Sura Ya 41: Safari Ya Kidini Na Kisiasa

Mwaka wa sita ulikuwa ukimalizikia na matukio yake yote machungu na matamu pale kwa ghafla Mtume (s.a.w.w.) alipoiota ndoto yenye kupendeza kwamba Waislamu walikuwa wakizifanya ibada za Hajj kwenye Masjidu’l-Haram. Aliwasimulia masahaba zake ndoto hii nao wakaichukulia kuwa ni ndege njema kwa Waislamu kwa kuwa karibuni tu watalifikia lengo lao lililokuwa likiwatia kiherehere mno nyoyoni mwao.1

Mtume (s.a.w.w.) aliwaamrisha Waislamu wajitayarishe kuifanya safari ile ya kwenda Hijja na pia aliyaalika makabila ya jirani waliokuwa bado ni washirikina kufuatana na Waislamu kwenye safari ile. Vile vile alitangaza katika sehemu zote za bara Arabu kwamba Waislamu watakwenda Makka katika mwezi wa Dhil Qa’ad.

Safari hii ya kiroho, ukiachilia mbali kule kuwa kwake na faida za kiroho, vile vile ilikuwa na kiwango fulani ya faida za kijamii na kisiasa. Ilikifanya kuwa bora zaidi cheo cha Waislamu kwenye Rasi ya Uarabuni nayo ikawa njia ya kuuenezea Uislamu miongoni mwa Waarabu kutokana na mambo yafuatayo:

1. Makabila ya Waarabu waliyokuwa washirikina yalikuwa yakidhania kwamba Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akizikana itikadi na ibada zao zote zile za kitaifa na zile za kidini ikiwa ni pamoja na Hijja na ‘Umrah, ibada zilizokuwa kumbukumbu ya jadi zao, na kwa sababu hii walimwogopa Mtume (s.a.w.w.) na dini yake. Kushiriki kwa Mtume (s.a.w.w.) na masahaba zake kwenye ibada ya Hija na ‘Umrah kwenye safari hii kungeweza kuipunguza ile hofu na wasiwasi akilini mwa baadhi ya makabila ya Waarabu washirikina, na kuwadhihirishia kivitendo kuwa, sio tu kwamba Mtume (s.a.w.w.) hakuipinga Hija ya Nyumba ya Allah na ibada ya Hija, jambo lililo moja ya ibada zao za kidini na kumbukumbu zao za kitaifa, bali anaifikiria kuwa ni tendo lililo wajibu.

Aidha, vile vile alikuwa akijitahidi kama alivyofanya jadi wake Nabii Isma’il (a.s.) katika kuzihuisha na kuzihifadhi ibada hizi. Kwa njia hiii, aliweza kuyavutia kwake yale makabila yaliyoufikiria Uislamu kuwa ni wenye kuzipinga kabisa kumbukumbu zao za kitaifa na kidini na aliweza kuipunguza hofu yao.
2. Kama Waislamu wakifaulu kuitekeleza Hija na kuweza kuyatekeleza majukumu yao ya kidini kwa uhuru kabisa kwenye Masjidu’l-Haram, mbele ya macho ya Waarabu washirikina, kitendo hiki kitakuwa ni chanzo kikuu cha kuuhubiri Uislamu, kwa sababu kwenye majira ya Hajj washirikina na Waarabu kutoka kwenye sehemu zote za Penisula ile watakusanyika mjini Makka na wakati wa kurejea makwao, watazichukua taarifa juu ya Waislamu. Kwa njia hii, ujumbe wa Uislamu utazifikia sehemu zote hizo ambazo Mtume (s.a.w.w.) hakuweza kuzipelekea wahubiri na utakuwa na athahri zake pale.

3. Mtume (s.a.w.w.) aliwakumbusha watu wa Madina juu ya ule mwezi mtakatifu na akasema: “Tunakwenda kwenye Hija ya Nyumba ya Allah.” Vile vile aliwaamrisha Waislamu kutochukua silaha yoyote ile ila upanga ambao kwa kawaida msafiri aliuchukua anaposafiri. Matendo yake haya yaliwafanya watu wengi wasiokuwa Waislamu wauelekee Uislamu, kwa sababu, kinyume na propaganda walizokuwa wakizifanya Waquraishi dhidi ya Uislamu, waliona kwamba kama walivyo watu wengine, Mtume (s.a.w.w.) naye aliyachukulia mapigano kwenye miezi hii kuwa ni haramu na ilikuwa katika kuipendelea kama miezi mitakatifu ya amani.

Mtume (s.a.w.w.) alifikiria kwamba, kama Waislamu wakifaulu katika wakati ule watakuwa wameifikia moja ya shauku zao kubwa (yaani kuzitekeleza ibada za ‘Umrah na Hija), na wale waliokuwa mbali kutoka maskani mwao wataweza kukutana na ndugu na marafiki zao. Na kama wakikumbwa na kizuizi, Waquraishi watakipoteza cheo chao kwenye ulimwengu wa Kiarabu, kwani wawakilishi wa makabila yasiyounga mkono upande wowote (ule wa Waislamu wala ule wa Waquraishi) wataona jinsi Waquraishi watakavyowatendea Waislamu.

Watashuhudia Waisilamu walitaka kufanya ‘Umrah na Hija ilihali hawakuwa wamechukua silaha zozote zile ila ile silaha ya msafiri, na ingawa Masjidu’l-Haram na ibadi za Hija ni kwa Waarabu wote, na Waquraishi ni wadhamini tu wa Haram ile, lakini waliwazuia. Hivyo basi, hapo unyoofu wa Waislamu na uonevu wa Waquraishi vitadhihirika, na Waquraishi hawataweza kujiunga na makabila mengine dhidi ya Uislamu na kuunda ushirika, kwa sababu watakuwa wamewazuia Waislamu mbele ya maelfu ya mahujaji kuzifaidi haki zao za halali.

Mtume (s.a.w.w.) alizifikiria faida na hasara za jambo hili na akawaamrisha watu waanze safari. Akavaa Ihr?m mahali paitwapo Dhul- Hulayfah pamoja na watu 14002 au 16003 au 18004 na ngamia sabini waliotiwa alama maalumu kwa ajili ya kuchinja, na kwa nia hiyo wakalidhihirisha lengo la safari ile.

Watu wa idara ya usalama wa Mtume (s.a.w.w.) walitangulia mbele ili kwamba kama wakipambana na adui humo njiani, waweze kumuarifu Mtume (s.a.w.w.). Kwenye sehemu fulani karibu na Asf?n mtu mmoja wa kabila la Khuzaa’i, aliyekuwa mmoja wa wale watu wa usalama wa Mtume (s.a.w.w.) alimjia Mtume na kumuarifu hivi: “Waquraishi wameitambua safari yako. Wameyakusanya majeshi yao na wameapa kwa majina ya Laat’ na Uzza’ kwamba watazuia kufika kwako mjini Makka.

Wazee na watu maarufu wa Waquraishi wamekusanyika mahali paitwapo Zi Tuwaa (mahali fulani kariubu na Makka) ili kuzuia maendeleo ya safari ya Waislamu, wamempeleka kamanda wao shujaa Khalid bin Walid mahali paitwapo Kiraa’ul Ghamim jangwa lililoko kiasi cha kilomita kumi na tatu hivi kutoka Asfaan pamoja na askari wanaopanda farasi mia mbili nao wamepiga kambi hapo5 ili kuwazuia Waislamu wasiingie Makka, au sivyo watayatoa maisha yao katika kulifikia lengo hili.”

Baada ya kuisikia taarifa ile Mtume (s.a.w.w.) alisema: “Ole wao Quraishi. Vita vimewamaliza! Ningelipendelea kwamba wangaliniacha nishughulike na makabila mengine yenye kuyaabudu masanamu.
Ikiwa wao (yaani yale makabila mengine) yakishinda dhidi yangu, Waquraishi wangelikuwa wamelifikia lengo lao, na kama nikipata ushindi dhidi ya makabila hayo, wao (Waquraishi) wangelipigana nami kwa majeshi yao waliyoyaweka akiba. Ninaapa kwa jina la Allah! Nitaziendeleza juhudi zangu kwa ajili ya kuihubiri itikadi ya Upweke wa Allah hadi Allah aifanye dini ishinde au niutoe uhai wangu kwa ajili ya kulifikia lengo hili.”

