Sura Ya 45: Kadha Ya Umrah

Yalipotiwa saini yale mapatano ya Hudabiyah, Waislamu walipata haki ya kwenda Makka baada ya mwaka mmoja tangu tarehe ya kufanyika kwa yale mapatano, nao waliwajibika kutoka mjini humo baada ya kukaa siku tatu na kufanya Umrah.1 Katika siku hizo hawakuruhusiwa kuchukua silaha yoyote zaidi ya silaha ya msafiri (ambayo ni upanga).

Mwaka ulipita tangu pale yalipofanyika yale mapatano, hivyo muda ulifika kwa Waislamu kuweza kuitumia ile fursa waliyopewa na mapatano yale, na wale Waislamu muhajiriina walioyaacha maskani yao yapata miaka saba iliyopita kwa ajili ya Uislamu na wameichagua nchi ya kigeni kuwa maskani yao, sasa wanaweza kwenda Makka tena kufanya Hija ya Ka’abah na vile vile kuwaona ndugu zao. Kwa sababu hiyo, pale Mtume (s.a.w.w.) alipotangaza kwamba wale watu walionyimwa kuitembelea Ka’abah mwaka mmoja uliopita, wajitayarishe kwenda Makka, shauku isiyo na kifani ilitokea miongoni mwao na machozi ya furaha yalitiririka mashavuni mwao. Kama katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita Mtume (s.a.w.w.) alisafiri na watu 1300, idadi ya wale waliofuatana naye mwaka mmoja baadae ilifikia watu elfu mbili.

Watu mashuhuri miongoni Muhajirina na Ansar waliweza kuonekana miongoni mwa wale waliojitayarisha kwa safari hii. Walimfuata Mtume (s.a.w.w.) kwenye sehemu zote na walichukua ngamia themanini waliokuwa na alama za kutolewa kafara shingoni mwao. Mtume (s.a.w.w.) alivaa Ihr?m msikitini na wengineo wakamfuatia. Hivyo watu elfu mbili waliovaa Ihraam na wenye kutamka kwa dhati neno Labbayk midomoni mwao, waliondoka kwenda Makka.

Msafara huu ulikuwa na utukufu na heshima nyingi nao ulivutia mno kwa Waislamu pamoja na waabudu masanamu, kiasi kwamba iliwafanya waabudu masanamu kuelekea kwenye imani na ukweli wa Uislamu.

Kama tukisema kwamba safari hii ilikuwa safari ya kiuhubiri na watu hawa kwa kweli walikuwa jeshi la Uislamu, tutakuwa bado hatujatia chumvi, kwani matokeo ya kiroho ya safari hii yalitokea upesi sana na hatimaye wale maadui wakuu wa Uislamu kama vile Khalid bin Wadid, yule shujaa wa vita vya Uhud, na Amr bin Aas mwanasiasa wa Uarabuni, walipata mwelekeo wa kwenye Uislamu kutokana na kuuona utukufu huu na mara tu baada ya hapo waliipokea dini hii.

Mtume (s.a.w.w.) hakuwa na imani na Waquraishi kutokana na udanganyifu na kijicho chao. Ulikuwako uwezekano kwamba wangaliwashambulia Mtume (s.a.w.w.) na masahaba wake kwa kuwashitukizia atakapokuwa kwenye ukanda wa Makka na kumwaga damu ya baadhi yao, hasa pale ambapo wao (Waislamu) hawakuchukua silaha yoyote mbali ya zile silaha za msafiri. Hii ni kwa sababu kufuatana na masharti ya mapatano yale hawakuweza kuingia Makka wakiwa na silaha.

