na wala hatokuchukia ila mnafiki.

Anasema: ‘’Hadithi hii imewekwa haina msingi ulio sahihi, kwa sababu kumpenda asiye Mwenyezi Mungu na Mtume wake hakufai kuwe kipimo cha imani wala kigezo cha itikadi, kwa sababu mapenzi ya watu wema yanafuatia bila shaka kule kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala hayajitengi.’’

Tunasema: Kwanza: Kwa nini amemuengua Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), ikiwa kipimo ni kufuatia basi kumpenda Mtume wake na waja wake wema kunatokana na kumpenda Mwenyezi Mungu.

Pili: Ikiwa kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake kunapelekea kuwapenda watu wema, basi pia kuwapenda watu wema kunapelekea kumpenda Mtume wake na kumpenda Mwenyezi Mungu. Na hilo lathibitisha usahihi wa Hadithi, kwa sababu Hadithi iko katika kubainisha jinsi ya kumtambua mnafiki, na kuwa ambaye adhihirisha kumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawezi kutangaza kutompenda kwake Mwenyezi Mungu na Mtume wake, vinginevyo angeitwa mnafiki, lakini anaweza kutangaza chuki yake kwa mtu mwingine yoyote, na kwa kuwa Imam Ali (a.s.) ni miongoni mwa watu wema bali ni miongoni mwa vielelezo vya kweli kabisa, hivyo mwenye kumchukia kwa mujibu wa kanuni ya kufuatia anamchukia Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kwa hiyo Hadithi hii inatufanyia kipimo yakinifu cha kuwatambua wanafiki.

Tatu: Ikiwa anwani yako ni kuwa: Kupenda na kuchukia si vipimo vya imani wala si vigezo vya itikadi, basi ni kwa nini mnasema Shia kafiri, kwa sababu ya kuwachukia kwao baadhi ya Swahaba, kulingana na dhana yako!

Na kwa nini wewe unawapenda Swahaba na unawapenda Salafu Swalih pamoja na Bani Umayyah na Bani Abbas na unakuwa jasiri katika kuwahami?! Je hutarajii kwa hilo thawabu?! Ikiwa jibu ni hapana basi maneno yako yote ni upuuzi na ni ya kupoteza wakati.

Hadithi ya nne:

‘’Mimi ni Jiji la elimu na Ali ni lango lake.

Anasema: ‘’Kwa kuwa tamko la Hadithi linaonyesha uhafifu wake, na uhafifu wa aliyelinasibisha kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), kwa sababu ya kutokuwepo uwiano kati ya neno Jiji na neno elimu. Wala hakuna ulingano wowote katika kufahamika kwa maneno mawili hayo wala ulingano wa tamko lao. Lau angesema: ‘Mimi ni bahari ya elimu na Ali ni ukingo wake.’ ingelingana’’
Pia anatoa dalili: “Kwa nini Mtume wa Mwenyezi Mungu aiweke elimu ndani ya Jiji na aweke ufunguo wake kwa Ali, na asiliweke wazi bila milango ili watu wote waweze kuingia watakavyo….”

Hicho ndio kiwango cha elimu yake na upeo wa dalili yake, yaani kukataa. Na kwa taarifa tu ajue kuwa Hadithi haikuwa mahususi kuitambulisha elimu ili aseme: Bahari. Ila tu alitaka kubainisha mafungamano kati yake na Ali (a.s.). Kwa hiyo Hadithi inaangalia uhusiano kwa ujumla wake kati ya wawili hawa, kwa hiyo mfano wa Jiji ulikuwa wazi mno kwa kutoweza kuliingia ila kwa njia ya lango.

Ama kuhusu kauli yake: “Na asiliweke wazi bila milango,” itamtosha kauli yake (s.w.t): ‘’Waulizeni wenye ukumbusho ikiwa nyinyi hamjui.’ (Surat an-Nahl: 43).