Kisha aliomba muongoza njia wa kuwaongoza (yaani Mtume na masahaba zake) katika njia ambayo haitawapambanisha na Khalid. Mtu mmoja wa kabila liitwalo Aslam alilichukua jukumu la kuuongoza msafara ule na akaupitisha kwenye njia ya mabonde yenye mashimo shimo na kuwafanya watue mahali paitwapo Hudaybiyah. Ngamia wa Mtume (s.a.w.w.) alipiga magoti mahali pale naye Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Huyu mnyama ametua mahali hapa kwa amri ya Allah ili kwamba jukumu letu lidhihirike.” Kisha akawaamrisha wote washuke na kukita mahema yao.

Wapanda farasi wa Waquraishi walilijua lengo la Mtume (s.a.w.w.) na wakajisogeza karibu na Waislamu. Kama Mtume angalipenda kuendelea na safari yake basi ingelimlazimu kuzitawanya safu za wapanda farasi wa Waquraishi na kuimwaga damu yao. Lakini wote walikuwa wanafikiria kwamba hakuwa na lengo lolote jingine ila kufanya Hija ya Ka’abah Tukufu.

Mahali hapa ugomvi na kumwaga damu kungeleta pigo kwenye ile nafasi na madai ya makusudio ya amani ya Mtume (s.a.w.w.). Zaidi ya hapo, hata kule kuwaua hawa wapanda farasi kusingelikiondoa kizuizi kile kwenye njia yake kwa sababu daima vikosi vingine vilikuwa vikiletwa na Waquraishi na suala hili halikuwa likiufikia mwishilizo wake. Mbali na hili, Waislamu hawakuwa na silaha zozote zile zaidi ya zile silaha za wasafiri na halikuwa jambo lifaalo kujitia kwenye mapigano kwenye hali ile. Kinyume na hivyo ilifaa kulitatua suala hili kwa njia ya mazungumzo.

Kutokana na sababu hizi, Mtume (s.a.w) aliwageukia masahaba wake baada ya kushuka kwenye mnyama wake na akasema: “Kama leo hii Waquraishi wanataka kitu chenye kuimarisha mafungamano ya udugu nitawapa na nitaishika njia ya upatanisho.”6

Maneno ya Mtume (s.a.w.w.) yaliyafikia masikio ya watu na maadui nao waliyatambua. Hivyo Waquraishi waliwatuma watu kwa Mtume (s.a.w.w.) kwenda kupata taarifa sahihi.

Wawakilishi Wa Quraishi Waja Na Kukutana Na Mtukufu Mtume (S.A.W.W)

Waquraishi waliwatuma wawakilishi wengi kwa Mtume (s.a.w.w.) ili kupata taarifa juu ya lengo la kuchukua kwake safari ile. Budayl Khuzaa’i na baadhi ya watu wa kabila la Khuza’ah walionana na Mtume (s.a.w.w.) wakiwa ni wawakilishi wa Waqureishi. Mtume (s.a.w.w.) aliwaambia: “Sikuja kupigana. Nimekuja kufanya Hija ya Ka’abah.” Wale wawakilishi walirejea na kuwaarifu Waquraishi kuhusu ile hali. Hata hivyo wale Waquraishi wasiosadiki hawakuyakubali maneno yao na wakasema: “Tunaapa kwa jina la Mungu! Japo awe kaja kwa ajili ya Hija ya Ka’abah hatutamruhusu aingie Makka.”

Kisha Mikraz akiwa yu mwakilishi wa Waquraishi alikutana na Mtume (s.a.w.w.). Vile vile naye alirudi na kuyathibitisha yale aliyoyasema Budayl, lakini Waquraishi hawakuziamini taarifa alizozitoa.

Ili kuumaliza mgongano huu walimtuma Hulyas bin ‘Alqamah kwa Mtume (s.a.w.w.) aliyekuwa mpiga mishale mkuu wa Uarabuni.7 Alikuwa bado yu mbali kidogo pale Mtume (s.a.w.w.) alipomwona na kusema: “Mtu huyu anatokana na kabila safi na lenye uchamungu. Watoeni kafara wale ngamia mbele yake ili atambue kwamba hatukuja kupigana, na kwamba hatuna lengo lolote jingine ila kufanya Hija ya Ka’abah”.
Hulays aliwaona wale ngamia sabini waliokuwa na njaa kali kiasi kwamba walikuwa wakila sufi zao wenyewe kwa wenyewe. Alirudi kutoka mahali pale hata bila ya kuonana na Mtume (s.a.w.w.). Aliwahutubia Waquraishi kwa nguvu na kusema: “Sisi hatukufanya mapatano hata kidogo nanyi ili muwazuie mahujaji wa Ka’abah kufanya Hija. Muhammad hana lolote ila kufanya Hija.

Naapa kwa jina la Yule Mwenye nguvu zote, Aliyeutawala uhai wangu! Kama mkimzuia Muhammad asiingie (Makka), mimi pamoja na watu wote wa kabila langu ambao wengi wao ni wapiga mishale tutakutoeni na kukukateni kateni vipande vipande!”

Maneno haya ya Hulays hayakupendwa na Waquraishi. Hata hivyo, wakichelea upinzani wake walishauriana juu ya jambo hili na kumwambia: “Tulia kwa uhakika. Sisi wenyewe tutalitafutia jambo hili ufumbuzi utakaoukubali wewe.”

Hata hivyo, kwenye hatua ya nne walimtuma ‘Urwah bin Mas’ud Saqafi ambaye kwa busara, akili na uaminifu wake walimwamini. Mwanzoni alikataa kuwawakilisha Waquraishi kwa kuwa aliona vema jinsi walivyowachukulia wawakilishi wao wa awali, lakini walimthibitishia kwamba cheo chake kwao kilithaminiwa, nao hawatamlaumu kwa kuvunja uaminifu.

Urwah bin Mas’ud alimjia Mtume (s.a.w.w.) na kusema: “Ewe Muhammad! Umejikusanyia makundi mbalimbali na sasa umeamua kuishambulia sehemu uliyozaliwa (Makka). Hata hivyo, Waquraishi watakuzuia kwa nguvu zao zote nao hawatakuruhusu kuingia mji wa Makka. Hata hivyo, mimi nachelea kwamba kesho makundi haya yatakuacha pasipo msaada wowote.”

Alipomaliza kuyasema hayo, Abu Bakr aliyekuwa kasimama nyuma ya Mtume (s.a.w.w.) alimgeukia ‘Urwah na kumwambia: “Umekosea. Marafiki zake Mtume (s.a.w.w.) hawatamwacha, kwa hali yoyote ile.”

‘Urwah aliutumia ujuzi wote wa diplomasia kwenye kauli yake na akajaribu kuithibitisha nguvu ya Waquraishi na kuudhoofisha moyo wa Mtume (s.a.w.w.); na kwa lengo la kukishusha cheo cha Mtume (s.a.w.w.) alizigusa ndevu zake alipokuwa akizungumza. Mughayrah bin Shu’bah kwa kurudia rudia alipiga mkono wake na kusema: “Kuwa mwenye heshima na usiwe mtovu wa adabu kwa Mtume (s.a.w.w.).” Urwah alimwuliza Mtume (s.a.w.w.): “Ni nani huyu?”8 Mtume akasema: “Huyu ni mwana wa nduguyo, Mughayrah bin Shu’bah.” Urwah alichukizwa na akasema: “Ewe mtu mwenye hila! Jana niliinunua heshima yako.

Uliwauwa watu kumi na watatu wa kabila la Saqaf muda mfupi tu kabla ya kusilimu kwako, nami nililipa fidia ya damu kutoka mfukoni mwangu ili kuizuia miali ya vita kuwaka miongoni mwa koo za Saqaf.”