Ili kuondoa aina yoyote ile ya wasiwasi, Mtume (s.a.w.w.) alimteua mmoja wa maafisa wake aliyeitwa Muhammad bin Maslamah akifuatana na watu mia mbili waliokuwa na silaha zilizokuwa muhimu kama vile deraya na mikuki na walikuwa na farasi mia moja wepesi wa kukimbia ili kuutangulia ule msafara na kwenda kupiga kambi kwenye bonde la Marruz Zahraan (lililoko karibu na Haram) na kusubiri hapo hadi Mtume (s.a.w.w.) awasili. Majasusi wa Waquraishi waliokuwa wakiziangalia harakati za Mtume (s.a.w.w.), waliwaarifu machifu wa Waquraishi jambo hili.
Mikriz bin Hafs alikutana na Mtume (s.a.w.w.) akiwa yu mwakilishi wa Waquraishi na akamfikishia kutopendelea kwao kitendo kile. Mtume (s.a.w.w.) alijibu akasema: “Mimi au masahaba zangu hututafanya jambo lolote lililo kinyume na yale mapatano (yetu) na sisi sote tutaingia kwenye Haram tukiwa hatuna silaha.

Ama kuhusu afisa huyu na wale watu mia mbili wenye silaha, watabakia hapa.” Kwa kauli hii Mtume (s.a.w.w.) alimfanya yule mwakilishi wa Waquraishi atambue kwamba kama wakifanya mashambulizi ya kustukiza wakati wa usiku na kuchukua fursa isiyostahili kutokana na Waislamu kutokuwa na silaha, hili jeshi la msaada lililowekwa ukingoni mwa Haram pamoja na silaha, lingekuja upesi kuwasaidia na kuwapatia silaha mikononi mwao.

Waquraishi wakatambua umaizi wa Mtume (s.a.w.w.) na wakawafungulia Waislamu malango ya mji wa Makka. Viongozi wa waabudu masanamu na walio chini yao wakatoka mjini na kwenda kwenye vilima na vichuguu vya kaburini, ili kwamba wasionane na Mtume (s.a.w.w.) na masahaba zake na vilevile waweze kuyaona mishughuliko yao yote kwa mbali.

Mtume (S.A.W.W.) Aingia Mjini Makka

Mtume (s.a.w.w.) aliingia mjini Makka akiwa amepanda ngamia wake maalum huku akifuatana na watu elfu mbili waliomzunguka na sauti ya tamko lao, Allahumma labbaik ikipaa na kupiga mwangwi mji mzima. Sauti ya huu mkusanyiko teule ilivutia mno kiasi kwamba watu wote wa Makka walivutiwa nayo, na wakaanza kuwa na mvuto maalum na hisia juu ya Waislamu nyoyoni mwao. Wakati huo huo, umoja wa Waislamu ulijenga hofu isiyo kifani nyoyoni mwa waabudu masanamu.

Wakati wa kutoka kwa sauti ya neno Labbayk lililotamkwa na wale Waislamu, Abdullah Ram?hid aliyekuwa amezishikilia hatamu za ngamia wa Mtume (s.a.w.w.) mikononi mwake alisoma tenzi zifuatazo kwa sauti yenye kuvuma na ya kuvutia, akasema: “Enyi wana wa kufuru na kuabudu masanamu. Mpisheni njia Mtume wa Allah. Hamna budi kutambua kwamba yeye ndiye chanzo cha ustawi na wema. Ee Mola! Ninayaamini maneno yake nami ninayazingatia maamrisho Yako kuhusiana na kuutambua Utume wake.”2

Mtume (s.a.w.w.) alifanya Tawaaf ya Kaabah akiwa amepanda ngamia. Alipoifikia hatua hii aliamrisha kwamba Abdullah bin Rawaah aisome dua maalum ifuatayo na wale wengine wasome pamoja naye. Dua hiyo ni hii: “Hakuna mungu ila Allah (tu). Yeye Yu Mmoja tu na Asiye kifani. Ameitimiza ahadi Yake (Aliyoahidi kwamba Waislamu watafika kwenye Ka’abah hivi karibuni). Amemsaidia mja wake. Amelitukuza jeshi la upweke wa Allah, na kuyashutumu na kuyatupilia mbali majeshi ya kufuru na ushirikina.”

Katika siku ile vituo vyote vya hija na zile sehemu zifanyikako ibada za Umrah, ikiwa ni pamoja na mle msikitini Ka’abah, Safaa na Marwah zilikuwa chini ya utawala wa Waislamu. Sasa ibada za bidii na shauku kubwa kwenye sehemu iliyokuwa kitovu cha ibada ya masanamu na ushirikina kwa kipindi kirefu zimepiga pigo kubwa mno la kiakili kwa uongozi wa ushirikina na wafuasi wao kiasi kwamba ushindi wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) ulithibitika bara Arabuni kote.