Hii ndio njia yake ambayo yajulisha kuwa yeye ni mwenye chuki na Ahlul-Bayt, na chuki yake dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu na dhuria yake iliyo tohara ni kali mno. Hivyo basi fikra kama hii ya juu juu na dalili za kuchekesha haziwezi wathibitishia sifa njema Ahlul-Bayt. Kinyume chake anasahihisha kila riwaya dhaifu na Hadithi zisizokubalika kimatamshi na kisanad kwa kuwa hizo zinathibitisha fadhila za mwingine yeyote yule miongoni mwa Salafu.

Enyi wanavyuoni wa Ahlu Sunna! je mnamkubali huyu kuwa ndio mwanachuo miongoni mwa wanachuoni wenu, ana wahami na anawakilisha rai yenu?! Ikiwa ndio, basi As-Salaam kwa Ahlu Sunna. Na endapo itakuwa hapana, basi ni kwa nini hamumpingi na kumsimamisha nafasi yake. Kitabu hiki ambacho kipo mkononi mwangu ni chapa ya tatu, na inawezekana kimepigwa chapa mara nyingi, msimamisheni basi! Yasikitisha sana kuwa juu yake kimeandikwa: “Kimepigwa chapa kitabu hiki kwa idhini ya uongozi wa idara ya tafiti za kielimu, fatwa, daawa na mwongozo.”

Subhanallah! jina linapingana kabisa na kitabu hiki. Hivi ni tafiti gani za kielimu nazo hazikutafiti nafsi ya kitabu hiki. Vinginevyo idara hii itanasibishiwa alilonasibishiwa mtungaji wake miongoni mwa ujahili na upumbavu wa kiakili na uchache wa ufahamu, kupotosha na kubadilsha ukweli! Kwa kuwa kukiri jambo ni kulisadikisha. Daawa gani hii, na mwongozo gani huu?! Ila ni daawa ya kwenye mfarakano na kutofautiana, na mwongozo wa kwenye mtanguano huu unaoaibisha. Mpaka lini Uwahabi utaishi katika mpingano kama huu?!

Dk. Turabi alipoidhaifisha Hadithi ya nzi kwa dalili za kimantiki na thibitisho za kielimu, walimchomolea panga zao na walitoa fatwa kuwa yeye ni kafiri, lakini nashangaa Jabhani anapozidhoofisha Hadithi nyingi zilizo sahihi na zilizo mutawatiru kwenu, alizozieleza Bukhari na Muslim, haimtikisi aliye kimya..!

Je kwenu nzi ana heshima mno kuliko hata Ahlul- Bayt wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w)!? Ni kweli ewe Ali, hakupendi ila muumini wala hakuchukii ila mnafiki.

b) Mifano ya uzushi wake dhidi ya Shia:

i) Amesema katika Uk. 494: “Na zaidi ya hayo ni kuwa adhana yao inatofautiana na adhana yetu na swala yao inatofautiana na swala yetu, na swaumu yao inatofautiana na swaumu yetu, na wao hawaitambui Zaka wala wanaostahiki.”

ii) Anasema katika Uk. 495: ‘’Kuwa wao hawatoadhibiwa kwa kutenda dhambi kubwa wala ndogo, na wasiokuwa wao watabakia motoni milele. Halafu kuhalalisha kwao kuacha wazi tupu za wanawake, na kuondoa kwao swala ya Ijumaa na ya Jamaa, na hadi za kisheria, kwa hoja ya kuwa Imam yuko ghaibu. Na kuuita kwao umma wa Muhammad kuwa ni umma uliolaaniwa, na itikadi yao kuwa kuwalaani Swahaba na kuwalaani wake wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kuwa ni miongoni mwa matendo matukufu mno ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.”

iii) Na anataja katika Uk. 222: “Huenda asisadiki msomaji mtukufu kuwa kumuoa mama kwao ni miongoni mwa wema kwa wazazi wawili, na kwao wao ni miongoni mwa matukufu mno ya kujikurubisha.”

iv) Na katika Uk: “Shia anakunyooshea mkono wake ili kukupa mkono, ili akushughulishe mbali na mkono mwingine ulionyooka mpaka mfukoni mwako.”

v) Na katika Uk. 28: “Kila azaliwaye katika siku za Ashura yeye ni Sayyid, na kila ambaye mama yake aliibeba mimba yake siku za Ashura yeye ni Sayyid japo iwe mimba isiyo ya kisheria.”