Mtume (s.a.w.w.) aliyakatisha yale mazungumzo ya ‘Urwah na akamweleza lengo la safari yake kama alivyokwisha kuwaeleza wale wawakilishi wa Waquraishi, wale wa awali. Hata hivyo, ili kutoa jibu lenye pigo kwa vile vitisho alivyovitoa ‘Urwah, Mtume alisimama na akafanya wudhu (akatawadha), Urwah akaona kwa macho yake kwamba masahaba zake Mtume hawakuruhusu japo tone la yale maji ya udhu wake kuangukia ardhini.

‘Urwah aliamka na akaufikia ule mkusanyiko wa Waquraishi. Aliwataarifu machifu wa Waquraishi waliokusanyika mahali paitwapo Zi Tuwaa juu ya mkutano wake na Mtume (s.a.w.w.) na lengo la Mtume (s.a.w.w.). Vile vile aliongeza: “Nimewaona wafalme wakuu.

Nimeziona nguvu kuu kama vile nguvu za Mtawala wa Iran, Kaisari wa Dola ya Kirumi na Mfalme wa Ethiopia, lakini sijapata kuona cheo cha yeyote yule kati yao miongoni mwa mataifa yao kilicho kikuu kama kile alichonacho Muhammad miongoni mwa wafuasi wake.

Nimeona kwa macho yangu kwamba hawakuliruhusu japo tone moja la maji aliyotawadhia kuanguka ardhini, nao waliligawana miongoni mwao likiwa ni tabaruk (yaani zawadi takatifu iletayo mibaraka). Kama unywele wake mmoja ukianguka huuokota mara moja. Hivyo basi, machifu wa Waquraishi hawana budi kuifikiria hii hali ya hatari.”9

Mtume Wa Uislam (S.A.W.W) Amtuma Mwakilishi Wake

Mazungumzo ambayo wawakilishi wa Waquraishi waliyafanya na yule kiongozi mkuu wa Uislamu hayakutoa matokeo mema yeyote. Mtume (s.a.w.w.) aliweza kufikiria vyema kwamba wale wawakilishi wa Waquraishi hawakuweza kuufikisha ukweli kwa wazee wa Waquraishi au hawakufanya hivyo waziwazi kwa kuchelea kukemewa. Hivyo aliamua kumpeleka mwakilishi wake atakayewaeleza Waquraishi lengo lake hasa la kuifanya safari ile, ambalo halikuwa lolote jingine ila Hija ya Ka’abah.

Khirash mtu hodari wa kabila la Khuzaa’ah, aliteuliwa kwa kazi hii na Mtume (s.a.w.w.) alimtoa ngamia kwa ajili yake. Khir?sh alikutana na kundi la Waquraishi na akaifanya ile kazi aliyopewa. Hata hivyo, kinyume na ilivyotegemewa, na pia kinyume na desturi ya mataifa ya ulimwengu kwamba balozi yu huru kabisa kutokana na madhara, wao (Waquraishi) waliikata miguu ya ngamia wake na walikuwa karibu wamuuwe, lakini uhai wake uliokolewa kwa njia ya wale wapiga mishale wa Uarabuni. Kitendo hiki kiovu kilithibitisha kwamba Waquraishi hawakuwa na nia ya kulimaliza jambo hili kwa njia ya amani na kwamba walikuwa wakielekea kwenye mapigano.

Mara baada ya tukio hili watu hamsini wenye uzoefu kutoka miongoni mwa Waquraishi walitumwa kwenda kandokando ya sehemu ambayo Waislamu wamepiga kambi na ikiwezekanza wazinyakue mali zao na kuwateka baadhi yao. Hata hivyo, mpango wao huu ulishindwa na kinyume chake watu wale walitekwa na kuletwa mbele ya Mtume (s.a.w.w.). Ingawa waliwatupia Waislamu mishale na kuwavurumisha mawe, lakini Mtume (s.a.w.w.) aliwaelekeza Waislamu kuwaachia huru wote. Hivyo, kwa mara nyingine tena aliuthibitisha ukweli wake na akadhihirisha ya kwamba hakuwa na nia ya kupigana.10

Mtume (S.A.W.W) Ampeleka Mwakilishi Mwingine

Ingawa yalikuwako yote hayo, lakini Mtume (s.a.w.w.) hakukata tamaa ya amani, naye kwa uaminifu kabisa alitaka kulitatua tatizo lile kwa njia ya mazungumzo na kwa kuzibadili fikira za Waquraishi. Safari hii alitaka kumpeleka mwakilishi ambaye hajaimwaga damu ya Waquraishi. Hivyo Ali, Zubayr na wapiganaji wengine wa Uislamu waliowahi kupambana na wapingaji wa Waquraishi na Waarabu na kuwauwa baadhi yao, hawakufaa kuwa wawakilishi. Mwishowe aliamua kumtuma Umar bin Khatab kwa lengo hili, kwa kuwa hadi katika siku ile alikuwa bado hajamwaga japo tone moja la damu ya waabudu masanamu. Hata hivyo, Umar alitoa udhuru wa kutoweza kulibeba jukumu lile na akasema: “Mimi nina waogopa11

Waquraishi kwa kuwa nayachelea maisha yangu, na mjini Makka hakuna mtu yeyote wa familia yangu awezaye kunisaidia. Hata hivyo, mimi nampendekeza Uthman bin Aff?n mwenye uhusiano wa karibu zaidi na Abu Sufyani naye anaweza kuufikisha ujumbe wako kwa machifu wa Waquraishi.”

Hivyo, Uthman akapewa jukumu lile na akaondoka kwenda Makka. Alipokuwa njiani alikutana na Ab?n bin Sa’id bin Aas na akaingia mjini Makka chini ya ulinzi wake.

Ab?n alimwahidi kwamba hakuna yeyote atakayemwingilia mpaka pale atakapoufikisha ule ujumbe wa Mtume (s.a.w.w.) waziwazi. Hata hivyo, Waquraishi waliujibu ujumbe ule wa Mtume (s.a.w.w.) kwamba wao wameamua kwa kiapo kwamba hawatamruhusu Muhammad kuuingia mji wa Makka kwa nguvu, na kwa sababu ya kiapo hiki mazungumzo yoyote yahusuyo kuingia kwa Waislamu mjini Makka hayana mjadala tena. Walimruhusu Uthman kufanya Tawaaf ya Ka’abah, lakini yeye alikataa kufanya hivyo ikiwa ni ishara ya heshima kwa Mtume (s.a.w.w.). Walichokifanya Waquraishi kuhusiana na Uthman ni kwamba walimzuia asirejee na huenda lengo lao lilikuwa kwamba wakati ule wangeliweza kupata ufumbuzi wa tatizo lile.12

Mkataba Wa Ridhwaan

Waislamu walipatwa na fadhaa kubwa kutokana na kuchelewa kurejea kwa Uthman. Kisha ulipatikana uvumi kwamba Uthman ameuawa. Kusikia hivyo, Waislamu waliwakwa na ghadhabu nao wakataka kulipiza kisasi. Ili kuiimarisha dhamira yao ile, Mtume (s.a.w.w.) alisema: “Sitaitoka sehemu hii hadi nilimalize jambo hili.”

Katika wakati huu ambao hatari ilikuwa karibu sana, na Waislamu hawakuwa na silaha, Mtume (s.a.w.w.) aliamua kuchukua viapo vya utii kutoka kwa Waislamu na akakaa chini ya mti kwa lengo hili. Masahaba zake wote walimshika mkono ikiwa ni ishara ya kiapo na wakaapa kwamba wataihami ile dini takatifu ya Uislamu hadi mwishoni mwa uhai wao. Hii ndio ile suluhu ya Ridhwaan iliyotajwa katika Qur’ani Tukufu kwa maneno haya:

لَقَدْ رَضِيَ اللَّهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ فَعَلِمَ مَا فِي قُلُوبِهِمْ فَأَنْزَلَ السَّكِينَةَ عَلَيْهِمْ وَأَثَابَهُمْ فَتْحًا قَرِيبًا {18}

“Bila shaka Allah amewawia radhi waumini walipofungamana nawe chini ya mti, na Alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi akateremsha utulivu juu yao, na akawapa ushindi wa karibu.” (Sura al-Fath, 48:18).