Wakati wa sala ya adhuhuri ukaingia. Sasa ilikuwa muhimu kwamba Waislamu walitimize hili jukumu la Allah kwa jamaa mle msikitini na mwadhini wao atoe adhana kwa sauti kuu. Kama alivyoamrishwa na Mtume (s.a.w.w.), Bilal yule mtumwa Mwethiopia aliyekuwa akiteswa mjini humo kwa kipindi kirefu kutokana na kusilimu kwake, alipanda juu ya paa la Kaabah na akaiweka mikono yake masikioni mwake, alitamka kwa sauti maalum zile sentensi tunazozitaja sote. Alizitamka kwenye sehemu ambayo tangazo la Upweke wa Allah na Utume wa Muhammad katika kipindi fulani lilikuwa ni kosa kubwa kwa mujibu wa makafiri wa Kiquraishi.

Sauti yake na zile thibitisho ambazo Waislamu walizifuatisha baada ya kuisikia kila sehemu ya adhana viliyafikia masikio ya waabudu masanamu na maadui wa Upweke wa Allah, na vikawatia wasiwasi mno kiasi kwamba Safwan bin Umayyah na Khalid bin Usayd wakasema: “Mungu na asifiwe kwamba jadi zetu walikufa nao hawakuisikia sauti ya huyu mtumwa Mwethiopia.”

Suhayl bin Amr alipomsikia Bilal akiyatamka maneno: Allah Akbar aliuficha uso wake kwa leso. Hawakupatwa na wasiwasi mno tu kutokana na sauti ya Bilal, bali walijihisi kwamba wamo katika mateso ya kiakili kutokana na vile vifungu mbalimbali vya adhana vilivyokuwa kinyume kabisa na itikadi zao walizozirithi kutoka kwa jadi zao.

Mtume (s.a.w.w.) alianza kufanya Sai (kutembea) baina ya vilima vya Safaa na Marwah. Kwa kuwa wanafiki na waabudu masanamu walieneza uvumi kwamba hali mbaya ya hewa Madina imewadhoofisha Waislamu, aliamua kufanya Harwalah3 katika sehemu ya ile Sai, na Waislamu nao wakamwiga. Baada ya kufanya Sai Waislamu waliwatoa kafara wale ngamia na wakavua Ihraam na wakanyoa nywele za vichwa vyao. Baada ya hapo Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha kwamba watu mia mbili waende Marruz Zahran wakalinde zile silaha na zana nyingine za kijeshi ili kwamba wale watu waliokuwa wakishika kazi ile waje kwenye Haram na kufanya ibada za Umra.

Ibada za Umra zikamalizika Muhajiriin walikwenda majumbani mwao kuwasalimu ndugu zao. Vilevile waliwakaribisha baadhi ya Ansar huko majumbani kwao na hivyo wakawaonyesha fadhila kwa yale makaribisho na huduma walizotendewa na Ansar katika kile kipindi cha miaka saba.

Mtume (S.A.W.W.) Aondoka Mjini Makka

Utukufu na heshima ya Uislamu na Waislamu vilijenga hisia kali zaidi akilini mwa watu wa Makka, na wakapata ujuzi zaidi wa fikara za jumuia ya Waislamu. Machifu wa Waquraishi walitambua kwamba kule kukaa kwa Mtume (s.a.w.w.) na masahaba wake kumezidhoofisha nyoyo za watu wa Makka kuhusiana na imani yao juu ya ibada ya masanamu na uadui wa itikadi ya Upweke wa Allah, na wamejenga huba na mvuto baina ya haya makundi mawili. Hivyo ulipomalizika wakati wa mwisho wa zile siku tatu mwakilishi wa Waquraishi aliyeitwa Huwaytab alimjia Mtume (s.a.w.w.) na kumwambia: “Kipindi cha siku tatu kilichowekwa kwenye yale mapatano kwa wewe kuweza kukaa Makka kimekwisha, na hivyo basi, huna budi kutoka nchi yetu upesi iwezekanavyo.”