Hakuishia hapo, ulimi wake umerefuka mpaka kwa Imam Jafar Swadiq (a.s.) mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), ambaye kundi la waislamu, linaitakidi kuwa yeye ni Imam ma’sum. Na kundi lingine linaitakidi kuwa yeye ni miongoni mwa wanachuoni waliobobea katika elimu, na maimamu wa madhehebu manne wamekiri ubora wake.

Historia haijatwambia kuwa kuna yeyote aliyemtia dosari, japo awe miongoni mwa maadui zake wakali, mpaka alipokuja mwana wa Jabhani aliyesema kumhusu: “Kwa kweli kauli ya Ja’far: ‘Mwenye kuitaka dunia hakupi nasaha na mwenye kuitaka akhera hafuatani na wewe’ ni kauli ya aliyebobea katika mbinu za vitimbi na ni mdanganyifu mzuri. Lakini ikiwa kauli: ‘Hakika watu hufuata dini ya wafalme wao’ ni sahihi, basi kuwa sahihi kauli ya kuwa wao wanafuata dini ya maimamu wao ni awla, na kwa kuwa ninyi ni nakala inayolingana na asili (Jafar) ambaye mnakiri kuwa ni muasisi mkuu wa itikadi zenu zote.”28

Hebu tazama kwa kiwango gani amefikia katika chuki na uadui dhidi ya Ahlul-Bayt wa risala!

vi) Aliyeubuni mwendo huu sio Jabhan, bali ametanguliwa na Ustadhi wake muasisi wa Uwahabi Muhammad bin Abdul-Wahabi. Imekuja katika risala Fii Radi Alar-Rafidhah Uk. 34. “Kuhalalisha kwao ndoa ya muta, na wanaijaalia kuwa ni bora kuliko ndoa sabini za daima. Na Sheikh wao al-Ghaliy Ali bin al-Aaliy amewaruhusu wamfanyie ndoa ya muta watu kumi na mbili mwanamke mmoja katika usiku mmoja, na akipatikana kutokana na watu hawa mtoto watapiga kura kati yao na mwenye kushinda kura, mtoto atakuwa wake.”

vii) Na katika Uk. 44 ameandika: “Na miongoni mwayo ni kuwa mayahudi waligeuzwa ngedere (nyani) na nguruwe. Na imenakiliwa kuwa hilo limewatokea baadhi ya Rafidha – yaani Shia – katika mji wa Madina na miji mingine, bali yasemekana kuwa wao hugeuzwa sura zao na nyuso zao wakati wa kufa. Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi mno.”

Hii ndio njia yao kuwajibu Shia, haiko mbali na ngano za ‘Elfu leyla wa leyla,’ na ndoto za Qamar Zaman na Shahru Zad.

4) Ama kuhusu masingizio ya Ahmad Amiin yaliyo katika kitabu Dhuhal- Islam, yenyewe tutayafumbia macho. Hasa baada ya kutufikia uombaji radhi wake kuhusu aliyoyaandika kuwahusun Shia. Na hilo analitaja Imam Sheikh Muhammad Huseiyn Aal Kashiful-Ghita’a katika kitabu chake Aslus-Shia Wausuluha, Uk. 72: “Na miongoni mwa matukio yasiyotazamiwa ni kwamba Ahmad Amin katika mwaka uliopita 1349 H.A. baada ya kitabu chake kuenea na kusimama wengi miongoni mwa wanavyuoni wa Najaf dhidi yake alifanya ziara ya mji wa kielimu Najaf, na alipata hadhi ya kutabaruku na vizingiti vya mji ule, katika msafara wa kimisri uliokuwa na watu karibu 30 katika walimu na wanafunzi, alituzuru na kundi lake. Walikaa kiasi fulani sehemu ya usiku miongoni mwa mikesha ya Ramadhan, kwenye maskani yetu katika mahfali ya watu wengi. Tulimlaumu kwa makosa yale lawama nyepesi. Na tulimsamehe msamaha. Na tulipenda tuende naye kiheshma, na tumwambie amani.