Baada ya kula kiapo cha utii kwa Mtume (s.a.w.w.) jukumu la Waislamu likawa wazi. Imma Waquraishi wawaruhusu kuingia Makka na kufanya Hija ya Ka’abah au waupinge ukaidi wa Waquraishi kwa gharama ya uhai wao.

Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akifikiria hili wakati Bwana Uthman alipotokea kwa mbali, na jambo hili lenyewe lilikuwa ni utangulizi wa amani aliyoitamani mno Mtume (s.a.w.w.) na kusema: “Tatizo katika njia ya Waquraishi ni kiapo walichokiapa na mwakilishi wa Waquraishi atafanya mazungumzo nawe kuhusu ufumbuzi wa tatizo hili.”

Suhayl Bin ‘Amr Aonana Na Mtume (S.A.W.W)

Suhayl bin ‘Amr alitumwa na Waquraishi na maagizo maalum ili kuumaliza ule ugomvi kwa njia ya mapatano tutakayoyasoma baadae. Macho ya Mtume (s.a.w.w.) yalipomwangukia Suhayl, alisema: “Suhayl amekuja kufanya mapatano ya amani baina yetu na Waquraishi.” Suhayl akaja akakaa. Akasema kila aina ya vitu, na kama alivyo mwanadiplomasia stadi aliuamsha mwelekeo wa Mtume (s.a.w.w.) katika kuyatimiza mambo fulani fulani. Alisema: “Ewe Abul Qaasim! Makka ni Haram na makao makuu ya heshima yetu. Ulimwengu wa Kiarabu unafahamu kwamba wewe umepigana dhidi yetu. Kama ukiingia Makka katika hali iliyopo hivi sasa, iliyoandamana na nguvu, na uwezo, utaufanya unyonge wetu na utovu wetu wa msaada utambulike kwenye ulimwengu mzima wa Kiarabu. Kesho makabila yote ya Kiarabu watafikiria kuichukua nchi yetu.

Ninakuomba kwa jina la Mungu kuufikiria ufalme unaoshirikiana nasi, na vile vile uikumbuke heshima ya mji wa Makka na ambao vile vile ndio sehemu uliyozaliwa.”

Suhayl alipokuwa akiyasema haya, Mtume (s.a.w.w.) aliyaingilia mazungumzo yake na akasema: “Unalenga nini?” Suhayl akajibu: “ Machifu wa Waquraishi wana maoni ya kwamba mrudi Madina mwaka huu na muiahirishe Hija hadi mwaka ujao.

Mwaka ujao Waislamu wataweza kufanya Hija kama makabila yote mengine ya Uarabuni, kwa masharti ya kwamba hawakai mjini Makka kwa zaidi ya siku tatu na wasilete silaha yoyote nyingine ila zile ambazo kwa kawaida huchukuliwa na msafiri.”

Matokeo ya mazungumzo baina ya Mtume (s.a.w.w.) na Suhayl ni kwamba, iliamuliwa kwamba yafanywe mapatano ya ujumla na marefu baina ya Waislamu na Waquaishi. Suhayl alikuwa akiudhihirisha ukali usio kifani kuhusiana na yale masharti na maelezo ya mapatano yale, na katika nyakati fulani fulani ilionekana kwamba mapatano yale ya amani yatavunjika. Hata hivyo, kwa kuwa pande zote mbili zilitaka amani na maafikiano, ule uelekeo wa mazungumzo ulikuwa ukishikwa kila mara.

Ingawa yalikuwako yote hayo kuhusu ukali wa Suhayl, yale mapatano yalikamilika na iliamuliwa kwamba maelezo yake yaandikwe katika makala mbili na makala hizo zisainiwe na pande zote mbili.

Kama ilivyoandikwa na wanahistoria wengi, Mtume (s.a.w.w.) alimwelekekeza Sayyidna Ali (a.s.) kuyaandika mapatano haya ya Amani, na akasema: “Andika kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu,” na Saidina Ali (a.s.) aliandika hivyo.

Suhayl akasema: “Mimi siifahamu sentensi hii. Andika hivi: “Kwa jina Lako, Ee Allah!” Mtume (s.a.w.w.) aliikubali ile sentensi iandikwe kama ilivyotamkwa na Suhayl. Sayyidna Ali (a.s.) aliandika hivyo. Kisha Mtume (s.a.w.w.) alimwamrisha Sayyidna Ali (a.s.) aandike: “Huu ni mkataba ambao Muhammad Mtume wa Allah, ameufanya na Suhayl mwakilishi wa Waqurashi.”

Suhayl akasema: “Sisi hatuutambui rasmi utume wako na kama tungalikutambua kuwa u Mtume tusingelipigana vita dhidi yako. Huna budi kuandika jina lako na lile la baba yako na huna budi kutokitia cheo hiki kwenye mapatano haya.”

Baadhi ya Waislamu hawakukubali kwamba Mtume (s.a.w.w.) akubaliane na Suhayl kiasi kile.

Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) alilikubali hata hilo kwa kuzingatia maslahi yaliyo makubwa zaidi yatakayoelezwa hapo baadae, na akamwamrisha Sayyidna Ali (a.s.) afute kifungu cha maneno kisemacho: “Mtumbe wa Allah.”

Katika hatua hii Sayyidna Ali (a.s.) aliona uzito na akasema kwa heshima na taadhima: “Haitowezekana kwangu mimi kulichukua uhuru wa kukifuta cheo chako cha ‘Mjumbe’ na ‘Mtume’ kutoka karibu na jina lako takatifu.” Mtume (s.a.w.w.) alimwamrisha Sayyidna Ali (a.s.) kukiweka kidole cha Mtume (s.a.w.w.) kwenye neno lile ili aweze kulifuta yeye mwenyewe.

Sayyidna Ali (a.s.) akakiweka kidole cha Mtume (s.a.w.w.) juu ya neno lile na akakifuta cheo cha Mjumbe wa Allah.”13

Upole na moyo aliouonyesha Mtume (s.a.w.w.) katika kuyaandika mapatano haya havina kifani ulimwenguni. Kwa vile hakuvutiwa na fikara za kiulimwengu na mwelekeo wa majisifu, na alitambua kwamba ukweli haubadiliki kwa kuandika jambo lolote lile au kulifuta, ili kuhakikisha kwamba amani inapatikana, yeye alishika msimamo wa upatanisho na akayakubali maoni ya mpinzani wake ingawa alikuwa mkali kiasi kile.

Historia Inajirudia Yenyewe

Mwanafunzi wa kwanza na maarufu zaidi wa mafundisho ya Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.), naye pia alikabiliwa na fadhaa ya aina ileile, na kutokana na jambo hili mwanafunzi huyu Sayyidna Ali (a.s.) aliye mfano halisi wa Mtume (s.a.w.w.), kwa sababu fulani fulani amekuwa mfano halisi wa sifa zake zilizofanana na zake (s.a.w.w.) katika hatua mbalimbali. Wakati Amirul-Mu’minin (a.s.) alipotoa udhuru kuhusu kuyafuta yale maneno ‘Mtume wa Allah’ (s.a.w.w.) alimgeukia na kumwarifu kuhusu siku zake za baadae zilizofanana mno na zile zake (s.a.w.w.) kwa maneno haya; “Kizazi cha jamii hii kitakuita kwenye kitendo kama hiki nawe utakubali chini ya uonevu mkubwa.”14

Sayyidna Ali (a.s.) alilikumbuka jambo hili hadi katika Vita vya Siffin na wafuasi wenye fikara ndogo wa Imamu Ali (a.s.) walivutiwa na matendo ya kiudanganyifu ya askari wa Sham waliokuwa wakipigana chini ya uongozi wa Muawiyah na ‘Amr bin Aas na wakamshauri akubali kufanya Amani.