Baadhi ya masahaba waliona wasiwasi kutokana na ukali wa yule mwakilishi wa Waquraishi. Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) si mtu achelewaye katika kuyatekeleza mapatano. Hivyo basi, Waislamu waliamrishwa kulitoka eneo la Haram upesi sana.

Maimuna (dada yake Ummi Fazal, mkewe Abbas) alivutika mno na hamasa za Waislamu kiasi kwamba alimweleza shemeji yake Abbas, ami yake Mtume (s.a.w.w.) kwamba alikuwa tayari kuolewa na Mtume (s.a.w.w.) na akalichukulia jambo hilo kuwa ni heshima kwake. Mtume (s.a.w.w.) alimkubalia na hivyo akauimarisha uhusiano wake na Waquraishi. Mwelekeo wa mwanamke kwa mwanaume aliye na umri mkubwa kuliko wake wenyewe ni ushahidi utoshekezao wa mvuto wake wa kiroho. Vile vile Mtume (s.a.w.w.) alimwomba yule mwakilishi wa Waquraishi kumpa muda ili aweze kuifanya sherehe ya ndoa yake mle mjini Makkh na vilevile aweze kuwaalika machifu wote wa Makka kushiriki kwenye Walima. Hata hivyo, yule mwakilishi wa Waquraishi hakuikubali rai hiyo na akasema: “Sisi si wahitaji wa chakula chako.”

Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha kwamba Waislamu waondoke Makka wakati wa adhuhuri. Alimwelekeza mtumwa wake tu aliyeitwa Abu Raafi’ kubakia pale hadi wakati wa jioni ili aje na mkewe Mtume (s.a.w.w.).4

Baada ya kuondoka kwa Waislamu, maadui wa Mtume (s.a.w.w.) walimkemea Maimuna, lakini kwa vile alikuwa kaishajenga mvuto na Mtume (s.a.w.w.) na hivyo amejitolea kuolewa naye, maneno yao hayakuwa na athari kwake. Hivyo basi, ile ahadi iliyosimama juu ya ndoto ya kweli ya Mtume (s.a.w.w.) ambayo aliifanya na Waislamu mwaka mmoja uliopita juu ya Hija kwenye Ka’abah na kufunguliwa kwa malango ya Makka kwa ajili ya Waislamu ilitimizwa, Aya ifuatayo iliteremshwa:

لَقَدْ صَدَقَ اللَّهُ رَسُولَهُ الرُّؤْيَا بِالْحَقِّ ۖ لَتَدْخُلُنَّ الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ إِنْ شَاءَ اللَّهُ آمِنِينَ مُحَلِّقِينَ رُءُوسَكُمْ وَمُقَصِّرِينَ لَا تَخَافُونَ ۖ فَعَلِمَ مَا لَمْ تَعْلَمُوا فَجَعَلَ مِنْ دُونِ ذَٰلِكَ فَتْحًا قَرِيبًا {27}

“Bila shaka Allah Amemtimizia Mtume Wake ndoto ya haki. Bila ya shaka nyinyi mtauingia Msikiti Mtakatifu, Inshallah, kwa amani, na hali mmenyoa vichwa vyenu na mmepunguza nywele. Hamtakuwa na khofu. Na Mwenyezi Mungu anajua msiyoyajua. Basi alikupeni kabla ya haya ushindi ulio karibu.” (Sura al-Fatih, 48:27).

  • 1. Umrah ina ibada maalum ziwezazo kufanywa wakati wowote ule wa mwaka. Tafauti na ibada za Haj ziwezazo kufanywa kwenye mwezi wa Dhil–Haj tu.
  • 2. Siiratu Ibn Hisham, Juz. 2, uk 47.
  • 3. Harwalah ni aina ya utembeaji wa kuchanganya zaidi ya ule wa kawaida lakini hauna kukimbia.
  • 4. Siiratu Ibn Hishamu, Juz. 2, uk. 372