“Udhuru wa mwisho aliokuwa nao ni kutokuwa na habari ya kutosha na uhaba wa vitabu vya rejea. Tulimwambia: Hilo pia sio sawa, kwa kuwa anayetaka kuandika kuhusu maudhui fulani kwanza kabisa yamlazimu akusanye vifaa vya kutosha na afuatilie ufuatiliaji wa kikamilifu, vinginevyo haitokuwa jaizi aingiye na kujihusisha nayo. Vipi imekuwa maktaba za Shia ikiwemo maktaba yetu ina jalada zinazokaribia 5000 nyingi katika hizo ni vitabu vya wanavyuoni wa kisunni vikiwa katika mji kama Najaf ulio fakiri wa kila kitu isipokuwa elimu na wema inshaallah.
Hali ikiwa maktaba za Cairo ni zenye adhama na hadhi, iweje ziwe hazina vitabu vya Shia ila kitu kidogo kisichoweza kutajika. Naam, jamaa hawajui chochote kuhusu Shia nao wanaandika kila kitu kuuhusu Ushia!”

 • 1. As-Shafi Uk. 19. Katika maneno ya Muhakiki.
 • 2. Dalailus-Swidqi Juz. 1, Uk. 3.
 • 3. Ni miongoni mwa maneno ya mhakiki.
 • 4. Mkoa mmojawapo Kaskazini mwa Jamhuri ya Syria.
 • 5. Murajaatu, Uk. 59.
 • 6. Murajaatu, Uk. 424.
 • 7. Aqidatul-Masiihi ad-Dajaal, Uk. 9.
 • 8. Mimi nimefasiri ibara hii kulingana na maelezo ya mwandishi wa kitabu hiki, waila mimi binafsi sijui uwahabi wake - Mtarjumi.
 • 9. Dalailus-Swidiq Juz. 1, kwenye utangulizi.
 • 10. Juz.1. Uk.301.
 • 11. Juz.1. Uk.307
  3 Ikumbukwe kwamba jina hili la Ahlu Sunnah wamelipewa na Muawiyah kwenye mwaka wa 42AH. ulioitwa - Mwaka wa Jamaa - Mtarjuma
 • 12. Al-Ihtijaju, Uk. 321.
 • 13. Juz. 2, Uk. 551.
 • 14. Juz. 2, Uk. 551.
 • 15. Juz. 2, Uk. 551.
 • 16. as-Shafiy Fii Sharhil-Kafiy Juz. 2, Uk. 62.
 • 17. Shia Wal-Qur’ani. Uk.7.
 • 18. Nahjul-Balagha Sharhu ya Muhammad Abduh, Uk. 22.
 • 19. Shia Wa Ahlul-bayt. Uk. 41- 42.
 • 20. Shia Wa Ahlul-bayt. Uk. 41- 42.
 • 21. Uyunu Akhbari Ridha. Uk. 85
 • 22. Nahjul-Balaghah Uk. 136. Hotuba ya 92.
 • 23. Al-Ihtijaj cha Tabrasiy. Uk.87.
 • 24. Tabdiidu dhwalam Uk. 90.
 • 25. Tabdiidu dhwalam Uk. 91.
 • 26. Hapa ni kufuata bila hoja, kama ambavyo ndugu zetu Ahlu Sunna huwafuata maswahaba bila hoja ilimradi tu yeye ni Swahaba!
 • 27. Tabdiidu dhwalam Uk. 40.
 • 28. Uk. 206.