Ulifanyika mkutano wa kuandika mapatano ya amani. Katibu wa Amirul- Mu’minin (a.s.) aliyeitwa Ubaydullah bin Abi Raafi’ alielekezwa na Amirul-Mu’minin (a.s.) kuyaandika yale mapatano ya Amani kwa maneno haya; “Haya ndio mambo yaliyokubaliwa na Ali, Amirul-Mu’minin.”

Hapa ‘Amr bin Aas (aliyekuwa mwakilishi rasmi wa Muawiyah na jeshi la Sham) alimgeukia yule Katibu wa Sayyidna Ali (a.s.) na kusema: “Andika jina la Ali na baba yake, kwa sababu kama hapo awali tungalimtambua kuwa yu Amir wa Waumini, tusingelipigana naye kabisa”. Majadiliano juu ya jambo hili yalirefushwa. Amirul-Mu’minin (a.s.) hakuwa tayari kutoa udhuru wowote kwa wale marafiki zake wajinga. Sehemu ya siku ilitumiwa katika kutoafikiana kwa pande hizi, mpaka kutokana na msisitizo wa mmoja wa maafisa wake mwenyewe, aliruhusu kwamba kile kifungu cha maneno kisemacho: ‘Amirul-Mu’minin’ kifutwe. Kisha akasema: “Allah Yu Mkubwa! Huku ni kuiangalia kwa mbali Hadith ya Mtume (s.a.w.w.)” Baada ya hapo alilirudia lile tukio la Hudaybiah mbele ya watu na aliyoambiwa na Mtume (s.a.w.w.) wakati ule.15

Hati Ya Mapatano Ya Hudaybiyah

Waquraishi na Waislamu wamekubaliana kwamba hawatapigana au kushambuliana kwa kipindi cha miaka kumi, ili kwamba usalama wa jamii na amani ya watu wote iweze kudumishwa kwenye sehemu mbalimbali za Uarabuni.

Kama mtu kutoka miongoni mwa Quraishi atautoka mji wa Makka bila ya ruhusa ya wazee wake na akasilimu na akajiunga na Waislamu, ni lazima Muhammad amrudishe kwa Waquraish. Hata hivyo, iwapo mmoja wa Waislamu atakwenda kwa Waquraishi, hawatalazimika kumrudisha kwa Waislamu.
Waislamu na Waquraishi watakuwa huru kufanya mapatano na kabila lolote wapendalo.

Mwaka huu Muhammad na masahaba zake warudi Madina kutoka pale Hudaybiyah. Hata hivyo, kwenye miaka ifuyatiayo, watakuwa huru kuingia Makka na kufanya Hija ya Ka’abah, chini ya sharti la kwamba hawatakaa mjini Makka kwa zaidi ya siku tatu na kwamba hawatachukua silaha yoyote zaidi ya zile azichukuazo msafiri. 16

Kwa mujibu wa mapatano haya, Waislamu waishio Makka wako huru kuzitekeleza ibada zao za kidini na Waquraishi hawatakuwa na haki ya kuwatesa au kuwalazimisha kuikana dini yao au kuidhihaki dini yao.17
Watia saini wa mapatano haya wanakubali kuziheshimu mali za watu wa upande wa pili na kuepuka udanganyifu na hila dhidi ya wenzao na kuziweka nyoyo zao huru kutokana na mfundo dhidi ya wenzao. Uhai na mali za Waislamu wafikao Makka kutoka Madina vitaheshimiwa.18

Haya ndio maneno ya mapatano ya amani ya Hudaybiyah yaliyokusanywa kutoka kwenye vitabu mbali mbali. Mapatano haya yaliandikwa katika makala mbili. Baadhi ya watu kutoka miongoni mwa Waquraishi na Waislamu waliyashuhudia mapatano haya ambayo baada ya hapo, nakala moja alipewa Suhayl na nyingine akapewa Mtume (s.a.w.w.).19

Bishara Njema Ya Uhuru

Bishara njema ya uhuru kama ilivyo kwenye mapatano haya ilimfikia kila mtu. Ingawa kila kifungu cha mapatano haya kinastahili kujadiliwa, sehemu iliyo nyeti yenye kuhitaji kufikiriwa sana ni kifungu cha pili kilichoamsha hasira za baadhi ya watu katika siku ile. Ingawa masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) walikuwa na wasiwasi kutokana na ubaguzi huu na waliyatamka maneno yasiyostahili kusemwa kuhusiana na ule uamuzi uliochukuliwa na kiongozi kama vile Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.). Lakini kifungu hiki kikiwa bado ni chenye kuangaza kinaionyesha namna ya fikira ya Mtume (s.a.w.w.) katika mambo ya uhubiri wa Uislamu. Inaonyesha kikamilifu heshima kuu ambayo huyu kiongozi mkuu aliitoa kwenye kanuni za uhuru.

Katika kuujibu ukanusho uliotolewa na baadhi ya masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) kuhusu ni kwa nini wawasalimishe wakimbizi waliotoka kwa Waquraishi ambapo wao Waquraishi hawawajibiki kuwasalimisha watu wao, alijibu akisema: “Kama Mwislamu anatwaa ushirikina, na akaikimbia bendera ya Uislamu, na akayapendelea mazingira ya waabudu masanamu na dini isiyo ya kibinaadamu badala ya yale mazingira ya Uislamu na Upweke wake Allah, inaonyesha kwamba hakusilimu kwa moyo wote, na imani yake haikupata msingi ustahilio na uwezao kuyatosheleza maumbile yake, na Mwislamu wa aina hiyo, hana faida kwetu. Na kama tukimsalimisha mkimbizi atokaye kwa Waquraishi, ni kwa sababu hii kwamba sisi tumetosheka kwamba Allah atawapatia njia ya wokovu wao.”20

Mustakabali wa baadae ulithibitisha kwamba utabiri wa Mtume (s.a.w.w.) juu ya jambo hili (kwamba Allah Atawapatia njia ya wokovu wao) ulikuwa sahihi kabisa, kwa sababu mara tu baada ya hapo, wao Waquraishi wenyewe waliomba kifungu hiki kifutwe kutokana na matukio mengi yasiyopendeza waliyobidi kuyakabili kwa sababu ya kifungu hiki.

Kifungu hiki kilikuwa ni jibu lenye kunyamazisha kwa udhaifu wa wengi wa mustashirik wanaosisitiza kwamba sababu ya kuendelea kwa Uislamu ilikuwa ni matumizi ya upanga. Hawawezi kustahimili kuona kwamba utukufu wa Uislamu umo kwenye ukweli wa kwamba katika kipindi kifupi sana ulienea kwenye maeneo mengi ya ulimwenguni. Hivyo basi, kutokana na malengo ya ubinafsi, na kwa lengo la kuzitia sumu akili, wanalazimika kusema kwamba sababu ya maendeleo ya Uislamu ilikuwa ni nguvu za mabavu.

Mapatano haya ya amani yalifanyikiwa katika siku za awali za Uislamu mbele ya kiongozi mkuu wa Uislamu, kama yanavyoakisi moyo wa Uislamu na mafundisho matakatifu na misingi ya ubinadamu iliyomo kwenye sheria zake zote. Ni uonevu mkuu kwamba tulazimike kusema kuwa Uislamu umeenezwa kwa nguvu ya upanga.

Kwa mazingatio ya kifungu cha tatu, kabila la Khuzaa’ah lilifanya mapatano ya ulinzi na Waislamu na kabila la Bani Kinanah waliokuwa maadui wa Bani Khuza’ah wa tangu kale, waliamua kufanya ushirikiano baina yao na Waquraishi.

Juhudi Za Mwisho Katika Kuhifadhi Amani

Utangulizi wa mapatano ya amani na maandishi yake unaonyesha dhahiri kwamba sehemu yake kubwa ilikuwa na mwelekeo wa kielimu, na sababu zilizomfanya Mtume (s.a.w.w.) ayakubali mapatano haya na kukubali kukifuta kifungu cha maneno kisemacho: ‘Mtume wa Allah’ na kule kuanza kwake na maneno: Kwa jina lako, Ee Allah (kwa kuwa ulikuwa ndio mtindo katika zama za ujinga); ilikuwa kwamba alitamani mno kuidumisha amani Barani Arabu.

Na alipokubali kwamba wakimbizi wa Kiislamu kutoka miongoni mwa Waquraishi wasalimishwe kwa watawala wa serikali ya waabudu masanamu, ilitokana na ukaidi mkubwa wa Suhayl. Hivyo kama Mtume (s.a.w.w.) asingelikubaliana na Suhayl katika jambo hili, kwa mtazamo wa kuzihami haki za kundi hili (yaani wakimbizi wa Kiislamu kutoka miongoni mwa Waquraishi) na kuziheshimu fikira za kawaida zilizokuwa kinyume cha ubaguzi katika kule kuwasalimisha wale wakimbizi, bila shaka amani ya jumla ingelihatarika na hii baraka kuu ingelipotea.

Hivyo basi, kwa nia ya kulifikia lengo lililo kuu na tukufu zaidi, Mtume (s.a.w.w.) alilivumilia shinikizo na matakwa yote haya ili kwamba ile fursa kuu ya kuhakikisha amani hii isipotee, juu ya hali ambayo usumbufu wote huu ulikuwa ni kitu kidogo mno. Na kama angaliyajali maoni ya kawaida na haki za kundi lile, basi Suhayl kutokana na ukaidi wake angelianzisha cheche za vita.

Tukio lifuatalo ni ushahidi wa dhahiri wa jambo hili: Majadiliano kuhusiana na maneno yaliyomo kwenye Mkataba wa amani yalimalizika na Sayyidna Ali (a.s.) alikuwa akishughulikia uandishi wake, ambapo kwa ghafla Abu Jandal bin Suhayl, mtoto wa yule mwakilishi wa Waquraishi katika kufanya yale mapatano ya amani, alitokea mahali pale akiwa kafungwa minyororo miguuni. Watu wote walishangazwa na kufika kwake pale, kwa kuwa tangu muda mrefu alikuwa kafungwa na kutiwa minyororo na baba yake. Alikuwa ni mfungwa asiye na hatia, ila kosa lake pekee lilikuwa kwamba kasilimu na alikuwa akichukuliwa kuwa yu mmoja wa wafuasi wa Mtume (s.a.w.w.). Kutokana na mazungumzo yaliyofanyika karibu na jela yake alifahamu kwamba Waislamu wamewasili Hudaybiyah.21 Hivyo basi, alifaulu kutoroka mle jela kwa hila maalum na akawasili katikati ya Waislam kwa kutwaa njia iliyochepuka kupitia milimani.

Macho ya Suhayl yalipomwona mwanawe alikasirika mno kiasi kwamba, akiwa kajawa na hasira kubwa, alimpiga kofi kubwa mno usoni mwake. Kisha alimgeukia Mtume (s.a.w.w.) na kusema: “Huyu ni mtu wa kwanza ambaye ni lazima arejee Makka kwa mujibu wa hiki kifungu cha pili cha mapatano haya.” Maana yake ilikuwa kwamba, Abu Jandal kwa vile yu Mquraishi aliyeukimbia mji wa Makka hana budi asalimishwe kwao.

Hakuna kuukana ukweli uliopo kwamba dai la Suhayl halikuwa na haki wala lenye msingi, kwa sababu yale mapatano yalikuwa bado hayajamalizwa kuandikwa na kutiwa saini na pande zihusikazo. Je, vipi mshirika wa mkataba anaweza kuyategemea mapatano ambayo bado hayajapitia kwenye hatua zake za mwisho? Kwa sababu hii Mtume (s.a.w.w.) alimwambia Suhayl: “Mapatano yetu bado hayajatiwa saini.” Suhayl akajibu akasema: “Kwa sababu hiyo, mimi ninautupilia mbali mchakato wote huo na kuufanya kuwa batili na usio na faida.” Alikuwa mkaidi mno kwenye jambo hili kiasi kwamba Mikraz na Huwaytab, watu wawili waliokuwa wakuu wa Waquraishi walichukizwa mno na ukali wake. Mara moja wakamtoa Abu Jandal kutoka kwa baba yake, wakamwingiza kwenye hema na kumwambia Mtume (s.a.w.w.): “Ewe Muhammad! Hivi sasa Abu Jandal yuko kwenye ulinzi wako.”

Walitaka kuumaliza mzozo ule kwa njia hii lakini kung’ang’ania kwa Suhayl kuliukwamisha mpango wao. Aliyashikilia maneno yake na akasema: “Kutegemeana na maoni ya maafikiano yetu, tayari mapatano yameshafanyika.”
Mtume (s.a.w.w.) alilazimika kufanya juhudi za mwisho katika kuihifadhi misingi ya amani kitu kilichokuwa na faida mno kwa uhubiri wa Uislamu. Hivyo basi, alikubali kule kurejea Makka kwa Abu Jandal pamoja na baba yake. Ili kumfariji yule Mwislamu aliyetiwa minyororo na aliyetakiwa kusalimishwa kwa makafiri mbele ya mamia ya Waislamu mashujaa, alisema: “Ewe Abu Jandal! Kuwa mwenye subira.

Tulipenda kwamba baba yako akutoe na akuweke mikononi mwetu kwa njia ya huba na upendo.
Sasa, kwa vile hajapenda kufanya hivyo, huna budi kuwa na subira na uvumilivu na huna budi kutambua kwamba Allah atakufungulia njia ya kuachiliwa, wewe na wengineo walio kwenye kifungo.”

Mkutano ule ukafikia ukomo. Zile nakala za mapatano zikasainiwa. Suhayl na marafiki zake wakaondoka kwenda Makka na Abu Jandal naye akaenda Makka akiwa chini ya ulinzi wa Mikraz na Kuwaytab. Kwa nia ya kuimaliza ile hali ya kuwa kwenye Ihr?m, Mtume (s.a.w.w.) alimchinja ngamia wake na kunyoa nywele za kichwa chake na wengineo nao wakafanya vivyo hivyo.22

Tathmini Ya Mkataba Wa Amani Wa Hudaybiyah

Mapatano ya amani yalifanyika baina ya Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) na viongozi wa ushirikina, na baada ya kukaa pale Hudaybiyah kwa muda wa siku kumi na tisa Waislamu wakarejea Madina na wale waabudu masanamu wakarejea Makka.

Zilitokea tofauti na kutoafikiana baina ya masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) wakati wa kuandikwa kwa yale mapatano na vilevile baada ya hapo. Kundi moja miongoni mwao waliyafikiria mapatano yale kuwa ni yenye faida kwa Uislamu, na kundi jingine ambalo watu wake waliweza kuhesabika kwa vidole vya mkono, waliukadiria kwamba uko nje ya malengo yake. Hivi sasa ni karne ya kumi na nne tangu yafanyike mapatano yale, tumeamua kuyatathmini kwa jinsi isiyo ya upendeleo na iliyo ya hakika, na tutaimalizia Sura hii baada ya kuzidokeza zile tofauti zilizotajwa hapo juu. Maoni yetu ni kwamba, haya mapatano ya amani yalithibitika kuwa ni yenye manufaa kabisa kwa Uislamu na kuufanya ushindi wake kuwa wa mwisho. Zifuatazo hapa chini ndizo hoja ambazo tungelitaka kuzitoa:

1. Vita zilizokuwa zikiendelea na mashambulizi ya Waquraishi na uchochezi wao wa ndani na wa nje tuliotaja kwenye maelezo ya vita za Uhud na Ahzaab hayakuacha nafasi ya muda kwa upande wa Mtume (s.a.w.w.) kuweza kuhubiri Uislamu miongoni mwa makabila mbalimbali, pamoja na maeneo yaliyo nje ya Bara Arabuni pia, na wakati huu wenye thamani ulitumika karibuni wote katika kujihami na kuibatilisha mipango miovu ya adui. Hata hivyo, baada ya kufanywa kwa haya mapatano ya amani, Waislamu na yule kiongozi wao mkuu waliondolewa ile hatari kutoka kwenye eneo la Kusini, na sasa uwanja umeshatayarishwa kwa uhubiri wa Uislamu kwenye nchi nyingine.

Athari za mapatano haya ya amani zilidhihirika baada ya miaka miwili, kwa sababu pale mapatano ya Hudaybiyah yalipokuwa yakifanyika Mtume (s.a.w.w.) alifuatana na watu 1400, lakini miaka miwili baadae, alipokuwa akienda rasmi kuuteka mji wa Makka watu wengi kiasi cha elfu kumi walikwenda pamoja naye chini ya kivuli cha bendera ya Uislamu na tofauti hii ya dhahiri katika idadi ya watu waliofuatana naye, ilikuwa ni matokeo ya mapatano ya Hudaybiyah. Hii ilitokana na ukweli uliopo kwamba hapo awali, watu wengi hawakuweza kujiunga na Waislamu kutokana na kuwaogopa Waquraishi. Lakini pale Waquraishi walipoanza kutambua kuwako kwa Uislamu na kuyaacha huru makabila kujiunga nao, ule woga uliokuwamo akilini mwa watu wa makabila mengi ulitoweka na Waislamu wakawa kwenye hali ya kuweza kuuhubiri Uislamu kwa Uhuru kabisa.

2. Faida ya pili waliyoipata Waislamu kutokana na mapatano haya ilikuwa kwamba lile pazia la chuma waliloliweka wale waabudu masanamu baina ya mtu wa kawaida na dini ya Uislamu liliondolewa, na matokeo yake yakawa kwamba kufanya safari za mjini Madina kukawa huru.

Watu wakawa na mawasiliano zaidi na Waislamu katika nyakati za misafara ya kwenda Madina na wakaweza kuyafahamu mafundisho matakatifu ya Uislamu.

Walishangazwa walipoiona nidhamu na utaratibu mwema miongoni mwa Waislamu na uaminifu wao katika ibada na utii kwa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.). Usafi wa Waislamu na utawadhaji katika nyakati za sala, safu zao zilizopangwa vizuri, hotuba za Mtume (s.a.w.w.) zenye kuathiri na kuzivutia nyoyo na Aya tamu za Qur’ani Tukufu, pamoja na urahisi na ufasaha wake, viliwavutia upesi sana kwenye Uislamu. Waislamu walisafiri kwenda Makka na kwenye viunga vyake kwa ajili ya shughuli mbalimbali, baada ya kufanywa kwa mapatano yale, walikutana na ndugu na marafiki zao wa kale, wakawalingania Uislamu miongoni mwao na wakawafundisha maadili, sheria na kanuni, na vitu vilivyo halali na vilivyo haramu katika dini hii.

Na jambo hili lenyewe likawa chanzo cha idadi kubwa ya viongozi wa ushirikina kama vile Khalid bin Walid na ‘Amr bin Aas kujiunga na Waislamu kabla ya kutekwa kwa mji wa Makka. Kwa kweli aina hii ya maarifa ya watu juu ya Uislamu ilijenga msingi wa kutekwa kwa Makka na ikawa sababu ya hiki kituo kikuu cha ibada ya masanamu ulimwenguni kuangukia chini ya utawala wa Waislamu. Matokeo yake ni kwamba, watu walisilimu kwa idadi kubwa. Ushindi huu mkuu ulikuwa matokeo ya mawasiliano ya karibu zaidi, kuondoka kwa hofu kutoka nyoyoni na ulinganiaji wa Uislamu miongoni mwa waabudu masanamu bila ya mgogoro au kipingamizi.

3. Mawasiliano ya karibu na Mtume (s.a.w.w.) wakati wa kuyafanya ule mkataba kuliondoa kutoelewa kwingi kutoka kwenye akili za viongozi wa ushirikina, kwa sababu uadilifu bora zaidi wa Mtume (s.a.w.w.) na upole na uvumilivu wake vilivyo kinyume cha ukaidi wa lile kundi la pili vilimthibitisha kuwa yu chemchem ya maadili ya hali ya juu zaidi ya kibinadamu.

Bila kujali ukweli kwamba amepata taabu sana kutoka kwa Waquraishi, bado moyo wake ulikuwa umejawa na hisia za upendo wa kibinadamu. Waquraishi walishuhudia ya kwamba katika kufanya mkataba ule na kuvikubali vifungu vyake vya kulazimishwa, alitofautiana na maoni ya idadi kubwa ya masahaba zake mwenyewe na akaipendelea heshima ya Haram na Ka’abah, na sehemu ya kuzaliwa kwake (Makka) kuliko mwelekeo wa kundi lake.

Tabia hii iliitangua ile propaganda ya kinyume iliyokuwa ikifanywa juu ya mwenendo wa Mtume (s.a.w.w.) na ilithibitisha kwamba alikuwa rafiki wa binadamu na mtu wa amani, ambaye asingeweza kuonyesha mfundo na uadui kwa maadui zake, japo itokee kupata nafasi ya kuitawala Arabia nzima. Hata hivyo hatuwezi kukana ukweli uliopo kwamba, kama Mtume (s.a.w.w.) angelijitia kwenye vita katika siku ile angeliweza kushinda kama ilivyoelezwa na Qur’ani Tukufu, na maadui zake wangelikimbia: “Na lau makafiri wangelipigana nanyi basi bila shaka wangeligeuza migongo, kisha wasingelipata mlinzi wala msaidizi.” (Sura al-Fath, 48:22). Hata hivyo, alidhihirisha hisia za huruma na huba kwa wanadamu kwa upole wake na kuzibatilisha propaganda za kinyume dhidi yake.

Kutokana na mwanga wa hoja hizi wasomaji hawana budi kuutambua utukufu wa kauli ya Imamu wetu wa Sita, Imamu Ja’far Sadiq (a.s.) juu ya mapatano haya ya amani. Anasema: “Katika kipindi cha uhai wa Mtume (s.a.w.w.) hakuna tukio lililokuwa na faida zaidi kuliko yale mapatano ya Amani ya Hudaybiyah.”

Matukio yaliyofuatia yalithibitisha kwamba kuyakataa mapatano haya pamoja na maneno yake kulikofanywa na masahaba wachache wa Mtume (s.a.w.w.) ambao kiongozi wao alikuwa Bwana ‘Umar bin Khatab23 hakukuwa na msingi hata kidogo. Wanahistoria wametoa maelezo kamili ya maneno ya wale walioyakataa.24

Faida ya mapatano haya ilidhihirika kutokana na ukweli uliopo kwamba Mtume (s.a.w.w.) alikuwa bado hajawasili Madina pale ilipofunuliwa Sura al-Fath, iliyowaashiria Waislamu, na ikayaita mapatano haya ya Amani ya Hudaybiyah kuwa ni ushindi katika Jihad. Inasema: “Bila shaka Tumekupa ushindi ulio wazi.” (Sura al-Fath, 48:1).

Waquraishi Wasisitiza Kufutwa Kwa Kifungu Kimoja Cha Mkataba

Hata hivyo, mara tu baada ya haya, matukio machungu yaliwalazimisha Waquraishi kumwomba Mtume (s.a.w.w.) kukifuta kifungu cha pili cha ule Mkataba wa Amani. Kilikuwa ni kifungu kilekile kilichowaudhi masahaba zake Mtume (s.a.w.w.) na ambacho yeye amekikubali kutokana na ukaidi usio kifani wa Suhayl. Kifungu hiki kinasema hivi:

“Kama mtu kutoka miongoni mwa Quraishi atautoka mji wa Makka bila ya ruhusa ya wazee wake na akasilimu na akajiunga na Waislamu, ni lazima Muhammad amrudishe kwa Waquraishi. Hata hivyo, iwapo mmoja wa Waislamu atak- wenda kwa Waquraishi, hawatalazimika kumrudisha kwa Waislamu.”

Kifungu hiki kiliamsha hasira za baadhi ya watu katika siku ile, lakini Mtume (s.a.w.w.) alikikubali kwa moyo mmoja na kusema: “Allah Ataifungua njia kwa ajili ya faraja ya Waislamu wanyonge walio wafungwa wa Waquraishi.”

Njia ya faraja hiyo na sababu ya kufutwa kwa kifungu hiki ilikuwa kama ifuatavyo: Mwislamu mmoja aliyeitwa Abu Basir aliyekuwa kafungwa na waabudu masanamu kwa kipindi kirefu aliweza kutorokea Madina.

Watu wawili wakuu walioitwa Azhar na Akhnas walimwandikia barua Mtume (s.a.w.w.) na kumkumbusha kwamba kufuatana na kifungu cha pili cha mkataba, Abu Basir hana budi kurudishwa kwao. Walimpa mtu mmoja anayetokana na kabila la Bani ?mir barua ile, ambaye alifuatana na mtumwa wao na kumwomba ampe Mtume (s.a.w.w.) barua ile.

Kufuatana na yale mapatano aliyoyafanya, Mtume (s.a.w.w.) alimwambia Abu Basir: “Huna budi kurejea kwa watu wako na katu si sahihi kwamba tufanye ukaidi dhidi yao. Mimi ninao uhakika kwamba Allah Mwenye nguvu zote atafanya njia ya kukuachia wewe na wengine.”

Abu Basir akasema: “Je unanitoa na kuniweka mikononi mwa waabudu masanamu ili wanifanye niikane dini ya Allah?” Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) aliirudia tena ile sentensi tuliyoitaja na hatimaye akamkabidhi Abu Basir kwa wale wawakilishi wa Waquraishi.

Kisha wale watu watatu waliondoka kwenda Makka. Walipofika mahali paitwapo Zil-Hulayfah,25 yule Abu Basir aliegemea kwenye ukuta kutokana na uchovu. Kisha akamwomba yule mtu wa kabila la Bani ?mir kwa njia ya kirafiki, ampe upanga wake ili autazame. Ule upanga ulipofika mikononi mwake, upesi sana alimuuwa yule ‘?mir. Yule mtumwa akakimbia kwa woga. Akarejea Madina na kumwambia Mtume (s.a.w.w.): “Abu Basir amemwua yule mwenzangu.” Mara tu baada ya hapo Abu Basri naye akafika na kuisimulia hadithi yake na kusema: “Ewe Mtume wa Allah! Wewe umeyatekeleza mapatano uliyoyafanya. Hata hivyo, mimi siko tayari kujiunga na watu wenye kuifanyia mzaha dini yangu.”.

Baada ya kuyatamka maneno hayo alikwenda Pwani ya bahari iliyokuwa njia ya misafara ya Waquraishi na kwenda kukaa mahali paitwapo Eis. Waislamu wa Makka walipata taarifa za kisa cha Abu Basir na kiasi cha watu sabini miongoni mwao wakaenda kujiunga naye. Hawa Waislamu sabini ambao maisha yao yalifanywa na Waquraishi kuwa ya taabu, waliamua kuiteka nyara misafara ya kibiashara ya Waquraishi au kumwua yeyote yule waliyeweza kumkamata.
Waliitekeleza mipango yao kwa ustadi kiasi kwamba Wakureishi hawakuweza kuvumilia, kutokana na usumbufu ule walimwandikia barua Mtume (s.a.w.w.) akifute kifungu kile kwa mapatano ya pande zote mbili na amuite Abu Basir na wenzie warudi Madina. Mtume (s.a.w.w.) alikifuta kifungu kile kwa maafikiano ya watu wote na akawaamrisha wale wakimbizi waliokuwa wakiishi pale Eis warejee Madina.26

Kitendo hiki kilitoa faraja kubwa kwa watu wote kwa ujumla na Waquraishi walitambua kwamba waumini wa kweli hawawezi kufanywa mateka daima na lilikuwa ni jambo la hatari kumweka mtu wa aina hiyo katika hali ya kuwa mateka, kwa sababu wakati wowote ule apatapo nafasi ya kutoroka atataka kulipiza kisasi.

Wanawake Wa Kiislamu Hawaku Salimishwa Kwa Waquraishi

Mapatano ya Hudaybiyah yalisainiwa. Ummi Kulthumu, binti wa Uqbah bin Abi Mu’ayt, alikuja Madina kutoka Makka. Kaka zake walioitwa Amm?rah na Walid walimwomba Mtume (s.a.w.w.) amrudishe kwao kwa mujibu wa kifungu cha pili cha mapatano yale. Mtume (s.a.w.w.) aliwajibu akisema: “Wanawake hawakujumlishwa kwenye kifungu hicho kwa kuwa kifungu kile kinawahusu wanaume tu.”27 Nayo Sura al-Mumtahinah inaidhihirisha hali hii kuhusiana na wanawake. Inasema:

“Enyi mlioamini! Watakapokufikieni wanawake walioamini wanao- hama, basi wajaribuni, Allah ndiye Ajuaye zaidi imani yao, kama mki- jua kuwa wao ni waumini basi msiwarudishe kwa makafiri. Hawa si halali kwao, wala wao si halali kwao, na warudishieni mali walizotoa.
. . .” (Surah al-Mumtahinah, 60:10).

Hii ndio hadithi ya Hudaibiyah. Kama matokeo ya amani yaliyoletwa na mapatano haya, Mtume (s.a.w.w.) alikuwa kwenye nafasi ya kuwasiliana na wafalme na watawala wa ulimwenguni kote na kuwafikishia mwito na Utume wake kwa wanadamu wote.

 • 1. Majma’ul Bayaan, Juz. 9, uk. 126.
 • 2. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 309.
 • 3. Rawzatul-Kaafi, uk. 322.
 • 4. Majma’ul Bayaan, Juz. 2, uk. 488.
 • 5. Bihaarul Anwwar, Juz. 20, uk. 330.
 • 6. Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 270-272.
 • 7. Kufuatana na ilivyonukuliwa na Tabari (Juz. 2, uk. 276) Hulays alikuja kuo- nana na Mtume (s.a.w.w.) baada ya Urwah Saqafa kuonana naye.
 • 8. Inaelekea kwamba watu waliomzunguka Mtume (s.a.w.w) walizificha nyuso zao.
 • 9. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 314; Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 274-275.
 • 10. Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 278.
 • 11. Mwenye macho haambiwi tazama, bali hali halisi yamsukuma kutaka kuujua uko wapi huo ushujaa wa Umar? – Mhariri.
 • 12. Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 278-279.
 • 13. Irshad Mufid, uk. 6; A’laamul Waraa, uk. 106; Bihaarul Anwar, Juz. 20, uk. 368; lakini Tabari alikosea kuhusu jambo hili naye ameeleza kwamba Mtume (s.a.w.w.) yeye mwenyewe aliliandika Jina Lake.
 • 14. Tarikh, Juz. 2, uk. 138; Bihaarul Anwaar, Juz. 20, uk. 353.
 • 15. Tarikhul Kamil, Juz. 3, uk. 162.
 • 16. Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 24 na vitabu vingine.
 • 17. Bihaarul Anwwar, Juz. 20, uk. 353 na vitabu vingine.
 • 18. Majma’ul Bayaan, Juz. 9, uk. 117.
 • 19. Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 25-26.
 • 20. Siiratu Halabi, Juz. 3, uk. 12; Bihaarul Anwwar, Juz. 20, uk. 312.
 • 21. Mahali hapa Hudaybiyah pako umbali wa kilometa kumi hadi kumi na nne hivi kutoka Makka na ardhi yake kubwa ni sehemu ya Haraam.
 • 22. Tarikhut-Tabari, Juz. 2, uk. 281; Bihaarul Anwwar, Juz. 2, uk. 352 na Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 281.
 • 23. Imepokewa ndani ya vitabu vya historia vya kisuni kuwa kutokana na Mtume kukubali sharti lile la Suhayl la kufuta neno “Mtume wa Allah” Umar bin Khatab alisema: “Hakuna siku niliyokuwa na shaka na utume wa Mtume kama siku hii.”– Mhariri.
 • 24. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 316.
 • 25. Hii ni sehemu iliyoko kiasi cha kilomita kumi au kumi na moja kutoka Madina. Watu huvaa Ihraam hapa waendapo Makka.
 • 26. Maghaazil al-Waaqidi, Juz. 2, uk. 624; Tarikhut-Tabari Juz. 2, uk. 284.
 • 27. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 323.